► Someni Yohana 14 pamoja. Jadilini jinsi kifungu hiki kinaonyesha kwamba Mungu ni Utatu.
Watu wengi wamekanganywa na kanuni ya Utatu wa Mungu kwa sababu inasema kwamba Mungu ni watatu katika maana moja, na ni mmoja katika maana nyingine.
Lakini tunapotazama ulimwengu tunaona mfano mwingine wa tatu katika moja. Ulimwengu una vipengele vitatu - nafasi, wakati na mata. Bila mojawapo ya vitu hivyo vitatu, kusingekuwa na ulimwengu.
Kila moja ya vipengele hivyo vitatu pia ina vipengele vitatu.
Nafasi inajumuisha urefu, upana, na kimo - tatu katika moja. Bila mojawapo ya vipimo hivyo, kusingekuwa na nafasi.
Wakati unajumuisha wakati uliopita, uliopo na ujao - tatu katika moja. Bila mojawapo ya vipengele hivyo, kusingekuwa na wakati.
Mata inajumuisha nishati iliyo katika mwendo inayozalisha matukio – tatu katika moja. Kusingekuwa na nishati, kusingekuwa na mwendo au matukio. Kusingekuwa na mwendo, kusingekuwa na nishati au matukio. Kusingekuwa na matukio, ingekuwa ni kwa sababu hakuna nishati au mwendo.
Inaonekana ni kana kwamba ulimwengu umeundwa katika muundo wa tatu katika moja. Labda Mungu kimakusudi aliupatia ulimwengu muundo unaoonyesha asili yake mwenyewe.
Biblia inafundisha nini kuhusu Utatu wa Mungu? Inathibitisha kwa uwazi kuwepo kwa nafsi tatu tofauti ambazo zote zinatambuliwa kama Mungu mmoja wa ulimwengu. Huu si ukinzani kwa sababu hatusemi kwamba Mungu ni nafsi moja na nafsi tatu kwa wakati mmoja. Wala hatusemi kwamba Mungu ni Mungu mmoja na Miungu watatu. Tunasema kwamba Mungu ni mmoja katika asili na watatu katika nafsi. Kama vile ulimwengu mmoja uko kama nafasi, wakati na mata, Mungu mmoja yuko kama Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Ushahidi wa Kibiblia wa Utatu wa Mungu
Kauli ya 1: Kuna Mungu mmoja tu.
Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja (Kumbukumbu la Torati 6:4).
Maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi (Isaya 46:9).
Kauli ya 2: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wote ni Mungu.
Mungu Baba (Wagalatia 1:1).
Neno alikuwa Mungu… Neno alifanyika mwili (Yohana 1:1, 14).
Kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu…? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu (Matendo 5:3-4).
Kauli ya 3: Hawa watatu wanahusiana kati yao kama nafsi tofauti.
► Je, tunajuaje kwamba nafsi hizi ni nafsi tatu wala si nafsi moja inayotekeleza majukumu tofauti?
Katika Marko 1:10-11, Yesu anabatizwa, Roho Mtakatifu anashuka kama njiwa, na sauti kutoka mbinguni inasema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Tunaona hapa kwamba Baba, Mwana na Roho Mtakatifu hawawezi kuwa nafsi moja; wanatekeleza majukumu tofauti kwa wakati mmoja.
Kuelekea mwisho wa huduma yake, Yesu alisema atamwomba Baba amtume Msaidizi mwingine kwetu — Roho Mtakatifu (Yohana 15:26). Je, unaona nafsi tatu tofauti zikihusika katika ombi hili?
Ukisoma Yohana 14-17, utaona marejeleo mengi ya mwingiliano kati ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Hitimisho: Mungu mmoja wa kweli wa Biblia amejidhihirisha kuwa katika nafsi tatu tofauti: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mungu ni mmoja katika asili, lakini watatu katika nafsi.
Hivyo, ingawa neno Utatu halionekani katika Biblia, kanuni ya Utatu wa Mungu inatokana na kauli zilizo wazi katika kimaandiko. Neno Utatu ni neno tunalotumia kusema kwa ufupi yote ambayo Biblia inafundisha kuhusu kanuni hii.
