► Someni Zaburi ya 85 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu wokovu?
Msalaba
Ishara muhimu zaidi ya Kikristo ni msalaba. Msalaba unawakilisha tukio ambalo ni kitovu cha historia yote. Msalaba unawakilisha tofauti kati ya imani ya Kikristo na imani zingine zote.
Msalaba ni fumbo kwa watu wengi. Hawaelewi kwa nini Yesu alikufa. Hata wakisikia kwamba alikufa kwa sababu anatupenda na anataka kutuokoa, hawaelewi kwa nini hilo lilihitajika. Wanauliza, “Ikiwa Mungu alitaka kutusamehe, kwa nini hakufanya tu hivyo?”
Mkanganyiko kuhusu msalaba ulianza tangu mwanzo, wakati Wakristo wa kwanza walianza kuhubiri injili. (Soma 1 Wakorintho 1:22-23.) Wayahudi walifikiri kwamba Mungu
angejionyesha kuwa mwenye nguvu. Walifikiri wokovu waliohitaji ni ukombozi kutokana na ukandamizaji, lakini msalaba ulionekana kuonyesha udhaifu na kushindwa.
Wagiriki walifikiri kwamba Mungu angejionyesha kuwa mwenye hekima. Walifikiri wokovu waliohitaji ulikuwa ni maelezo kuhusu jinsi ya kupata kilicho bora zaidi maishani, lakini msalaba ulionekana kuwa upumbavu na kushindwa.
► Je, kwa nini baadhi ya watu wanachukizwa na msalaba?
Msalaba ni chukizo kwa watu wengi. Watu wengi wako tayari kushikilia dini. Wako tayari kuamini mambo fulani, kufuata desturi za kidini, na kupata ushauri. Lakini wanakasirishwa na wazo kwamba wao ni wenye dhambi sana kiasi kwamba msalaba ulihitajika ili wapate msamaha. Wanafikiri Mungu hapaswi kupinga matendo au tabia zao. Msalaba unawachukiza kwa sababu unamaanisha kwamba wao ni wenye dhambi wanaohitaji msamaha.
Ili kuelewa kifo cha Yesu kama dhabihu msalabani, ni lazima tuelewe kwamba hali ya mwanadamu mwenye dhambi na asili takatifu ya Mungu vilisababisha mtanziko mkubwa. Ni lazima tuelewe kwa nini upatanisho ulimfanya Mungu aweze kusamehe.
Hali ya Mwanadamu
[1]Kwa sababu ya dhambi ya Adamu, kila mtu tayari ametenganishwa na Mungu anapozaliwa (Warumi 5:12). Hiyo ina maana kwamba kila mtu ni mbinafsi na anafuata njia zake mwenyewe.
Mara tu mtu anapoanza kufanya maamuzi, anaanza kutenda dhambi. Kila mwenye dhambi ana hatia ya kutenda matendo mengi ya dhambi. (Soma Warumi 3:23.)
Dhambi ni ukiukaji wa sheria ya Mungu (1 Yohana 3:4; Yakobo 2:10-11). Kwa sababu Mungu ni mwenye kuzingatia haki kikamilifu, hapuuzi dhambi, na kila mtu atahukumiwa kwa kile alichokifanya (2 Wakorintho 5:10; Ufunuo 20:12-13). Hakuna shaka yoyote kuhusu hatia ya mtu yeyote au hukumu anayostahili. Kila mtu asiyeamini tayari ameshahukumiwa. (Soma Yohana 3:18-19.)
Mwenye dhambi ambaye hajatubu ni adui wa Mungu (Warumi 5:10). Mwenye dhambi hawezi kuingia katika uhusiano na Mungu isipokuwa makosa yake dhidi ya Mungu yaondolewe.
Mwenye dhambi pia yuko katika hali inayomfanya asistahili kuwa na uhusiano na Mungu. Mwenye dhambi amepotoka katika matamanio yake (Waefeso 2:3). Kwa sababu yeye ni mtumwa wa dhambi, mwenye dhambi hana uwezo wa kubadilisha hali yake. (Soma Warumi 6:20; Warumi 7:23.)
Hivyo, mwenye dhambi anahitaji wokovu gani? Kwa sababu mwenye dhambi ana hatia, wokovu unamaanisha msamaha. Kwa sababu yeye ni adui wa Mungu, wokovu unamaanisha upatanisho. Kwa sababu amepotoka, wokovu unamaanisha utakaso. Kwa sababu hana uwezo, wokovu unamaanisha ukombozi. Hivi ni baadhi tu ya vipengele vichache vya wokovu ambavyo mwenye dhambi anahitaji.
