Neno la Kiebrania lililotafsiriwa utakatifu au utakaso linatokea zaidi ya mara 600 katika Agano la Kale. Maneno ya Kiebrania na Kigiriki yanayotafsiriwa takatifu kimsingi yanamaanisha kutengwa, kujitolea kwa kusudi fulani. Kitu kilichotakaswa kinaacha kutumiwa kwa matumizi ya awali na kinatengwa kwa ajili ya kusudi jipya mahususi. Tazama vitu kadhaa ambavyo viliwekwa wakfu na kuchukuliwa kuwa vitakatifu katika Agano la Kale:
Uwanja Mtakatifu. Mungu alitenga uwanja kama mahali pa kukutania na Musa (Kutoka 3:5).
Hema na Hekalu Takatifu. Vitu vingi vitakatifu vilihusishwa na Hema la Kukutania na Hekalu, vikiwemo mavazi ya kuhani (Mambo ya Walawi 16:32), mkate (Kutoka 29:34), na samani (Kutoka 40:9). Vitu hivi vilitengwa kwa ajili ya kumwabudu Mungu.
Siku Takatifu. Siku ya Sabato ilitengwa kama siku takatifu (Mwanzo 2:3; Kutoka 20:8). Sikukuu nyingine za Kiyahudi kama Siku ya Upatanisho pia zilikuwa maalum (Mambo ya Walawi 23:26-29). Siku hizi zilitengwa kwa ajili ya mapumziko, tafakari na ibada.
Mungu Mtakatifu. Mfano mkuu zaidi wa utakatifu katika Biblia ni Mungu mwenyewe. Kila kitu kumhusu Mungu ni kitakatifu. Jina lake ni takatifu (Mambo ya Walawi 22:2); maneno yake ni matakatifu (Yeremia 23:9); njia zake ni takatifu (Zaburi 77:13). Utakatifu unamaanisha Mungu ametengwa kabisa na kitu chochote chenye dhambi, najisi, cha kawaida au kisichofaa kwa nafsi na nafasi yake ya kiungu
Katika Agano Jipya Yesu anatajwa kama mtakatifu (Yohana 17:19; Matendo 4:27, 30) na asiye na dhambi (2 Wakorintho 5:21). Malaika (Marko 8:38), mitume na manabii (Waefeso 3:5) wanaelezwa kama watakatifu. Wote hawa walitengwa kwa ajili ya kusudi maalum.
Biblia inawahamasisha watu wa Mungu kuwa watakatifu (Mambo ya Walawi 11:44-45;
1 Wakorintho 1:2; 1 Petro 1:15-16). Somo hili litaeleza utakatifu ambao Mungu anatarajia kutoka kwetu.
Waabudu Watakatifu wa Mungu
► Someni Zaburi 119:33-40 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu jinsi Mungu anavyombadilisha muumini?
Mungu alipoanza kujifunua, kusudi lake la kwanza lilikuwa kuonyesha yeye ni Mungu wa aina gani. Mungu kimsingi alijieleza kama mtakatifu. Isaya mara nyingi alimtaja Mungu kama “Mtakatifu wa Israeli.”
Utakatifu wa Mungu ulikuwa mada ya ibada:
Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu. Mtukuzeni BWANA, Mungu wetu; Sujuduni penye kiti cha miguu yake; Ndiye mtakatifu (Zaburi 99:3, 5).
Utakatifu wa Mungu ndio msingi wa jinsi anavyotaka mwanadamu awe. Kwa sababu yeye ni mtakatifu, anawahamasisha wale wanaomwabudu wawe watakatifu. Alisema, “Iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu” (Mambo ya Walawi 11:44-45, Mambo ya Walawi 19:2, Mambo ya Walawi 20:26, Mambo ya Walawi 21:8).
Mungu wa Israeli alikuwa tofauti na miungu ya uongo ya wapagani na alihitaji aina tofauti ya ibada.
Ni nani atakayepanda katika mlima wa BWANA? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila (Zaburi 24:3-4).
Swali hapa ni, “Mungu anakubali ibada ya nani?” Si kila mtu anakubaliwa kama mwabudu Mungu. Waabudu Mungu lazima wawe watakatifu.
