Kikundi cha vijana kinacheza kwa pamoja. Yohana anasema, “Nyie, tucheze mpira.” Inaonekana hakuna anayeonyesha kuwa na taarifa kwamba Yohana amezungumza. Kisha Thomasi akasema, “George, nenda ukalete ile miti, na tutacheza kama sisi ni wanajeshi.” George akaenda kuchukua ile miti, na wale vijana wakaanza kujipanga kucheza kana kwamba wao ni jeshi.
► Je, ni nani kiongozi katika kikundi hiki, Yohana au Thomasi? Kiongozi ni nani? Kwa nini tunaweza kusema kwamba uongozi siyo lazima umaanishe ni nafasi ya mamlaka?
Tafsiri ya Uongozi
Wakati mwingine mtu aliyeko kwenye nafasi fulani ya mamlaka siyo kwa uhalisia awe kwamba ndiye mtu aliye katika utawala wote. Wakati mwingine mtu ambaye hayuko kwenye nafasi rasmi ya mamlaka ndiye unayekuta kwamba watu wanamfuata yeye. Hii ina maana kwamba uongozi ni zaidi ya kuwa kwenye nafasi.
Kiongozi ni mtu ambaye watu wanamfuata yeye.
Uongozi ni ushawishi.
Wakati wowote unapojikuta unajaribu kushawishi mawazo na matendo ya watu wengine katika kukamilisha lengo aidha kwenye maisha yao ya kawaida ya binafsi au ya kitaaluma unajihusisha na uongozi.[1]
Baadhi ya mpangilio wa matukio ya kawaida
Meneja wa kiwanda anatangaza kanuni mpya. Anapokuwa ameondoka, mmojawapo wa wafanyakazi anawaelekeza wafanyakazi wenzake ni jambo gani hasa wanalotakiwa walifanye.
Kikundi cha watu kinasafiri kwa pamoja kwenye basi la abiria. Kisha linapata hitilafu. Mtu mmoja anatoka nje ya gari kwa ajili ya kutafuta njia nyingine mbadala ya kuendelea na safari.
Mchungaji anawaelezea kundi la waumini wake kile ambacho anafikiria kwamba kanisa linaweza kufanya. Waumini wanamsikiliza lakini hawatoi majibu ya uhakika. Wanamsubiri mtu fulani ambaye bado hajafika ili aje awaambie ni nini wanachotakiwa wakifanye.
Katika kila kipengele kilichoainishwa hapa, ni nani kiongozi? Ni yule ambaye watu wameamua kuchagua kumfuata.
Hapa bado tunafafanua kuhusu uongozi. Bado hatujaanza kufafanua kiongozi mzuri ni nani au kiongozi aliye na matokeo mazuri ya muda mrefu ni yupi. Matendo ya kiongozi yanaweza yakawa mazuri au mabaya na yanaweza pia kuwa na matokeo mazuri au mabaya. Mtu anaweza akawa ni yule kiongozi ambaye watu humfuata kwa haraka, lakini akawa siyo mtu anayekamilisha matumaini yao. Anaweza akawa na mfumo ambao mara nyingi huwavutia wafuasi wengi wapya lakini kwa muda fulani mfupi akawa amewapoteza.
Kama mtu akifanya kitendo cha uamuzi na watu wakafuata, yeye ni kiongozi kwa wakati ule. Mtu anaweza akawa ni kiongozi kwa wakati mmoja na siyo kwa watu wengine. Anaweza akaongoza kwenye mazingira kadhaa na siyo wengine kwa sababu ya vipaji maalumu.
Endapo kama tutafafanua uongozi kwamba ni ushawishi, Yesu alikuwa kiongozi mkuu kuliko wote kwa wakati wote. Mamilioni ya watu wanafuata mafundisho yake. Taasisi mbalimbali zimesheheni dunia nzima kwa makusudi ya kutii maagizo yake.
Yesu alifafanua uongozi kama ni huduma (Mathayo 20:25-28). Kwa ufafanuzi huu pia, Yesu alikuwa kiongozi mkuu kuliko wote kwa wakati wote kwa kuleta ukombozi au wokovu.
