► Someni Warumi 6 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu athari za wokovu?
Ushahidi wa Wokovu
Uhakikisho wa kibinafsi wa wokovu ni mojawapo ya mada kuu za waraka wa 1 Yohana. Yohana alieleza sababu yake ya kuandika waraka huu; “Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu” (1 Yohana 5:13).
► Je, mtu anapaswa kufanya nini ikiwa ana shaka kwamba ameokoka?
Mtume alijua kwamba kutakuwa na wakati ambapo muumini atahitaji hakikisho kwamba ameokoka. Anaonyesha kwamba muumini anafaa kutafuta ushahidi wa hakikisho lake. Katika waraka wake wote, anatoa mifano kadhaa ya ushahidi, akisema “hivi ndivyo
tunavyojua”.[1] Alisema kwamba waumini wanaweza kutumia ushahidi huo ili kutuliza mioyo yao (1 Yohana 3:19).
Tabia ya muumini ambayo imesisitizwa zaidi katika waraka wote wa 1 Yohana ni ushindi dhidi ya dhambi. Mtume anasema, “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi” (I Yohana 2:1). Kwa kauli hii, mtume anaonyesha kwamba muumini anapaswa kuishi maisha ya kuwa huru kutokana na dhambi ya makusudi.[2] Anaandika ili kuwaonyesha umuhimu wa kuishi kwa ushindi.
…Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote (1 Yohana 2:1-2).
Hapa Yohana anatambua kwamba dhambi inaweza kutokea, ingawa si lazima. Anatuhakikishia kwamba muumini akitenda dhambi, dhabihu ya Kristo inaweza kulipia dhambi hiyo. Hilo halimaanishi kwamba muumini anaweza kutenda dhambi tena na asemehewe moja kwa moja bila kutubu. Kifungu hiki kinasema kwamba dhabihu inapatikana, kwa vile ni ya ulimwengu wote na dhambi zote. Tunajua kwamba ulimwengu wote haujaokolewa moja kwa moja. Muumini akitenda dhambi, ni lazima atubu kwa ajili ya uhusiano wake na Mungu.
Vifungu vifuatavyo kutoka 1 Yohana vinaonyesha kwamba sifa bora zaidi ya muumini ni ushindi dhidi ya dhambi ya makusudi. Maneno yaliyo ndani ya mabano ni maoni ya kuongezwa.
Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. [Mtu asiyemtii Mungu hadhihirishi ushahidi huu]. Yeye asemaye, “Nimemjua,” wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake (1 Yohana 2:3-4).
Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua (1 Yohana 3:4-6).
Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki [Si mtu ambaye kwa namna fulani anahesabiwa haki huku akiendelea kutenda dhambi], kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi (1 Yohana 3:7-8).
Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu
(1 Yohana 3:9).
Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa. (1 Yohana 3:24). [Kukaa ndani ya Kristo hakuambatani na kuendelea kuvunja amri za Mungu.]
Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito (1 Yohana 5:2-3). [Upendo wa kweli huchochea utiifu. Kutotii kunaonyesha ukosefu wa upendo.]
Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu [majaribu yake na roho yake]; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu (1 Yohana 5:4).
Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi (1 Yohana 5:18).
► Ni sifa gani kuu ya muumini inayojitokeza wazi katika vifungu hivi?
Kutokana na vifungu hivi, inaonekana wazi kwamba sifa kuu ya muumini ni kwamba anaishi kwa kumtii Mungu. Ushindi dhidi ya dhambi ya makusudi ni fursa kubwa ya muumini.
[2]Dhambi ya makusudi imejadiliwa kwa kina katika Somo la 5.
Maelezo kuhusu 1 Yohana 1:8
Wakati mwingine watu wanaokana kwamba muumini anaweza kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi ya makusudi hunukuu 1 Yohana 1:8: “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.” Lakini maana ya kuwa na dhambi ni nini? Je, ina maana hata waumini wanaendelea kutenda dhambi kwa makusudi? Hilo haliwezi kuambatana na kauli zilizo katika 1 Yohana 3 ambazo zimenukuliwa hapo juu. Yohana angewezaje kusema maneno hayo katika sura ya 3 kama angesema hapo awali kwamba, “Kila mtu, ikiwemo kila muumini, huendelea kutenda dhambi”? Hilo halingeweza kuwa na maana.
