Kwa nini Uvuvio wa Maandiko unamaanisha kwamba haina makosa.
Maneno iliyovuviwa, isiyo na makosa, na sahihi.
Kwa nini Biblia imemalizika na haiwezi kupanuliwa/kuongezwa?
Ni kwa namna gani Biblia ni chanzo cha msingi na mamlaka ya mwisho kwa ajili ya mafundisho?
Ni kwa namna gani Biblia ni muhimu kwa Maisha ya kila siku ya mkristo.
Tamko la Imani ya Kikristo kuhusiana na Biblia.
(2) Mwanafunzi aepuke kusikiliza mamlaka isiyo sahihi au kujifunza Biblia akiwa na kusudi lenye mipaka.
Utangulizi
Angalizo kwa kiongozi wa darasa: Mara zote kipindi kitaanza na jaribio juu ya somo lililopita na kurudia malengo ya somo lililopita. Kwa sababu hili ni somo la kwanza, nenda katika kusoma kifungu cha maandiko hapa chini.
► Soma Zaburi 119:1-16 kwa pamoja. Kifungu hiki kinatueleza nini kuhusu Biblia?
Mungu, Muumbaji wa ulimwengu, ameongea. Amejifunua mwenyewe na kusudi la uumbaji wake. Kweli ya Mungu imefunuliwa kwetu sisi inaitwa ufunuo. Kwenye Biblia kuna kitabu kinaitwa “Ufunuo,” lakini neno Ufunuo linaweza pia kutumika kwa ajili ya kweli ambayo Mungu ameifunua.
► Ni baadhi ya njia gani ambazo Mungu amefunua kweli yake kwetu sisi?
Aina mbalimbali za Ufunuo
Kwa sababu Mungu amefunua kweli katika njia tofauti tofauti, tunazungumzia makundi mawili: Ufunuo wa Jumla na Ufunuo Maalumu.
Ufunuo wa Jumla
Ufunuo wa Jumla ni ule ambao Mungu ametuonesha sisi kuhusu Yeye kupitia uumbaji. Tunaona ufahamu wa ajabu na nguvu ya Mungu katika muundo/usanifu wa ulimwengu.
Uumbaji mkuu wa Mungu ni mwanadamu. Tunajifunza baadhi ya vitu kumuhusu Mungu tunapotazama namna wanadamu walivyosanifiwa/walivyotengenezwa. Ukweli kwamba tunaweza kuwaza kimantiki, kutambua na kukubali uzuri, na kuweza kutofautisha kati ya jema na baya (ingawaje si kikamilifu) inatuonesha sisi kwamba Muumbaji wetu ni lazima ana sifa hizo katika hali ya juu zaidi. Tunafahamu kwamba Mungu ni lazima awe ambaye anaweza kufikiri na kuwasiliana kwa sababu sisi tuna uwezo huo.
Kwa sababu Ufunuo wa Jumla unatuonesha sisi kwamba Mungu anaweza kuongea, tunatambua kwamba Ufunuo Maalumu unaweza kutokea. Kwa sababu Mungu anaweza kuongea, inawezekana kuwa na jumbe kutoka kwa Mungu na hata kuwa na kitabu kutoka kwa Mungu.
Kwa Ufunuo wa Jumla, watu wanafahamu kwamba kuna Mungu, kwamba wanapaswa wamtii, na kwamba tayari wameshamuasi. (Soma Warumi 1:20-21.) Lakini Ufunuo wa Jumla hautuambii namna ya kuja katika uhusiano sahihi na Mungu. Ufunuo wa Jumla unatuonesha sisi uhitaji wa Ufunuo Maalumu kwa sababu unatuonesha kwamba watu ni waovu na hawana udhuru mbele za Muumbaji, lakini hautuambii sisi suluhisho.
Ufunuo Maalumu
[1]Mungu alitupa sisi Ufunuo Maalumu kupitia maandiko yaliyovuviwa na Yesu, mwana wake. Ufunuo Maalumu unaelezea hali tuliyo nayo kwa sasa kama inavyooneshwa na Ufunuo wa Jumla: anguko na hatia. Ufunuo Maalumu unamuelezea Mungu, unaelezea Anguko na dhambi, na unaonesha njia ya kupatana na Mungu.
