► Someni Ufunuo 5:11-14 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu Yesu?
Makristo wa Uongo
Biblia inatabiri kwamba katika siku za mwisho, makristo wa uongo na manabii wa uongo watadanganya wengi. Watu wengi wanaweka imani yao katika makristo wa uongo au wa kjibunia ambao hawawezi kuwaokoa. Huenda ukakutana na wawili kati ya makristo hao wa uongo, waliotambulishwa kwako na Wamormoni na Mashahidi wa Yehova.
Yesu wa Wamormoni
Ikiwa Mormoni atabisha hodi kwenye mlango wako, atamletea Yesu ambaye ni ndugu wa kiroho wa Lusifa. Wamormoni wanafundisha kwamba huyu Yesu ni mmoja wa mabilioni
ya watoto wa kiroho ambao “Baba yetu wa Mbinguni” na “Mama yetu wa Mbinguni” waliwaleta katika ulimwengu huu. Kulingana na Wamormoni, Yesu alipoishi duniani, alikuwa na wake kadhaa, mmoja wao akiwa Maria Magdalene. Baada ya kifo na ufufuo wake, alienda Amerika kuwahubiria Wenyeji wa Amerika.
Yesu wa Mashahidi wa Yehova
Mashahidi wa Yehova watakuambia kwamba Yesu ni Malaika Mkuu Mikaeli, kiumbe wa kwanza aliyeumbwa, ambaye alifanywa akawa mwanadamu na akafa kwenye nguzo badala ya msalaba. Alifufuliwa kama kiumbe wa kiroho, akawa Malaika Mkuu Mikaeli tena, huku mwili wake ukiyeyushwa na kuwa gesi.
Yesu wa Kweli
Nina hakika unatambua kwamba madhehebu haya potovu yana Yesu ambaye ni tofauti na Yesu wa Biblia, lakini, je, unaweza kueleza jinsi Yesu wa kweli, wa Biblia, alivyo? Mamilioni ya watu wana dhana ya kiakili ya Kristo wa uongo, ambaye hawezi kuwaokoa.
Ni muhimu kwako kuwa na uhakika na yale unayoamini juu ya Yesu ili usidanganywe, na hivyo unaweza kumtambulisha kwa wengine.
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Kwa habari zaidi kuhusu kile ambacho dini zingine zinafundisha kuhusu Yesu, tazama sehemu iliyo mwishoni mwa somo hili yenye kichwa “Kile Ambacho Dini Zingine Zinasema.”
Yesu Masihi
► Je, baadhi ya tabiri za Biblia kuhusu Masihi ni zipi?
Injili nne zinamwonyesha Yesu kama Masihi aliyetarajiwa wa Israeli. Mambo kadhaa yalitabiriwa kuhusu Masihi. Atakuwa mzao wa Mfalme Daudi na hivyo atastahili kuwa mfalme. Atawaokoa watu wake kutokana na ukandamizaji na utumwa. Atatiwa mafuta maalum na Mungu ili kutimiza utume wake. Neno Masihi linamaanisha “Mtiwa-Mafuta” ambalo lilikuwa jina la heshima la wafalme katika nchi ya Israeli.
[1]Baadhi ya maelezo muhimu zaidi kuhusu Masihi katika Agano la Kale hayakuelezwa kwa uwazi hadi wakati Agano Jipya lilipoandikwa. Kipaumbele chake kilikuwa kuwakomboa watu wake kutokana na dhambi. (Soma Mathayo 1:21; Luka 1:74-75.) Ufalme wake haukuwa wa kidunia, bali wa kiroho na wa mbinguni (soma Yohana 18:36), Hata hivyo, hatimaye ufalme wake utaenea katika dunia yote (Wafilipi 2:10-11; Ufunuo 19:11-16; Ufunuo 20:6).
Neno Masihi ni neno la Kiebrania. Neno la Kigiriki lenye maana sawa ni Christos, ambalo linatupatia neno Kristo. Kutumia kirai “Yesu Kristo” ni kusema kwamba Yesu ndiye Masihi.
