► Someni Mwanzo 3 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu dhambi?
► Je, kwa nini tunahitaji kuelewa dhambi?
Lazima tuelewe dhambi:
1. Ili tuelewe hali ya ulimwengu. Biblia inatuambia kwamba dhambi ndio chanzo cha mateso ya wanadamu. Ni kupitia dhambi ndio kifo kilikuja ulimwenguni. (Soma Warumi 5:12.) Kwa sababu ya laana ya dhambi, kuna magonjwa, kuzeeka na uchungu. Matendo ya dhambi kama vile kusema uongo, kuiba, kuua, uzinzi, ulevi na ukandamizaji yamejaza dunia mateso. Matendo ya dhambi yanatokana na dhambi iliyo moyoni, kama vile chuki, tamaa ya kimwili, kutamani vitu vya wengine, kiburi na ubinafsi.
2. Ili tuelewe neema na wokovu. Mungu anatoa neema ili kutuokoa kutokana na dhambi (Mathayo 1:21; Warumi 5:20-21).
3. Ili tuelewe utakatifu. Dhambi ni kinyume cha utakatifu. Ni kinyume cha kujitolea kwa Mungu. Ili mtu awe mtakatifu jinsi Mungu anavyotarajia (1 Petro 1:15-16), ni lazima atengwe na dhambi.
Asili ya Dhambi
Uumbaji wa Mungu ulikuwa kamili, na hakuna kitu alichoumba ambacho kilikuwa na kasoro. Mungu alipomaliza uumbaji, aliona kuwa ni mzuri sana (Mwanzo 1:31). Kwa hivyo, tunajua kwamba dhambi haikuwa kosa la Mungu.
Adamu na Hawa walikuwa katika uhusiano na Mungu. Walitamani kumpendeza Mungu na walikuwa na uwezo wa kufanya kila kitu kilicho sahihi. Shetani alikuja kumjaribu Hawa ili asimtii Mungu. Kupitia tukio hilo tunajua kwamba dhambi tayari ilikuwepo katika ulimwengu. Shetani alikuwa tayari ameanguka katika dhambi. Lakini dhambi ilikuwa bado haijaingia katika mwanadamu au sehemu ya uumbaji ambayo ilikuwa chini ya mamlaka ya mwanadamu.
Adamu na Hawa walikuwa na uhuru wa kuchagua. Dhambi iliwezekana kwa sababu waliweza kufanya chaguo halisi. Walichagua kuvunja sheria ya Mungu, na huo ukawa mwanzo wa dhambi ya wanadamu.
Tendo la kwanza la dhambi lilitenganisha mwanadamu na Mungu. Dhambi pia iliharibu asili ya ubinadamu. (Soma Zaburi 51:5.) Watoto wote watakaozaliwa baadaye watakuwa na asili iliyoharibika na watatenda dhambi. (Soma Warumi 5:12, 14, 18-19.)
Dhambi ilileta laana kwa viumbe wote (Mwanzo 3:16-19). Maisha yalibadilishwa kwa sababu ya dhambi. Uchungu, kuzeeka na kifo vilianza. (Soma 1 Wakorintho 15:22.) Kufanya kazi na kujikimu kimaisha kukawa kugumu. Mahusiano ya kibinadamu yakajaa migogoro. Kadiri miaka ilivyopita na watu kuongezeka, matokeo ya dhambi yaliongezeka zaidi ya vile Adamu na Hawa wangeweza kufikiria.
Maneno ya Kiebrania na Kigiriki Yanayomaanisha Dhambi
Lugha nyingi zina visawe tofauti vya dhambi. Kiebrania na Kigiriki, lugha asili za maandiko, pia zina maneno mengi tofauti yanayoeleza au kufafanua dhambi, ambayo yameelezwa hapa chini. Yanapochukuliwa pamoja, maneno haya yanatoa taswira kamili ya dhambi.
[1]Dhambi kama kukataa mamlaka—uasi (Zaburi 51:1). Yakobo alitumia neno hili la Kiebrania alipomwambia Labani kwa hasira amwambie ni kosa gani alilomtendea (Mwanzo 31:36). Neno hilo pia linaeleza kitendo cha mfalme wa Moabu dhidi ya Mfalme Yehoramu (2 Wafalme 3:7).