[1]Ken Blanchard and Phil Hodges, The Servant Leader: Transforming Your Heart, Head, Hands, and Habits (Nashville: Thomas Nelson, 2003), 10
Uongozi ni zaidi ya kuwa kwenye nafasi.
Kuwa kwenye nafasi fulani rasmi kunakupa wewe haki ya kutumia madaraka yake, lakini haikufanyi moja kwa moja kuwa kiongozi.
Usijaribu kudhania kwamba unaongoza kwa sababu tu umeshikilia nafasi ya madaraka, hasa unapokuwa hujawekwa kwenye nafasi hiyo na watu unaojaribu kuwaongoza. Nafasi ya madaraka inakupa wewe nafasi ya kuja kuwa kiongozi, Nafasi ya madaraka, kama yenyewe ilivyo, haikufanyi kuwa kiongozi.
► Fafanua kauli hii: “Nafasi ya madaraka ni mlango tu wa uongozi.”
Wakati mtu anapowaambia watu anaowaongoza kwamba: “Mimi hapa ndiye bosi” au “mimi hapa ndiye mchungaji,” mara nyingi hutoa kauli hii kwa sababu watu hawakubaliani na mamlaka yake. Anayo nafasi ya madaraka, lakini watu hawafuati. Anakuwa akijaribu kuweka shinikizo la mamlaka ya nafasi yake aliyo nayo kwa sababu ushawishi wake hauna uzito wa kutosha.
► Je, kauli hii inamaanisha nini: “Kamwe hupaswi kuhitajika kuwakumbusha watu kwamba wewe ndiye kiongozi wao”?
Samweli alikuwa ni nabii na kuhani mkuu kabla ya kuwepo kwa mfalme katika Israeli. Alitumika kama mwamuzi kwa ajili ya watu. Watoto wake hawakufuata mfano wake wa utauwa: kwa hiyo wakati Samweli alipofikia kwenye uzee wake, watu walikuja kwake wakimtaka awape mtu atakayekuwa mfalme wao (1 Samweli 8:5).
Hapa tunauona ushawishi wa Samweli kwa ukweli kwamba watu walijua kwamba ni yeye peke yake anayeweza kumchagua mfalme. Hawakujaribu kutaka kumchagua mfalme kwa njia nyingine yeyote. Alipowaambia kwamba Sauli ndiye angefaa kwenye nafasi hiyo, siyo kila mtu alimkubali Sauli: lakini kulikuwa hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa na ushawishi wa kutosha wa kuweza kumfanya mtu awe mfalme.
Ushawishi wa Samweli ulikuwa na msingi wake kwenye muda mrefu wa maisha yake wa kudhihirisha hekima na tabia. Watu waliwakataa watoto wa Samweli kwa sababu watoto hawakudhihirisha tabia ya baba yao. Hakuna kiwango chochote cha uwezo kinachoweza kuwa mbadala wa tabia.
Uongozi ni zaidi ya Uzalishaji
[1]Mzalishaji ni mtu ambaye anafanya kazi vizuri sana na anayekamilisha malengo kwa juhudi zake. Mzalishaji ni mtu wa thamani sana. Kila shirika ni tegemezi kwa wazalishaji wake.
Kiongozi ni mtu anayefikiria ni nini kinachoweza kufanyika kwa kuwashawishi watu wengine kufanya kazi kwa pamoja. Kama kiongozi ataweka fokasi yake zaidi kwenye kuwa mzalishaji, atakuwa hakamilishi jukumu lake la kuongoza. Kazi yake haipo tu katika kufanya kazi nzuri, bali pia kuwaongoza watu wengine katika kufanya kazi nzuri kwa pamoja.
Wazalishaji
Viongozi
Mzalishaji hujisikia kuwajibika kwa juhudi ya kazi yake mwenyewe.
Kiongozi hujisikia kuwajibika kwa ajili ya yale yanayofanywa na watu wengine, kwa sababu anajijua kwamba ana uwezo wa kuwashawishi.
