Mapema katika miaka ya 60 B.K., Paulo alikuwa akishikiliwa chini ya kizuizi cha nyumbani kule Rumi kwa miaka miwili. Ingawa alikuwa mfungwa, aliishi katika nyumba iliyopangishwa na aliruhusiwa kupokea wageni (Matendo ya Mitume 28:30-31). Wakati wa kifungo chake, Paulo aliandika nyaraka nne (pia ziliitwa nyaraka za kifungoni). Barua tatu kati ya hizi ziliyaelekea makanisa; ya nne ilimuelekea mtu aliyegeuzwa chini ya huduma ya Paulo.
Barua hizi ni baadhi ya barua za furaha sana za Paulo. Zinaonyesha ushindi wake dhidi ya nyakati ngumu katika maisha, na zinatutia moyo kuendelea kutunza roho ya furaha wakati wa mateso yetu binafsi.
Barua hizi pia ziko kwa vitendo sana. Zinaelezea mambo kama mahusiano ya kifamilia na vita vya kiroho (Waefeso), utu na umoja (Wafilipi), imuhimu thabiti wa Kristo (Wakolosai),na msamaha na urejesho (Filemoni).
Waefeso
Usuli wa Waefeso
Mazingira ya Kihistoria
Kanisa la Efeso lilipandwa wakati wa safari ya tatu ya kimishenari ya Paulo. Mwandishi mahiri Apolo alihubiri Efeso; Prisila na Akila walifanya kazi pale; na Paulo alitumia miaka mitatu pale akihubiri na kufundisha. Mji ukawa kitovu cha uinjilisti na kufikia majimbo yaliyozunguka; kutoka Efeso, wote waliokaa Asia walisikia neno la Bwana Yesu (Matendo ya Mitume 18:24-19:10).
Efeso ilikuwa ni nyumba ya hekalu maarufu kwa mungu Diana (pia aliitwa Artemi). Vitendo vya kishirikina vilikuwa vya kawaida, na uchumi wa mji ulikuwa ukishikiliwa kwa upana na mauzo ya vitu vilivyohusiana na hekalu. Huduma ya Paulo ilivuruga maslahi haya yote. vitabu vya sanaa ya uchawi vyenye thamani kama vile dola milioni 6’ vilichomwa na waamini wapya (Matendo ya Mitume 19:19).[1] Matokeo yake, Demetrio na mafundi stadi wengine waliojipatia maisha kupitia kuuza vitu vilivyomuheshimu Diana walianzisha mgomo kupinga huduma ya Paulo. Vita vya kiroho ni dhana muhimu katika Waefeso.
Kigezo kimoja cha ziada lazima kitajwe kuhusu Waefeso. Si kawaida kwa barua za Paulo kutohusisha salamu binafsi kwa watu katika kanisa. Hata barua kwa Rumi, ambapo Paulo hakuwa ametembelea bado, ilihusisha salamu kwa waumini wa kanisa waliojulikana na Paulo. Katika barua kwa Efeso, kanisa ambalo Paulo alihubiri miaka mitatu, mmoja angetaraji mlolongo mkubwa wa majina. Badala yake, Waefeso haijabeba salamu yoyote binafsi. Sababu inayodhaniwa hasa ni kwamba Waefeso, kama Wakolosai, ilikusudiwa kusambazwa katika ya makanisa mengi katika Asia ndogo. Tikiko alichaguliwa kuwasilisha Waefeso na Wakolosai na kuleta salamu kwa makanisa haya (Waefeso 6:21, Wakolosai 4:7).
Yaliyomo katika Waefeso
Muhtasari wa Waefeso unaonesha sehemu kubwa mbili:[2]
1. Mafundisho: Nini Mungu amefanya kwa jili ya kanisa (Waefeso 1-3).
2. Matumizi: Nini Mungu anafanya ndani ya kanisa (Waefeso 4-6)
Katika sehemu ya kwanza, Paulo anaelezea fundisho la uchaguzi na kanisa. Katika sehemu ya pili, Paulo anahimiza wasomaji wake kuishi katika namna inayopasa nafasi zao kama kanisa lililochaguliwa la Bwana.
Fundisho: Kile Mungu alichofanya kwa kanisa (Waefeso 1-3)
Wokovu wa waamini (Waefeso 1:3-2:10)
Baada ya salamu fupi, Paulo anaanza na maombi ambapo anataja baraka tulizopokea katika Kristo. Waefeso 1:3-14 ni kielelezo kizuri cha ibada ambapo Paulo anakumbusha wasomaji wake faida za kiroho tunazopokea kupitia nafasi zetu katika Kristo..
► Soma Waefeso 1:3-14. Ni baraka gani za kiroho tunazipokea katika Kristo?
Wokovu wetu unahusisha nafsi zote tatu katika Utatu Mtakatifu:
1. Baba: Uchaguzi (Waefeso 1:3-6). Baba ametuchagua katika Kristo kabla ya misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu na tusio na mawaa mbele za baba yetu katika upendo. Mpango wa wokovu ulikuwa ni muundo wa Baba.
