Watu wengi wanakuwa kwenye mishughuliko lakini hawafikirii sana kuhusu yale wanayoshughulika nayo. Wanadhania kwamba hakuna haja ya kufikiria kuhusu ni nini wanachotakiwa wafanye.
► Je, inatokea nini kama mtu hatafikiria kwa kumaanisha kuhusu vipaumbele?
Tafakari taarifa hizi:
Kuna mambo mengi bora zaidi ya kufanya kuliko yale mambo tunayofanya.
Kuna njia bora zaidi za kufanya mambo kuliko njia tunazotumia kufanya hayo mambo.
Tunaweza tukapata matokeo bora zaidi kuliko tunavyopata
► Kama hizi taarifa ni za kweli, je, tutajifunzaje kufanya kwa ubora zaidi?
Kwa mujibu wa John Maxwell, ni jambo la kawaida kwa:
Watu kuwa mvivu mno kiasi kwamba hawawezi kuwa wazuri katika fikra zenye lengo.
Watu kuwa wasio na nidhamu kiasi kwamba hawawezi kupata manufaa ya fikra za kimkakati.
Watu kuwa na mawazo mepesi kiasi kwamba hawawezi kuhoji fikra zinazopendwa na wengi.
Watu kuwa na kiburi sana kiasi kwamba hawawezi kushirikiana na wengine katika kubadilishana mawazo.
Watu kuwa na mtazamo wa kujifikiria wao wenyewe kiasi kwamba hawawezi kupata manufaa ya kuwa na moyo wa kujitoa.
Watu kuwa wasio na kujitolea ya kutosha kulenga matokeo ya mwisho.[1]
[2]Unapokuwa unajua vipaumbele vyako, maamuzi mengi huwa marahisi. Vipaumbele hupima malengo yako na njia ya kuyafikia hayo malengo.
Vipaumbele hukuwezesha wewe kutambua na kuchagua kutoka katika fursa zilizopo. Mtu ambaye hana vipaumbele vilivyo wazi atakuwa anakengeushwa na fursa ambazo hazina uhusiano na malengo sahihi.
[1]John Maxwell, How Successful People Think (New York: Center Street, 2009), 82-83.
► Je, ni vipaumbele gani ambavyo kila Mkristo anapaswa awe navyo?
Kwa Mkristo, baadhi ya maadili yanapaswa yaongoze vipaumbele binafsi.
Kwanza, wokovu na uhusiano wako binafsi na Mungu ndiyo vipaumbele kamili.
Kamwe hupaswi kufikiria kuhusu kitu chochote ambacho kitakufanya ukubali kulegeza msimamo wa maadili hayo. Hii inamaanisha kuwa na utii kabisa kwa Mungu.
John Wesley alifundisha kwamba tunajua tu baadhi ya mambo kuhusiana na mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Tunajua kwamba Mungu anatutaka sisi tuwe watu wazuri na tufanye mambo mazuri. Kwa hiyo, tunapokuwa tunafikiria kuhusu uamuzi wowote, tunapaswa tuchague kitendo ambacho kitaendana na kuwa kizuri na kinachofanya vizuri. Hatupaswi kujiweka sisi wenyewe kwenye hali ambazo kuna uwezekano kwamba hazitatufanya tubakie na tukae kwa utakatifu katika mioyo na matendo yetu, au zikawa na uwezekano mkubwa wa kutuzuia tusikamilishe mambo mazuri.
Kanuni hii inahusisha maamuzi kama ya mahali tunapoishi, mahali tunapofanyia kazi, nani wa kuoa au kuolewa, aina gani ya elimu tunayotafuta, tunafanya biashara gani, tuchague jambo gani la kutustarehesha, na tuwe na marafiki wa aina gani. Kwa Mkristo, ukweli wa Neno la Mungu na mapenzi yake unapaswa uwe ndiyo msingi kwa ajili ya kila shirika, na siyo tu kwa ajili ya mashirika ya huduma. Mkristo hapaswi kuendesha biashara ambayo ni kinyume na haiendani na Neno la Mungu.
Pili, wito wa Mungu kwenye maisha ya huduma una mamlaka juu yako.
