Namna Utatu Mtakatifu unajibu swali la “Mungu ni nani?”
Namna imani yetu juu ya Utatu Mtakatifu inavyotusaidia sisi kuomba na kumuabudu Mungu kiundani zaidi.
Namna Utatu Mtakatifu unavyofunuliwa katika Injili.
Mistari mikuu katika Biblia kuhusiana na fundisho la Utatu Mtakatifu.
Umuhimu wa maneno mahususi ambayo tunayatumia kuzungumza kuhusiana na Utatu Mtakatifu, na ambayo yanapaswa kutumika.
Ni kwa namna gani Utatu Mtakatifu unaelezea mapenzi ya Mungu kwa uumbaji, ukombozi,na kanisa.
Tamko la Imani ya Kikristo kuhusiana na Utatu Mtakatifu.
(2) Mwanafunzi atakuwa na uwezo wa kutambua mafundisho potofu au uzushi ambayo yanamuwasilisha Mungu kama aliyegawanyika katika vipande vipande au kwamba kushindwa kutofautisha kati ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Fikiria unakutana na mtu kwa mara ya kwanza.[1] Kisha wanapouliza, “Wewe ni nani?” unaweza kusema “Mimi nina nguvu, mwenye hekima, na mwema”? au “mimi ni mwanadamu—nina mwili na nafsi”? Hapana! Majibu haya yanaeleza jinsi ulivyo (mwenye nguvu, mwema, mwanadamu mwenye hekima), lakini hayatuambii wewe ni nani. Mtu anapotuuliza sisi ni akina nani, tunataja majina yetu binafsi—kwa mfano, “Mimi ni Furaha” au “Mimi ni Barnabas.”
Sasa, zingatia swali, “Mungu ni nani?” watu wengi wangeweza kusema “Mungu ni mwenyezi, mwema kikamilifu, na mkamilifu mwenye hekima” au “Mungu ni nafsi ya kiuungu; ni roho.” Mambo haya yote ni ya kweli na ni muhimu sana. Hata hivyo, majibu haya yanatueleza sisi Mungu ni nini (mwenye enzi, mwema, na roho yenye hekima). Njia nzuri ya kujibu swali hili ni kusema, “Mungu ni Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.” Hii ni Mungu ni Nani, uelewa ambao unatuwezesha sisi kuhusiana vizuri na Mungu. Kuna kitu utatu kuhusiana na Mungu ni nani. Neno la kilatini trinitas (Utatu Mtakatifu) lina maana “tatu.” Utatu Mtakatifu ni jibu kwa swali “Mungu ni nani?”
Ni njema/vema kusema, “Ninamwaminii Mungu,” au ninaomba, “Mungu, nisaidie.” Lakini hata hivyo Myahudi au Muislamu anaweza kuzungumza au kuongea na hata kuomba kwa namna hii. Ni Mkristo tu ndiye anaweza kusema, “Ninamwamini Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Ni mkristo tu ndio anayeweza kuomba, “Baba, toa kwa ajili yangu. Yesu, nisamehe. Roho Mtakatifu, niongoze.” Ni mkristo tu ndiye anayeweza kumfahamu Mungu kweli kweli. Nii ndio sababu Gregori mwanatheolojia aliandika, “Ninaposema ‘Mungu,’ Ninamaanisha ‘Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.’”[2]
[1]Nyenzo katika somo hili zilitolewa na Johnathan Arnold kwa mashauriano na Dr. Tom McCall na Dr. David Fry, pamoja na mwandishi kiongozi, Dr. Stephen Gibson.
[2]Oration 38. Gregory Mwanatheolojia, pia alijulikana kama Gregory wa Nazianzus, alikuwa msomi mkubwa wa Kikristo kutoka Uturuki ya leo.
Sala ya Ufunguzi
Endapo Utatu Mtakatifu ni jibu la swali “Mungu ni nani?” basi kujifunza kwetu juu ya fundisho hili kunapaswa kutusaidia sisi kumfahamu na kumtukuza Mungu. Fundisho la Utatu Mtakatifu linafanya maisha yetu ya maombi kuwa ya ndani kabisa kwa sababu linatusaidia sisi kumuabudu Mungu kama jinsi alivyo. Hapa chini ni mfano wa aina ya maombi ambayo yanamsaidia mtu kukua katika uhusiano binafsi na Utatu Mtakatifu.
► Someni sala kwa pamoja kama darasa.[1] Endapo mnasoma somo hili mchana au jioni, mnaweza kusema “habari za mchana, Baba wa mbinguni” au “Habari za jioni, Baba wa mbinguni.”
Habari za asubuhi, Baba wa mbinguni.
Habari za asubuhi, Bwana Yesu.
Habari za asubuhi, Roho Mtakatifu.
Baba wa mbinguni, ninakuabudu kwa sababu wewe ni muumbaji na mtunzaji wa ulimwengu.
Bwana Yesu, ninakuabudu kwa sababu wewe ni mwokozi na Bwana wa ulimwengu.
Roho Mtakatifu, ninakuabudu kwa sababu wewe unatakasa watu wa Mungu.
Utukufu kwa Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.
Baba wa mbinguni, ninaomba kwamba siku ya leo niishi katika uwepo wako na kukupendeza wewe zaidi na zaidi.
Bwana Yesu, ninaomba kwamba leo nichukue msalaba wangu na nikufuate wewe.
Roho Mtakatifu, ninaomba kwamba siku hii ya leo unijaze mimi na wewe mwenyewe na usababishe tunda lako kukomaa ndani ya maisha yangu: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.
Utatu Mtakatifu, uliobarikiwa, mtakatifu na wenye utukufu, nafsi tatu katika Mungu mmoja, unihurumie. Amina.