2. Mwana: Ukombozi (Waefeso 1:7-12). Kwa sababu ya kifo cha upatanisho cha Yesu, tuna ukombozi kupitia damu yake, msamaha wa dhambi, kwa kadri ya utajiri wa neema ya Mungu. Kumkomboa mtu humaanisha kumfidia kutoka katika uteka. Mfano mkubwa katika Agano la Kale ni ukombozi wa Israeli toka katika utumwa kule Misri. Katika agano jipya, wote wanaomwamini Yesu wamekombolewa kutoka katika utumwa wa shetani.
3. Roho: Uhifadhi (Waefeso 1:13-14). Kupitia Roho, tumewekwa chapa ya umiliki wa Mungu. Katika muonekano mzuri, Paulo anasema kuwa Roho ni malipo ya awali juu ya urithi wetu katika ufalme wa milele wa Mungu. Kwa sababu ya Roho, sisi ni milki iliyonunuliwa wa Mungu na tuna ahadi ya mbingu.
Fundisho la ukombozi linaendelea katika Waefeso 2, ambapo Paulo anatukumbusha kuwa sisi tulikuwa “…wafu kwa sababu ya makosa na dhambi” (Waefeso 2:1). Wokovu wetu si kwa kustahili kwetu wenyewe.
… Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema (Waefeso 2:4-5).
Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu (Waefeso 2:8-9).
Mchakato mzima ni zawadi ya Mungu. Hatuwezi kujisifu kwa chochote.
[2]Imechukuliwa kutoka Walter A. Elwell and Robert W. Yarbrough, Encountering the New Testament. (Ada: Baker Academic, 2005).
Kuangalia kwa Makini Uchaguzi
Paulo anaandika kwamba sisi tumechaguliwa tangu asili kwa ajili ya kuasiliwa/kufanywa wana kupitia Yesu Kristo (Waefeso 1:5). Tulichaguliwa katika Yeye kabla ya misingi ya ulimwengu (Waefeso 1:4).
Baadhi ya watu hutumia neno uchaguzi kumaanisha kuwa, kabla ya misingi ya ulimwengu, Mungu alichagua kila mtu ambaye angeokolewa. Wanasema kuwa wale waliochaguliwa wamekusudiwa wokovu. Kimsingi, hii humaanisha kuwa watu wengine wote wamekusudiwa kukataliwa na hawawezi kuokolewa. Hitimisho hili huonekana kupingana na ujumbe wa Biblia: Mungu anapenda watu wote.
Wengine hutumia uchaguzi kumaanisha kuwa hakuna zaidi ya maarifa ya awali ya Mungu kwa wale watakao chagua kuokoka. Huhoji kuwa kukusudiwa ni maarifa ya awali ya Mungu ya uchaguzi binafsi. Katika mtazamo huu, wokovu umejikita katika uchaguzi binafsi. Hata hivyo, uelewa huu huonekana kukinzana na msisitizo wa Biblia juu ya Ukuu wa Mungu.
Kanuni hizi mbili (ukuu wa Mungu na upendo wa Mungu) zimeamuliwa katika vifungu viwili vya msingi juu ya Kuchaguliwa tangu asili: Warumi 9-11 and Waefeso 1. Warumi 9-11 inaonyesha haki ya Mungu katika kuamua njia ya wokovu. Mungu ni mkuu, hakuna nayeweza kuokolewa isipokuwa kupitia imani katika Kristo Yesu, njia ambayo Mungu ameitangaza milele kama njia pekee ya wokovu.
Katika Waefeso 1, Paulo anaonyesha kuwa wokovu ni kwa watu binafsi kwa sababu ya nafasi zetu katika Kristo. Kabla ya misingi ya dunia, Kristo alichaguliwa kama yule ambaye kupitia yeye wokovu huja. Wote wanaoamini wamechaguliwa katika yeye. Kwa sababu ya upendo mkuu wa Mungu, njia ya wokovu iko wazi kwa wote waaminio.
Uwioano huu pia unaonekana katika Agano la Kale. Israeli ilikuwa taifa teule, watu waliochaguliwa na Mungu. Hata hivyo, si kila aliyezaliwa na Israeli alikuwa mali ya Israeli. (Warumi 9:6). Uchaguzi wa Mungu wa Israeli kama taifa teule haukumaanisha kuwa kila muisraeli aliokolewa. Kupitia kutokutii, baadhi (kama Akani, Yoshua 7) walipoteza ahadi Wengine ambao hawakuzaliwa Israeli (kama Rahabu, Yoshua 2 na Yoshua 6) waliamini ahadi za Mungu na kurithi ahadi zilizokuwa za Israeli. Wokovu ulitaka kuwa watu waamini na kushiriki ahadi za Mungu.
Katika namna ile ile, Kristo alichaguliwa kabla ya misingi ya ulimwengu kama mtu pekee ambaye kupitia yeye wokovu unatolewa. Tunapokuwa katika Kristo kupitia imani, tunapokea baraka za wokovu ambazo ni zake. Tumechaguliwa katika Kristo.
Uchaguzi ni uamuzi wa Mungu mkuu kwa imani katika Kristo kuwa njia pekee ya wokovu. Matendo ya Mitume 4:12 inasema, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Wazo hili hili linaonekana pia katika 1 Petro 1:18-20. Tumekombolewa , si kwa vitu viharibikavyo, bali kwa damu ya thamani ya Kristo. Petro anasema Kristo alijulikana hapo awali kabla ya misingi ya ulimwengu. Kwa hiyo, uchaguzi ni kwa Kristo mwenyewe na kupitia Kristo pekee.