Yesu ni Bwana
Kanisa la awali lilitumia neno Bwana kumaanisha kwamba Yesu ndiye mwenye mamlaka makuu zaidi ambaye mtu lazima ajinyenyekeze kwake. Waliposema “Yesu ni Bwana,” walikuwa wakimaanisha kwamba yeye ni Bwana wa wote, Muumba na Mungu wa ulimwengu wote. Kauli hii ya imani iliwatofautisha Wakristo na wengine, kwa sababu ni Wakristo pekee ndio walioamini kwamba mwanadamu Yesu ambaye alitembea duniani pia ndiye Mungu mmoja juu ya wote.
Maneno “Bwana Yesu Kristo” yanatoa kauli kuu. Yanasema kwamba Yesu ndiye Masihi na kwamba yeye pia ni Mungu. Maneno yote matatu yako katika Wafilipi 2:10-11. Kifungu hicho kinatuambia kwamba wakati utafika ambapo kila mtu ulimwenguni atalazimika kukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana.
Siku Tatu Maalum
Kanuni zetu za msingi kuhusu Yesu zinaweza kugawanywa katika vikundi vitatu, vinavyohusiana na siku tatu maalum.
mwenye umungu mmoja na Baba; ambaye vitu vyote vimeumbwa naye.”
Kanuni ya Imani ya Nisea
Tunasherehekea Krismasi kwa sababu ya Umwilisho
Krismasi husherehekea kuzaliwa kwa Yesu na mama bikira, kwa maana Yesu alichukuliwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. (Soma Luka 1:34-35.) Ingawa Yesu alikuwa mwanadamu kwa sababu alizaliwa na mwanamke, yeye pia ni Mungu mwenyewe, Muumba wa ulimwengu alioingia. Hili ni jambo la ajabu lakini ni kweli: Yesu alipokuwa mtoto, mama yake Maria alimshika yule ambaye alimuumba.
Neno wana wa Mungu linatumika kwa waumini na malaika (Yohana 1:12; Ayubu 1:6), lakini Yesu ni Mwana wa Mungu kwa njia ya kipekee (Yohana 3:16). Yeye ndiye kiumbe pekee aliye na asili kama ya Baba kikamilifu. Yeye ni mfano kamili wa Baba kiasi kwamba yeye ni Mungu kama vile Baba alivyo. (Soma Waebrania 1:2-3.)
Asili ya Mungu na asili ya mwanadamu zilikuja pamoja katika nafsi ya Yesu. Huu unaitwa umwilisho, ambayo inamaanisha Mungu kuchukua mwili wa mwanadamu, na kuwa
mwanadamu. Yesu pekee ndiye angeweza kuwa Mwokozi wetu kwa sababu yeye ndiye mtu pekee katika ulimwengu ambaye ni mwanadamu na Mungu.
Yesu ni Mwanadamu
Si vigumu kumtambua Yesu wa Agano Jipya kama mwanadamu halisi. Alitungwa mimba katika tumbo la mama, akakua, akajifunza, na akakomaa kama mtu. (Soma Luka 2:52.) Alichoka, alilala, alijaribiwa, na alifanya karibu kila kitu ambacho wanadamu hufanya, isipokuwa dhambi (Waebrania 4:14-15). Hata alikufa. Kwa kweli alijitambulisha na jamii ya wanadamu kwa kuwa mmoja wetu. (Soma Yohana 1:14.)
► Je, kwa nini ni muhimu kwamba Yesu ni mwanadamu?
Kwa sababu Yesu ni mwanadamu:
1. Angeweza kuteseka na kufa kama dhabihu (Waefeso 5:2, Waebrania 7:26-27). Ikiwa angekuwa Mungu lakini si mwanadamu, hangeweza kuteseka kimwili na kufa.
2. Haki yake inaweza kutufanya tuwe wenye haki na kutupa uzima. Adamu wa kwanza aliwakilisha wanadamu wote alipofanya dhambi na kutenganishwa na Mungu. Tukio hilo ilileta mauti kwa watu wote. Yesu aliishi maisha yasiyo na dhambi na alitimiza matakwa yote ya Mungu. Anawapa uzima wa milele wote wanaojitambulisha naye. Anaitwa Adamu wa mwisho katika maandiko (1 Wakorintho 15:22, 45-49; Warumi 5:17-19).