Kanuni hii ya kibiblia imefundishwa na kanisa tangu enzi ya mitume. Huu hapa ni mchoro ambao kanisa limetumia kwa karne nyingi kueleza Utatu wa Mungu.
Kanuni ya Utatu wa Mungu ni Muhimu
► Je, kwa nini ni suala muhimu ikiwa mtu anaamini au haamini Utatu wa Mungu?
Kanuni ya Utatu wa Mungu ni msingi wa mafundisho makuu ambayo ni muhimu kwa injili. Kwa mfano, baadhi ya wale wanaokana Utatu wa Mungu wanakana kwamba Yesu ni Mungu. Lakini ikiwa Yesu unayemwamini si Mungu, basi huna Yesu anayeweza kukuokoa! Ni mtu asiye na dhambi tu ndiye angeweza kufa kwa ajili ya dhambi za watu wote. Angepaswa kuwa dhabihu isiyo na kikomo kwa sababu tumemtenda dhambi Mungu asiye na kikomo. Kwa sababu Yesu ni Mungu, alikuwa dhabihu isiyo na dhambi na isiyo na kikomo ambayo ililipa dhambi za watu wote kwa wakati wote.
Ikiwa tunakana kwamba Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni nafsi tofauti, tunamnyang’anya Mungu sifa zake za asili za kibinafsi au za kiuhusiano. Kwa mfano, Mungu asingekuwa Mungu mwenye upendo tangu asili ikiwa angengoja hadi baada ya uumbaji ili ampende mtu yeyote. Lakini ikiwa Mungu ana zaidi ya nafsi moja, nafsi hizo zingeweza kupendana tangu asili. Ni muhimu kumwamini Mungu huyu wa uhusiano (anayeishi katika upendo wa kujitoa) kwa sababu hilo linaathiri jinsi tunavyohusiana sisi kwa sisi na vilevile jinsi tunavyohusiana na Mungu.
Labda jambo zito zaidi ni kwamba ni lazima tumwabudu Mungu. Watu wanaokana Utatu wa Mungu kwa kawaida hukana kwamba Yesu na Roho Mtakatifu ni Mungu, hivyo hawawaabudu. Mojawapo ya makosa mabaya zaidi ambayo mtu anaweza kufanya ni kumwabudu mtu ambaye si Mungu au kutomwabudu mtu ambaye ni Mungu.
Sala ya John Stott ya Kila Siku ya Utatu wa Mungu
Baba uliye Mbinguni, naomba kwamba niweze kuishi siku hii katika uwepo wako na kukupendeza zaidi na zaidi.
Bwana Yesu, naomba kwamba siku hii niuchukue msalaba wangu na nikufuate.
Roho Mtakatifu, naomba kwamba siku hii unijaze na wewe na usababishe matunda yako kukomaa katika maisha yangu: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.
Utatu ulio Mtakatifu, uliobarikiwa na mtukufu, nafsi tatu katika Mungu mmoja, unirehemu.
Mwenyezi Mungu, Muumba na mhimili wa ulimwengu, ninakuabudu.
Bwana Yesu Kristo, Mwokozi na Bwana wa ulimwengu, nakuabudu.
Roho Mtakatifu, mtakasaji wa watu wa Mungu, ninakuabudu.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama ilivyokuwa mwanzo, na sasa, na itakuwa hata milele, Amina.
Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu Ni Nafsi Zinazoishi katika Uhusiano
Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu kila mmoja ana nafsi na siku zote wameishi katika uhusiano wa kibinafsi wao kwa wao. Tunawaita nafsi kwa sababu wanaishi katika uhusiano wao
kwa wao. Wanapendana, wanatoa kila mmoja kwa wenzake, wanasemezana na kila mmoja anaishi kwa ajili ya wenzake. Hii inaonyesha kuwa wao ni nafsi.
