► Someni Zaburi 139 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu Roho wa Mungu?
[1]Watu wengine hufikiri kwamba Roho Mtakatifu ni kitu kinachochochea tu hisia zao, nguvu wanayojaribu kutumia, nguvu isiyo na utu, au uwepo fulani tu. Kwa mfano, Shahidi wa Yehova atasema hivi: “Roho mtakatifu si mtu, wala si sehemu ya Utatu wa Mungu. Roho mtakatifu ni nguvu ya Mungu anayotumia kutimiza mapenzi yake.… Kwa kiasi fulani, inaweza kulinganishwa na umeme.”[2]
► Ni nini ambacho si sahihi kuhusu maoni ya Mashahidi wa Yehova kuhusu Roho Mtakatifu?
Mashahidi wa Yehova wanamwona Roho Mtakatifu kama nguvu isiyo na utu. Kwa sababu hawana ufahamu wa kibiblia juu ya Mungu, hawawezi kuwa na uhusiano sahihi naye.
Hatupaswi kutarajia kuelewa mambo yote kuhusu Roho Mtakatifu. Yesu alisema kwamba kazi ya Roho ni kama upepo; unaisikia, lakini hujui itokako wala iendako (Yohana 3:8). Lakini kuna mambo fulani ambayo tunaweza kujua kuhusu Roho, na ni muhimu katika uhusiano wetu na Mungu.
Sehemu ya maandiko inayotupa maelezo mengi zaidi kuhusu mwingiliano kati ya Roho Mtakatifu na kanisa [3]ni kitabu cha Matendo. Hapo tunaona mfano wa jinsi kanisa la hapo mwanzoni lilivyomwitikia Roho Mtakatifu.
1. Walimheshimu Roho Mtakatifu katika uungu wake. (Soma Matendo 5:3-4.)
2. Walikuwa na ufahamu wa uwepo, mwongozo, na kazi ya Roho Mtakatifu. (Soma Matendo 15:28.)
3. Walitambua utegemezi wao kwa Roho Mtakatifu na wajibu wao wa kumwitikia. (Soma Matendo 4:24, 31.)
Ili kuwa na uhusiano wa aina hiyo na Roho Mtakatifu, ni lazima tutambue kwamba yeye ni mtu na kwamba yeye ni Mungu.
“Tunamwamini Roho Mtakatifu aliyenena katika torati, na ambaye manabii walifundisha kumhusu, aliyeshuka Yordani, aliyezungumziwa na Mitume, na anakaa ndani ya watakatifu; hivi ndivyo tunavyoamini kumhusu: kwamba yeye ni Roho Mtakatifu, Roho wa Mungu, Roho kamili, Msaidizi, ambaye hakuumbwa, atokaye kwa Baba na kupokewa na Mwana,
ambaye tunamwamini.”
Kanuni ya Imani ya Epifania, Mwaka wa 374 B.K.
Roho Mtakatifu ni Mtu
Roho Mtakatifu hana mwili wa nyama kama Yesu, lakini yeye ni mtu. Mtu halisi ana sifa za utu, ambazo ni pamoja na akili, nia na hisia. Je, Roho Mtakatifu ana nia? Anagawa karama za kiroho kwa Wakristo kama apendavyo (1 Wakorintho 12:11). Je, Roho Mtakatifu ana akili? Yeye huchunguza kila kitu, hata mafumbo ya Mungu na kuyajua (1 Wakorintho 2:10). Je, Roho Mtakatifu ana hisia? Tunaambiwa tusimhuzunishe Roho Mtakatifu (Waefeso 4:30). Ikiwa Roho Mtakatifu anaweza kuhuzunishwa, basi ana hisia. Kwa sababu Roho Mtakatifu ana akili, nia na hisia, tunajua kwamba yeye ni mtu.
► Je, kwa nini ni muhimu kwetu kujua kwamba Roho Mtakatifu ni mtu?
Mtu mwenye utu ana uwezo kuwa na mahusiano na wengine. Kama Roho Mtakatifu ingekuwa nguvu isiyo na utu, tusingeweza kuwa na uhusiano naye. Lakini kulingana na Wafilipi 2:1 na 2 Wakorintho 13:14, Roho anaweza kuwa na ushirika nasi, hivyo lazima awe ni mtu.