Waefeso (Mwendelezo)
Yaliyomo katika kitabu cha Waefeso (Mwendelezo)
Fundisho: Kile Mungu alichofanya kwa kanisa (Waefeso 1-3) (Mwendelezo)
Umoja wa kanisa (Waefeso 2:11-3:21)
► Ni nini siri ya Injili ambayo Paulo anairejelea katika Waefeso 3:3-9?
Katika Waefeso 1, Paulo anafurahi katika wokovu wa waamini. Katika Waefeso 2-3, anafurahi katika uumbaji wa Mungu, kanisa. Dhamira muhimu ya Waefeso ni umoja wa kanisa: mwili mmoja ulioundwa na Wayahudi na mataifa pia. Mataifa, ambao hapo awali walikuwa wageni kwenye maagano ya ahadi, sasa wameletwa karibu kwa damu ya Kristo. (Waefeso 2:12-13). Kutokea mwanzo, mpango wa Mungu ulikuwa kuwahusisha mataifa katika familia yake. Kwa ndugu Wayahudi wa Paulo, hiki kilikuwa kipengele cha kushangaza cha Injili: Kanisa limeundwa na Wahayudi na mataifa pia katika Kristo. Hio ndio siri ya injili ambayo Paulo anarejelea.
Katika Biblia, siri si kitu ambacho hakiwezi kujulikana: bali, siri ni kitu ambacho hapo awali hakikujulikana lakini sasa kimefunuliwa. Katika Waefeso 3, Paulo anaielezea siri: “…Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili” (Waefeso 3:6). Kama ishara ya nguvu za neema ya Mungu, Paulo amechaguliwa “ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika” (Waefeso 3:8)—Paulo, ambaye hujichukulia mwenyewe “mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote” na ambaye hapo zamani alimuudhi Kristo na kanisa lake. Paulo anahitimisha sehemu ya fundisho kwa ombi kwamba waamini wa Efeso, ambao tayari ni watakatifu na waaminifu katika Kristo Yesu, wajazwe kwa utimilifu wote wa Mungu.
Matumizi: Kile Mungu anachofanya katika kanisa. (Waefeso 4-6)
Katika nusu ya pili ya barua yake, Paulo anatoa changamoto kwa waamini : “…mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa” (Waefeso 4:1). Maisha yanayostahili mwito wetu:
Huleta umoja katika kanisa (Waefeso 4:1-16).
Hupelekea mwenendo wa kimaadili (Waefeso 4:17-5:21).
Huathiri uhusiano wa kifamilia na kazi (Waefeso 5:21-6:9).
Unauishi tu katika nguvu za uweza wa Bwana (Waefeso 6:10-18).
Fundisho la kikristo haliwezi kutenganishwa na maisha ya mkristo. Fundisho la kanisa lazima lionekane katika maisha ya kanisa ambapo kila sehemu inafanya kazi ipasavyo, kanisa ambalo linajijenga lenyewe katika upendo (Waefeso 4:16). fundisho la wokovu kwa neema linaonekana katika tabia ya “utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli” (Waefeso 4:24).
Paulo anamalizia barua yake kwa kulitia moyo kanisa kuwa linaweza kutimiliza utume wake na kuzishinda nguvu za giza. Anahitimisha kwa kuomba maombi kwa ajili ya muendelezo wake wa kuitangaza injili na kwa baraka.
Wafilipi
Usuli wa Wafilipi
Mazingira ya kihistoria
Kanisa la Filipi lilipandwa wakati wa safari ya pili ya umisheni wa Paulo. (Matendo ya Mitume 16:9-40). Lilikuwa ni kanisa la kwanza kuanzishwa barani Ulaya. Paulo na Sila walisafiri kwenda Filipi baada ya Paulo kuwa na maono ya mtu toka Makedonia akiomba msaada. Ingawa Filipi ilikuwa ni mji mkuu wa sehemu ya Makedonia, haikuwa na idadi kubwa ya Wayahudi. Kikundi cha wanawake kilikutana kando ya mto kwa ajili ya maombi kwa sababu hakukuwa na sinagogi (Matendo ya Mitume 16:13).[1]
Mmoja kati ya waamini wa kwanza katika Filipi alikuwa Lidia, mwanamke mwenye utajiri. Baada ya ubatizo wake, nyumba ya Lidia ilikuwa mahala pa kukutanikia waamini. Katika miji yenye Wayahudi wengi, upinzani wa Injili mara nyingi ulitokea kwa viongozi wa kidini wa Kiyahudi; lakini katika Filipi, upinzani uliinuka baada ya Paulo na Sila waliharibu kipato cha watu waliokuwa wakimdhibiti binti mfungwa aliyepagawa na roho chafu. Paulo na Sila walikamatwa, kupigwa, na kuwekwa gerezani. Usiku ule, tetemeko lilifungua malango ya gereza, na wafungwa walifunguliwa minyororo yao. Hakuna mfungwa alitoroka, na Paulo na Sila wakapata fursa ya kuhubiri injili kwa walinzi wa gereza.
