Agiza kikundi kujadili taarifa ifuatayo hapa chini. Je, inamaanisha nini? Je, ni kweli? Je, kwa nini iwe ni muhimu?
Kamwe hakuna jambo lolote la maana lililowahi kupatikana kwa mtu anayefanya akiwa peke yake.
► Timu ni nini?
Timu si kundi tu la watu wanaomfuata kiongozi mmoja. Timu ni kundi lililounganishwa na lengo kubwa, maadili ya kawaida, ushirikiano, na uongozi uliokubaliwa.
Anza kwa kufikiria timu yako wewe ni nani? Timu siyo kanisa lote. Timu siyo tu wale watu walioko kwenye nafasi rasmi za uongozi.
[1]Timu mbalimbali zina rasilimali zaidi, mawazo, na nguvu kuliko angekuwa mtu mmoja. Timu zinaongeza nguvu za mtu na kulinda udhaifu wake. Kiongozi anatakiwa ahakikishe kwamba watu wanakuwa na majukumu sahihi na nafasi sahihi za uongozi ili kwamba nguvu yao iweze kuwa na ufanisi wa hali juu na madhaifu yao yaweze kupunguka.
Timu zinasaidia kutoa mitazamo kadhaa ya jinsi ya kukabiliana na hali inayojitokeza. Woodrow Wilson, raisi wa zamani wa Marekani, alisema, “Hatupaswi tu kutumia akili zetu zote tulizo nazo, lakini tunaweza kutumia akili zote tunazoweza kukopa.”
Kama malengo yako yanaweza kufanikishwa na wewe peke yako, malengo yako hayo ni madogo sana. Malengo makubwa yanahitaji timu nzuri pamoja na uongozi bora. Kwa jinsi ambavyo malengo ni makubwa, ndivyo hivyo na timu inapolazimika kuwa bora zaidi.
John Maxwell alitumia kielelezo cha kupanda mlima katika kuelezea hitaji la kuwa na timu yenye nguvu. Kielelezo hicho anakiita kanuni ya Mlima Everest.[2] Kwa jinsi ambavyo changamoto inaongezeka kuwa kubwa, vivyo hivyo na hitaji la kazi ya pamoja ya timu linaongezeka kuwa kubwa zaidi.
Ili kufikia katika ndoto kubwa, lazima uwe na timu kubwa. “Timu yenye ndoto kubwa” ni ya watu wabunifu, wenye umoja, wanaonyumbulika (wanaoweza kubadilika kwa urahisi kupokea mazingira mapya), waliohamasika, wenye kuheshimu, waliodhamiria na wenye uzoefu.
Timu ni lazima iende sambamba na ndoto yao. Siyo kweli kusema kwamba timu inaweza ikafanya na kukamilisha jambo kubwa kama siyo timu kubwa. Ni lazima kukuza timu na pia kukuza ndoto sahihi inayofaa kufikiwa. Unapaswa ufanye kazi ya kuikuza timu kabla ya kukuza ndoto.
“Hakuna mtu atakayeweza kuwa kiongozi mkuu na maarufu ambaye atataka kufanya mambo yote yeye mwenyewe au kupata thawabu kwa kutenda hayo mambo peke yake.”
- Andrew Carnegie
[2]Kanuni nyingine kutoka kwa John Maxwell katika somo hili ni pamoja na “kiungo dhaifu zaidi,” “tunda lililoharibika,” na “ubao wa kukalia,” ingawa maneno na ufafanuzi wa maelezo ya kanuni hayafanani.
Vipengele vya Timu Imara
Timu haiwi na nguvu kwa sababu tu ya kuwa na watu wenye nguvu. Kipaji cha mtu binafsi hakitaweza kuifanya timu iwe yenye uwezo mkubwa hadi pale wanachama wake watakaposhikamana kwa ushirikiano. Timu ni kikundi cha watu kilichoungana kwa ajili ya lengo kubwa, uthamani wa maadili wa kawaida unaofanana, ushirikiano, na kuwa na uongozi uliokubalika.
Kama wanachama wana malengo yao binafsi yanayoingiliana na malengo ya timu, timu haitaweza kuwa na nguvu.
Kama wanachama watakuwa na uthamani na maadili yaliyotofautiana, timu haitaweza kuendelea kuwa na nguvu kwa kipindi kirefu.
