► Someni Waefeso 3:3-10 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu kanisa?
Katika kipindi cha karne zilizotangulia Agano Jipya, kanisa lilikuwa fumbo ambalo halikuwa limefunuliwa kikamilifu. Kulikuwa na watu waliopata neema ya Mungu na wakaishi katika uhusiano naye (Warumi 4:1-8), lakini kanisa lilikuwa bado halijaanzishwa.
► Kanisa lilianza wakati gani?
Kanisa lilianza na maisha na huduma ya Yesu. Kanisa lilijengwa kwenye msingi wa wokovu aliotoa (Mathayo 16:16-18). Enzi ya kanisa ilianza Siku ya Pentekoste. Kuanzia siku hiyo, kanisa limekuwa likifanya kazi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, bila uongozi wa kimwili na unaoonekana wa Kristo duniani (Yohana 16:7).
Yesu aliwapa wanafunzi wake mamlaka ya kueneza na kuanzisha kanuni zake kote duniani (Mathayo 28:18-20) na aliahidi kwamba Roho Mtakatifu atawaongoza kwenye kweli yote (Yohana 16:13). Kanisa linaweza kuitwa la kitume kwa sababu mafundisho ya mitume ndio kanuni za msingi za kanisa. Kanuni zozote zinazopingana na kanuni hizo za msingi hazipaswi kuitwa za Kikristo.
Kanisa lilianza kutokana na:
1. Huduma ya Yesu
2. Wokovu uliotolewa na Kristo
3. Tukio lililotokea Siku ya Pentekoste
4. Ukuzaji wa kanuni za kitume
Kanisa Kama Taasisi Iliyo Hai
Kanisa linalinganishwa na familia ambapo Mungu ni Baba na waumini ni kaka na dada (Mathayo 12:48-50, Wakolosai 1:2). Kanisa linaitwa taifa ambalo halina kabila moja wala asili ya kawaida (1 Petro 2:9-10). Kanisa linalinganishwa na mwili, ambao Kristo ndiye kichwa chake (Waefeso 4:15-16, Waefeso 5:30). Washiriki wa mwili huo wanafanya kazi pamoja na kujaliana (1 Wakorintho 12:14, 26).
Kama mshiriki wa mwili, Mkristo lazima asiwe na mtazamo wa kujitegemea bila kanisa. Anahitaji washiriki wengine, nao wanamhitaji (1 Wakorintho 12:21). Ni makosa kwa Mkristo kuishi kana kwamba anaweza kujitosheleza mwenye kiroho bila kanisa.
Kujitenga na kanisa ni kujitenga na kile ambacho Kristo anafanya duniani. Kutoheshimu na kutopenda kanisa ni kutomheshimu na kutompenda Kristo.
Kanisa kama kutaniko lililo hai la kieneo
Kuna kanisa moja la dunia nzima, hata hivyo pia kuna kanisa la kieneo. Washiriki wa mwili hawawezi kufanya kazi isipokuwa wawe pamoja mahali pamoja. Paulo aliwaandikia waumini wa Korintho akiwaambia kwamba wao ni mwili wa Kristo (1 Wakorintho 12:27), ambayo ina maana kwamba kanisa la kieneo ni mwili wa Kristo mahali hapo.
Mungu ameunda kanisa la kieneo kuwa familia ya imani:
1. Likifanya kazi kama mwili wenye karama za kiroho
2. Likikidhi mahitaji mbalimbali ya wale walio katika ushirika (kupitia rasilimali za kibinadamu na za kiungu)
3. Likionyesha ulimwengu hekima ya Mungu katika kila nyanja ya maisha
4. Likiwaalika wasioamni waongoke na kuingia katika familia
Ushirika wa kweli unajumuisha uchumi kwa sababu wale walio katika ushirika wanashiriki maisha pamoja na kuyajali mahitaji ya wengine (Yakobo 2:15-16, Yakobo 1:27). Hitaji la kaka au dada katika Kristo ni jukumu la kanisa ikiwa mshiriki huyo anashiriki katika maisha ya kanisa na anachukua majukumu kadiri anavyoweza.
Mungu hutoa karama za kiroho na miito maalum kwa ajili ya huduma ili kuimarisha na kujenga kanisa la kieneo (Waefeso 4:11-12).
Kanisa la kieneo hutumikia jamii inayoizunguka. Kipaumbele cha kwanza ni cha kiroho, kuhubiri injili na kukuza ukweli wa Mungu katika masuala yote. Kanisa hukidhi mahitaji ya kimwili katika jamii lakini huwapa kipaumbele watu walio katika ushirika wa kiroho wa kanisa (Wagalatia 6:10).
