► Someni 2 Yohana pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu umuhimu wa kanuni za asili za kanisa?
Asili ya Kanuni za Imani
Kanuni ya imani ni muhtasari wa kanuni za msingi za Kikristo. Kanisa la awali liliona haja ya kufanya muhtasari wa kanuni za Biblia.
► Je, kwa nini kanisa lilihitaji kanuni za imani? Biblia haikutosha?
Siku zote kuna watu wanaodai kuamini Biblia ilhali wanafundisha kanuni zinazopingana na Biblia. Kanisa lilibuni kauli za kanuni za Biblia ambazo zilitofautisha Ukristo halisi na kanuni za uongo. [1]
Mojawapo ya kauli za kwanza za kanuni ilikuwa “Yesu ni Bwana,” ambayo ilimaanisha kwamba Yesu ni Mungu. Maneno, Bwana Yesu Kristo pia yalitoa kauli, yakisema kwamba
Yesu ndiye Masihi (Christos) na kwamba yeye ni Mungu. Mtu aliyekataa kusema kwamba Yesu ni Bwana au kutumia maneno Bwana Yesu Kristo alichukuliwa kuwa si muumini.
Baadaye kulikuwa na watu waliodai kuwa Wakristo lakini hawakuamini kwamba Yesu kweli alikuwa mwanadamu. Ndio maana katika waraka wa 1 Yohana tunapata kanuni hii ya imani, “Kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu” (1 Yohana 4:2-3). Mtume pia alisema kwamba mtu akikana kanuni za msingi za Kristo, anafanya dhambi na si wa Mungu (2 Yohana 1:9).
Kanuni ya imani ya kale zaidi inayotoa kauli kadhaa iko katika 1 Timotheo 3:16:
Mungu alidhihirishwa katika mwili, akajulika kuwa na haki katika roho, akaonekana na malaika, akahubiriwa katika mataifa, akaaminiwa katika ulimwengu, akachukuliwa juu katika utukufu.
Hatujui masuala yote yaliyokuwa yanashughulikiwa na kanuni ya imani ya 1 Timotheo, lakini inasisitiza uungu na ubinadamu wa Yesu inaposema kwamba Mungu alidhihirishwa katika mwili.
Kauli hizi fupi za imani zilitimiza kusudi fulani. Ikiwa Mkristo wa awali angekutana na mtu mwingine aliyedai kumwamini Yesu, Mkristo huyo angeweza kuuliza, “Je, unaamini kwamba Yesu ni Bwana?” au “Je, unaamini kwamba Yesu ni Mungu aliyekuja katika mwili?” Ikiwa mtu huyo angesema “hapana,” basi Mkristo huyo alijua kwamba mtu huyo hajui au hakubali yale ambayo Yesu na mitume walifundisha.[2]
[3]Katika karne chache za kwanza baada ya Pentekoste, kanisa liliona ni muhimu kutoa kauli za wazi kuhusu Utatu wa Mungu, umwilisho wa Kristo, na utambulisho wa Roho Mtakatifu. Waliweka viwango vya kanuni kama kinga dhidi ya mafundisho potovu. Kanuni za imani zilikusudiwa kuwa mihtasari ya kweli za msingi ambazo kila Mkristo aliamini.
Kanuni hizo za imani hazingeweza kuzingatia kila suala, lakini mtu hangechukuliwa kuwa Mkristo ikiwa angekana chochote katika kanuni hizo za imani za kale. Zilikuwa ni jaribio la kufafanua imani ya Kikristo.
[2]Atanasi, aliyeishi takriban miaka ya 296-373, aliandika makala maarufu kwa jina “Kuhusu Umwilisho,” ambapo alieleza kwa nini uungu kamili na ubinadamu kamili wa Yesu ulikuwa muhimu sana kwa imani ya Kikristo. Alikuwa na ushawishi mkubwa katika Baraza la Nisea, ambalo lilitoa Kanuni ya Imani ya Nisea.
