Kwa nini dhana ya mtu kuhusu Mungu ni muhimu sana.
Jinsi ukweli kwamba Mungu ni Muumba unamfanya awe tofauti na vitu vingine vyote.
Sifa za Mungu: maana ya yeye kuwa mwenye nafsi, roho, wa milele, mwenye Utatu, mweza yote, yuko kila mahali, asiyebadilika, ajuaye yote, mtakatifu, mwenye haki, na mwenye upendo.
Jinsi kila sifa ya Mungu ilivyo muhimu katika uhusiano wetu naye.
Mtazamo wa kibiblia wa ukuu wa Mungu.
Kauli ya kanuni za Kikristo kuhusu Mungu.
(2) Mwanafunzi ataepuka kosa la kutoelewa umuhimu wa aina za ibada.
► Someni Isaya 40 pamoja. Jadilini kile kifungu hiki kinatuambia kuhusu Mungu.
► Je, kwa nini suala la ikiwa mtu ana dhana sahihi ya Mungu au la ni muhimu?
Mungu ni nani? A. W. Tozer alionyesha umuhimu wa swali hili aliposema, “Ninaamini kwamba hakuna makosa katika kanuni au kushindwa katika kutumia maadili ya Kikristo ambayo hayawezi kufuatiliwa na hatimaye kubainika kuwa yanatokana na mawazo duni kuhusu Mungu”.[1] Yesu alimwambia mwanamke Msamaria pale kisimani kwamba tatizo la ibada ya Wasamaria ni kwamba hawakumjua ni nani waliyemwabudu. Sifa muhimu zaidi ya mtu yeyote ni dhana yake kuhusu Mungu. Dhana ya mtu kuhusu Mungu ndio msingi wa dini yake. Hakuwezi kuwa na kosa kubwa zaidi kuliko kupotoka kuhusu jinsi Mungu alivyo.
Ulinganisho hautoshi kueleza kikamilifu jinsi Mungu alivyo, kwa kuwa ni dhahiri kuwa yuko juu sana kuliko sisi. Hata Biblia haitupi ufafanuzi rasmi wa Mungu ni nani, lakini kila mahali inaeleza uwepo wake na nguvu zake. Kitabu cha Mwanzo kinatuambia jinsi Mungu alivyoziumba mbingu na nchi; mimea; jua, mwezi, na nyota; na wanyama; na hatimaye wanadamu. Fundisho la kwanza la maandiko liko wazi kabisa: Mungu ndiye Muumba wa vyote vilivyopo. Hivyo, yeye ni tofauti na vitu vingine vyote vilivyopo, kwa kuwa yeye si sehemu ya uumbaji wake.
Katika Biblia yote kuna kauli zingine nyingi kuhusu Mungu. Wanatheolojia wamefupisha kwa uangalifu taarifa za Biblia katika orodha za sifa za Mungu. Hatuwezi kamwe kuelewa sifa zake kikamilifu kwa kutumia ufahamu wetu usio mkamilifu. Hata hivyo, kuchunguza sifa za Mungu kwa heshima kuu ni zoezi la kiroho lenye thamani. Hivyo, tunazingatia kauli zifuatazo kuhusu Mungu. Zinatokana na kujifunua kwake katika Biblia, na kwa sababu hiyo tunajua kwamba ni za kweli.
[1]A. W. Tozer, The Knowledge of the Holy (New York: Harper and Row, 1961), 10.
Sifa za Mungu
Tutakachoangazia si orodha kamili ya sifa za Mungu, bali ni zile sifa ambazo ni muhimu zaidi kwetu kujua.
► Je, ni sifa gani za Mungu ambazo unaweza kuziorodhesha?
Mungu ni Mwenye Nafsi
Hii ina maana kwamba yeye ni mtu halisi, aliye hai na mwenye akili, hisia, na nia.[1] Yeye si jumla ya sheria za asili au nguvu zisizo na utu kama vile umeme au uvutano. Anaumba, anatenda, anajua, ana nia, anapanga na ananena.
► Je, ingeleta tofauti gani kwetu kama Mungu asingekuwa na nafsi?