3. Anaweza kuwa kuhani wetu anayetuwakilisha mbele za Mungu. Akiwa mpatanishi wetu, hazungumzi tu kwa niaba yetu, bali pia anatuwakilisha kikweli. Ilikuwa ni lazima kwake kuwa mwanadamu ili kuleta upatanisho kati yetu na Mungu. (Waebrania 2:17.) Jukumu lake kama kuhani linatoa wokovu wa milele (Waebrania 5:9, Waebrania 10:5-7). Ubinadamu wa Yesu ni sehemu muhimu ya injili. (Soma 1 Yohana 5:1.)
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Kwa ushahidi zaidi wa Biblia kwamba Yesu alikuwa mwanadamu, tazama sehemu ya “Uthibitisho wa Kimaandiko wa Ubinadamu wa Yesu” mwishoni mwa somo hili.
Yesu ni Mungu
Yesu alidai kuwa Mungu.
[1]Yesu wa Biblia ni mwanadamu lakini si mwanadamu tu. Yeye pia ndiye Mungu mmoja asiye na kikomo wa ulimwengu. Yesu alitoa dai hili mwenyewe. Alisema, “Mimi na Baba tu umoja” (Yohana
10:30). Aliposema hivyo, Wayahudi walianza kumpiga mawe kwa sababu walielewa kuwa alisema kwamba yeye ni sawa na Mungu. Je, Yesu aliwaambia, “Hapana, hamkunielewa. Mimi si Mungu kikweli!”? Hapana, Yesu alikubali ufasiri wao wa maneno yake. Alifundisha kwamba alikuwa sawa na Mungu Baba.
Yesu aliposema, “Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko,” (Yohana 8:58) alikuwa anadai kuwa yeye ni MIMI NIKO wa Kutoka 3:14, Mungu wa ulimwengu ambaye hakuumbwa. Wayahudi walijaribu kumpiga mawe kwa sababu ya dai hilo pia (Yohana 8:59).
Yesu alifanya matendo ya kiungu alipokuwa duniani.
Yesu alifanya matendo ya kiungu alipokuwa duniani. Alitoa uzima wa milele. (Soma Yohana 10:28.) Alisamehe dhambi (Marko 2:10). Haya ni mambo ambayo Mungu pekee ndiye anayeweza kufanya.
Yesu aliposamehe dhambi za yule mtu aliyepooza, alimponya mtu huyo ili kuthibitisha kwamba alikuwa na mamlaka duniani ya kusamehe dhambi (Marko 2:5, 10-12). Tendo moja lilikuwa thibitisho la lingine, likionyesha wazi kwamba Yesu hakuwa amefanya muujiza wa uponyaji kama tu nabii aliyetiwa mafuta na Mungu. Yesu alikuwa na mamlaka na uwezo wa kiungu wa kusamehe na kuponya pia.
Yesu pia alimfufua Lazaro baada ya kusema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima” (Yohana 11:25). Hili lilikuwa ni tendo lingine la kiungu lililoambatana na dai la kiungu. Mungu pekee ndiye anayeweza kudai kwa haki kuwa yeye ndiye Ufufuo kwa sababu ni nguvu ya Mungu pekee ndio inayoweza kumfufua mtu kutoka kwa wafu. Yesu alidai kuwa mwenye kutoa Uhai kisha akampa Lazaro uhai, akionyesha kwamba yeye ni Mungu kama alivyodai. Katika tukio hili, Yesu alijitofautisha kwa uwazi na manabii wengine na mitume waliofufua watu kutoka kwa wafu kwa uwezo wa Mungu. Hakuna hata mmoja wao aliyedai kuwa na uwezo ndani yake mwenyewe wa kufanya miujiza. Walikuwa tu vyombo vya Mungu. Katika Yohana 5:21, Yesu alisema kwamba yeye huwafufua wafu kama vile Baba huwafufua wafu.
Yesu alipofanya miujiza yake, alidhihirisha utukufu wake, (Yohana 2:11) utukufu wa Mwana pekee aliyetoka kwa Baba, amejaa neema na ukweli (Yohana 1:14). Miujiza hiyo ilikuwa madhihirisho ya nguvu tukufu za Mungu Mwana, ikithibitisha kwamba alikuwa na asili ya uungu.
Yesu ni Muumba na Mhimili.
Kulingana na Mitume Yohana na Paulo, Yesu aliumba kila kitu na anashikilia kila kitu pamoja, na kila kitu kipo kwa ajili yake. (Soma Yohana 1:3; Wakolosai 1:17.) Hakika hayo hayangeweza kusemwa juu ya yeyote ila Mungu.
