Baadhi ya watu wanaamini kwamba kwa kuwa wote tuna hadhi moja inayofanana mbele za Mungu, hakupaswi kuwepo na mtu yeyote mwenye mamlaka juu ya wengine katika kanisa. Watu wengi wanasema wanaamini katika uongozi, lakini wanafanya au wanatenda kana kwamba wao ni watu walio huru kutoka katika mamlaka yeyote ya kiroho.
► Je, Biblia inafundisha kwamba inapaswa kuwepo na mamlaka kwenye kanisa? Toa mifano.
Biblia inarejea kuwepo kwa mamlaka kwenye kanisa katika maeneo mengi. [1] (Baadhi ya mifano ni Waebrania 13:7, 17; Tito 1:5; Warumi 12:8; 1 Wakorintho 14:40; na 1 Timotheo 5:17.)
Kufafanua uongozi kama ushawishi kunatusaidia sisi kuona majukumu ya uongozi katika kanisa. Baadhi ya majukumu maalumu yamewekwa na Mungu ili kwamba viongozi waweze kupatikana na kupewa nguvu za kuongoza kanisa katika kukamilisha malengo yake.
► Mwanafunzi anapaswa asome Waefeso 4:11-12 kwa ajili ya kikundi.
[2]Siyo majukumu yote maalumu yanayoweza kutambuliwa pamoja na miito maalumu katika orodha hii. Kwa mfano. Mwanamuziki au kiongozi wa ibada siyo mojawapo katika hivi. Hata hivyo, kila jukumu la uongozi wa huduma unapaswa uelekeze fokasi yake katika kulisaidia kanisa kukamilisha malengo yake.
Majukumu ya uongozi hayako tu katika kuhubiri, kufundisha, na uinjilisti. Jukumu la kanisa ni pana kuliko mambo haya. Watu wa kanisa pia hufanya kazi katika kufikia mahitaji ya vitendo. Mtu anayeongoza watu kuchangia vifaa kwa ajili ya kutengeneza bustani analisaidia kanisa katika kukamilisha malengo yake. Majukumu ya kanisa huleta ulazima wa majukumu mengi ya uongozi kuliko yale yanayotokea ndani ya jengo la kanisa.
[1]Kama mtu yeyote katika kikundi atabishana kwamba uongozi katika kanisa siyo muhimu na siyo kibiblia, kikundi kinaweza kuyapima maandiko yaliyoandikwa ndani ya alama za kufunga na kufungua. Jaribu kuepuka kutumia muda mrefu katika jambo hili.
.
“Nilikuwa namwomba Mungu aweze kunisaidia. Kisha nikamwomba kama mimi ninaweza kumsaidia yeye. Niliishia katika kumwomba afanye kazi yake kupitia kwangu.”
Maandiko tunayojifunza katika somo hili yanatumika mahsusi kwa ajili ya wachungaji na mashemasi au wanadaikonia. Hata hivyo, sifa nyingi zinahusiana na tabia, na siyo vipaji. Wakristo wote wanapaswa kuwa na tabia zinazoelezewa hapa. Viongozi wanaweza kuwa wenye mafanikio zaidi kama watakuwa na tabia hizi. Kama utakavyokuwa unaangalia kila ubora wa tabia, jaribu kufikiria ni kwa jinsi gani inaathiri ushawishi wa mtu binafsi.
Mtume Paulo alichagua viongozi kwa ajili ya makanisa mapya kla Ilipotokea kuwepo na vikundi vya watu waliookoka (Matendo 14:23). Wengi wa hawa wachungaji wapya walikuwa ni wale waliokuwa na muda mfupi tu tangu walipookoka. Ni wazi kwamba hawakuwa wameweza kukidhi kwa ukamilifu mahitaji ya hizi sifa zote, lakini Paulo aliweza kuchagua viongozi wazuri kwa kadri walivyokuwa wanaweza kupatikana. Walikuwa ni watu wenye kuwa na uwezo kwa ajili ya maendeleo. Mungu anaweza kumtumia mtu ambaye amekuwa na msimamo kamili kwa Kristo na huduma, hata kama sifa zote zitakuwa bado hazijendelezwa kwa kamilifu wote.