[1]Haya ni maombi ya John Stott, aliyokuwa anaomba kila siku asubuhi alipoamka. Stott alikuwa mwanatheolojia kutoka Uingereza ambaye aliishi tangu mwaka 1921 hadi 2011.
Mungu Mmoja na wa Pekee
Katika Agano la Kale, Mungu aliwafundisha watu wake kukiri kwamba kuna Mungu mmoja tu. “Sikiza, Ee Israeli; BWANA [Yahweh] Mungu wetu, BWANA [Yahweh] ndiye mmoja” (Kumbukumbu la Torati 6:4). Imani hii iliwatenga Israeli na mataifa mengine ambayo yaliamini juu ya miungu mingi. Yesu na mitume waliendelea kufundisha kwamba kuna Mungu mmoja tu (Marko 12:29, 1 Timotheo 2:5). Hakuna miungu watatu au miungu 10. Kuna Mungu mmoja tu asiyeonekana, roho mwenye enzi ambaye tunaweza kumuita “Mungu”.
Wakatu huo huo, kuna dondoo katika Agano la Kale kwamba kitu kama utatu au uwingi katika Mungu mmoja. Mungu alipomuumba Adamu na Eva, alisema, “Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu…” (Mwanzo 1:26). Mungu alikuwa anazungumza na nani? Kwa nini anasema “mfano wetu” (wingi)? Isaya alipoona maono ya Mungu akiwa hekaluni, alisikia malaika wakilia “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu…” (Isaya 6:3), na Bwana akasema, “…naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” (Isaya 6:8). Katika Zaburi 110:1, Yahweh anazungumza na mwingine ambaye anatambulishwa kama Bwana wa Daudi. Ni kwa namna Bwana azungumze na Bwana?
Jibu zuri la maswali haya limetolewa katika Agano Jipya. Biblia ni habari moja kubwa. Kuna baadhi ya kweli ambazo mwandishi alichagua kutozifichua hadi mwisho wa habari, wakati ambapo tungekuwa tumeandaliwa vyema kuzipokea. Mungu alifunua kweli ya kina zaidi kuhusu Yeye ni nani wakati Mungu Baba alipomtuma Mwana wake ili avae mwili na baadae alipomtuma Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Injili inatuonesha sisi kwamba kwa hakika kuna utatu katika Mungu mmoja. Utatu Mtakatifu ni ufunuo mkuu zaidi wa kuhusu Yeye kwa wanadamu. Ni kitovu cha Imani ya Kikristo.
Kufanyika Mwili: Mwana wa Mungu Kufunuliwa
Mungu alijifunua zaidi kuhusu Yeye mwenyewe, ulipotimia utimilifu wa wakati timilifu, “…Mungu alimtuma Mwanawe…” (Wagalatia 4:4).[1] “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee…” (Yohana 3:16). Kama Mungu alimtuma Mwana wake, basi Mungu mmoja huyo lazima awe Baba ambaye ana Mwana. Kama Mwana alitumwa duniani, basi alikuwa Mwana wa Mungu kabla hajatumwa.
Yesu alidai kuwa Mwana wa Mungu katika namna ya kipekee ambayo ilimfanya Yeye kuwa sawa na Baba. Yohana 5:18 inasema, “Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.” Yesu aliposema, “…Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko” (Yohana 8:58), alikuwa akitangaza kuwa yeye ni Yahweh (Kutoka 3:14). Katika 1 Wakorintho 8:6, Paulo alithibitisha Kumbukumbu la Torati 6:4 (“…BWANA ndiye mmoja”), lakini ilijumuisha Bwana Yesu Kristo ndani ya utambulisho wa Muumbaji mmoja.
Katika Yohana 14:28, Yesu alisema, “…Baba ni mkuu kuliko mimi.” Mstari huu haumaanishi kwamba Mwana si Mungu kamili, kwa sababu Injili yote ya Yohana inathibitisha Yesu na Baba kuwa sawa sawa.[1] Yohana 14:28 lazima isomwe katika muktadha. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “…Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.” Yesu alikuwa anajitofautisha mwenyewe kama mwanadamu ambaye yuko duniani (pamoja na mateso yake yote) na Baba yake ambaye yuko mbinguni (katika utukufu wake wote). Anawaambia wanafunzi wake kwamba kama wanampenda, wangetaka Yesu kutukuzwa katika uwepo wa Baba kwa utukufu ule ambao alikuwa nao pamoja na Baba kabla ya ulimwengu kuwako (Ona Yohana 17:5.) Kumbuka: Yesu ni Mungu kweli na Mwanadamu kweli kwa wakati mmoja. Kama Mungu (kulingana na asili ya uungu), Mwana ni sawa na Baba. Kama mwanadamu (kulingana na asili yake ya uanadamu), mwana aliyevaa mwili yuko chini ya na ni mtii kwa Baba. Augustine anaelezea, "Tunapaswa kutambua asili mbili za Kristo—uungu, ambao kwa huo yuko sawa na Mungu, na uanadamu, ambao kwa mlengo huo Baba ni mkuu."
Kufanyika Mwili: Mwana wa Mungu Kufunuliwa (inaendelea)
Kama Mwana wa Mungu Baba, Yesu si Baba. Mwana si nafsi ile ile kama Baba. Katika Yohana 1, Yesu anaitwa “Mungu” (1:1), na bado anasema “kwa Mungu [Baba]” (1:18) yeye ni “Mwana pekee atokaye kwa Baba” (1:14). Mwana alitumwa na Baba (Yohana 5:23), aliomba kwa Baba (Mathayo 26:39), na alimuomba Baba kumtukuza Yeye kama ambavyo Yeye (Mwana) amemtukuza Baba (Yohana 17:1). Kama mwana angekuwa Baba, basi Mwana angekuwa amejituma yeye mwenyewe, amejizungumzisha, amejisemesha, na angejiomba kujitukuza yeye mwenyewe ili kwamba aweze kujitukuza yeye mwenyewe. Hii isingeleta mantiki.