Ukamilifu wa Kanisa
Yesu alijitoa kwa ajili ya kanisa, ili kulifanya liwe takatifu na bila dosari yoyote (Waefeso 5:27). Kanisa halipaswi kamwe kuvumilia dhambi, ingawa lazima liwe tayari kusamehe. Viongozi lazima wawe mifano ya maisha matakatifu (1 Timotheo 3:2-3). Mshirika wa kanisa akitenda dhambi, lazima akabiliwe na hatimaye kuondolewa katika ushirika ikiwa hatatubu (1 Wakorintho 5:11-13).
► Kwa nini kanisa si kamilifu?
Watu wa kanisa hawatakuwa wakamilifu katika kila njia. Kwa sababu kanisa linahubiri Injili, kuna watu katika kutaniko ambao bado hawajatubu dhambi. Hata kati ya wale ambao wameokoka, kutakuwa na mapungufu katika maisha yao kwa sababu bado hawaelewi jinsi ya kutumia ukweli katika mambo yote ya maisha yao. Hata miongoni mwa Wakristo waliokomaa, kunaweza kuwa na mapungufu na mitazamo isiyofaa kwa sababu hata Mkristo aliyekomaa bado yuko katika mchakato wa kukua kiroho. Ni sehemu ya kazi ya kanisa kuendelea kufundisha na kutumia Neno la Mungu, likiwawezesha watu kukomaa kiroho (Waefeso 4:11-16; 2 Timotheo 3:16-17).
Kufafanua Kanisa
Kanisa la dunia nzima linajumuisha waumini wote wa nyakati zote na mahali pote. Wakati mwingine linaitwa kanisa lisiloonekana kwa sababu hakuna shirika la kidunia ambalo linasimamia kanisa la dunia nzima au lenye orodha ya washiriki wake.
Kanisa la kieneo ni jamii ya waumini katika sehemu moja ambao kwa pamoja wanafanya kazi ya mwili wa Kristo. Kikundi si kanisa ikiwa kimeundwa kwa ajili ya kusudi finyu zaidi.
Huu hapa ni ufafanuzi wa kina zaidi wa kanisa la kieneo ambao unalitofautisha na aina nyingine za vikundi: “Kikundi la waumini waliobatizwa [wameungana] pamoja kwa ajili ya ibada, kujengana, huduma, ushirika, na kuwafikia wengine; kukubali uongozi wa kiroho; tayari kuhudumia makundi yote ya jamii kupitia karama mbalimbali katika mwili; na kutekeleza desturi za kanisa mara kwa mara”.[1]
[1]David Dockery, Southern Baptist Consensus and Renewal: A Biblical, Historical, and Theological Proposal (Nashville: B&H Publishing Group, 2008), 127
Umoja wa Kanisa la Dunia Nzima
Kuna kanisa moja la mahali pote na nyakati zote. Yesu alisema, “Nitalijenga kanisa langu,” si “makanisa.” Mtume Paulo aliandika kwamba kuna mwili mmoja, na Roho mmoja, na tumaini moja, kama vile kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja (Waefeso 4:4-6).
[1]Kanuni za imani za Kikristo za kale zilirejelea “kanisa katoliki.” Hilo halikurejelea Kanisa Katoliki la Roma, bali kanisa la dunia nzima linalojumuisha Wakristo wote wa kweli.
Msingi wa umoja wa kanisa la dunia nzima hauko katika kuwa shirika moja, chini ya utawala mkuu mmoja. Hilo halitatokea kamwe kabla ya kurudi kwa Kristo. Watu wengine wanatamani jambo hilo litokee, lakini linaonekana si mapenzi ya Mungu kwa sababu Yesu aliwasahihisha wanafunzi walipofikiri kwamba mtu hapaswi kufanya huduma nje ya shirika lake (Luka 9:49-50). Ikiwa Yesu angetaka kuwa na utawala mkuu juu ya kanisa la dunia nzima, angebaki duniani kimwili ili kuliongoza. Hata hivyo, Yesu aliona kwamba kazi mbalimbali za Roho Mtakatifu kote ulimwenguni hazingefanyika kama inavyopaswa ikiwa Yesu angebaki duniani kimwili (Yohana 16:7).
► Je, msingi wa umoja wa kanisa la dunia nzima ni upi?
Msingi wa umoja wa kanisa la dunia nzima ni
1. Kanuni za mitume
2. Uhusiano na Kristo unaobadilisha maisha
[2]Umoja wa kikanuni haumaanishi kwamba Wakristo wanakubaliana kuhusu kila kitu, hata kuhusu kanuni zote muhimu. Unamaanisha kwamba wanakubaliana kuhusu kanuni za msingi juu ya asili ya Mungu na Kristo na mambo ya kimsingi juu ya injili. Bila hayo, wasingekuwa wanamwabudu Mungu yule yule au kuishi chini ya neema yake.
Kanuni si kitu pekee kinachohitajika kwa ajili ya umoja wa Kikristo. Wakristo wanashiriki uhusiano wa karibu kati yao kwa sababu ya uhusiano wao na Kristo unaobadilisha maisha. Kwa sababu wametubu dhambi, wameweka imani yao katika Kristo na wana Roho Mtakatifu, wana uhusiano maalum. Wakristo hutambuana kote ulimwenguni licha ya kuwa tofauti kwa njia nyingi.
“Ikiwa moyo wako uko sawa na moyo wangu, kama wangu ulivyo sawa na moyo wako, basi nipende kwa upendo mwororo, kama rafiki aliye karibu zaidi kuliko ndugu; kama ndugu katika Kristo, raia mwenzako wa Yerusalemu Mpya, askari mwenzako anayepigana vita vile vile kama wewe, chini ya Jemedari yule yule wa wokovu wetu. Nipende kama mwenzako katika ufalme na katika kuvumilia kwa subira kama Yesu, na mrithi wa utukufu wake pamoja nawe.”
John Wesley
Imefupishwa kutoka katika mahubiri yanayoitwa “Roho ya Kikatoliki”
“Nimefikia hatua ya kuamini kwamba alama ya mtu mwenye moyo uliotakaswa kweli ni kwamba anajali zaidi wokovu wa mwingine kuliko jinsi unavyojali ustawi wake mwenyewe.”
Dennis Kinlaw
Umoja wa Kanisa la Kieneo
Tunaweza kumkubali kama Mkristo mtu yeyote anayeamini kanuni za msingi na anayeonekana kuwa katika uhusiano na Kristo unaobadilisha maisha. Lakini makubaliano ya kikanuni ya kanisa la kieneo lazima yawe ya kina zaidi.
Kanisa la kieneo ni kikundi cha watu ambao wamejitolea kuabudu pamoja, kufanya uinjilisti, kuwafundisha waongofu na vijana kuwa wanafunzi, kutumikia jamii, na kufundisha masuala ya kiutendaji ya maisha ya Kikristo. Ili watu watimize kusudi hilo pamoja, ni lazima wakubaliane kuhusu mambo mengi ya kikanuni.
Kwa mfano, labda mtu katika kanisa la kieneo anawaambia vijana wote na waongofu wote wapya waombe kwa ajili ya kupokea karama ya kunena kwa lugha. Lakini viongozi wengine katika kanisa hilo hawaamini kwamba kila muumini ameahidiwa karama ya kunena kwa lugha. Wana wasiwasi kwamba watu wataingia katika mkanganyo wa kiroho ikiwa watajaribu kupata kitu ambacho si mapenzi ya Mungu. Ni dhahiri kwamba itakuwa vigumu watu hao kufanya kazi pamoja katika kanisa la kieneo. Hata kama viongozi wanamchukulia mtu huyo kuwa muumini, hawapaswi kumruhusu kufundisha kanuni zinazoweza kuleta mkanganyo katika kutaniko hilo.
Kanisa la kieneo linahitaji kukubaliana kuhusu kanuni zinazoathiri jinsi wanavyoshiriki maisha pamoja na kufanya huduma. Ni vizuri kanisa kuwa na taarifa iliyoandikwa ya kanuni wanazoshiriki. Kauli hiyo haitumiwi kubaini iwapo mtu fulani ni muumini. Badala yake, inaonyesha ni kanuni gani zinaunganisha kikundi hicho cha waumini kwa ajili ya ibada na huduma ya mara kwa mara yenye umoja.
Sakramenti za Kanisa
Yesu alitoa sakramenti mbili kwa kanisa. Wanaweza pia kuitwa desturi au sherehe.
Ubatizo ni ishara ya kifo na ufufuo wa Kristo (Warumi 6:3-4). Ubatizo ni ushuhuda kwamba muumini anajitambulisha na Kristo na amekuwa mfu kwa dhambi na akapata maisha mapya katika Kristo. Ubatizo haumwokoi mtu. Ubatizo ni ushuhuda wa hadharani kwamba uongofu umetokea (Yohana 3:7-8).