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Kwa ushahidi zaidi wa Biblia kuhusu utu wa Roho Mtakatifu, tazama sehemu ya “Ushahidi wa Biblia Kuhusu Utu wa Roho Mtakatifu” mwishoni mwa somo hili.
Roho Mtakatifu Ni Mungu
Roho Mtakatifu ni Mungu mjua yote, anayeona yote na aliye kila mahali. Unakumbuka simulizi ya Anania na Safira? Kabla Anania hajauawa, Petro alimwambia, “Kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu…? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu” (Matendo 5:3-4). Kutokana na hayo, tunaona kwamba kumdanganya Roho Mtakatifu ni sawa na kumdanganya Mungu; kwa hivyo, Roho Mtakatifu ni Mungu.
Roho Mtakatifu anajua mambo yote. Tunaona katika 1 Wakorintho 2:10-11 kwamba anajua mambo yote ya Mungu. Hiyo inahitaji akili isiyo na kikomo. Alihamasisha maandiko ya Agano la Kale, ikiwemo unabii, ambayo ingehitaji maarifa yote. (Soma 2 Petro 1:21.) Tunaambiwa kwamba maandiko yana pumzi ya Mungu (2 Timotheo 3:16), hivyo Roho Mtakatifu ni Mungu.
Roho Mtakatifu yuko kila mahali. Zaburi 139:7-10 inatuambia kwamba hakuna mahali ambapo mtu anaweza kwenda ili kuepuka uwepo wa Roho wa Mungu. Yupo pamoja na kila muumini, kwa sababu Biblia inasema kwamba ikiwa mtu hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo (Warumi 8:9). Muktadha unaonyesha kwamba Roho wa Kristo ni Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu ana nguvu zote. Anafanya mambo ambayo Mungu pekee ndiye anaweza kufanya. Anasadikisha ulimwengu juu ya dhambi, haki, na hukumu (Yohana 16:8). Ili kufanya hivyo, lazima aweze kufikia dhamiri ya kila mtu na kushawishi akili zao kuhusu kweli fulani. Pia ana uwezo wa kumpa kila muumini nguvu ya ndani. (Soma Waefeso 3:16.) Roho huzaa matunda ya kiroho katika maisha ya kila muumini, kila mahali ulimwenguni. (Soma Wagalatia 5:22-23.) Hakuna kitu kingine kingeweza kufanya hivyo isipokuwa nguvu za kiungu.
Tunaambiwa katika Luka 12:10 kwamba Roho Mtakatifu anaweza kukufuriwa. Mungu pekee ndiye anayeweza kukufuriwa, kwa hivyo Roho Mtakatifu lazima awe ni Mungu.
Roho Mtakatifu ni wa milele (Waebrania 9:14).
Miili yetu inaitwa hekalu la Mungu kwa sababu Roho Mtakatifu anaishi humo (1 Wakorintho 3:16).
Kutokana na ushahidi wa Biblia, tunajua kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe, nafsi ya tatu ya Utatu wa Mungu.
► Je, kwa nini ni muhimu kwetu kuamini uungu wa Roho Mtakatifu?
Ni muhimu kuamini uungu wa Roho Mtakatifu ili uweze kumpa heshima anayostahili. Ni kosa kubwa sana kukataa kumwabudu Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu Ni Tofauti na Baba na Mwana
Kusema kwamba Roho Mtakatifu ni tofauti na Baba na Mwana hakumaanishi kwamba wao ni tofauti kama vile ilivyo katika wanadamu. Kila mtu wa Utatu wa Mungu anaishi ndani ya mtu mwiingine na watu wote ni Mungu mmoja, lakini wako tofauti vya kutosha kiasi kwamba wanaweza kusemezana, kupendana, na kuwa na mahusiano ya kweli na ya kibinafsi kati yao na kati yao na sisi.
Maandiko yanafundisha tofauti kati ya nafsi za Utatu wa Mungu. Kwa mfano, tena na tena katika Yohana 14-16, Yesu alizungumza kuhusu Msaidizi atakayemtuma atakaporudi kwa Baba. (Soma Yohana 14:16-17, 26; Yohana 15:26; Yohana 16:7, 13-15.) Msaidizi huyo atawaongoza na kuwafundisha wanafunzi. Ikiwa Yesu na Roho Mtakatifu wangekuwa mtu mmoja, Yesu kumtaja Roho Mtakatifu kama msaidizi mwingine kusingekuwa na maana. Bila shaka Yesu alikuwa akimzungumzia mtu mwingine aliye tofauti naye.