Kuna utofauti kati ya Baba na Mwana, lakini (nafsi) zimeungana kikamilifu katika Mungu mmoja. Katika Yohana 14:11 Yesu alisema, “Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu…” Baba na Mwana wanakaa ndani ya kila mmoja kikamilifu kwa sababu hao ni Roho moja ya milele isiyoonekana. Sio roho mbili au miungu miwili tofauti.
Fundisho la Utatu Mtakatifu ni matokeo ya tafakari ya ndani sana juu ya mafundisho ya Yesu, pia juu ya mafundisho yake kuhusiana na Roho Mtakatifu.
Pentekoste: Roho Mtakatifu Anafunuliwa
Mara kwa mara Yesu alizungumza kuhusiana na Baba yake, lakini pia alizungumza kuhusiana na mwingine: Roho Mtakatifu. Yesu aliahidi kumuomba Baba kumtuma Roho (Yohana 14:16–17). Pia aliahidi kumtuma Roho ambaye anatoka kwa Baba (Yohana 15:26). Yesu aliwahakikishia wanafunzi kwamba Baba angemtuma Roho kwa jina lake (Yohana 14:26). Baada ya ufufuo na kupaa, Yesu alipokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, na akamwaga Roho juu ya wanafunzi wake siku ya Pentekoste (Matendo ya Mitume 2:33).
Kama Roho wa Mungu, Roho Mtakatifu ni sawa na Baba na Mwana. Mwanadamu alipodanganya, Petro alimuuliza, “Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu…? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu” (Matendo ya Mitume 5:3–4). Roho Mtakatifu ni Mungu. Ni wa milele (Waebrania 9:14) na anajua yote (1 Wakorintho 2:10–11).
Kwa wakati huo huo, Roho Mtakatifu sio Baba au Mwana. Roho Mtakatifu ni nafsi nyingine, kama ambavyo Mwana ni nyingine (sio Baba). Roho alitumwa na Baba na Mwana, anazungumza kile tu anachosikia kutoka kwa Baba na Mwana, (Yohana 16:13), na amekuja kumtukuza Mwana (Yohana 16:14). Kama Roho angekuwa Baba na Mwana, kwa hiyo Roho angekuwa amejituma, angeongea au kuzungumza kile ambacho amekisikia kutoka kwake mwenyewe, na angetafuta kujitukuza. Hiyo isingekuwa na mantiki!
Maandiko Makuu
Mathayo 3:13–17 ni muhimu sana kwa fundisho la Utatu Mtakatifu kwa sababu linaonesha muingiliano wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Yesu alibatizwa, Baba akaongea kutoka mbinguni (“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye”), na Roho Mtakatifu anafunua muonekano wake kwa kutokea kama hua na kuja na kukaa juu ya Yesu. Haitakuwa na mantiki kusema kwamba Baba ni Mwana au Roho Mtakatifu ni Mwana. Kama hivyo ndivyo ingekuwa, basi Mwana angekuwa ameitupa au kuirusha sauti yake mbinguni ili kusema namna anavyojipendeza, wakati huo huo angeshuka juu yake mwenyewe na kukaa juu yake mwenyewe! Walikuwa nafsi tatu katika ubatizo wa Yesu.
Kanuni ya ubatizo katika Mathayo 28:19 ni kitovu cha fundisho la Kikristo juu ya Utatu Mtakatifu: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Katika Agano la Kale, Mungu aliliweka Jina lake (Yahweh) juu ya watu wake, na akawaita ili kulibeba jina lake kwa mataifa (Hesabu 6:27, Kumbukumbu la Torati 28:10). Katika Agano Jipya, Mungu ameliweka jina la Baba, na Mwana, na la Roho Mtakatifu juu ya watu wake, na akawatuma ulimwenguni katika utume maalumu. Hii inaonesha kwamba Baba, Mwana, na Roho kila mmoja ni Mungu, na bado kila mmoja ni tofauti na mwingine. Fundisho la Utatu Mtakatifu linawasaidia wanafunzi kuelewa inamaanisha nini kubatizwa katika jina la Utatu Mtakatifu. Kiukweli, theolojia yote ya kikristo imejengwa kutoka katika pointi hii kuu.
► Mchoro katika ukurasa huu unaitwa “Ngao ya Utatu Mtakatifu.” Unafupisha baadhi ya kweli muhimu ambazo tumejifunza hadi sasa. Chora nakala ya mchoro; huu utakusaidia wewe kukumbuka.
Suala la Maneno: Maneno Makuu katika Historia ya Kanisa
Injili inafunua kwamba kuna jambo la utatu kuhusu Mungu mmoja. Hata hivyo, Mungu si watatu na mmoja katika maana ileile. Hakuna miungu watatu na Mungu mmoja. Hilo lingekuwa mkanganyiko (na kukataa mafundisho ya wazi ya Biblia!). Tunahitaji maneno ya kuelezea maana ambayo Mungu ni utatu, na maana ambayo “…BWANA ndiye mmoja” (Kumbukumbu la Torati 6:4).
Watu wengi katika kanisa la kwanza walizungumza Kigiriki/Kiyunani au Kilatini, na walitumia karne nyingi kujadili ni maneno gani yatumike. Haipaswi kutushangaza kwamba wakati mwingine ni vigumu kupata lugha ya kuelezea kuhusu Mungu. Lugha ya wanadamu haiwezi kumwelezea Mungu kikamilifu. Hata hivyo, hakuna jambo muhimu zaidi kuliko kile tunachoamini kuhusu Mungu, kwa hiyo lazima tuchague maneno yetu kwa uangalifu mkubwa ili tusichanganye au kupotosha wengine.