Utakatifu ambao Mungu anatarajia si tu wa sherehe au kujifanya; ni utakatifu halisi. Kiwango cha utakatifu kwa waabudu Mungu kinarudiwa katika Agano Jipya:
Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, “Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu” (1 Petro 1:15-16).
Mwenendo unarejelea tabia na mtindo mzima wa maisha ya mtu. Mungu haombi tu kwamba wanaomwabudu wawe watakatifu kisherehe, au waitwe watakatifu wakati wao si watakatifu. Anatarajia wanaomwabudu waishi maisha matakatifu.
► Je, baadhi ya sababu zinazofanya utakatifu uhusishwe na ibada ni zipi?
Utakatifu ni muhimu kwa ibada kwa sababu
1. Tunampenda Mungu na tunataka kuwa kama yeye. Kumwabudu Mungu ni kuona kwamba yeye ndiye kiumbe wa ajabu zaidi aliyepo na kumpenda jinsi alivyo. Kuabudu ni kuthamini sifa za asili yake. Asili ya Mungu kimsingi ni takatifu, hivyo ikiwa tunapenda sana asili ya Mungu, tutachukia dhambi na uchafu, hata kama tunauona ndani yetu.
2. Tunampenda Mungu na tunataka kumpendeza. Takwa la Mungu halitushangazi ikiwa tunaelewa ibada ni nini hasa. Hatumuabudu kwa sababu ya hofu. Hatumuabudu kwa sababu tu anatubariki. Tunamwabudu kwa sababu tunampenda.
Utakaso Wakati wa Kuongoka
Biblia inatumia neno utakaso kurejelea kile ambacho kimetokea katika maisha ya kila muumini. Paulo aliandika “Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu” (1 Wakorintho 1:2). Paulo aliandika, “…lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.”
(1 Wakorintho 6:11). Wakorintho walikuwa tayari wametakaswa ingawa hawakuwa wamekomaa kiroho na walikuwa bado watu wa kimwili, kama watoto wachanga katika Kristo (1 Wakorintho 3:1).
[1]Neno takasa, linaporejelea Wakorintho hao, linatumiwa katika maana yake ya jumla. Wakorintho walikuwa wameitwa kutoka katika dhambi na ulimwengu na walikuwa wametengwa kwa ajili ya Mungu. Hakika
hawakuwa wamekomaa katika utakaso, lakini walikuwa wametengwa na maisha ya zamani na sasa walikuwa sehemu ya familia ya Mungu.
Tunapokutana na Mungu kwa mara ya kwanza, dhambi ni kikwazo katika uhusiano wetu naye. Ndio maana uhusiano wetu na Mungu hauwezi kuanza hadi tutubu, tusamehewe, na tupewe moyo mpya.
Wakati huo huo tunapopatanishwa na Mungu, tunabadilishwa (Tito 3:5). Kiroho, tunafanywa viumbe wapya. Tunawekwa huru kutokana na nguvu za dhambi, na tunatamani kumpendeza Mungu. Utakatifu wa Kikristo huanza mtu anapookoka.
Biblia inatufundisha kwamba wokovu husababisha maisha matakatifu mara moja. Neema ya Mungu iletayo wokovu inatufundisha kuishi maisha ya kiasi, ya uadilifu, na utauwa katika nyakati hizi (Tito 2:11-12). Kusudi la wokovu ni kutuweka huru kutokana na dhambi na kutufanya tuwe watakatifu, ili tuweze kuishi katika uhusiano na Mungu (Luka 1:74-75, Warumi 6:2, 11-16).
“Mzee mmoja Mhindu alimuuliza Amy Carmichael, ‘Tumesikia mahubiri mengi,
je, unaweza kutuonyesha maisha
ya Bwana wako Yesu?”
Kukua Katika Utakaso
Tunapoishi katika uhusiano na Mungu, tunaendelea kukua katika utakatifu kadiri tunavyozidi kuelewa ukweli wake. Kuenenda katika nuru kunamaanisha kuendelea kumtii Mungu kadiri tunavyozidi kujifunza ukweli wake (1 Yohana 1:7). Kadiri tunavyoelewa vyema zaidi kile kinachompendeza na kisichompendeza, tunabadilishwa na ukweli wake na nguvu ya Roho Mtakatifu.