Tuna vifungu viwili vinavyohusiana na sifa za wachungaji na mashemasi. Zilikuwa zimeandikwa na Mtume Paulo kwa Timotheo na Tito. Timotheo alikuwa mwangalizi wa makanisa ya Efeso, na Tito alikuwa mwangalizi wa makanisa ya Krete. Walikuwa na kazi ya kuchagua wachungaji kwa kila kusanyiko la mtaa.
► Mwanafunzi anapaswa asome 1 Timotheo 3:1-7 kwa ajili ya kikundi.
Sifa za Wachungaji
(1) Asiye na lawama
Mchungaji hapaswi kuwa mtu anayeonekana na hatia au anayetenda mambo ya uovu. Mchungaji hawezi kumwongoza mtu mwingine afanye jambo sahihi kama yeye mwenyewe hafanyi mambo yaliyo sahihi. Mchungaji ni lazima awe mtu ameonyesha tabia endelevu ya Kikristo kwa kipindi cha muda mrefu. Jambo hili ni muhimu ili kwamba kanisa liweze kumwamini na kuwa na ushuhuda mzuri katika jumuiya.
Kwenye eneo ambalo kanisa hakijaanzishwa kwa muda mrefu, inawezekana mchungaji akawa hajakaa kwenye Ukristo kwa muda mrefu. Hataweza kuwa na tabia zote za ukomavu, lakini anapaswa aonyeshe maisha ambao yanaonyesha msimamo wake kwa Mungu. Atapaswa awe tayari kwa hiari yake mwenyewe kukiri makosa na kufanya masahihisho ya tabia yake mwenyewe.
Kwa miaka mingi, mchungaji mmoja kule Asia alikuwa anatumiwa sana na Mungu katika kijiji kimoja. Mafanikio yake yalimwingiza kwenye jaribu la kuwa na majivuno na uzembe katika mambo ya kiroho. Siku moja usiku mwanamke mmoja akamwomba waende pamoja naye kwenye pikipiki yake. Kwa ujinga wake alikubaliana naye, ingawaje alijua wazi kwamba itamsababisha kuingia kwenye majaribu na kwamba ingeweza ikamharibia hadhi yake kwenye jamii. Wanachama wake walipopata habari za kitendo chake, walipoteza matumaini yao katika uadilifu wake. Hatimaye ilimbidi ajiuzulu kutoka katika huduma yake. Kwa neema ya Mungu, mchungaji huyu alijinyenyekesha mbele za Mungu na wale watu aliokuwa amewaumiza. Alikubaliana na adhabu ya nidhamu kutoka kwa mwangalizi wake wa kiroho. Hatua kwa hatua, uaminifu kwake ulirejeshwa tena, na mafanikio yake katika huduma yake yaliongezeka.
► Je, ni kitu gani kinatokea ikiwa kiongozi haaminiki?
(2) Mume wa mke mmoja
Katika maeneo mengi ya dunia, ndoa ya wake wengi imekuwa desturi ya kawaida. Mpango wa Mungu ni mwanamume kuwa na mke mmoja. Wachungaji wanapaswa kuwa mfano huo. Sharti hili linaonyesha kwamba mchungaji anapaswa kujitahidi kuwa mume bora kwa kadri inavyowezekana. Anapaswa awe mwaminifu na mwenye upendo kwa mke wake.
(3) Mwenye kiasi
Mchungaji anaweza kufananisha na mchungaji wa kondoo anayelinda kundi lake. Mchungaji ndiye mlinzi wa kusanyiko lake. Anapaswa awe makini na mafundisho ya dini ya uongo na ushawishi mbaya. Ni lazima awafundishe watu wake ili waweze kuwa salama katika mafundisho yao mbalimbali ya imani. Ni lazima awe tayari kuwaonya watu wake kuhusiana na hatari yeyote ya kiroho. Hapaswi kuruhusu mafundisho ya imani yenye kuhatarisha yafundishwe ndani ya kanisa.