Katika Matendo ya Mitume, Luka inahusiha kwa kina kuwa Filipi ilikuwa ni koloni la Rumi (Matendo ya Mitume 16:12). Usemi huu rahisi ulibeba maana kubwa kwa wasomaji wa awali wa Matendo ya Mitume. Filipi lilifanywa koloni la Rumi mwaka wa 42 B.K na jemadari mkuu wa Rumi Antony. Askari wengi walistaafia katika mji huu, na raia wake walipokea msamaha wa kodi nyingi za kirumi. Hadhi ya Filipi kama koloni ilikuwa ni sababu ya kiburi kwa raia wake. Wakati Paulo anawaandikia Waamini katika Filipi, kwa makusudi alitumia maneno mawili ya kigiriki akimaanisha uraia:
Kwa maana sisi, wenyeji wetu (politeuma) kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo (Wafilipi 3:20).
Lakini mwenendo wenu (politeuomai) na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo… (Wafilipi 1:27).
Kwa kutumia lugha hi, Paulo anawaita Wafilipi kuishi kama raia wa mbinguni.
Kusudi
Wafilipi ni moja kati ya barua chanya, inayoonesha matatizo machache ambayo anayaelezea katika barua zake kwa Korintho na Galatia. Kuna malengo mawili kwa barua hizi:
1. Kusudi Binafsi: Kuleta habari za ufungwa wa Paulo na kuonyesha shukurani kwa msaada wa kifedha wa kanisa kwa huduma yake (Wafilipi 4:14-18). Paulo anafurahia uaminifu wao na anawatia moyo kuishi maisha ya furaha.
2. Lengo la Kimaelekezo: Kuelezea hatari mbili zinazowakabili kanisa la Filipi:
Hatari ya nje : Mafundisho ya uongo ya Judaizers.[2]
Hatari ya ndani: mgawanyiko kati ya waamini katika kanisa.
Yaliyomo katika Wafilipi
Furaha licha ya mazingira (Wafilipi 1)
Ingawa Paulo yuko kifungoni, ana ujasiri kuwa Mungu anafanyia kazi makusudi yake. (Wafilipi 1:12). Kwa sababu ya kukamatwa kwa Paulo, anapata fursa ya kuhubiri injili kwa walinzi wa kasri (jumba la mfalme). (Wafilipi 1:13). Paulo hajui kama kufungwa kwake kutamalizika kwa kufunguliwa au mauti (Wafilipi 1:19-20). Lakini bila kujali matokeo, anafurahi kwa sababu kuishi ni Kristo na kufa ni faida (Wafilipi 1:21).
Mazingira mengine ambayo yangetishia furaha ya Paulo ni wivu wa waamini wenza (Wafilipi 1:15). kikundi katika Rumi kinamhubiri Kristo kwa ushindani, kuongezea mateso ya Paulo (Wafilipi 1:17). Hata hivyo, mbali na nia zao, Paulo anafurahi kwa sababu injili inahubiriwa. (Wafilipi 1:18). Paulo ana ujasiri kuwa mema yatatokea kwenye injili inayohubiriwa, bila kujali nia zisio sahihi za watu hawa. Hali binafsi ya Paulo si ya muhimu sana kuliko ufalme wa Mungu.
Unyenyekevu kama Ufunguo wa Umoja (Wafilipi 2)
Baadae katika barua, Paulo ataelezea mgawanyiko kati ya wanawake wawili katika kanisa la Filipi (Wafilipi 4:2-3). Ni wafuasi waaminifu wa Kristo ambao wamefanya kazi ngumu na Paulo kwa ajili ya injili. Bahati mbaya, ugomvi binafsi baina ya dada hawa wawili katika Kristo unatishia umoja wa kanisa. Kabla ya kuongelea mgawanyiko huu, Paulo anaelekezea mfano wa Kristo kama kielelezo cha umoja wa Kanisa.
Ugomvi mwingi ni matokeo ya tamaa zetu kulinda haki zetu. Katika Wafilipi 2:5-11, Paulo anaelekezea mfano wa Kristo, ambaye alikatilia mbali vipaumbele vyake kama Mungu ili kuokoa wanadamu. Yesu hakujiambatanisha na upendeleo wa Mungu lakini alikuwa mtii mpaka mauti, hata mauti ya msalaba. Alikumbana na kila fedheha, Alisulubiwa hata kifo cha aibu, ili kuleta wokovu. Matokeo yake, Mungu akamtukuza Yesu katika nafasi yake sahihi ya mamlaka ya ulimwengu.
Kila mfuasi wa Yesu lazima awe na nia hii ya unyenyekevu, kuangalia mahitaji ya waamini wenza. “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine” (Wafilipi 2:4).
Inamaanisha nini kwamba Yesu “Alijinyenyekesha”?
Wafilipi 2:5-11 mara kwa mara huitwa “Hymn of Christ” (“Wimbo wa Kristo”) kwa sabau inafupisha maisha ya Yesu , kifo, ufufuo, na kupaa kwake.
Watu wengi wamehojiana kuhusu maana ya Wafilipi 2:8 ambapo Paulo anaongea kuhusu Yesu kujinyenyekesha. Yesu hakukatilia mbali uungu wake. Alikatilia mbali heshima yake kama mfalme wa ulimwengu. Alijinyenyekesha kwa kuchukua uanadamu; hakukatilia mbali asili yake ya uungu.