Hii ina maana kwamba Mungu huongoza nia ya maisha yako. Anaweza akakugeuza kutoka kwenye malengo yako, kukupeleka kwenye malengo yake yaliyo kwa ajili yako. Unapaswa ukumbuke kwamba utapata tu ukamilifu utakapokuwepo kwenye mapenzi ya Mungu. Hupaswi kujaribisha kuyafanya mapenzi ya Mungu yawe ndiyo fokasi ya muda mfupi ya maisha yako, wakati ukiweka fokasi yako kwenye malengo yako mwenyewe.
Mtu mmoja alijisikia kuwa na wito wa kuwa mchungaji, lakini hakuwa na uhakika ni kwa jinsi gani ataweza kusaidia familia yake. Alipewa kazi nzuri ya kufanya kwenye uwanja wa ndege, na akaamua kuifanya. Alikuwa anatakiwa awe akihudhuria kazini hata kwenye siku za Jumapili na kwa hiyo, hangeweza kushiriki katika ibada za Jumapili za kanisa, lakini alisema, “Kazi hii [hapa kwenye uwanja wa ndege] ndiyo kanisa langu.” Alijua kuwa hakuwa anafuata wito wa Mungu wa kuwa mchungaji, lakini hakuwa na imani kwamba Mungu angemhudumia yeye na familia yake ikiwa angeacha kazi hiyo. Alifanya kazi ya uwanja wa ndege kwa muda wa miaka thelathini. Mwishoni, alistaafu akiwa na malipo ya pensheni ya kila mwezi na akaamua kufanya jambo kwa ajili ya Mungu akiwa katika umri wa uzeeni. Je, mtu huyu alikuwa na vipaumbele sahihi?
Yesu alisema, “Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yohana 4:34). Je, inamaanisha nini kama mapenzi ya Mungu ni chakula chako? Chakula ndicho kinachokutosheleza. Kwa hiyo, chakula chako ndicho kinachokupa wewe motisha.
Vipaumbele vinavyoelezwa katika sehemu hii havina ulazima wa kuorodheshwa kwa mfuatano au mpangilio wa umuhimu wake.
Kipaumbele kingine cha tatu kwa ajili ya Mkristo ni familia.
Biblia inatuambia kwamba mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini (1 Timotheo 5:8). Jukumu ka kiongozi kwa ajili ya familia yake siyo tu msaada wa kifedha, lakini pia kuwatunza kiroho, pamoja na mahitaji mengine.
Kazi ya huduma inapaswa iende kwa pamoja na utoaji wa mahitaji ya familia. Mapenzi ya Mungu kwako siyo kukuweka kwenye mgogoro na majukumu ya familia yako, kwa sababu majukumu hayo ni sehemu ya mapenzi ya Mungu kwa ajili yako. Wakati mwingine watu ambao wameshafikia kwenye mambo makubwa katika huduma hawajaweza kuwa mifano mizuri ya kuigwa katika utunzaji wa familia zao. Mtu anayedhania kwamba anaweza akaidharau familia yake kwa ajili ya huduma ana makosa.
Yoshua alikuwa kiongozi wa taifa lililokuwa uhamishoni ambalo lilikuwa na ushawishi wa dini za aina mbalimbali. Walipofika kwenye nchi ya miadi ambayo Mungu alikuwa amewaahidi, ilikuwa ni wakati wao wa kuweka msimamo kwenye Agano la Mungu. Yoshua aliwataka watu wake wachague kama watamtumikia Mungu au laa, Lakini hakusubiri upigaji kura kabla ya kufanya uamuzi wake mwenyewe. Aliwaambia kwamba lolote watakalochagua, yeye na nyumba yake watamtumikia Bwana (Yoshua 24:15). Huu ulikuwa ni uongozi wenye nguvu uliokuwa na msingi wake kwenye usadikishaji. Kama taifa lingechagua kumtumikia mungu mwingine tofauti, Yoshua hangendelea tena kuwa kiongozi wao; hakuwa tayari kukubali kubadilisha msimamo wake wa uaminifu kwa Mungu. Ujasiri na usadikishaji wake wa ukweli ulisababisha taifa kuwa na chaguo lililokuwa sahihi.