Mchungaji ni lazima awe makini kuhusiana na huduma yake. Hapaswi awe mtu anayelipuka ambaye hufanya maamuzi ya pupa au ya haraka sana. Anapaswa awe na uwezo wa kufikiri akiwa ametulia kuhusu masuala nyeti. Hapaswi kuruhusu akili yake ivurugwe na mambo ya binafsi, starehe, au majaribu.
(5) Anayeheshimika
Mchungaji anapaswa awe na tabia ya utaratibu. Hapaswi kuonyesha tabia ambayo haistahili. Tabia inapaswa iende sambamba na kanuni za kiungu ambazo anafundisha.
Anapaswa ajifunze jinsi ya kuonyesha heshima na unyenyekevu kwa misingi ya tamaduni za mahali ambapo huduma yake ipo. Kama atajitambua kwamba ametenda kosa ambalo limemfanya akawa amemkosea mtu mwingine, atapaswa awe mnyenyekevu na mwenye kuomba msamaha.
(6) Mkarimu
Kuwa mkarimu kunamaanisha kutimiza mahitaji ya mtu anayesafiri na anayehitaji chakula na malazi. Mchungaji anapaswa kuwa mtu anayejali mahitaji ya wengine. Anapaswa kuwa tayari kushiriki. Anapaswa kuwa mkarimu na msaidizi hata kwa watu anaokutana nao kwa mara ya kwanza.
► Kwani nini ubora huu ni muhimu kwa kiongozi?
(7) Ajuaye kufundisha
Mchungaji ni lazima awe na uwezo wa kuelezea ukweli ili watu waweze kuulewa. Ni lazima achukue jukumu la kusoma na kujielimisha yeye mwenyewe.
(8) Asiwe mlevi
Mchungaji asiruhusu yeye mwenyewe kushawishiwa na vinywaji vya kulevya. Hapaswi kamwe kufanya kama mtu ambaye amedhurika na ulevi. Kanuni hii inahusiana na kitu kingine chochote ambacho kina madhara yanayofanana.
(9) Asiwe mkali bali awe mpole
Mchungaji asitake kupeleka suala kwa njia vitisho vya kutumia nguvu. Hapaswi kuwa tayari kumwumiza mtu yeyote anayemuudhi au anayemkosea (Ona pia 2 Timotheo 2:24-25).
► Je, ni njia zipi sahihi kwa mchungaji za kuweza kuonyesha aina sahihi ya hasira au ghadhabu anayoweza kuwa nayo?
(10) Asiwe mgomvi wala mpenda fedha
Watu wa dunia hii hubadili yale wanayozungumza kwa ajili ya faida. Watu kwenye nafasi zao mbalimbali kama wanasheria, wafanyabiashara, au wanasiasa wanajaribiwa kuubadili ukweli kwa ajili ya kuwafurahisha watu. Mchungaji pia hujaribiwa, kwa sababu ukweli wa Neno la Mungu haumfurahishi kila mtu. Mchungaji ni lazima awe mwaminifu kwenye ukweli aidha kama unamfaidisha kifedha au laa.
Mchungaji atapenda kuona huduma ya kanisa ikiwezeshwa kifedha. Ni lazima aongoze kanisa kufanya kazi kama familia inayojali kwa ajili ya wanachama wake, kuliko kila siku kufikiria ni nini watakachoweza kumpa.
(11) Aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri
Uwezo wa mchungaji wa uongozi ni lazima uthibitike kuanzia nyumbani. Atapaswa awe na uongozi kwa watoto wake. Kama hawezi kuiongoza nyumba yake mwenyewe, hatakuwa na uwezo wa kuliongoza kanisa. Haimaanishi kwamba watoto wake lazima wawe na tabia kamilifu, bali kwamba mchungaji anawaongoza na kuwarekebisha kwa uaminifu. Hii haijumuishi watoto ambao wameshakuwa watu wazima wwanaojitegemeza wenyewe na ambao hawako kwenye mamlaka yake kwa sababu bado hawawajibiki kwa ajili yao tena.