Fikiri kwamba haukufahamu kwamba kuna Biblia. Unatambua kwamba kuna Mungu. Na unafahamu kwamba umemkosea Mungu. Haufahamu nini kinafuata baada ya kifo. Haufahamu kusudi la maisha. Haufahamu namna ya kumwendea Mungu.
Kisha tafakari kwamba kuna mtu anakuonesha kitabu na anakuambia kwamba kimetoka kwa Mungu ili kujibu maswali hayo. Unaweza kufikiri kitabu hiki kitakuwa na thamani kiasi gani?
“Siamini kwamba mtu yeyote anaweza kuhubiri injili ambaye hajahubiri Sheria. Dharau sheria na uzime mwanga ambao kwa huo mwanadamu huelewa hatia yake.”
– Charles Spurgeon
Madai ya Biblia
► Biblia inadai nini kuhusu yenyewe? Toa baadhi ya mifano ya matamko kutoka katika Biblia yanaonesha madai kwamba imetoka kwa Mungu.
Hebu tuzungumze kuhusiana na madai ya Biblia kuhusiana na biblia yenyewe. Kisha, tutatazama Ushahidi kwamba Biblia ni ya kweli. Biblia inasema kuwa yenyewe ni neno la Mungu. Katika Agano la Kale, kuna matamko zaidi ya 3,000 kwamba ujumbe ulitoka kwa Mungu, mara nyingi ikitajwa kama, “BWANA akanena….”[1] Yesu alilichukulia Agano la Kale kuwa limevuviwa na Mungu. (Soma Mathayo 5:17-18; Yohana 10:35; Marko 12:36.) waandishi wa Agano Jipya walilichukulia Agano la Kale kuwa limetoka kwa Mungu. (Soma Matendo ya Mitume 3:18; 2 Timotheo 3:16; 2 Petro 1:20-21.) Waandishi wa Agano Jipya walilichukulia Agano Jipya kuwa limevuviwa na Mungu. (Soma 1 Wakorintho 14:37; 2 Petro 3:16.)
Endapo mtu hatakubali madai ya Biblia kuhusiana na yenyewe, anapaswa kutazama Ushahidi. Fikiri tena kwamba haukuifahamu Biblia. Unafahamu kwamba Mungu ni nafsi na anaweza kuzungumza kama akitaka kufanya hivyo. Kwa hiyo, unafahamu kwamba kitabu kutoka kwa Mungu kinawezekana. Kisha mtu anakuonesha kitabu na anakuambia kwamba kimetoka kwa Mungu.
► Ni kwa namna gani unafahamu kwamba Biblia kweli ni Neno la Mungu? Unategemea kingekuwa namna gani?
[2]Mahali ambapo injili inahubiriwa, mahali popote ulimwenguni, watu wapata msukumo wa ndani kwa kweli yake. Wanapoamini injili na kutubu, wanapata uzoefu au ujuzi wa msamaha wa Mungu na Maisha yaliyobadilishwa. Kwa watu wengi, hiyo ndiyo sababu yao ya kwanza ya kuamini Biblia. (Soma 1 Wathesalonike 1:5.)
Kisha kwa wale ambao wapo katika mahusiano na Mungu, Roho wa Mungu anazungumza kupitia maandiko, akiwapa msukumo uelewa na msukumo wa ndani. Namna ambayo Roho Mtakatifu anatumia Biblia inathibitisha kwamba ni Neno la Mungu. (Soma Waefeso 6:17.)
Tunapotembea katika mahusiano na Mungu, tunagundua kwamba Biblia inafunua kwa usahihi asili yake na namna anayotenda kazi pamoja ndani yetu. Biblia inatuonesha sisi njia au namna ya kuanza mahusiano na Mungu na njia au namna ya kuendelea Naye. Huu ni Ushahidi kwamba Biblia ni Neno la Mungu. (Soma Zaburi 119:1-2.)
