Baadhi ya viongozi wana mipaka kwenye maendeleo yao. mipaka hii inaweza kumzuia kiongozi kupandishwa cheo katika nafasi za juu au kumzuia kufanya vizuri kwenye nafasi yake anayoshikilia kwa wakati huo.
Hapa chini ni baadhi ya majina ya viongozi wa kufikirika ambao wameonyesha kuwa na uongozi wenye kikomo:
Yusufu alikuwa na matatizo binafsi (kama vile ya kifedha ya kifedha au mahusiano) ambayo hakuweza kuyatatua. Hakuweza kuweka fokasi yake kwenye shirika kwa sababu ya haya matatizo. Kazi yake mara kwa mara ilikuwa inaingiliwa na migogoro iliyokuwa ikitokea nyumbani kwake.
Badala ya kuongoza, Mathayo hulaumu wenzake kwa kushindwa kwenye shirika lake, husubiri watu wengine wamfanyie maamuzi, na hujifikiria kwamba hawajibiki kulifanya shirika liwe na mafanikio. Huwa anaelezea kwamba kushindwa kwa shirika ni kutokana na vigezo ambavyo yeye hana mamlaka navyo.
Ruth hayuko tayari kujiendeleza yeye mwenyewe, hakubaliani na makosa yake, na ni mwenye hasira kwa kila swali linaloulizwa kutokana na utendaji wake.
Michaeli anaridhika na shirika lake, haoni umuhimu wa kulifanyia uendelezaji, na hafikirii kulifanya liwe na mabadiliko yeyote. Shirika lake litakuwa halina ufanisi kuendana na mabadiliko ya dunia
[1]Ezra anafikiri kwamba yeye ndiye peke yake ambaye shirika linamhitaji. Anategemea kwamba kila mtu awaye yote kimsingi atafuata maelekezo yake tu. Hapendi kuwa na timu; anachotaka yeye ni kupata wasaidizi. Haelewi ni kwa nini watu hawapendi kuendelea kumsaidia zaidi.
Daudi Alianzisha shirika kama njia ya kujinufaisha mwenyewe na kuonyesha umaarufu wake binafsi. Hana mpango wa kampuni kuwa maarufu pasipo yeye.
Paulo ana tabia dhaifu. Anapokuwa chini ya shinikizo, anatoa miadi asizoweza kuzitekeleza, anatumia fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya mtu mwingine, haendi kwenye miadi alizoweka, na hupenda kusema uongo. Timu yake mara nyingine huwa inapata shida na aibu kutokana na sifa zake.
Viongozi hawa katika muda mfupi sana hufika katika kikomo cha ukuu wao. Hawataweza kuongoza vizuri hadi watakapokabiliana na kuondoa hali hizo za kuwa na kikomo binafsi. Kama hawatakuwa tayari kubadilika, mashirika yao hayataweza kuwa na maendeleo hadi pale viongozi hao watakapoondolewa au watakapong’olewa kwenye madaraka yao.
► Kwa kutafakari kila mmoja wa hawa viongozi wa kufikirika, jiulize swali hili, “_______ atawezaje kubadilika kabla ya shirika lake halijaweza kufanya vizuri zaidi?”
“Sina hofu na jeshi la simba linaloongoza na kondoo; nina hofu na jeshi la kondoo linaloongozwa na simba.”
- Alexander Mkuu
Sauli – Kiongozi Aliyefikia Kikomo
Sauli alikuwa ameanza kuongoza vizuri kama mfalme wa Israeli. Alikuwa mnyenyekevu na alijifikiria mwenyewe kama asiyestahili kuwa kwenye nafasi hiyo. Hata baadhi ya watu walikataa kumtambua kama mfalme.
Baada ya ushindi wa kwanza wa kijeshi wa Sauli, baadhi ya watu walitaka kuwauwa watu ambao hawakuwa wametaka kumtambua Sauli kama mfalme tangu pale awali. Sauli alisema kwamba Mungu amempa ushindi, na haikuwa muda muafaka kwa ajili ya kulipiza kisasi. Inasemekana kwamba hakukaa na tabia hii kwa kipindi cha muda mrefu.