“Inahitajika kwa ajili ya wokovu wa milele kwamba mtu pia aamini ipasavyo umwilisho wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa maana imani sahihi ni kwamba tuamini na tukiri kwamba Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ni Mungu na Mwanadamu.”
Kanuni ya Imani ya Atanasi
Kanuni ya Imani ya Mitume
Kanuni ya Imani ya Mitume haikuandikwa na mitume, lakini iliandikwa katika karne ya pili ili kueleza kanuni za mitume.
Namwamini Mungu Baba mwenyezi, Muumba wa mbingu na nchi;
Namwamini Yesu Kristo Mwana wake wa pekee, Bwana wetu. Aliyechukuliwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na akazaliwa na Bikira Mariamu. Aliteswa mikononi mwa Pontio Pilato, akasulibiwa, akafa, akazikwa. Akashuka kuzimu. Siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu. Akapaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba Mwenyezi; kutoka huko atakuja kuwahukumu watu walio hai na waliokufa.
Namwamini Roho Mtakatifu, kanisa Takatifu Katoliki, ushirika wa watakatifu, ondoleo la dhambi, kufufuliwa kwa mwili, na Uzima wa milele. Amina.
Inaonekana kwamba kanuni hii ya imani ilikusudiwa kufichua makosa ya wale waliokana kwamba Yesu kweli alikuwa mwanadamu na alizaliwa na bikira. Pia kulikuwa na wengine waliokana kwamba Yesu alikufa kweli au kwamba alifufuka kimwili kutoka kwa wafu.
Machache sana yanasemwa kuhusu Roho Mtakatifu katika Kanuni ya Imani ya Mitume. Hiyo si kwa sababu kanisa halikujua Roho Mtakatifu ni nani; ni kwa sababu mafundisho potovu kuhusu utambulisho wake bado hayakuwa yanaleta changamoto kwa kanisa.
Neno katoliki linamaanisha “ya dunia nzima” ambayo inamaanisha kwamba kuna kanisa moja la kweli.
“Msamaha wa dhambi” unamaanisha wokovu kwa neema badala ya matendo au desturi.
Kanuni ya Imani ya Nisea
Kanuni ya Imani ya Nisea ilizinduliwa katika baraza la kanisa mwaka 325. Kusudi lake lilikuwa kulinda kanuni ya uungu wa Kristo na Roho Mtakatifu. Kauli chache ziliongezwa katika baraza lingine mwaka 381. Kanuni hii ya imani hii inashughulikia masuala ambayo hayakuwa yameibuka hapo awali.
Tunamwamini Mungu mmoja, Baba Mwenyezi, Muumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.
Tunamwamini Bwana mmoja, Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, aliyezaliwa kutoka kwa Baba kabla ya enzi zote, Mungu kutoka Mungu, yu Nuru kutoka Nuru, yu Mungu kweli kutoka Mungu kweli; aliyezaliwa bila kuumbwa; mwenye uungu mmoja na Baba. Kupitia yeye huyu vitu vyote viliumbwa. Aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu na kwa ajili ya wokovu wetu; akatwaa mwili kwa uweza wa Roho Mtakatifu na Bikira Mariamu, akawa mwanadamu. Akasulibiwa kwa ajili yetu mikononi mwa Pontio Pilato; aliteswa, akafa, akazikwa. Siku ya tatu akafufuka kama yanenavyo Maandiko Matakatifu. Akapaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Baba. Naye atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu walio hai una wafu. Na ufalme wake hauna mwisho.
Tunamwamini Roho Mtakatifu, Bwana, mtoa uzima. Anatoka katika Baba na Mwana, anaabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Alinena kwa vinywa vya manabii.
Tunaamini Kanisa moja takatifu la katoliki na la kitume. Tunakiri ubatizo mmoja kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Tunatazamia ufufuo wa wafu, na uzima wa ulimwengu unaokuja. Amina.
► Je, ni yapi baadhi ya mambo unayoyaona katika kanuni hii ya imani ambayo hayakuwa katika Kanuni ya Imani ya Mitume?