► Je, kwa nini ni muhimu kwetu kujua kwamba Yesu ni Mungu?
Kwa sababu Yesu ni Mungu,
1. Kifo chake kama dhabihu kina thamani isiyo na kikomo — kimetosha kwa ajili ya msamaha wa dhambi za ulimwengu (1 Yohana 2:2).
2. Ana uwezo wa kutuokoa; yeye ndiye njia, kweli na uzima (Yohana 14:6).
3. Ni lazima tumwabudu kama tunavyomwabudu Baba (Soma Yohana 5:23).
Tukikosa kumwona Yesu kama Mungu, hatutamheshimu kama Mungu. Hatuwezi kuokolewa ikiwa hatuheshimu Baba na Mwana kama Mungu.
Msingi wa Ukristo si mafundisho na matendo ya Yesu pekee, bali pia nafsi ya kipekee ya Yesu. Yeye si tu mwalimu wa ujumbe wa wokovu. Yeye mwenyewe ndiye Mwokozi, na ni yeye tu—Mungu-mwanadamu— ndiye angeweza kuwa Mwokozi.
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Kwa ushahidi zaidi wa Biblia kwamba Yesu ni Mungu, tazama sehemu ya “Uthibitisho wa Kimaandiko wa Uungu wa Yesu” mwishoni mwa somo hili.
Yesu ni Nafsi Moja
Ingawa Yesu ana asili yote ya Mungu na asili yote ya mwanadamu, yeye si nafsi mbili zilizowekwa pamoja. Asili hizo mbili zinaunda nafsi moja ndani yake, zikiwa na upatano kamili. Yesu ndiye Mungu-mwanadamu mmoja, na kila tendo la Yesu linapaswa kueleweka kwa mtazamo wa ubinadamu wake kamili na uungu wake kamili. Kanisa siku zote limefundisha kwamba asili mbili ndani ya Yesu haziwezi kutenganishwa, hata hivyo hazijachanganyika kwa njia ambayo inasababisha asili yoyote ipoteze sifa zake.[2]
Huenda ikasaidia kulinganisha asili ya Yesu na asili ya Maandiko Matakatifu. Kama Yesu, Biblia ni ya kiungu kikamilifu na ni ya kibinadamu kikamilifu. Kikiwa kitabu cha kibinadamu, kina sifa za kitabu chochote kingine cha kibinadamu, isipokuwa haina makosa. Kwa kuwa ni ya kitabu cha kiungu, kinaonyesha sifa ambazo hakuna kitabu kingine kinaweza kuonyesha. Vivyo hivyo, Yesu anaonyesha sifa za kibinadamu na za kiungu. Ukweli kwamba Biblia inaonyesha sifa za kiungu hauondoi sifa yake kama kitabu cha kibinadamu. Vivyo hivyo, ukweli kwamba Yesu anafanya kazi katika uungu wake hauondoi ubinadamu wake. Na ukweli kwamba Yesu anafanya kazi katika ubinadamu wake hauondoi uungu wake.
Makosa ya Kikanuni Yanayojitokeza Sana
Makosa ya kikanuni yanayofanywa sana na watu wanapozungumza kuhusu Kristo ni haya:
Kukana kwamba Yesu ni Mungu
Kukana kwamba Yesu ni mwanadamu
Kupunguza uungu wake au ubinadamu wake kana kwamba si muhimu
Kuukana umoja wa nafsi ya Kristo
Yoyote kati ya makosa haya ni kuukana umwilisho. Umwilisho ulihitajika kwa ajili ya wokovu wetu, hivyo ikiwa mtu anakana umwilisho ataamini injili ya uongo na njia ya uongo ya wokovu.
“Kama vile Baba anavyotumia usemi huu MIMI NIKO, Kristo pia anautumia, kwani unamaanisha uwepo unaoendelea, usiyoathiriwa na wakati.”
John Chrysostom
[2]Kanuni ya Imani ya Chalsedonia (451 B.K.), ambayo imejumuishwa katika Somo la 15, inasema kwamba asili mbili za Kristo hazibadiliki, hazigawanyiki, hazitenganishwi, na hazina mkanganyo.