Muda mfupi baadaye Sauli hakumtii tena Mungu. Wakati mtume alipokabiliana naye Sauli aliwalaumu watu, kuliko angebeba dhamana kama kiongozi (1 Samweli 15:21). Mtume alimwambia Sauli kwamba Mungu atautwaa ufalme wake ampe mtu mwingine ambaye atakuwa na utii.
Kwenye kipindi chote cha utawala wa Sauli, alikuwa tayari kufanya lolote ili tu kuendelea kung’ang’ania kwenye uongozi. Kamwe hakuwahi kutubu na alikuwa anajaribu kupata upendeleo wa Mungu. Kamwe hakuwa amekubaliana na ukweli kwamba Mungu alikuwa anakwenda kumbadilisha kwenye nafasi yake. Kama angekuwa ametubu, roho yake ingekuwa imeokolewa. Angeweza akatumika kama mfalme hadi pale ambapo Mungu atakuwa ameleta mtu mwingine badala yake, na angeweza akamaliza kwa heshima. Baadhi ya wazee, wanaotumika kwa muda mrefu humaliza bila ya kuwepo heshima kwa sababu ya tabia walizokuwa nazo hao wazee kwenye miaka ya mwishoni ya uongozi wao, wakipigania nafasi zao wakati wakiwa hawana tena uwezo wa kuendelea kuongoza vizuri.
Kwenye siku moja ya mapigano, Sauli alisema, “Hakuna mtu awaye yote atakayekula chakula chochote hadi vita itakapokoma, ili nijilipizie kisasi juu ya adui zangu” (1 Samweli 14:24). Amri hiyo haikuwa ni ya hekima, kwa sababu baada ya masaa kupita ya mapigano kila mtu alikuwa amechoka sana. Pia amri hiyo inaonyesha kwamba fokasi yake ilikuwa ni ya kibinafsi. Kwenye akili yake, vita ilikuwa ni kwa ajili yake peke yake.
Sauli alikuwa katika hali ya kutokuwa salama kiasi kwamba hakuweza kukiri kosa. Ilikaribia kidogo sana amwue mtoto wake Yonathani kwa sababu kwa kutokujua alikataa kutii amri ya baba yake, ingawaje matendo ya Yonathani yalileta ushindi mkubwa.
Kwenye vita nyingine, Sauli alikuwa anamngojea Samweli afike kwa ajili ya kutoa dhabihu ya taifa na kuomba msaada wa Mungu. Siku zilikuwa zinapita, na watu wengi wa Sauli walikuwa wanaondoka kwa sababu ya hofu. Sauli aliamua kuifanya dhabihu hiyo yeye mwenyewe, ingawaje ni kuhani peke yake aliyekuwa ameruhusiwa na Mungu kuitenda kazi hiyo. Wakati sherehe ilipokuwa ikiendelea, Samweli akawasili. Alimkemea Sauli, lakini Sauli alimtaka aendelee hadi mwisho kuikamilisha sherehe ili watu wasitambue kwamba kuna jambo lolote lililofanyika vibaya au kinyume (1 Samweli 15:30). Sauli alihusika zaidi na maoni ya watu kuliko kibali cha Mungu.
Sauli alikuwa na wivu kwa mafanikio ya watu wengine, hasa ya Daudi. Alitumia muda wake mwingi na rasilimali katika kumuwinda Daudi, ingawaje Daudi hakutaka kumdhuru.
Alikuwa na mashaka na akalalamika kuhusu ukosefu wa uaminifu wa watu wake. Kutokana na mashaka yake, alisikiliza maneno ya watu wasemao uongo mwingi dhidi ya watu wengine (1 Samweli 24:9). Alisikiliza ushauri wa uongo kutoka kwa washauri wake wabaya. Alilalamika kwamba kila mtu alikuwa kinyume chake na kwamba hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa akimpa taarifa alizokuwa anazihitaji (1 Samweli 22:8).
