Nguvu ya Mawasiliano
"Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha." (Mithali 25:11). Neno sahihi linenwalo kwa wakati wa kufaa, na kunenwa vizuri, ni kazi ya sanaa. Kuwasiliana vizuri ni ujuzi unaoweza kustawishwa.
Watu hupata hisia zao za akili yako, kujiamini na vipaji yako kutokana na uwezo wako wa kuwasiliana. Ufanisi wako katika huduma unategemea ustadi wako ulio nao wa kuwashawishi watu wengine.
Huduma nyingi huwa zina mawasiliano. Kuhubiri, kufundisha, kushauri, na kutia moyo yote haya yanafanyika kwa njia ya mawasiliano. Viongozi wengi wa huduma ni wazungumzaji wazuri. Ni jambo lisilokuwa la kawaida kwa mtu ambaye siyo mzungumzaji mzuri kuweza kuwa kiongozi mwenye ufanisi.
► Kuna msemo wa zamani unaosema, “Kalamu ina nguvu kuliko upanga.” Unadhani msemo huu unamaanisha nini?
Nguvu za kimwili haziwezi kulinganishwa na wazo lililowasilishwa kwa ufanisi. Silaha hulazimisha watu kufanya jambo fulani, lakini wazo hupata nyoyo na akili zao. Hii ndiyo sababu baadhi ya serikali zilizopo madarakani zinazuia uhuru wa kuongea.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Yakobo 3:1-8 kwa ajili ya kikundi. Jadili kifungu hiki kinasema nini kuhusiana na nguvu ya mawasiliano.
Kifungu katika Yakobo kinazungumzia zaidi juu ya uwezekano wa ulimi kusababisha madhara. Nguvu ya mawasiliano inaweza ikatumika kwa mambo mema au mambo ya kuleta madhara. Mungu alichagua mawasiliano ya kibinadamu, yanayowezeshwa na kutiwa nguvu na Roho Mtakatifu, kama njia ya kukamilisha mpango wake wa wokovu.
Kwa sababu ya nguvu ya mawasiliano, Mkristo anapaswa siku zote aitumie kwa uangalifu mkubwa. Kama mnenaji, unapaswa ufuate maadili ya Kikristo. Siku zote unatakiwa uwe katika upande wa ukweli. Kamwe usipende kulikuza jambo ambalo wewe huna imani nalo. Kamwe usijaribu kuwamiliki au kuwadhibiti watu kwa kuwaambia mambo ambayo kwa uhakika siyo ya kweli, au ukajizuia kutoa taarifa ambayo ingekuwa muhimu kwao.