Kile Ambacho Dini Zingine Zinasema
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshiriki wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Mashahidi wa Yehova wanasema kwamba Yesu alikuwa mwanadamu. Wanaamini kwamba alikuwa mtu mkuu zaidi aliyewahi kuishi, lakini bado ni mwanadamu tu. Ndio maana hawaamini kwamba kifo chake ni dhabihu tosha kwa ajili ya wokovu wetu. Wana injili ya wokovu kwa matendo. Wanadai kuwa Wakristo, lakini wao ni dini tofauti.
Wamormoni wanaamini kwamba Yesu awali alikuwa roho aliyeumbwa na Mungu, kama ndugu wa Lusifa. Alitumwa ili azaliwe duniani akiwa mwanadamu Yesu. Wamormoni hawaamini kwamba Yesu ni Mungu.
Waislamu wanaamini kwamba Yesu alikuwa nabii aliyetumwa na Mungu. Hawaamini kwamba yeye ni Mungu au kwamba kuna Utatu wa Mungu. Hawaamini kwamba alisulubiwa au alifufuka kutoka kwa wafu.
Wahindu na Wabudha wanaamini kwamba Yesu alikuwa mtu mtakatifu ambaye alifanya miujiza. Hana umuhimu katika dini zao. Hawamwamini Mungu ambaye ni Muumba na Bwana, kwa hivyo hawaamini kwamba Yesu ni umwilisho wa Mungu.
Tunasheherekea Ijumaa Kuu kwa sababu ya Upatanisho
Ijumaa Kuu ni siku ambapo Yesu alisulubiwa. Katika siku hii ya kuogofya na ya ajabu, Yesu alipeleka dhambi zetu msalabani. Alikufa kama dhabihu kwa ajili ya dhambi zetu ili sisi tupate kusamehewa.
Dhabihu Ilihitajika
Dhabihu ilihitaji kutolewa ili Mungu aweze kutusamehe na bado abaki kuwa mwenye kuzingatia haki na mtakatifu. Kanuni hii ilifundishwa katika Agano la Kale kupitia dhabihu ambazo Mungu alihitaji (Waebrania 9:22). Ikiwa Mungu angesamehe tu dhambi bila msingi wowote, hiyo ingeonyesha kwamba yeye si mwenye kuzingatia haki na kwamba dhambi si jambo zito sana. Lakini hakuna mtu angeweza kutazama kifo cha Yesu kwa kusulubiwa na kusema kwamba dhambi si mbaya. Kujitoka kwake kama dhabihu yake kulitoa msingi wa msamaha wetu.
Yesu Pekee Ndiye Angeweza Kuwa Dhabihu ya Kutosha
► Kwa nini Yesu pekee ndiye angeweza kuwa dhabihu ya dhambi?
Haki ya Mungu na uzito wa dhambi ulihitaji dhabihu kubwa kuliko kitu chochote kilichoumbwa. (Soma Waebrania 10:4.) Tumetenda dhambi dhidi ya Mungu asiye na kikomo, jambo linalotuletea hatia isiyo na kikomo. Ndio maana Yesu pekee ndiye angeweza kuwa dhabihu. Alistahili kwa sababu yeye ni Mungu na kwa sababu yeye ni mwanadamu. Kwa sababu ya uungu wake, hakuwa na dhambi, na kujitoa kwake kama dhabihu kulikuwa na thamani isiyo na kikomo. Kwa sababu ya ubinadamu wake, angeweza kutuwakilisha na kufa kwa niaba yetu.
Damu ya Yesu Inawakilisha Kifo chake cha Kujitoa kama Dhabihu
Mungu aliwafundisha watu kuhusu upatanisho kwa kuanzisha utoaji dhabihu. Makuhani walichinja wanyama na kutoa damu yao kuwakilisha kifo cha wanyama hao. Kitabu cha Waebrania kinasema kwamba pasipo kumwaga damu hakuna msamaha wa dhambi (Waebrania 9:18-22).
Mungu aliwaamuru watu washughulikie damu kwa njia maalum kwa sababu iliwakilisha uhai wa kiumbe (Mambo ya Walawi 17:11, 14). Kumwaga damu kulimaanisha kuua (Mwanzo 9:5-6). Damu iliyotumika Hekaluni ilimaanisha kwamba mnyama alikuwa ameuawa.
