Uongozi wa huduma mara nyingi ni utamaduni unaoingiliana kwa sababu ya jukumu la kanisa la kuifikia dunia kwa njia ya uinjilisti, na kwa sababu umoja wa kiroho wa kanisa hufanya huduma ya utamaduni unaoingiliana kuwa kitu kinachowezekana.
Mtu anayetumika kikazi kwenye utamaduni mwingine kwa kawaida anafikiriwa kama ni kiongozi kwa sababu ya mafunzo na hadhi yake katika shirika lililompeleka. Kwa hiyo, mtu aliye katika huduma ya utamaduni unaoingiliana anapaswa ajifunze uongozi.
► Je, ni mifano gani uliyo nayo ya kanisa ambalo linajihusisha na utamaduni zaidi ya mmoja?
Kuongoza katika tamaduni tofauti ni kuwahamasisha watu wanaotoka katika tamaduni mbili au zaidi kushiriki nawe katika kujenga jamii yenye uaminifu, kisha wakufuate na wawezeshwe nawe kufanikisha maono yenye mvuto ya imani.[1]
Kujenga Jumuiya yenye Imani
[2]Kwanza, jenga jumuiya ambayo inashirikishana maisha pamoja, na kisha tafuta maono ya kitu ambacho jumuiya hiyo inaweza ikakifanya kwa ukamilifu. Katika jitihada za kuanzisha kanisa, jamii inaweza kuwa timu ndogo kabla ya kuwepo kwa kusanyiko lililoimarika. Katika juhudi za kuanzisha kanisa, jumuiya inaweza ikawa ni timu ndogo kabla ya kuanza kwa kusanyiko la kanisa. Kadri kusanyiko linavyoendelea kukua, litakuwa na vipengele vyote vya maisha vinavyohusiana na kanisa Ili hilo liweze kutokea, itabidi timu iwe na malengo juu ya hilo, haswa kama timu hiyo inaundwa na au inahusisha wageni walio wengi. Ni lazima kimawazo wakatae dhana ya “sisi na wao”.
Kuaminiana kunakujaje? Ni lazima liwepo na kusudi. Inahitajika uthubutu, makosa yasiyoepukika, na upendo wa kutosha na uaminifu katika kufanya marekebisho na kujenga uhusiano. Kama hali hizo hazitakuwepo kwenye uhusiano, uhusiano huo ni mdhaifu, na hakutakuwepo na kujenga kuaminika kwa kiasi kikubwa.
► Je, itakuwa inamaanisha nini kuwaamini watu kama hivi?
Je, “kuchochea” inamaanisha nini? inamaanisha zaidi ya kuleta hisia chanya. Inahusisha kuunda mitazamo na kuhamasisha vitendo. Hili linahitaji maudhui ya imani pamoja na ari ya wanajumuiya.
Maono ya kuchochea ya Imani
Kwa uongozi wa huduma, maono ya kuchochea yatahusisha pamoja na mambo mengine injili, kuishi maisha ya utakatifu, kanisa, na uinjilisti. Usiwe na haraka sana ya kuona ni kwa jinsi gani mambo haya yataweza kuonekana katika utamaduni mpya.
Je, kwa nini neno “kuvutia sana” limetumika hapa? Maono yaliyoelezwa hapa yanakuja na mamlaka ya kibiblia ambayo yana wito wa kujitolea kuwajibika. Maono haya yanapaswa yawe ya shuruti kwa wanachama wa kikundi ili wajitolee kuwajibika kwa kina sana.
Kuongoza Njia
Kiongozi lazima awe mfano wa kuigwa—kwanza kwa kundi la ndani la watu waliojitolea kwa maono na maadili ya shirika, kisha kupanua wigo. Ni jukumu lake kusaidia kuunda kikundi kinachoonyesha jinsi maono yanavyotekelezwa katika maisha halisi.
Kuwaita Watu Wengine Kufuata.
Kiongozi atawaalika watu wengine wafuate maono. Atafanya hivyo kwenye mahusiano binafsi, kwa kutoa ushauri kwa watu binafsi, kwa kufundisha, na kwa kuwaalika watu wachukue majukumu.