Mtu anayempenda Mungu atatamani kuwa mtakatifu kabisa. Hataki kubadilisha matendo yake tu. Anataka nia zake ziwe safi kabisa. Daudi aliomba kwamba aweze kuishi kwa ushindi kamili dhidi ya dhambi, kisha akaomba kwamba maneno yake na hata mawazo ya moyo wake yampendeze Mungu. (Zaburi 19:12-14. Tazama pia Zaburi 119:7, 34, 36, 69, 80, na 112.)
Mchakato mzima wa kupata ukomavu wa kiroho unaitwa utakaso. Utakaso ni mchakato wa maisha yote wa kuzidi kutengwa na dhambi na dunia, na kujitoa zaidi kwa Mungu. Hili linadhihirishwa na onyo la Paulo dhidi ya kufuata mfano wa dunia na himizo lake kwamba “mgeuzwe [wakati wote] kwa kufanywa upya nia zenu” (Warumi 12:2). Kutengwa na dunia na mabadiliko ya nia si matukio yanayokamilishwa kwa wakati maalum katika maisha ya Mkristo. Muumini huendelea kukua kadiri anavyotembea na Bwana. Haya yote yamejumuishwa katika neno utakaso.
Upotovu wa Kurithi na Utakaso
Upotovu wa kurithi ni upotovu wa asili ya kimaadili ya mtu ambao unampa msukumo wa kutenda dhambi tangu anapozaliwa. Wanatheolojia wakati mwingine huuiita “dhambi ya asili,” kwa sababu ni asili yetu ya dhambi tunayozaliwa nayo kwa sababu ya dhambi ya Adamu.
Kila mtu huzaliwa na nia ambayo ni ya ubinafsi na yenye msukumo wa kutenda dhambi. Nia zetu hazina uhuru wa kuchagua kile kilicho sahihi isipokuwa Mungu atupe hamu na nguvu ya kufanya hivyo (Warumi 6:16-17). Upotovu wa kurithi huchochea dhambi za ndani kama vile kiburi, wivu, chuki, na kutosamehe. Pia huchochea matendo ya dhambi.
► Je, baada ya mtu kuokoka, bado ana upotovu wa kurithi?
Mtu ambaye ameokoka hayuko tena chini ya udhibiti wa upotovu wa kurithi. Kama bado angekuwa anadhibitiwa nao, angekuwa anaishi katika dhambi na hajaokoka. Biblia inatuambia kwamba mtu anayedhibitiwa na akili ya kimwili amehukumiwa (Warumi 8:6-8, 13). Mtu aliyeokoka hayuko chini ya udhibiti wa upotovu wa kurithi na anaweza kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Warumi 8:1, 9, 13).
Hata hivyo, mtu aliyeokoka bado ana ushawishi wa upotovu wa kurithi ndani yake hadi atakapotakaswa kutokana nao. Paulo aliwaambia waumini wa Korintho kwamba bado walikuwa watu wa kimwili na walikuwa na mitazamo kama ya watu wa dunia, ingawa walikuwa wameokolewa. (1 Wakorintho 3:1-3.) Isitoshe alidokeza kwamba ni jambo la kawaida kwa Mkristo mpya kuwa katika hali hiyo. Alisema kwamba kuwa na mtazamo wa kimwili ni kuwa kama mtoto mchanga katika Kristo.
Muumini aliye katika hali hiyo anampenda Mungu, lakini hawezi kumpenda Mungu kwa moyo wake wote, nafsi yake yote, akili yake yote na nguvu zake zote (Mathayo 22:37). Hawezi kusema, kama Paulo, kwamba ana nia moja ya kufuata wito wa Mungu (Wafilipi 3:13-15). Anajua kwamba baadhi ya tafakari za moyo wake hazikubaliki kwa Mungu (Zaburi 19:14).[1]
Mungu hatuachi katika hali hiyo. Hata hapo zamani za kale Mungu aliahidi Israeli kwamba atafanya kazi ya neema ambayo itawafanya waweze kumpenda kwa mioyo yao yote. (Soma Kumbukumbu la Torati 30:6.)