Kifo cha Kristo kilikuwa dhabihu kuu zaidi ambayo ilifanya wokovu upatikane kwa kila mtu wakati wote. (Soma Waebrania 10:4, 12.) Aliwasilisha damu yake mbinguni ili kuwakilisha kifo chake cha kujitoa kama dhabihu. (Soma Waebrania 9:12, 24.) Damu ya Yesu, ikiwakilisha kifo chake, inatoa wokovu kwa sababu alikufa kama dhabihu ili tupate kuokolewa.
Kwa nini Yesu alikufa msalabani badala ya kufa kwa njia nyingine? Katika enzi ya Agano la Kale, mtu kutundikwa kwenye mti kulikuwa ni ishara ya laana ya Mungu (Kumbukumbu la Torati 21:23). Mtume Paulo anatuambia kwamba Yesu alijitwika laana ya Mungu kwa kusulubiwaa kwenye mti (Wagalatia 3:13).
Yesu Alipatanisha Mungu na Mwanadamu
Yesu alikuja kupatanisha pande mbili zilizotengana — Mungu na mwanadamu. Kama mpatanishi, Yesu alipaswa kuwakilisha pande zote mbili kwa wakati mmoja. Kama Mungu, alimwakilisha Mungu kwa mwanadamu. Kama mwanadamu, alimwakilisha mwanadamu kwa Mungu. Kwa kuwakilisha pande zote mbili kikamilifu, Yesu alipatanisha mwanadamu na Mungu. Alifanya kile ambacho kila upande ulipaswa kufanya ili kuleta upatanisho.
Tunasherehekea Pasaka kwa sababu ya Ufufuo
Kuna njia nyingi za kitamaduni za kusherehekea Pasaka, lakini watu wengi hawatambui maana ya mambo wanayofanya, na huenda hawajui ni nini lililo muhimu kuhusu ufufuo wa Yesu. Yesu alifufuka kutoka kaburini asubuhi ya Pasaka, siku ya tatu baada ya kusulubiwa. Alionyesha kwamba ana nguvu ya kushinda dhambi, mauti na ibilisi. Hakujitwika tu kifo chetu tu, bali pia alikishinda kwa uzima. Kwa sababu alishinda, sisi pia tunaweza kushinda!
Yesu Alifufuka Kimwili
Kuna wakati Yesu aliwaambia Wayahudi, “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.” Ingawa Wayahudi walifikiri kwamba alikuwa akimaanisha hekalu ambalo Herode alijenga, Injili ya Yohana inaeleza kwamba Yesu alikuwa anazungumzia mwili wake (Yohana 2:19-21). Injili zote zimerekodi ukweli kwamba kaburi la Yesu lilikuwa tupu siku tatu baada ya yeye kuzikwa humo. Yesu aliwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake, akisema, “Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo” (Luka 24:39). Alikuwa anathibitisha kwamba alikuwa amefufuka kimwili kutoka kwa wafu.
► Je, ingeleta tofauti gani kama Yesu hangefufuka kutoka kwa wafu?
1. Ufufuo wa Yesu kimwili ulionyesha ushindi wake kamili dhidi ya dhambi na mauti. (Soma Wakolosai 2:12-15; Ufunuo 1:17-18.)
2. Ufufuo wa Yesu kimwili ulithibitisha kwamba alikuwa kile alichodai kuwa (Mathayo 17:22-23, Yohana 2:16-22). Hivyo, tukio hilo pia lilithibitisha injili. Watu wanaokana kwamba Yesu alifufuka kutoka kwa wafu pia wanakana injili. (Soma 1 Wakorintho 15:17.)
3. Ufufuo wa Yesu unatuhakikishia kwamba sisi pia tutafufuliwa kutoka kwa wafu. Yesu aliahidi kwamba atawafufua wafu. Ahadi hiyo isingeaminika isipokuwa yeye mwenyewe afufuke (Yohana 5:28-29). Tutafufuliwa kuwa na miili kama mwili wa Yesu uliotukuzwa. (Soma 1 Yohana 3:2.)
Yesu Bado Ni mwanadamu
Ufufuo unatuonyesha kwamba umwilisho ni hali ya kudumu. Yesu daima atakuwa mwanadamu na pia Mungu. Yesu, ambaye bado ni Mungu-mwanadamu, sasa anatuombea mbele za Baba (Warumi 8:34), na siku moja atarudi kutupeleka mbinguni (1 Wathesalonike 4:16-17).