Kuwawezesha Wale Watu Watakaofuata
Kiongozi wa kweli hutoa majukumu kwa watu wengine. Hukubaliana na hali za uthubutu, huruhusu ubunifu, na hutengeneza nafasi za uongozi kwa ajili ya watu wengine kwenye kundi.
► Je, unaona kitu gani kwenye mtazamo huu wa uongozi? Je, ni mambo gani yenye nguvu? Je, kuna matatizo gani?
[1]Sherwood Lingenfelter, Leading Cross-Culturally (Ada: Baker Academic, 2008), 117
“Kufanyia kazi mambo matano chini ya hali zote kunajumuisha usafi kamili;
haya mambo matano ni umakini, ukarimu wa nafsi, uaminifu, bidii, na wema.”
- Confucius
Mitazamo ya Kitamaduni ya Kupanda Cheo
Kwenye baadhi ya tamaduni, mtu hupandishwa cheo au daraja la nafasi ya uongozi akiwa amekaa na kushiriki tu kwenye utumishi kwa uaminifu kwa miaka mingi. Viongozi kwenye utamaduni mmoja walisema kwamba walihitaji kumwangalia kiongozi mtarajiwa kwa miaka kumi. Kwenye tamaduni hizi, ni vigumu sana kwa mtu mpya kuweza kupanda hadi kwenye nafasi za uongozi za juu. Wamisionari wakati mwingine hujisikia kuvunjika moyo wanapokuwa wanajaribu kujaza nafasi ya uongozi yenye kuhitaji ustadi au uwezo maalumu, kwa sababu viongozi wenyeji wanataka kumtumia mtu ambaye amejithibitisha mwenyewe na kuwa mwaminifu kwa muda mrefu, badala ya kutumia mtu ambaye ana sifa zinazohitajika kwenye ustadi au uwezo maalumu.
Yoeli alikuwa amefanya kazi ya umishenari kwa miaka mingi kwenye utamaduni ambao mkalimani wake alikuwa tu ni mtu anayefanya kazi. Wakati wote Yoeli alikuwa akijitahidi kupata mtu sahihi atakayeweza kufanya ukalimani vizuri zaidi, hata kama atakuwa hajamjua mtu huyo kwa muda mrefu.
Sasa, Yoeli alikuwa anafanya kazi kwenye utamaduni ambao nafasi ya mkalimani ilikuwa ni nafasi ya juu katika shirika hilo. Viongozi wangeruhusu tu mkalimani ambaye walikuwa wanamjua kwamba ni mwanachama mwaminifu kwa kanisa. Wakati mwingine ilimpasa Yoeli kuhubiri pamoja na mkalimani ambaye hakuwa na uwezo wa kuifanya huduma hiyo vizuri, wakati huo kukiwa na mkalimani mzuri aliyekuwa amekaa tu kwenye kusanyiko bila kutumika.
Baadhi ya tamaduni huheshimu sana umri na uzoefu zaidi kuliko elimu na kipaji. Wamisionari mara nyingi hufundisha vijana kwa sababu ni wenye nia, wako tayari kubadilika, na ni wepesi kufundishika kuliko wazee. Hata hivyo, takribani katika tamaduni nyingi, makanisa yatapingana na uongozi mchanga kwa sababu hiyo inaonekana ni kutowaheshimu viongozi wazee au wa zamani. Viongozi wazee wanapaswa wajaribu kuachilia madaraka kwa viongozi wachanga na kuruhusu timu ya uongozi kupanuka.
► Je, ni kwa jinsi gani mafunzo yanaweza kufanywa kwa njia inayoheshimu umri na uzoefu?
Maoni ya Kitamaduni ya Vyeo vya Mamlaka.
Je, kiongozi anachaguliwa vipi? Je, kiongozi anatunzaje nafasi yake? Kuna mitazamo miwili iliyo kinyume ya kitamaduni kuhusiana na hadhi ya kiongozi.
