► Someni Danieli 7:9-14 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu siku za baadaye?
Mada katika unabii wa Biblia ni pamoja na: alama ya mnyama, baragumu, dhiki kuu, mpinga Kristo, miaka saba, miaka 1,000, kiti cha enzi kikubwa cheupe, mji unaoshuka, ziwa la moto.
► Je, wewe hufikiria juu ya masuala gani katika unabii wa Biblia?
Viwango vya Umuhimu
Majadiliano kuhusu unabii mara nyingi huzingatia maswali yasio na umuhimu mkubwa badala ya kweli kuu. Si mada zote katika unabii zina umuhimu sawa. Hatutajaribu kuzingatia kila kitu kuhusu unabii katika kozi hii.
Wakati mwingine watu hujiuliza alama ya mnyama itafananaje, mpinga Kristo atatoka nchi gani, na wale mashahidi wawili watakuwa akina nani. Haya ni maswali ambayo Biblia haijibu kwa uwazi, na kubishana juu ya maswali hayo hakuna faida.
Kuna mada zingine ambazo Biblia inafafanua zaidi. Baadhi ya mifano ni kama Yesu atarudi mwanzoni, katikati, au mwishoni mwa dhiki kuu; na kama milenia ni miaka 1,000 au la. Hata hivyo, kanuni hizi hazina umuhimu wa msingi kwa injili. Hupaswi kuvunja ushirika na mtu kwa sababu hukubaliani na maoni yake kuhusu mojawapo ya maswali haya.
Kuna kweli muhimu katika unabii wa Biblia. Hizi ni kweli ambazo ziko wazi sana kiasi kwamba kila mtu anayeamini Biblia anazikubali. Kanuni hizi zinaathiri maisha ya Kikristo na mfumo mzima wa kanuni za Kikristo. Hebu tuangalie kweli nne muhimu zilizofunuliwa katika unabii wa Biblia kuhusu matukio ya mwisho.
Yesu atarudi katika dunia hii akionekana. Ingawa kiroho yuko pamoja na waumini duniani sasa, atarudi katika umbo lake lililotukuzwa la ufufuo akionekana na dunia nzima. (Soma Ufunuo 1:7.)
► Je, ni mambo gani yatakayotokea Yesu atakaporudi?
Kurudi kwa Kristo kutakuwa kilele cha historia ya dunia. Falme za ulimwengu zitakuwa falme za Kristo. Wale ambao wamekuwa waaminifu kwake watapewa thawabu na kuheshimiwa. Wale ambao wamekuwa katika uasi dhidi yake watawekwa chini, naye atakuwa na nguvu ambazo zitashinda upinzani wote. (Soma Mathayo 26:64.) Kila goti litapigwa, na kila ulimi utakiri kwamba Yesu ni Bwana (Wafilipi 2:10-11).
Wakristo waliokufa watafufuliwa ili watawale pamoja na Kristo (2 Timotheo 2:12). Wao na waumini walio hai watanyakuliwa juu ili kumlaki Bwana atakapotokea (1 Wathesalonike 4:16-17).
Kurudi kwa Yesu ni tumaini lenye baraka la Wakristo wote. (Soma Tito 2:13.) Fikiria yote ambayo kurudi kwake kunamaanisha kwetu: mwisho wa mateso, dhiki, na huzuni; kuungana tena na watakatifu na
wapendwa Wakristo; uthibitisho kwamba imani yetu haikuwa kazi bure; kumwona Yesu mwenyewe; na kuingia mbinguni na utimilifu wa uzima wa milele pamoja na Mungu. Mambo haya yote hayategemei wakati wa kurudi kwake, bali yanategemea tu ukweli kwamba atarudi kama alivyoahidi.
Yesu alisema kwamba atarudi katika nguvu na utukufu (Mathayo 24:30). Aliahidi kwamba atakuja kuwachukua watu wake ili waishi naye (Yohana 14:3). Malaika walisema kwamba atarudi kwa njia ile ile aliyopaa kwenda mbinguni (Matendo 1:11). Mitume walihubiri toba huku wakingoja Kristo arudi ili aanzishe mpango mkuu wa Mungu kwa ajili ya ulimwengu huu. (Soma Matendo 3:19-21.) Kurudi kwa Yesu duniani tena katika nguvu na utukufu ni jambo linalofunzwa tena na tena katika Agano Jipya.[2]
Ingawa kuna ishara zitakazotangulia kuja kwa Yesu mara ya pili, hatuwezi kujua ni lini hasa atarudi. Ni vizuri kwa waumini siku zote kutazamia kuja kwa Yesu na kuishi ipasavyo. (Soma Marko 13:33-37.)