(12) Asiwe mtu aliyeokoka karibuni.
Kama mtu atawekwa kwenye nafasi ya mamlaka kwa haraka sana, ni rahisi kushawishika kuwa na kiburi. Kiburi ndiyo dhambi iliyomsababisha Shetani kuanguka. Upandishwaji kwenye ngazi nyingine ya mamlaka unapaswa ufanyike polepole ukiambatana na uzoefu.
► Je, kunakuwa na uharibifu gani kama atawekwa kwenye mamlaka kwa haraka na akawa hafanyi vizuri?
(13) Awe na sifa njema
Kabla mtu hajateuliwa kuwa mchungaji, ni lazima awe mtu mwenye sifa njema miongoni wa watu nje ya kanisa. Wanapaswa waelewe kwamba ni mtu wa ukweli na mwaminifu katika yote ayafanyayo. Kama atakuwa ni mtu ambaye hakuwa na sifa nzuri kabla ya kuokoka, patahitajika awe na muda maalumu wa kutengeneza sifa zake kabla hajafanyika kuwa mchungaji. Mchungaji mmoja barani Afrika alihubiri mahubiri yake ya asubuhi ya Jumapili, kisha akapanda basi kurejea nyumbani. Baada ya kulipa nauli, aligundua kwamba kondakta alikuwa amemrudishia chenji nyingi kuliko inavyostahili. Kwa kuwa yule mchungaji alikuwa mtu mwenye uadilifu wake, alimrejeshea fedha ya ziada aliyokuwa amerudishiwa kwenye nauli na kondakta akisema, “Nisamehe sana bwana, kwa bahati mbaya umenirejeshea salio la ziada katika nauli yangu. Kondakta alimjibu, “Hapana, sijafanya hivyo kwa bahati mbaya. Nilikuwa nimesimama kando ya kanisa lako nikasikia mahubiri yako yaliyohusiana na kuwa mwaminifu. Niliamua nione kama unayaishi yale unayohubiri! Biblia inasema kwamba heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi (Mithali 22:1). Kwa hiyo, umaskini mkubwa sana ambao mtu anaweza kuwa nao ni umaskini wa kuwa na jina lenye maswali mengi. Ni nini kinachojitokeza kwenye akili za watu wengine wakati jina lako linapokuwa limetajwa?
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Tito 1:5-11 kwa ajili ya kikundi.
Sifa nyingi za mchungaji zilizoorodheshwa katika Tito pia zimeorodheshwa kwenye kifungu cha kuanzia 1 Timotheo.
► Je, kuna sifa gani nyingine za ziada za mchungaji zilizoko kwenye kifungu kilichoko katika Tito?
Kifungu kinasisitiza juu ya uwezo wa mchungaji kuweza kuwajibika dhidi ya mafundisho potofu ya imani. Mchungaji ni lazima awe ameelimishwa vizuri na kwa upeo mkubwa kuhusu mafundisho ya imani ya kweli na awe na uwezo wa kuyaelezea kwa ushawishi mkubwa. Lengo ni ili kuwasahihisha wale walioko kwenye mafundisho ya imani potofu, na jambo lililo muhimu zaidi ya hapo, ni kulilinda kusanyiko katika kuingizwa kwenye upotofu. Mchungaji ambaye hajapata elimu ya kutosha atapaswa aongezee ufahamu wake kwa njia ya kujifunza.
“Nipe wahubiri mia moja wasiokuwa na hofu ya jambo lolote isipokuwa dhambi na wasiotamani kitu chochote isipokuwa Mungu… hao peke yake watatingisha malango ya kuzimu na kuanzisha ufalme wa Mungu juu ya dunia.”
- John Wesley
Sifa za Mashemasi
Mwanafunzi atapaswa kusoma Matendo 6:1-6 kwa ajili ya kikundi. Je, kuna tatizo gani lililoelezwa kwenye kifungu hiki?
Mashemasi wa mwanzo walichaguliwa mara tu baada ya Pentekoste. Mitume walihitaji kuwa na fokasi yao kwenye maombi na kuhubiri. Watu wapatao saba waliteuliwa katika mambo ya kulisimamia kanisa.
Shemasi humsaidia mchungaji katika mambo yote yanayohusiana na huduma ya kanisa. Shemasi anaweza akawa ni mhubiri, lakini pia siyo lazima.
► Je, sifa za mashemasi wa mwanzo zilikuwa ni nini?
Sifa za mashemasi wa mwanzo zilikuwa kwamba walikuwa na sifa ya uaminifu, waliojazwa na Roho Mtakatifu na hekima. Wangeweza kusimamia pesa za kanisa, hivyo sifa ya uaminifu ilikuwa ni muhimu. Kazi zao zingekuwa na matokeo ya kiroho katika kanisa, hivyo ilikuwa muhimu kwao wajazwe na wamejazwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kupata uongozi wake, kupokea upako, na usafi. Walishughulika na hali nyingi zilizokuwa ngumu, kwa hiyo hekima ilikuwa jambo la muhimu.
Mtume Paulo aliorodhesha baadhi ya sifa kwa ajili ya mashemasi:
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Timotheo 3:8-13 kwa ajili ya kikundi.
(1) Anayeheshimika
Shemasi anapaswa awe mtu ambaye anaheshimika kwenye mahusiano yake na familia, marafiki, na jumuiya.
(2) Awe mkweli
Shemasi anapaswa awe mtu ambaye anaaminika katika yale anayosema. Atasikia malalamiko kuhusu watu ndani ya kanisa na atasikia maoni mengi sana kuhusu matatizo ndani ya kanisa. Anapaswa awe mtu ambaye ni mkweli.
(3) Wasiokuwa walevi
Shemasi hapaswi awe mtu ambaye amedhurika na ulevi. Tabia yake inabidi iwe ya kuheshimika na iliyo thabiti.
(4) Wasiotamani faida isiyo halali
Shemasi atawajibika kutunza fedha kwa ajili ya kanisa na kujali mahitaji ya watu walioko ndani ya kanisa. Hapaswi awe mtu ambaye anajaribu kujipatia faida yeye mwenyewe kutoka katika huduma yake.
(5) Wanaoishika mafundisho mazuri kwa dhamiri njema
Wakati mtu anapoanguka katika dhambi, mara nyingi huanza kuamini mafundisho potofu ya imani. Kama mtu anaishi kwenye ushindi wa kiroho, atakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushikamana na mafundisho ya kweli ya imani.
(6) Wapimwe kwanza uwezo wao
Kabla mtu hajapewa nafasi ya kuwa Shemasi, anapaswa awe na nafasi ya kuonyesha kwamba ana hekima na ni mwaminifu katika huduma. Viongozi wenye hekima watawapa watu wao nafasi za kutumika kabla ya kuwapa nafasi za mamlaka.
► Je, kuna mifano gani ya njia ambazo mtu anaweza kusaidia huduma ya kanisa bila ya kuwa amepewa nafasi ya mamlaka?
(7) Wawe na wanawake wenye heshima.
Huduma ya Shemasi inapata madhara kama mke wake atakuwa ni mtu wa umbeya na siyo mfano wa Mkristo mwema.
(8) Aweze kusimamia nyumba yake vyema
Kama ilivyo kwa mchungaji, Shemasi anapaswa aweze kuimiliki familia yake vyema.
Sifa za Mchungaji Anayeliongoza Kanisa Vizuri
► Jadili umuhimu wa kila sifa, ukianzia na swali, “Je, kwa nini sifa hii ni muhimu?”