Muktadha unaonyesha maana. Katika 1 Yohana 1:7, utakaso wa dhambi umeahidiwa. Utakaso huu ni kwa wale wanaotembea katika nuru, ambayo inamaanisha kuishi kulingana na ukweli, kwa kumtii Mungu. Wale ambao sasa wanaishi kwa kumtii Mungu wanatakaswa kutokana na dhambi zao za zamani kwa damu ya Kristo.
Lakini kunaweza kuwa na watu wanaokana kwamba wametenda dhambi na wanahitaji kutakaswa. Hao ndio wanaosema kuwa hawana dhambi na wanajidanganya. Wanadai
kwamba hawajawahi kamwe kutenda dhambi, au kwamba wametatua tatizo lao la dhambi bila Kristo.
Tena katika 1 Yohana 1:9, msamaha na utakaso vimeahidiwa. Katika 1 Yohana 1:10, Yohana anasema tena kwamba wale wanaosema kwamba hawajatenda dhambi wanampinga Mungu mwenyewe.
Yohana alikuwa anaandika ili kusahihisha kosa la wale ambao wanafikiri hawahitaji utakaso na msamaha unaotolewa na Kristo—wale wanaofikiri kwamba hawakuhitaji kuokolewa. Hakuwa akisema kwamba hata waumini wanaendelea kutenda dhambi, kwa kuwa hilo lingepingana na msisitizo wake mkuu na kauli za moja kwa moja katika waraka huu.
Neema ya Mungu kwa ajili ya Maisha ya Ushindi
Kuishi katika ushindi si rahisi siku zote kwa sababu ya upotovu wa kurithi na udhaifu wa kibinadamu. Kwa sababu ya hayo, watu wengi wanaamini kwamba haiwezekani kuishi bila kufanya dhambi ya makusudi. Lakini neema ya Mungu ina suluhu ya matatizo yote mawili.[1]
► Upotovu wa kurithi ni nini?
Upotovu wa kurithi ni upotovu wa asili ya kimaadili ya mwanadamu ambayo inamsukuma kutenda dhambi tangu anapozaliwa. Baada ya kuongoka, muumini hupambana na msukumo huo wa kutenda dhambi. Lakini Mungu hutoa neema si tu kwa ajili ya ushindi wa kila siku, bali kwa ajili ya utakaso wa upotovu wa kurithi (Matendo 15:9; 1 Wathesalonike 5:23; 1 Yohana 1:7).
Asili ya dhambi si hali ambayo lazima itutawale maisha yetu yote hapa duniani. Ili kuishi kwa ushindi, muumini anahitaji kufikia hatua ya kumkabidhi Mungu moyo wake kikamilifu (Warumi 12:1). Roho Mtakatifu anapomjaza muumini, anamwezesha muumini huyo kumpenda Mungu kikamilifu.
► Udhaifu wa kibinadamu ni nini?
Udhaifu wa kibinadamu ni mapungufu ya kimwili au kiakili. Kwa sababu ya anguko la Adamu katika dhambi, na kuzorota kwa hali ya wanadamu kupitia dhambi inayoendelea, sisi ni dhaifu kiakili, kimwili, na kihisia kuliko jinsi Mungu alivyotuumba kuwa.
Udhaifu wa kibinadamu hutufanya tufanye makosa. Huenda tusijue jambo sahihi la kufanya katika hali fulani. Huenda tukawa na maoni yasiyo sahihi kuhusu watu wa matabaka fulani au makabila fulani. Mawazo potovu hayarekebishwi moja kwa moja mtu anapookolewa. Mawazo potovu husababisha matendo mabaya kwa sababu mtu akiwa na wazo potovu kuhusu kile anachopaswa kufanya, atafanya jambo baya.
Udhaifu unaweza kusababisha mtu awe na matatizo kwa sababu kadhaa. Labda hajajifunza jinsi ya kutumia kanuni za kimaandiko. Labda hajakuza nidhamu ambazo zingemsaidia kupinga misukumo yake. Labda hana tabia za kila siku ambazo zingemsaidia kuwa na nguvu. Labda haelewi umuhimu wa kuenenda katika Roho.