Kama wanachama wa timu hawatakuwa na ushirikiano wa kufidia madhaifu ya watu binafsi, timu hiyo haina nguvu.
Kama kutakuwepo na migogoro ya wanachama kwa sababu ya kutofuata mamlaka moja inayofanana, timu hiyo haina nguvu.
Baadhi ya aina nyingine za uongozi hazina uwezo wa kuijenga timu. Kama kiongozi anataka tu kupata msaada wa malengo yake, anataka tu afanye kazi mwenyewe kiasi kwamba juhudi za watu wengine zitakuwa hazihitajiki, au siku zote anafanya maamuzi ili kwamba kusiwepo na majadiliano, hataweza kuijenga timu.
Mtume Paulo alitumia kielelezo cha mwili wa nyama katika kuelezea umoja wa kanisa katika 1 Wakorintho 12. Kuwa na shauku ya maslahi binafsi ni tatizo wakati wanachama wanaposhindwa kuwasilisha maslahi yao kuhusiana na malengo ya timu. Kuwa na shauku ya maslahi binafsi husababisha wivu na kutafuta nafasi ya cheo kwa sababu zisizo sahihi. Kuwa na shauku ya maslahi binafsi husababisha ushindani usiokuwa na msingi miongoni mwa wanachama.
Tatizo lingine ni wakati wanachama wanapojihisi kwamba wana uwezo wa kuyafikia malengo yao bila ya kupata msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote. Pia kuna tatizo lingine la wanachama kutaka kufanana na wanachama wengine badala ya kusimama kwenye nafasi zao mahsusi.
Kanuni ya Kiungo Dhaifu zaidi
Nguvu ya mnyororo ni kubwa tu sawa na nguvu ya kiungo chake dhaifu zaidi. Vivyo hivyo, nguvu ya timu hupunguzwa na mwanachama wake dhaifu zaidi.
Kila mwanachama katika timu analo jukumu ambalo linagusa ufanisi wa kazi za wanachama wengine. Kama mwanachama atakuwa anashindwa katika jukumu lake linalompasa, atakuwa anapunguza ufanisi wa kila mwanachama mwingine kwa kushindwa kufanya kazi ambayo itawasaidia wanachama wote. Uwezo wa mfanyakazi mwenye haraka hauna thamani kama itabidi asubiri mtu mwenye kujivuta.
Baadhi ya kazi zinaweza zikafanywa na watu ambao hawana majukumu maalumu. Kwenye masuala kama hayo, kanuni ya kiungo dhaifu zaidi haifanyi kazi. Kwa mfano, kama utakuwa unajaribu kusukuma gari la mizigo ambalo litakuwa limekwama kwenye matope, watu wote wanaotoa msaada wanaweza wakalisukuma kwa pamoja, na yule mwenye nguvu zaidi kuliko wengine hawekewi ukomo na wale walio wadhaifu zaidi.
Hali kama hiyo inaweza kuonekana wakati wa kuvuna mavuno shambani. Watu wavivu hawawezi kuwazuia watu walio na bidii; na kama utahitaji msaada wa ziada, unaweza ukaongeza watu wengine zaidi.
Kanuni ya kiungo dhaifu inatumika katika hali ambapo watu binafsi wanajaza majukumu muhimu. Kwa mfano: Ikiwa wafanyakazi kadhaa wa kuweka tofali wanamsubiri mtu mmoja kuchanganya mchanganyiko, hakuna anayeweza kufanya kazi kwa sababu yule mtu yupo pole pole.
Katika mashirika mengi, kuna watu kadhaa katika nafasi za kipekee. Kila mmoja anafanya kazi ambayo ni muhimu kwa wengine. Ikiwa hafanyi kazi yake vizuri, kila mtu anathiriwa. Shida haiwezi kutatuliwa kwa kuongeza watu zaidi kusaidia kwa sababu wengine hawawezi kufanya kazi yake kwa niaba yake.
Kuna mfano unaoitwa “shingo ya chupa.” Wakati chupa au jagi iliyojaa kimiminika inapogeuzwa kuelekea chini, kimiminika huwa hakimwagiki nje kwa mara moja. Umiminikaji unakuwa una kikomo chake kutokana na ukubwa wa shingo ya chupa. Hali kadhalika, kwenye mashirika mengi kuna shughuli na programu nyingi ambazo zimepunguzwa kasi yake kwa sababu ni lazima zisubiri mtu fulani aje aifanye kazi yake.