Mfumo katika Utatu wa Mungu
Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu siku zote wamekuwa katika mfumo wa mahusiano. Baba ndiye kichwa, kisha Mwana, kisha Roho. Nafsi hizi tatu za milele na zilizo sawa zina nafasi za mamlaka kulingana na mahusiano yaliyopo kati yao. Mfumo huu wa mamlaka unadhihirishwa katika familia na katika kanisa. Kama washiriki wa Utatu wa Mungu, washiriki wote wa familia au kanisa wana thamani sawa, lakini si wote wana nafasi ile ile ya mamlaka.
Uhusiano Kati ya Mwana na Baba Yake
Mwana anahusianaje na Baba? Yesu alisema kwamba kama Mwana, Baba alimwezesha kuwa na uzima ndani yake, kama vile Baba ana uzima ndani yake (Yohana 5:26). Mwana daima amekuwa Mwana pekee wa Baba (Yohana 3:16). Mwana anaishi milele kama Mungu na ana asili sawa na Baba, lakini kuwepo kwake kunatoka kwa Baba. Mwana daima amehusiana na Baba kama Mwana na Baba daima amehusiana na Mwana kama Baba, ingawa si katika maana ya kimwili.
Yesu ni sawa na Baba katika asili yake. Anapaswa kuabudiwa na kutukuzwa kwa kiwango sawa na Baba. Yesu alisema kwamba wote wanapaswa kumheshimu kama vile wanavyomheshimu Baba (Yohana 5:23).
Uhusiano Kati ya Roho Mtakatifu na Baba na Mwana
Katika Yohana 15:26, Yesu alisema kwamba atatutumia Roho Mtakatifu, atokaye kwa Baba. Ingawa Roho anatoka kwa Baba, yeye ni sawa na Baba na Mwana, na anapaswa kuheshimiwa kwa kiwango sawa na Baba na Mwana. Kumbuka kwamba Roho kutoka kwa Baba na kutumwa ni mambo yanayotendeka kati ya nafsi tatu zinazoishi katika uhusiano wa upendo.
Kulinda Umoja wa Mungu
Nafsi tatu za Utatu wa Mungu hazipaswi kuchukuliwa kuwa nafsi tofauti. Umoja wa nafsi hizo unamaanisha kuwa zina asili ile ile na kwamba nafsi hizo tatu zinapenyana, kila moja inaishi ndani ya nyingine na zinashiriki sifa zao kati yao. Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu kila mmoja anaishi ndani ya mwingine kwa njia ambayo haiwezekani katika wanadamu.
Kila mwanadamu ni mtu mmoja tu na nafsi moja tu. Mungu ni nafsi tatu, lakini ni mmoja tu. Ili kusaidia kulinda dhana ya kibiblia ya umoja wa Mungu, hatuzungumzii washiriki wa Utatu wa Mungu kama watu tofauti, bali kama nafsi tofauti.
Tunaakisi Nafsi na Mahusiano ya Mungu
Mungu alituumba kwa mfano wake kama watu — tukiwa na uwezo wa kuhusiana sisi kwa sisi na pia kuhusiana na Mungu. Kila mmoja wetu ana akili, nia na hisia kwa ajili ya kusudi la kuwa na mahusiano.
Tukiwa Peke Yetu Hatujakamilika
Baada ya Mungu kumuumba Adamu, alisema, “Si vema huyo mtu awe peke yake” (Mwanzo 2:18). Kisha akamuumba Hawa. Adamu hakuwa kamili bila Hawa kwa sababu, bila Hawa, hakuwa na mwanadamu mwingine wa kuhusiana naye. Kwa kweli, andiko moja linapendekeza kwamba Adamu na Hawa pamoja waliakisi mfano wa Mungu: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Mwanzo 1:27). Inaonekana kuna kitu kuhusu uhusiano kati ya Adamu na Hawa ambacho kiliwafanya kwa pamoja waakisi mfano wa Mungu kuliko jinsi Adamu angelifanya akiwa peke yake.