Kipaumbele cha nne ni kanisa la mahali pamoja.
Kanisa la mahali pamoja ni mwili wa Kristo na utimilifu wa Mungu duniani. (Waefeso 1:23). Mungu huliwezesha kanisa kukamilisha malengo yake (Waefeso 4:11-13). Kupitia kanisa Mungu atatukuzwa milele (Waefeso 3:21). Kwa hiyo, Mkristo hapaswi kufikiri kwamba vipaji vyake na wito wa huduma vimetenganishwa na kanisa. Ikiwa hajitolei kwa kanisa, hafanyi mapenzi makamilifu ya Mungu katika maisha yake.
Vipaumbele vilivyotajwa hapo juu ni rahisi kuvitamka, lakini ni vigumu zaidi kuvitumia au kuvitendea kazi katika mahitaji ya maisha. Wakati mwingine tunajishughulisha sana na mambo ya kina ya familia, huduma, na biashara, tukiharakisha bila kusimama kufikiria juu ya vipaumbele vyetu. Shughuli unazofanya zinapaswa kuchaguliwa baada ya kufikiri kwa makini. ikiwa unajishughulisha sana hata ukashindwa kutulia na kufikiri, huenda unafanya mambo yasiyofaa. Huenda hufanyi kazi kulingana na vipaumbele unavyovikiri.
► Kwa nini ni vigumu kufuata vipaumbele vyako mara kwa mara?
Kanuni ya Pareto
Kanuni ya Pareto ilipatikana kutokana na mtu aliyeitwa Vilfrido Pareto, raia na mchumi kutoka katika nchi ya Italia ambaye aligundua kwamba asilimia 80% ya ardhi ilikuwa inamilikiwa na asilimia 20% ya wananchi wote. Aligundua kwamba asilimia 80% ya zao la kunde lililokuwa linavunwa kutoka katika shamba lake lilitokana na asilimia 20% ya maganda. Aliona kwamba asilimia hizi zinawiana na mambo mengi. Watu wengi wamekuwa wakitumia kanuni hii kwenye uongozi, muda, na biashara.
Asilimia 20% ya wauzaji kwenye kampuni hufanya asilimia 80% ya mauzo yote.
Asilimia 20% ya wateja hufanya asilimia 80% ya manunuzi yote
Asilimia 20% ya wateja hufanya asilimia 80% ya malalamiko.
Asilimia 20% ya wagonjwa wanaohitaji tiba hutumia asilimia 80% ya rasilimali zote za tiba
Asilimia 20% ya wanafunzi hutumia asilimia 80% ya muda wote wa mwalimu.
Asilimia 20% ya wanachama wa kanisa hufanya asilimia 80% ya kazi zote za kanisa.
Asilimia 20% ya wanachama wa kanisa hutoa asilimia 80% ya msaada wa kifedha.
Kwa watu walio wengi, asilimia 20% ya nguvu zao hutengeneza au huzalisha asilimia 80% ya mafanikio yao. Watu wengi wanahitajika waelekeze fokasi ya nguvu zao kwa njia nzuri zaidi. Wanahitajika watumie muda wao mwingi zaidi kwenye shughuli zenye kuleta ufanisi zaidi na watumie muda wao mchache kwenye shughuli zenye kuleta mafanikio kidogo.
Tumia kielelezo kinachoonekana ili kuhakikisha kwamba dhana hii inaeleweka. Chora duara kubwa kwenye karatasi. Igawanye kwenye asilimia 20% na asilimia 80%. Fanya hivyo tena kwenye karatasi nyingine. Sasa elezea kwa kuonyesha kutoka karatasi moja hadi nyingine. Asilimia 80% ya watu (ikilenga sehemu kubwa kwenye karatasi) kwenye kampuni hufanya asilimia 20% (ikilenga sehemu ndogo kwenye karatasi katika ukurasa mwingine) ya kazi zote. Asilimia 20% ya watu (ikilenga sehemu ndogo kwenye karatasi ya kwanza) hufanya asilimia 80% (ikilenga kwenye sehemu kubwa kwenye karatasi ya pili) ya kazi zote.