Hatupaswi kuwa wepesi kuwahukumu wengine, kwa sababu hatuwezi kujua wakati wote wakati wanapofanya dhambi kwa makusudi. Mara nyingi watu hufanya makosa kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu na ukomavu wa kiroho.
Je, umewahi kukabiliwa na jaribu ambalo ulifikiri hakuna mtu mwingine amewahi kukabiliwa nalo? Je, umewahi kujiuliza kama kweli inawezekana kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi kikamilifu? Mungu ameahidi neema inayowezesha ambayo inatosha kabisa kufidia udhaifu wetu katika majaribu:
Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. (1 Wakorintho 10:13).
► Je, ni mambo gani tunajua kutokana na kifungu hiki?
Kifungu hiki kinatuambia mambo kadhaa muhimu.
1. Majaribu huja kwa sababu ya ubinadamu wetu. Hiyo ina maana kwamba mapambano yako si ya kipekee.
2. Mungu anajua mipaka yetu. Anaelewa tunaweza kustahimili kwa kiwango gani. Hatujui tunaweza kustahimili kwa kiwango gani, lakini yeye anajua.
3. Mungu huweka mipaka katika majaribu yanayotujia. Anataka tuishi kwa ushindi. Kulingana na kifungu hiki, ushindi wakati wote unawezekana.
4. Mungu hutoa kile tunachohitaji kwa ajili ya ushindi. Anatuandalia njia ya kujinasua. Mungu anataka tuishi kwa ushindi. Anatoa neema kwa ajili ya kuishi kwa ushindi.
“Watu hawana mwelekeo wa Utakatifu. Kando na juhudi zinazosukumwa na neema, watu hawana mwelekeo wa utauwa, maombi, kutii maandiko, imani, na kumfurahia Bwana. Tuna mwelekeo wa kulegeza msimamo na tunauita stahamala; tuna mwelekeo wa uasi na tunauita uhuru; tuna mwelekeo wa ushirikina na tunauita imani. Tunathamini utovu wa nidhamu wa kupoteza uwezo wa kujidhibiti na tunauita kujivinjari; tuna mwelekeo wa kuwa wavivu katika maombi na kujidanganya kwamba tumeepuka mtazamo wa kuzingatia sheria; tunateleza katika mwelekeo wa kutomcha Mungu na kuamini kuwa tumewekwa huru.”
D.A. Carson
Maisha katika Roho
► Nenda katika Warumi 8 na uangalie vifungu vilivyotumiwa katika sehemu hii.
Warumi 8 inatoa maelezo mazuri sana kuhusu kazi ya Roho katika maisha ya muumini. Warumi 8:26 inatuambia kwamba hata hatujui jinsi ya kuomba ipasavyo, lakini Roho Mtakatifu huomba kupitia sisi.
Sura hii inatueleza jinsi ya kuishi maisha ya ushindi. Hatutahukumiwa ikiwa tunafuata Roho badala ya mwili (Warumi 8:1, 4). Tunaweza kutimiza haki ambayo Mungu anatarajia tutimize, kwa sababu nguvu ya Roho inafanya kazi ndani yetu (Warumi 8:4).
Ikiwa mtu anatawaliwa na asili ya dhambi, hawezi kumpendeza Mungu (Warumi 8:8), amehukumiwa (Warumi 8:1), na amehukumiwa na Mungu (“kufa” katika Warumi 8:13). Lakini kwa uwezo na mwongozo wa Roho Mtakatifu, tunaweza kukomesha matendo ya dhambi (Warumi 8:13-14).
Katika Yohana 15:1-10 kuna sitiari maarufu ya mzabibu na matawi. Inajibu maswali muhimu.
Je, ni jinsi gani tunakaa ndani ya Kristo? “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake” (Yohana 15:10). Kuacha kukaa ndani ya Kristo kunamaanisha kwamba mtu ameacha kumtii Kristo. Basi nini kitatokea?
“Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea” (Yohana 15:6). Ikiwa mtu ataacha kutii, na hivyo basi akaacha kukaa ndani ya Kristo, anakataliwa. Mfano wa matawi yanayoteketezwa unaonyesha kukataliwa kabisa.
“Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu” (Yohana 15:4). “Kila tawi ndani yangu lisilozaa
huliondoa” (Yohana 15:2). Ikiwa hatutakaa ndani ya Kristo kwa kumtii, hatuwezi kuzaa matunda. Kuzaa matunda kunamaanisha kuishi maisha yaliyobadilishwa, yenye baraka, na yanayoongozwa na neema ya Mungu. Mtu asipomtii Mungu, anajitenga na mtiririko wa uzima ambao Mungu anatoa na hawezi tena kuishi chini ya neema ya Mungu. Asiyezaa matunda anakataliwa.
Kristo ni kama mzabibu unaotupatia uzima (Yohana 15:6). Wokovu unapatikana kwa njia ya uhusiano. Kutengwa na Kristo ni kutengwa na wokovu. Tunadumisha uhusiano unaookoa na Kristo kwa kumwamini na kumtii Mungu (Yohana 15:10).
Balbu za mwanga na umeme ni kielelezo cha kisasa cha dhana hiyo ya uhusiano na Kristo. Balbu huwa na mwanga wakati nguvu ya umeme inapita ndani yake. Balbu haiwezi kuendelea kuwaka ikiwa imetenganishwa na chanzo chake cha nguvu za umeme. Vivyo hivyo, tuna uzima wa milele kupitia uhusiano wetu na Kristo (Yohana 17:3). Uzima wake unatiririka ndani yetu. Hatuwezi kudumisha uzima huo tukijitenga naye.
“Lazima iwe muhimu kwa Mungu, kwani anatuambia kwamba ‘pasipo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Bwana’ (Waebrania 12:14). Utakatifu si orodha ya mambo unayopaswa kufanya na usiyopaswa kufanya. Badala yake, ni kufanana na Kristo.”
Jim Cymbala
Maonyo Katika Maandiko
Watu wengine husema kwamba jina haliwezi kuondolewa kutoka kwenye kitabu cha uzima kwa njia yoyote baada ya kuandikwa humo. Lakini kuna angalau njia moja ambayo kwayo jina linaweza kuondolewa:
Na mtu ye yote akiondoa lolote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki (Ufunuo 22:19).
Kuna watu wachache sana ambao wana hatia ya kuondoa sehemu ya kitabu cha Ufunuo. Hata hivyo, hoja inatolewa kwamba inawezekana jina kuondolewa kutoka kwenye kitabu cha uzima.
Yesu alitoa ahadi na onyo aliposema, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima” (Ufunuo 3:5).
Kuna wakati ambapo Paulo alikuwa na wasiwasi kwamba waongofu wake katika mji wa Thesalonike huenda wameacha imani yao. Alisema kwamba kama hilo lingetokea, juhudi zake za kuwahubiria Injili zingekuwa kazi bure (1 Wathesalonike 3:5). Hii inaonyesha kwamba inawezekana muumini kuanguka kutoka katika imani yake kabisa kiasi kwamba uongofu wake wa awali unakuwa hauna thamani yoyote.
Katika 2 Petro 2:18-21 tunaona kwamba kuna walimu wa uongo wanaowapotosha baadhi ya waumini ambao walikuwa wameepuka uchafu wa dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Waumini hao wa awali walikuwa wameijua njia ya haki lakini wakaiacha. Andiko hili linasema kwamba afadhali wasingejua njia ya Kristo kuliko kurudi kwenye
maisha ya dhambi. Hii inaonyesha kwamba inawezekana mtu kupoteza wokovu wake kwa kurudi katika dhambi. Kama isingewezekana mtu kupoteza wokovu wake, mtu asingeweza kuwa katika hali mbaya zaidi kuliko kabla ya kuokoka.
Uwana unaweza kubadilishwa. Wakati mmoja tulikuwa watoto wa Ibilisi (Yohana 8:44) na wana wa ghadhabu (Waefeso 2:2), lakini uwana huo unabadilishwa tunapofanywa wana wa Mungu (Warumi 8:15). Mwana mpotevu alipoteza faida zote za uwana alipokuwa amejitenga na baba yake. Aliporudi, baba yake alisema kuwa alikuwa amekufa (Luka 15:32).