Tunajisalimisha kwa Yesu kwa sababu ya Yeye Ni Nani na Kile Alichofanya
Kama waumini, tunaishi katika uhusiano wa kila siku na Kristo. Yeye si mtu wa kihistoria tu, wala si Mungu aliye mbinguni tu, bali yuko pamoja nasi. Aliahidi kuwa pamoja na wanafunzi wake daima (Mathayo 28:20).
Yuko kanisani kwa namna maalum. Yeye ndiye kichwa cha kanisa, na kanisa linaitwa mwili wake (Waefeso 1:22-23). Analiongoza kanisa, analishikilia pamoja, na kukidhi mahitaji yake. (Soma Wakolosai 2:19.)
Mtu anayekubali ukweli kuhusu Yesu anapaswa kuliitikia kwa imani na utiifu. Unaweza kuwasaidia wengine kuwa waumini kwa sala kama hii hapa chini.
Baba, nakushukuru kwa kunipenda vya kutosha ili kumtuma Mwanao Yesu duniani kwa ajili yangu. Ninaamini kwamba Yesu ni Mungu-mwanadamu asiye na dhambi ambaye alikufa na kufufuka ili niweze kusamehewa dhambi zangu na kurejeshwa katika uhusiano na wewe. Naomba msamaha kwa dhati kwa ajili ya dhambi zote nilizotenda. Najua kwamba dhambi zangu zilimsulubisha Yesu msalabani. Sasa, ninajitenga na kila kitu ninachojua si sahihi, na ninampokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wangu. Niongoze kuanzia sasa. Nitaishi kwa ajili yako milele! Asante kwa kunisamehe. Nakupenda. Amina.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Yesu ndiye Masihi na Bwana wa wote, Mwana wa Mungu aliyezaliwa na bikira, akiwa na asili ya kibinadamu kikamilifu na asili ya kiungu kikamilifu katika nafsi moja. Aliishi maisha yasiyo na dhambi na akafa kama dhabihu ili dhambi zetu ziweze kusamehewa. Alifufuka kutoka kwa wafu na atawafufua waumini wote atakaporudi. Ufalme wake ni wa ulimwengu wote na hauna mwisho.
Uthibitisho wa Kimaandiko wa Ubinadamu wa Yesu
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Sehemu hii na sehemu inayofuata ni za hiari. Wanafunzi wanaweza kuzizingatia ikiwa wanataka uthibitisho zaidi wa kibiblia kuhusiana na hoja hizi.
Yesu alikuwa mzao wa Hawa (Mwanzo 3:15), mzao wa Abrahamu (Mwanzo 22:18 - linganisha na Matendo 3:25), aliyezaliwa na mwanamke (Wagalatia 4:4), aliyezaliwa na Mariamu (Mathayo 1:21 -25), aliyeitwa Mwana wa Adamu (Mathayo 13:37), na alipitia mchakato wa kawaida wa kukomaa (Luka 2:40, 52).
Aliporudi katika mji wake wa nyumbani, itikio la watu linaonyesha kwamba utoto wake ulikuwa wa kawaida (Mathayo 13:54-56).
Alikuwa na mwili ili aweze kutii jinsi mwanadamu anavyopaswa kutii (Waebrania 10:5-9); alifanyika mwili na damu (Waebrania 2:14); aliumbwa kama sisi ili apate kuteseka kama sisi (Waebrania 2:10-18); alifanywa kuwa kamili kwa njia ya mateso (Waebrania 2:9-10); na alipitia majaribu ya wanadamu (Waebrania 4:15).
Alichukua mfano wa mwanadamu (Wafilipi 2:6-8).
Alikuwa Neno la milele la Mungu na alifanyika mwili na kuishi duniani (Yohana 1:14).
Ubinadamu wa Yesu ni kauli muhimu ya imani ya Kikristo (Yohana 1:14; 1 Yohana 4:2-3).
Uthibitisho wa Kimaandiko wa Uungu wa Yesu
Yesu anathibitishwa kuwa Mungu kwa njia tatu:
1. Anaitwa Mungu.
2. Anaonyeshwa kuwa na sifa za Mungu.
3. Anaonyeshwa katika majukumu ya Mungu.
Yesu anaitwa Mungu
Yohana 1:1, 14, inasema kwamba Neno la milele ni Mungu.
Yohana 12:41 inatuambia kwamba Isaya alimwona Yesu.