Kiongozi ambaye anajishughulisha na mambo mengi sana anapaswa asimamishe kufanya baadhi ya mambo. Je ni kitu gani unachoweza kukiondoa cha hasara ndogo?
Wachungaji wengi hutumia asilimia 20 ya muda wao kwa asilimia 80 ya watu, na asilimia 80 ya muda wao kwa asilimia 20 ya watu. Swali ni, je, wanazingatia watu sahihi? Kawaida, tunatumia muda wetu mwingi kwa watu wenye matatizo mengi. Tunawapa muda mdogo watu wenye uwezo mkubwa, kwa sababu tayari wanafanya vizuri. Tunapaswa kuwekeza muda wetu kwa watu wanaojibu kwa njia bora Zaidi.
► Angalia tena kwenye karatasi zilizo na miduara. Asilimia 80% ya shughuli zako hukamilisha asilimia 20% ya matokeo. Asilimia 20% ya shughuli zako hukamilisha asilimia 80% ya matokeo. Orodhesha unayowajibika nayo na majukumu yako. Je, sehemu ya shughuli zako inakupa matokeo madogo? Je, ni shughuli gani unazopaswa uzifanye zaidi?
Uwiano wa Haraka na Umuhimu
Baadhi ya watu wana shughuli nyingi sana na wanajihisi kwamba kamwe hawawezi wakaweza kutimiza kufanya kazi zao zote. Wanafanya kila jukumu wanaloliona, na wanajisikia kwamba majukumu yote ni muhimu. Wanakuwa na wasiwasi kwamba watawakatisha tamaa watu wao wanaowategemea, lakini hawawezi wakamaliza kila kitu kwa wakati wake. Mara nyingi wamekuwa wamechoka na wenye kuwa na shinikizo kwa ajili ya kazi. Hawawezi wakachukua muda wao kwa ajili ya kupanga, kujifunza, na mambo ya maendeleo, kwa sababu siku zote wana kitu ambacho ni cha haraka kukifanya.
Tunahitaji uwiano kati ya haraka na muhimu. Kazi za mtu zinaweza zikagawanywa katika viwango vinne.[1]
Mambo ya haraka na muhimu huchukua usikivu wetu kwa urahisi. Kiwango hiki kinahusisha pamoja na mambo mengine kutayarisha mahubiri, kumsaidia mtu mwenye hitaji la haraka la msaada wa matibabu, na kuchangisha fedha kwa ajili ya mahitaji ya haraka.
Shughuli ambazo ni za haraka lakini siyo za muhimu kwa kawaida huhusiana na majukumu ambayo tumeyabeba ambayo hatungepaswa kuyafanya. Wakati mwingine ni miradi ya binafsi ambayo haina uhusiano na huduma. Inawezekana ikawa ni shughuli za kibiashara ambazo hazizalishi sana au kuchukua muda mwingi nje ya vipaumbele vizuri zaidi. Shughuli hizi zinaweza ni za haraka kwa sababu zinapaswa zifanyike katika muda muafaka, na bado siyo muhimu katika yale yanayopatikana kutokana nazo.
Shughuli ambazo siyo za haraka na wala siyo za muhimu hazina hitaji lolote la maana. Kama hazingefanyika, hakungekuwepo na hasara kubwa. Wakati mwingine zinahusiana na programu ambazo hazikidhi tena ukamilishaji ambao ulikuwa unakamilishwa hapo mwanzoni.
Shughuli ambazo siyo za haraka lakini ni za muhimu mara nyingi zinapuuzwa.
Hizi ni shughuli ambazo hazimaliziki kwa haraka lakini zina uthamani wa muda mrefu. Mifano ni pamoja na mafunzo ya elimu (kama mwalimu au mwanafunzi) aina mbalimbali za mafunzo, ujenzi, na uandaaji wa nyaraka zilizoandikwa. Kwa kuwa haziwezi zikamalizika leo, na hazitakuwa na msaada kwetu leo, tunajielekeza kuiweka fokasi yetu kwenye vitu ambavyo ni vya muhimu zaidi. Kiongozi anapaswa kuwekeza muda wake na rasilimali kwenye vitu ambavyo vitakuwa na thamani kwa wakati ujao. Kwa jinsi itakavyowezekana, uwekezaji huu unapaswa uwe wa kila siku.