Hapa tunaona kauli zilizofafanuliwa kuhusu nafsi zote tatu za Utatu wa Mungu. Uungu kamili wa Kristo unasisitizwa kwa njia ya kuulinda dhidi ya wale wanaodai kuamini kwamba Yesu ni Mungu na bado wanadidimisha uungu wake. Yeye ni wa milele (tangu kabla ya enzi zote), hajaumbwa, na ana asili moja na Baba. Yesu anapaswa kuitwa Mungu kwa sababu zile zile zinazofanya Baba aitwe Mungu.
Roho Mtakatifu anapaswa kuabudiwa kama Baba na Mwana, ambayo inathibitisha kwamba yeye ni Mungu.
Kanuni ya Imani ya Chalsedonia
Kanuni ya Imani ya Chalsedonia iliandikwa mwaka 451. Kusudi lake lilikuwa kulinda kanuni ya umwilisho wa Kristo. Lengo la waandishi lilikuwa kulinda kanuni ya uungu kamili na ubinadamu kamili wa Kristo, bila kipengele chochote kati ya hivyo viwili kudidimishwa sana kiasi cha kukifanya kiwe hakina maana.
Mwishowe waandishi walisema kwamba walichukulia kwamba kanuni hizo zina msingi wa kimaandiko na zimekuwa sehemu ya desturi za kanisa. Hawakuwa wanakuza mawazo mapya bali walikuwa wanatetea kile ambacho kanisa limekuwa likiamini siku zote.
Kwa hivyo, tukiwafuata baba watakatifu, sote tunaungana katika kufundisha kwamba tunapaswa kumkiri Mwana mmoja, Bwana wetu Yesu Kristo, mtu yule yule mkamilifu katika uungu na pia mkamilifu katika ubinadamu; Mungu kweli na mwanadamu kweli, mwenye nafsi ya kimantiki na mwili. Yeye ni mwenye asili sawa na Baba kulingana na uungu wake, na ni mwenye asili sawa na sisi kulingana na ubinadamu wake, kama sisi katika mambo yote, lakini bila dhambi. Kabla ya wakati, alizaliwa kutokana na Baba kulingana na uungu wake. Katika siku za mwisho, kwa ajili yetu na kwa ajili ya wokovu wetu, alizaliwa na Bikira Mariamu, mama ya Mungu kulingana na ubinadamu wake. Yeye ni Kristo, Mwana, Bwana, na mzaliwa wa pekee yule yule, ambaye anajulikana katika asili mbili ambazo hazipaswi kukanganywa, hazibadiliki, haziwezi kugawanywa, na hazitenganishwi. Tofauti kati ya asili zake haiharibiki hata kidogo kwa sababu ya muungano wao, badala yake, sifa za kila asili zimehifadhiwa, na hutokea kwa wakati mmoja katika mtu mmoja na katika uhai mmoja, ambao haujatenganishwa au kugawanywa katika nafsi mbili, bali yeye ni Mwana mmoja, na mzaliwa wa pekee, Mungu Neno, Bwana Yesu Kristo. Hivyo ndivyo manabii walivyonena juu yake tangu mwanzo, na ndivyo alivyotufundisha Yesu Kristo mwenyewe, na Baraza la akina baba limetukabidhi imani.
► Je, unaona mambo fulani yaliyosisitizwa katika kanuni hii ya imani?
Uungu wa Kristo haikuwa sifa ambayo Yesu alikuwa nayo mbinguni tu lakini si duniani. Wakristo wa awali waliamini kwamba Yesu kweli alikuwa Mungu katika mwili. Alikuwa na sifa za Mungu na za mwanadamu kikamilifu alipokuwa duniani. Walichukulia asili hiyo ya Kristo kuwa sifa yake ya kipekee iliyomwezesha kuhitimu kama Mwokozi.
Karne nyingi zimepita tangu kanisa lianze. Ulimwengu umebadilika kwa njia nyingi. Imani nyingi za kidini zimesitawi.
Watu wengine wanafikiri kwamba hakuna kanuni ambazo ni lazima zibaki vile vile. Wanahisi wako huru kuamini chochote wanachotaka na bado wajiite Wakristo.