Daudi aliomba kwa ajili ya kazi ya neema ambayo ni zaidi ya msamaha. Alikuwa ametenda dhambi na kutambua kwamba hilo lilitokea kwa sababu ya tatizo moyoni mwake. Alijua kwamba dhambi ilikuwa katika asili yake, lakini aliamini kwamba Mungu alimtaka awe mtakatifu kikamilifu. Aliomba kwa ajili ya utakaso kamili. (Soma Zaburi 51:5-10.)
Waumini wa Agano Jipya walihamasishwa kupitia tukio lingine maalum baada ya kuongoka. Waumini wa Thesalonike walikuwa mfano mzuri wa waumini ambao walikuwa wameikubali
injili, wamejitenga na sanamu, wamevumilia mateso, walikuwa na furaha katika Roho Mtakatifu, na walikuwa wakingoja kurudi kwa Yesu (1 Wathesalonike 1:6-10). Lakini bado kuna kitu kilichokuwa kimekosekana katika imani yao. Halikuwa jambo litakalotolewa kwa muda mrefu au baada ya kifo, kwa sababu Paulo alisema kwamba linaweza kutokea wakati atakapowatembelea. (1 Wathesalonike 3:10.) Aliomba hivi:
Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. (1 Wathesalonike 5:23-24).
[2]Paulo aliomba kwamba waumini hao watakaswe kikamilifu. Matokeo yake ni kwamba waumini watakuwa bila lawama katika mwili, nafsi, na roho wakati Bwana atakaporudi.
Wanafunzi wa Yesu walipitia kazi maalum ya neema siku ya Pentekoste. Tunajua kwamba walikuwa tayari wameokolewa kabla ya wakati huo, kwa sababu Yesu alisema kwamba wao si wa dunia, kwamba wao ni wake na wa Baba, na kwamba majina yao yameandikwa mbinguni (Yohana 15:3, Yohana 17:14; 9-10; Luka 10:20). Lakini walikuwa na ubinafsi na hawakuzingatia vipaumbele vya Mungu. Yesu aliwarekebisha tena na tena kwa ajili ya mitazamo yao yenye dhambi. (Soma Marko 9:33-34; Marko 10:35-41; Luka 9:54-55.)
Baada ya kufufuka kwa Yesu, kabla tu hajarudi mbinguni, aliwaambia wanafunzi wake kwamba watakuwa mashahidi wake ulimwenguni. Lakini aliwaambia kwamba ni lazima kwanza wabatizwe kwa Roho Mtakatifu. (Luka 24:49; Yohana 20:22; Matendo 1:2-5, 8.) Tayari alikuwa amewaambia mengi kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu, hasa katika Yohana 14-16.
Wanafunzi walijazwa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste (Matendo 2:4). Ujazo huo ulibadilisha nia, vipaumbele na matendo yao. Katika matukio mengine yote ya Agano Jipya, wanafunzi walionyesha mitazamo na vipaumbele kama vya Kristo, ingawa bado walikuwa na kutoelewana na walifanya makosa. Nyaraka zilizoandikwa
na Petro na Yohana zinadhihirisha ujumbe na moyo wa Kristo. Ujazo wa Roho Mtakatifu uliwawezesha kumpenda Bwana Mungu wao kwa mioyo yao yote, kwa roho zao zote, kwa akili zao zote, na kwa nguvu zao zote na kuwapenda majirani wao kama nafsi zao (Mathayo 22:37-39). Kwa sababu walikuwa wamejitoa kikamilifu kwa Roho Mtakatifu, aliishi kupitia kwao, kama vile alivyoishi kupitia Kristo (Luka 4:1, 14, 18; Matendo 2:22).