Yesu alisema kwamba Roho Mtakatifu hatanena kwa mamlaka yake mwenyewe bali atafunua mambo ya Kristo, ambayo Kristo aliyapokea kutoka kwa Baba (Yohana 16:13-15). Ikiwa Yesu na Baba wangekuwa mtu mmoja na Roho Mtakatifu, kauli hii isingekuwa na maana.
Yesu alipobatizwa, sauti kutoka mbinguni ilisema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu,” na Roho Mtakatifu, kama njiwa, akashuka juu ya Yesu (Marko 1:10-11). Washiriki wote watatu wa Utatu wanahusika kwa wakati mmoja katika tukio hili, kila mmoja akiwa tofauti na wenzake.
Kama mtu tofauti, Roho Mtakatifu siku zote ameishi katika uhusiano wa upendo na Baba na Mwana. Mungu alituumba ili tushiriki katika uhusiano huo. Mungu anataka tufurahie ushirika naye (1 Yohana 1:3-4), kwani kila mshiriki wa Utatu wa Mungu amefurahia ushirika na wale washiriki wengine tangu kabla ya mwanzo wa wakati. (Soma Yohana 17:22-23.)
Roho Mtakatifu Anafanya Kazi
Tangu wakati wa Uumbaji, Roho Mtakatifu amekuwa akifanya kazi ulimwenguni. Alikuwepo na alihusika dunia ilipoumbwa (Mwanzo 1:2, 26). Alitoa uwezo maalum kwa watu walioitwa
kufanya kazi maalum (Kutoka 35:30-31; Waamuzi 3:9-10; Waamuzi 15:14-15). Alitoa jumbe kwa manabii (Isaya 61:1). Alihamasisha maandiko (2 Petro 1:21). Siku zote amekuwa akifanya kazi katika mioyo ya watu, akijaribu kuwaelekeza kwa Mungu (Matendo 7:51).
Anaitwa Roho wa uzima. (Soma Waroma 8:2.) Yeye ndiye Roho aliyetuumba na kutupa uhai. Kama angejiondoa kutoka katika ulimwengu, uhai wote ungekoma, na mwanadamu angerudi mavumbini. (Ayubu 33:4; Ayubu 34:14-15.)
Agano Jipya lilianzisha kipengele kipya cha kazi ya Roho Mtakatifu. Yohana Mbatizaji alisema kwamba Yesu atawabatiza watu kwa Roho Mtakatifu (Mathayo 3:11). Yesu aliwaambia wanafunzi wake watarajie ahadi ya Baba, ubatizo wa Roho Mtakatifu ambao ulifanyika siku ya Pentekoste (Matendo 1:4-5, 8).
Yesu aliwaahidi wanafunzi kwamba Roho Mtakatifu atakuwa pamoja nao, akiwakumbusha mambo ambayo Yesu alifundisha na kuwaongoza katika ukweli (Yohana 14:26, Yohana 16:13). Yesu alisema kwamba Roho Mtakatifu atakuwa Msaidizi mwingine (Yohana 14:16, 26; Yohana 15:26; Yohana 16:7). Neno la Kigiriki ambalo Yesu alitumia linarejelea mtu aliye pamoja nasi, anayetutia moyo na kutusaidia. Neno hilo linaweza pia kurejelea mwakilishi. Roho Mtakatifu anamwakilisha Yesu na hutukumbusha maneno yake.[1]
► Je, baadhi ya mambo yanayofanywa na Roho Mtakatifu ni yapi?
Kazi ya Roho Mtakatifu ulimwenguni haiwezi kuelezwa kikamilifu, lakini hii hapa ni orodha ya baadhi ya kazi zake.
1. Anasadikisha juu ya dhambi (Yohana 16:8; 1 Wakorintho 2:4; 1 Wathesalonike 1:5). Vinginevyo isingewezekana mtu kutambua kwamba anahitaji kutubu na kusamehewa.