Yonathani, aliyekuwa mtoto wa Sauli, alikuwa tofauti kabisa na baba yake. Alishatambua kwamba Daudi ilikuwa awe mfalme wa Israeli na akakubaliana na ukweli huo. Sauli hakuweza kuelewa ni kwa nini Yonathani hakutaka kumchukia Daudi. Yonathani na Daudi walikuwa marafiki wakubwa. Yonathani alikuwa na imani iliyokuwa inamtegemea Mungu ambayo ilikuwa inampa ujasiri wa kupata matokeo makubwa hata baada ya Sauli kuwa amepoteza imani yake. Kwa masikitiko makubwa, Yonathani aliuawa kwenye mapigano kwa sababu ya makosa ya baba yake.
Sauli alikuwa mtu wa vitani katika maisha yake yote. Kila alipomwona mtu ambaye alionekana kuwa na nguvu, alimlazimisha ajiunge na jeshi lake (1 Samweli 14:52). Hii inamaanisha kwamba alikuwa mara kwa mara anayaweka mapenzi yake kwa mtu yeyote bila ya kujali mahitaji yao. Kamwe hakuwahi kufikiria kwamba alikuwa na msaada wa kutosha. Jambo hili lilisababisha watu kumwepuka Sauli.
Hapa tunaona tofauti kubwa ya ulinganifu kati ya Sauli na Daudi. Daudi aliwavutia mashujaa, lakini watu walimkwepa Sauli. Watu wa Daudi walikuwa na upendo mkubwa kwake kiasi kwamba watu walidiriki kuhatarisha maisha yao kwenda kuchukua maji ya kunywa kwa ajili ya Daudi kutoka katika eneo ambalo alikuwa analipenda. Mara nyingi Sauli alikuwa analalamika kwamba watu wake walikuwa hawana uaminifu wa kutosha kwake, lakini yeye hakuweza kumwamini Daudi, aliyekuwa mwaminifu kabisa kwake.
Maelezo ya John Maxwell kuhusu Viwango vya Uongozi
[1]John Maxwell alifafanua viwango vya uongozi vya ushawishi. [2] Viwango hivi havirejei viwango vya nafasi za uongozi. Mtu aliye katika nafasi yeyote ya uongozi anaweza akawa kwenye kiwango kimojawapo katika viwango vya uongozi vya ushawishi. Kiongozi wa kipekee na aliye mzuri sana atakuwa anapanda kupitia viwango hivi kwa wakati hata kama atakuwa amebakia kwenye nafasi yake aliyoko.
(1) Uongozi wa Nafasi
Uongozi wa mtu unaweza ukaanza kwa kuwa kwenye nafasi. Watu wengi walioko kwenye nafasi hudhania kwamba hawahitajiki kufanya jambo lolote la ziada ili kuweza kuwa kiongozi. Hawatambui kwamba wanahitajika wapate kuaminiwa na watu wao. Viongozi walioko kwenye nafasi zinazotambulika wana tabia ya kutegemea mamlaka iliyopo ili kupata ushirikiano. Wanaweza wakawa tegemezi kwenye vichocheo kama malipo na adhabu kuliko kuwashawishi watu kushirikishana malengo yao. Aina hii ya uongozi ni ya kawaida lakini ni mara chache sana inaweza ikaleta matokeo mazuri yanayotegemewa.
Kiongozi aliyeko kwenye nafasi mpya anapaswa aweze kuonyesha kwamba anaelewa historia na utamaduni wa shirika. Hapaswi kupendekeza mawazo na kufanya mabadiliko pasipo kuonyesha kwamba anaridhika na kile ambacho kilikuwa kimefanyika kabla ya hapo. Anapaswa aonyeshe kwamba anashirikisha thamani na faida za shirika.
Kiongozi anapaswa ahakikishe watu wanakuwa na vile vitu ambavyo vitawafanya waweze kufanya vizuri kwenye nafasi zao. Anapaswa afanye mambo makubwa kuliko walivyokuwa wanategemea afanye kutoka kwake kwa ajili ya majukumu ya nafasi yake aliyo nayo. Atapaswa afanye baadhi ya mabadiliko ambayo watu walioko katika shirika lake watatambua kwamba ni mazuri.