“Jinsi mwenye dhambi anavyoweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu ni suala muhimu kwa kila mtu, kwani hakuwezi kuwa na amani ya kweli au furaha ya kudumu wakati sisi ni maadui wa Mungu, iwe ni wakati wa sasa au katika umilele.”
John Wesley
“Kuhesabiwa Haki kwa Imani”
Mtanziko
Watu hawangeweza kulipia gharama ya dhambi zao wenyewe. Sababu moja ni kwamba kila kitu tulicho nacho tayari ni cha Mungu. Sababu muhimu zaidi ni kwamba dhambi ni kosa dhidi ya Mungu asiye na kikomo, na wanadamu hawana kitu chochote chenye thamani isiyo na kikomo wanachoweza kutumia kulipia dhambi zao.
Hakukuwa na chochote kabisa ambacho watu wangeweza kufanya kuhusu hitaji lao; hivyo, hakuna sharti lolote lingeweza kuwekwa ambalo lingeweza kutimiza wokovu. (Soma Wagalatia 3:21.) Ikiwa watu wangeweza kutimiza wokovu wao wenyewe, Yesu asingehitaji kufa msalabani. (Soma Wagalatia 2:21.)
► Ikiwa Mungu alitaka kusamehe, kwa nini hakusamehe tu bila msalaba?
Kwa sababu Mungu ni mtakatifu na mwenye kuzingatia haki, lazima ahukumu kulingana na ukweli na haki (Warumi 2:5-6). Neno upatanisho linarejelea ukweli kwamba kujitoa kwa Yesu kama dhabihu ndio njia yetu ya kupatanishwa na Mungu.
Fikiria kama Yesu asingejitoa kama dhabihu. Je kama Mungu angesamehe tu dhambi bila upatanisho?
Ikiwa Mungu angesamehe dhambi bila upatanisho, ingeonekana kana kwamba dhambi si muhimu. Ingeonekana kana kwamba Mungu si mwenye kuzingatia haki, wala si mtakatifu. Ingeonekana kana kwamba machoni pa Mungu kuna tofauti ndogo kati ya mtu anayefanya mema na mtu anayefanya maovu.
Kama msamaha ungetekelezwa bila upatanisho, Mungu asingeweza kuabudiwa kama Mungu anayezingatia haki na mtakatifu jinsi alivyo. Msamaha bila upatanisho hatimaye ungemkosea Mungu heshima badala ya kumheshimu, hivyo hilo lisingeweza kufanyika.
Lakini Mungu ni mwenye upendo na anataka kusamehe. Hakutaka kuwaacha wanadamu wote katika hali ya dhambi, wapotee milele, ingawa hilo ndilo walilostahili.
Kujitoa kwa Yesu kama dhabihu msalabani kulitoa dhabihu yenye thamani isiyo na kikomo ambayo ilihitajika. Yesu alistahili(1)kwa sababu ya kutokuwa na dhambi (mkamilifu na asiyehitaji wokovu yeye mwenyewe, 2 Wakorintho 5:21), na (2) kwa sababu ya kuwa Mungu na mwanadamu.
Upatanisho unatoa kile kinachohitajika kama msingi wa msamaha. Sasa Mungu anaweza kumsamehe mtu anayetubu na kuamini ahadi yake. Hakuna mtu anayeelewa dhabihu ya msalabani anaweza kufikiri kwamba dhambi si jambo zito kwa Mungu.
Upatanisho unatoa njia ambayo kwayo Mungu anayezingatia haki anaweza kumhesabia haki mwenye dhambi anayeamini ahadi yake. (Soma Warumi 3:26.) Warumi 3:20-26 inatoa maelezo ya kimantiki kuhusu jinsi upatanisho unavyofanya kazi.
Biblia inatuambia kwamba njia ya wokovu ambayo Mungu alitoa ndio njia pekee kabisa. Ikiwa mtu anakataa wokovu kwa neema kwa njia ya imani katika Kristo, hawezi kuokolewa. (Soma Marko 16:15-16; Matendo 4:12; Waebrania 2:3.)
Ndio maana ni muhimu kujua kanuni ya wokovu kwa neema pekee, unaopokewa kwa imani pekee. Wokovu ni kwa neema pekee kwa sababu hakuna tunachoweza kufanya ili kuustahili. Ni kwa imani pekee kwa sababu hakuna kitu tunachoweza kufanya ili kuutimiza. Tunaweza tu kuamini ahadi ya Mungu.