Maneno ousia (Kigiriki/Kiyunani) na substantia (Kilatini) yalitambuliwa kama maneno mazuri zaidi kuonesha kile ambacho ni umoja kuhusu Mungu—kile ambacho ni sawasawa kwa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Bwana ni mmoja ousia au substantia. Maneno haya yanaelekeza kwa nini kitu fulani ni (rejea kielelezo mwanzoni mwa somo hili). Mungu ni roho isiyoonekana, ya milele, kamilifu katika nguvu, yenye hekima, na njema. Katika kiswahili, neno asili/dutu linatumika kwani ni kimoja kuhusu Mungu. Maneno asili, kiumbe, au kiini pia yametumika. Kuna asili au kiumbe mmoja tu wa kiuungu.
Maneno hypostasis (Kiyunani/Kigiriki) na persona (Kilatini) yalitumika kuonesha kitu gani ni utatu kuhusu Mungu. Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni hypostases tatu halisi na tofauti au personae. Maneno haya yanaonesha mtu ni nani. Tena: Utatu Mtakatifu ni jibu kwa swali “Mungu ni Nani?” Katika Kiswahili, neno nafsi limetumika kwa ajili ya nini ni utatu kuhusiana na Mungu. Hatutumii maneno haya kwa watu au mtu, kwa sababu linaonesha kwamba ni viumbe au dutu tofauti.
Hata maneno haya yana udhaifu wake na mipaka yake, na ni lazima yaelezewe kwa uangalifu ili kuepuka mchanganyo au kutokuelewana. Katika kila lugha, wanatheolojia wanapaswa kufikiri kwa makini ni maneno gani watumike. Wakati mwingine lugha haina maneno mazuri ya kutumia. Lakini kutafuta maneno yanayotambuliwa na kueleweka kwa upana ni msaada mkubwa sana. Kwa mfano, maneno haya hutusaidia kufafanua kwa uwazi kile ambacho Yohana 10:30 inamaanisha na kile isichomaanisha. Yesu aliposema, “Mimi na Baba tu umoja,” alimaanisha, “Mimi na Baba tu kiumbe mmoja”; hakumaanisha, “Mimi na Baba ni nafsi ileile.” Yohana alipoandika, “…Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” (Yohana 1:1), alimaanisha, “Mwana alikuwa pamoja na nafsi ya Mungu Baba, na Mwana alikuwa na asili ileile ya uungu (au alikuwa wa dutu ile ile) kama Baba.”
Kwa Nini Tunahangaika Kuelewa
Wakati tofauti hizi ni za msaada, Utatu Mtakatifu bado ni dhana ngumu kwetu kuelewa. Kwa sehemu, hii ni kwa sababu fahamu zetu za kibinadamu zina mipaka na haziwezi kumuelewa Mungu asiye na mipaka. Lakini pia ni kwa sababu hakuna viumbe wengine katika uumbaji ambao ni nafsi tatu katika dutu moja. Mara nyingu sisi hujifunza kwa kulinganisha mambo mapya na yale ambayo tayari tunayafahamu, lakini hakuna kitu cha kulinganisha: hakuna kiumbe hata mmoja ambaye ni nafsi tatu.
Mwangalie mtu. Katika kila mwili na nafsi ya mwanadamu ambayo inaishi, kuna nafsi moja tuu —“Yoktani” au “Hellenita.” Kama mtu mmoja anadai kuwa zaidi ya nafsi moja, haitaleta mantiki, kwa sababu tunafahamu kwamba hivyo si namna ambavyo watu wanaishi. Hata hivyo, Mungu si mwanadamu/mtu! Mungu ni tofauti kabisa na viumbe wengine ambao tunaweza kuwachunguza. Mungu amejifunua kwetu kwamba katika kiumbe mmoja wa kiuungu, kweli kuna nafsi tatu. Kwa kweli tunapokea na kuamini kwa imani kile ambacho Mungu amekifunua. Akili zetu haziwezi kumuelewa Mungu kikamilifu, lakini tunafurahia katika kile ambacho Mungu amekifunua na kusubiri ili kumfahamu Mungu vizuri zaidi tutakapofika mbinguni.
Makosa la Kuepuka: Mafundisho Potofu Kuhusiana na Utatu
Baadhi ya watu wanajaribu kuuweka Utatu Mtakatifu ili uweze kutosha katika uelewa wao, kwa msingi wa kile ambacho wanaweza kukiangalia katika uumbaji. Wanaoamini Utatu wanapaswa kuwa makini ili kamwe: (1) wasigawanye dutu moja ya Mungu, (2) wasichanganye nafsi nafsi tatu ndani ya Mungu, au (3) wasichukulie nafsi yeyote ya uungu kama duni au isiyo sawasawa na nyingine katika dutu.
1. Usigawanye Dutu. Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu sio sehemu tatu zinazotengeneza kitu kimoja. Mungu hana vipande vipande. Mungu si kama yai moja lenye sehemu tatu (ganda gumu, kiini, na ute mweupe). Mungu si kama ua moja lenye petali tatu. Mifano hii inaakisi uzushi unaoitwa partialism.
2. Usichanganye (usishindwe kutofautisha) nafsi. Baadhi ya watu hudai kwamba Mwana ni Baba tu aliyevaa vazi tofauti, au kwamba Roho ni Mwana anayejitokeza katika umbo lingine. Hata hivyo, kama tulivyokwisha kuona,Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu wanahusiana kama nafsi zilizo tofauti. Baba sio Mwana; Mwana si Roho Mtakatifu. Mungu sio kama molekyuli moja ya maji inayoweza kuwapo katika hali tatu (kama barafu iliyoganda, kimiminika, au mvuke). Mungu si kama mtu anayebadilisha kofia au mavazi matatu tofauti. Mungu si kama mtu mwenye majukumu matatu (baba, mume, na mfanyakazi). Vielelezo hivi inaakisi uzushi unaoitwa modalism ambao unakana kwamba Mwana na Roho ni nafsi tofauti. Modalism pia inaitwa Sabellianism (iliitwa kwa kufuata mwalimu wa uzushi au upotovu katika karne ya tatu aliyeitwa Sabellius).