(2) Uongozi wa Kibali
Ngazi hii inarejea kwenye “Kibali” kwa sababu watu sasa wanataka wamfuate kiongozi wao. Kiongozi aliweza kufika katika hatua hii kwa kukuza mahusiano yake na watu wake. Alionyesha dhamira binafsi ya kuhusika nao katika mambo yanayohusiana na maisha yao, badala ya kazi tu. Anawalinda dhidi ya kunyanyaswa na shirika. Anatafuta njia za kuweza kuwasaidia watu wake kibinafsi.
(3) Uongozi wa Uzalishaji
Wakati kiongozi akiwa kwenye ngazi ya tatu, watu hawamfuati tu kwa sababu ya uhusiano uliopo, bali kwa sababu ya matokeo mazuri. Matendo ya kiongozi yanawasaidia kufikia kwenye malengo, kwa hiyo watu wanaonyesha ushirikiano kwa sababu wanapenda kile kinachotendeka kupitia kwake. Kwa sababu ya kiongozi, shirika linafanikiwa, na watu wanafanikiwa kibinafsi. Kufikia kwenye hatua hii, kiongozi ndiye anayewasilisha malengo, anayetengeneneza jinsi mambo yatakavyokwenda, na kudumisha uwajibikaji wa matendo yake mwenyewe na ya watu wake.
(4) Maendeleo ya watu.
Ngazi ya nne ni maendeleo ya watu, ambapo baadhi ya watu wanafanyika kuwa viongozi wakiwa na muunganiko binafsi na kiongozi, Wanaamini katika matokeo anayoyapata, wana uhusiano binafsi na kiongozi, na wanajisikia kuwa na uzoefu wa utoshelevu wa binafsi. Katika ngazi hii, kiongozi anapaswa awekeze angalao kwenye asilimia 20% ya watu walio juu katika kuleta ufanisi. Atapaswa awe anajenga kundi la watu ambao watakuwa wanamsaidia katika kuongoza.
(5) Watu
Ngazi ya tano Maxwell anaiita “Watu,” kwa sababu kiongozi amekuwa ni mtu anayejulikana sana kwamba watu humfuata kwa jinsi alivyo. Anajulikana kuwa kiongozi kwa sifa zake na watu humfuata yeye hata kabla hawajakuwa na muunganiko binafsi na yeye
Hitimisho
Kiongozi hawezi akawa kwenye ngazi moja na watu wake wote. Kwa mfano, baadhi ya watu wake wanaweza wakamfuata kisa tu ni kwa sababu yuko kwenye nafasi ya mamlaka (uongozi wa nafasi), wakati wat wengine wanaoshirikiana naye kwa sababu wanaona kwamba uongozi wake unaleta matokeo mazuri (uongozi wa uzalishaji).
Kiongozi anatakiwa aifanyie tathmini ngazi yake mwenyewe na atambue ni kitu gani anahitajika kufanya ili kufika kwenye ngazi inayofuata. Hapaswi aridhike na kubakia kwenye ngazi ile moja ambayo hapo mwanzoni ndiyo iliyokuwa imempatia uzoefu wa mafanikio. Kwa mfano, baadhi ya viongozi wanaridhika kubakia kwenye ngazi ya pili, mahali ambapo wanakuwa wanapendwa na watu wanaowaongoza. Kiongozi kwa wakati wote anapaswa awe na lengo la kwenda kwenye ngazi ya juu ya uongozi.
“Majukumu yanatolewa kwa yule mtu ambaye imani iko kwake. Jukumu siku zote ni alama ya kuwa na imani na mtu.”
- James Cash Penney
[2]Maelezo ya Ngazi hizi hayatoki yote kwenye maandiko ya Maxwell. .