Mungu anataka waumini wajihisi salama, lakini si kwa kuruhusu hisia zao zishawishiwe na hakikisho la uongo linalofanya wajiweke hatarini. Hatupaswi kuwaahidi waumini kitu ambacho Mungu hajaahidi. Hajaahidi kwamba tutakuwa salama kutokana na kupoteza wokovu wetu haijalishi tunafanya nini. Anaahidi kwamba atatuongoza na kutuwezesha kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi. Hilo ni hakikisho linalotosha kutufanya tusiwe na hofu.
Wakati mwingine waumini huwa na shaka na wokovu wao. Wanaweza kuwa na uhakika kwamba waliwahi kuokoka, lakini wana shaka kwamba bado wako katika uhusiano unaookoa na Mungu. Biblia haituachi na shaka yoyote kuhusu suala hili muhimu. Ni mapenzi ya Mungu kwamba muumini awe na uhakika kabisa na wokovu wake kiasi kwamba awe na ujasiri kwa ajili ya siku ya hukumu, (1 Yohana 4:17) bila kujiuliza kama atapita mtihani wa Mungu au la.
Muumini anapokuwa na shaka, hatakiwi kuipuuza kwa sababu ana uhakika kwamba aliwahi kuokoka wakati fulani. Unafaa kujichunguza ili uone kama uko katika imani (2 Wakorintho 13:5). Ikiwa mtu anajua kwamba aliokolewa kwa kufuata hatua za maandiko za wokovu, na kwamba anakaa ndani ya Kristo kwa kuenenda katika uhusiano wa utiifu naye, anaweza kuwa na uhakika kwamba ana uzima wa kiroho.
Makosa ya Kuepuka: Matarajio Duni
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Washirika wawili wa darasa wanaweza kueleza sehemu hii na sehemu inayofuata.
Ushindi dhidi ya dhambi unaonekana hauwezekani kwa watu kwa sababu ya mambo mawili: udhaifu wa kibinadamu na upotovu wa kurithi. Ni lazima tukumbuke kwamba Mungu hatuhukumu kwa kuwa tuna mapungufu ya kibinadamu. Mungu hutoa nguvu kwa Roho wake ili tuweze kutimiza mapenzi yake. Si dhambi kuwa na udhaifu, na si lazima mtu yeyote atende dhambi kwa sababu ya udhaifu.
Ushawishi wa upotovu wa kurithi huendelea baada ya kuongoka, lakini Mungu hutoa neema kwa ajili ya utakaso. Hatulaumiwi kwa kuzaliwa na upotovu wa kurithi, lakini ni kosa letu ikiwa tutaendelea kuathiriwa nao. Kwa hivyo, udhaifu wa kibinadamu na upotovu wa kurithi havipaswi kutufanya tupoteze tumaini la kuishi kwa ushindi.
Kupitia imani katika Kristo, tunaunganishwa naye. Tunajitambulisha naye katika kifo na ufufuo wake, na kwetu hilo linamaanisha kuwa wafu kwa dhambi na ufufuo katika maisha mapya (Warumi 6:3-11). Yuko ndani yetu, nasi tuko ndani yake. Maisha ya Kikristo si tu kwamba tujaribu kufuata mfano wake, tukijaribu kadiri tunavyoweza. Tunaishi maisha ya Kikristo kwa kuwa na Kristo ndani yetu. Alipata ushindi dhidi ya dhambi alipotembea duniani, na bado anaishi kwa ushindi ndani yetu.
Kwa Nini Hilo ni Muhimu
Mwanamke maskini aliyevalia matambara ameketi kando ya barabara ya jiji kubwa. Nywele zake zimesokotana na kuchanganyikana na uchafu. Ngozi yake ni chafu. Ameketi katika hali ya kukata tamaa na kukosa tumaini. Ghafla, kuna mtafaruku mkubwa na anayejitokeza barabarani akiwa kwenye gari la farasi ni mwanafalme mkuu wa ufalme pamoja na watu wake wakuu. Mwanafalme huyo ni mwenye sura ya kuvutia, mwenye nguvu, na mkarimu! Gari lake lilipokuwa linapita mahali ambapo mwanamke huyo mchafu alikuwa amekati, mwanafalme huyo anamwambia dereva wake, “Simama!”