Mtazamo wa kwanza wa kitamaduni:
Kiongozi anapewa nafasi yake kwa sababu ya uwezo wake na tabia yake. Anaweza akachaguliwa na watu anaowaongoza. Ataendelea kutumikia kama kiongozi kwa sababu anaongoza vizuri. Hana mamlaka yatoe kamili lakini anawajibika kwa kikundi fulani. Ikitokea akawa mdhaifu kimwili hata kushindwa kuendelea kufanya kazi, atategemewa ajiuzulu. Kama hatakuwa anaongoza vizuri inavyotakiwa, anaweza akaondolewa na akawekwa mtu mwingine kwa njia ya kufanya uchaguzi wa kupiga kura. Kama akifanya vitendo vya kifisadi au tendo lolote la kuvunja heshima, haonekani tena kwamba anafaa kuendelea kuwa kiongozi, hasa kwenye shirika la Kikristo.
Mtazamo wa pili wa kitamaduni:
Katika aina nyingine ya utamaduni, kiongozi hupewa nafasi yake kwa sababu amekuwa sehemu ya shirika kwa muda mrefu na anajulikana kwa uaminifu wake. Anateuliwa na wachache wenye mamlaka. Ikiwa kuna uchaguzi, si wa kweli; watu hupiga kura kwa mtu ambaye wanajua tayari ameidhinishwa na wenye mamlaka. Hatimaye, hupata mamlaka karibu yote. Anaweza kusikiliza ushauri, lakini maamuzi yake hayawezi kupingwa.
Baada ya kuwa kiongozi kwa miaka mingi, nafasi yake haiwezi kutegemea jinsi anavyoongoza. Yuko nje ya uwajibikaji wa kawaida na hategemei kuulizwa maswali kuhusu matendo yake. Hata vitendo vya kinyume na maadili au udanganyifu vinaweza visiwe sababu ya kumuondoa madarakani. Hata anapozeeka au anapougua kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yake, anaweza kuendelea kushikilia nafasi yake, hata kama hatimizi majukumu yake mara kwa mara. Wafuasi wake hawatamwondoa madarakani isipokuwa katika hali za nadra sana ambapo anapoteza kabisa heshima na uaminifu.
Kwa utamaduni huu, uhamishaji wa madaraka kutoka mtu mmoja kwenda mwingine haufanyiki kwa amani labda iwe kiongozi kwa hiari yake mwenyewe awe amepitisha nafasi hiyo ichukuliwe na mrithi wake. Kama kikundi kitataka kumwondoa kiongozi bila hiari yake mwenyewe, matokeo yake yanaweza yakawa ni mashitaka, kukataa kushirikiana, hatua za kisheria kuchukuliwa, migogoro ya hadharani, na hatari ya kugawanyika kwa shirika. Kwa masikitiko makubwa, mashirika ya huduma yamekuwa mara nyingi yakifuata mfano huu wa utamaduni na yamekuwa yakiharibu sana ushuhuda wao wa Ukristo
Yohana aliliongoza kanisa kwa miaka mingi. Alipofika kwenye umri wa uzee wake hali yake ya afya ilikuwa mbaya. Aliondoka kwenda kwenye jiji lingine, na kanisa likaongozwa na waliokuwa wachungaji wasaidizi watatu. Yohana aliendelea kushikilia uongozi wa kanisa, ingawaje alikuwa akienda mara chache sana kwenye kanisa hilo.
Anasi alikuwa kuhani mkuu katika Yerusalemu. Baada ya kujiuzulu, kuhani mkuu mpya alikuwa ni Kayafa, aliyekuwa mkwe wake. Anasi aliendelea kuwa ndiye mamlaka ya juu, ingawaje alikuwa hana nafasi rasmi tena. Wakati Yesu alipokamatwa, askari hawakumpeleka kwanza kwa Kayafa bali kwa Anasi (Yohana 18:12-13, 24).
Wakati mwingine Wamisionari kutoka katika tamaduni nyingine hujitaabisha kupata dhana ya mamlaka iliyoko kwenye shirika. Wanashindwa kuelewa ni kwa nini mtu abakie kwenye nafasi ya mamlaka wakati hawezi kuendelea kufanya kazi. Hawaelewi ni kwa nini mabaraza na kamati zenye mamlaka hufuata maamrisho kutoka kwa kiongozi wa juu.