► Je, ni muhimu kwetu kuamini kanuni za imani za kale za kanisa?
Mungu wa Biblia, aliyeelezwa katika kanuni za imani za kale, habadiliki. Wakristo wa mapema walijua kwamba Mungu aliwaokoa kwa sababu ya itikio lao la imani kwake. Kauli hizi kuhusu asili ya Mungu na njia za wokovu zilikuwa ni Ukristo wa msingi tangu mwanzo.
Inawezekana mtu kuokoka bila kujua kanuni hizi zote au kuzielewa kwa usahihi. Si kanuni zote ni muhimu kwa injili. Mtu hawezi kukana kile anachojua ni kweli na bado awe Mkristo, lakini anaweza kukosea katika mambo fulani.
Kanuni za imani za kale katika somo hili zinazungumza tu kuhusu kanuni za msingi. Ikiwa kanisa fulani lina mtazamo wa Mungu ambao ni tofauti na kanuni hizi za msingi, lazima pia wabuni njia tofauti ya wokovu, ambayo ni injili nyingine. Wakifanya hivyo, hawapaswi kujiita Wakristo kwa sababu wanabuni dini mpya.
Bila shaka, kila mtu yuko huru kufikiria kile anachotaka, lakini ikiwa hafuati kanuni za Kikristo, yeye si mfuasi wa kweli wa Yesu.
Katika karne chache za kwanza hapakuwa na madhehebu kama tulivyo nayo leo. Kulikuwa na kanisa moja. Kwa hivyo kanuni za imani zilikuwa ni kauli za kanisa zima. Leo, makanisa yanayoheshimu mamlaka ya Biblia yanashikilia imani ya kanuni za imani, ingawa hayakubaliani katika masuala mengine mengi.
Kanisa la awali lilijua kwamba kuwa na uhusiano na Mungu ndio jambo la muhimu zaidi. Walijua kwamba waliokolewa kupitia uhusiano wao na Mungu. Ndio maana ilikuwa muhimu sana kwao kuhakikisha kwamba wanajua jinsi Mungu alivyo.
Kitabu cha Yuda kinatuonya kwamba ni lazima tutetee imani iliyopewa kanisa hapo mwanzoni (Yuda 1:3). Mungu na autie mafuta ukweli wake tunapohudumu kwa uaminifu katika kuhubiri injili, kuwafundisha waumini, na kuwafundisha wale anaowaita katika huduma.
“Lakini kanuni yoyote mpya lazima iwe potovu; kwani dini ya zamani ndio dini pekee ya kweli; na hakuna kanuni inayoweza kuwa sahihi, isipokuwa iwe lile lile ‘iliyokuwako tangu mwanzo.’”
John Wesley
“Kuhusu Dhambi Katika Waumini”
Makosa ya Kuepuka: Kiburi cha Kidhehebu
Kundi la makanisa lililounganishwa katika shirika moja linaitwa dhehebu. Kuna maelfu ya madhehebu ambayo yanadai kuwa ya Kikristo. Pia kuna maelfu ya makanisa huru ambayo si sehemu ya dhehebu lolote.
Wakati mwingine madhehebu huanza na uinjilisti. Ikiwa kuna waongofu wengi katika eneo fulani, na hakuna dhehebu linalowatunza, dhehebu jipya linaweza kujitokeza. Dhehebu linaweza kuanza kutokana na kazi ya shirika la misheni katika nchi.
Wakati mwingine dhehebu huanzishwa na kundi la watu wanaoamini kwamba kanuni muhimu inakanwa au kupuuzwa na kanisa lao. Wanaanzisha dhehebu jipya wakiwa na nia ya kuwa sahihi kikanuni. Kadiri muda unavyozidi kupita, wanaendelea kukuza kanuni zao. Kwa sababu wanaelewa Biblia kwa njia tofauti na vikundi vingine vya Wakristo, baadhi ya kanuni zao ni tofauti na madhehebu mengine.
Madhehebu pia hukuza desturi kuhusu aina sahihi za ibada na mambo ya maisha ya Kikristo. Madhehebu hutofautiana katika desturi zao.
