Utambulisho wa Shirika na Kusudi
Mashirika mengi, ikiwa ni pamoja na makanisa, kamwe hayajawahi kupitia katika mchakato wa kufikiri juu ya lengo lao kwa sababu inaonekana kwamba lengo lao ni dhahiri. Kwa kuwa wanaamini katika lengo lao, inaonekana dhahiri kwamba wanapaswa wafanye baadhi tu ya shughuli. Malengo yao, ni kufanikiwa tu katika shughuli hizo.
Wasimamizi au mameneja hujaribu kusimamia kazi zifanyike vizuri, lakini viongozi wanapaswa kufikiri juu ya kazi gani ambayo inahitajika kufanyika. Ni vizuri kufanya mambo vizuri na kwa usahihi, lakini kwanza ni lazima tuweze kufanya mambo yaliyo sahihi. Mchungaji hapaswi kuwa msimamizi au meneja tu, bali anapaswa awe kiongozi.
Kuna mchakato wa maendeleo ambao ni muhimu kwa kila shirika aidha iwe ni huduma, biashara, au aina nyingine yeyote ya shirika.
Kanisa linaweza kudhania liko tu kwa ajili ya kuwa na ibada nzuri, kutunza wanachama wake, na kufanya uinjilisti kwa jamii. Lakini makanisa mengi kamwe hayafanyi mpango wa kuyafanya mambo hayo yatokee kwa makusudi maalumu.
Shirika linapaswa lipitie katika mchakato wa maendeleo ambao unajumuisha pamoja na kujipima-binafsi:
-
Je, ni jambo gani muhimu zaidi kwetu?
-
Je, kwa nini shirika hili lipo?
-
Je, ina maana gani kwetu sisi kufanikiwa?
-
Je, ni mafanikio gani mahususi ambayo tunaweza kupanga kuyafikia?
-
Je, kwa sasa tunaweza kufanya nini ili kufikia malengo yetu?
Maswali haya yanahusiana na hatua tano za kwanza za maendeleo ya shirika. Mchakato wa maendeleo ya shirika una hatua hizi:
1. Maadili
2. Kusudi
3. Maono
4. Malengo
5. Mkakati
6. Hatua
7. Mafanikio
Hatua hizi siyo kwamba ziko tofauti kabisa. Kwa mfano, shirika labda tayari linapanga mkakati na kuchukua hatua hata wakati linapokuwa ndio linagundua maadili yake. Programu na idara mbalimbali katika shirika zinaweza zikawa zinafanya kazi kwenye hatua mbalimbali tofauti za mchakato huu.
Mpangilio ni muhimu kwa sababu kila hatua huathiri hatua nyingine inayofuata. Mabadiliko katika hatua yeyote yatasababisha mabadiliko kwenye hatua zinazofuata. Kwa mfano, kama shirika litabadili ufahamu wake wa kusudi lake, litakuwa limebadili pia malengo yake na ufafanuzi wake wa mafanikio.
Mchakato hautokei kwa mara moja tu. Maadili na kusudi havipaswi kubadilika baada ya kuwa vimeeleweka vizuri, lakini vitu vingine vyote vinaweza vikabadilika. Aidha kama malengo yamefikiwa au laa, malengo mengine mapya ni lazima yawekwe. Baada ya kufanikiwa au kushindwa, shirika linapaswa kuangalia tena maadili na kusudi lake, kufafanua maono yake, kuweka malengo mapya, kutengeneza mkakati mpya, na kadhalika. (n.k.)
► Je, ni kwa nini mashirika mengi kamwe hayatoi ufafanuzi wa malengo yao?
[1]Hatua ya 1: Kugundua Maadili
Maadili ni neno mahususi kwa ajili ya mambo tunayofikiri kwamba ni muhimu sana. Watu binafsi wanayo maadili; vikundi vinaundwa na watu wanaoshirikishana maadili. Shirika lina maadili yake. Shirika lipo kwa ajili ya kuhudumia maadili hayo.