► Je, Yesu atarudi tena kwa nini?
Tunaishi katika ulimwengu ambapo watu wengi wanamwasi Mungu. Uumbaji wote unateseka kutokana na laana ya dhambi. Ulimwengu hautafanywa kuwa mkamilifu kamwe kupitia hatua za kisiasa, mageuzi ya kijamii, elimu iliyoboreshwa, au mafanikio ya kiuchumi. Yesu ataingia ghafla katika uumbaji wake kama mfalme anayerudi ili kuuweka sawa.
Watu wote ni wenye dhambi, lakini wakijiunga na ufalme wa Mungu kwa hiari sasa, wanaweza kuepuka hukumu inayokuja. Ufalme wa Mungu tayari unafanya kazi kati ya wale wanaotubu na kuamini (Marko 1: 14-15, Marko 9: 1). Ufalme huo utakuja kikamilifu na kwa uwazi wakati wa kurudi kwa Yesu.
► Je, tunapaswa kuishi vipi kwa sababu tunajua Yesu anarudi?
Ni lazima tukumbuke vipaumbele vya Wakristo wa awali. Tunahamaishwa kudumisha imani yetu (1 Wakorintho 16:13) na kuvumilia hadi mwisho (Mathayo 24:13). Tunaonywa tusiruhusu anasa na mambo ya dunia yatufanye tusahau kuhusu kuja kwa Kristo (Luka 21:34-36). Tunaishi kulingana na maadili ya milele kwa kuwa mambo ya ulimwengu huu yatapita (2 Petro 3:11-13). Tunaambiwa tukeshe, si kwa kutazama anga kwa ajili ya kuonekana kwake, bali kwa kukaa macho kiroho ili ujio wake usitupate tukiwa hatujajitayarisha (Marko 13:33-37). Tunaomba kwa ajili ya usafi na kuishi maisha safi kwa sababu tunataka kuwa kama yeye (1 Yohana 3:3).
Wale wanaoishi leo kana kwamba Yesu hatarudi hawatakuwa tayari kwa kurudi kwake. Ujio wa Yesu utakuwa kama umeme (Mathayo 24:27; 1 Wakorintho 15:52), utakuwa wa
ghafla sana kiasi kwamba hakuna mtu atakayekuwa na wakati wa kubadilisha chochote baada ya kutokea kwake. 1 Wathesalonike 5:1-6 inaonyesha kwamba wale walio gizani, wale wanaoishi kwa ajili ya ulimwengu huu, watashtushwa na kurudi kwa Bwana. Kwao, kurudi kwake kutakuwa kama kuingiliwa na mwizi. Kwa waumini, kurudi kwake hakutawashtua, bali kutawaleta furaha kuu, kama vile bwana harusi anavyokuja kumchukua bibi harusi wake (Yohana 14:2-3).
“Hakuna mtu amepiga hatua mbele katika shule ya Kristo ambaye hasubiri kwa furaha siku ya kifo na ufufuo wa mwisho. Tusubiri ujio wa Bwana kwa hamu kwa sababu hilo ndilo jambo la kufurahisha zaidi kuliko yote. Atakuja kwetu kama Mkombozi na atatuongoza katika urithi huo uliobarikiwa wa uzima na utukufu wake.”
John Calvin
Imetolewa kutoka katika kitabu kinachoitwa Institutes
[2]1 Wathesalonike 4:15-16; 2 Wathesalonike 1:7, 10; Tito 2:13; Waebrania 9:28; Yakobo 5:7-8; 1 Petro 1:7, 13; 2 Petro 1:16, 2 Petro 3:4, 12; 1 Yohana 2:28
Ufufuo wa Kimwili wa Watu Wote
Tunajua kwamba mwili una thamani ya milele kwa sababu Biblia inafundisha ufufuo wa watu wote. Kanuni ya ufufuo ni muhimu. Tunajua hilo kwa sababu Mtume Paulo alitumia 1 Wakorintho 15 yote kutetea kanuni hiyo. Alieleza kwamba kukana ufufuo ni kukana injili. Ikiwa hakuna ufufuo, basi Yesu asingeweza kufufuka (1 Wakorintho 15:13). Ikiwa Yesu hakufufuka kutoka kwa wafu, injili haiwezi kuwa ya kweli, na hakuna mtu ambaye ameokoka (1 Wakorintho 15:17).