Onyo dhidi ya Maadui wa Injili (Wafilipi 3)
Ingawa Wafilipi kwa upana ni chanya, Paulo anaandika tahadhari kuu dhidi ya kundi la waletao matatizo ambao hutishia kanisa. Hawa ni Judaizers wanaoonekana mapema katika barua kwa Galatia. Wanasisitiza kuwa waamini lazima watahiriwe na sheria ya Kiyahudi. Paulo huwarejelea kama “mbwa,” “watendao mabaya,” na “wajikatao” (Wafilipi 3:2).
Katika Wafilipi 3:4-6, Paulo anawajibu Judaizers’ akisisitiza katika kuzingatia matambiko ya sheria kwa kujielekezea maisha yake mwenyewe kama mfano. Kama kuzingatia sheria kulileta wokovu, Paulo angekuwa na ujasiri katika mwili. Alitahiriwa kwa mujibu wa sheria; alikuwa wa kabila lililopendelewa la Benyamini, muebrania wa Waebrania; alikuwa farisayo ambaye alitii sheria kwa umakini; alikuwa na bidii kwa imani ya kiyahudi, hata kiasi cha kuwatesa wafuasi wa Kristo; kuhusu sheria, Paulo hakuwa na hakulaumiwa. Hata hivyo, vitu vyote hivi huhesabika kama takataka kwa sababu ya thamani ya kumjua Kristo inayozidi yote (Wafilipi 3:8). Paulo aliokolewa, Wafilipi waliokolewa, na tumeokolewa, si kwa kuzingatia sheria, bali kwa ufahamu wa Kristo Yesu, Bwana wetu (Wafilipi 3:8-9).
Mahusia Yanayohitimisha (Wafilipi 4)
Katika Wafilipi 4:2, Paulo anamhimiza Euodia na Sintike kuonyesha umoja ambao alifundisha katika Wafilipi 2. Kama wanawake hawa wana nia ya Kristo, watatatua ugomvi wao. Anahimiza kanisa kufurahi katika Bwana katika hali zote na kutunza amani ya Mungu katika mioyo yao na akili zao (Wafilipi 4:4-9). Anahitimisha kwa shukurani kwa mkono wa shirika toka katika kanisa kwa huduma yake (Wafilipi 4:10-19).
[1]Mji wowote ambao ndani yake wanaume 10 wa Kiyahudi walikaa walikuwa na Sinagogi.
[2]Kwa taarifa zaidi kuhusu Judaizers, ona sehemu juu ya Wagalatia katika somo la 6.
Wakolosai
Usuli wa Wakolosai
Muundo wa kihistoria
Wakolosai iliandikwa wakati wa ufungwa wa Paulo katika Rumi. Timotheo anaitwa pia mwandishi. Wakolosai 1:1), pengine akihudumu kama karani wa Paulo.
Hakuna ushahidi kuwa Paulo alitembelea kanisa katika Kolosai. Muunganiko unaodhaniwa kati ya Paulo na kanisa ni Epafra (Wakolosai 1:7, Wakolosai 4:12). Epafra, mzaliwa wa asili wa Kolosai, aweza kuwa aliokoka wakati wa huduma ya Paulo katika Efeso, umbali wa kama kilomita 160.[1] Epafra alirejea kupanda kanisa katika Kolosai, vile vile katika miji ya karibu ya Laodikia na Hierapoli. Paulo aliandika nyaraka kwa yote mawili Laodikia na Kolosai, akiwaelekeza waamini katika kila mji kusoma barua zote (Wakolosai 4:16).
Malengo
Wakati wa kifungo cha Paulo, Epafra aliripoti uzushi ambao ulitishia kanisa katika Kolosai. Paulo aliandika Wakolosai kuelezea fundisho hili hatari. Kwa kuongezea, Paulo aliandika kuwatia moyo waumini Wakolosai kuendelea mbele na ukomavu katika Kristo. Kitabu hujuisha maonyo dhidi ya fundisho la uongo na msisitizo wa kuuendea ukuaji wa kiroho.
Yaliyomo katika Wakolosai
Wakolosai inashiriki dhana nyingi na Waefeso: umoja wa kanisa, uhalisia wa vita vya kiroho, na umuhimu wa kuishi katika namna inayostahili mwito wetu kama wafuasi wa Kristo. Mfanano huu haushangazi kwa sababu Paulo anaandika barua hizi wakati unaofanana na barua zinaelezea mahitaji yale yale.
Wakati maelezo ya uzushi uliofundishwa katika Kolosai waweza kutofautiana na mafundisho ya uongo ambayo yanatishia kanisa la leo, ujumbe wa Paulo unabaki kuwa wa muhimu:
Kristo ndiye mkuu juu ya uumbaji wote
Kristo ndiye kichwa cha kanisa.
Tunatakiwa kuishi katika namna inayostahili mwito wetu kama watoto wa Mungu.