Ukweli kwamba ana nafsi unatuwezesha kuwa na uhusiano naye. Kama asingekuwa na nafsi, tusingeweza kumwomba. Kama asingekuwa na nafsi isingewezekana yeye kufurahishwa au kuchukizwa.
Mungu ni Roho
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yohana 4:24).
Ukweli kwamba yeye ni roho unatoa msingi wa ushirika wetu wa kiroho naye na ibada yetu kwake. Sala na ibada hazitegemei vitu vinavyoweza kuonekana, mikao mahususi ya
mwili, ratiba mahususi au jengo. Mambo hayo yanaweza kutusaidia kuelekeza akili zetu katika ibada, lakini ibada haitegemei mambo hayo.
Ukweli kwamba Mungu ni roho ni sababu moja iliyomfanya atukataze tusitengeneze sanamu yake. (Soma Kutoka 20:4-6.) Akiwa roho, hatuwezi kumwona Mungu (1 Timotheo 1:17) isipokuwa anapochagua kuchukua umbo linaloonekana. (Soma Mwanzo 18:1; Isaya 6:1.) Kwa sababu uwezo wetu wa kumwona Mungu una mipaka, hata wakati anapoonekana katika umbo linaloonekana, ni kweli kusema kwamba hakuna mtu ambaye amemwona Mungu kikamilifu (Kutoka 33:20; Yohana 1:18; Yohana 6:46).
Mungu ni wa Milele
Hakujawahi kuwa na wakati ambapo Mungu hakuwepo, na hakutawahi kuwa na wakati ambapo hatakuwepo; Mungu hana mwanzo wala mwisho. Mungu alijidhihirisha kwa jina, MIMI NIKO AMBAYE NIKO (Kutoka 3:14). Anaelezwa na Yohana kama yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi (Ufunuo 1:8). Tangu milele hata milele yeye ni Mungu (Zaburi 90:2). Baadhi ya dini zina hekaya kuhusu wakati miungu yao ilizaliwa, lakini Mungu wa kweli ni wa milele.
Mungu ni Mwenye Utatu
Biblia inasema kuna Mungu mmoja lakini inataja nafsi tatu tofauti kuwa Mungu. Kuna Mungu mmoja tu, lakini katika asili yake kuna nafsi tatu. Ingawa hatuwezi kuelewa kikamilifu Utatu wa Mungu, hilo si jambo lisilo la kimantiki, kwa kuwa hatusemi kwamba kuna vitu vitatu na kitu kimoja ambavyo ni kitu kile kile. Kuna Mungu mmoja, aliye na nafsi tatu. Kwa sababu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ambao wote wana sifa zote za uungu, kila mmoja wao anaweza kustahili kuitwa Mungu na kuabudiwa kama Mungu. (Mengi zaidi yatasemwa kuhusu Utatu wa Mungu katika somo linalofuata.)
Mungu ni Mweza Yote
Anaweza kufanya chochote anachotaka. “Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, alitakalo lote amelitenda” (Zaburi 115:3). Hana mipaka isipokuwa kamwe hatendi kinyume na asili yake takatifu na siku zote anatekeleza yale aliyoahidi kutekeleza. Hakuna jambo gumu au ambalo ni changamoto kwa Mungu. “Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki” (Ufunuo 19:6).
► Je, kujua kwamba Mungu ni mweza yote kunaleta tofauti gani kwetu?
Hili ni jambo la kutia moyo, kwa kuwa tunajua kwamba katikati ya mapambano yetu anaweza “kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu” (Wefeso 3:20). Hata kama mambo yanaonekana yameenda marama kabisa, tunajua kwamba mpango mkuu wa Mungu utatimizwa. Tunaweza kuomba tukiwa na uhakika kwamba Mungu anaweza kuingilia kati katika hali yoyote.