Hatua zinazohitajika kwa ajili ya shirika zinaweza zikagawanywa kwenye aina au makundi mawili:
Maendeleo hulipeleka shirika mbele kwenye viwango vingine vya fursa na ukuaji.
Utawala huimarisha utendaji wa wakati uliopo.
Endapo kiongozi kwa makusudi hataelekeza fokasi yake kwenye maendeleo, atakuwa anajielekeza kwenye kutoa muda wake na kuweka usikivu wake kwenye utawala. Kuna msemo usemao: “Gurudumu linalotoa mlio mwembamba ndilo linalowekwa mafuta ya grisi.” Hii inarejea kwenye mwelekeo wetu wa kuweka usikivu wetu kwenye matatizo ambayo yanatukera kwa sasa hivi.
Baadhi ya viongozi hutoka kwenye tatizo moja na kwenda kwenye tatizo lingine, lakini kamwe hawawekezi kwa ajili ya baadaye. Mashirika ambayo yana mafanikio ya muda mrefu kwa kawaida ni yale ambayo yamewekeza muda na rasilimali kwenye utafiti, maendeleo, na mafunzo. Shirika ambalo haliwekezi kwa ajili ya baadaye litapoteza ufanisi wake wakati hali zinapokuwa zinabadilika.
► Kila mwanafunzi anapaswa aandae orodha ya shughuli zake na majukumu yake aliyo nayo. Kisha tengeneza mchoro wa pembe mraba kama ulivyo hapo juu na ugawanye shughuli hizo kwenye sehemu nne za pembe mraba katika mchoro huo. Tafakari: Ni mambo gani unayopuuzia ambayo ni muhimu lakini siyo ya haraka? Je, unapoteza muda wako mwingi kwenye mambo ambayo siyo ya muhimu na siyo ya haraka?
[1]Dhana hii imenukuliwa kutoka kwa Stephen Covey, 7 Habits of Highly Effective People: The Ultimate Revelations of Steven Covey, (New York: KMS Publishing, 2011).
Uwakilishi
Kiongozi anawajibika kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanyika, lakini hahitajiki kufanya kila kitu yeye mwenyewe. Anapaswa kukabidhi majukumu kwa watu wengine. Bado ni kai yake kuhakikisha kwamba kazi inafanyika inavyotakiwa. Anapaswa kuwa kila mara akipanga mafunzo na maendeleo kwa ajili ya wanachama wa timu na wale wanachama muhimu katika timu ili kwamba waweze kufanya mambo ya ziada katika wakati ujao.
Jukumu linaweza lisikabidhiwe kwa sababu siyo muhimu. Jukumu linakabidhiwa kwa sababu mtu mwingine anaweza akifanya au anaweza akafundishwa kulifanya, na kwa sababu siyo kitu ambacho ni lazima kiwe kimewekwa kwenye jukumu la kiongozi.
Baadhi ya majukumu hayawezi yakakabidhiwa kwa mtu mwingine kwa sababu ni kiongozi tu anayepaswa kuyafanya. Analiwakilisha shirika na ni msemaji wake katika njia ambayo hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kufanya hivyo. Anapaswa pia awajibike na mambo yanayohusiana na hatima ya baadaye ya shirika. Anapaswa azione fursa zinazojitokeza, hatari zilizopo, na mabadiliko yanayokuja kwa njia bora zaidi kuliko watu wengine.
Inawezekana kukawepo na majukumu ambayo kiongozi ana ustadi au uwezo nayo; kwa hiyo, kwa kawaida hapaswi kuyakabidhi majukumu hayo kwa mtu mwingine. Hata hivyo, kiongozi hapaswi kuyaweka au kuyahodhi majukumu yote kwake ambayo anaweza kuyagawa kwa watu wengine. Baadhi ya viongozi kamwe hawaridhiki na kazi zinazofanywa na watu wengine, na wanataka wao wenyewe wazifanye kazi zote na kuona kwamba zinafanyika vizuri inavyotakiwa.