Kwa Mkristo, aidha iwe ni kwenye biashara au huduma, kumpendeza Mungu ndiyo thamani kuu. Maadili ya shirika lililoundwa kwa ajili ya kumpendeza Mungu (na haipaswi pawepo na kusudi la aina nyingine) yatachukua kwa umakini mkubwa ukweli wa kibiblia, kanisa na injili.
Hata yale mashirika ambayo hayakiri kuwa ya Kikristo kwa kawaida yanategemea msingi wake kwenye baadhi ya maadili mazuri, kwa sababu yapo ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu. Shirika moja la kibiashara liliorodhesha maadili yake kwa njia hii: uadilifu katika mambo yote, utunzaji wa ubora, mahusiano, na kujifunza.
Kwa biashara yeyote, thamani moja muhimu ni kupata faida, kwa sababu biashara haiwezi kutimiza kusudi lake bila faida. Hata hivyo, hata kwenye biashara, faida siyo thamani muhimu sana.
Biashara nyingine kubwa iliorodhesha maadili haya: usalama, huduma, furaha, na mafanikio. Mafanikio yatakuwa na maana ya faida kwa biashara, lakini hayangeweza kupatikana pasipokuwepo na maadili mengine. Maadili mengine huongeza uwezekano wa kupata faida, kwa sababu watu hawapendi kuwa wateja wa biashara ambayo haikidhi hitaji lao.
Inawezekana kwa shirika kuwa na msingi wa maadili ambayo siyo mazuri, kama vile uwezo usio na kikomo wa mtu fulani au chuki ya kikundi fulani cha watu. Shirika kama hilo ni mara chache sana kuweza kuwa na nguvu kwa muda mrefu na kila wakati huwa ni la kuharibu.
Maadili huelezea jinsi watu wa shirika wanavyopaswa kutenda na kujiheshimu wakati wakiwa wanafanya kazi kwa ajili ya malengo. Haitoshi tu kufikia malengo. Mtu anahitaji kuridhika na jinsi alivyofika kwenye malengo hayo. Kwa mfano, mtu hapaswi tu kuridhika na jinsi alivyoshinda mchezo ikiwa alishinda kwa njia za udanganyifu. Mtu anayetaka furaha ya ushindi halisi wa kweli wa mchezo hawezi kudanganya, kwa sababu atakuwa amejidanganya mwenyewe kwa ushindi halisi wa kweli.
► Jaribu kufikiria kuhusu lengo ulilo nalo. Kwa nini ni muhimu kuridhika kuhusu jinsi ulivyofikia lengo lako?
Maadili yanaorodheshwa kwa mpangilio wa kipaumbele. Kwa mfano, biashara moja iliorodhesha uadilifu kwanza kwa sababu uadilifu kamwe haupaswi utolewe kama dhabihu ili kupata thamani nyingine. Biashara nyingine iliweka usalama kabla ya huduma, kwa sababu usalama wa watu ni muhimu zaidi kuliko urahisi wao.
Mpangilio wa maadili ni muhimu. Kwa mfano: Ikiwa biashara inathamini faida na pia inathamini uaminifu, mfanyakazi atafanya nini wakati kuna nafasi ya kupata faida kwa kutokuwa mwaminifu? Atafanya nini kama wakati uaminifu unaweza kugharimu faida? Kama uaminifu utakuwa ni kabla ya faida katika orodha ya maadili, anajua jambo la kufanya. Shirika linaundwa kwa jinsi linavyoshughulikia migogoro iliyoko kati ya maadili. Thamani kuu ya kanisa kupita zote ni kumheshimu Mungu, na hakuna kusudi ambalo linaweza kufikiwa kwa njia ambayo haimheshimu Mungu.
Shirika ni lazima litafute maadili yake kwa lenyewe kujichunguza. Kama tayari linafuata maadili, hayo maadili yanapaswa yagunduliwe.
Shirika haliwezi tu kukiri maadili. Baadhi ya mashirika yanadai kuwa na maadili ambayo kiuhalisisia hawayafuati kabisa, na wafanyakazi na wateja wao wanajua wazi kwamba tamko lao la maadili halimaanishi kitu chochote.