Matendo 20:28 inasema kwamba kanisa la Mungu lilinunuliwa kwa damu yake mwenyewe.
Warumi 9:5 inasema kwamba Kristo alikuja, ambaye ni Mungu mwenye kuhimidiwa milele.
Tito 2:13 inamtaja kuwa Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Mathayo 1:23 (ikinukuu Isaya 7:14) inasema kwamba jina lake linamaanisha “Mungu pamoja nasi.”
Isaya 9:6 inasema kwamba ataitwa jina lake Mungu Mwenye Nguvu.
1 Timotheo 3:16 inasema kwamba Mungu alidhihirishwa katika mwili, akahubiriwa katika mataifa, na akachukuliwa juu katika utukufu.
Katika Yohana 10:30, 33, Yesu alisema kuwa yeye na Baba ni kitu kimoja.
Katika Yohana 5:17-18, Wayahudi walijua kwamba alisema yeye ni sawa na Mungu.
Katika Yohana 14:9 alisema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba.”
Katika Yohana 20:28-29, Tomaso aliona majeraha yake na akasema, “Bwana wangu na Mungu wangu,” kisha Yesu akawabariki wale wanaoamini.
Katika Yohana 8:58, Yesu alijiita MIMI NIKO, na Wayahudi walijua kwamba hilo likuwa dai kuwa yeye ni Mungu.
Katika Ufunuo 1:17, Ufunuo 2:8, na Ufunuo 22:13, Yesu alidai kuwa wa Kwanza na wa Mwisho, na Isaya 44:6 inaonyesha hilo lilikuwa jina la Mungu.
Waebrania 1:2-3 inatuambia kwamba yeye ni mfano kamili wa Baba.
Katika Waebrania 1:8, anaitwa Mungu.
Yesu Ana Sifa za Mungu
Yuko kila mahali. Katika Mathayo 18:20, Yesu alisema kwamba yuko mahali popote ambapo waumini wawili au watatu wanakutana. Katika Mathayo 28:20, aliahidi kwamba atakuwa pamoja na waumini daima.
Ana uwezo wote. Waebrania 1:3 inasema kwamba ameshikilia kila kitu kwa uwezo wake. Wafilipi 3:21 inasema kwamba ameweka vitu vyote chini yake.
Ni wa milele. Waebrania 13:8 inatuambia kwamba yeye ni yule yule milele. Waebrania 1:12 pia inasema kwamba yeye ni yeye yule yule milele. Kifungu hiki ni nukuu ya Zaburi 102:25-27 inayozungumza kuhusu Mungu.
Mjua yote. Yohana 2:24-25 inatuambia kwamba anawajua watu wote, na anajua yale yaliyo mioyoni mwao. Katika Yohana 10:15, alidai kwamba anamjua Baba jinsi Baba anavyomjua.
Yesu Ana Majukumu ya Mungu
Yesu ndiye Muumba (Wakolosai 1:16; Waebrania 1:10).
Yesu alisamehe dhambi (Luka 5:20-24, Luka 7:48).
Yesu atakuwa hakimu katika hukumu ya mwisho (Mathayo 25:31-46; 2 Wakorintho 5:10).
Yesu anaabudiwa kama Baba (Yohana 5:22-23; Waebrania 1:6; Ufunuo 5:12-13).
Mazoezi ya Somo la 7
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Marko 1:1-12
Yohana 5:19-26
Yohana 6:44-51
Yohana 8:51-59
Matendo 2:22-36
Ufunuo 1:12-18
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 7. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 7
(1) Je, kipaumbele cha Masihi kilikuwa kipi?
(2) Je, kanisa la awali lilimaanisha nini waliposema “Yesu ni Bwana”?
(3) Je, ni jinsi gani Yesu ni Mwana wa pekee wa Mungu?
(4) Je, umwilisho ni nini?
(5) Orodhesha sababu tatu zinazofanya iwe muhimu kwamba Yesu ni mwanadamu.
(6) Orodhesha sababu tatu zinazofanya iwe muhimu kwetu kujua kwamba Yesu ni Mungu.
(7) Je, ni sababu gani mbili zilizofanya dhabihu ihitajike?
(8) Je, kwa nini Yesu alikufa msalabani badala ya kufa kwa njia nyingine?
(9) Orodhesha sababu tatu zinazofanya ufufuo wa Yesu kimwili uwe muhimu.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.