[1]Kila mtu atafufuliwa, lakini si watu wote kwa wakati mmoja. Wakati wa kurudi kwa Yesu, atawachukua Wakristo wote, akiwafufua wale waliokufa (1 Wathesalonike 4:16-17; Ufunuo 20:6). Wale waliokufa katika dhambi zao hawatafufuliwa katika ufufuo wa kwanza. Watafufuliwa baadaye ili wahukumiwe hukumu (Ufunuo 20:13).
Wakristo watafufuliwa katika miili iliyotukuzwa kama Yesu (1 Yohana 3:2). Wenye dhambi ambao hawajaongoka watafufuliwa kwa namna nyingine kwa ajili ya adhabu ya milele (Yohana 5:28-29).
► Je, ikiwa huamini kwamba mwili utafufuliwa, hilo lingeleta tofauti gani kwako?
Imani ya kwamba siku moja tutafufuliwa huathiri mtindo wetu wa maisha. Tunaweza kuona athari za kiutendaji za kanuni hiyo tunapoangalia mifano ya watu wanaolikana. Watu fulani katika kutaniko la Korintho walikana kwamba mwili wa mwanadamu utafufuliwa. Wale walioamini kosa hilo waligawanyika katika misimamo miwili.
Kuna wale waliosema, “Kwa kuwa mwili hautafufuliwa,roho pekee ndio yenye umuhimu. Hiyo ina maana kwamba dhambi tunazofanya kupitia mwili si mbaya. Tunaweza hata kuzini kwa sababu mwili utatupiliwa mbali.”
Baadhi ya Wakorintho walionekana kuwa na kauli mbiu inayosema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” ikimaanisha kwamba mwili hauna kazi yoyote isipokuwa kukidhi tamaa. Paulo aliwaambia kwamba watu watahukumiwa kwa ajili ya matumizi mabaya ya mwili (1 Wakorintho 6:13). Alisema kwamba mwili ni kwa ajili ya Bwana, na kwamba Mungu ataifufua miili yetu kama alivyoufufua mwili wa Yesu (1 Wakorintho 6:14).
Wengine walisema, “Kwa kuwa mwili hautafufuliwa, ni lazima uwe hauna thamani na mwovu. Tunapaswa kuzuia tamaa zote za mwili, tusile chochote chenye ladha nzuri wala tusifurahie ndoa.”
Makosa haya yote mawili yalitokana na kukana ufufuo. Kukataa ufufuo kunashusha thamani ya mwili. Lakini kanuni ya Kikristo ya ufufuo inaupatia mwili thamani.
► Soma 1 Wakorintho 6:14, 15, 19-20.
Vifungu hivi vinaonyesha kwamba miili ya Wakristo ni yenye thamani kwa sababu Wakristo
Wamekombolewa
Ni mahekalu ya Roho Mtakatifu
Ni viungo vya Kristo
Watafufuliwa na kutukuzwa
Kanuni ya ufufuo ni muhimu kwa sababu inamaanisha kwamba
kwa maana Kristo, akiwa amefufuka kutoka kwa wafu,
amekuwa Kiongozi na Mfufuaji
wa wale waliokufa.
Utukufu na nguvu ni zake milele na milele. Amina.”
Chrysostom,
“Hotuba ya Pasaka”
Hukumu
Siku ya Hukumu hakika ni mwisho kwa wale ambao majina yao hayamo katika kitabu cha uzima. Si mwisho wa uhai wao, lakini ni mwisho wa fursa yao ya kufanya maamuzi. Katika umilele unaofuata, watu watapata matokeo yasiyo na kikomo ya maamuzi yao, ambayo hayawezi kutenguliwa.
Hukumu inayapa maamuzi yetu umuhimu zaidi ya matokeo yao ya hapo mwanzoni. Watu wengine hufikiri kwamba mradi tu wanaweza kudhibiti matokeo ya matendo yao, hakuna kitu kingine cha kuwatia wasiwasi. Wanataka kuamini kwamba dhambi yao si mbaya ikiwa haina madhara yoyote. Kwa kweli, dhambi zote zina madhara. Lakini hata kama haikuleta madhara katika maisha haya, dhambi ni jambo zito kwa sababu ya hukumu. Neno la Mungu linasema kwamba watu watahukumiwa kwa ajili ya matendo yao. (Soma 2 Wakorintho 5:10; Waroma 2:6-11.)