Mzalishaji huweka nguvu zake zote katika kukamilisha jukumu analolifanya.
Kiongozi huweka kwa pamoja juhudi zake mwenyewe na juhudi za watu wengine katika kukamilisha jukumu.
Mzalishaji hujiongeza hatua kwa hatua katika kukamilisha majukumu yake.
Kiongozi hujiongeza katika ukamilishaji wa majukumu yake akiwa pamoja na timu yake.
Kama utakuwa unafanya kazi kubwa zaidi inayofanywa na shirika lako, utakuwa unashindwa kuwaongoza watu wengine kama ambavyo ungetakiwa ufanye. Kama kila wakati wewe ni mtu uliye na mishughuliko mingi kwa ajili ya shirika, utakuwa na uwezekano mkubwa wa kushindwa kuongoza.
► Jaribu kupima shughuli na malengo ya kazi yako. Je, unajiona unazo tabia za aina gani zinazohusiana na mzalishaji? Je, unajiona unazo tabia za aina gani zinazohusiana na kiongozi?
Watu wengi hawaelewi ni kwa jinsi gani kiongozi anautumia muda wake. Kama atakuwa anaongoza shirika kubwa, anaweza akawa na majukumu machache maalumu ya kufanya.
Kwa mfano, jaribu kufikiria kuhusu meneja mkuu wa biashara kubwa. Yeye haajiri wafanyakazi wengi, kwa sababu atakuwa amekabidhi jukumu hilo kwa mtu mwingine. Hashughuliki na kuendesha mashine. Hawajibiki na kununua mali ghafi au vifaa. Hafanyi matengenezo ya majengo. Yeye siyo muuzaji wa bidhaa zinazozalishwa. Kwa watu walio wengi, inawezekana ikaonekana kwamba yeye ni mtu wa kutembea tu huku na huko akipiga simu na kufanya vikao. ikiwa angeondoka kwenye biashara kwa siku chache, ingeendelea vizuri asipokuwepo yeye.
Kwa mfano, fikiria meneja mkuu wa biashara kubwa. Haajiri wafanyakazi wengi, kwa sababu amempa mtu jukumu hilo. Hatumii mitambo. Yeye hanunui vifaa. Hatengenezi jengo. Yeye hauzi bidhaa. Kwa watu wengi, inaweza kuonekana kwamba anatembea tu na kupiga simu na kufanya mikutano. Ikiwa angeacha biashara kwa siku chache, ingeendelea vizuri bila yeye.
Lakini meneja mkuu ndiye anayeona jinsi utendaji na uendeshaji unavyohusiana. Atawaweka mameneja wasimamizi kwenye nafasi za idara mbalimbali akihakisha kwamba wana uwezo wa kuzifanya kazi zao. Atasimamia ubora wa jumla wa biashara na kumsaidia kila mtu kuelewa ni jambo gani lililo muhimu. Ataanzisha mifumo ambayo italeta matokeo ya uzalishaji endelevu. Ataboresha hali ya biashara. Pasipo yeye, kwa ukweli biashara itaanguka.
Katika shirika dogo, kiongozi atapaswa awe tayari kufanya lolote litakalotakiwa lifanyike. Hata hivyo, atapaswa kila siku atafute watu ambao wamepitia mafunzo, watakaowajibika na watakaofanya kwa hiari.
Kwenye shirika ambalo linabadilika, kiongozi anaweza kuhitaji kuhusishwa kwenye kila kazi ya idara ili kuhakikisha kwamba watu wote wanaelewa kuhusu mabadiliko hayo. Hata hivyo, itabidi awe anawaendeleza watu wa kuongoza idara mbalimbali pasipo yeye kuhusika moja kwa moja.
Mchungaji anapaswa awe tayari kuhudumia mahitaji ya watu wake na hatapaswa kuliona jukumu lolote kwamba ni dogo kulingana na hadhi yake. Hata hivyo, ni lazima awaongoze watu wengine katika kuyakubali majukumu na kuchukua uongozi kwenye programu za kanisa. Ikiwa mchungaji hataweza kufanya haya, huduma haitaweza kukua Zaidi ya kazi ambayo anaweza kufanya yeye bin afsi.