2. Anamwezesha mtu kuzaliwa upya, akimpa uzima mtu ambaye alikuwa mfu katika dhambi (Tito 3:5; Waefeso 2:1; Yohana 3:5).
3. Anampa muumini hakikisho la kibinafsi kwamba ameokolewa (Warumi 8:16).
4. Anaishi ndani ya kila muumini (kila mtu aliyeokoka ana Roho Mtakatifu) (Warumi 8:9; 1 Wakorintho 6:19).
5. Anawezesha uelewa wa ukweli wa Mungu (1 Wakorintho 2:9-10, 13-14; 2 Wakorintho 3:14-17; Waefeso 6:17).
6. Anawaita watu kwenye huduma maalum na kuongoza maamuzi katika huduma (Mdo 13:2-4, Mdo 15:28, Mdo 16:6-10).
7. Anamtakasa muumini, akiusafisha moyo wake ili kumfanya awe mtakatifu (Matendo 15:8-9; 1 Petro 1:2).
8. Anatoa uwezo wa kuishi kwa ushindi dhidi ya dhambi (Warumi 8:1, 5, 13; Wagalatia 5:16).
9. Anazaa matunda ya kiroho katika maisha ya muumini (Wagalatia 5:22-23).
10. Anatoa karama kwa ajili ya huduma (1 Wakorintho 12:4-10, 28-30; Warumi 12:6-8; 1 Petro 4:10-11).
11. Anatoa upako maalum wa nguvu kwa ajili ya huduma (Matendo 1:8, Matendo 13:9; Wagalatia 3:5; 1 Petro 1:12).
12. Anamsaidia muumini kuomba kulingana na mapenzi ya Mungu (Warumi 8:26-27; Waefeso 6:18).
13. Anakuza umoja na ushirika wa kanisa (Waefeso 4:3; Wafilipi 2:1).
[1]Neno hilo hilo liko katika 1 Yohana 2:1, inayosema kwamba Yesu ni mwakilishi wetu kwa Baba.
Baadhi ya Kanuni kuhusu Karama za Kiroho
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshirika wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
1. Roho hufanya kazi kupitia karama, shughuli na usimamizi mbalimbali (1 Wakorintho 12:4-6).
2. Karama za kiroho zinagawanywa kulingana na mapenzi ya Mungu, si kulingana na hali ya kiroho ya mtu (1 Wakorintho 12:11, 1 Wakorintho 4:7).
3. Kila mtu ana uwezo fulani aliopewa na Roho (1 Wakorintho 12:7).
4. Hakuna karama ambayo kila muumini anatarajiwa kuwa nayo (1 Wakorintho 12:8-11, 14-30).
5. Karama siku zote zinapaswa kutumiwa kwa ajili ya kuwatumikia wengine kwa utukufu wa Mungu (1 Wakorintho 12:21-22, 25; 1 Petro 4:10-11).
Karama ya Lugha
Si Wakristo wote wanakubaliana kuhusu matumizi ya karama ya lugha. Wakristo wengine wanaamini kwamba kila muumini atanena kwa lugha atakapopokea Roho Mtakatifu.
Wakristo wengine wanaamini kwamba karama ya lugha hutolewa kwa baadhi ya waumini kwa ajili ya mawasiliano na watu wanaozungumza lugha tofauti. Wanaamini hivyo kwa
sababu siku ya Pentekoste wasemaji walieleweka katika lugha nyingi (Matendo 2:6). Wanaamini kwamba Mungu hutoa karama hiyo, na karama nyingine yoyote ya kiroho, kwa yeyote kama apendavyo (1 Wakorintho 12:4-11). Wanaamini kwamba hakuna karama moja ambayo kila muumini anapaswa kuwa nayo (1 Wakorintho 12:29-30), na kwa hivyo karama ya lugha haithibitishi kitu chochote kuhusu muumini husika (1 Wakorintho 14:22), ingawa kila muumini ana Roho Mtakatifu (Warumi 8:9).
Maoni tofauti kuhusu karama ya lugha yanaweza kuwazuia waumini kushirikiana kwa karibu katika aina fulani za huduma, lakini waumini hawapaswi kuhukumiana kuhusu maoni yao juu ya suala hili.
Roho Mtakatifu yuko katika Uhusiano na Muumini
Ikiwa uko katika uhusiano na Mungu, uko katika uhusiano na Roho Mtakatifu. Haiwezekani kujua nafsi moja tu ya Utatu wa Mungu. (Soma Waefeso 2:18; Yohana 6:44.)
Si lazima mtu aelewe kanuni ya Roho Mtakatifu kabla ya kuokoka. Wanafunzi hawakujua mengi kuhusu Roho, lakini Yesu aliwaambia kwamba wanamjua Roho na kwamba alikuwa pamoja nao tayari. (Soma Yohana 14:17.)
Kujua kanuni sahihi kuhusu Roho Mtakatifu hutusaidia kuhusiana naye kwa njia sahihi na humruhusu afanye mengi zaidi maishani mwetu. Kujua kwamba yeye ni mtu kunaturuhusu kujua kwamba tunaweza kuwa na uhusiano naye. Tunaweza kuzungumza naye, naye atazungumza nasi. Kwa kawaida haneni nasi kwa sauti inayosikika, lakini anatusaidia kuelewa mapenzi ya Mungu na upendo wa Mungu. Ikiwa kweli tunataka kufanya mapenzi ya Mungu, Roho Mtakatifu atatuongoza ingawa hatutahisi akifanya hivyo kila wakati.
Kujua kwamba yeye ni mtu kunamaanisha kwamba hatutatenda kana kwamba yeye ni nguvu au hisia fulani tu. Tunapomwabudu Mungu, tunafikiria yeye ni nani na jinsi alivyo, si kufurahia tu hisia fulani bila kutafakari. Tunapoomba, tunazungumza tukitumia akili na tunajaribu kuelewa kile anachoweza kutuonyesha badala ya kutumia maneno bila kufikiria, kwa njia ya kimazingaombwe, kama wanavyofanya watu wa dini nyingine.
Kujua kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu kunapaswa kutupatia mtazamo wa ibada yenye heshima kuu. Tunapoomba na kuhisi mwongozo wake, tunahitaji kukumbuka kwamba yeye ndiye Mungu anayetupenda, anatujua kikamilifu, na anajua mustakabali wetu. Yeye pia ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi, ambaye tunapaswa kumtii.
Yuko nasi wakati wote. Maandiko yanasema kwamba tunaishi katika Roho na tunapaswa kuenenda kwa Roho (Wagalatia 5:25). Tunapaswa kuishi kana kwamba tuko mbele zake, na tusifikiri kwamba tunakuja mbele zake kanisani tu. Hayuko pamoja nasi tu, bali pia anaishi ndani yetu. Hiyo ni sababu ya kutufanya tufahamu kwamba tunapaswa kuishi maisha safi na matakatifu. (Soma 1 Wakorintho 6:19.)
Ni lazima tukumbuke kwamba kipaumbele kikuu zaidi cha Roho ni kutupa ushindi dhidi ya dhambi na kutakasa mioyo yetu (Warumi 8:13; Wagalatia 5:16; Matendo 15:8-9). Hatupaswi kuomba kwa ajili ya mambo mengine ikiwa hatumruhusu atimize kipaumbele chake kikuu zaidi. Tunapaswa kuomba kwa imani, tukiamini kwamba atatufanya tuwe watakatifu kikamilifu. (Soma 1 Wathesalonike 5:23.)
Katika mapambano ya maisha, anatupa nguvu ya ndani (Waefeso 3:16). Anatuelewa, anaelewa hali zetu, na anaweza kutupa kile tunachohitaji.
Katika huduma, ni lazima tumtegemee ili atupe mwongozo, alipe nguvu Neno lake, na kutimiza matokeo ya kiroho katika mioyo ya wengine. Tunaona hayo katika kitabu cha Matendo. Hakuna uwezo wa kibinadamu unaoweza kuchukua nafasi ya kazi ya Roho.
Hata kama tayari umejazwa Roho, hupaswi kusahau kudumisha uhusiano naye. Amri ya kujazwa Roho ni amri ya kujazwa wakati wote. (Waefeso 5:18.) Tunahitaji kujazwa wakati wote, na hilo linatokea kupitia uhusiano wetu naye.
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu ya Utatu wa Mungu, nafsi yenye uungu kikamilifu kama Baba na Mwana. Anasadikisha juu dhambi, anawezesha kuzaliwa upya na anaishi ndani ya kila muumini, akiwezesha ushidi dhidi ya dhambi na utakaso wa moyo. Yeye ndiye uhai unaounganisha kanisa, na hulibariki kanisa kwa tunda la Roho na karama za kiroho kwa ajili ya huduma.
Ushahidi wa Biblia Kuhusu Utu wa Roho Mtakatifu
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Sehemu hii ni ya hiari na inaweza kuzingatiwa ikiwa wanafunzi wanahisi kwamba wanahitaji ushahidi zaidi wa Biblia kuhusiana na hoja hii.
Watu wengine wanakana utu wa Roho na husema yeye ni nguvu isiyo na utu kama umeme au nguvu ya uvutano. Hata hivyo, haiwezekani kwamba nguvu isiyo na utu ingeelezwa kama vile Biblia inavyomweleza Roho Mtakatifu. Umeme hauzungumzi wala haufikirii sababu; nguvu ya uvutano haiwezi kudanganywa. Nguvu isiyo na akili haiwezi kuelewa mapenzi ya Mungu.
Watu wengine husema kwamba maandiko yanatumia tamathali ya tashihisi, yakizungumza juu ya kitu kisicho na utu kana kwamba kina utu bila kumaanisha hivyo. Hata hivyo, maandiko yanazungumza juu ya Roho kwa kutumia maneno yanayoashiria utu, na watu walimwitikia kana kwamba ana utu. Katika sehemu chache, Roho anazungumziwa kitamathali kana kwamba yeye ni kitu, kwa mfano mahali ambapo Biblia inasema kwamba Roho atamwagwa (Matendo 2:17). Mifano hii inapaswa kuzingatiwa kuwa ya kitamathali kwani kwa kawaida Biblia huzungumza kuhusu Roho kama mtu mwenye utu.
Ushahidi wa Biblia wa uutu wa roho mtakatifu:
Katika Mathayo 28:19, tunaambiwa tubatize kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, ambayo inamaanisha kwamba wote watatu wana mamlaka.
2 Wakorintho 13:14 inataja ushirika wa Roho Mtakatifu, ambayo inamaanisha mawasiliano yanayotumia akili.
Katika Marko 13:11, waumini waliahidiwa kwamba Roho Mtakatifu atanena kupitia kwao wakati wa mateso.
Katika Yohana 14:17, 26, Roho Mtakatifu anaitwa Roho wa kweli atakayefundisha na kukumbusha.
Katika Yohana 16:7-11, Yesu aliahidi kwamba Roho Mtakatifu atasadikisha ulimwengu juu ya dhambi, haki, na hukumu, ambayo inahitaji mawasiliano yanayotumia akili.
Yohana 16:13-15 inasema kwamba Roho Mtakatifu hatanena kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atatangaza mambo ya Kristo.
Kulingana na 1 Wakorintho 12:11, Roho Mtakatifu huchagua jinsi karama za kiroho zinavyopaswa kutolewa.
Anashuhudia roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu (Warumi 8:16).
Yeye hutuombea kwa Baba na ana akili ambayo inaweza kuelewa mapenzi ya Mungu (Warumi 8:26-27).
Kulingana na Waefeso 4:30, anaweza kuhuzunishwa, ambayo inamaanisha kwamba anaelewa miitikio yetu na ana hisia.
Anaweza kudanganywa, ambayo inamaanisha kwamba anaelewa mawasiliano (Matendo 5:3).
Yeye hunena, hutoa mwongozo, na ana mapenzi ambayo watu wanapaswa kufuata (Matendo 13:2-4).
Aliwaongoza mitume katika safari zao za umisionari na wakati mwingine aliwaambia wasiende mahali fulani (Matendo 16:6).
Mazoezi ya Somo la 10
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Matendo 1:4-8
Warumi 8:1-14
1 Wakorintho 2:9-16
1 Wakorintho 12:1-13
Wagalatia 5:22-26
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 10. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 10
(1) Orodhesha sifa tatu za mwitikio wa kanisa la awali kwa Roho Mtakatifu.
(2) Je, tunajuaje kwamba Roho Mtakatifu ana utu?
(3) Orodhesha njia tano ambazo kwazo tunajua kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.
(4) Orodhesha kazi tisa za Roho Mtakatifu.
(5) Je, ni kipi kipaumbele cha juu zaidi cha Roho Mtakatifu katika kazi yake maishani mwetu?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.