Fikiria hilo linamaanisha nini kwetu. Hatuishi kama watu kamili tusipokuwa katika uhusiano na wengine, kama nafsi za Utatu wa Mungu zilivyo. Hilo halimaanishi kwamba tunapaswa kufunga ndoa (hakuna mtu atakayekuwa katika ndoa mbinguni, lakini bado tutakuwa watu), lakini tunahitaji kuwa na ushirika na wengine.
Kuhusiana ili Kuakisi Mfano wa Mungu
Kuna ulinganisho wa ajabu kati ya asili ya Mungu na asili ya kanisa. Ndani ya Mungu na kanisa, kuna umoja na utofauti. Kulingana na 1 Wakorintho 12, mwili wa Kristo ni umoja unaojumuisha sehemu nyingi zinazofanya kazi pamoja kwa kusudi fulani. Je, unaweza kuona jinsi mwili wa Kristo unavyoakisi mfano wa Mungu? Paulo alitarajia washiriki wote mbalimbali wa kanisa wakue pamoja kama kitu kimoja katika Kristo. Paulo aliomba kwamba tuweze:
Kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo (Waefeso 4:15-16).
Sote tunapaswa kutumia karama na uwezo wetu kusaidiana kukua katika umoja wa Kristo. Mungu anatamani kwamba tuakisi asili yake ya kiuhusiano kwa kusaidiana kukua katika neema. Ukuaji wa kiroho hutokea katika jamii, katika ushirika wa karibu na wa kujitolea na waumini wengine. Hilo linaakisi asili ya Mungu ya kijamii.
Ikiwa washiriki wa Utatu wa Mungu wameishi daima katika upendo wa kujitolea kila mmoja kwa mwenzake, tunapaswa kuishi katika mahusiano ya upendo na wengine. Tuliumbwa kwa mfano wa Mungu kama viumbe wa kijamii na wa kimahusiano, hivyo tunapaswa kuzingatia wengine badala ya sisi wenyewe. Tunapaswa kusisitiza zaidi kuishi kijamii kuliko kuishi kibinafsi. Mungu atatubariki kadiri tunavyojaribu kuakisi mfano wake wa Utatu katika mahusiano yetu na wengine.
Ibada ya Utatu wa Mungu
[1]Ibada ya Utatu wa Mungu inatambua kwamba tunakuja kwa Baba kwa usaidizi wa Roho na kwa msingi wa kazi ya upatanisho ya Mwana. Kama watu wanaoamini Utatu wa Mungu, tunapaswa kuomba kwa Baba, katika Roho na kupitia kwa Mwana.
Lengo muhimu la ibada ni sisi kuingia katika uhusiano wa upendo kama ule wa washiriki wa Utatu wa Mungu. Fikiria upendo uliopo kati ya Baba na Mwana. Fikiria kile Kristo alichofanya msalabani ili tuishi katika upendo huo. Baba na Mwana wanaishi katika ushirika wa ajabu, na kwa sababu ya kazi ya upatanisho ya Mwana, Roho anaweza kutusaidia kushiriki katika uhusiano huo wenye upendo wa dhati.
Kama watu wanaoamini Utatu wa Mungu, hatuombi tu kwa Baba, katika Roho na kupitia Mwana, bali pia tunaomba kwa Baba, kwa Mwana na kwa Roho. Kila mmoja wa washiriki wa Utatu wa Mungu anapaswa kuabudiwa na kutukuzwa, kwa kuwa wote ni Mungu na wanapaswa kuheshimiwa kwa kiwango sawa. Ibada ya Utatu wa Mungu huleta utukufu kwa kila mshiriki wa Utatu wa Mungu kwa kiwango sawa, tukitambua jukumu la kila mmoja katika wokovu wetu.
“Mwenyezi Mungu wa milele, umetupatia sisi watumishi wako neema kwa kukiri imani ya kweli ili tuamini utukufu wa Utatu wa milele, na katika uwezo wa Ukuu wa kiungu kuabudu umoja huo. Utudumishe imara katika imani hii, ili tupate kulindwa daima na maadui wote: katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu, anayeishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja, sasa na hata milele. Amina.”
- Book of Common Prayer
Makosa ya Kuepuka: Nadharia kuhusu Utatu wa Mungu
Kidokezo kwa kiongozi wa darasa: Mshiriki wa darasa anaweza kueleza sehemu hii.
Hatuelewi kwa nini mbegu hukua kwenye udongo, au jinsi ubongo unavyofanya kazi, au ni nguvu gani zinashikilia nyota mahali pao. Wanasayansi wanaona yale yanayotokea, lakini hawawezi kueleza kwa nini na jinsi yanavyotokea. Si jambo la busara mtu kukataa kanuni ya Utatu wa Mungu kwa sababu hawezi kuifafanua kikamilifu. Hatuna uwezo wa kueleza kanuni yoyote kuhusu Mungu. Kwa mfano, hakuna mtu anayeweza kueleza jinsi Mungu anavyoweza kuwa kila mahali na kujua mambo yote. Si kwamba mambo ya kweli kuhusu Utatu wa Mungu si ya kimantiki, bali yanapita uwezo wa mwanadamu. Samaki wa baharini, hata kama angekuwa na akili kiasi gani, hawezi kuelewa jinsi ilivyo kuwa mwanadamu, hata kama angeelezwa.
Ukweli wa Utatu wa Mungu ni kwamba kuna Mungu mmoja anayeishi katika nafsi tatu zinazofanana katika asili na ziko sawa katika uungu. Watu wamejaribu kuelezea jambo hili, lakini mara nyingi hupoteza sehemu muhimu. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya makosa.
1. Mungu kwa kweli ni mmoja lakini amechukua majukumu tofauti. Katika nadharia hii, mbinguni Mungu ni Baba, duniani alikuwa Yesu na sasa ananena nasi kama Roho Mtakatifu. Lakini katika sura zote za Yohana 14-16, maneno ya Yesu yanaeleza mwingiliano kati yake na Baba na Roho Mtakatifu. Maelezo hayo hayangekuwa na maana ikiwa watatu hao si nafsi tatu tofauti.
2. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni nafsi tatu tofauti. Katika nadharia hii, kunaweza kuwa na tofauti katika asili yao. Kwa mfano Baba anaweza kuwa ndiye anayetaka kuhukumu lakini Mwana anataka kuonyesha rehema. Wazo hili linakinzana na kanuni ya Biblia kwamba kuna Mungu mmoja tu.
3. Nafsi moja katika Utatu wa Mungu ni duni kuliko nyingine. Mtu anayeamini wazo hili humwona Baba kama Mungu na Mwana na Roho Mtakatifu kama nafsi zingine zilizo chini yake. Anaweza kukana kuwepo kwa nafsi ya Roho na kumwona Mwana kama mtu maalum ambaye Mungu alimtumia. Kosa hili huwafanya watu wasimuabudu Mwana na Roho Mtakatifu kama Mungu na linaweza kusababisha injili ya uwongo.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Mungu anaishi katika Utatu, Mungu mmoja katika nafsi tatu, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Watatu hawa wanatekeleza majukumu tofauti, lakini wana asili sawa na sifa sawa za kiungu na wote wanastahili kuabudiwa.
Mazoezi ya Somo la 3
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Yohana 15:26
Yohana 17:1-5
Waefeso 1:17-23
Wakolosai 1:12-19
Waebrania 1:1-3, 8
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 3. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 3
(1) Je, ulimwengu unaonyeshaje asili ya Mungu?
(2) Je, ni kauli gani tatu za kibiblia ambazo ni msingi wa kanuni ya Utatu wa Mungu?
(3) Je, mfumo wa mahusiano ndani ya Utatu wa Mungu ni upi?
(4) Je, mfumo wa familia au kanisa unalinganaje na mfumo wa Utatu wa Mungu?
(5) Kama watu wanaoamini Utatu wa Mungu, tunapaswa kuomba nani?
(6) Taja nadharia tatu potovu za kawaida kuhusu Utatu wa Mungu.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.