Mungu Yuko Kila Mahali
[2]Hakuna mahali ambapo hayuko, na hakuna kinachotokea ambacho hakioni. “BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu” (Isaya 66:1). Yeye ni Mungu wa ulimwengu wote, na nguvu zake hazikomi katika eneo lolote. “Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami?” (Yeremia 23:24). Hilo linatuhakikishia kwamba Mungu anajua hali zetu na matatizo yetu. Pia linatuambia kwamba hakuna mtu anayeweza kujificha kutoka kwa Mungu, au kutenda dhambi mahali ambapo Mungu hawezi kuona. Vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake. (Soma Waebrania 4:13.)
Mungu Habadiliki
Hakujawahi kuwa na wakati ambapo Mungu alifanyika kuwa Mungu, na hataacha kuwa Mungu. (Soma Yakobo 1:17.) Kuna dini zinazoamini kwamba Mungu yuko katika mchakato wa kuendelea kufanyika Mungu, lakini Biblia inatuambia kwamba katika nafsi yake na asili yake, na katika sifa na makusudi yake, Mungu habadiliki kamwe. (Soma Malaki 3:6.) Siku zote anapenda kile kilicho sahihi, na siku zote anachukia kile kilicho kibaya. Mungu wa Milele aliyejidhihirisha kwa Musa kama MIMI NIKO AMBAYE NIKO ndiye MIMI NIKO AMBAYE NIKO wa leo. Hana kikomo, ni wa milele na hawezi kubadilika katika nafsi, hekima, nguvu, utakatifu, haki, wema na ukweli wake. Yeye ni yule yule siku zote na miaka yake haitakuwa na mwisho (Zaburi 102:27).
Mungu ni Mjua Yote
“Akili zake hazina mpaka” (Zaburi 147:5). Mungu hahitaji mchakato wa kujifunza, kwa kuwa anajua kila kitu. Mungu hajawahi kujifunza kitu chochote kutoka kwa mtu yeyote na hakuna mtu anayeweza kumshauri. (Soma Isaya 40:13-14.) Mungu anajua mambo ya siku zijazo na kwa hivyo hashangazwi au hawezi kukosa kuwa tayari kwa lolote litakalotokea (Zaburi 139:4).
► Je, kujua kwamba Mungu ndiye anayejua yote kunaleta tofauti gani kwetu?
Hekima ya Mungu inahusiana na maarifa ya Mungu, yanayodhihirishwa katika uumbaji na hasa katika mpango wa wokovu. (Soma Zaburi 104:24; Warumi 11:33.) Kwa kuwa anajua na anaelewa yote, siku zote anajua kile kilicho sahihi kufanya. Mapenzi ya Mungu siku zote ni bora kwetu kwa sababu Mungu anaelewa kila hali kikamilifu na anajua matokeo ya kila tendo yatakuwaje.
Mungu ni Mtakatifu
Mungu amejieleza mwenyewe kuwa mtakatifu kimsingi. Nabii Isaya alimrejelea Mungu tena na tena kama “Mtakatifu wa Israeli.” Malaika wanasema “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu” mbele zake daima (Ufunuo 4:8, Isaya 6:3). Utakatifu wa Mungu ulikuwa mada ya ibada: “Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu” (Zaburi 99:3). Yeye ndiye kiwango kamili cha ukamilifu wote wa kimaadili. Matendo yake yanadhihirisha uwepo wa wema wote na kutokuwepo kwa uovu wowote na haiwezi kuwa vinginevyo. Utakatifu wa Mungu unaonyesha kwamba mwanadamu hastahili kutumikia na kuabudu bila kwanza kubadilishwa kwa neema. (Soma Isaya 6:5.) Mungu anataka tuwe watakatifu kama yeye. “Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, ‘Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu’” (1 Petro 1:15-16).
Mungu ni Mwenye Haki
Matendo ya Mungu ni sahihi siku zote. Matendo yake yanatokana na asili yake takatifu. (Soma Kumbukumbu la Torati 32:4.) Asili yake mwenyewe ndio kiwango cha kile kilicho sahihi. Yeye siku zote hutimiza ahadi zake na kamwe hasemi uwongo (Hesabu 23:19; 2 Samweli 7:28).
► Je, kwa nini ni jambo muhimu kwetu kwamba Mungu ni mwenye haki?