Dhambi kama upotovu au upotoshaji—kile ambacho kimekunjika au kupindika (Zaburi 51:2a). Shetani hawezi kuumba kitu chochote, kwa hivyo dhambi zote ni upotoshaji wa kitu kizuri ambacho Mungu ameumba.
Dhambi kama kukosa shabaha au kushindwa kufikia lengo. Neno la Kiebrania la dhambi lililotumika katika Zaburi 51:2b lina maana hii. Neno hilo hilo linatumika kwa maana isiyo ya kimaadili katika Waamuzi 20:16, ambayo inaeleza kuhusu wapiganaji 700 waliotumia mkono wa kushoto ambao waliweza kupiga unywele mmoja kwa jiwe bila kukosa shabaha wakitumia kombeo. Dhambi ni kukosa shabaha ya ukweli, utakatifu, au haki ya Mungu.
Neno la Kigiriki katika Agano Jipya lina maana sawa na hilo. Neno hilo linaweza kutumika kwa ajili ya dhambi za ulimwengu mzima (Mathayo 1:21) au dhambi za mtu mahususi kama vile dhambi za mwanamke aliyeosha miguu ya Yesu (Luka 7:48-50) au dhambi ya mtu binafsi kama vile dhambi ya kumuua Stefano (Matendo 7:60). Dhambi ni kukengeuka kutoka kwenye mapenzi ya Mungu.
Dhambi kama kitu kibaya, kinyume cha kitu chema (Zaburi 51:4). Neno hilo hilo la Kiebrania limetumika kueleza kuhusu wale ng’ombe saba waliokonda katika ndoto ya Farao (Mwanzo 41:19) na tini ambazo hazingeweza kuliwa katika Yeremia 24:2.
Dhambi kama kukataa kusikia, na hivyo kusababisha kutotii (Warumi 5:19). Mfano wa tabia hii umetolewa katika Matendo 7:57, ambapo wale waliokuwa wakimpiga Stefano mawe waliziba masikio yao. Muhtasari bora zaidi wa neno hili la Kigiriki ni kutotii.
Dhambi kama kuvunja sheria fulani mahususi—kufanya kinyume cha kile ambacho Mungu anataka (1 Yohana 3:4). Neno hilo la Kigiriki limeundwa na maneno mawili ambayo kwa pamoja yanamaanisha “hakuna sheria” au “kuasi sheria.”
Dhambi kama kugeuka kando kwa makusudi au kuvuka mipaka ya kile kinachojulikana na kuhitajika na Mungu (Kutoka 32:7-8). Katika kifungu hiki, watu walianza kugeuka kando kutoka kwa Mungu wakati Musa alikuwa juu ya Mlima Sinai.
Dhambi ambazo si za makusudi (Mambo ya Walawi 4:2). Aina hii ya dhambi inajadiliwa katika Agano la Kale na Agano Jipya. Neno la Kigiriki linalotumiwa katika Waebrania 9:7 linatokana na kitenzi kinachomaanisha “kutojua,” au “kutoelewa,” na kwa hivyo linamaanisha “kutenda dhambi kwa kutojua.” Kifungu hiki kinaeleza upatanisho ambao Kuhani Mkuu alifanya kwa ajili ya dhambi za watu ambazo si za makusudi.
Kutokana na maneno haya tunaona kwamba dhambi ni tatizo lenye vipengele vingi. Baadhi ya maneno yanaeleza dhambi katika maana yake ya jumla. Maneno mengine yanaonyesha dhambi inayotokana na kukataa kusikia Neno la Mungu, dhambi zinazotokana na kushindwa kuishi kulingana na kiwango fulani, dhambi za makusudi za kudhamiria, au dhambi zinazotokana na kutojua au hata bahati mbaya. Vyovyote ilivyo, ni baraka kukumbuka kwamba Yesu alikufa msalabani ili kuwaokoa watu kutokana na dhambi zao (Mathayo 1:21).
“Dhambi na mwana wa Mungu hawaambatani. Wanaweza kukutana mara moja moja lakini hawawezi kuishi kwa amani"
John Stott
Dhambi ya Makusudi
► Dhambi ya makusudi ni nini?
Dhambi ya makusudi ni ukiukaji wa makusudi wa mapenzi ya Mungu yanayojulikana. (Soma 1 Yohana 3:4; Yakobo 4:17.) Ni wakati mtu anachagua kufanya au kuendelea kufanya yale ambayo anajua ni mabaya au kutofanya kile kilicho sahihi. Ni kufanya makosa kwa makusudi.
Katika 1 Yohana 3:5-6 Mtume Yohana anaandika,
Nanyi mnajua ya kuwa yeye [Yesu] alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.
Dhambi inayozungumziwa hapa ni mazoea ya kuendelea kutenda dhambi ya makusudi. Tafsiri iliyopanuliwa ya kifungu hicho itakuwa hivi: Yeyote anayeendelea kukaa ndani ya Yesu hatendi dhambi mara kwa mara au kwa mazoea, na yeyote ambaye anaendelea au ana mazoea ya kutenda dhambi hajamwona wala hajamjua.
Ikiwa mtu atafasiri kwamba kifungu hiki kinazungumzia dhambi katika maana yake ya jumla (ikijumuisha dhambi kutokana na kutojua na dhambi zisizo za makusudi), kauli hii haina maana. Wakristo bado wana mapungufu ambayo si ya makusudi. Hata hivyo, ikiwa mtu anaelewa kwamba dhambi (katika kifungu hiki) inamaanisha “kukataa kwa makusudi sheria ya Mungu,” basi kifungu hicho kinaleta maana nzuri kabisa.
Upotovu wa Kurithi
► Je, unaweza kuelezeaje asili ya dhambi ambayo watu huzaliwa nayo?
Upotovu wa kurithi ni upotovu wa asili ya kimaadili ya mwanadamu ambao unampa msukumo wa kutenda dhambi tangu anapozaliwa. Wakati mwingine unaitwa dhambi ya asili. Ni asili ya dhambi ambayo tunazaliwa nayo kwa sababu ya dhambi ya Adamu.
Watu wote wana msukumo huo wa kutenda uovu tangu wanapozaliwa. (Soma Zaburi 58:3.) Asili ya mtu tayari imepotoshwa na msukumo wa kutenda dhambi tangu anapozaliwa. Mtu
huanza kutenda dhambi mara tu anapoanza kufanya maamuzi. Msukumo wa kutenda dhambi si kitu anachojifunza kutokana na mazingira yake.
Daudi alisema kwamba alizaliwa katika uovu na mimba yake ilitungwa katika dhambi. (Soma Zaburi 51:5.) Hakumaanisha kwamba mama yake alifanya makosa. Alimaanisha kwamba wakati mtoto mchanga anaumbwa tumboni, asili yake tayari huwa imesharibiwa na dhambi.
Kwa sababu ya asili iliyoharibika, mfano wa Mungu ulio ndani ya watu umeharibiwa. Kila mtu amezaliwa na nia ambayo ni ya ubinafsi na yenye msukumo wa kutenda dhambi (Warumi 3:10-12). Nia zetu hazina uhuru wa kuchagua haki isipokuwa Mungu atupe hamu na nguvu ya kufanya hivyo. (Soma Warumi 6:16-17.)
Upotovu wa kurithi huchochea dhambi za ndani kama vile kiburi, wivu, chuki na kutosamehe. Pia huchochea matendo ya dhambi.
Kwa kawaida watu wana mtazamo wa kuasi mamlaka ya Mungu na wana hasira na sheria yake. Wanaotenda dhambi watahukumiwa si tu kwa ajili ya matendo yao ya dhambi bali pia kwa ajili ya mtazamo wao wa kumuasi Mungu. (Soma Yuda 1:15.)
Mtu aliye na asili ya dhambi kwa kawaida ni mwenye ubinafsi. Anataka kudai mapenzi yake mwenyewe badala ya kujiweka chini ya mamlaka ya Mungu na wengine. Anataka kutosheleza tamaa zake mwenyewe badala ya kumpendeza Mungu. Anajiamini na hataki kumtegemea Mungu. Mafanikio yake mwenyewe ni muhimu zaidi kwake kuliko utukufu wa Mungu.