► Je, itakuwa inamaanisha nini kwa kiongozi kuwa “mwenye shughuli nyingi sana katika kuongoza”?
“Kiongozi mkuu na maarufu sana siyo lazima awe ndiye anayefanya mambo makubwa sana. Yeye ndiye anayeweza kuwafanya watu watende mambo makubwa sana.”
- Ronald Reagan
Tabia za Kiongozi
Tumefafanua hapa kuhusu uongozi katika hali yake ya msingi kama ushawishi. Kiongozi ni mtu ambaye watu humfuata. Hata hivyo, kama mtu ataendelea kuwa kiongozi wa kikundi au shirika, angalao tabia nyingine nne zinatakiwa pia ziwepo:
(1) Kiongozi ana mamlaka.
Mamlaka maana yake ni kwamba watu wengine wanakubali kuwa chini ya nia yake, aidha kwa hiari au kwa njia isiyokuwa ya hiari. Mtu yeyote ambaye watu wanamfuata kwa hiari yao wanakuwa wenye nguvu, kwa sababu watu wanaolazimishwa kuwa chini ya nia ya mtu mwingine watafanya mambo kiasi kidogo kama watakavyoweza. Watu wanaolazimishwa kuwa chini ya mtu mwingine hawatatumia vipaji vyao na ubunifu wao katika kukamilisha malengo.
(2) Kiongozi ana jukumu la kufanya.
Ni mtu anayetegemewa awe na elimu, vipaji, na mbinu ambazo ni muhimu kwa ajili ya kikundi kufanikiwa. Kama kikundi hakitakuwa na mafanikio, kiongozi hulaumika. Kiongozi hawezi akawa mtu mwenye kutoa visingizio kwa ajili ya kushindwa na kulaumu wenzake. Hawezi akawa ni mtu ambaye anataka watu wengine wawe wanafanya maamuzi ili asije akalaumika kwa matokeo yeyote.
Pointio Pilato alikuwa gavana wa Kirumi katika nchi ya Yuda. Alikuwa ameteuliwa kutawala na kugandamiza mageuzi. Wakati wa uongozi wake, Pilato alifanya makosa. Alikuwa na wasiwasi kwamba utawala wa Roma haungekubali kuthibitisha utawala au uongozi wake.
Wakati Yesu aliposhutumiwa kwamba yeye alikuwa mwasi, Pilato hakuamini kwamba Yesu alikuwa na hatia. Hata hivyo, viongozi wa Kiyahudi walionyesha kwamba wangelimfitini Pilato kwa kushindwa kumhukumu Yesu kwa ajili ya kuwa mwana mapinduzi (Yohana 19:12).
Pilato alijua wazi kwamba angekuwa kwenye matatizo makubwa sana kama angefitiniwa kwa utawala wa Roma. Kwa hiyo, aliamua kumtoa kafara mtu ambaye hakuwa na hatia yeyote kwa kuruhusu auawe.
Pilato alijaribu kukana kwamba ilikuwa uamuzi wake. Aliosha mikono yake mbele ya viongozi wa Kiyahudi ili kuashiria kwamba hakuwa na lawama.
Kiongozi hawezi akawa mtu wa kulaumu watu wengine kwa maamuzi ambayo ni lazima ayafanye. Endapo kama ataruhusu watu wengine wafanye maamuzi kwa ajili yake, bado yeye atakuwa ni mtu wa kulaumiwa.
Kiongozi anaweza akanaibisha mamlaka takribani majukumu yote muhimu kwa watu wengine, lakini hawezi akanaibisha jukumu lake la mwisho kwa ajili ya mafanikio ya shirika. Kiongozi hawezi akawalaumu watu wengine kama shirika linaelekea kushindwa. Kiongozi analo jukumu la mwisho kwa ajili ya kila idara katika shirika.