Orodha ya msingi ya maadili inapaswa iwe fupi, iliyoelezwa kwa njia rahisi, inayojulikana na kila mtu, na inayoweza kutumika katika hali yeyote ile. Orodha ya maadili inapaswa iwe orodha fupi (ikiwezekana 4-5), kwa sababu watu hawataweza kuweka fokasi yao kwa orodha iliyo na mambo mengi.
Maadili hayachaguliwi kwa sababu yanazalisha matokeo mazuri. Ikiwa maadili yamechaguliwa kwa sababu hiyo, yangebadilishwa ili kupata matokeo bora. Maadili huchaguliwa si kwa sababu yanafanya kazi vizuri, bali kwa sababu ndiyo yaliyo na umuhimu wa kweli.
Wakati mwingine shirika linaanzishwa na kuwa na mafanikio katika bidhaa fulani au wazo. Watu katika shirika wanaweza kufikiria kwamba shirika lipo kwa ajili ya kutoa bidhaa hiyo au kufuata wazo hilo, Hata hivyo, bidhaa hiyo au wazo hilo haviwezi wakati wote vikakamilisha maadili ya shirika. Ni bora kwa shirika kuanzisha maadili yake lenyewe, kisha liwe tayari kufanya jambo lolote litakaloweza kutimiza maadili hayo.
Shirika la umisheni lilikuwa linasaidia makanisa mengi kwa msaada wa kifedha wa kila mwezi. Bajeti zao nyingi zilitumika katika kusaidia matumizi ya kawaida. Hata hivyo, viongozi walianza kutambua kuwa maadili yao muhimu zaidi ilikuwa kukuza makanisa yanayoongozwa na kuungwa mkono ndani ya jamii zao. Utaratibu wao wa kawaida wa kutoa msaada kwa makanisa ulizuia mafanikio ya lengo lao. Walianza kubadili mikakati na matendo yao ili iendane na maadili yao.
Walitambua kwamba kusudi lao lilikuwa ni kuyasaidia makanisa kwa njia ambayo ingesaidia kuyafanya yawe na nguvu badala ya kuyafanya yaendelee kuwa tegemezi.
“Chanzo pekee cha uthabiti cha kweli kinachoaminika ni kiini cha ndani chenye nguvu [ya maadili] na nia ya kubadilisha na kurekebisha kila kitu isipokuwa kiini hicho.”[2] Shirika ni lazima lionyeshe maadili yake katika mambo yote linayofanya, kwa uhalisi na kwa uthabiti.
[3]Maadili ya shirika hayawezi kushikiliwa na timu ya uongozi pekee. Ni muhimu kwamba watu wa shirika wakaamini katika maadili na kuyafuata. Ikiwa watu wenye ushawishi kwenye shirika kiuhalisia hawaamini na kuunga mkono maadili, shirika haliwezi kuwa na nguvu. Shirika linahitajika mara kwa mara kukuza watu wanaoshikilia maadili yake. Watu ambao hawazingatii maadili hawapaswi kuendelea na uongozi. Mazingira yanapaswa yaunge mkono maadili kwa nguvu sana kiasi cha kwamba baadhi ya watu watachagua kuondoka na wengine watavutiwa kukaa.
Nidhamu kali katika shirika haimaanishi kwamba hakuna kunyumbulika na aina mbalimbali. Ikiwa watu wana kujitolea kabisa katika shirika, wanaweza kuwa na mambo mchanganyiko isipokuwa maadili. Nidhamu kali inamaanisha kwamba watu wa shirika ni lazima waunge mkono maadili katika kila watakochokuwa wanafanya.
Maadili huwa halisi pale tu unapoyaonyesha kwa jinsi unavyotenda na jinsi unavyotaka watu wengine watende. Kama uko tayari kutenda kinyume na maadili yako unayojinadi nayo ili kuweza kupata jambo fulani lifanyike, maadili yako ya kujinadi siyo maadili yako sahihi. Kuna kitu fulani kingine ambacho ni cha muhimu zaidi kwako.
Imejengwa ili Kudumu
Collins na Porras walifanya utafiti wa Makampuni ambayo yamedumu na kuwa bora zaidi kwa muda mrefu wakati makampuni yanayofanana nayo yameanguka. Waliyaita makampuni hayo bora kuwa ni “Makampuni yenye maono.”[4]
Makampuni yaliyo na maono hufundisha wafanyakazi wao maadili ya msingi kwa uwazi zaidi kuliko makampuni yanayorudi nyuma. Wanatengeneza mila ambazo zina nguvu sana kiasi kwamba wanaonekana ni wa kidini katika maadili yao.
Makampuni yaliyo na maono hulea na kuchagua menejimenti kwa uangalifu zaidi kulingana na jinsi ambavyo wanaonekana wanafaa kuwa kwenye kiini cha maadili yao kuliko makampuni yanayorudi nyuma.
Makampuni yaliyo na maono husababisha watu wao kuwiana kwa uthabiti maadili ya msingi kuliko makampuni yanayorudi nyuma.
Shirika ni lazima litafute njia za kusisitiza maadili ya msingi, kufundisha matumizi yake, na kuzingatia mazoezi kwa ajili ya kupata mrejesho na masahihisho. Vitendo na sera zote za kampuni ni lazima zionyeshe uwepo wa maadili.
Hatua ya 2: Kutambua Kusudi
Kampuni yenye kusudi imetegemezwa kwenye maadili ya msingi. Kusudi hili halina haja liwe la kipekee kutokana na mashirika mengine.
Kusudi linaelekeza na kuhamasisha ubora. Shirika linapaswa litathiminiwe kwenye misingi ya jinsi linavyofanya kazi vizuri na kutimiza kusudi lake.
Kusudi pia halibadiliki. Sio sawa na malengo ambayo huwa yanapatikana, kisha kubadilishiwa hapo mengine. Wakati mwingine shirika linabidi libadilishe njia ya jinsi linavyotimiza kusudi lake. Shirika linapaswa kujitohoa au kujirekebisha katika kubadilisha mahitaji kwa kusudi la kuhifadhi lengo lake la awali.
Kabla ya umeme kuwepo, kulikuwa hakuna majokofu majumbani kwa watu. Makampuni yalisambaza maziwa kila siku majumbani kwa watu. Kwenye majiji mengi kwa wakati huu, watu wana majokofu majumbani kwao na wanaweza wakahifadhi maziwa kwa siku kadhaa. Kama kampuni itakuwa ipo tu kwa ajili ya kusambaza maziwa, baada ya muda itakuwa haihitajiki tena. Hata hivyo, ikiwa kusudi lake lingekuwa kutoa bidhaa kwa njia rahisi, huenda lingepata njia nyingine ya kutimiza kusudi hilo. Labda ingeanzisha kituo ambapo maziwa na bidhaa zingine za maziwa zinauzwa. Pengine lingetafuta aina mbalimbali za bidhaa za kusambaza majumbani badala ya maziwa. Pengine kampuni ikatafuta bidhaa mbalimbali mchanganyiko ambazo zinaweza kusambazwa majumbani kwa watu badala ya maziwa.
Jengo la kanisa lilikuwa liko kwenye eneo la ujirani ambao ulikuwa unabadilika. Watu wengi wa vikundi vya lugha mbalimbali waliokuwa maskini walikuwa wanaingia na kukaa katika eneo hilo jirani. Watu wa kanisa walikuwa hawajui jinsi ya kufanya uinjilisti kwa kundi la hawa watu wageni waliohamia kwenye ujirani huo. Kwa kuwa kanisa lilikuwa halina kusudi ambalo lingewapa maono ya jinsi ya kuufikia ujirani ule kwa uinjilisti, watu wa kanisa waliamua kuliuza lile jengo la kanisa na kuhamia katika eneo lingine.
Hatua ya 3: Kushirikishana maono
Maono ni maelezo ya jinsi ambavyo mambo yanatakiwa yakae. Maono ni jibu la swali hili: “Je, mambo yatakuwaje endapo tutafanikiwa kabisa?”
Maono ni ukweli kama ambavyo ingetakiwa iwe kama shirika lingefanikiwa kabisa. Kiongozi anapaswa awe na picha hii kwenye akili yake na kuiwasilisha kwenye shirika lote kwa njia mbalimbali. Kiongozi anapaswa awasilishe maono na kuwa na mwenendo mzuri ambao kwa njia hiyo watu wa shirika hawatakuwa na shaka naye kuhusu shauku na uwajibikaji wa kiongozi katika maono hayo.
Watu hufanya kazi nje ya msingi wa ufahamu wa msingi wa ukweli ambao unathibiti mtazamo wao wa jinsi wanavyoyaona masuala ya mtu binafsi. Wana ufahamu wa jinsi mambo yalivyo na jinsi wao wanavyopaswa wawe. Uelewa huo anasimamia njia ambayo maswali binafsi yanajitokeza.
Albert Mohler alisema, “Kiongozi ni lazima atengeneze jinsi wafuasi wake wanavyofikiri juu ya kile kilicho halisi, kile ambacho ni cha ukweli, kile ambacho ni sahihi, na kile ambacho ni muhimu…. Viongozi wanalenga kufikia mabadiliko ya kudumu na usawa wa kawaida juu ya maswali haya.”[5] Kiongozi anapaswa awe anafafanua mara kwa mara, jinsi mambo yalivyo na ni kwa jinsi gani yanapaswa yawe.
Kikundi cha waumini kilianzisha kanisa katika eneo linaloishi watu maskini sana kwenye jiji kubwa. Walichokuwa wamethamini wao ni injili, kanisa la mtaa, na familia. Lengo lao lilikuwa ni kudhihirisha maisha ya pamoja katika kanisa na kwenye eneo lililokuwa na watu maskini sana. Maono yao yalikuwa kwamba eneo lile la kijiografia libadilishwe kwa jinsi watu watakavyoendelea kuishi maisha ya kanisani kama Mungu alivyokusudia. Malengo yao yalikuwa ni kuwasilisha uhai wa kanisa kwa jamii kwa njia maalumu kabisa.
Hatua ya 4: Kuweka Malengo
Malengo ni hatua maalumu katika kufikia maono. Yanapaswa yapimwe yawe rahisi kuonekana.
Malengo yana msingi wake kwenye maadili kwa sababu yanaonyesha ni kwa jinsi gani maadili hayo yataweza kuleta athari kwa wateja, timu ya kazi, jamii, na dunia. Malengo yote ni lazima yaonyeshe uzito wa maadili yatakavyokuwa.
Blanchard alielezea uhusiano ulipo kati ya maadili na malengo kama ifautavvo: “Malengo ni ka ajili ya baadaye. Maadili ni sasa. Malengo yanawekwa. Maadili watu wanaishi nayo. Malengo hubadilika. Maadili ni kama miamba inayoweza kutegemewa. Malengo huwafanya watu kusonga mbele. Maadili hudumisha juhudi zilizofanyika.”[6]
Malengo hayapaswi yawe ya kudumu. Yanahitajika yabadilike wakati hali nazo zinapobadilika. Maadili hayabadiliki, lakini malengo lazima yabadilike ili yaweze kuhudumia maadili hayo katika hali zinazobadilika.
Kampuni moja huko Marekani ilitengeneza bidhaa za kuendeshwa na farasi kama vile mikokoteni. Lakini, baada ya magari kuanza kutumika kwa wingi, watu hawakununua tena bidhaa za kuendesha farasi. Kampuni hiyo ilishindwa kubadilika na kuja na malengo ya kutengeneza bidhaa mpya, hivyo ikafa.
Ken Blanchard aliandika, "ufunguo wa timu bora, yenye hamasa, inayoweza kubadilika, na inayokamilisha majukumu kwa wakati ni kuhakikisha kuwa watu wako wanazingatia maadili badala ya kufuata malengo pekee.”[7]
Timu nzuri huhamasishwa na lengo kubwa. Lengo halipaswi liwe kubwa sana kiasi kwamba timu inaanza kufikiri kwamba kwa ukweli haitawezekana, kwa kuwa basi kiuhalisia sio lengo. Hata hivyo, ikiwa lengo litakuwa la juu sana ambalo litakuwa na mafanikio makubwa juhudi kubwa sana itahitajika. Watu ambao hawako kwenye shirika wanaweza wakafikiria kwamba lengo lililowekwa kamwe halitawezekana, lakini lengo linapaswa liwe kitu ambacho timu iliyohamasishwa italiona kuwa inawezekana.
Mafanikio ya malengo yanabidi yasherehekewe na kupongezwa ili yaonekane kama ni alama zilizo barabarani kuelekea kwenye maono.
► Je, inatokea nini kama kikundi kitajaribu kufanya kazi kwa bidii bila ya kuwa na malengo maalumu?
Hatua ya 5: Kupanga Mkakati
Mkakati ni kutengeneza mpango kazi wa utekelezaji ambao utafikia malengo. Mkakati unapaswa uwe kwenye mtazamo halisi wa hali zilizopo; upatikanaji wa rasilimali na uwezo unaopatikana; na malengo ya kuridhisha lakini yaliyo na changamoto.
Mkakati pia unajumuisha kuweka sera. Watu katika shirika wanahitaji mifano ya kufuata inayothibitisha maadili na kufikia lengo. Vinginevyo, hakutakuwa na ubora wa mara kwa mara.
Kanisa linapaswa kufundisha watu jinsi ya kusalimiana na mgeni, jinsi ya kuomba na mtu aliyeko madhabahuni, ufuasi wa aina gani utolewe kwa mwamini mpya, jinsi ya kushughulikia mahitaji ya kimwili kwenye kusanyiko, na mambo mengine ya kutendea kazi. Kama kanisa halitakuwa linajadili mambo haya na kuamua juu ya mpango mzuri, haliwezi kutarajia haya mambo yafanyike vizuri.
Kupanga malengo kunakuja kabla ya kupanga mikakati, lakini malengo yatakuwa yakiboresha wakati mikakati ikiwa inaendelea kufanyiwa kazi. Mikakati itafanyiwa maboresho wakati wa utendaji kadri utakavyokuwa unaendelea kuona matokeo ya utendaji wako. Ni mara chache sana kwamba mkakati unaweza kuwa mkamilifu sana kiasi cha kutohitaji marejeo. Kuendelea kushikilia msimamo kwenye mwelekeo wenye makosa ni kosa kubwa sana kuliko kuanzia kwenye njia yenye makosa.
Mabadiliko makubwa ya mkakati yanaweza yakagharimu muda, kazi na rasilimali, kwa hiyo kufanya mkakati wako uwe mzuri kadri itakavyowezekana mapema kwenye utekelezaji. Endapo utaweza kupata njia ya kufanyia majaribio kwa kufanya kitu fulani kwa njia ndogo kwanza, ndipo utakapojua kama mkakati utafanya kazi au laa. Ni jambo zuri kuwekeza katika kupanua kitu ambacho kimeshafanyiwa majaribio na tayari kinafanya kazi.
Jeshi la taifa limeundwa kwa ajili ya kulilinda taifa kwenye wakati wa vita. Mataifa mengi hayako vitani kwa muda wao mwingi. Kwahiyo, maelfu ya watu wamepelekwa katika mafunzo kwa ajili ya lengo hilo, kisha kutumia muda wao mwingi katika kufanya mambo mengine. Jeshi lina matatizo katika kujitafutia lengo lake lenyewe wakati likiwa haliko vitani. Mara nyingi jeshi huongeza amri na sera zake ambazo zitawaweka wanajeshi kwenye mishughuliko isiyokuwa na malengo yaliyo wazi.
Kama kanisa litakuwa halina lengo lililo wazi, linaweza likamilikiwa na ukuaji wa sheria, sera na taratibu nyingi nyinginezo.
Hatua ya 6: Kuchukua Hatua
Kuchukua hatua kunatakiwa kufuate baada ya mkakati. Kuchukua hatua kunahusisha pamoja na msaada wa mafunzo ya awali, kuhakikisha kazi zinafanyika, kuendelea kuwaweka watu kwenye motisha, na kusimamia ufanisi.
Shirika la umisheni lilitoa msaada kwa makanisa katika nchi kadhaa. Hata hivyo, kwa kufikiria kuhusu maadili yao, wakatambua kwamba shirika hapo mwanzoni lilianza na watu waliokuwa wanapeleka injili kwa watu ambao walikuwa hawajafikiwa na Habari Njema. Walikuja kujitambua kwamba kusambaza injili kulikuwa ndiyo msingi wao wa maadili, na kisha kupeleka injili kwenye maeneo mapya ambayo yalikuwa hayajafikiwa kulikuwa ndiyo lengo lao. Waliamua kuweka malengo mapya na kuandaa mipango mipya. Badala ya kutoa misaada kwa makanisa ambayo tayari yalikuwa yameshaanzishwa, walilenga kufanya mafunzo ya awali na kutuma wamisionari kwenda kwenye maeneo mapya.
Hatua ya Saba 7: Kupata Mafanikio
Mafanikio siyo tu kufuzu kwenye lengo kubwa. Mafanikio pia ni pamoja na kufuzu kwa malengo mengi katika safari. Hatua yeyote endelevu ya kuelekea kwenye maono ni mafanikio.
Shirika la umisheni lilifanya kazi ya kuanzisha makanisa ikijumuisha kwa pamoja mafunzo na miradi ya maendeleo.Walikuwa na idadi kubwa ya makanisa wakiwa na uhusiano pamoja nao. Mengi ya makanisa hayo hayakuwa yameanzishwa na hili shirika la umisheni, lakini yaliimarika kwa ushawishi wa shirika la kimisheni. Viongozi wa shirika walikuja kutambua kwamba maadili ya shirika lao yalikuwa ni kuendeleza na kuimarisha makanisa. Kwa hiyo, lengo lao kimsingi halikuwa ni kufanya uinjilisti na kufungua makanisa, bali kuongeza uwezo wa makanisa wa kufanya kazi. Walianza kuweka fokasi yao kwenye kuendeleza mafunzo kwa ajili ya makanisa.
Timu ya Wakristo ilishirikishana injili pamoja na watu waliokuwa waathirika wa madawa ya kulevya na au pombe. Baadhi yao walikuwa watu waliokuwa wameokoka. Walihudhuria makanisa mbalimbali, lakini walikuwa matatizo la kupata kanisa ambalo lingewaelewa na kuwakubali. Wakaanzisha kanisa jipya, lililoongozwa na timu ambayo iliwafanyia uinjilisti. Maadili ya hili kanisa yalikuwa ni injili na kuleta mabadiliko kwa waathirika wa madawa ya kulevya. Lengo lao lilikuwa ni kuwezesha uinjilisti na kuwafanya wanafunzi kwa waathirika. Mkakati wao ulikuwa ni kupanga shughuli na programu ambazo zitakidhi mahitaji ya kiroho ya waathirika wa madawa ya kulevya na hata wale wa zamani.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha makusudi au matendo yao kutokana na somo hili.
“Matumizi ya maana hayakusudiwi kupunguza imani yetu kwa Mungu, na imani yetu kwa Mungu haikusudiwi kutuzuia sisi kutumia jinsi au njia yeyote ile ambayo Mungu ametupa kwa ajili ya ukamilishaji wa makusudi yake mwenyewe.”
- J. Hudson Taylor
“Mafanikio hayawezi kutoka kwa timu ya uongozi pekee. Mbinu huwa zinabadilika, na watu ni lazima wabadilike pamoja nazo.”
- James Cash Penney