Haki yake ndio msingi wa sheria yake, ambayo ndio kiwango kamili cha wajibu wetu kwake na kwa wengine. Anatekeleza sheria yake kwa haki, akiwapa thawabu wale wanaoitii na kuwaadhibu wale wanaoivunja. Hilo linawafariji wale wanaoteseka na kukandamizwa, lakini pia linatuonya kwamba hakuna mtu atakayeepuka adhabu iwapo atatenda mabaya. “Hukumu za BWANA ni kweli, zina haki kabisa” (Zaburi 19:9). Atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake (Warumi 2:6). “Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu” (Warumi 14:10).
Mungu ni Upendo
Sifa hii ni muhimu sana. Hebu fikiria jinsi lingekuwa jambo la kuogofya sana ikiwa Mungu mwenye uwezo wote na maarifa yote asingetupenda! Ingekuwaje kama angekuwa mtakatifu na mwenye haki, lakini hakutupenda? Pamoja na uwezo wake na utakatifu wake kamili, Mungu anatupenda. (Soma Warumi 5:8.) Mungu hubariki uumbaji wake kwa jumla (Soma Mwanzo 1:22, 28). Yeye hasa hubariki wanadamu kwa kuwapa vitu vizuri vya maisha, na aliumba ulimwengu kuwa mahali ambapo watu wanaweza kuishi kwa furaha.[3] Kwa wale wanaompenda na kumtumikia, yeye hugeuza kila jambo la maisha kuwa baraka (Warumi 8:28). Neema, rehema, subira, na amani yake hutubariki kwa sababu ya upendo wake. (Soma Kutoka 34:6; Waefeso 1:7, Waefeso 2:4-5.)
[4]“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16). Licha ya dhambi na uasi wetu, yeye hutuonyesha rehema, akitualika tuje kwake kwa njia ya Yesu, ambaye amemtoa kama dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu (1 Yohana 2:2). Msalabani Mungu anatuonyesha moyo wake, ambao umejaa upendo na huruma kwa ajili yetu. “Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu” (1 Yohana 4:10). Mungu anawapenda watu wote, bila kushawishiwa na makabila yao, uwezo wao wa asili au hadhi yao ya kidunia, na anatoa msamaha kwa wote. (Soma Warumi 2:11; Yakobo 2:1-5.) Kwa hivyo, Mungu anataka tuwapende watu wote na tuwe tayari kusamehe mtu yeyote anayetukosea. Upendo na msamaha ni alama za watoto wa Mungu. (Soma Mathayo 5:43-45.)
Mungu alituumba kwa mfano wake. Ingawa sisi tuna kikomo na yeye hana kikomo, tunafanana naye zaidi kuliko kitu chochote kingine katika uumbaji wake. Alituumba ili tuweze kumjua, kumwabudu na kumpenda. Ametuumba kwa ajili yake mwenyewe, na kama Agostino anavyotukumbusha, hatutapata utulivu kamwe hadi tupate utulivu ndani
yake. Tofauti na Mungu, vitu vyote vya kidunia si vya maana, na ni kwake tu ndio tunastahili kujitoa kikamilifu. Haiwezekani kupata uradhi wa kudumu popote pengine isipokuwa katika Mungu. Kwa neema yake tunaweza kukombolewa na kufanywa kuwa na uwezo wa kumwabudu yeye kando na vitu vyote vingine, kumwamini kama Baba yetu wa Mbinguni na kutekeleza mapenzi yake katika kila nyanja ya maisha yetu.
“Umetuumba kwa ajili yako, ee Bwana, na mioyo yetu haijatulia mpaka ipate utulivu ndani yako.”
Agostino wa Hippo
Mungu ni Mkuu
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshiriki wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Mungu ana uwezo kamili na mamlaka kamili. Kama mtawala wa ulimwengu, anaweza kutimiza chochote anachotaka (Zaburi 115: 3, Zaburi 135: 5-6).