3. Usichukulie nafsiyeyote kama duni au isiyo sawa katikaDutu. Fundisho lingine lenye uharibifu mkubwa ni kwamba Mwana ni duni kuliko Baba. Baadhi ya watu hudai kwamba Mwana alikuwa kiumbe wa kwanza na mkuu zaidi aliyeumbwa na Baba. Wanaweza kumtukuza Yesu na kumwita “mungu,” lakini hawafundishi kwamba yeye ni sawa na Baba au kwamba amekuwapo milele. Uzushi huu unaitwa Arianism (uliopewa jina kutokana na jina la mwalimu wa uongo wa karne ya nne aitwaye Arius). Wanaounga mkono uzushi huu wanafundisha kwamba Mwana ana kiini kinachofanana tu na ya Baba, na kwamba yeye ni duni. Hata hivyo, Biblia inafundisha kwamba Mwana ni “mwenye kiini sawa kama Baba” (kama inavyojawa katika Tamko la Imani la Nikea). Mwana na Roho ni sawa na Baba katika nguvu, utukufu, na umilele. Wanastahili kuabudiwa na wana uwezo wa kutuokoa kwa nguvu zao kuu.
► Je, umewahi kusikia vielelezo vingine vya Utatu Mtakatifu? Kwa nini vinaweza kuwa vinapotosha au vyenye matatizo?
Sababu za Kila Jina
Ili kuelewa kiukweli fundisho la Utatu Mtakatifu, tunahitaji kuangalia kwa makini katika nafsi tatu. Kwa nini nafsi ya kwanza na ya pili zinaitwa“Baba” na “Mwana”? Kwa nini nafsi ya tatau inaitwa “Roho Mtakatifu”? Majina haya yana maana. Majina yanatuambia sisi jambo la kweli na la milele kuhusu Mungu. Hata kabla ya ulimwengu kuumbwa, Mungu alikuwa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
“Baba” na “Mwana”
Ingawaje Mungu ni Baba yetu wa mbinguni (Mathayo 6:9), nafsi ya kwanza ya Utatu Mtakatifu haiitwi “Baba” kwa sababu hii. Nafsi ya kwanza inaitwa “Baba” kwa sababu ni Baba wa milele wa Mwana! Vivyo hivyo, nafsi ya pili inaitwa “Mwana” kwa sababu yeye ni Mwana wa milele wa Baba. Majina Baba na Mwana yanaonesha uhusiano wa milele baina yao. Baba na Mwana wote wana uzima wa milele ndani yao, uzima ambao haukuumbwa ambao ni wa Mungu pekee, lakini uzima huu Baba anautoa kwa Mwana (Yohana 5:26).
Kwa sababu Baba na Mwana ni wa milele, Baba “hakutoa” uzima kwa Mwana katika kipindi fulani mahususi cha muda. Baba hakumuumba Mwana. Baba “alimzaa” tangu milele au alimleta Mwana katika namna ambayo Mungu pekee anafahamu. Hiki ndicho kitovu cha mafundisho ya Tamko la Imani la Nikea: “Tunaamini …….Bwana mmoja Yesu Kristo Mwana wa pekee wa Mungu, aliyezaliwa na Baba kabla ya nyakati zote; Mungu kutoka kwa Mungu, Nuru kutoka kwa Nuru, Mungu wa kweli kutoka kwa Mungu wa kweli; aliyezaliwa, si kuumbwa.”
Hii ni siri kubwa. Hatuwezi kuelewa kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa mwanadamu! Je, ni kwa kiasi gani tunaweza kuelewa inamaanisha nini kwa Mungu Baba kumleta Mwana tangu milele? Mababa wa kanisa mara zote wameonesha Waebrania 1:3, ambayo inasema kwamba Mwana ni “…mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake...” Nuru mara zote hutoa mwanga wake.[1] Kwa kadiri ambavyo mshumaa unawaka, unatoa mwanga wa nuru yake. Kwa sababu Baba ni Nuru ya milele, mara zote anatoa mwanga ambao ni Mwana wake. Baba kamwe hakuanza kummulika Mwana. Na kamwe hataacha kummulika Mwana. Baba na Mwana wapo katika uhusiano wa milele ambao unaweza kuitwa “muwako/muangazo” na “kuangazwa.” Yesu ni “Mungu kutoka kwa Mungu [Baba], Nuru kutoka kwa Nuru [Baba]” (Tamko la Imani la Nikea).
“Roho”
Jina Roho pia linaelekeza kitu ambacho milele ni kweli kuhusiana na nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu. Kifungu cha maneno Roho wa Mungu sio kama kifungu cha maneno roho ya Musa au roho ya Abrahamu, ambapo “roho” inarejelea ya kiroho au sehemu isiyoshikika ya mwanadamu. Mungu ni roho tu na hana sehemu kadhaa. Badala yake, kifungu cha maneno “Roho ya Mungu” kinaonesha Roho ni kutoka kwa Baba, kama ambavyo Mwana ametoka kwa Baba. Neno la kibilia la Roho linaweza pia kutafsiriwa kama “Pumzi.” Kama mtu anavyopumua pumzi yake, Roho“hutoka” kutoka kwa Baba (Yohana 15:26). Wakristo wanaamini kwamba Roho pia ametoka kwa Mwana tangu milele.[2]
Kwa sababu Roho ni wa milele, Roho hakutetwa katika kipindi fulani cha wakati. Roho hakuumbwa na Baba. Baba tangu milele anapumua Roho. Hatufahamu kwa uhakika inamaanisha nini kwamba Roho “ametoka” kwa Baba tangu milele, lakini tunafahamu kwamba si sawa na “kuzaliwa.” Vinginevyo, Baba angekuwa na mwana mwingine!