Meza ya Bwana ilianzishwa na Yesu kwenye mlo wake wa mwisho pamoja na wanafunzi kabla ya kusulubiwa kwake (1 Wakorintho 11:23-25). Mkate na divai vinawakilisha mwili na damu ya Yesu iliyotolewa kama dhabihu kwa ajili ya wokovu wetu. [1] Kama vile tunavyokula chakula kwa ajili ya uhai wa kimwili, tunategemea dhabihu yake kwa ajili ya uhai wetu wa kiroho (Yohana 6:53-58).
Sakramenti zinaweza kuitwa “njia za kupata neema.” Hazitoi neema ikiwa zinafanywa bila imani na utiifu. Ni desturi ambazo Mungu ametupatia, na zikifanywa kwa imani, ni njia za kupokea neema kutoka kwa Mungu.
► Je, baadhi ya makusudi ya kanisa ni yapi?
[1]Picha: “Meza ya Bwana” iliyopigwa na Allison Estabrook mnamo Oktoba 14, 2022, ilitolewa kutoka kwenye https://www.flickr.com/photos/sgc-library/52476662295/, iliyoidhinishwa chini ya CC BY 4.0.
Baadhi ya Makusudi ya Kanisa la Kieneo Yanayopatikana katika Agano Jipya
5. Kutuma na kuwasaidia mamisionari (Matendo 13:2-4; Warumi 15:24)
6. Kuwasaidia washirika wenye mahitaji (Warumi 12:13; 1 Timotheo 5:3)
7. Kuwatia nidhamu washirika wanaoanguka katika dhambi (1 Wakorintho 5:9-13)
8. Kutekeleza ubatizo na Meza ya Bwana (Mathayo 28:19; 1 Wakorintho 11:23-26)
9. Kuwafunza waumini hadi wafikie ukomavu (Waefeso 4:12-13)
10. Kuhudumia mahitaji ya jamii (Wagalatia 6:10; Waefeso 4:28; Waebrania 13:16)
Mengi ya mambo haya hayawezi kutekelezwa na mtu mmoja anayefanya kazi peke yake. Makusudi haya yanategemea ushirikiano katika kikundi cha waumini na mfumo wa uongozi.
Mungu anahamasisha kila muumini kujitolea katika kanisa la kieneo na kusaidia kanisa hilo kutimiza kusudi lake ulimwenguni. Mshirika asipotumika kanisani, hatimizi kusudi lake kama sehemu ya mwili wa Kristo.
“Siamini kwamba Mungu anataka maisha yetu katika kanisa yazingatie majengo na huduma. Badala yake, Mungu anataka makanisa yetu—haijalishi makutaniko yetu yanachukua muundo gani—yazingatie uanafunzi hai, utume, na kutafuta umoja.”
Francis Chan
Makosa ya Kuepuka: Ubinafsi wa Kiroho
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshiriki wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Baadhi ya watu hawajitolei kamwe kuwa sehemu ya kanisa la kieneo. Wanataka kujihisi kuwa wako huru kuhudhuria kanisa lolote Jumapili yoyote. Hawawezi kusaidia katika huduma yoyote ya kanisa kwa sababu kanisa haliwezi kuwategemea. Hawana mahusiano yanayoruhusu ushirika wa kiroho na uwajibikaji. Ikiwa Wakristo wote wangefanya hivyo, kusingekuwa na makanisa.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Kristo amejenga kanisa moja takatifu, la dunia nzima, linalodhihirishwa kama mwili wa Kristo katika makutaniko ya kieneo. Kanisa linashikilia kanuni za mitume na kutetea ukweli wote. Kanisa ni familia ya Mungu, yenye ushirika unaohudumia mahitaji yote. Kanisa linamwabudu Mungu, linaeneza injili ulimwenguni, na kuwafunza waumini.
Mazoezi ya Somo la 12
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
1 Wakorintho 5:1-13
1 Wakorintho 6:1-8
1 Wakorintho 12:14-31
Waefeso 4:11-16
Yakobo 2:1-9
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 12. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 12
(1) Je, enzi ya kanisa ilianza wakati gani?
(2) Je, kwa nini kanisa linaweza kuitwa la kitume?
(3) Je, vipengele vinne vya asili ya kanisa ni vipi?
(4) Je, kanisa la dunia nzima ni akina nani?
(5) Je, kanisa la kieneo ni nini?
(6) Je, neno kanisa katoliki lilimaanisha nini hapo awali?
(7) Je, kanisa la dunia nzima limeunganishwa na mambo gani mawili?
(8) Je, kwa nini ni vizuri kwa kanisa kuwa na taarifa iliyoandikwa ya kanuni wanazoshiriki?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.