Walimu wa Kikristo huzingatia mchakato wa utakaso, na wengine huzingatia tukio maalum. Matukio ya Pentekoste na ubatizo wa Roho Mtakatifu ni mfano wa watu wanaopitia tukio maalum la utakaso. Ukweli kwamba hali fulani inaweza kuwa kamili au mtu anaweza kuipitia kikamilifu inamaanisha kuwa hali hiyo inatokea katika wakati fulani. Ni muhimu kwamba tusiweke mipaka katika kile ambacho injili inaweza kufanya, hata katika dakika moja ya kuwa na imani na kujisalimisha kikamilifu (Warumi 12:1-2). Yote ambayo Yesu alitoa kupitia kifo na ufufuo wake yanapatikana na wote ambao:
1. Wanajichukulia kuwa wafu kwa dhambi pamoja na Yesu (Warumi 6:11)
2. Hawaruhusu dhambi itawale katika miili yao (Warumi 6:12)
3. Wanatoa miili yao kama vyombo vya haki (Warumi 6:13)
Katika historia, Wakristo wakuu wameshuhudia kuhusu nyakati ambapo waliingia katika maisha yaliyojazwa Roho na uhusiano wa kina zaidi na Mungu, wakiwemo wanaume na wanawake kama vile John Bunyan, Hudson Taylor, Dwight L. Moody, Sammy Morris, Oswald Chambers, Frances Ridley Havergal na Amy Carmichael.[3]
Ingawa ni muhimu kwamba tusiweke mipaka katika kile ambacho Mungu anaweza kufanya katika muda mfupi, ni muhimu pia tusisahau kazi ya Roho Mtakatifu kupitia michakato. Ingawa aina hii ya utakaso wakati mwingine huelezwa kuwa kamili, kiwango hiki hakimaanishi kwamba hakuwezi kuwa na ukuaji zaidi. Kwa mfano, baada ya kujifunza kuzungumza Kifaransa haimaanishi kwamba mtu hawezi kuendelea kujifunza kuzungumza Kifaransa kwa njia bora zaidi. Wale ambao wametakaswa kikamilifu wamewahi kufikia mahali ambapo walipitia utakaso ambao hawakuwa wameupitia hapo awali. Hata hivyo, hiyo si hali ya kuwa kamili. Ni maisha ya utakatifu ambapo muumini anaendelea kukua.
“Utakaso si wazo langu la kile ninachotaka Mungu anifanyie; utakaso ni wazo la Mungu la kile anachotaka kunifanyia, na hana budi kuniweka katika mtazamo wa akili na roho ambapo kwa gharama yoyote ile nitamruhusu anitakase kikamilifu.”
“Kanisa lina wajibu maradufu kuhusiana na ulimwengu unaotuzunguka. Kwa upande mmoja tunapaswa kuishi, kutumika na kushuhudia ulimwenguni. Kwa upande mwingine tunapaswa kuepuka kuchafuliwa na ulimwengu. Kwa hivyo hatutakiwi kutafuta kuhifadhi utakatifu wetu kwa kuukimbia ulimwengu wala kupoteza utakatifu wetu kwa kufuata ulimwengu.”
John Stott
[3]Unaweza kusoma hadithi nyingi kati ya hizi katika kozi ya Mafundisho Na Mazoezi Ya Maisha Matakatifu kutoka Shepherds Global Classroom.
Utakaso na Ukomavu wa Kikristo
Biblia inaeleza maisha ya muumini aliyekomaa. Roho Mtakatifu hufanya kazi katika maisha ya muumini ili kukuza sifa za Kikristo. Kazi ya Roho inajumuisha nyakati maalum za utakaso au upako na pia michakato inayotendeka hatua kwa hatua. Muumini hatakiwi kuridhika na maisha ya kiroho ambayo hayalingani na maelezo ya Biblia kuhusu muumini aliyekomaa.
Mwandishi wa kitabu cha Waebrania alisema kwamba baadhi ya wasomaji wake walikuwa bado kama watoto (Waebrania 5:12). Aliwahimiza kuacha kanuni za kimsingi za Kristo na kuendelea hadi kufikia ukomavu (Waebrania 6:1).
Maombi ya mitume kwa ajili ya waumini yanatuonyesha mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu.
Upendo
Paulo aliomba akisema, “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote…” (1 Wathesalonike 3:12-13). Pia aliwaombea Waefeso akisema:
Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo, ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu (Waefeso 3:17-19).