Baadhi ya viongozi hujaribu kufanya kila kitu wao wenyewe na huwa hawataki kukabidhi majukumu kwa watu wengine. Wanapokuwa wamekabidhi kazi, wao huzitazama hizo kazi kwa karibu sana na kufanya maamuzi yote. Huu siyo uongozi mzuri. Kiongozi mzuri hujenga timu ya watu ambao watawekeza nguvu zao na mawazo yao, wataweka malengo, wataendeleza mbinu na kushiriki katika maamuzi mbalimbali.
Kiongozi mzuri hawezi tu kuwagawia kazi wale walio chini yake; anawagawia uongozi wake. Anawaruhusu wengine kuongoza shughuli. Ikiwa anawaambia hasa ni nini cha kufanya na jinsi ya kukifanya, atakuwa hajawaruhusu kuongoza.
Kiongozi anapokuwa ameweka vipaumbele vyake, anapaswa atafakari baadhi ya maswali:
1. “Je, ni nani atakayeweza kunisaidia?” Kama kuna majukumu mengi ambayo watu wengine wanaweza wakayafanya lakini hawafanyi, huongozi kwa utoshelevu.
2. “Je, ni majukumu gani ambayo hayawezi kufanywa bila mimi?” Kiongozi anapaswa aweke mazingatio katika majukumu hayo. Mifano ni kama uendelezaji wa timu, kutengeneza maono, na upangaji wa muda mrefu. Kazi hizo siyo lazima zifanywe na kiongozi peke yake, lakini kwa kawaida haziwezi kufanywa bila kuwepo na kiongozi.
Kujitoa Mhanga
Watu walio wengi wanafikiri kwamba kiongozi ana marupurupu mengi. Wanafikiri kwamba mamlaka yake aliyo nayo yanamruhusu kufanya jambo lolote analotaka. Ukweli ni kwamba kiongozi hujitoa mhanga kwenye haki zake ili kundi lake liweze kufanikiwa. Kiongozi hawezi akafanikiwa endapo kikundi chake kitakuwa hakina mafanikio.
[1]Kwa jinsi kiongozi anavyopanda cheo, haki zake huwa zinapungua na majukumu yake huongezeka. Kwa mfano, katika kiwango cha chini kabisa cha biashara, mtu hufanya kazi kwa masaa fulani, hufanya majukumu fulani, na hawezi akalaumika kwa mambo yaliyo juu ya wajibu wake.
Kwenye viwango vya juu vya shirika, kiongozi hufanya kazi kwa masaa yasiyo na kikomo na ni lazima afanye chochote kile kinachohitajika. Anaweza aachilie marupurupu yake mengi aliyo nayo. Kuna wakati ambao anataka kupumzika, lakini atautoa mhanga muda wake kwa ajili ya kutumikia shirika. Viongozi wengi huhitajika kwa ajili ya matatizo yanayojitokeza wakati wowote wa mchana au usiku.
Jinsi majukumu ya mtu yanavyozidi kuongezeka, ndivyo hivyo anavyokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi makubwa kwenye shirika; lakini hujitoa kuachilia marupurupu yake binafsi. Mchakato huu umeelezwa katika michoro ya piramidi. Mtu akiwa pale chini kabisa anakuwa na kiasi kidogo cha majukumu lakini akiwa na haki zake nyingi, kwa sababu anaweza akaamua ni kwa kiwango gani atumike. Jinsi atakavyokuwa anaongezeka kwenye majukumu yake, haki zake za binafsi hupungua.
Tafakari mfano wa mwanariadha. Mwanariadha wa kiwango cha juu sana aliyefanikiwa anaweza akafurahia umaarufu na utajiri. Hata hivyo, hufuata masharti makali ya matumizi ya milo au chakula, mazoezi, na huzoesha ustadi wake kwa masaa mengi kila siku. Maisha ya mwanamuziki mkubwa yanafanana hivyo.