Ukuu wa Kristo (Wakolosai 1)
Mada kuu ya Wakolosai ni ukuu wa Kristo aliyefufuka. Katika sentensi nzuri kutoka Wakolosai 1:15-23, Paulo anaonyesha ukuu wa Kristo juu ya vitu vyote vilivyoumbwa, mamlaka yake juu ya kanisa, na kazi yake ya ukombozi. Kristo ni muumbaji (vitu vyote viliumbwa kupitia yeye) , na vitu vyote humilikiwa na yeye (vitu vyote viliumbwa kwa ajili yake). Kristo ni kichwa cha mwili, cha kanisa. Kupitia Kristo na damu ya msalaba wake. Sisi ambao hapo awali tulikuwa tumetengwa na tuliofungwa akilini, tukifanya matendo maovu sasa tumepatanishwa na Mungu. Kristo ni chanzo cha uumbaji, kichwa cha kanisa na Bwana wa ukombozi.
Fundisho Potofu la Kolosai (Wakolosai 2)
Baada ya hii sentensi chanya juu ya asili ya Kristo, Paulo anasogea kwenye onyo hasi dhidi ya fundisho la uongo ambalo hutishia kanisa katika Kolosai. Asili thabiti ya uzushi/fundisho potofu la Kolosai si wazi. Hata hivyo, mwitikio wa Paulo hufunua baadhi ya tabia za uzushi huu. Uzushi wa Kolosai ulijumuisha mchanganyiko wa mawazo ya uongo kutoka katika ushawishi wa aina tatu:
Uyudaizimu wa Kiothodoksi: Wayahudi wa kiothodoksi waliwataka waamini wa Kolosai kutazama sherehe za kiyahudi, sheria za vyakula na tohara (Wakolosai 2:16, Wakolosai 3:11).
Jewish mysticism: Fumbo la kiyahudi liliwataka waumini wa kolosai kufunga ili kuungana na ibada zilizotukuka za malaika kwa Mungu (Wakolosai 2:18).[2]
Upagani: Wapagani waliwatia moyo waumini wa kolosai kufanya matambiko kwa ajili ya ulinzi dhidi ya roho chafu, Paulo hakatai nguvu za roho chafu lakini anaweka sawa kuwa jibu halipatikani katika matambiko ya kipagani, lakini katika ushindi kwamba Kristo alishashinda nguvu za giza (Wakolosai 2:15).
► Uzushi wa Kolosai unahusiana vipi na sisi leo?
Syncretism hurejelea mchanganyiko wa dini zaidi ya moja. Katika Kolosai, syncretism ilichanganya vipengele vya uyahudi, Jewish Mysticism, upagani na ukristo. Leo, makanisa katika tamaduni za kipagani mara chache hujaribiwa kuchanganya fundisho la kikristo na vitendo vya tamaduni zinazozunguka (kwa mfano: ibada za mizimmu, sherehe za siku takatifu za kipagani, na ushiriki wa matambiko kuondoa mzimu na roho chafu). katika karne ya 1 na 21, jibu kwa mafundisho yote haya ni lile lile: Yesu ni Bwana. Amezishinda nguvu za giza, na tunao ushindi kupitia Kristo pekee. Hakuna matambiko au desturi nyingine zenye nafasi katika desturi za Kikristo.
Ukuaji katika ukomavu wa Kikristo (Wakolosai 3-4)
Kama katika Waefeso, Paulo hutoka katika fundisho kwenda katika vitendo. Tangu Kristo aketi katika mkono wa kuume wa Mungu, sisi tuliofufuliwa katika Kristo lazima tuweke akili zetu katika vitu vya mbinguni. Badala ya kuzingatia mafundisho ya uongo. Lazima tukumbuke kuwa tulikufa katika mambo hayo na sasa tunaishi na Kristo katika Mungu. (Wakolosai 3:1-3).
Maisha yaliyofichwa katika Kristo yanafananaje? Paulo anaelezea maisha yake mapya kwa vitendo, maisha haya hubeba mambo mawili ya msingi:
1. Tunatakiwa kuvua utu wa kale na matendo yake (Wakolosai 3:5-9). Lazima tuue yale yaliyo ya dunia: uasherati, tamaa mbaya, hasira, mazungumzo machafu, kukosa uaminifu na zaidi. Vitendo hivi hustahili ghadhabu ya Bwana.
2. Tunatakiwa kuvaa utu mpya ambao ni sura ya Kristo (Wakolosai 3:12-17). Tabia za utu mpya ni huruma, wema, utu, upole, uvumilivu, msamaha, na zaidi ya yote, upendo. Tunapokuwa na tabia hizi, amani ya Mungu itatawala mioyoni mwetu, na neno la Kristo litadumu ndani yetu. Maidha haya mapya hubadili mahusiano ya familia na kazi (Wakolosai 3:18-4:1) na kufanya injili iwe yenye kuvutia kwa wasioamini (Wakolosai 4:5-6).
[2]Katika mstari huu, “kuabudu malaika” pengine hakukumaanisha kwamba walikuwa wanaabudu malaika (ambapo ingekuwa kinyume na mafundisho yote ya Kiyahudi). Badala yake, kifungu hiki cha maneno pengine kilirejelea dhana za kisiri za Kiyahudi ambazo kupitia matendo ya ascetic (taratibu za kidini za kujikana), kama vile kufunga kwa muda mrefu, wanaoabudu wanaungana na malaika katika kiti cha enzi cha Mungu mbinguni. Waalimu wa uongo katika Kolosai walikuwa wanawaalika waamini kufuata taratibu hizi.
Filemoni
Usuli wa Filemoni
Mazingira ya Kihistoria
Barua fupi ya Paulo inaelekezwa kwa Filemoni, mwamini tajiri kutoka Kolosai. inaonekana kuwa Filemoni aliokoka wakati wa huduma ya Paulo katika Efeso. Nyumba yake ikawa mahala pa kukutania kwa kanisa la Kolosai.
Kama ilivyokuwa kawaida katika karne ya kwanza, Filemoni alikuwa akimiliki watumwa. Onesimo, mtumwa wa Filemoni, alikimbilia Rumi. Rumi ulikuwa ni mji uliosongamana sana katika ngome, mahala salama kwa wakimbizi kujificha. (Wakimbizi siku hizi husafiri kwenda New York City, Mexico City, Lagos, au miji mingine mikuu na kupotolea huko.)
Hata hivyo, Onesimo asingeweza kujifichwa kwa Mungu. Katika mji huu mkubwa,Mungu alimleta Paulo na mtumwa mkimbizi pamoja. Onesimo aligeuzwa na kuanza kumsaidia Paulo.
Wakati fulani, muamini huyu mpya alilazimishwa kuikabili historia yake ya nyuma. Inawezekana kuwa aliiba fedha toka kwa bwana wake kabla ya kukimbia (Filemoni 1:18). Onesimo alikabiliana na uwezekano wa kuadhibiwa; mtumwa mtoro hakuwa na chapa katika paji la uso kama mkimbizi au mfungwa au hata kuuawa. Akilijua hili, Paulo aliandika barua kumuimea msamaha Onesimo kumchukua tena wakati ataporudi kumkabili Filemoni.
Kusudi
Lengo la Paulo katika kuandika barua hii ni kukata shauri la patano. Onesimo amepatanishwa na Mungu; Paulo sasa anamuomba Filemoni apatanishwe na mtumwa wake aliyetoroka.
Paulo anaanza kwa kumshukuru Filemoni kwa ukarimu wake kwa waamini wenzie, Upendo wa Filemoni kwa kaka na dada zake katika imani utakuwa msingi wa rufaa ya Paulo kwa niaba ya Onesimo, ambaye sasa ni mmoja wao.
Paulo anaomba si kwa mamlaka yake ya kitume (kama katika Wagalatia), lakini katika misingi ya upendo. Ni kama yuko nusu ya barua yake kabla hajasema sababu ya kuandika kwake: “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu...yaani, Onesimo…” (Filemoni 1:10). Filemoni ni mwana wa Paulo katika imani; sasa Paulo ana mwana mwingine, mtumwa wa Filemoni.
Jina Onesimo humaanisha “yenye manufaa” ama “ya faida”; lilikuwa ni jina lililozoeleka kwa watumwa. Paulo anaandika, “ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia” (Filemoni 1:11). Onesimo sasa ataishi kulingana na jina lake. Kupitia nguvu ya Kristo, amekuwa wa manufaa.
Paulo anadokeza kuwa Filemoni angeweza kumfungua Onesimo, lakini hashurutishi (Filemoni 1:13). Anamuomba Filemoni ampokee Onesimo katika roho ile ile ambayo Filemoni angempokea Paulo (Filemoni 1:17).
Paulo anahitimisha kwa kumuomba Filemoni aombee kuachiliwa kwa Paulo. Anaandika kuwa anatumai kumtembelea Filemoni baada ya kuachiliwa toka gerezani. Je unadhani hii ni ukumbusho kuwa Paulo hivi punde ataona jinsi Filemoni anavyomchukulia Onesimo?
Watu wengi wamelalamika kwa sababu Paulo hakuhukumu utumwa. Hata hivyo, Paulo anaamuru mabwana watengeneze mazingira ambayo utumwa hautadumu.[2] Haiwezekani kumshikilia katika utumwa mtu ambaye unamuona kama ndugu au dada katika Kristo kweli kweli.
Hitimisho la kihistoria
Andiko halisemi kilichotokea baada ya Onesimo kurudi kwa Filemoni. Hata hivyo, historia inatoa dokezo mbili zinazo pendekeza kuwa Filemoni alimwachia Onesimo:
Andiko la kale katika Laodikia (iliyokuwa karibu na Kolosai) mfungwa ameliekeza kwa Bwana wake aliyemwachia. Jina la Bwana huyu ni Marcus Sestius Philemon (Marcus Sestius Filemoni).
Miaka michache baada ya barua hii. Mtu alieitwa Onesimo alikwa Askofu wa kanisa la Efeso.
Yawezekana kuwa Filemoni alimwachia Onesimo arudi kwa Paulo, ambaye hapo alimfundisha Onesimo kama Mchungaji. Kama ndivyo, huduma ya Paulo katika Efeso yaweza kuwa imeendelea kupitia mafundisho ya Onesimo, mtumwa wa awali wa Filemoni, ambaye hapo mwanzo aliokoka chini ya mafundisho ya Paulo kule Efeso. Makusudi ya Mungu ni zaidi ya yale tuyaonayo.
[1]“Sisi sote ni Onesimi wa Bwana. Tusio na faida na tukawa wa faida. Ni picha ya kudumu ya Kristo akishughulika na wanadamu. Sisi sote ni watumwa tunaokimbilia dhambi." - Martin Luther.
1. Fundisho lazima zitendewe kazi katika maisha ya kila siku. Katika nyaraka hizi, Paulo anawapa changamoto wasomaji wake kuishi katika namna inayoustahili mwito wao kama waaminio. Haitoshi tu kukiri mfundisho sahihi; lazima tuiishi imani yetu katika maisha ya kila siku.
2. Vita vya kiroho ni halisi, lakini Kristo amekwisha shinda ushindi wa mwisho. “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:12).
Tunapigana kwa ujasiri kwa sababu Kristo amekwisha kushinda vita. Umakini wetu wa kwanza lazima uwe kwake, si kwa adui anayepigana vita aliyoishindwa.
3. Lazima tuiishi Injili ya upatanisho katika dunia halisi. Paulo hakuridhishwa na ujumbe ambao haufanyi kazi katika maisha halisi. Alisisitiza kuwa injili ile ile iliyompatanisha Mungu na mwenye dhambi ingeweza pia kumpatanisha Filemoni na mtumwa. Katika ulimwengu uliojaa ugomvi na mahusiano yaliyovunjika. Lazima tonyeshe nguvu ya injili katika kuleta upatanisho.
Hitimisho
Waamini katika Dola ya Rumi walijifunza nini maana ya kuiishi injili katika dunia iliyoanguka. Paulo aliandika kuwa waamini lazima waishi kama watoto wa Mungu bila lawana yoyote katikati ya kizazi kilichoharibirika na kutikiswa. Tufanyapo hivyo, tunang’aa kama nuru katika ulimwengu (Wafilipi 2:15). Paulo alijua kuwa nuru ya kanisa hung’aa kwa mwanga zaidi kadri dunia inavyozidi kuwa giza.
Katika siku za giza za himaya ya Rumi, baadhi ya wafuasi wa Kristo walijulikana kwa jina la“Gamblers for Christ” (“Wacheza kamari wa Kristo”) kwa sababu walihatarisha maisha yao ili kuwaokoa wengine.. Paulo anatumia kifu hii akimzungumzia Prisila na Akila in Warumi 16:3-4, “Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.”
Katika karne ya 1 , waamini wa kirumi walijihatarisha dhidi ya gadhabu ya jamii ili kuokoa watoto wachanga waliokuwa hawatakiwi ambao walikuwa wametupwa katika majalala ya mji. Katika karne ya 3, askofu wa Carthage aliita kusanyiko lake pamoja wakati wa mapigo, akiwataka wawajali walio katika hali ya kufa na kuwazika waliokwisha kufa, wakihatarisha maisha yao kuokoa mji.
Kanisa la awali lilijua kuwa kuvua utu wa kale na kuvaa utu mpya humaanisha zaidi ya kuhudhuria makusanyiko ya ibada. Humaanisha kuishi maisha mapya yanayomilikiwa na Mungu na kusudi lake. Inaweza hata kumaanisha kuwa tayari kuyatoa maisha yetu ili kung’aa kama nuru katika ulimwengu.
Somo la 7 Mazoezi
(1) Andaa ujumbe au somo la Biblia kwa msingi wa kitabu/mada zilizounganishwa katika orodha hapa chini. Unaweza kuwasilisha hii ama katika maandishi (kurasa 5-6) au wasilisha rekodi ukiwa unahubiri au kufundisha.
Chagua mojawapo ya chaguo zifuatazo:
Waefeso – Familia
Waefeso – Kanisa
Wafilipi – Furaha katika maisha ya Kikristo
Wakolosai – Maisha yetu mapya ndani ya Kristo
(2) Mwanzoni mwa somo linalofuata, utafanya jaribio kulingana na somo hili. Soma maswali ya jaribio kwa umakini katika maandalizi.
Somo la 7 Jaribio
(1) Lini na kutoka mji gani ambapo Nyaraka za Kifungoni ziliandikwa?
(2) Kwa nini hakuna salamu binafsi zilizojumuishwa katika Waefeso?
(3) Taja sehemu kubwa mbili za Waefeso.
(4) Kulingana na Waefeso 1, nini ni wajibu wa Baba katika wokovu wetu? Wa Mwana? Na wa Roho Mtakatifu?
(5) Fafanua uchaguzi.
(6) Kulingana na Waefeso 3, siri ya Injili ni nini?
(7) Orodhesha hatari mbili zilizokuwa zinawakabili kanisa la Filipi?
(8) Katika Wafilipi 2, inamaanisha nini kwamba Yesu Kristo “alijinyenyekesha”?
(9) Uzushi wa Kolosai ulijumuisha mchanganyiko wa mawazo ya uongo kutoka katika ushawishi gani wa aina tatu?
(10) Syncretism inarejelea nini?
(11) Taja mambo matatu ambayo Nyaraka za Kifungoni zinalifundisha kanisa la leo.
(12) Andika Waefeso 4:11-16 na Wakolosai 3:1-4 kutoka katika kumbukumbu.
Free to print for ministry use. No changes to content, no profit sales.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom.