Kila mtu anatakiwa kuwa kiongozi kwa mantiki kwamba anawashawishi watu wengine. Kwa mfano, kila mzazi wa kike au wa kiume anapaswa kuwaongoza watoto wake. Kanuni tunazojifunza katika kozi hii zitamsaidia mtu katika hizo nafasi za asilia. Hata hivyo, kozi hii imeweka fokasi yake zaidi kwenye kanuni za uongozi zilizo juu ya nafasi za uongozi za asili ambazo kila mtu anapaswa ajisikie kuwa nazo.
Mtu anaweza akawa na sababu mbalimbali za kutaka kuwania kuwa kiongozi. Sababu sahihi ni ile nia ya kutaka kutumikia watu wengine.
[1]Mafunzo yanaweza yakamfanya mtu kuwa bora sana dhidi ya watu wengine katika ufahamu na ustadi. Anaweza akaanza kujihisi kwamba yuko juu sana kwa thamani kuliko watu wengine. Anaweza akaanza kutegemea kupata huduma maalumu kutoka kwa watu wengine siyo tu heshima kwa ajili ya nafasi yake, bali kwa sababu ya hisia ya ukuu wa asili.
Mtume Paulo alionya kwamba, “Ujuzi huleta majivuno” (1 Wakorintho 8:1). Hakuwa anamaanisha kwamba ujuzi ni kitu kibaya au kwamba moja kwa moja ni kitu chenye madhara. Kwenye muktadha huu, alikuwa anazungumzia kuhusu mtu ambaye alijua mambo kadhaa lakini hakuwa amepewa motisha kwa upendo katika njia aliyotumia ujuzi wake.
Mafunzo yanaweza yakamfanya mtu akawa mtendaji mzuri sana kwa ajili ya ufalme wa Mungu, lakini ikiwa tu kama matamanio yake ni kutumika kwa unyenyekevu.
“Mtu mmoja anayetafuta utukufu hawezi akakamilisha mambo yaliyo mengi.”
- Sam Walton
Kuwa Kiongozi
Je, ni kwa jinsi gani mtu huwa kiongozi? Kumbuka, hatuzungumzii tu kuhusu nafasi rasmi ya uongozi. Kiongozi ni mtu ambaye ana ushawishi, ni mtu ambaye watu humfuata.
Baadhi ya watu wamezaliwa na uwezo wa asili wa kuweza kushawishi watu wengine. Watu hawa huonyesha kujiamini, ni wepesi katika kutafuta suluhisho, na watu huwafuata bila hata kufikiria. Kwa kuwa sifa hizi zipo, unaweza ukadhania kwamba baadhi ya watu wamezaliwa kuwa viongozi na wengine hawakuzaliwa kwa ajili ya kuwa hivyo. Hata hivyo viongozi wanafanyika kutokana na sababu mbalimbali mchanganyiko.
Kutokana na hadithi ya zamani ya Ukraine, kijana mmoja alikwenda kwa mchungaji wake akamwuliza, “Baba, nilikuwa nimeota kwamba mimi ni kiongozi wa watu 10,000. Je, hiyo itatokea kuwa kweli? Mchungaji akamjibu, “Kitu kinachokosekana tu ni kwa watu 10,000 kuota kwamba wewe ni kiongozi wao.”
Sababu zinazomfanya mtu kuwa Kiongozi.
Mtu anaweza kuwa kiongozi kutokana na sababu mojawapo zinazofuata au kutokana na mchanganyiko wa sababu hizo. Hata hivyo, hakuna hata mojawapo katika hizi ambazo zina utoshelevu wa kumfanya mtu awe kiongozi mwenye ufanisi na wa muda mrefu kama anakosekana kwenye maeneo mengine.
(1) Uwezo dhahiri wa asili.
Mtu anayeonekana kujiamini anaweza kuwa kiongozi mara moja popote atakapokwenda. Hata hivyo, ikiwa atashindwa kutimiza matarajio anayoyaanzisha, hataendelea kuongoza. Hata mtu ambaye ana uwezo wa asili ni lazima afuate kanuni za uongozi ili aendelee kuwa mwenye ufanisi.
(2) Kuleta majibu kwenye mgogoro
Viongozi wengi wamejitokeza kutokana na tatizo fulani. Janga kubwa linaweza kumdhihirisha kiongozi. Mtu huyo anaweza kuitikia janga hilo kwa hisia ya ndani ya wito au uwajibikaji, tofauti na mtu ambaye huangalia tu na kulalamika.
Janga huleta fursa kwa kiongozi mwenye uwezo, lakini sifa nyingine zinahitajika ili kuongoza baada ya janga kupita. Wakati mwingine, mtu anayeongoza vyema wakati wa janga hawezi kuongoza vyema katika mazingira mengine.
(3) Kuwa mtu wa kutegemewa kwa muda mrefu
Wakati mwingine mtu anakuwa ni kiongozi kwa sababu amekuwa ni mtu anayetegemewa na mwaminifu kwa muda mrefu wa miaka mingi. Watu wanamwamini kwa sababu wanajua kwamba ni mtu mwenye msimamo katika shirika.
(4) Kuwa na ujuzi au utaalamu
Mtu anaweza kuwa kiongozi kwa sababu amepata ujuzi na ustadi katika eneo maalumu. Anaweza tu akaongoza kwenye mazingira fulani na katika kutatua matatizo fulani.
(5) Aliyejifunza kanuni za uongozi
Mtu anaweza akajifunza kuongoza kwa kutumia kanuni tulizojifunza katika kozi hii. Hata hivyo, mafunzo hayawezi yakamfanya mtu akawa kiongozi mwenye ufanisi wa kiwango cha juu hadi awe amekuwa na uwezo wa asili.
(6) Wito wa Kimungu
Mungu alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu (Waefeso 4:11). Kwenye mashirika ya dunia, Mungu ni mwenye nguvu pekee ya kuwainua watu kuwa kwenye nafasi za juu (Zaburi 75:7, Danieli 2:21). Wakati mwingine, watu wanashangazwa Mungu anapomwita ambaye haonekani kuwa na uwezo wa asili, lakini Mungu siku zote humpa mtu uwezo wa kukamilisha wito wa Mungu.
Endapo watu watamwona kiongozi ni mtu mwenye msimamo kabisa kwenye kusudi la Mungu na anawezeshwa na Mungu, wanaweza wakamfuata kwa ajili ya kusudi hilo watakalokuwa wanaliamini. Ili kutunza uaminifu wao kwake, ni muhimu adhihirishe uhodari, utegemezi, na tabia.
Sababu za kumfanya mtu kuwa Kiongozi kutoka katika Maandiko
Tuangalie ni kwa jinsi gani baadhi ya watu katika Maandiko walivyoanza uongozi wao.
Elisha: Kuongoza katika kipindi cha mpito.
Elisha ni mtu aliyekuwa amechaguliwa na Mungu kuwa nabii wa kuwaongoza Waisraeli baada ya Eliya. Kipindi hiki cha mpito kinaelezwa katika 1 Wafalme 19:19-21 na 2 Wafalme 2:1-15.
Wito wa Mungu ulikuwa ni sababu ya wazi iliyomfanya Elisha akawa kiongozi. Hata hivyo, kuna mambo mengine zaidi ya msingi. Elisha alikuwa amehiari kuacha shamba lake kubwa ili mwenyewe ajikite kwenye huduma. Wito wa Mungu ulikuwa ni muhimu zaidi kwa Elisha kuliko utajiri. Gehazi alikuja kuwa baadaye ni mtumishi wa Elisha, alipoteza nafasi yake ya huduma kwa sababu ya kupenda fedha (2 Wafalme 5:20-27).
[1]Elisha alikuwa amehiari kuwa mtumishi kama sehemu yake ya mafunzo. Pasipo uhiari huu, hangeweza akawa na mafanikio kwenye huduma.
Elisha alitambua kwamba nabii aliyekuwa amemtangulia, Eliya, alifanya mambo ya kushangaza kupitia nguvu za Mungu. Aliweza kuwa ameisimamisha mvua isinyeshe kwa muda wa miaka mitatu. Alikuwa ametabiri kifo cha mfalme na malkia kwa ajili ya maovu yao. Alikuwa ameomba moto ushuke kutoka mbinguni. Elisha alikuwa ametambua kwamba hatima ya majukumu yake hayangeweza yakakamilishwa kwa mafunzo tu ya taratibu za kibinadamu. Alitambua kwamba ni lazima awe na upako wa Roho Mtakatifu wa Mungu.
Baada ya Eliya kuwa amenyakuliwa na Mungu kwenda mbinguni, Elisha aliichukua kanzu ya Eliya na akaitumia kuyapiga maji, akisema, “Yuko wapi Mungu wa Eliya?” Manabii wadogo walikuwa wakimwangalia kuona kama huduma ya kiongozi wao mpya ingekuwa na nguvu za Mungu. Walipoona muujiza wakasema, “Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha” (2 Wafalme 2:15). Walishuhudia uhamishwaji wa nguvu za Mungu kutoka kwa Eliya kwenda kwa Elisha.