Kiongozi anayehudumu kwenye utamaduni mwingine ni lazima atumie muda wake kujifunza ni kwa jinsi gani maamuzi yanafanywa kwenye utamaduni huo. Kamwe haitoshi tu kupata watu wengi kwa ajili ya kupigia kura kitu fulani. Kupiga kura kunamaanisha kwamba kila wazo la mtu lina haki sawa, jambo ambalo kwa kweli hakuna mtu anayeamini. Baadhi ya watu wana ushawishi mkubwa kwenye shirika zima, na haja zao ni lazima zitekelezwe kabla shirika halijaweza kufanya maamuzi.
Umbali wa Mamlaka
Katika tamaduni zingine, viongozi hujaribu kujenga mahusiano na watu kwenye ngazi zote za shirika hilo. Mmiliki wa anaweza kutembea kwenye kiwanda akifanya mazungumzo na wafanyakazi na akijaribu kukumbuka majina yao. Kiongozi anapaswa asaidie kupakua mizigo kwenye gari la mizigo au afanye usafi wa jengo.
Katika tamaduni zingine, kiongozi anachukuliwa kuwa mbali na watu wengi wa shirika. Hawatarajii kama wanaweza kuzungumza naye moja kwa moja. Hawaoni kama ni jambo linalofaa kwake kufanya kazi yeyote inayoonekana ni duni kwake. Ikiwa atafanya mazungumzo na wao, wanaweza kufurahishwa na usikivu wake kwao, au wanaweza wakajisikia kuwa na wasiwasi sana.
Duane Elmer alikuwa anatumika kama mkuu wa shule ya Biblia kwenye nchi ya kigeni. Siku moja Jumamosi mchana, aligundua kwamba majani yalikuwa hayajakatwa, kwa hiyo akaamua kuifanya kazi hiyo yeye mwenyewe. Alikuwa na mategemeo kwamba kitendo chake hicho kingelisababisha kujenga unyenyekevu na kuwavutia waliokuwa wakimwangalia katika kujitolea kwake kufanya kazi kwa hiari. Hata hivyo, wakati wanafunzi na wafanyakazi walipoona hivyo, walifadhaishwa. Walisema kwamba kitendo chake hicho kitawafanya watu wafikirie kwamba muundo wa mamlaka ya shule ulikuwa mdhaifu sana kiasi kwamba mkuu wa chuo hakuwa na uwezo wa kumwagiza mtu yeyote akate majani. Ilimaanisha pia kwamba shirika lilikuwa dogo na lisilokuwa na umuhimu kwa sababu mkuu wa chuo ilibidi afanye kazi iliyo duni sana. Alijitahidi sana kufanya mambo yaonekane mazuri zaidi kwenye miezi mingine michache iliyofuata kwa kusimama nje kama mtu mwenye mamlaka akiangalia watu jinsi wanavyofanya kazi.[1]
Wamisionari Wamarekani waliokuwa katika ziara walikuwa wakila kwenye nyumba ambayo wanawake wawili walikuwa wameajiriwa kupika. Wamarekani walisisitiza kwamba wapishi hao wakae mezani ili wale pamoja nao. Walibishana hadi mwishowe wale wanawake wakawakubalia kukaa pamoja nao mezani, lakini wanawake wakawa na wasiwasi mwingi na hawakula kitu chochote.
Viongozi wa Kikristo wanaofanya kazi kwenye utamaduni mwingine ni lazima wawe waangalifu sana kutumia kanuni za Kikristo kwenye utamaduni. Tunajua wazi kwamba hadhi ya mifumo ya kidunia haipaswi iwe inafuatwa katika kanisa (Wagalatia 3:28). Hatupaswi tuwatendee watu wengine vizuri zaidi kuliko wengine kwa sababu ya utajiri wao au nafasi zao (Yakobo 2:1-4). Yesu alisema kwamba kiongozi anapaswa kuwa tayari kutumika hata kwenye kazi ya chini kabisa (Yohana 13:14-16). Mara nyingi Yesu aliwashangaza watu wakati alipoacha kutumia desturi zilizohusu hadhi (Yohana 4:9, Luka 18:15-16).