Katika hukumu, watu wengine watapelekwa kwenye adhabu ya milele na wengine kwenye thawabu ya milele. Maandiko yanaeleza tukio moja la hukumu kwa wenye dhambi ambao hawajaongoka watakaofufuliwa ili kukabiliwa na hukumu kwa ajili ya matendo yao ya dhambi. (Tazama Ufunuo 20:11-15.) Kuna hukumu nyingine kwa Wakristo, ambapo watapewa thawabu kwa ajili ya matendo yao yenye matokeo mazuri na yenye kudumu. (Soma 1 Wakorintho 3:14-15.)
Hukumu inamaanisha kwamba siku moja dhambi haitakuwepo tena. Ni vigumu kufikiria ulimwengu usio na dhambi, lakini siku moja uasi wote dhidi ya Mungu utakomeshwa.
Mungu hataki tuishi kwa hofu wakati wote, au hofu hiyo iwe kitu kinachotutia motisha kuishi kwa haki. Hata hivyo, kufahamu kwamba kuna hukumu inayokuja kunatupatia hisia ya uwajibikaji inayoongoza maisha yetu.
Lazima tujue kuhusu hukumu ili tuelewe
1. Umuhimu wa dhambi
2. Uwajibikaji wetu kwa Mungu
3. Umuhimu wa maamuzi yetu
4. Mwisho wa dhambi zote
Ufalme wa milele wa Mungu
Kulingana na falsafa na dini zingine, wakati unaendelea milele katika mizunguko, bila mwanzo wala mwisho, na hakuna matukio yanayobadilisha mambo milele. Lakini kulingana na Biblia, wakati una mwanzo na mfululizo wa matukio yanayoendelea hadi kufikia tamatisho. Biblia inaeleza kuhusu uumbaji, kisha anguko la kusikitisha la mwanadamu, kisha mpango wa wokovu ambao Mungu anautekeleza katika karne za historia ya mwanadamu.
Katika Mwanzo 3 tunapata mwanzo wa dhambi. Katika Ufunuo dhambi hairuhusiwi katika mji wa milele wa Mungu (Ufunuo 21:27). Katika Mwanzo tunaona kupotea kwa mti wa uzima na hukumu ya kifo (Mwanzo 3:22-24). Katika Ufunuo tunaona urejesho wa mti wa uzima, majina katika kitabu cha uzima, na mwaliko kwenye mto wa maji ya uzima (Ufunuo 22:1-2, 19).
Ujio wa ufalme mkamilifu na wa milele wa Mungu kutatimiza mpango wa Mungu. Mungu siku zote amekuwa Mfalme wa ulimwengu wake, lakini tangu anguko la mwanadamu, wanadamu wengi wamekuwa katika uasi dhidi ya ufalme wa Mungu. Uasi huo utaisha ghafla, na Mungu atatawala milele bila mpinzani. Ulimwengu utakuwa mkamilifu kama vile Mungu anavyotaka, kama vile ilivyo mbinguni.
Makosa ya KUEPUKA: Kuzingatia Mambo ya Kidunia
Kuna mwelekeo wa mwanadamu wa kuishi kana kwamba maisha ya dunia yataendelea milele. Tunajaribu kuboresha hali zetu, kutatua matatizo yetu, na kuunda mazingira yanayoturidhisha. Tunahitaji kuwa kama Abrahamu ambaye alikuwa akitarajia makao ya milele alipokuwa akiishi katika hema na kuhamahama mara kwa mara (Waebrania 11:8-10, 14-16). Tunapaswa kukumbuka kwamba vitu tunavyojenga, vitu tulivyo navyo, na hali tunazounda vyote ni vya muda tu. Tunapaswa kufanyia kazi vitu ambavyo vina thamani ya milele.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Yesu atarudi kama alivyoahidi, akiwafufua waumini wa zamani, na kuwachukua waumini wote ili watawale katika ufalme wake. Kila mtu atafufuliwa kutoka kwa wafu ili ahukumiwe kwa ajili ya matendo yake. Atapewa thawabu ya milele au kuhukumiwa adhabu ya milele. Ufalme wa Mungu utakuja kikamilifu, na Mungu atatawala milele.
Mazoezi ya Somo la 14
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Danieli 2:31-45
Mathayo 25:31-46
1 Wakorintho 15:51-58
2 Petro 3:1-14
Ufunuo 20:11-15
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 14. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 14
(1) Je, ni zipi kweli nne muhimu zilizotolewa katika unabii wa Biblia kuhusu matukio ya mwisho?
(2) Je, nini kitatokea kwa Wakristo Yesu atakaporudi?
(3) Je, tunapaswa kusubirije ujio wa Yesu?
(4) Je, kwa nini kanuni ya ufufuo ni muhimu?
(5) Tunapaswa kujua kuhusu hukumu ili tuelewe mambo gani manne?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.