Lakini vipi kama unataka Ushahidi ambao hauna msingi katika uzoefu wako wa Kiroho? Watu katika dini nyingine wana uzoefu pia, uzoefu wao hauna misingi katika kweli. Ni kwa namna gani tunaweza kufahamu kwamba uzoefu wetu unamsingi katika kweli?
► Kuna Ushahidi wowote kwamba Biblia ni sahihi katika mambo inayosema?
Biblia imeandikwa na waandihi zaidi ya 40, wengi wao hawafahamiani na wenzao, katika kipindi cha zaidi ya miaka 1,500. Mara nyingi tungetegemea nini kwa kitabu kama hicho? Tugeweza kuchukulia kwamba kingekuwa na makosa ya kila namna na mgongano au kupingana. Lakini zingatia kweli zifuatazo kuhusiana na Biblia. Maelfu ya maeneo ya kijiografia yaliyotajwa katika Biblia yameonekana; maelfu ya matukio ya kihistoria na watu waliotajwa katika Biblia wamethibitishwa katika historia; hakuna hata ugunduzi mmoja uliopinga matamko ya Biblia; na kamwe Biblia haijawahi kujipinga yenyewe. Matamko hayo si kweli kwa kitabu chochote ambacho kimewahi kuandikwa. Ushahidi unaunga mkono madai ya Biblia kuwa imevuviwa na Mungu.
Tunaweza kufupisha Ushahidi ambao unaunga mkono madai ya Biblia kuwa ni neno la Mungu katika dondoo sita. Tunafahamu kwamba Biblia ni neno la Mungu kwa sababu:
Uvuvio kazi ya muujiza ambayo kwa hiyo Mungu alijifunua mwenyewe na akafanya ufunuo huo uwekwe katika maandishi. Biblia ni zao (matokeo) la mwisho la Uvuvio. Biblia imevuviwa na hakuna kitabu kingine kilichovuviwa. Uvuvio wa Biblia una maana kwamba ni Neno la Mungu kamilifu, hata katika maneno yaliyotumika.
Wakati mwingine watu huhisi kwamba wamevuviwa wanapokuwa na mawazo makubwa, lakini Biblia inamaanisha Zaidi ya hivyo inasema kuwa imevuviwa na Mungu.
Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki (2 Timotheo 3:16).
Kupitia maandiko yaliyotoka katika kalamu za mikono ya wanadamu, msisitizo wa mstari huu ni kwamba Biblia imetoka kwa Mungu. Kwa sababu Biblia imetoka kwa Mungu, ni ya kuaminiwa na kutegemewa kwa mafundisho. Ni bora kuliko kitu wanachoweza kufanya watu wazuri na mashuhuri.
Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu (2 Petro 1:20-21).
Mistari hii katika 2 Petro inasema kwamba waandishi walichukuliwa na Roho Mtakatifu. Usahihi wa waandishi wa Biblia haukutegemea fahamu zao wenyewe. Ukweli kwamba walisukumwa, au walichukuliwa na Roho Mtakatifu katika kuandika kwao, unaonesha kwamba kutegemewa na kuaminiwa kwa maandiko kulimtegemea Mungu. Biblia ni ya kutegemewa na kuaminiwa kama Mungu.
Uvuvio ukoje?
► Ni baadhi ya njia gani ambazo waandishi wa Biblia walipokea kweli ya Mungu kabla hawajaiandika?
Baadhi ya watu hushangaa namna ambavyo Uvuvio unafanya kazi. Ni kwa namna gani Mungu aliwasilisha kweli yake na akahakikisha inarekodiwa kwa usahihi? Kweli ya kwanza ambayo tunapaswa kuiona kuhusiana na muundo wa ufunuo ni kwamba una namna mbali mbali. Yeye hafungwi na aina fulani ya njia. (Soma Waebrania 1:1.)