Watu hawapambanui kwa usahihi mema na mabaya, kwa sababu akili zao zimetiwa giza. (Soma Waefeso 4:17-18.) Kwa sababu ya asili yao, wanafuata mwelekeo wa ulimwengu wenye kuasi, udhibiti wa Shetani, na tamaa zao zilizopotoka; na wanajiweka chini ya ghadhabu ya Mungu. (Soma Waefeso 2:2-3.) Msukumo wao wa asili ni kutenda dhambi kila wakati (Mwanzo 6:5).
Bila msaada wa neema ya Mungu, watu wasingeweza kufanya kitu chochote kizuri; wala wasingetamani hata kutenda mema. Wasingeweza kutubu au kumtafuta Mungu. (Soma Yohana 6:44.) Wamekufa katika makosa na dhambi (Waefeso 2:1). Wanatheolojia wanafafanua hali hii kama “upotovu kamili.”
Ni muhimu kujua jinsi neema ya Mungu inavyoitikia upotovu wa kurithi. Kwanza, nguvu ya Mungu huja na ujumbe wa injili, ikimpa mtu aliyepotea hamu na uwezo wa kuitikia injili. (Soma Warumi 1:16.) Kisha, mtu anapookolewa, anakombolewa kutokana na udhibiti wa dhambi (Warumi 6:11-14). Hata hivyo, ushawishi wa upotovu wa kurithi unaendelea katika maisha ya Mkristo mpya.
Ushawishi wa upotovu wa kurithi katika maisha ya Mkristo unadhihirika kwa njia kadhaa.
1. Mkristo mpya wakati mwingine atapambana na nia yake mwenyewe wakati wa majaribu.
2. Mkristo mpya atahisi nia mbaya ambazo lazima azipinge.
3. Mkristo mpya atakuwa na miitikio na mitazamo mibaya ambayo yatatokea kabla hajaitambua.
Mkristo mpya lazima atiwe moyo ili asiache imani yake kwa sababu anahisi kwamba angali ana msukumo wa kutenda dhambi. Anapaswa kuendelea kutafuta nguvu na mabadiliko yanayotimizwa na Roho wa Mungu.
Mchungaji lazima awe na subira na Wakristo wapya. Ni lazima atambue kwamba hawatakuwa Wakristo thabiti katika yote wanayosema na kufanya. Huenda wasione mapungufu yao mara moja.
Ukiukaji usiokuwa wa makusudi
Wakati mwingine kwa bahati mbaya au kutojua mtu anakiuka Neno la Mungu bila kukusudia. Katika Mambo ya Walawi 4:2-3, tunaona kwamba katika hali hiyo, mtu alihitaji kutoa dhabihu mara tu baada ya kutambua kwamba amefanya makosa. Kwa sababu kifo cha Kristo kinachukua nafasi ya dhabihu zote za Agano la Kale, tunajua kwamba Wakristo wamekombolewa kutokana na ukiukaji usio wa makusudi.
Ukiukaji usiokuwa wa makusudi hauepukiki mradi uelewa wetu ni mdogo. Hauvunji uhusiano wetu na Mungu kwa sababu haupingani na upendo wetu kwa Mungu. Mungu alisema kwamba kumpenda kikamilifu kunatimiza yale anayotaka tufanye. (Soma Mathayo 22:37-40; Warumi 13:8-10.) Hatuwajibiki juu ya mambo ambayo hatuyajui. (Soma Yakobo 4:17.)[1]
Kadiri tunavyoenenda katika nuru (kuishi kulingana na ukweli tunaoujua), tunatakaswa kutokana na dhambi zote. (Soma 1 Yohana 1:7.) Hatuhitaji kuogopa kwamba ukiukaji usiokuwa wa makusudi utavunja uhusiano wetu na Mungu, kwa sababu tunatumainia upatanisho wa Kristo.
Kitabu cha Mambo ya Walawi kinaonyesha kwamba tunapotambua kwamba tumefanya makosa bila kukusudia tunapaswa kutubu, kumwomba Mungu msamaha, na kurekebisha maisha yetu yawe jinsi Mungu anavyotaka.
Kadiri tunavyojifunza Neno la Mungu, kumfuata Roho Mtakatifu, kuwa na ushirika na waumini wengine, na kukua katika ukomavu, tunapaswa kubadilisha tabia zinazotufanya tukiuke mapenzi ya Mungu bila kukusudia.
► Je, kwa nini tunapaswa kutaka kujua na kufanya mapenzi ya Mungu vizuri zaidi?
Sababu kwa nini tunapaswa kutaka kuelewa mapenzi ya Mungu vizuri zaidi na kuyafuata kikamilifu:
1. Hatutaki kufanya jambo lolote lisilompendeza Mungu.
2. Kuna matokeo mabaya ya kutenda mabaya hata kama ni bila kukusudia.
3. Tunahitaji kuwa mifano bora kama Wakristo.
4. Tukijaribu kuepuka mapenzi ya Mungu tunakuwa na hatia ya dhambi.
Kadiri tunavyokua katika kuelewa mapenzi ya Mungu, wakati mwingine tunatambua makosa katika maisha yetu. Ikiwa tunatambua kwamba jambo tunalofanya si sahihi, lakini tukachagua kulifanya hata hivyo, hilo si kosa linalotokana na kutojua tena. Tukikataa kubadilika, kosa hilo linakuwa dhambi ya makusudi.
“Ukuu katika ufalme wa Mungu unapimwa kwa misingi ya utiifu.”
John Stott
Hitimisho
Wakati mwingine wanatheolojia hawatofautishi kati ya aina za dhambi. Wanaweza kusema kwamba kila kitu ambacho si kamili ni dhambi, au wanaweza kusema kwamba tendo la kukusudia tu ndio dhambi. Tukielewa aina za dhambi, tunaweza kuelewa vizuri zaidi kile ambacho Mungu anataka kutufanyia kwa neema yake.
Dhambi ya makusudi inapaswa kushindwa wakati mtu anazaliwa mara ya pili. Yohana anatangaza kwamba mtu aliyezaliwa mara ya pili hatendi dhambi kwa mazoea (1 Yohana 3:4-9). Dhambi ya makusudi haiambatani na imani katika Kristo. Uasi wa makusudi si sehemu ya tabia ya muumini wa kawaida.
Utakaso ni kazi ya Mungu ya kushughulikia dhambi za asili ya mwanadamu, ili waumini wawe watakatifu kabisa (1 Wathesalonike 5:23). Roho, nafsi, na miili yao yote inakuwa bila lawama. Utakaso hushinda dhambi za asili ya mwanadamu.
Dhambi za kutojua si kutotii kwa makusudi, na hazitokani na asili ya dhambi, bali zinatokana na mwili na akili iliyoanguka. Hakuna uwezekano wa kukombolewa kikamilifu kutokana na aina hii ya dhambi wakati wa maisha ya hapa duniani. Wakati wa ufufuo, mtakatifu aliyetukuzwa atakuwa huru kutokana na aina zote za dhambi kikamilifu na milele.
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Dhambi ya mwanadamu ilitokana na uamuzi wa hiari wa kutomtii Mungu uliofanywa na watu walioumbwa kwanza. Watu wote isipokuwa Yesu wamerithi upotovu wa Adamu na pia wana hatia ya kutenda matendo ya dhambi. Huenda makosa ya wanadamu yakakiuka sheria ya Mungu lakini hayavunji uhusiano wetu na Mungu. Kila mtenda dhambi ataadhibiwa milele ikiwa hatapata msamaha wa Mungu kabla ya hukumu ya mwisho.
Mazoezi ya Somo la 5
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Warumi 1:21-32
Warumi 3:10-20
Wagalatia 5:16-21
Waefeso 5:1-8
Tito 1:10-16
Yakobo 4:1-4
2 Petro 2:9-17
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 5. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 5
(1) Orodhesha sababu tatu kwa nini ni lazima tuelewe dhambi.
(2) Je, tunajuaje kwamba dhambi haikuwa kosa la Mungu?
(3) Toa ufafanuzi wa sentensi moja kwa kila moja ya yafuatayo: dhambi ya makusudi, upotovu wa kurithi, na ukiukaji usio wa makusudi.
(4) Je, ni kwa nini tunapaswa kutaka kuelewa na kutekeleza mapenzi ya Mungu vizuri zaidi?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.