1. Uaminifu wake haujagawanyika kwa mashirika mengine.
2. Yuko tayari kujenga timu ya huduma na kutumia uwezo na vipaji vya watu wengine.
3. Anaongoza kusanyiko lake kushirikishana maisha kama familia ya kiroho, inayowajibika na mahitaji yote.
4. Analihudumia kanisa lake kwa upendo kwa ajili ya Mungu na watu, na siyo kwa ajili ya faida binafsi.
5. Vipaumbele vya kiroho kama vile ibada, uinjilisti, na kukua kiroho ni fokasi ya huduma yake.
6. Ana uaminifu na kujiamini na watu wake.
7. Yuko tayari kulijenga kanisa kama taasisi ya kudumu ambayo siyo mali yake
8. Analiongoza kanisa katika kukua, akifundisha kuhusu zaka na ushirika wenye kujali mahitaji ya wengine.
9. Ni mkweli katika mambo yote, ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha.
10. Anaonyesha uwezo wa kumiliki fedha pamoja na watendakazi.
Sifa za Kiongozi wa Mradi wa Huduma
Mtu anayechaguliwa kuongoza mradi wa biashara wa kanisa anapaswa awe na sifa hizi. Viongozi wa kanisa wanapaswa wafanye kazi ya kukuza sifa hizi kwa wanachama wake ambao wataweza kusaidia katika jukumu la kanisa na waingizwe kwenye timu ya viongozi.
► Jadili umuhimu wa kila sifa, ukianzia na swali, “Je, kwa nini sifa hii ni muhimu?”
1. Ni mwaminifu kwa kanisa la mtaa kwa mahudhurio yake, hutoa zaka, anashiriki na anao ushuhuda wa Kikristo unaoaminika.
2. Tayari anakuwa amewekeza juhudi zake na shauku yake katika kanisa la mtaa.
3. Anao uaminifu wa kutosha na hisia ya hali ya juu ya maadili.
4. Tayari anakuwa ameshaonyesha uwezo wa kuanzisha mambo na motisha wa kufanya vizuri kwa kadri inavyowezekana.
5. Binafsi ni mtu mwenye nidhamu, amehamasika, na siku zote akiendelea kuwa mzuri zaidi.
6. Anadhihirisha uwezo wake na kipaji cha kupanga na kuwaongoza watu wengine, siyo tu uwezo wa kufanya kazi wakati anapoelekezwa na mtu mwingine.
7. Anao uzoefu wa kutosha wa kutekeleza jukumu lake linalomhusu katika huo mradi.
Ruhusu baadhi ya wanafunzi washirikishane kuhusu ni kwa jinsi gani wanategemea kubadilisha malengo au matendo yao kutokana na somo hili.
Muhtasari wa Taarifa Tano.
1. Mungu amelisimika kanisa lifanye kazi chini ya uongozi wa kiroho.
2. Majukumu mengi ya uongozi yanahitajika kwa ajili ya majukumu ya kanisa.
3. Sifa nyingi kwa ajili ya uongozi zinahusiana na tabia nzuri.
4. Mchungaji au kiongozi wa huduma nyingine anapaswa bila kikomo akuze sifa nzuri endelevu.
5. Kiongozi wa huduma anahitaji kutegemewa, motisha na uaminifu.
Kazi za kufanya Somo la 2
1. Andika aya inayotoa muhtasari wa dhana ya kubadilisha maisha kutoka katika somo hili. Elezea kwa nini ni muhimu. Je, ni jambo gani zuri linaloweza kufanywa? Je, ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwa kutojua?
2. Elezea ni kwa jinsi gani unavyoweza kutumia kanuni zilizoko katika somo hili kwenye maisha yako mwenyewe. Je, ni kwa jinsi gani somo hili linabadilisha malengo yako? Je, ni kwa jinsi gani umejipanga kubadilisha matendo yako?
3. Fanya kukariri Taarifa Tano kwa Muhtasari zilizoko katika somo la 2. Kuwa tayari kuziandika bila ya kunakili kutoka katika kumbukumbu za ufahamu wako mwanzoni mwa kipindi kinachofuata cha darasa.
4. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa soma 1 Samweli 2:12-36. Andika uchunguzi wako kuhusu uongozi wa Eli.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.