Neema ya Kwanza
► Je, ni nani anayechukua hatua ya kwanza kwa ajili ya wokovu wa mtu, Mungu au mtu mwenyewe?
Mungu amechukua hatua za kwanza za kumleta mwenye dhambi kwenye wokovu. Alionyesha nia yake ya kusamehe kwa kutoa dhabihu ya Yesu msalabani. Sasa neema ya Mungu inafika ndani ya moyo wa mwenye dhambi, ikimsadikisha juu ya dhambi zake na kumfanya atamani msamaha. (Soma Tito 2:11; Yohana 1:9; Warumi 1:20.) Mwenye dhambi hana uwezo wa kuacha dhambi zake bila msaada wa Mungu (Yohana 6:44). Mungu humpa mwenye dhambi uwezo wa kuitikia injili. Ikiwa mtu hajaokoka, si kwa sababu hakupewa neema, bali ni kwa sababu amekataa kutikia neema ambayo Mungu amempa.
Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote, na Mungu anataka kila mtu aokolewe. (Soma 2 Petro 3:9; 1 Yohana 2:2; 1 Timotheo 4:10.) Neema ya Mungu humpa kila mtu uwezo wa kuitikia, lakini hamlazimishi yeyote. Ndio maana Mungu anamhamasisha mwenye dhambi kuchagua kutubu na kuamini (Marko 1:15).
Toba
► Toba ni nini?
Kutubu ni kugeuka na kuchukua mwelekeo tofauti. Kitheolojia, ina maana kwamba mwenye dhambi anajiona kuwa ana hatia na anastahili adhabu, lakini yuko tayari kuacha dhambi zake.
Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa (Isaya 55:7).
Kutubu hakumaanishi kwamba mwenye dhambi ni lazima arekebishe maisha yake na awe mwenye haki kabla ya Mungu kumsamehe. Hilo haliwezekani. Lakini mwenye dhambi lazima awe tayari kumruhusu Mungu amkomboe kutokana na dhambi zake.
► Wokovu hupokewa kwa neema, basi kwa nini toba ni muhimu kwa wokovu?
Imani ndio sharti pekee la msamaha, lakini imani kwa ajili ya wokovu haiwezi kuwepo bila toba. Ikiwa mtu hataki kutubu, hataki kuokolewa kutokana na dhambi.
Ikiwa Mungu angewasamehe watu wanaoendelea kutenda dhambi na wamekataa kutubu, hilo lingemwondolea heshima yake kama hakimu wa dunia anayezingatia haki. Toba inahitajika, kwa sababu ikiwa mtu hatatubu, basi hakubali uovu wa dhambi. Ikiwa haoni kwa nini anapaswa kujitenga na dhambi, basi haoni kwa nini anahitaji msamaha.
Ikiwa mtu hajaona kuwa kweli ana hatia, hawezi kujitetea, na anastahili adhabu, hajatubu kikamilifu. Ikiwa anakiri kwamba yeye ni mwenye dhambi lakini anataka kuendelea kutenda dhambi, toba yake haijakamilika, kwa sababu anataka kuendelea kufanya yale ambayo alisema hayataki.
Imani Inayookoa
[1]► Ikiwa mtu ana imani inayookoa, anaamini nini?
Ikiwa mtu ana imani inayookoa, anaamini kwamba:
(1) Hawezi kufanya lolote ili kujihesabia haki.
Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu (Waefeso 2:8-9).
Anatambua kwamba hakuna chochote anachoweza kufanya (matendo) kitamfanya astahili kuokolewa, hata kwa kiasi fulani.
(2) Dhabihu ya Kristo inatosha kwa ajili ya msamaha wake.
Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote (1 Yohana 2:2).
Kipatanisho inamaanisha dhabihu inayotuwezesha kusamehewa. Hakuna kitu chochote kinachohitajika mbali na kujitoa kwa Yesu kama dhabihu kwa ajili ya msamaha wetu.
(3) Yesu alifufuka kutoka kwa wafu, akishinda dhambi na mauti.
…Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka (Warumi 10:9).
Njia pekee ambayo kwayo dhambi na mauti vingeweza kushindwa ilikuwa ni kufufuka kwa Yesu. Yesu alifufuka, akithibitisha ushindi wake kamili dhidi ya vitu hivyo viwili.
(4) Mungu anamsamehe kwa msingi wa imani pekee.
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote (1 Yohana 1:9).