Paulo alikuwa anaomba kwamba waumini hao wawe na upendo zaidi. Katika 1 Wakorintho 13, Paulo alieleza jinsi upendo huo unapaswa kuonekana katika muumini aliyekomaa. Maisha ya utakaso ni kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na nguvu zako zote na kumpenda jirani yako kama nafsi yako (Luka 10:27). Hiyo ndio aina ya uhusiano walio nao watu watakatifu na Mungu na wanadamu wenzao.
Kutokuwa na Lawama
Paulo aliwaombea Wathesalonike, kwamba Mungu aifanye mioyo yao iwe bila lawama katika utakatifu (1 Wathesalonike 3:12-13). Sura mbili baadaye, anaomba kwamba watakaswe ili roho, nafsi na miili yao ihifadhiwe bila lawama wakati wa kuja kwake Bwana Yesu Kristo (1 Wathesalonike 5:23). Kutokuwa na lawama hakumaanishi ukamilifu katika kila njia. Mtu asiye na lawama hufanya makosa lakini ana tabia anayopaswa kuwa nayo.
Nguvu ya Ndani
Paulo aliomba kwamba waumini wa Efeso wafanywe imara kwa nguvu katika utu wao wa ndani kupitia Roho wa Mungu (Waefeso 3:15-16). Tabia ya ndani inakuwa na nguvu kadiri mtu anavyozidi kuwa na imani. Nguvu ya ndani ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kukataa maamuzi mabaya.
Kristo Akikaa Ndani Yetu
Paulo aliendelea na maombi kwa ajili ya Waefeso kwa kuomba kwamba Kristo akae ndani ya mioyo yao (Waefeso 3:17). Neno lililotafsiriwa “akae” katika kifungu hiki linamaanisha kukaa kwa kudumu si tu kukaa kwa muda mahali fulani. Usemi huu wa mfano unaonyesha
kwamba Yesu anataka kuishi nasi si kutembelea tu. Kristo huhisi kuridhika na wale wanaoishi maisha thabiti ya kiroho.
Utimilifu wa Mungu
Paulo anatamatisha sehemu ya maombi ya sala yake kwa ajili ya Waefeso kwa kuomba kwamba wajazwe utimilifu wote wa Mungu (Waefeso 3:14-19). Hii ni kutumia mfano wa kimwili kuelezea ukweli wa kiroho. Inamaanisha kwamba Mungu anataka kudhibiti kikamilifu sehemu zetu zote; akili, nia, hisia, shughuli, mitazamo, matamanio, na miitikio yetu. Kati ya maelezo yote ya maisha matakatifu yanayopatikana katika Biblia, huenda haya ndio makuu zaidi—kujazwa na utauwa kiasi kwamba upotovu wowote usipatikane kwako.
Mistari miwili inayofuata inahitimisha sala hii:
Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina (Waefeso 3:20-21).
Tamko hili la baraka linasema kwamba Mungu anaweza kufanya zaidi ya vile tunavyoweza kuomba au kufikiria. Paulo hazungumzi kuhusu kuwa na fedha nyingi bali kuhusu maisha ya kiroho. Hatupaswi kudharau viwango vya utakatifu na ukomavu ambavyo nguvu inayofanya kazi ndani yetu inaweza kutusaidia kufikia.
Tabia za Kikristo
Agano Jipya linatupatia tabia za kutuwezesha kupiga hatua katika utakatifu na ukomavu.
[1]Dumisha dhamiri njema. Paulo anamwarifu Timotheo kwamba njia ya kupigana vita vilivyo vyema (mfano wa maisha ya Kikristo yenye ushindi), ni kwa kuwa na imani na dhamiri njema (1 Timotheo 1:18-19).[2] Paulo pia alisema, “Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu
siku zote” (Matendo 24:16). Kusikiliza dhamiri zetu kunaweza kutufanya tutubu, tutoe fidia, tupatanishwe na mtu fulani, au tubadili tabia zetu. Kuwa na dhamiri njema kunamaanisha kwamba watu watakirir dhambi na kuzitubu wakati wowote wanapotambua kwamba wamefanya makosa.