[1]“Ni lini mtu aliona mwanga pasipo uangavu wa muwako wake, hilo linaweza kusemwa kuhusiana na Mwana, ‘Kulikuwa na wakati ambapo yeye hakuwepo,’ au ‘Kabla ya kizazi chake hakuwepo’?” (Athanasius, Discourse I Against the Arians 14.12).
[2]Katika karne ya sita, kanisa la Magharibi liliongeza maneno “na Mwana” (filioque kwa Kilatini) katika Tamko la Imani la Nikea: “Roho Mtakatifu… anatoka kwa [na Mwana].” Baadhi ya hoja za kawaida zinazounga mkono filioque ni kwamba “Roho wa Mungu” pia anaitwa “Roho wa Kristo” katika Warumi 8:9, na kwamba kutumwa kwa Roho na Mwana (Yohana 15:26) pamoja na kumpulizia Roho (Yohana 20:22) katika wakati kunaakisi uhusiano wa milele kati ya Mwana na Roho, kama vile kutumwa kwa Mwana na Baba kunavyoonyesha uhusiano wake wa milele na Mwana.
Dondoo Kuu za Ufupisho
Kweli kuu ambazo zinahitaji kufahamika na waamini wote zimefupishwa katika Tamko la Imani la Athanasi:
1. Baba hatoki kwa yeyote. Hakuumbwa au kuzaliwa. (Hakuzaliwa).
2. Mwana ametoka kwa Baba pekee. Hakuumbwa au kutengenezwa. Amezaliwa tangu milele.
3. Roho Mtakatifu ametoka kwa [na Mwana]. Hakutengenezwa, hakuumbwa, au hakuzaliwa. Tangu milele ametoka.
4. Kwa hivyo, kuna Baba mmoja, na si Baba watatu, kuna Mwana mmoja, na si wana watatu. Kuna Roho Mtakatifu mmoja, na si Roho Mtakatifu watatu.
Nguvu ya Kuelezea
Mafundisho haya yanaelezea kwa nini kwa kawaida tunasema Baba, Mwana, na Roho (kwa mpangilio huo), badala ya Roho, Mwana, na Baba (au mpangilio mwingine wowote). Nafsi hizi tatu ni sawa katika nguvu na mamlaka kwa sababu ni Mungu mmoja; hata hivyo, Baba ndiye chanzo cha milele cha Mwana, na [pamoja na Mwana] ndio chanzo cha milele cha Roho. Kwa hiyo, inafaa kuwarejelea katika mpangilio wa Baba, Mwana, na Roho.
Mafundisho haya pia yanaeleza kwa nini Biblia inasema “Mwana wa Mungu” na “Roho wa Mungu” badala ya “Mungu Mwana” au “Mungu Roho Mtakatifu.” Kwa sababu Mwana na Roho wote ni Mungu, tunaweza kuwarejelea kwa namna hiyo. Hata hivyo, inafaa zaidi kumtaja Mwana na Roho katika uhusiano wao na Baba. Kifungu “Mungu Mwana” kinasisitiza kwamba Yesu ni Mungu; kifungu “Mwana wa Mungu” kinaonyesha kwamba Yesu ni “Mungu kutoka kwa Mungu” (Tamko la Imani la Nikea).
Mwisho, fundisho hili linatusaidia sisi kuelewa vema Injili. Nafsi yeyote ya Utatu Mtakatifu ingeweza kuwa mwanadamu na kutuokoa. Hata hivyo, inakaa vema kwamba Mwana ambaye tangu milele amezaliwa na Baba atatumwa na Baba. Inakaa vema kwamba Mwana ambaye tangu milele amezaliwa na Baba pasipo mama atazaliwa na mama wakati fulani pasipo baba. Inakaa vema kwamba Roho ambaye tangu milele anatoka kwa [na Mwana] atatumwa na Baba na Mwana kutupa sisi uzima. Injili inaakisi kitu ambacho milele ni kweli kuhusiana na Mungu!
Kushiriki Upendo wa Utatu Mtakatifu
Tumejifunza fundisho la Utatu Mtakatifu, tumeanza kuelewa vizuri Mungu ni nini, na hii inatusaidia sisi kuelewa ni kwa nini Mungu anafanya kile anachofanya. Katika kuhitimisha, zingatia dondoo tatu kuu.
1. Utatu Mtakatifu unaelezea inamaanisha nini kusema “Mungu ni upendo.” Fikiria mtu anaishi peke yake ndani ya kabati kati kati ya jangwa na kamwe hajawahi kuzungumza na yeyote. Kisha, baada ya miaka 20, anatoka ndani ya kabati lake na kukuambia, “mimi ni wa upendo.” Je, utamwamini? Pengine hapana! Mtu mwenye upendo huishi katika mahusiano na wengine. Hajitengi na wengine. Biblia inasema, “…Mungu ni upendo” (1 Yohana 4:8). Kama Mungu ni nafsi moja tu, Mungu alimpenda nani kabla hajaumba ulimwengu? Lakini kama Mungu ni nafsi tatu basi inaleta mantiki kusema kwamba Mungu ni Upendo. Yesu aliomba kwa Baba yake na akasema, “…ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yohana 17:24). Kama ukienda nyuma zaidi katika milele iliyopita kabla ya Mwanzo 1:1, kutakuwa na kitu kimoja tu kimebakia: Mungu mwenye upendo. Baba akimpenda Mwana na Roho; Mwana akimpenda Baba na Roho; na Roho akimpenda Baba na Mwana. Ni picha gani ya ajabu! Katika kiumbe mmoja Mungu ni mawasiliano ya nafsi zinazopendana! Mungu ni Upendo!