Yeye hufanya mambo yote kulingana na mapenzi yake mwenyewe, bila kuhitaji kumtii mtu mwingine yeyote (Waefeso 1:11). Chochote anachoamua kufanya hakika kitatendeka, kwa maana hakuna mtu anayeweza kumzuia wala hakuna hali inayoweza kumfanya ashindwe kufanya kile anachotaka. (Soma Isaya 46:9-11.) Yeye hudhibiti matendo ya watawala wa dunia wakati wowote anapotaka (Mwanzo 50:20; Matendo 4:27-28).
Lakini Mungu amewapa watu uwezo wa kufanya maamuzi. Wanaweza kuchagua kati ya mambo mazuri, lakini pia wanaweza kuchagua kati ya mema na mabaya. Wanaweza kuchagua kumtii Mungu au kutomtii. Watu wa kwanza kabisa aliowaumba walifanya uamuzi wa kutenda dhambi. Tangu wakati huo kila mtu amefanya maamuzi, na ingawa wengine wamefanya maamuzi mazuri, wote pia wametenda dhambi.
Ikiwa Mungu ndiye Bwana anayetawala mambo yote, anatimizaje mapenzi yake katika ulimwengu ambapo mabilioni ya viumbe wanafanya maamuzi yao wenyewe?
Ni mapenzi ya Mungu kwamba viumbe wake wafanye maamuzi halisi. Hiyo inamaanisha kwamba hatawafanyia maamuzi yao yote. Inamaanisha pia kwamba lazima kuwe na matokeo halisi kwa kile wanachofanya; la sivyo, hawatakuwa wanafanya maamuzi halisi. Ikiwa kwa njia fulani Mungu angekuwa anadhibiti matokeo ya matendo ya mtu ili mabaya yasitokee, basi atakuwa anachukua kutoka kwa mtu huyo uwezo wa kuchagua uovu.
Haki ya Mungu ni haki ya kweli kwa sababu atakuwa akiwahukumu watu kwa ajili ya matendo yao ya hiari. (Soma Ufunuo 20:12-13.) Ikiwa Mungu angedhibiti matendo yote, isingekuwa jambo la busara kwake kutoa adhabu na thawabu.
Mungu anatamani watu wachague kile kilicho sahihi, lakini zaidi ya yote anatamani wafanye maamuzi halisi. Ndio maana dunia iko jinsi ilivyo. Ulimwengu ni mchanganyiko tata wa mambo mema kutoka kwa Mungu, matokeo ya matendo mema ya wanadamu, matokeo ya matendo mabaya ya wanadamu, na mema ambayo Mungu huleta hata kutokana na matendo mabaya ya wanadamu.
Tunaona vipaumbele vya Mungu katika mpango wa wokovu. Anatoa wokovu kwa wote na anataka wote waokolewe (1 Timotheo 2:3-4). Anampa kila mtu uwezo wa kuitikia injili lakini halazimishi mtu kuitikia. Ndio maana mialiko na ushawishi unatumiwa katika maandiko.[1] Mungu anawapa watu chaguo na kuwaeleza matokeo ya chaguo hilo.
Tunahubiri injili kwa ujasiri tukiwa na uhakika kabisa kwamba kila mtu anaweza kuokolewa. Dhamira yetu ni kushirikiana na Roho Mtakatifu katika kuwashawishi watu kujisalimisha kwa Mungu. (Soma 2 Wakorintho 5:11.)
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kuna Mungu mmoja, aliyeumba ulimwengu na ni Bwana juu ya vyote. Yeye ni Roho wa milele, asiyebadilika. Yeye ni mwenye uwezo wote, mjua yote na yuko kila mahali. Yeye ni mtakatifu kikamilifu katika tabia yake na mwenye haki katika yote anayofanya. Anabariki uumbaji wake na anampenda kila mtu, akitoa msamaha na uhusiano naye.
Mazoezi ya Somo la 2
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Zaburi 139:1-4
Mithali 9:10
Isaya 46
Ufunuo 4:9-11
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 2. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 2
(1) Je, sifa muhimu zaidi ya mtu ni ipi?
(2) Je, fundisho la kwanza la maandiko ni lipi?
(3) Taja sifa ya Mungu inayolingana na kila kauli:
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.