Jitoe kwa Mungu. Katika himizo lenye nguvu katika Warumi 12:1, Paulo anaandika, “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Waumini wa Rumi walikuwa tayari wamejitoa kwa Mungu walipoongoka. Hata hivyo, hapa Paulo anahimiza kujitoa kwa Mungu kikamilifu zaidi.
Usifuate namna ya dunia (Warumi 12:2). Kufuata namna ya dunia ni kushawishiwa na mtazamo wa jamii ya wasioamini, hadi kufikia hatua ya kukubali maadili yake na kuwa na tabia kama za wasioamini. Watu wa kidunia hupata sababu za kuhalalisha mtazamo wa kuwa na ubinafsi, kutozingatia haki na kutimiza tamaa za mwili kwa njia za dhambi. Muumini yuko tofauti (2 Wakorintho 10:3-4).
Fanya upya nia yako. Paulo anaendeleza himizo kwa Warumi kwa kusema,
… bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu (Warumi 12:2).
Kadiri mtu anavyozidi kukataa mtazamo wa dunia na kukumbatia mtazamo wa Mungu, ndivyo atakavyozidi kubadilika.
Enenda katika nuru. Yohana aliandika, “Bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7). Nuru ni tamathali ya usemi inayowakilisha ukweli. Hivyo, kuenenda katika nuru kunamaanisha kuendelea kujifunza ukweli na kuufuata.
Vumilia mateso kwa imani. Tamko la baraka la Petro katika 1 Petro 5:10 linaashiria lengo tukufu la kuwa muumini aliyerejeshwa, mwenye nguvu, na aliye imara, lakini inaeleza njia isiyopendeza ya kufikia hali hiyo. “Mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu” (1 Petro 5:10). Mateso hutakasa mitazamo yetu na kurekebisha tabia zetu. Mungu huruhusu mateso yanayotujenga. Ni lazima tuyakubali na tujaribu kujifunza kile ambacho Mungu anatufundisha (2 Wakorintho 12:7-10).
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
“Neema duni ni neema [ya kujibunia] tunayojitolea sisi wenyewe. Neema duni ni kuhubiri msamaha bila kuhitaji toba, ubatizo bila nidhamu ya kanisa, Meza ya Bwana bila maungamo... Neema duni ni neema bila uanafunzi, neema bila msalaba, neema bila Yesu Kristo, aishiye na aliyefanyika mwili.”
Dietrich Bonhoeffer
[2]Paulo alitaka sana kwamba wachungaji wawe na dhamiri safi kwa sababu alisisitiza suala hili mara tatu zaidi katika nyaraka zake za kichungaji kwa Mchungaji Timotheo, ikiwemo “dhamiri njema” (1 Timotheo 1:5) na “dhamiri safi.” (1 Timotheo 3:8-9; 2 Timotheo 1:3).
Kauli ya Imani
Utakatifu wa Kikristo huanza wakati mwenye dhambi anapotubu na kubadilishwa na neema ya Mungu. Muumini huyo anakua kiroho kadiri anavyozidi kukua katika uelewa wake wa mapenzi ya Mungu na kuendelea kutii. Utakaso ni kazi ya Mungu ambapo anamtakasa muumini na kumwezesha kuwa na tabia takatifu na maisha matakatifu.
Mazoezi ya Somo la 11
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Isaya 6:1-8
Matendo 2:1-18
1 Wakorintho 10:1-13
1 Wathesalonike 5:14-24
Tito 2:11-14
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo la 11. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 11
(1) Je, ni nini maana ya msingi ya neno takatifu?
(2) Je, inamaanisha nini Mungu kuwa mtakatifu?
(3) Je, kwa nini utakatifu ni muhimu kwa ibada?
(4) Je, utakatifu wa Kikristo huanza wakati gani?
(5) Je, inamaanisha nini kuenenda katika nuru?
(6) Je, ni nini kinatokea kwa muumini wakati wa mchakato wa utakaso wa maisha yote?
(7) Je, upotovu wa kurithi ni nini?
(8) Je, muumini anawezaje kukosa lawama katika mwili, nafsi na roho wakati Bwana atakaporudi?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.