2. Utatu Mtakatifu unaelezea kwa nini Mungu aliuumba na kuuokoa ulimwengu. Mungu hakuumba ulimwengu kwa sababu alikuwa mpweke. Hakuhitaji mtu wa kumpenda. Bali ni asili ya upendo wake kujishiriki mwenyewe na kuleta maisha mapya. Mungu aliumba ulimwengu kutokana na upendo na wema kamilifu. Alimuumba mwanadamu ili kushiriki upendo wake. Adamu na Eva walitembea na Mungu katika wakati wa kupunga katika Bustani ya Edeni (Mwanzo 3:8). Wanadamu waliumbwa ili kufahamu, upendo, na kumfurahia Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Tuliumbwa kwa ajili ya Utatu Mtakatifu! Wanadamu walipochagua kumuasi Mungu na kuanguka dhambini, Mungu hakututelekeza. Baba alimtuma Mwana na Roho Mtakatifu ili kutuokoa ili kurejesha kusudi ambalo kwalo tuliumbwa. Kusudi la wokovu ni kutuleta sisi tena nyumbani kwa Utatu Mtakatifu!
3. Utatu Mtakatifu unaelezea kusudi la kanisa na hatma ya mwisho ya kanisa. Mungu alimuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:26), na akasema kwama si vema huyo mtu awe peke yake (Mwanzo 2:18). Tunaakisi upendo wa Utatu Mtakatifu tunapoishi katika mahusiano yenye upendo baina yetu. Baadhi hujisifu kwa kuwa pekee. Wanasema, “Simuhitaji yeyote yule!” Haya ni matokeo ya kusikitisha ya anguko. Pengine wameumizwa na watu wengine na wanataka kujilinda. Mungu hakukusudia sisi tuishi kwa namna hii. Kwa sabau Mungu ni Utatu Mtakatifu, lazima tuthubutu kuishi katika jamii yenye upendo na wengine. Katika kanisa, Mungu anawaunganisha wanadamu, ambao wamegawanywa na dhambi. Katika Yohana 17:22, Yesu aliomba kwamba kanisa liwe na umoja kama vile yeye na Baba walivyo na umoja. Ni wazi kwamba, washirika wengi wa kanisa hawawi mwanadamu mmoja. Bali tunapoishi kwa umoja na mshikamano, tunaakisi ushirika kamilifu wa Utatu Mtakatifu. Mbinguni, kanisa litaishi katika ushirika kamilifu na Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Ni siku ya ajabu sana iliyoje!
Hitimisho
Hitimisha somo hili kwa sifa na kuabudu. Ibada ya Wakristo ni ya Utatu Mtakatifu tangu mwanzo hadi mwisho, kwa sababu Utatu Mtakatifu ndiye tunayemwabudu!
► Semeni ombi lifuatalo la sifa kwa pamoja. Ombi hili la kale la kuusifu Utatu Mtakatifu bado linatumika na waamini wengi katika maombi yao ya kila siku na katika kila ibada ya kanisa.
Utukufu kwa Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa mwanzo, na sasa, na hata milele itakuwa, ulimwengu pasipo mwisho. Ameni
► Sema 2 Wakorintho 13:14 kwa pamoja. Baraka hii pia inatumiwa na wafuasi wengi wa Kristo katika maombi ya kila siku na katika ibada zao za kanisa.
Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae [nasi] sote.
► Someni Tamko la Imani kwa pamoja angalau mara mbili.
Tamko la Imani
Katika Mungu mmoja wa kweli na anayeishi, kuna nafsi tatu ambazo ni lazima zitofautishwe: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Wao ni dutu moja, nguvu, na umilele, ambavyo hazitakiwi kutenganishwa. Mwana amezaliwa na Baba tangu milele, na tangu milele Roho hutoka kwa [na Mwana].
Tamko la Imani la Athanasi
Angalizo kwa kiongozi wa darasa: Si lazima kusoma hii darasani.
Tamko la Imani la Athanasi imepewa jina hilo kwa heshima ya Athanasius wa Alexandria, ambaye alitetea Imani ya Kikristo katika karne ya nne wakati ambapo ilikuwa chini ya mashambulizi ya mwalimu wa uongo Arius. Ilianza kwa onyo kwa wale ambao “hawaitunzi au kuishika” Imani—yaani, wale ambao wameipokea Imani ya kweli lakini wanafanya uchaguzi wa kuikataa. Makanisa mengi yalisoma kanuni hii katika ibada ya hadhara wakati wa jumapili ya Utatu Mtakatifu, jumapili baada ya Pentekoste.
KILA atakae okoka: zaidi ya yote imenilazimu kuishika imani katholiko [ya kiulimwengu].
Ambayo, mtu asipohifadhi kamili na bila kuiharibu: Bila shaka atapoteza milele.
Na imani katholiko [ya kiulimwengu] ndiyo hii:
Tumwabudu Mungu mmoja katika utatu, na utatu katika umoja.
Tusizichanganye nafsi
Wala kuugawa Uungu [asili, hali ya kuwa].
Kwa maana Nafsi ya Baba mbali,
Nafsi mwana mbali [nafsi tofauti],
Na nafsi ya Roho mtakatifu mbali [nafsi tofauti].
Bali uungu [uungu, asili ya uungu] wa baba,
na Mwana, na wa Roho Mtakatifu ni uungu mmoja,
Utukufu wao ni sawa Ukuu wao ni wa milele.
Kama alivyo Baba.
Ndivyo alivyo Mwana:
alivyo Roho Mtakatifu.
Baba hakuumbwa,
Mwana hakuumbwa,
Roho Mtakatifu hakuumbwa.
Baba hana mpaka [hawezi kupimwa],
Mwana hana mpaka,
Roho Mtakatifu hana mpaka.
Baba ni wa milele,
Mwana ni wa milele,
Roho Mtakatifu ni wa milele.