Kama mtu atashindwa kutimiza wajibu au majukumu yake katika nafasi aliyo nayo:
Wanachama wengine katika timu hawataweza kufanya kazi vizuri.
Baadhi ya wanachama wengine katika timu wanaanza kuchukia kiungo dhaifu.
Timu inakosa au inapoteza matumaini kwa kiongozi wao kwa sababu anashindwa kusahihisha tatizo.
Timu hupunguza matarajio yake katika kile ambacho kingeweza kufanyika.
Mtu ambaye ni “kiungo dhaifu” katika timu ni lazima aondolewe na kuwekwa katika nafasi nyingine ili kwamba asiweze kuikwamisha timu.
► Je, ni aina gani ya kazi nyingine unazoweza kufikiria ambazo zinaweza kuelezea kuhusu mfano wa “shingo ya chupa”?
Kanuni ya Tunda Lililoharibiwa
[1]"Wakati kipande cha matunda kilichooza kikiwekwa katika kikapu chenye vipande vingine vya matunda, vipande vingine vitaharibika hivi karibuni. Tukio hili linaonyesha athari za mtazamo. Mitazamo mizuri na mibaya inaathiri wengine, lakini mitazamo mibaya inaathiri zaidi."
Unapomchagua mshiriki wa timu, angalia mtazamo zaidi kuliko uwezo. Mtu mwenye mtazamo sahihi anaweza kufundishwa na kuhamasishwa, lakini mtu mwenye mtazamo mbaya hawezi. Usimajiri mtu mwenye mtazamo mbaya na kufikiri kwamba unaweza kumbadili. Mtu kwenye timu mwenye mtazamo mbaya lazima aondolewe ikiwa hatabadilika.
Kumtambua Msumbufu wa Mazoea
Watu wasumbufu hujaribu kupata heshima na hisia za kuwa watu muhimu kwa kuwashambulia watu walioko kwenye nafasi za uongozi (na siyo tu kiongozi wa juu peke yake). Wanaweza wakachagua mtu mmoja wa kumshambulia mara kwa mara. Watu hawa ni waharibifu kwa watu binafsi na mashirika. Kiongozi ni lazima ajifunze jinsi ya kuwatambua na kuwalinda watu wengine dhidi yao. Mtu msumbufu anaweza akasababisha wasaidizi wako wazuri sana wakaachana na wewe.
Tabia za mtu aliye msumbufu:
Anakuwa na rekodi iliyopita ya uharibifu.
Kwa sasa anafanya uharibifu.
Anarejea kwa washirika wasiojulikana kwa umaarufu wakati anapokuwa akilalamika.
Anamkosoa kiongozi aliyekuweko madarakani wakati huo akimsifia kiongozi mpya aliyeingia madarakani.
Huonekana kumfanya rafiki kwa haraka kiongozi mpya aliyeingia madarakani.
Anakusifia sana.
Anapenda kuwapata watu wakiwa na makosa.
Huwa hajawahi kukaa na kanisa au taasisi kwa kipindi kirefu.
Huwa ni mtu anayesema uongo.
Huwa ni mkali na anaweza akawa mtu mbaya sana.
Anapenda kuonyesha fedha alizo nazo.
Atafanya mambo yasiyoendana na Ukristo kwa sababu zake mwenyewe.
Anachukia mtu yeyote ambaye hakubaliani naye.
Anapenda kuchochea na kusababisha watu wengine kuingia kwenye hasira na au kuchanganyikiwa.
Anazungumzia kuhusu siku zake za nyuma zilizowahi kuwa ngumu kwake ambazo zilimfanya awe na nguvu.
“Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kutumia fikra zile zile zinazofanana tulizokuwa tukizitumia wakati tulipozianzisha.”
- Albert Einstein
Kanuni ya Benchi
Timu ya mchezo huwa na wachezaji wengi kuliko idadi ya wachezaji halisi wanaotakiwa kucheza kwenye mchezo husika. Makocha huwabadilisha wachezaji wakati wa mchezo ukiwa unaendelea ili kuingiza vipaji vingine tofauti na kutoa nafasi kwa wachezaji wao bora wawe na mapumziko. Benchi linahusisha wachezaji ambao wako tayari kucheza. Baadhi yao wanakuwa ni wachezaji vijana ambao bado wanaonekana kukua kimchezo.
Shirika ni lazima lifanye kazi endelevu ya kuipanua timu. Ni lazima kuwepo na viongozi vijana wanaokuwa. Kunapaswa kuwepo na watu wenye uwezo maalumu watakaounganishwa kwenye timu.
“Benchi” kwenye shirika ni kama benchi la timu za michezo. Mara nyingi, watu walioko kwenye benchi ni watu wasio na ujuzi mkubwa na wanaokuwa. Benchi la shirika linahusisha watu wenye ujuzi wa ziada.
Usitake tu kujaza nafasi zilizopo kwenye timu. Endelea kuijenga na kuipanua timu. Tafuta watu ambao wanaonyesha uwezo na kujitolea kabisa kutumika. Waache watoe msaada unaohitajika. Kama wakifanya vizuri, wakabidhi majukumu ya kufanya.
► Je, njia zipi zitumike katika kuendeleza timu ya kanisa la mtaa? Elezea jukumu la mtu na aina ya mtu ambaye anaweza akajumuishwa kwenye “benchi.”
Jinsi ya kuajiri wanachama kwenye Timu
Timu nzuri itawavutia wanachama wazuri. Jaribu kufikiria aina ya watu ambao wanavutiwa na timu yako. Je, ni nani anayetaka kujiunga? Je, ni nani anayetaka kuondoka? Mabadiliko hayo yataonyesha kama timu yako inapata nguvu au inakuwa dhaifu.
Wanachama wa timu husaidia kwa sababu mbalimbali – ikiwa ni pamoja na uhusiano wa kibinafsi na watu wengine, mapenzi mema, watu wenye hamasa kwa ajili ya kusudi, na matamanio au shauku ya kufanya jambo muhimu.
Tafuta shauku unapowajiri, badala ya kudhani kwamba unaweza kuhamasisha shauku hiyo baadaye. Awali, tulijifunza kuhusu Kiongozi wa Kiwango cha 5. Huyu ni mtu mwenye matarajio ya shirika kufanikiwa na siye anayejiendeleza kwa ubinafsi. Kiongozi anapaswa kuwa na matarajio haya na anatakiwa kutafuta wengine ambao wanashiriki matarajio hayo.
Taka kupata maoni ya watu ambao wanaweza kuisaidia timu. Wasikilize, waalike wawe washiriki, wakilisha kwao mambo ya kufanya, na kisha fanya upanuzi wa majukumu yao.
Kwa kila kitu utakachokuwa unakifanya, jiulize, “Je, ni nani anayeweza kunisaidia?” Fanya upanuzi na utegemezi wa kikundi kidogo cha watu ambao wana uwezo na uhusiano maalumu na wewe.
► Je, unawezaje kuelezea mazungumzo kati ya kiongozi na mshiriki wa timu anayetarajiwa? Je, ni kwa jinsi gani kiongozi anaweza kuvutiwa naye?
Hatua kwa ajili ya Kazi ya Timu
1. Fanya maamuzi ya kuijenga timu – hatua hii inaanzisha uwekezaji.
2. Kusanya timu nzuri kwa kadri inavyowezekana – hatua hii inawainua wenye uwezo.
3. Lipa gharama kwa kuikuza timu – hatua hii inahakikisha ukuaji.
4. Fanya mambo yote kama timu – hatua hii inajenga jumuiya.
5. Wawezeshe wanachama kwenye majukumu na mamlaka – hatua hii inajenga viongozi.
6. Toa pongezi za mafanikio kwa timu – Hatua hii inainua motisha wao.
7. Kuwa mwangalifu kuhakikisha kwamba uwekezaji uliouweka unalipa – Hatua hii inaleta uwajibikaji.
8. Tengeneza nafasi mpya – hatua hii inaongeza uwezo wa timu.
9. Wape kile kinachohitajika kwa ajili ya kuleta mafanikio – hatua hii inaleta kupatikana kwa matokea bora zaidi.
Somo kutoka katika Maandiko
Absalomu alikuwa mtoto wa kiume wa mfalme Daudi. Alikuwa kijana mtanashati na aliyekuwa anafahamika sana katika taifa lake. Ilipotokea watu kuja katika jiji wakiwa na matatizo, alisema, “Kama ningelikuwa mfalme, ningeweza kuwasaidia,” Watu walianza kuhisi kwamba kila kitu kitakwenda vizuri endapo Absalomu angekuwa mfalme (2 Samweli 15:3-4).
Absalomu angeweza kutumia uwezo wake kwa kumsaidia mfalme kutatua matatizo ya watu. Badala yake, alisababisha watu kukosa uaminifu. Kwa kuwa mfalme hakuwa amepanga utaratibu wa kujua na kutatua matatizo ya watu wake, kulikuwa na nafasi ya mtu mwingine kuitumia kwa ajili ya kusababisha watu kukosa uaminifu kwa mfalme. Kila kiongozi anapaswa ahakikishe kwamba watu wake wana njia nzuri ya kuwasilisha matatizo yao.
Maelfu ya watu waliungana na uasi wa Absalomu, yumkini hata marafiki wa karibu sana na mfalme Daudi. Absalomu alikuwa na matarajio ya watu kujitolea kufa kwa ajili ya matamanio yake. Kipaumbele chake hakikuwa kwa ajili ya mafanikio ya watu lakini kwa ajili ya hadhi yake mwenyewe.
Kuendeleza Wanachama wa Timu
Kiongozi anatakiwa atafakari ni aina gani ya uongozi na usimamizi kila mwanachama katika timu anahitaji. John Maxwell alisema:
Mwanachama anayeanza kwa shauku kubwa anahitaji mwongozo.
Mwanafunzi aliyeishiwa na imani anahitaji mafunzo elekezi.
Mwanafunzi anayemaliza mafunzo kwa umakini mkubwa anahitaji kupatiwa msaada.
Mtu anayejitegemea kupata matokeo binafsi anahitaji apewe majukumu ya kufanya.[1]
Unapoajiri mtu kwa ajili ya nafasi ya uongozi, tafakari aina ya mtu ambaye nafasi hiyo itakuwa inamhitaji. Maxwell alielezea aina hizi za watu:
Mtu anayeonekana wazi au mtu anayefanya kazi kwa nyuma.
Mtu wa mambo yote kwa jumla au mtaalamu.
Mzalishaji au mtunzaji.
Mtu wa watu au mtu wa makaratasi.
Kiongozi au msaidizi.
Mtaalamu au mwanafunzi
Mwanafikra mbunifu na mwanafikra wa dhana.
Mtu ambaye wakati wote anahitaji asimamiwe au mtu anayehitaji usimamizi mdogo.
Mchezaji katika timu au mtu atendaye binafsi.
Mtu mwenye kujitolea kwa muda mfupi au mtu wa kujitolea kwa muda mrefu.[2]
Kiongozi ni lazima siku zote ashirikishe pongezi kwa ajili ya mambo yaliyofikiwa na timu. Watu wanaoshirikishana mafanikio watakuwa wamehamasika kufanya vizuri zaidi kadri itakavyowezekana.
Unapokuwa unaitambulisha timu kwa watu wa nje, kiongozi hapaswi kuwashutumu wanachama katika timu kwa mambo yanayosababisha timu kushindwa. Kiongozi anapaswa abebe lawama za kushindwa kwa timu, akitambua kwamba angeweza akawa kiongozi mwenye ufanisi zaidi. Kama akiwalinda wanachama wa timu yake, watakuwa waaminifu kwake.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili.
[1]John Maxwell, 17 Indisputable Laws of Teamwork: Embrace Them and Empower Your Team (New York: HarperCollins Leadership, 2001), 50
[2]John Maxwell, Developing the Leader within You (Nashville: Thomas Nelson, 2005), 188
Muhtasari wa Taarifa Tano.
1. Hakuna kitu kikubwa kilichowahi kufanywa na mtu akifanya peke yake.
2. Timu ni kikundi cha watu kilichounganishwa na lengo kubwa, maadili ya pamoja, ushirikiano na uongozi uliokubalika.
3. Unapaswa ufanye kazi kwenye maendeleo ya timu kabla ya kuendeleza ndoto.
4. Mtazamo ni muhimu zaidi kuliko uwezo wa mwanachama wa timu.
5. Shirika ni lazima liendelee kufanya kazi endelevu ya kupanua timu.
Kazi za kufanya Somo la 10
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Fanya kukariri Taarifa Tano kwa Muhtasari zilizoko katika somo la 10. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.