Ikiwa mtu anafikiri kuna masharti mengine ya wokovu, anatarajia kuokolewa kwa kiasi fulani kwa matendo badala ya kuokolewa na neema pekee.
Hakikisho
► Je, ni jinsi gani watu wanaweza kujua kwa uhakika kwamba ameokoka?
Watu wengine hutegemea hisia zao, lakini hisia zinaweza kubadilika na zinaweza kupotosha.
Biblia inatuambia kwamba tunaweza kujua kwa hakika kwamba tumeokolewa (1Yohana 5:13). Tunaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu ametukubali. Hatupaswi kuishi kwa hofu, kwa sababu Roho wa Mungu anatuhakikishia kwamba tumekuwa watoto wa Mungu. Mtume Paulo anasema kwamba Roho Mtakatifu hushuhudia roho zetu za kibinadamu kwamba sisi ni watoto wa Mungu (Warumi 8:15-16).
Hakikisho hili ni kamili sana kiasi kwamba hatupaswi kuogopa Siku ya Hukumu. (1 Yohana 4:17) Watu wengine husema kwamba wanatumaini kwamba watakubaliwa mbinguni, lakini tunaweza kuwa na hakikisho bora zaidi kuliko hilo. Haitoshi kuamini kwamba wokovu umetolewa kwa wanadamu kwa ujumla; mtu lazima ajue kwamba yeye mwenyewe ameokolewa.
Maisha yaliyobadilika ni ushahidi kwamba mtu ameokolewa, lakini ushahidi huo hauonekani hapo mwanzoni. Matokeo ya wokovu hayajapata wakati wa kuonekana. Hivyo, wakati wa kutubu, maisha yaliyobadilika si msingi wa uhakikisho.
Muumini anaweza kuwa na uhakika na wokovu wake kwa kujua kwamba amefuata njia ya kimaandiko ya wokovu. Ikiwa mtu ametubu kikweli na kuamini jinsi Biblia inavyoelekeza, ana haki ya kuamini kwamba Mungu amemsamehe na amekuwa mtoto wa Mungu.
Ikiwa mtu anajaribu kuhisi kwamba ameokoka wakati hajatubu kikweli, atachanganyikiwa na anaweza kujidanganya mwenyewe.
Ikiwa mtu (1) ametubu kikweli, (2) anatumainia ahadi za Mungu katika maandiko, na (3) amepokea ushuhuda wa Roho, hatadanganyika. Msingi wa hakikisho hilo ni Neno la Mungu, ambalo linategemeka kabisa. Mungu daima hutimiza ahadi zake.
“Imani inayookoa ni imani inayopumzisha,
tumaini ambalo
linamtegemea Mwokozi
kikamilifu.”
John Stott
Maneno 10 ya Vipengele vya Wokovu
Upatanisho: Neno hili linamaanisha kwamba wale waliokuwa maadui hapo awali sasa wana amani kati yao. Katika wokovu, Mungu hutupatanisha na yeye na tunakuwa na amani naye. (Soma 2 Wakorintho 5:19; Warumi 5:1. Vifungu hivi vinazungumza kuhusu kuhesabiwa haki na upatanisho.)
Kufidia: Neno hili linamaanisha kuwa rekodi fulani imefutwa. Katika wokovu, rekodi yetu ya dhambi inafutwa. (Soma Waebrania 8:12.)
Uridhisho: Neno hili linarejelea kitu ambacho kilitolewa ili kuzuia ghadhabu ya mtu fulani. Katika wokovu, kujitoa kwa Yesu kama dhabihu kunazuia ghadhabu ya Mungu ya haki iliyokuwa dhidi yetu. (Soma 1 Yohana 2:2.)
Kuwekwa Huru: Neno hili linamaanisha kwamba mtu ameokolewa kutoka kwenye nguvu za mwingine. Katika wokovu, tumeokolewa kutoka kwenye nguvu za Shetani na dhambi. (Soma Luka 1:74; Waroma 6:6, 12-18.)
Ukombozi: Neno hili linamaanisha kwamba kuna gharama ililipwa ili mtu awe huru. Katika wokovu, kifo cha Yesu ndio gharama iliyolipwa ili tuwe huru kutokana na utumwa na adhabu ya dhambi. (Soma Waefeso 1:7; Tito 2:14.)