Kuondoka
Wakati mwingine kiongozi anayekua anaweza akaondoka kutoka shirika moja kwenda kwenye shirika lingine. Hata kiongozi aliyekomaa ambaye amekuwa kwenye nafasi ya uongozi wa mahali kwa muda mrefu anaweza akaondoka.
Je, ni kwa jinsi gani kiongozi anaweza akajua kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuondoka?
Wakati mwingine kiongozi wa huduma atajua kwamba Mungu anamwita kwenye eneo lingine la huduma. Mungu ni mwenye uwezo wa kudhihirisha kwa uwazi mapenzi yake. Mtu hapaswi kutegemea tu hisia zake za ndani; kunapaswa kuwepo na udhihirisho wa mwelekeo wa Mungu. Kwa kawaida kama Mungu anaelekeza mabadiliko, atafanya mabadiliko maalumu kwenye mazingira mbalimbali au kutoa katika njia ambayo inathibitisha mwelekeo wake.
Kuna mambo mengine pia ya kutafakari wakati wa kuamaua aidha kuondoka au kutoondoka:
Usipange kuondoka kwa sababu tu hauko tayari kuwa chini ya mamlaka.
Usipange kwenda kwenye nafasi mpya kwa sababu malipo ni makubwa.
Usipange kwenda kwenye shirika ambalo litakutaka wewe uingie kwenye maridhiano au makubaliano ya kubadilisha msimamo wa imani au maadili yako.
Usipange kukiuka vipaumbele vya uangalizi wa familia yako kwa ajili ya kupata fursa ya cheo. Wapatie familia yako kanisa zuri na mazingira ya shule yaliyo mazuri kwa kadri itakavyowezekana. Hatua hiyo itakuwa nzuri kwa ajili ya familia yako.
Nafasi mpya inapaswa iwe na uwezo uliopanuka kwa ajili ya kuendeleza uongozi. Nafasi mpya inapaswa iwe na ustadi na uwezo wa kufanana na ulio nao wewe.
Jaribu kuweka uhusiano wako mzuri na watu unaowaacha. Hata kama unafikiria wamekufanyia vibaya, usitoe kauli au matamshi yaliyo makali kwao. Jinsi muda utakavyokuwa unapita, wanaweza kukumbuka sifa zako na kusahau makosa yako. Huenda utawasiliana nao tena, na wanaweza wakawa na uwezo wa kukusaidia hapo baadaye. Usitengeneze maadui.
Mfano mbaya…
Dema alisafiri kwenda kwenye huduma akiwa na Mtume Paulo. Alikuwa sehemu ya timu ya umishenari iliyokuwa imepeleka injili kwenye maeneo mageni mapya, akiwa anashuhudia miujiza na maelfu ya watu wakiokoka. Makanisa mapya yalizinduliwa, yakitengeneza mtandao mkubwa kwenye kila jiji kubwa.
Kwa masikitiko, Dema hakutambua fursa ya ajabu aliyokuwa nayo. Paulo alisema, “Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa” (2 Timotheo 4:10).
Maelezo ya Jim Collin kuhusu Ngazi mbalimbali za Uongozi
Tulikuwa tumeangalia maelezo ya Jim Collin kuhusiana na ngazi za uongozi kwenye utumishi (somo la 5). Kwenye somo hilo, tulijifunza tabia maalumu za kiongozi wa Ngazi ya 5.
Katika somo hili tutaenda kuangalia tofauti zilizopo kati ya ngazi hizo. Hapa kuna maelezo ya Collin kuhusiana na ngazi tano za uongozi. Uandishi wa maneno umesahihishwa na kufanywa bora zaidi na maelezo yameongezwa.
Ngazi ya 1: Mtu binafsi mwenye uwezo sana.
Mtu huyu hufanya vizuri sana kwa sababu ya kipaji, ufahamu, stadi alizo nazo na tabia ya kufanya kazi zilizo nzuri. Mtu huyu anaweza asiwe kwenye nafasi ya uongozi, lakini ana ushawishi mkubwa kutokana na utendaji wake wa kazi nzuri.