Wamisionari wanapaswa wawe kielelezo cha upendo na heshima kwa watu wote, na kuwa tayari kutumikia. Hata hivyo, wanapaswa wawe na huruma na mahitaji halali ya watu kwenye utamaduni. Wanapaswa waonyeshe kwamba wanaheshimu desturi zilizopo na kwamba hawatasababisha uvurugaji.
Musa alikuwa na nafasi ya kuwa mtawala katika taifa lililokuwa na nguvu sana duniani kwa wakati ule (Misri). Badala yake, alichagua kujitambulisha na taifa la watumwa (Waebrania 11:25). Wakati akifanya maamuzi haya, hakuwa amejua kwamba Mungu atakwenda kumfanya mmoja wa viongozi wakubwa sana wa wakati wote. Ataliongoza taifa la watumwa hadi kwenye uhuru, akiliongoza taifa kupita katika taifa katili la adui kwa miaka 40, akitoa taratibu za sheria, ambazo zingeshawishi mataifa yote yaliyoendelea baada ya hapo, na kuanzisha aina ya ibada ambayo ilidumu kwa karne nyingi na iliyoandaliwa kwa ajili ya Ukristo.
Uamuzi mkubwa wa Musa alioufanya ni kujitambulisha na watu wa Mungu, akizikataa dini za uongo na starehe za maovu za Misri. Kama angekuwa amefanya maamuzi mabaya, kamwe hangekaa awe mtu muhimu sana kwenye mpango wa Mungu.
Musa alijifunza masomo mengi sana. Alijifunza kumsikiliza Mungu kabla hajategemea watu wamsikilize yeye. Ingawaje alikuwa mkuu sana, alikuwa mnyenyekevu kwa sababu ya kuwa tegemezi kwa Mungu peke yake. Nia yake ya kumfahamu Mungu (Kutoka 33:18) ilimpa kibali cha kuzungumza kwa ajili ya Mungu. Alisisitiza kwamba Israeli haikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote pasipo uwepo wa Mungu (Kutoka 33:15). Alitambua kwamba uongozi wake haukuwa kwa kusudi la kujitukuza yeye mwenyewe.
Musa aliwapenda watu aliowaongoza. Wakati mmoja, Mungu alitishia kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, akimpa Musa nafasi ya kuwa kiongozi mkuu wa watu wengine. Hata hivyo, Musa alisema kuwa angependa ahukumiwe badala ya Israeli kuliko kuwa kiongozi mkubwa bila wao (Kutoka 32:32). Ikiwa kiongozi anaweza kuwaacha watu wake kwa urahisi kwa nafasi nyingine mahali pengine, basi hana moyo wa uongozi kama wa Musa.
Waamerika hupenda kudhania kwamba tuzo binafsi na kupewa heshima ndiyo vichocheo vizuri zaidi, ili kwamba mtu aweze kuvipata kwa juhudi zake mwenyewe. Hata hivyo, tamaduni nyingi huamini kwamba tuzo za mafanikio zinatakiwa ziwe ni za kikundi. Wanaweza wakakasirika na kumzuia mtu anayejaribu kuyafikia malengo yeye mwenyewe. Hawataki mafanikio ya mtu binafsi yapewe heshima.
Wajapani wana msemo usemao: “Msumari unaong’ang’ania mahali utang’olewa kwenda chini.” Hii ikimaanisha kwamba mtu hapaswi kujaribu kujitafutia umakini kwa ajili yake mwenyewe badala ya kufanya kazi na kikundi.
Kiongozi anayefanya kazi kwenye utamaduni mwingine anapaswa aelewe huo mtazamo wa malengo na tuzo. Huenda ikawa tuzo zinapaswa zitolewe kwa vikundi vinavyoweza kufikia malengo kama timu.
Kuepuka Ushindi wa Kitamaduni
Mara nyingi injili haikupelekwa kwenye utamaduni mpya kwa njia iliyoonyesha heshima kwa utamaduni huo. Injili iliwasilishwa kama ujumbe kutoka kwa utamaduni wa hali ya juu zaidi, vielelezo vya kitamaduni vikiwa vimeambatanishwa. Kwa watu wengi waliofikiwa na huduma ya uinjilisti, kukubaliana kwao na injili kulimaanisha kwamba walijisalimisha pia kwenye utamaduni wa kigeni.