Kuhesabiwa Haki: Neno hili linamaanisha kwamba mtu fulani anatangazwa kuwa mwenye haki, au hana hatia. Katika wokovu, mwenye dhambi aliye na hatia anahesabiwa kuwa mwenye haki kwa sababu Yesu aliteseka kwa niaba yake. (Soma Warumi 5:1; 2 Wakorintho 5:19. Vifungu hivi vinazungumza kuhusu kuhesabiwa haki na upatanisho.)
Utakaso: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anafanywa mtakatifu. Katika wokovu, mwenye dhambi aliye na hatia anabadilishwa kuwa mtoto mtakatifu wa Mungu. Nyaraka nyingi zinawarejelea waumini kuwa “watakatifu.” (Soma Waefeso 1:1, Wafilipi 1:1, Wakolosai 1:2.)
Kufanywa Wana: Neno hili linamaanisha mtu anakuwa mtoto halali wa mtu mwingine. Katika wokovu tunafanyika watoto wa Mungu. (Soma Yohana 1:12; Waroma 8:15.)
Kuongoka / Kuzaliwa Upya: Neno hili linamaanisha mtu anaanza maisha upya. Katika wokovu muumini huanza maisha mapya kupitia ufufuo wa maisha ya kiroho ndani yake. (Soma Waefeso 2:1; Yohana 3:3, 5.)
Kutiwa Muhuri: Neno hili linamaanisha kitu kilichotiwa alama ili kuonyesha ni nani anayekimiliki. Katika wokovu, Roho Mtakatifu ndani yetu hututambulisha kama watu wa Mungu. (Soma Waefeso 1:13-14.)
Makosa ya Kuepuka: Dini Bila Toba
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshirika wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Kuna aina ya mtu anayefikiri kwa urahisi kwamba ameokolewa anaposikia kwamba wokovu ni kwa neema kupitia imani. Hajatubu kikweli kwa sababu hakuona kwamba anahitaji kufanya hivyo. Hakujiona kamwe kuwa mwenye dhambi anayestahili hukumu ya Mungu. Anafikiri neema inamaanisha kwamba anaweza kufuata njia zake mwenyewe. Kwa sababu anakubali ukweli wa Ukristo, anafikiri yeye ni Mkristo, ingawa maisha yake hayajabadilika. Hakusalimisha mapenzi yake; badala yake, alimkubali Mungu kama sehemu ya maisha yake, na bado anaishi kwa kiwango kikubwa kulingana na mapenzi yake mwenyewe. Huu si mwanzo wa uhusiano unaookoa na Mungu, kulingana na maelezo ya maandiko.
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Maisha, kifo na ufufuo wa Yesu Kristo vinatoa upatanisho kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Kila mtu ana hatia ya dhambi na hana uwezo wa kujiokoa. Kila mwenye dhambi anayetubu anaweza kupokea neema ya Mungu kwa imani. Muumini anasamehewa na kuwekwa huru kutokana na nguvu na adhabu ya dhambi. Roho Mtakatifu humbadilisha muumini kutoka kuwa mwenye dhambi na kuwa mwabudu mtakatifu wa Mungu. Hakuna njia nyingine ya wokovu. Uumbaji kwa ujumla umekombolewa na hatimaye utarejeshwa na Mungu.
Wokovu katika Agano la Kale
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Sehemu hii na sehemu inayofuata ni za hiari. Wanafunzi wanaweza kuzizingatia ikiwa wanataka kushughulikia mada hizi.
Katika Agano la Kale, Mungu alitoa utaratibu wa ibada na dhabihu. Dhabihu hazikutoa wokovu kwa njia sawa na kifo cha Yesu. Biblia inatuambia kwamba “haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi” (Waebrania 10:4). Basi kwa nini dhabihu zilitolewa? Zilikuwa ni aina za ibada zilizoashiria dhabihu ya Kristo itakayokuja katika siku zijazo (Waebrania 10:1).
Hiyo haimaanishi kwamba wokovu haukupatikana hadi katika enzi ya Agano Jipya. Mtume Paulo alipoeleza kanuni ya kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani, alitoa mifano ya Abrahamu na Daudi kuonyesha kwamba hilo halikuwa wazo jipya (Warumi 4:1-8). Yesu alisema kwamba Nikodemo alipaswa kujua kuhusu kuzaliwa upya kwa sababu alikuwa mwalimu wa Agano la Kale (Yohana 3:10). Paulo alimwambia Timotheo kwamba maandiko ya Agano la Kale yanaweza kumfanya awe na hekima kuhusu wokovu (2 Timotheo 3:15). Kwa hivyo, injili ilipatikana katika Agano la Kale ingawa haikuelezwa kwa uwazi kama katika Agano Jipya.