Walakini hakuna watatu walio wa milele;
Bali mmoja aliye wa milele.
Kadhalika hakuna watatu wasioumbwa,
wala watatu wasio na mpaka:
Bali asiyeumbwa ni mmoja tu,
na asiye na mpaka ni mmoja tu.
Kadhalika Baba ni Mwenyezi,
Mwana Mwenyezi,
Na roho Mtakatifu Mwenyezi.
Walakini hakuna watatu walio wenyezi:
Bali aliye Mwenyezi ni mmoja tu.
Vivyo hivyo baba ni Mungu,
na Mwana ni Mungu:
Na roho Mtakatifu ni Mungu.
Walakini hakuna mungu watatu:
Ila aliye Mungu ni mmoja tu.
Vivyo hivyo Baba ni Bwana,
na Mwana ni Bwana:
Na Roho Mtakatifu ni bwana.
Walakini hakuna Mabwana watatu.
bali Bwana ni mmoja.
Kwa maana kama tunavyoshurutisha kwa kanuni ya kweli ya kikristo:
Kukiri ya kuwa kila nafsi ni Mungu na Bwana.
Kadhalika tunagombezwa na imani katholiko:
tusiseme ya kuwa wako miungu mitatu, au mabwana watatu.
Baba hakuumbwa kwa aliye yote: hakuhulukiwa wala kuzaliwa.
Mwana anatoka katika baba tu: hakuumbwa:
wala hakuhulukiwa: bali yu mwana wa azali.
Roho mtakatifu anatoka katika baba na mwana:
Hakuumbwa,wala hakuhulukiwa, wala hakuzaliwa;bali anatoka.
Basi yupo Baba mmoja tu, si baba watatu;
yupo Mwana mmoja tu, si mwana watatu:
yupo Roho Mtakatifu mmoja tu,
si roho watakatifu watatu.
Na katika utatu huu
hapana aliye wa kwanza na aliye wa baadaye:
Hapana aliye mkuu zaidi na aliye mdogo.
Bali nafsi zote tatu ni wa milele: Wa sawa wote.
Basi, katika mambo yote kama tulivyokwisha kusema:
Imetupasa kuuabudu Umoja katika Utatu,
na Utatu katika umoja.
Kwa hiyo yeye atakae kuokoka:
Na aone hivyo juu ya utatu.
Na zaidi ya hayo, ili apate wokovu wa milele:
imempasa kuamini kwa moyo kufanyika mwili kwake
Bwana wetu Yesu Kristo.
Na imani kamili ndo hii:
Tuamini na kukiri ya kuwa Bwana wetu Yesu Kristo,
Mwana wa Mungu na Mwanadamu.
Yu Mungu, ana uungu [asili/dutu] wa baba,
Yu Mwana Kabla ya zamani zote;
Ni mwanadamu ana utu [asili/dutu] wa mama yake,
alizaliwa katika ulimwengu;
Mungu kamili na Mwanadamu:
Ana Roho yenye akili na mwili wa kibinadamu;
Yu sawa na baba kwa kuwa ni Mungu.
Yu chini ya baba kwa kuwa ni mwanadamu.
Na ijapokuwa yu Mungu tena mwanadamu,
yeye si wawili; bali ni Kristo mmoja.
Yeye ni mmoja,
si kana kwamba uungu umebadilika uwe mwili
bali kwa kuutwaa utu wa mwanadamu na kuunga na mungu.
Mmoja kabisa ,
si kwa kuuchanganya uungu na utu,
bali kwa kuwa nafsi moja tu.
Kwa maana kama vile nafsi yenye akili pamoja na mwili huwa mwanadamu mmoja.
Kadhalika mungu na mwanadamu pamoja ni Kristo mmoja.
Aliyeteswa kwa wokovu wetu;
Akashuka mahali pa wafu;
akafufuka siku ya tatu;
Akapa mbinguni;
ameketi mkono wa kuume wa Baba Mungu Mwenyezi;
Kutoka huko atakuja kuwahukumu waliohai na waliokufa.
Naye atakapokuja, wanadamu wote watafufuliwa na miili yao [katika mwili]
na watatoa habari ya matendo yao
Nao walitenda mema wataingia katika uzima wa milele,
na waliotenda mabaya katika moto wa milele.
Hii ndio imani katholiko:
ambayo mtu asiposadiki kwa uaminifu hawezi kuokoka.
Somo la 3 Mazoezi
(1) Zoezi la Kifungu: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu na kuandika aya kuhusiana na somo la somo hili.
Yohana 17:1–5
Waefeso 1:3–14
Waefeso 1:15–23
Wakolosai 1:9–19
Waebrania 1
(2) Jaribio: Utaanza kipindi kijacho cha darasa kwa jaribio juu la Somo 3. Jifunze kwa umakini maswali wakati wa maandalizi.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kuripoti muda wako wa kufundisha nje ya darasa.
(4) Kwa umakini soma Tamko la Imani la Athanasi hapo juu.
Somo la 3 Jaribio
(1) Ni nini jibu zuri la swali “Mungu ni nani?”
(2) Ni kwa namna gani fundisho la Utatu Mtakatifu linafanya maombi yetu kuwa ya kina?
(3) Ni matukio gani makubwa mawili ya Agano Jipya ambayo kupitia hayo Mungu alijifunua mwenyewe kama Utatu Mtakatifu? Ni nafsi gani ya Utatu iliyofunuliwa katika kila moja?
(4) Je, Mungu ni kama yai? Kwa nini ndiyo au siyo?
(5) Je, Mungu ni kama mwanadamu mwenye mavazo au wajibu tofauti tofauti? Kwa nini ndiyo au siyo?
(6) Kwa nini nafsi ya kwanza na ya pili ya Utatu Mtakatifu inaitwa “Baba” na “Mwana”?
Free to print for ministry use. No changes to content, no profit sales.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom.