► Someni Mathayo 4:1-11 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu pepo waovu?
Watu wanapozungumza kuhusu malaika, mara nyingi swali la kwanza ni, “Malaika wanaonekanaje?” Wachoraji wengi wamejaribu kueleza jinsi walivyo.
► Je, malaika wanaonekanaje?
Je, malaika wana mabawa? Maserafi ambao Isaya aliwaona walikuwa na mabawa sita (Isaya 6:2). Sanamu ya makerubi ambayo Mungu alimwambia Musa aweke juu ya Sanduku la Agano ilikuwa na mabawa (Kutoka 25:20). Makerubi ambao Ezekieli aliwaona walikuwa na mabawa manne (Ezekieli 1:6, Ezekieli 10:15).
Hatujui kwamba malaika kwa ujumla wana mabawa. Kwa ujumla hawahitaji mabawa ili kusafiri, kwa sababu wao ni roho na husafiri kwa kasi kubwa zaidi kuliko kuruka kwa mabawa. Kama roho, pia hawana miili ya nyama. Kwa malaika, mabawa kawaida si lazima.
Kinyume na michoro mingi tunayoona, Biblia haisemi kuwa malaika wanafanana na wanawake au watoto. Wamejitokeza katika umbo la kiume, lakini hawana jinsia katika maana ya kibinadamu. Hawana uhusiano wa ndoa au mahusiano ya kifamilia. (Soma Mathayo 22:30.) Kila mmoja wao aliumbwa kibinafsi.
Malaika kwa kawaida hawaonekani na watu, lakini wanaweza kujitokeza wakati kuna kusudi la kufanya hivyo. Wakati mwingine malaika alipojitokeza, mwanzoni watu walifikiri kwamba yeye ni mtu wa kawaida (Mwanzo 19:1-2). Wakati mwingine malaika walijitokeza wakiwa na mng’ao mkubwa kiasi kwamba watu walianguka chini kwa hofu (Mathayo 28:2-4). Malaika alipomtokea mtu, kwa kawaida alimsalimu mtu huyo kwa kusema “Usiogope.” (Soma Luka 1:13, 30; Luka 2:10.)
Malaika ni roho (Waebrania 1:14),[1] lakini hatupaswi kufikiria kuwa wao si viumbe halisia kwa sababu ya hilo. Biblia inadokeza kwamba roho zina nguvu zaidi kuliko kitu chochote chenye mwili unaoonekana. (Soma Isaya 31:1, 3.)
Malaika wanaitwa wana wa Mungu (Ayubu 1:6) na wana asili ya Mungu, lakini si kama ilivyo katika wanadamu. Malaika wana nguvu na akili kuliko wanadamu kwa sasa, lakini siku moja wanadamu watakuwa juu ya malaika. (Soma 1 Wakorintho 6:3.)
Uumbaji wa malaika haujatajwa katika kitabu cha Mwanzo. Waliumbwa kabla ya dunia, na walisherehekea walipomwona Mungu akiiumba (Ayubu 38:4-7).
Malaika hawafi (Luka 20:36). Ukweli kwamba waliumbwa kabla ya dunia unamaanisha kwamba malaika wote wameishi kwa maelfu ya miaka na wameona historia yote ya wanadamu.
Malaika wana nafsi. Wanaweza kusema na kuwa na mazungumzo (Luka 1:18-20). Wanamwabudu Mungu, kumaanisha kwamba wanaweza kuelewa asili yake na wanaweza kuiitikia kwa heshima kuu (Waebrania 1: 6). Wanafurahi wakati mtenda dhambi anatubu, kuonyesha kwamba wana hisia. (Soma Luka 15:10.) Wana hamu kubwa ya kuelewa mpango wa wokovu, kuonyesha kwamba wana uwezo wa kiakili. (Soma 1 Petro 1:12.) Walisherehekea tangazo la kuzaliwa kwa Yesu (Luka 2:13-14).
Malaika wote hawafanani, kwa sababu kuna wengine wanaoitwa makerubi (Zaburi 80:1) na maserafi (Isaya 6:2). Pia kuna viwango vya malaika, kwa maana Biblia inazungumza juu ya malaika aina mbili na angalau malaika mkuu mmoja na pia inataja “Ibilisi na malaika wake” (Mathayo 25:41). Kuna mfumo wa mamlaka kati ya malaika, unaojulikana kama falme, mamlaka, na enzi. (Soma Waefeso 6:12; Wakolosai 1:16.)
Katika utamaduni wa Kiyahudi na wa Kikristo mengi yameandikwa kuhusu malaika, zaidi ya kile tunachojua kutoka kwenye maandiko.
Si mengi yamesemwa katika maandiko kuhusu tofauti kati ya malaika. Neno malaika mkuu limetumika mara mbili pekee katika Biblia. Mikaeli anaitwa malaika mkuu, na kutakuwa na sauti ya malaika mkuu wakati wa kurudi kwa Yesu (1 Wathesalonike 4:16; Yuda 1:9). Neno malaika mkuu kimsingi linamaanisha “mkuu wa malaika.” Hatujui ni malaika wangapi wakuu waliopo.
Maserafi wametajwa katika Biblia katika Isaya 6 pekee. Wana mabawa sita. Mbali na mabawa yao, huenda ikawa walionekana kama wanadamu, kwa sababu wana mikono, miguu na nyuso.
Makerubi na upanga wa moto viliwekwa kwenye Bustani ya Edeni baada ya Adamu na Hawa kufurushwa (Mwanzo 3:24). Hilo lilikuwa ni ili kufanya bustani isiweze kufikiwa. Maelezo ya Ezekieli kuhusu makerubi aliowaona ni tofauti sana na kiumbe mwingine wowote tunaomjua. Walikuwa na mabawa manne, nyuso nne ambazo zote zilikuwa tofauti, mikono kadhaa, mng'ao kama moto, miale ya umeme, na kasi kama umeme (Ezekieli 1:5-14, Ezekieli 10:15).
Sanamu za makerubi wawili ziliwekwa kwenye ncha za Sanduku la Agano, Kiti cha Rehema kikiwa katikati yao.[2] Mungu anaitwa tena na tena Yeye aketiye juu ya makerubi.[3] Hilo lilimtambulisha kuwa Mungu wa Israeli ambaye aliabudiwa Hekaluni na pia lilionyesha kwamba hakuweza kufikiwa isipokuwa kwa njia alizoagiza.
Nguvu na ukuu wa Mungu unaonekana katika aina ya watumishi alionao. Makerubi ni viumbe ambao mtu akimwona mmoja wao atafikiri anamwona Mungu, na atataka kumwabudu, kumbe ni mtumishi wa Mungu tu.
Ukweli kwamba Mungu anahudumiwa na malaika wengi unaonyesha ukuu wake. Mtume Yohana aliona umati wa malaika uliokuwa umezunguka kiti cha enzi cha Mungu. Alisema “hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu” (Ufunuo 5:11).
Nguvu za malaika zina kikomo, kwa kuwa tunasoma kwamba malaika mmoja alicheleweshwa na mzozo alipokuwa amebeba ujumbe kwa Danieli. (Soma Danieli 10:12-13.) Hata hivyo, Mungu anaweza kuwapa nguvu nyingi kadiri wanavyohitaji kwa ajili ya kazi yoyote anayowapa, kama vile wakati ambapo malaika mmoja aliwaua wanajeshi 185,000 (2 Wafalme 19:35).
Inaonekana kwamba malaika hupewa majukumu. Biblia inatuambia kwamba huwa wanatumwa kuwatumikia wale wanaopokea wokovu. (Soma Waebrania 1:14.) Malaika huwazunguka na kuwalinda watu wanaomtumikia Mungu (Zaburi 34:7). Tunaweza kuchukulia kwamba malaika wengi wako pamoja nasi wakati wote. Yesu alisema kwamba watoto wana malaika wanaowatumikia. (Soma Mathayo 18:10.) Malaika mkuu Mikaeli anaitwa jemedari mkuu anayetetea taifa la Israeli (Danieli 12:1).
Biblia haisemi kamwe kwamba tunapaswa kuomba kwa malaika. Haisemi kwamba tujaribu kuwasiliana nao. Malaika si wapatanishi kati yetu na Mungu. Kuna onyo kuhusu watu wanaoabudu malaika na kujihusisha na mambo ya ulimwengu wa roho ambayo hawayaelewi. (Soma Wakolosai 2:18.) Tukijaribu kushirikiana na malaika kwa njia ambayo Mungu hataki, kuna uwezekano kwamba roho waovu watatuitikia badala ya malaika wa Mungu.
[1]Pepo pia wanaitwa “roho” katika Mathayo 8:16, Mathayo 12:45; Matendo 19:12; na katika vifungu vingine.
[3]Kwa mfano, 2 Wafalme 19:15, 1 Mambo ya Nyakati 13:6; Isaya 37:16
Shetani na Malaika Walioanguka
► Je, asili ya pepo waovu ni ipi?
Pepo waovu ni malaika waliomuasi Mungu. Tukio hilo lilitokea kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, na Biblia haisemi mengi kulihusu. Shetani alikuwa kiongozi wa uasi, na theluthi moja ya malaika walimfuata (Ufunuo 12:4). Yuda anazungumza kuhusu malaika walioacha nafasi yao ya kwanza (Yuda 1:6). Tayari wameshahukumiwa na hukumu ya Mungu. (Soma Yohana 16:11; 2 Petro 2:4.)
Kuna vifungu viwili katika vitabu vya manabii ambavyo huenda vinazungumzia anguko la Shetani (Isaya 14:12-17 na Ezekieli 28:12-19). Kila kifungu kinazungumza juu ya mfalme mwanadamu wa dunia, lakini huenda vinalinganisha anguko la wafalme na anguko la Shetani.
Inaonekana Shetani alishikwa na kiburi na alitaka kuwa huru kutokana na Mungu. Mtume Paulo alionya kwamba mtu anaweza kuwa na kiburi na kuanguka katika hukumu kama ya shetani. (Soma 1 Timotheo 3:6.) Hilo lilikuwa jaribu lile lile ambalo Ibilisi aliwatolea Adamu na Hawa aliposema, “Mtakuwa kama Mungu.” Ni jaribu la kukataa mamlaka ya Mungu na kuwa mungu wako mwenyewe.
[1]► Je, baadhi ya mambo tunayojua kuhusu Shetani ni yapi?
Shetani bado anaongoza uasi dhidi ya Mungu. Anaitwa mfalme wa uwezo wa anga (Waefeso 2:2). Shetani anaitwa mtawala wa ulimwengu huu kwa sababu watu wa ulimwengu huu kwa kiasi kikubwa wanamuasi Mungu (Yohana 12:31). Anadai umiliki wa falme za ulimwengu, akizitoa kwa muda mfupi kwa yeyote anayetaka (Luka 4:4-6). Anapofusha akili za wenye dhambi ili kuwazuia wasikubali injili. (Soma 2 Wakorintho 4:4.) Wenye dhambi ambao hawajatubu hakika ni wafungwa wake (2 Timotheo 2:26). Anaondoa Neno la Mungu kutoka kwenye akili za watu ili lisiwe na ushawishi wowote maishani mwao. (Soma Marko 4:15.) Aliweka ndani ya mioyo ya Anania na Safira mpango wa kudanganya kanisa na Roho Mtakatifu (Matendo 5:3), na alimpa Yuda nia ya kumsaliti Yesu (Luka 22:3). Anabuni kanuni potovu za kidini na kuwahimiza watu wazifundishe. (Soma 1 Timotheo 4:1.)
Shetani anamchukia Mungu na kwa hivyo anawachukia watu kwa sababu wameumbwa kwa mfano wa Mungu na wanapata kibali kikuu zaidi cha Mungu. Anatafuta kuwaleta watu wengi iwezekanavyo chini ya hukumu ile ile ambayo amepokea kwa kuwashawishi wamuasi Mungu.
Wale wanaomtumikia Shetani kwa kudhamiria ndio watu waliodanganyika zaidi ulimwenguni, kwa kuwa wako katika uasi usioweza kufanikiwa, na wanamtumikia bwana ambaye anawachukia na nia yake ni kuwaangamiza tu (1 Petro 5:8). Anatoa ahadi ambazo anajua hawezi kuzitimiza (Yohana 8:44).
Wengine wanamfuata Shetani pasipo kudhamiria wanapochagua kuishi katika dhambi (Waefeso 2:2-3). Ndio maana anatumia muda na nguvu nyingi katika majaribu na udanganyifu (2 Wakorintho 4:4, 2 Wakorintho 11:3, 14). Anataka kuwafanya watu wakatae kuweka imani katika Mungu, wakifanya vitu vilivyoumbwa kuwa sanamu zao badala ya kumwabudu Mungu (Warumi 1:25). Majaribu yake ni udanganyifu, kwa sababu hana chochote cha kutoa isipokuwa kupotosha kile ambacho Mungu ameumba. Ibilisi hajaumba furaha wala raha; Mungu aliumba yote hayo. Ibilisi anaweza tu kutoa raha kwa njia potovu ambazo ziko nje ya mapenzi ya Mungu. Kwa kweli, Shetani hawezi kuumba chochote; anaweza tu kupotosha vitu vizuri ambavyo Mungu ameumba.
Inaonekana kwamba pepo fulani waovu hulenga maeneo mahususi ya kijiografia au vikundi vya watu. Kama vile malaika Mikaeli alivyoitwa jemedari mkuu anayelinda Israeli, kulikuwa na roho waovu walioitwa wakuu wa Uajemi na Uyunani (Danieli 10:13, 20). Roho fulani zikawa miungu ya mataifa fulani.
Shetani anatamani kuabudiwa. (Soma Mathayo 4:9.) Roho waovu hufanya kazi kupitia dini za uongo. Biblia inatuambia kwamba watu wanapoabudu sanamu wanaabudu pepo. (soma Kumbukumbu la Torati 32:17; 1 Wakorintho 10:20-21.) Pepo huitikia ibada ya watu wasiojua kile wanachoabudu. Kama vile mwabudu Mungu anavyokuwa zaidi kama Mungu na kufurahia utakatifu, mwabudu pepo waovu anakuwa mwovu zaidi na kufurahia maovu. Labda ibada mbaya zaidi ambayo imewahi kutokea ni wakati watu walipotoa watoto wao wenyewe kuwa dhabihu kwa roho waovu. (Soma Zaburi 106:37-38.)
Shetani na roho waovu wengine hujaribu kuchukua udhibiti wa akili na tabia za watu kikamilifu. Hilo linaitwa “kupagawa na pepo.” Baadhi ya watu wamejitoa wenyewe kwa kudhamiria kwa aina hiyo ya kupagawa; pengine wengine wameruhusu hali hiyo bila kujua walichokuwa wakifanya. Watu wengine wameingia hatua kwa hatua katika hali hiyo, wakifikiri kwamba wanapata nguvu za kutumia kwa malengo yao wenyewe. Mtu aliyepagawa kwa namna hiyo anakuwa mtumwa wa pepo waovu, anasukumwa kwenye maangamizi yake mwenyewe, na kuteseka vibaya sana kiakili na kihisia. (Soma Marko 5:2-5.) Ni Yesu pekee ndiye anayeweza kumkomboa mtu kutoka katika utumwa huo.
“Shetani hujifanya kuwa mtawala wa moyo, macho, na ulimi wa mwenye dhambi. Hujaza moyo wake na upendo wa dhambi; hupofusha macho yake ili asione hatia na adhabu inayomngoja; na ulimi wake huuzuia kuomba.”
Adam Clarke
Christian Theology, “Good and Bad Angels”
Ushindi wa Mungu
Katika nchi ambazo injili imehubiriwa sana, kazi ya pepo waovu kwa kawaida huwa imefichika. Kinyume na matarajio, ni katika nchi hizi “zilizostaarabika” ndiko watu hawazingatii dini kwa kiasi kikubwa, wakikejeli kitu chochote kisicho cha kawaida na kukana uwepo wa roho. Katika mazingira kama hayo, pepo wabaya hawafanyi kazi waziwazi, kwa sababu wakiwatia hofu watu ambao wamesikia injili, wengi wa watu hao watamgeukia Mungu kwa ajili ya ukombozi na ulinzi.
[1]Katika nchi ambapo injili haijulikani sana, pepo wabaya hufanya kazi kwa uwazi zaidi. Watu walio katika nchi hizo hawajui kwamba wanaweza kumgeukia Kristo kwa ajili ya ukombozi, kwa hivyo nguvu za pepo huwatishia na kuwafanya wanyenyekee. Watu hao hutumikia roho, si kwa hiari wala kwa furaha, bali kwa hofu. Injili huja kwao kama ujumbe wa ajabu wa ukombozi na uhuru.
Kwa sababu ya mashambulizi ya ibilisi ya mara kwa mara, tuko katika vita vya kiroho. Tunaonywa kwamba tukumbuke vita vyetu ni katika ulimwengu wa roho na si dhidi ya maadui wa kimwili. (Soma Waefeso 6:12.) Tunaambiwa tujivike silaha za kiroho, ili tuweze kujilinda (Waefeso 6:13). Tunaweza kuwa na uhakika kwamba tutapata ushindi, kwa sababu ibilisi hawezi kupinga nguvu za Mungu zilizo ndani yetu, na tunapompinga ibilisi, atatukimbia (Yakobo 4:7).
► Je, ibilisi ni kinyume cha Mungu?
Ibilisi ana nguvu zaidi ya zile walizo nazo wanadamu katika hali yao ya sasa wakiwa na miili inayoweza kufa. Hata hivyo, nguvu zake si kitu zikilinganishwa na za Mungu. Hapaswi kufikiriwa kuwa kinyume cha Mungu, kana kwamba ana nguvu sawa na Mungu.
Wanafalsafa wengine wanafikiri kwamba nguvu za mema na mabaya duniani ziko sawa. Hiyo si kweli kabisa. Shetani hayuko kila mahali, si mjua yote, na hufanya makosa. Mungu ndiye Muumba wa roho, na haziwezi kumshinda. Kipindi cha majaribio ya mwanadamu kitakapokamilika, pepo wote waovu watahukumiwa, kufungiwa, na kuadhibiwa, pamoja na wenye dhambi.
Kushindwa kwa Shetani kuliahidiwa zamani sana. Mungu aliahidi kumtuma Mwokozi kuponda kichwa cha nyoka (Mwanzo 3:15). Yesu alikuja kuharibu kazi za ibilisi na kutupa ushindi dhidi ya dhambi. (Soma 1 Yohana 3:8.) Yesu, kwa kifo na ufufuo wake, hamruhusu Shetani kuwa na nguvu dhidi ya mauti (Waebrania 2:14; Ufunuo 1:18). Hatima ya mwisho na ya milele ya Shetani na pepo wengine waovu ni ziwa la moto. (Soma Mathayo 25:41.)
Tayari Mungu ameweka mipaka katika kile ambacho Shetani anaweza kufanya (Ayubu 1:12, Ayubu 2:6). Hilo linamaanisha kwamba hatuhitaji kuishi tukiogopa yale ambayo Shetani anaweza kutufanyia. Hakuna kinachoweza kutokea isipokuwa Mungu akiruhusu, na anajua kile tunachoweza kustahimili (1 Wakorintho 10:13).
Hatujalindwa tu dhidi ya mashambulizi ya Shetani, bali pia tuna uwezo wa kuendeleza ufalme wa Mungu dhidi ya ufalme wa Shetani. Yesu aliwapa wanafunzi wake nguvu, si mitume tu, kuwafukuza pepo waovu. (Soma Luka 10:17.) Kadiri tunavyohubiri injili, Mungu anaupatia nguvu ukweli wake, na kuwakomboa kutokana na Shetani wale wanaoitikia injili.
“Ibilisi hawezi kukushinda ukiendelea kumpinga. Ingawa yeye ni mwenye nguvu, Mungu hamruhusu kamwe kumshinda mtu anayeendelea kumpinga. Hawezi kulazimisha nia ya mwanadamu.”
Adam Clarke
Christian Theology, “Good and Bad Angels”
Makosa ya Kuepuka: Kuvutiwa na Ulimwengu wa Roho kwa Njia Mbaya
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshirika wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Watu wengine huvutiwa na ulimwengu wa roho. Wanaanza kusoma kuhusu malaika na wanaweza kujaribu kuingiliana nao. Biblia haisemi kamwe tuombe kwa malaika au tujaribu kuwa na uhusiano nao. Biblia inatuonya tusiwaabudu au kujaribu kujua zaidi ya kile tunachoweza kuelewa (Wakolosai 2:18).
Ni hatari zaidi ikiwa mtu atavutiwa sana na roho waovu. Watu wengine huvutiwa na nguvu zao na mambo wanayofanya. Kuna michezo inayoingiliana na roho waovu. Kuna njia ambazo watu hutumia kupata habari kutoka kwa roho waovu. Hatupaswi kamwe kujihusisha na roho waovu isipokuwa kuwapinga kwa nguvu za Mungu (Yakobo 4:7, 1 Petro 5:8-9).
Baadhi ya watu wamebuni maelezo tata na ya kina kuhusu ulimwengu wa roho na jinsi unavyofanya kazi. Hata hivyo, Mungu amefunua katika Biblia yote tunayohitaji kujua kuhusu ulimwengu wa roho.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Mungu aliumba roho wote. Malaika watakatifu wanamwabudu Mungu na kuwalinda waumini. Malaika ni viumbe wasioweza kufa, ambao wanaweza kuzungumza, kuabudu, na kutumia mantiki. Wamewahi kufanya maamuzi ya kimaadili. Shetani na malaika wengine walianguka katika dhambi na ni maadui wa Mungu na wanadamu. Mungu amewekea nguvu za Shetani mipaka na amemhukumu adhabu ya milele.
Mazoezi ya Somo la 6
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Mathayo 12:43-45
Luka 8:27-35
Matendo 12:7-11
2 Wakorintho 11:13-15
1 Petro 5:8-9
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 6. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 6
(1) Je, tunajuaje kwamba malaika kwa kawaida hawana miili ya nyama?
(2) Je, malaika waliumbwa wakati gani?
(3) Je, malaika hufa?
(4) Taja njia nne zinazotufanya tujue kuwa malaika wana nafsi.
(5) Taja maneno manne yanayotumiwa katika Biblia kurejelea malaika.
(6) Je, ni jambo gani ambalo malaika huwafanyia watu wanaomtumikia Mungu?
(7) Je, asili ya pepo waovu ni ipi?
(8) Je, mwabudu sanamu anaabudu nini hasa?
(9) Je, hatima ya mwisho ya Shetani na pepo wengine waovu ni ipi?
(10) Je, waumini wanapaswa kufanya nini ili kujilinda kutokana na mashambulizi ya kiroho?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.