Madhehebu mengi ya Kikristo hayadai kuwa kanisa pekee la kweli. Ikiwa shirika fulani linadai kuwa kanisa lote la Mungu duniani, halipaswi kuaminiwa.
Wasioamini mara nyingi hupinga Ukristo kwa sababu ya migawanyiko yake na aina mbalimbali za Ukristo zilizopo. Wasioamini hufikiri kwamba madhehebu mbalimbali ya Ukristo yote yanapingana. Watu wengi ulimwenguni hufikiri kwamba kuna kiwango kidogo cha umoja miongoni mwa Wakristo.
Dhehebu au kanisa la kieneo ambalo kweli ni la Kikristo huamini kanuni za imani za Kikristo za kale. Huo ndio umoja wa kikanuni uliopo miongoni mwa mashirika yote ya Kikristo. Kuna maoni mengi mbalimbali katika masuala madogo ya kikanuni na desturi, lakini hatupaswi kusema kwamba kanisa fulani si la Kikristo kweli kwa sababu ya tofauti hizo.
Makosa ya Kuepuka: Kutoelewa Masadikisho ya Kibinafsi
Mkristo anapoishi katika uhusiano na Mungu, anakuza uelewa wake wa ukweli wa Biblia. Hatafikia mahitimisho sawa na wengine siku zote. Kadiri anavyotumia ukweli katika maisha ya kila siku, atakuza kanuni na sheria kwa ajili yake mwenyewe ambazo zitakuwa tofauti na za Wakristo wengine.
Mtu anapofikiri juu ya imani yake, hapaswi kuhisi yuko huru kukataa kanuni za msingi za Ukristo wa awali isipokuwa awe ameamua kwamba yeye si Mkristo tena.
Mkristo anapaswa pia kuamini kanuni zilizowekwa za kanisa lake. Ikiwa anaamini kwamba kanuni za kanisa lake si sahihi, itakuwa vigumu kwake kujitolea kikweli kwa kanisa hilo kama mshirika.
Mkristo ataongozwa na mafundisho ya kanisa lake, lakini huenda akawa na masadikisho ya kibinafsi yanayotofautiana hata na ya washirika wengine wa kanisa lake. Sadikisho la kibinafsi si jambo linalosemwa moja kwa moja katika Biblia; ni jaribio la mtu kutumia ukweli wa Biblia katika suala fulani.
Kila Mkristo anapaswa kutumia ukweli wa Biblia kwa unyoofu katika hali zake, lakini hapaswi kuwa mwepesi kuwahukumu wengine kwa msingi wa mahitimisho yake mwenyewe. Ni sawa kwetu kutarajia Wakristo wote washikilie kanuni za imani za kale, na ni sawa kwetu kutarajia washirika wa kanisa washikilie kanuni za kanisa lao, lakini si sawa Mkristo kutarajia wengine wakubaliane na kanuni zake zote za kibinafsi.
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Maandiko yanatuambia tushikilie na tutetee kanuni za asili za Ukristo. Wakristo wa awali walitoa kauli za imani ambazo ni muhimu kwa injili na uhusiano wetu na Mungu. Kauli hizo bado zinafafanua Ukristo wa msingi.
Mazoezi ya Somo la 15
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
1 Timotheo 3:16
1 Timotheo 4:1-7
Tito 1:7-14
1 Yohana 4:1-3, 14-15; 1 John 5:12
Yuda 1:3-13
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 15. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 15
(1) Je, kanuni ya imani ni nini?
(2) Taja kauli mbili za kikanuni za kwanza kuhusu Yesu.
(3) Je, rejeo la kanuni ya imani ya kwanza katika maandiko ambalo linatoa kauli kadhaa ni lipi?
(4) Je, kusudi la Kanuni ya Imani ya Mitume lilikuwa lipi?
(5) Je, kusudi la Kanuni ya Imani ya Nisea lilikuwa lipi?
(6) Je, kusudi la Kanuni ya Imani ya Chalsedonia lilikuwa lipi?
Print Course
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.