Ngazi ya 2: Mwanachama mchangiaji kwenye timu
Mtu huyu husaidia kikundi chake katika kukamilisha malengo na kazi za kikundi vizuri akiwa pamoja na kikundi. Anaweza asiwe kiongozi wa kikundi, lakini hukishawishi kwa ushiriki wake.
Ngazi ya 3: Meneja mwenye uwezo
Mtu huyu huandaa watu na rasilimali katika kukamilisha malengo. Yeye hakuandaa hayo malengo, lakini anakubaliana na malengo ambayo yameandaliwa na kiongozi. Anachukua usimamizi wa rasilimali zinazopatkana na kazi zilizopo kwenye shirika lake.
Ngazi ya 4: Kiongozi mwenye ufanisi
Kiongozi huwasaidia watu wa shirika kuendeleza na kushirikisha maono. Anawasaidia kuweka malengo. Anawahamasisha kujitolea na kuweka bidii katika kufanikisha maono yaliyo wazi. Hasimamii tu kile kilichopo, bali anachukua jukumu la kuhakikisha mafanikio ya shirika kwa kutoa msaada, kutafuta rasilimali, na kurekebisha kusudi.
Ngazi ya 5: Mtendaji wa Ngazi ya 5
Mtu huyu anazo tabia za kiongozi wa ngazi ya 4, lakini pia anayo tabia moja ya kipekee na muhimu sana. Kwa sababu ya kujitoa kwake kikamilifu kwa ajili ya shirika, anakua anao unyenyekevu binafsi na dhamiri. Analijenga shirika katika kuwa na umaarufu wa muda mrefu.
Daudi – Kiongozi Aliyevuka Viwango
Daudi alisheheni katika majukumu mengi. Alikuwa mchungaji wa kondoo, mwandishi wa nyimbo, mwimbaji, mpiga zeze, kiongozi wa ibada, mtume, mpiganaji vita, jenerali wa jeshi na mfalme.
Daudi alikuwa mtoto wa mwisho katika familia yake iliyokuwa kubwa. Ni mara chache sana kwa mtoto wa mwisho kuwa kiongozi mkubwa na maarufu. Familia yake haikuwa imetegemea kuona uongozi kutoka kwake, lakini Mungu alimchagua.
Mwanzoni Daudi alianya kazi kama mchungaji wa kondoo. Hii haikuonekana kuwa kama ni kazi muhimu, lakini ilimwandaa kwa mambo mengi muhimu zaidi. Hisia yake ya kuwajibika ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba hakukimbia kutoka katika hatari yeyote. Alimtegemea Mungu kwa ajili ya nguvu za kukamilisha majukumu yake na alimwua simba na dubu kwa msaada wa Mungu.
Kama ilivyo kwa kila kiongozi wenye uwezo mkubwa, Daudi alikuwa anafundishwa bila ya yeye mwenyewe kujijua kwamba alikuwa kwenye mafunzo. Ushindi mbalimbali alioupata ulimtengeneza kuwa mtu mwenye ujasiri kutoka kwa Mungu. Alikuwa ni kiongozi ambaye hakuweza kuruhusu hofu imzuie katika kufanya kazi zake.
Fikiria ni kwa jinsi gani maisha ya Daudi yangekuwa tofauti kama angekuwa hazingatii ulinzi wa kondoo wake. Angeweza kukimbia wakati simba au dubu walipoingilia kundi. Baadaye, wakati aliposikia changamoto iliyokuwa ikitokea kwa Goliati, hangeweza kuwa na wazo la kupambana au kukabiliana na jitu lenye nguvu.
Mungu alimtuma Samweli kwenda kumpaka Daudi mafuta ya upako. Upako huo ulimaanisha kwamba Mungu amemchagua Daudi, na kwamba Mungu atampa msaada maalumu kwa ajili yake katika kukamilisha wito wake. Wakati baba yake Daudi alishangaa kwamba Samweli hakumchagua mmoja wa kaka zake wakubwa, Samweli alisema, “Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo” (1 Samweli 16:7). Mara nyingi Mungu amewashangaza watu kutokana na watu anaowachagua kwa ajili ya uongozi.
Changamoto kubwa zilizojitokeza kwa Daudi mwanzoni mwa maisha yake zilihusiana na fursa. Hata hivyo, ni mtu mmoja tu mwenye tabia ya Daudi ambaye angeweza akazitambua fursa hizo. Maelfu ya watu walimsikia Goliati na changamoto yake, lakini ni Daudi tu aliyeiona hiyo kwamba ilikuwa ni fursa kwake. Alishawishika kwa motisha wa kupewa zawadi, lakini hata zaidi ya hapo alipigana kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Daudi alisema, “Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?”
Uongozi ni ushawishi. Siku ambayo Daudi alimwua Goliati, alikuwa kiongozi wa kweli na wa uhakika wa jeshi, kwa sababu jeshi liliambatana naye baada ya ushindi wake. Ushindi wake uliwafanya waamini kwamba wataweza kupata ushindi.
Daudi alikuja kuwa askari kwa Sauli. Alitenda kwa busara katika njia zake na ushawishi wake ukaongezeka (1 Samweli 18:14). Ingawa Sauli alikuwa kiongozi aliyekuwa akishindwa na aliyemtendea Daudi yasiyo haki, Daudi bado alikuwa mwaminifu. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho kiliikuza zaidi tabia ya Daudi. Mara nyingi kiongozi mwenye nguvu ambaye ana stadi nyingi zenye nguvu hutendewa vibaya na kiongozi mtangulizi anayeshindwa. Kiongozi kijana hushawishiwa kutokuwa mvumilivu na kujaribu kuiondoa heshima yake kwa kiongozi mtangulizi.
Wakati Sauli alipojaribu kumwua Daudi, Daudi alijificha milimani. Watu wengi walijitokeza wakakusanyika pamoja naye, kwa sababu hali zao zilikuwa katika hali ya dhiki chini ya Sauli (1 Samweli 22:2). Ingawaje Sauli aliwachukulia kwamba ni maharamia, hawakugeuka kuwa majambazi. Waliendelea kupigana na maadui wa Israeli, ingawaje Sauli aliwaona kama ni maadui zake na akatumia muda wake mwingi katika kuwawinda.
Daudi alisaidia kuwalinda wakulima na wafugaji dhidi ya wanyang'anyi (1 Samweli 25:14-16). Wakati mmoja, alituma watu wake kuomba chakula kutoka kwa mfugaji ambaye walikuwa wamemlinda. Nabali, mmiliki wa shamba hilo, aliwakosea heshima, akasema kuwa wao ni watumishi waliotoroka mabwana wao, na hakuwapa kitu chochote. Daudi alikasirika na akachukua watu wake kwenda kumuua Nabali. Akiwa njiani, alikutana na Abigaili, mke wa Nabali, ambaye alikuja kufanya amani. Yeye alimkumbusha Daudi kwamba hadi wakati huo, hakuwahi kutumia vurugu kwa faida yake binafsi. Abigaili akasema, "Siku moja utakuwa mfalme. Usifanye jambo litakaloharibu sifa yako kama mtu mwenye haki" (1 Samweli 25:30-31). Daudi alisikiliza ushauri wake.
Daudi alikuwa tayari ameshapakwa mafuta ya upako kwa ajili ya kuwa mfalme, lakini bado kwa muda mrefu ilionekena kwamba haingetokea. Alikuwa anashawishika kujaribu kuchukua madaraka kwa nguvu, lakini badala yake alisubiri na kumngojea Mungu atende. Kwa ajili ya unyenyekevu wake na kumwamini Mungu, Daudi alifanywa kuwa mfalme mkuu.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili.
Kazi za kufanya Somo la 8
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Jifunze ngazi tano za uongozi zilizoelezwa na Maxwell na ngazi tano za uongozi zilizoelezwa na Collins. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
4. Kabla ya kipindi kijacho, soma 1 Wafalme 12. Viongozi wawili wamejadiliwa hapa. Andika kuhusu makosa ya viongozi hawa wawili.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.