Majukumu ya uongozi hupasishwa kwa njia isiyozuilika kutoka kwa viongozi wazee kwenda kwa viongozi vijana. Hata hivyo, nguvu za Mungu hazipasishwi moja kwa moja. Kizazi kipya cha viongozi ambao hawana imani kitapoteza nguvu za Mungu na kutegemea taratibu za kibinadamu.
Gideoni: Akiongoza katika Mgogoro
Gideoni hakuwa kiongozi katika taifa lake wala kabila lake. Taifa lake lilikuwa likivamiwa kila mwaka wakati wa mavuno. Gideoni hakuwa na wazo lolote la kubadilisha hali hiyo; alikuwa akijaribu kuficha chakula wakati mjumbe wa Mungu alipomjia. Alikuwa akijitahidi tu kuendelea kuishi na kukabiliana na hali yake. Hii si tabia ya kiongozi.
Mungu alimwita Gideoni "Ee shujaa" kwa sababu Mungu alijua kile alichoweza kufanya (Waamuzi 6:12). Gideoni alishangazwa na kuchaguliwa na Mungu na akaomba ishara kadhaa ili kuthibitisha.
Gideoni alimtii Mungu alipoangusha mahali pa ibada ya sanamu na kutoa dhabihu kwa Mungu. Kitendo chake hakikusababisha mageuzi ya kidini wakati huo, lakini kiliwafanya watu waanze kutilia shaka nguvu za sanamu.
Gideoni alimtegemea kabisa Mungu. Aliweza hata kutii maelekezo ya Mungu ya kuwaondoa na kuwarudisha nyuma wingi wa kundi la jeshi lake. Gideoni alipanga mpango wa mashambulizi usio wa kawaida, na Mungu akawapa ushindi mkubwa.
Kwa bahati mbaya sana, baada ya Gideoni kupata ushindi hakuwaongoza watu wake katika kumtumikia Mungu na badala yake wakageukia kwenye ibada ya sanamu. Ikiwa kiongozi hatakuwa thabiti kwa muda mrefu, atashindwa kukamilisha au kufikia uwezo wake wote kwa ajili ya Mungu.
Nehemia: Akiongoza kwa Maono
Nehemia alikuwa Myahudi aliyekuwa akifanya kazi kwa mfalme wa Babeli, mbali sana na nyumbani kwake. Alisikia kuhusu hali iliyokuweko katika Yerusalemu. Jiji lilikuwa limetekwa muda mrefu uliopita; kuta zilikuwa zimevunjwa na kushushwa chini, ikimaanisha kwamba watu walikuwa wako chini ya rehema za wavamizi wao.
Nehemia alijisikia kuwa na jukumu binafsi la kuchukua hatua. Watu walio wengi wangelisikitishwa na habari hizi bila ya kujisikia kuwa na wajibu wowote wa kuwajibika. Hawangeweza kuwa na tegemeo lolote la kuibadilisha hali iliyokuwepo.
Kiongozi hujisikia kuwa na jukumu la kufanya kwa sababu anafikiri kwamba kuna uwezekano wa kuweza kubadilisha hali iliyopo. Kwa kuwa ana uwezo wa kufanya hivyo, anajua kwamba ataweza kufanya.
Nehemia aliomba Mungu aingilie kati. Nehemia alijua kwamba kujijenga upya hakutawezekana bila ya msaada wa Mungu. Kiongozi wa Kikristo huwa hajaribu kuubadilisha ulimwengu ili uweze kufanana na maono yake mwenyewe, bali maono ya Mungu. Matumaini yake yako kwenye msingi wa Mungu, na siyo mwanadamu.
Mungu alitoa nafasi maalumu. Mfalme alionyesha kuwa na shauku katika tatizo la Nehemia. Kanuni tunayojifunza katika hili siyo kwamba tunahitaji watu wenye nguvu sana ili waweze kutusaidia. Kanuni ni kwamba kama lengo ni mpango wa Mungu, Mungu mwenyewe atatoa nafasi maalumu mbalimbali katika kukamilisha lengo hilo.
Nehemia alirejea Yerusalemu na kuelezea maono yake kwa viongozi waliokuwepo mahali pale. Maono yalianza na mtu mmoja, lakini mara moja wengine walianza kushiriki. Kiongozi hawezi kutegemea kila mtu awe anayaelewa maono kwa mara moja. Uungwaji mkono huanza na watu wachache.
Ni jambo la muhimu kuwa na watu wachache wa kushirikishana nao maono; vinginevyo, kiongozi atakuwa hamwongozi mtu yeyote. Maono yanapaswa yabebwe na kikundi cha watu walio na msimamo na waliojiachilia kabisa kwa ajili ya maono hayo. Kuwa na maono ni zaidi ya kukubaliana nayo na kutegemea kwamba yataweza kutokea. Watu wanaoshiriki katika maono wanapaswa wajisikie kwamba hayo maono ni mali yao.
Wale waliojitolea kwa maono ya Nehemia waliunda jamii. Walilazimika kujifunza jinsi ya kuishi pamoja, kusaidiana, na kusalia kuwa waaminifu katika maono hayo.
Nehemia ni mfano wa mtu ambaye alifanyika kuwa kiongozi ingawaje hapo awali alikuwa hana jukumu lolote kwa ajili ya haya matatizo. Hakuanza kwa kuwa na nafasi ya uongozi, bali alianza akiwa na dhima ya kufanya mabadiliko. Alikuja kuwa kiongozi kwa sababu ya maono yake.
Mfalme Sauli: Akiongoza kutokea kwenye Nafasi
Sauli alikuwa mfalme wa kwanza wa Israeli. Hangeweza kufuata mfano wowote wa mfalme mtangulizi. Alikuwa mkulima na hakuwa na uzoefu wowote kama mtawala wa aina yeyote ile.
Wakati alipoteuliwa kuwa mfalme, hakukuwepo na jeshi na hakukuwepo na watendakazi wa serikali, hakukuwepo na waamuzi rasmi, hakukuwepo na ofisi za serikali, na hakukuwepo na kodi kwa ajili ya serikali kutumia. Baada ya kuwa ameteuliwa kuwa mfalme, jukumu la Sauli lilikuwa halifafanuliki kiasi kwamba aliendelea kufanya kazi shambani kama mkulima.
Kisha kukatokea mgogoro (1 Samweli 11). Taifa dogo lililokuwa mshirika wa Israeli lilishambuliwa na waliokuwa maadui kwa Israeli. Hakuna hata mtu mmoja aliyekwenda shambani kumwelezea mfalme mpya kuhusu tukio hilo kwa sababu hawakuwa na tegemeo kama ataweza kufanya jambo lolote. Mwishoni mwa siku ndipo Sauli aliposikia taarifa hizo za kushambuliwa alipokuwa anatoka kufanya kazi shambani kwake.
Sauli alichukua hatua za nguvu na maamuzi. Alituma ujumbe katika hali ya kutisha; akatwaa jozi ya ng'ombe wa kulima, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe (1 Samweli 11:7). Jaribu kufikiria mjumbe akiwa anakimbia anawasili nyumbani kwa chifu wa kikabila. Anatupa ardhini mguu wa ng’ombe wenye kutapakaa damu na kutangaza, “Mfalme Sauli anasema kwamba yeyote asiyetoka kuja kusaidia katika tukio hili la dharura ng'ombe zake watatendwa vivi hivi.”
Maelfu ya watu walijitokeza pamoja kusaidia na wakapata ushindi mkubwa. Ushindi huu ulimjenga Sauli kama kiongozi mwenye nguvu.
Sauli ni mfano wa kiongozi aliyeanzia kwenye nafasi ya uongozi. Mwanzoni hakuwa anataka kuwa kiongozi, lakini kwa sababu alikuwa ameshikilia nafasi hii, alijisikia kwamba alikuwa na jukumu la kuwajibika.
► Je, ni kwa jinsi gani uwajibikaji wa Sauli kwenye mgogoro unatofautiana na wa Gideoni?
“Kutembea kwangu ni kwa uwazi hadharani. Biashara yangu iko duniani, na ni lazima niichanganye katika makusanyiko ya watu au niachane na kazi niliyoteuliwa ambayo kwa amri ya Mungu inaonekana alikuwa ameniteua mimi.”
- William Wilberforce
Sifa Bainishi za Kiongozi mwenye Nguvu
Ni kwa jinsi gani unaweza kujitathmini mwenyewe kwamba wewe ni kiongozi mwenye nguvu? Tafakari orodha hii ya sifa bainishi au tabia za kiongozi mwenye nguvu. Kama utajiona wewe ni mdhaifu kwenye baadhi ya sifa hizi bainishi, unaweza ukazikuza kwa msaada wa Mungu. Utakapokuwa unakua katika maeneo haya ya sifa hizi, utakuwa unaimarisha uongozi wako.
Kiongozi mwenye ufanisi…
1. Ana ushawishi kwa watu wake wanaomjua.
2. Ana nidhamu ya binafsi.
3. Ni mtu aliyekwisha kamilisha majukumu ya huko nyuma.
4. Yuko tayari kwa hiari yake kuchukua majukumu mapya ya uwajibikaji.
5. Anayehusiana vizuri na watu.
6. Ana utayari wa kuhudumia watu wengine.
7. Anayeweza kuanzisha jambo mwenyewe.
8. Aliye mwaminifu.
9. Anaweza kushughulikia msongo wa mambo.
10. Siyo mtu anayegubikwa na ghadhabu.
11. Ana roho yenye mtazamo chanya.
12. Ana uwezo wa kustahimili mambo yenye kukatisha tamaa.
13. Yeye ni mtu mwenye kujiamini.
14. Ana uadilifu.
15. Anakua akiwa karibu na Mungu.
16. Hajalemazwa na matatizo yake binafsi.
17. Ana uwezo wa kujifunza na matamanio endelevu ya kuendelea kusoma.
18. Ana uwezo wa kutatua matatizo.
19. Haridhishwi na hali zilizopo za wakati wa sasa.
20. Yuko tayari kufanya mabadiliko.
21. Anaona picha ya mambo makubwa.
22. Anaweza akaona ni mambo gani yanayotakiwa yafanyike baadaye.
Kuanza
Je, vipi kama unafanya kazi katika shirika ambalo wewe siyo kiongozi mkuu?
Je, vipi kama kiongozi wa shirika lako ana mipaka inayomzuia kufuata kanuni za uongozi unazojifunza katika kozi hii?
Wakati mwingine, kijana anayekua katika uongozi anajikuta amechanganyikiwa kwa sababu anajihisi kwamba hawezi akazitumia kanuni za uongozi anazozijua. Anakuwa na hisia kwamba uwezo wake una kikomo kwa sababu hayuko kwenye nafasi ya mamlaka.
Mtu anayetegemea kuwa kiongozi hapaswi angojee hadi awekwe kwenye nafasi ya mamlaka ndiyo aweze kuanza kutumia kanuni za uongozi. Anaweza akatumia kanuni zinazohusiana na ukamilishaji wa majukumu anayotekeleza, kujenga uaminifu, kuongeza ujuzi wake, kufanyia majaribio mambo yanayohitaji ustadi, kutengeneza jinsi ya kupata sifa njema kwa ajili ya kuwa mtu unayetegemewa, na kuonyesha msimamo wake kwa ajili ya mafanikio ya shirika badala ya faida binafsi. Mambo haya yote huongeza ushawishi wake kwa mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na viongozi walioko juu yake.
Kumbuka, kiongozi kwa kawaida ni mtu mwenye ushawishi. Kuna mambo mengi ambayo hukuza ushawishi wako, hata bila ya kuwa kwenye nafasi rasmi.
Usiwe na haraka kufikiri kwamba ni lazima uanze shirika jipya ndiyo uweze kuwa kiongozi. Kuna mambo mengi ya kufanya popote utakapokuwa.
Kwa nafasi yako yeyote ile, unaweza ukawatia moyo na kuwasimamia viongozi vijana na timu za wanachama. Inawezekana jambo hili likafanyika kama sehemu ya kawaida ya kazi yako katika shirika, au inawezekana ikafanyika hata nje ya shughuli zako za kawaida kwa wale wanaothamini msaada wako.
Tafuta kusimamiwa au kuongozwa na watu wengine wa ndani au wa nje ya shirika lako. Viongozi walio wengi wanafurahia kushirikishana hekima zao. Unaweza ukasimamiwa kwenye vipengele maalumu vya uongozi; anayekusimamia siyo lazima awe mfano kamili kwenye kila eneo. Anayekusimamia anaweza hata akawa mdogo kuliko wewe endapo atakuwa ni stadi zaidi kuliko wewe katika baadhi ya maeneo.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili.
Kazi za Kufanya Somo la 4
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Tafakari "Sababu za kumfanya mtu kuwa Kiongozi" na "Sifa bainishi za kiongozi mwenye nguvu" zilizoorodheshwa katika somo hili. Jiandae kuandika sababu na sifa nyingi kwa kukariri bila kunukuu mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kitakachofuata.
4. Kabla ya kuanza kwa kipindi kitakachofuata, soma Yohana 13:1-17. Andika ni nini kifungu hiki kinatueleza kuhusu uongozi.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.