Wakati mwingine Mungu alizungumza kwa sauti ya kusikika, kama alivyozungumza na Musa (Kutoka 33:11). Wakati mwingine alitoa maono na ndoto, na waandishi walizielezea.[1] Pengine sehemu ya maandiko ambayo ilikuja moja kwa moja zaidi kutoka kwa Mungu hadi kuandikwa ni agano na Israeli ambalo liliandikwa kwa kidole cha Mungu (Kumbukumbu la Torati 9:10). Sehemu nyingine inaonekana zilitamkwa, kwa sababu sehemu kubwa katika Kutoka, Mambo ya Walawi, na Hesabu zinakuja baada ya tamko, “BWANA akanena na Musa, na kumwambia…”
Uvuvio haumaanishi kwamba Mungu alizungumza maneno kwa waandihi katika sauti inayosikika. Tunaone tofauti katika silka na aina ya uandishi baina ya waandishi mbalimbali. Kwa mfano, aina ya uandishi ya Paulo ni tofauti na ya Petro. Mtazamo wetu wa Uvuvio unatambua Mungu kutumia silka, misamiati, aina za uandihi, elimu, na utafiti wa kihistoria wa waandishi.
Mtazamo sahihi wa Uvuvio ni kwamba Mungu alimvuvia mtu kwa ujumla wake, akitumia fikra za waandishi wanadamu na silka zao ili kuelezea kweli ya kimungu, sio tu kufunua kweli bali pia kusimamia mchakato wa uandishi ili kuleta usahihi.
Baadhi ya watu wanafikiri kwamba Mungu alitoa mawazo ambayo alitaka kuyawasilisha, na waandishi wanadamu wakayapanua mawazo hayo kwa namna nzuri waliyoweza, kufanya makosa ya kibinadamu hayaepukiki katika undani wa taarifa. Mtazamo huo haufai katika maelezeo ya Uvuvio. Biblia inawaelezea waandishi kwamba alichukuliwa na Roho Mtakatifu katika uandishi wao, kwa hivyo tunafahamu kwamba hawakuachwa ili waandike peke yao, huku wakifanya makosa.
Kwa sababu Biblia ni Neno la Mungu, halisemi chochote ambacho si sahihi kwa sababu Mungu hafanyi makosa. (Soma Mithali 30:5.) kwa sababu Mungu amejifunua mwenyewe katika historia iliyorekodiwa katika Biblia, taarifa lazima ziwe sahihi ili kwamba tuwe na ufunuo unaoaminika wa Mungu. Kwa hivyo, kwa sababu ya maelezeo ya kibiblia ya Uvuvio, tunafahamu kwamba Mungu aliongoza uandishi ili kwamba uwe sahihi kikamilifu.
[1]Kwa mifano ya ufunuo kwa maono, ona Danieli 7 na 8, na sehemu kubwa ya kitabu cha Ufunuo.
Maneno Yaliyotumika Kutetea Usahihi Kamili wa Biblia
Imevuviwa
Biblia imevuviwa, ambayo ina maana kwamba ni Neno la Mungu kikamilifu, hata katika maneno yaliyotumiwa. Neno hili kwa asili lilikuwa linatosha kabisa kutangaza uhakika, uaminifu, na usahihi wa Biblia, lakini sasa baadhi ya watu wanaosema wanaamini Biblia kuwa imevuviwa wanakana kwamba si sahihi kikamilifu. Maneno yafuatayo yamekuja katika matumizi ili kutetea nyanja muhimu na za msingi za Uvuvio.
Haina Makosa
Neno hili linamaanisha “haliwezi kuangusha.” Tunaposema kwamba Biblia haina makosa, tuna maana kwamba inaweza kuaminiwa na haiwezi kutukosesha wala kutupotosha. Biblia haina makosa sio tu katika matamko yake ya mafundisho, bali katika kila tamko ambalo Biblia inatamka.
Sahihi/Kamilifu
Neno hili linamaanisha “pasipo/bila makosa.” Biblia ni sahihi katika kila tamko ambalo inalitoa. Kwa sababu Mungu hawezi kudanganya au hawezi kufanya makosa (Soma Tito 1:2) na Biblia ni Neno la Mungu, tunaweza kuwa na uhakika kwamba haina makosa. Endapo mtu anasema kwamba Biblia inaweza kuwa na makosa kwa sababu wanadamu walihusika katika uandishi wake, anasahau maelezo ya Uvuvio katika 2 Petro 1:21: Waandishi waliongozwa na Roho Mtakatifu. Mtazamo wa Kibiblia, wa kihistoria wa Uvuvio ni kwamba Biblia nzima imevuviwa, hata katika kila neno, na kwa hivyo haina makosa. (Soma Mathayo 5:18.)