Gari linaposimama, mwanamfalme anawaambia watumishi wake, “Yule mwanamke aliyeketi kando ya barabara ndio mwanamke ninayetaka kumwoa!”
Sasa eneo linabadilika. Tunatazama ikulu ya mfalme siku ya harusi. Tunaona nini? Mwanamke mchafu akiwa bado amevalia matambara na mwenye nywele chafu zilizosokotana. Amezungukwa na wahudumu wake wa kibinafsi, wakiwa wameshika rinda la harusi, sabuni, na manukato, lakini bibi harusi hana haja na kujitayarisha kwa ajili ya siku yake ya harusi. Mmoja wa wanawake hao anauliza, “Bibi yangu, hutaki kujitayarisha kwa ajili ya harusi?” Bibi harusi anajibu, “Hivi ndivyo nilivyokuwa mwanafalme aliponiona na akataka kunioa, kwa hivyo nadhani haijalishi nitaonekanaje leo.”
Mtazamo huo ungetushtua. Kwa sababu mwanafalme anampenda, hataki abaki katika hali yake. Kwa sababu mwanamfalme alimpenda wakati hakuvutia, mwanamke huyo anapaswa kutaka kuonekana wa kuvutia zaidi kwake.
Mungu anatupenda wakati sisi ni wenye dhambi, lakini hilo halimaanishi kwamba dhambi si jambo zito. Kwa sababu anatupenda, anataka kubadilisha hali yetu. Kwa sababu anatupenda, tunapaswa kutaka kuwa na taswira na tabia inayompendeza.
Maagizo ya Kiutendaji ya Kuishi kwa Ushindi
Kote ulimwenguni ukweli wa Kikristo unachanganywa na ushirikina. Watu wengine hufundisha ushindi dhidi ya dhambi kupitia maombi ya kurudiwarudiwa, matukio ya kihisia, kukemea roho waovu (ambao wanafikiriwa kuwa chanzo cha dhambi fulani), kujiumiza, kuvaa hirizi fulani, kuweka ishara za kiroho sehemu mbalimbali za nyumba, au kupaka mafuta maalum kwenye mwili. Ni makosa kutarajia ushindi kupitia mazingaombwe ya kiroho!
Wengine pia hufundisha ushindi dhidi ya dhambi kwa mtazamo rahisi sana. Wanasema kwamba wokovu na ujazo wa Roho utavunja nguvu za dhambi milele. Hawasisitizi hitaji la kukua wa kiroho, nidhamu, na kuwa macho siku zote.
Wale ambao wanashindwa kupata ushindi thabiti dhidi ya ulimwengu na dhambi wanapaswa kujiuliza maswali yafuatayo:
1. Je, kweli nimezaliwa upya? Je, mimi ni mfu kwa maisha yangu ya zamani; nimetubia na kuiacha nyuma maisha yangu ya zamani? Je, nina maisha mapya katika Kristo—mitazamo mipya, matamanio mapya, shauku mpya kwa mambo ya Mungu (2 Wakorintho 5:17)? Je, Kristo amekuja kukaa ndani ya moyo wangu kwa njia ya Roho Mtakatifu? Je, ninajaribu kushinda dhambi kupitia nguvu za kibindadmu, au ninategemea nguvu ya Mungu inayokaa ndani yangu (Wagalatia 2:20)?
2. Je, nahifadhi Neno la Mungu moyoni mwangu? Mwandishi wa Zaburi alishuhudia akisema, “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11). Tunahitaji kula Neno la Mungu kama vile mtoto mchanga anavyokunywa kwa hamu maziwa ya mama yake (1 Petro 2:2).
3. Je, kweli ninajiona kuwa mfu kwa dhambi na hai kwa Mungu? “Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu” (Warumi 6:11). Je, ninakataa majaribu nikiwa na uhakika kwamba hayana nguvu juu yangu?