Kulikuwa na watu katika enzi ya Agano la Kale ambao walielewa neema. Hawakujua kwa kina kuhusu upatanisho au jinsi unavyofanya kazi, lakini waliamini kwamba Mungu alikuwa akitoa msingi wa msamaha. Dhabihu zilikuwa namna ya kuonyesha imani hiyo, kama vile tuna aina za ibada leo (kwa mfano, Meza ya Bwana). Dhabihu hazikuwa na thamani kama hazikutolewa kwa imani na utiifu, kama vile ibada zetu hazina thamani ikiwa hazidhihirishi moyo na maisha ambayo yamejinyenyekeza kwake Mungu. Zaburi 51 na Isaya 1:11-18 zinaonyesha kwamba toba na imani zilikuwa muhimu katika enzi ya Agano la Kale.
Zaburi 85, iliyoandikwa miaka mingi kabla ya kutokea kwa wa Kristo kutokea, inaeleza kwa uzuri neema ya Mungu na jinsi Mungu anavyosamehe dhambi. Inazungumza juu ya hasira yake kumalizika. Zaburi 85:10 inasema, “Fadhili na kweli zimekutana, haki na amani zimehusiana.” Hii ni taswira nzuri sana ya wokovu kupitia upatanisho. Bila upatanisho, rehema ya Mungu ingezuiwa na ukweli kwamba tuna hatia. Haki ya Mungu ingetufanya tuwe maadui wake badala ya kuruhusu amani kati yetu na yeye. Katika upatanisho, haki inatimizwa, na rehema inaonyeshwa.
Wokovu wa Uumbaji Wote
Maneno kuokolewa au wokovu yanatumika kwa mapana katika Biblia. Yanarejelea zaidi ya wokovu wa kibinafsi tu, ambao umeelezwa katika somo hili. Maneno haya yanarejelea kile kilichotekelezwa hapo zamani (Waefeso 2:8), kile kinachotendekea sasa (1 Wakorintho 1:18), na kile kitakachotendeka siku zijazo (Marko 13:13). Dhana ya wokovu inaweza kurejelea kile kinachowatendekea watu binafsi (ambacho ndicho kilichosisitizwa katika somo hili)
lakini pia inaweza kurejelea kile kinachotendekea vikundi vya watu, kama vile Wayahudi (Warumi 1:16), Mataifa (Warumi 11:11), nyumba (Luka 19:9), au familia (Waebrania 11:7), au inaweza kurejelea mtu anayeokolewa kutokana na hatari inayoweza kumdhuru kimwili (Mathayo 14:30).
Watu wa kwanza walipofanya dhambi, laana ilingia juu ya uumbaji wote (Mwanzo 3:17). Wokovu utakapokamilika, uumbaji pia utarejeshwa.
Wokovu huanza na kufanywa upya kiroho. Waumini wanaokolewa kutokana na dhambi, na wanaishi katika baraka za Mungu. Hata hivyo, bado hawajapata kuwekwa huru kutokana na athari za kimwili za laana ya dhambi. Bado wana miili inayozeeka na kufa.
Asili bado iko chini ya laana ya dhambi. Hatujaona ulimwengu jinsi Mungu alivyouumba hapo mwanzoni. Tunaona asili ambayo imejaa viumbe hatari na viumbe walio na migogoro kati yao. Katika ulimwengu wetu, viumbe wengi lazima wafe ili wengine waishi.
Wakati unakuja ambapo uumbaji wote utafanywa upya (Ufunuo 21:1; Waebrania 1:10-12). Warumi 8:18-25 inaeleza tumaini la Kikristo la ulimwengu uliowekwa huru kutokana na laana ya dhambi.
Mazoezi ya Somo la 8
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Zaburi 51
Isaya 1:11-18
Warumi 3:20-26
Warumi 8:19-25
Waefeso 2:1-10
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 8. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 8
(1) Je, kwa nini msalaba ni chukizo kwa watu wengi?
(2) Orodhesha mambo manne ambayo ni ya kweli kuhusu kila mwenye dhambi asiyetubu.
(3) Je, kwa nini msamaha bila upatanisho haumletei Mungu heshima?
(4) Je, ni kwa njia gani mbili Yesu alistahili kipekee kuwa dhabihu?
(5) Je, mtazamo wa mwenye dhambi anayetubu ni upi?
(6) Mtu akiwa na imani inayookoa, anaamini nini?
(7) Je, mtu anawezaje kujua kwa uhakika kwamba ameokoka?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.