Neno Ushindi wa Kitamaduni ni wa maana. Ushindi wa kitamaduni hauna maana tu kwamba utamaduni umeazima mambo mengine kutoka kwenye utamaduni mwingine. Ushindi wa kitamaduni hutokea wakati watu wengi wanapoona utamaduni wa kigeni kama ulio bora zaidi kuliko utamaduni wao na kujaribu kuufuata. Vijana haswa hujaribu kuigiza utamaduni wa kigeni kwenye mavazi, sauti, na maadili. Vijana wanapenda majukumu ambayo yalikuwa hayajawahi kuwepo tena kabla, kama vile kazi ya ukalimani ili waweze kufanya kazi na viongozi wapya au wageni.
Kwenye mazingira ambayo utamaduni unapokonywa au unachukuliwa na utamaduni mwingine, nafasi za awali za mamlaka na ushawishi zinafifishwa. Kwenye mazingira yanayobadilika kwa haraka, vijana wana manufaa na heshima kwa ajili ya kupungua kwa umri. Desturi za zamani zinakataliwa na kizazi kipya. Vijana wana shauku kidogo sana katika historia na alama za utamaduni za watu wao kwa kuwa wamepoteza ile heshima iliyokuwepo kwa ajili ya utamaduni wao wenyewe.
Wamisionari hawana chaguo la kuzuia uvamizi wa kitamaduni isipokuwa wawe wageni wa kwanza kuathiri utamaduni wa asili. Katika maeneo mengi, maslahi ya kibiashara ya kigeni tayari yameanza uvamizi wa kitamaduni.
Kwa bahati mbaya, wamisionari wengi wamehusika katika uvamizi wa kitamaduni na kuuleta ndani ya kanisa. Kazi ya umisionari ni kupanda maudhui ya wenyeji ya kanisa la kibiblia. Kanisa la wenyeji linajitegemea, linajiendesha lenyewe, na linajieneza lenyewe.
Maendeleo ya wenyeji hukwamishwa na:
Sera zinazoamuliwa kutoka mbali
Utangulizi na mwendelezo wa tamaduni za kigeni
Uongozi wa wageni
Michakato ya maamuzi isiyoendana na mazingira ya wenyeji
Matumizi ya fedha kwa njia ya udanganyifu au shinikizo[1]
Wamisionari wa kigeni mara nyingi huja na rasilimali na vifaa ambavyo viongozi wa shirika wa kitaifa hawako navyo. Mmisionari anayewajibika na kuanzisha au kupanda kanisa hapaswi awe ndiye mchungaji wa kanisa jipya. Kama mmisionari ndiye mchungaji wa kwanza wa kanisa, matumizi yake na utoaji wake vitaleta jukumu ambalo mchungaji wa kitaifa hatakuwa na uwezo wa kulitekeleza.
Mmisionari anapaswa kuonekana kila wakati kama mgeni anayejaza nafasi ya kipekee na ya muda mfupi. Anapaswa kutoa mafunzo ya ziada kwa watu wa eneo hilo wanaoonyesha ukuaji wa kiroho na kujitoa kwa Bwana, na mmoja wao anapaswa kuwa mchungaji wa kanisa jipya.
Wachungaji wa mtaa wanapaswa wapewe msaada na wenyeji wa maeneo hayo, na kwa kazi zao wenyewe ikiwa itabidi iwe hivyo. Kama watakuwa wakipewa msaada na wageni, kusanyiko la mtaa kamwe halitakaa lione wajibu wao kifedha au kuwajibika. Watakuwa wanafikiri kwamba kanisa ni mali ya shirika la nje na siyo kwa ajili yao.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha makusudi au matendo yao kutokana na somo hili.
[1]Ripoti ya Willowbank: Consultation on Gospel and Culture "Lausanne Occasional Paper 2" (1978). Imenukuliwa kutoka https://www.lausanne.org/content/lop/lop-2 on March 14, 2020.
Kazi za kufanya Somo la 14
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha makusudi yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Fanya kukariri ufafanuzi wa uongozi wa utamaduni unaoingiliana kutoka katika mwanzo wa somo hili. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.