4. Je, ninamtegemea Mungu kwa ajili ya ushindi? Mtume Yohana alitangaza kwamba mtu aliyezaliwa katika familia ya Mungu huushinda ulimwengu. “Na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” (1 Yohana 5:4). Mtume Paulo alisema kwamba hataweka imani katika kitu chochote isipokuwa msalaba wa Yesu, kwani ni kupitia msalaba ndio mambo ya kidunia yanapoteza uwezo wao wa kutuvutia na kututawala (Wagalatia 6:14). Haiwezekani sisi kuishi maisha ya ushindi thabiti ikiwa tutasahau chanzo cha haki yote, Yesu.
5. Je, ninajivika Bwana Yesu kwa imani kila sikuna kutopatia dhambi nafasi hata kidogo? Haijalishi tuko katika hatua gani katika safari yetu ya Kikristo, ushindi hauji moja kwa moja. Lazima nidhamirie kuchukua mtazamo wa Yesu juu ya dhambi na kufuata mfano wake. (Warumi 13:14; Waefeso 4:24)
6. Je, ninajivika silaha za kiroho za Mungu? Katika uwanja wa vita vya maisha waumini wengi hujeruhiwa na mishale ya Shetani yenye moto kwa sababu wamekosa kuwa waangalifu kuhusu ulinzi wao wa kiroho (Waefeso 6:11).
7. Je, ninazingatia nidhamu ya kibinafsi? Haijalishi tumekomaa kiasi gani katika imani yetu, siku zote tutahitaji kuzingatia nidhamu ya kibinafsi. Je, ninauzoeza mwili wangu na kuufanya uwe na nidhamu? Tamaa za asili nilizopewa na Mungu (kama vile hamu ya chakula, usingizi, au ngono) lazima zidhibitiwe, ili zitumike kwa makusudi ya nafsi yangu iliyozaliwa upya. Kwa sababu mwili wangu umeharibiwa na dhambi, tamaa zake hazina usawa.Ni lazima mwili usiruhusiwe kutawala; lazima utumikie roho. Paulo alisema kwamba aliutia mwili nidhamu wake na kuufanya umtii ili asiwe mtu aliyekataliwa kiroho (1 Wakorintho 9:25-27). Nidhamu hii ni muhimu kwa kila Mkristo.
8. Je, ninaishi kwa utiifu? “Tuenende nuruni” ni himizo la Mtume Yohana (1 Yohana 1:7). Kwa sababu kuna mitego mingi, mawe ya kukwaza, na sehemu hatari kwenye barabara ya kwenda mbinguni, lazima tuenende katika nuru ya Neno la Mungu (Zaburi 119:105) na uwepo wa Roho Mtakatifu (Yohana 14:26). Utiifu unabeba ahadi kwamba damu ya Yesu itatudumisha katika usafi. Kutembea gizani hufanya tukajikwaa na kuanguka na hatimaye kifo kwa wale wanaokataa kuirudia njia ya nuru.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Ni fursa na wajibu wa kila muumini kuishi maisha ya Kikristo yenye ushindi. Muumini ana uzima kutokana na uhusiano alionao na Kristo. Muumini anayekataa mapenzi ya Mungu na kurudi kwenye dhambi hudhoofisha na anaweza kuharibu imani yake, ambayo ndio inayotuunganisha na Mungu. Mungu hutoa neema ya kutia nguvu, ili muumini aweze kushinda kila jaribu.
Mazoezi ya Somo la 9
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Mathayo 13:18-23
Waebrania 10:23-39
Yakobo 1:21-27
2 Petro 1:1-11
Ufunuo 3:14-22
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 9. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 9
(1) Je, mojawapo ya mada kuu za 1 Yohana ni ipi?
(2) Je, 1 Yohana inasisitiza zaidi sifa gani ya muumini?
(3) Je, ni mambo gani manne tunayojua kutoka katika 1 Wakorintho 10:13?
(4) Je, muumini huendeleaje kukaa ndani ya Kristo?
(5) Je, tunadumishaje uhusiano unaookoa na Kristo?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.