Vipi Kuhusiana na Makosa ya Kunakili?
Kabla ya mashine za kunakili kugunduliwa, hati na nyaraka zote zilinakiliwa kwa mkono. Hatuna nakala za asili za mwanzo zilizoandikwa na Paulo, Isaya, au Musa. Kati ya nakala maelfu ya kale, yaliyoandikwa kwa mkono tuliyo nayo ya Kiyunani na Kiebrania, kuna tofauti chache, na wakati wote hatuwezi kufahamu kwa hakika maneno ya halisi yalikuwa yapi. Hata hivyo, tofauti ni ndogo sana kiasi kwamba hakuna hata fundisho moja linalotiliwa shaka kwa sababu ya tofauti hizo. Kwa sababu tunafahamu kwamba nakala halisi ilikuwa haina makosa, na kwa sababu utofauti katika kunakili ni ndogo sana, tunafahamu kwamba tunaweza kuamini kila tamko linatamkwa na Biblia.
► Ni kwa namna gani tunafahamu Biblia ni sahihi hata kama ilinakiliwa kwa mkono mara nyingi sana?
► Ni sababu gani mbalimbali zinazosababisha baadhi ya watu kufikiri kwamba Biblia ina makosa?
Kwa nini Baadhi ya Watu Wanafikiri kwamba Biblia ina Makosa?
Wakati mwingine watu wanadai kwamba Biblia ina makosa. Hiyo ni kwa sababu hawaelewi asili ya Biblia.
Biblia inatumia mawasiliano ya wanadamu. Kwa mfano, kuna mstari ambao unazungumza kwamba jua linatembea angani. Wanasayansi wengi huamini kwamba dunia ndio inayotembea, na si jua linalotembea, lakini pia wanazungumza kuhusiana na jua kuchomoza na kuzama. Kwa urahisi wanaelezea kitu kama wanavyokiona.
Pia kuna sentensi za kishairi, kama “Milima iliruka kama kondoo waume, Vilima kama wana-kondoo” (Zaburi 114:4), au “miti yote ya kondeni itapiga makofi” (Isaya 55:12). Hii ni aina ya mtindo wa fasihi ambayo si lugha ya moja kwa moja.
Wakati mwingine waandishi hunukuu watu, wakiwemo watu ambao hawakuvuviwa. (Kwa mfano, mazungumzo ya marafiki wa Ayubu waliandikwa, hata kama Mungu alisema hawakuongea kilichokuwa sahihi (Ayubu 42:7).)
Chochote hapo hakina tatizo na fundisho la Uvuvio. Mungu aliongoza mchakato wa uandishi ili kuhakikisha kwamba zao la mwisho ni Neno lake.
Wakati mwingine watu wanafikiri wanaona mgongano au ukinzani katika Biblia, lakini wanapaswa kuangalia kwa umakini zaidi. Kwa mfano, Marko 5:1-2 na Luka 8:26-27 wanatueleza kuhusiana na mtu aliyepagawa na mapepo ambaye alifunguliwa na Yesu. Mathayo 8:28 anatueleza kwamba walikuwa watu wawili waliofunguliwa. Huu sio mgongano. Luka na Marko hawakusema alikuwa mtu mmoja tu. Walichagua kuelekeza umakini kwa mtu mmoja ambaye alikuwa na historia katika eneo hilo. Endapo mtu anaona sentensi katika Biblia inayoonekana kukinzana na nyingine, hapaswi kufanya haraka kwenda katika hitimisho, bali achukue muda ili kuuelewa muktadha.
Biblia kwa ajili ya Wakristo
► Ni njia gani baadhi ambazo Wakristo wanaitumia Biblia?