Mtu anayejiandaa mwenyewe kushika nafasi kwenye fani ya udaktari au kufundisha kwenye kiwango cha juu ni lazima atumie miaka mingi ya kujifunza. Hawezi akatumia muda wake na fedha zake kama wanavyotumia watu wengine. Huwa anakosa kuhudhuria matukio ya burudani na starehe za aina nyingi. Anaweza hata akajinyima yeye mwenyewe mambo mengi muhimu ya msingi ili aweze kulifikia lengo lake.
Mtu anayejaribu kuanzisha biashara anapaswa kutoa rasilimali zake kwa ajili ya kusudio hilo. Hawezi akatumia fedha zote anazozipata. Atawekeza kwa ajili ya faida ya baadaye. Hatakuwa natumia fedha kama marafiki zake wanavyotumia. Rafiki zake wanaweza wakamlaumu kwa umakinifu wake anaoufanya, lakini hapo baadaye atakuwa na ziada kuliko walivyo navyo wenzake.
Mtu anayetegemewa kuwa kiongozi wa baadaye anapaswa awe mtu anayewekeza sasa kwa ajili ya baadaye. Kujitoa mhanga huanzia kwenye hatua za mwanzo za kukua kama kiongozi. Chagua kukua na kuwekeza kwenye hatima yako ya baadaye. Weka kipaumbele chako kwenye mafunzo, mazoezi ya huduma, na kuwa na muda wa kukaa na viongozi wengine.
Majukumu yako yanaweza yasionekane kama yenye maana, lakini yanakuza uwezo wako wa kufanya kazi na watu wengine na kukupa fursa ya kujenga sifa ya kuaminika
► Jadili vifungu vifuatavyo. Je, taarifa zinamaanisha nini? Je, baadhi ya matumizi yake ni yapi?
Lazima tuwe tayari kujitolea kuthibitishwa kwa mafanikio, usalama kwa umuhimu, faida za kifedha kwa uwezo wa baadaye, furaha ya haraka kwa ukuaji binafsi, uchunguzi kwa umakini, na mambo ambayo yanaweza kuwa ya kukubalika kwa ajili ya mambo ambayo ni bora.[2]
Fanyia mazoezi vipaumbele vyako kwa malengo. “Kabla ya kitu chochote kuwa tabia ni lazima kwanza kufanywa nidhamu.”[3]
Mtume Paulo alitoa ufafanuzi wa msimamo wa mwanariadha. Wanariadha hujitoa mhanga kwa sababu wana shauku au hamasa kubwa ya kufikia kwenye mafanikio (1 Wakorintho 9:25-27). Paulo anaelezea pointi hapa kwamba wanafanya kwa ajili ya heshima ya muda ya kidunia; sisi tunapaswa tufanye kwa ajili ya thawabu ya milele. Hamasa zetu ni tofauti na hamasa zao, lakini pia hazipaswi ziwe za kiwango cha chini.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili.
[2]John Maxwell, For Everything You Gain, You Give Up Something: Lesson #22 from Leadership Gold (Nashville: Thomas Nelson, 2012)
[3]Ken Blanchard and Phil Hodges, The Servant Leader: Transforming Your Heart, Head, Hands, and Habits (Nashville: Thomas Nelson, 2003), 85
Muhtasari wa Taarifa Tano.
1. Vipaumbele hubainisha malengo yako na jinsi unavyochagua kufikia malengo hayo.
2. Vipaumbele hukuwezesha kutambua fursa zilizopo na kukafanya uwe na uchaguzi kutoka katika hivyo vipaumbele.
3. Utapata utumilifu kwenye mapenzi ya Mungu pekee.
4. Kiongozi mzuri hagawi kazi tu; pia anawakabidhi uongozi walio chini yake.
5. Kwa kadri kiongozi anavyopanda katika daraja la nafasi ya uongozi, haki zake hupungua na majukumu yake huongezeka.
Kazi za Kufanya Somo la 7
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Fanya kukariri Taarifa Tano kwa Muhtasari zilizoko katika somo la 7. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
4. Kabla ya kuanza kwa kipindi kingine kinachofuata, soma 1 Samweli 13-15. Je, kulikuwa na matatizo gani kwenye uongozi wa Sauli?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.