Mchungaji alipokea malalamiko mengi kuhusu mtindo wa muziki kanisani mwake. Alisema haikuwa kosa lake kwa sababu suala la uchaguzi wa muziki ilikuwa ni jukumu la mtu aliyekuwa kiongozi wa ibada. Mchungaji Alikosea kwa kukataa uwajibikaji huo kwa sababu ilikuwa ni jukumu lake kumwongoza na kumsimia kiongozi wa ibada.
(3) Kiongozi anapaswa kuwajibika kwa watu anaowaongoza.
Uongozi wake unategemea uungwaji mkono na watu wengi. Kama uongozi wake hauna matokeo mazuri anapoteza ushawishi. Hata kama ataendelea kuwa kwenye nafasi yake ya uongozi, inawezekana watu wakawa wanamfuata mtu mwingine na siyo yeye.
► Je, itakuwaje kama kiongozi atatumia mamlaka yake lakini hajaribu kuhusika au kuwajibika?
(4) Kiongozi ana mtazamo mpana.
Kiongozi hawezi kuruhusu mafanikio madogo au kushindwa kumwondoa kwenye lengo lake kuu. Hapaswi kuruhusu kuchanganyikiwa kuwe ni kigezo cha kumkatisha tamaa. Ni mtu aliye tayari kujitoa dhabihu. Kama atakuwa mtu wa majivuno sana au asiyekuwa madhubuti katika kufanya mambo ya kujitoa dhabihu, hataweza kuendelea kuwa na mafanikio mkubwa.
Taifa lilikuwa likijilinda dhidi ya jeshi linalovamia. Mfalme alikuwa ametawala kwa miaka mingi na alipendwa na kuaminiwa na watu wake. Alipokea ujumbe kutoka kwa jenerali wa jeshi linalovamia. Jenerali alimpa changamoto mfalme aende kupigana naye binafsi pamoja na wanawe watatu dhidi ya yeye na watu wake mwenyewe watatu. Jenerali alisema kuwa mfalme atakuwa mwoga endapo hangekubaliana na changamoto hiyo.
Mfalme alihisi kwamba itakuwa ni fedheha ikiwa hangekubali changamoto hiyo. Alidhani alipaswa kuthibitisha ujasiri wake. Yeye na wanawe walikutana na maadui kupigana kwenye eneo la darajani. Katika pambano hilo, mfalme na wanawe waliuawa.Taifa liliachwa bila uongozi na likatekwa na wavamizi
Mshairi mmoja kutoka katika taifa lililoshindwa alihuzunishwa sana na kitendo cha kumpoteza mfalme na kupoteza uhuru wao. Alisema kuwa mfalme amefanya makosa kuongozwa na kiburi. Mfalme hakuwa na haki ya kuhatarisha taifa lote kwa ajili ya kiburi chake mwenyewe. Jukumu la mfalme lilikuwa ni kuliongoza taifa. Alipoondoka kwenda kupigana mwenyewe, aliliacha jukumu lake la kuongoza.
► Je, mshairi alikuwa na haki ya kusema kwamba mfalme alikuwa amekosea?
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili. Siyo lazima kwa wanafunzi wote kujibu swali. Usimpe shinikizo mwanafunzi kujibu maswali ya binafsi yaliyo nje ya uwezo wake. Kazi ya kufanya ya 2 inawapa nafasi ya kufikiri zaidi na kuandika maoni yao.
Muhtasari wa Taarifa Tano.
1. Kiongozi ni mtu ambaye watu wengine wanamfuata.
2. Uongozi ni ushawishi.
3. Kushikilia nafasi ya uongozi ni mlango wa kuwa kiongozi.
4. Kiongozi hawezi akawa tu ni mzalishaji.
5. Uongozi unahitaji mamlaka, kuhusika, kuwajibika, na mtazamo mpana.
Kazi za Kufanya ya 1
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Fanya kukariri Taarifa Tano kwa Muhtasari zilizoko katika somo la 1. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
4. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa soma 1 Timotheo 3:1-13, Tito 1:5-11, na Matendo 6:1-6. Andika baadhi ya mambo ya uchunguzi yanayohusiana na sifa kwa ajili ya uongozi wa huduma.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.