Biblia inatoa sheria ya Mungu. Kushika sheria hakutuokoi, lakini sheria inatuonyesha jinsi Mungu anavyotaka tuishi. Sheria ya Mungu inaonyesha tabia ya Mungu. Tunapaswa kuifuata kwa sababu tunataka kuwa kama Mungu. Kwa kuwa tunampenda Mungu, tunapaswa kuipenda sheria yake pia. Zaburi 119 inaelezea jinsi anayemwabudu Mungu anavyopaswa kuifurahia sheria ya Mungu. Mtu anayempenda Mungu ataomba Mungu aubadilishe moyo wake ufanane na mapenzi ya Mungu. Haiwezekani mtu anayempenda Mungu asiwe na shauku ya kumpendeza Mungu.
Neno la Mungu ni nuru. Mtume Petro anatuambia kwamba ulimwengu uko katika giza la kiroho, na Neno la Mungu ni nuru ya kuongoza njia ambayo tunapaswa kuiendea. (Soma 2 Petro 1:19-21; ona pia Zaburi 119:105.) Kamwe mtu hapaswi kufuata mawazo au hisia zinazopingana na Neno la Mungu. Roho Mtakatifu hawezi kumwongoza mtu kufanya jambo ambalo Biblia inasema ni dhambi.
[1]Neno la Mungu ni chakula chetu cha kiroho. Hamu nzuri ya kula ni dalili ya afya, na Mkristo atalitamani Neno la Mungu kama mtoto mchanga anavyotamani maziwa (1 Petro 2:2). Kwa kadiri Mkristo anavyokua, ndivyo anavyoweza kuelewa na “kumeng’enya” kweli zaidi ya Mungu, kama mtoto anavyojifunza kula chakula kigumu (1 Wakorintho 3:2). Mkristo lazima ale kiroho kila siku kwa Neno la Mungu.
Biblia ni ulinzi wetu dhidi ya Shetani. Tumeamriwa kujivika silaha za kiroho. Upanga anaotupatia Roho Mtakatifu ni Neno la Mungu (Waefeso 6:17). Yesu alijibu majaribu ya Ibilisi kwa kutumia Maandiko (Mathayo 4:3-4).
Neno la Mungu ni kweli ambayo inayohitaji mwitikio wetu. Yesu alilifananisha Neno na mbegu zinazopandwa (Luka 8:11-15). Baadhi ya mbegu hazikufanikiwa kwa sababu udongo ulikuwa haujaandaliwa. Tunaposoma Biblia, ni lazima tuitikie kweli yake na kumuomba Mungu alete matunda katika maisha yetu kupitia Neno lake.
“Uongo mkubwa wa aina mbili ambao tamaduni zetu zimeamini leo ni kwamba sisi ni watu wazuri na kwamba, kwa sababu Mungu ni wa upendo, hata adhibu dhambi.”
– Francis Chan
Kwa sababu Biblia ni Neno la Mungu…..
Kwa sababu Biblia ni Neno la Mungu…
Halitapitwa na wakati au kukosa umaana. Linatumika kwa watu wote mahali popote na wakati wowote.
Ni kiongozi kwa sisi kupambanua mapenzi ya Mungu, kwa sababu Mungu hawezi kujipinga mwenyewe au kubadilisha akili/mawazo yake.
Ni kiongozi chetu katika kupata mema katika Maisha, kwa sababu Mungu, muumbaji wetu, aliitoa ili iwe kiongozi chetu.
Ina kila kitu ambacho tunakihitaji ili kuokolewa na ili kutembea na Mungu.
Ingawaje tunawea kujifunza kutoka kwa wachungaji wetu na kutoka katika tamaduni za kanisa, hakuna wazo linaloweza kukubaliwa kama au endapo linapingana na maandiko kwa sababu maandiko ndio mamlaka ya mwisho.
Roho Mtakatifu anaangazia Neno la Mungu kwa ajili ya uelewa wetu na kutuongoza sisi kulitii Neno.
► Mungu bado anongea, lakini tutegemee kwamba kuna kitu kitaongezwa katika Biblia?
Je Biblia Imemalizika?
Tangu mtume wa mwisho alipokufa, kanisa limechukulia Biblia kuwa ni kitabu kilichokamilika. Kanisa halikuchagua tu maandiko na kuyaita maandiko yenye mamlaka; badala yake walitambua kwamba baadhi ya maandiko yalikuwa yamevuviwa na Mungu na yalikuwa yana mamlaka ya kimaandiko. Maandiko yaliyotambuliwa kama maandiko yalikidhi vigezo ambavyo hakuna maandiko mengine ya baadae yalikidhi.
Kwa ajili ya vitabu vya Agano la Kale, kanisa lilitunza vitabu ambavyo Israeli ilikuwa imevitunza kama maandiko. Hatimaye, vitabu vya Agano Jipya vilitambuliwa kama maandiko kwa kutumia vigezo vifuatavyo:
Uhusiano wa kihistoria na mitume
Sifa ya kujithibitisha yenyewe
Kukubalika na kanisa kwa kauli moja
Matumizi yenye heshima ya Agano la Kale
Umuhimu wake katika kupinga uzushi/Imani potofu
Mungu bado anazungumza, lakini kuna kitu kinaweza kuongezwa kwenye Biblia leo? Haiwezekani kwa maandiko mapya kufikia viwango kwa ajili ya kuingizwa katika maandiko halisi. Kwa mfano, hakuna maandiko mapya ambayo yamefungamanishwa na mitume, kwa sababu hawako pamoja nasi. Pia hakuna maandiko ambayo yanaweza kukubaliwa na kanisa la ulimwengu mzima.
Maandiko yamekamilika na yanajitosheleza kwa ajili ya wokovu na maisha ya Kikristo (2 Timotheo 3:14-17). Hakuna kitu muhimu na cha msingi ambacho kinaweza kuongezwa katika maandiko kwa sababu tayari yana kila kitu tunachokihitaji. Watu wanaodai kupokea mafunuo mapya wanapaswa kutumia muda wao mwingi kujifunza ufunuo ambao tayari Mungu ameutoa. Hapo watapata yote wanayohitaji na watalindwa na makosa.
Makosa ya Kuepuka
Angalizo kwa Kiongozi wa Darasa: Washiriki wawili wa darasa wanaweza kuelezea sehemu hii na sehemu inayofuata.
Kudhoofisha/Kuhujumu mamlaka ya Biblia
Mamlaka yako ya mwisho ni nini? Wakristo wengi wanaweza kusema kwamba Biblia ndio mamlaka yao ya mwisho, lakini kiukweli wanaamini hisia zao zaidi. Mtu anaweza kusema kwamba tendo hili ni sahihi kwa sababu haukumiwi wakati anapolitenda. Mtu huyu anafanya hisia zake kuwa mamlaka ya mwisho na si Biblia.
Zipo sababu nyingi za kwa nini watu hawaichukulii Biblia kwa uzito unaostahili. Pengine mtu wanayemuheshimu anapuuza mafundisho ya wazi ya Biblia, na hii inamtia moyo mtu huyo kufanya vile vile. Pengine wana hatia kutokana na kufanya jambo ambalo Biblia inalikataza, na wanajaribu kutafuta njia ya kutetea/kuyapa haki matendo yao. Pengine hawafahamu kile ambacho Biblia inafundisha. Lazima tufanye kila juhudi ili kuielewa Biblia na kujiweka chini ya mamlaka yake.
Kujifunza Biblia ukiwa na Makusudi Finyu
Biblia ni chanzo cha msingi cha mafundisho. Ni mamlaka ya mwisho kwa swali lolote la kimafundisho. Hata hivyo, kuna shida watu wanaposoma Biblia ili tu kutafuta kuthibitisha mafundisho yao. Hawaitumii Biblia kwa ajili ya chakula cha Kiroho. Wanafikiria tu namna ya kuonesha kwamba mwingine ana makosa. Ni sahihi kwetu kutengeneza na kutetea mafundisho yetu kwa kutumia maandiko. Hata hivyo, kama hayo ndio matumizi yetu pekee ya Biblia, tutapoteza furaha ambayo huja kutokana na kuitumia katika mahusiano yetu binafsi na Mungu.
Baadhi ya watu husoma Biblia kwa ajili tu ya kusudi la kujisikia anatiwa moyo, tunahitaji kukumbuka kwamba kusudi la Biblia linajumuisha maelekezo, ushawishi, na marekebisho (2 Timotheo 3:16). Hatutakiwi kuepuka maagizo ya Biblia, ili kutafuta ahadi zinazotufanya tujisikie vizuri. Pengine leo Mungu anataka kuturekebisha au kutushawishi au kutufundisha jambo.
Makosa ya Imani Potofu
Baadhi ya dini zinadai kuamini Biblia, lakini wanafanya kitu kingine kuwa mamlaka ya mwisho. Wanadai kwamba wao pekee ndio wanaweza kuielezea Biblia, wanatumia mafunuo, au mfumo maalumu ambao wao tu ndio wanao. Mafundisho yao muhimu hayawezi kuthibitishwa kutoka ndani ya Biblia.
Wanaweza kuwa na kitabu kingine ambacho wanakitumia kama nyongeza ya Biblia. Wanaweza kusema kwamba Biblia si ya kuaminika/kutegemewa kwa sababu ya makosa ya kunakili na ya kutafsiri.
Mawazo ya namna hiyo yanaonesha kwamba Biblia haijakamilika kama neno kamilifu la Mungu. Kwa watu hao, kitu kingine kinakuwa mamlaka ya mwisho.
► Someni Tamko la Imani kwa pamoja angalau mara mbili.
Tamko la Imani
Biblia ni neno la Mungu. Mungu amevuvia waandishi ili kwamba waandike pasipo makosa. Biblia inajumuisha kila kitu ambacho tunahitaji kufahamu ili kuokolewa kutoka dhambini na ili kutembea katika mahusiano na Mungu. Biblia ni chanzo cha msingi cha mafundisho na ni mamlaka ya mwisho. Wakristo wanapaswa kujifunza Biblia kila siku ili kumfahamu Mungu vema/kwa usahihi, kuongozwa na Mungu, kushibishwa Kiroho, na kuishi maisha yenye maana na ya furaha.
Somo la 1 Mazoezi
(1) Zoezi la Kifungu: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu na kuandika aya kuhusiana na somo la somo hili.
Zaburi 119:33-40
Zaburi 119:129-136
Mithali 30:5-6
Mathayo 5:17-19
2 Timotheo 3:15-17
2 Petro 3:15-16
Ufunuo 22:18-19
(2) Jaribio: Utaanza kipindi kijacho cha darasa kwa jaribio juu la Somo 1. Jifunze kwa umakini maswali wakati wa maandalizi.
(3) Zoezi la Kufundisha: Angalau mara tatu wakati wa kozi hii, utafundisha somo au sehemu ya somo kwa kwa watu ambao hawapo darasani. Mafundisho haya yanaweza kufanyika katika darasa kanisani, au kujifunza Biblia nyumbani, au katika kutaniko la kifamilia, au katika Mazingira mengine. Unawajibika kutengeneza fursa hizi na kuripoti kwa kiongozi wa darasa.
(4) Kumbuka mara zote kusoma somo linalofuata kwa ajili ya maandalizi ya darasa linalofuata.
Somo la 1 Jaribio
(1) Ufunuo wa Jumla ni nini?
(2) Ni kwa muundo gani wa aina mbili ambao Mungu ametoa Ufunuo Maalumu?
(3) Ni mambo gani matatu ambayo Ufunuo Maalumu unafanya ambao Ufunuo wa Jumla hauwezi kufanya?
(4) Ni madai gani ambayo Biblia inayatoa kuhusiana na yenyewe?
(5) Orodhesha sababu sita zinazotufanya kufahamu kwamba Biblia ni neno la Mungu.
(6) Kwa nini Biblia inafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, ma kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki? (2 Timotheo 3:16).
(7) Ni maelezo yapi ambayo Biblia inatoa kuhusiana na uvuvio ambayo yanatuthibitishia sisi kwamba waandishi walitunzwa ili wasifanye makosa?
(8) Orodhesha njia nne za uvuvio wa ambazo Mungu alizitumia.
(9) Inamaanisha nini kwamba Biblia imevuviwa?
(10) Inamaanisha nini kwamba Biblia haina makosa? tuna maana kwamba na.
(11) Inamaanisha nini kwamba Biblia ni Sahihi/Kamilifu?
Free to print for ministry use. No changes to content, no profit sales.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom.