► Someni Zaburi 8 pamoja. Je, kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu ubinadamu?
► Je, ni mambo gani yanayofanana kuhusu kila mtu duniani?
Fikiria juu ya kile kinachotupa utambulisho wetu. Je, ni nini hasa maana ya ubinadamu?
► Someni Mwanzo 1:26-27 pamoja.
Kuna kitu kuhusu asili yetu ambacho ni kama Mungu. Sisi si Mungu, lakini kuna kitu kinachotutenganisha na ulimwengu wa wanyama na kutufanya tuwe wa kipekee. Katika Zaburi 8:5, mwandishi anafurahi kwamba tumeumbwa kuwa chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni na tumevikwa taji la utukufu na heshima.
Mungu aliwapa wanadamu jukumu maalum la kusimamia dunia na viumbe wanaoishi duniani (Zaburi 8:6). Watu wanapaswa kusimamia dunia kwa uangalifu ili kuepuka kupotea kwa viumbe hai, kutumia rasilimali kwa hekima na kuacha dunia ikiwa katika hali nzuri kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mtazamo huu unaompa mwanadamu hadhi ya juu kwa hakika ni bora zaidi kwa ajili ya kujiheshimu sisi wenyewe kuliko kanuni ya mageuzi! Kakanuni ya mageuzi hakuna umuhimu maalum katika maisha ya mwanadamu, hakuna kusudi, hakuna maana, hakuna kitu maalum kuhusu kuwa mwanadamu.
Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi za kale, watu waliumbwa kwa bahati mbaya, bila kusudi, na hawapendwi na muumbaji yeyote. Lakini Biblia inafundisha kwamba sisi ni viumbe maalum, tulioumbwa kwa mfano wa Mungu. Hiyo inamaanisha nini?
Mfano wa Mungu katika wanadamu haimaanishi kufanana kimwili.
► Je, tunajuaje kwamba mfano wa Mungu katika wanadamu haumaanishi kufanana kimwili?
(1) Mungu ni roho (Yohana 4:24). Sulemani alitambua kwamba mbingu na dunia yote haiwezi kumtosha Mungu (1 Wafalme 8:27). Mungu angeweza kujidhihirisha kupitia mwonekano wowote aliotaka, lakini hakuna mwonekano wowote unaofanana na Mungu. Hiyo ndio sababu moja kwa nini hatupaswi kutengeneza sanamu za Mungu ili kuziabudu.
(2) Kutengeneza sanamu za Mungu zinazofanana na mwanadamu ni ibada ya sanamu. (Soma Warumi 1:23.)
(3) Watu wameumbwa kimwili kwa ajili ya maisha duniani, wakiwa na miguu ya kutembea, mikono ya kusogeza vitu na uwezo wa kuona na kusikia kwa ajili ya kutambua vitu. Mungu alituumba ili tuishi duniani. Lakini Mungu anaishi katika ulimwengu wote. Anaweza kuumba na kusababisha matukio kwa Neno lake. Hana mapungufu yoyote kama yetu. Hakuna sababu ya kufikiri kwamba ana umbo la kimwili la kibinadamu.
Vipengele vya Mfano wa Mungu Vilivyotolewa kwa Wanadamu
► Je, ni zipi baadhi ya sifa za wanadamu zinazoakisi mfano wa Mungu?
Wanatheolojia wamefikiria sana kuhusu maana ya mwanadamu kuwa katika mfano wa Mungu, na wengi wanakubaliana kuhusu sifa zifuatazo.
Silika ya Ubunifu
Tuna silika ya ubunifu inayotokana na mfano wa Mungu ulio ndani yetu. Muumba wetu ametufanya tuwe wabunifu! Wakati mwingine wanyama wamefunzwa kuchora alama ambazo watu wanaziita sanaa. Lakini hiyo ni tofauti sana na sanaa inayochorwa na mtu anayeeleza wazo fulani. Michoro ya kale imepatikana kwenye mapango. Hatujui mengi kuhusu watu waliozichora, lakini hakuna mtu aliye na shaka kwamba zilichorwa na watu wala si wanyama.
Ubunifu pia umedhihirishwa katika muziki. Muziki una uwezo wa ajabu wa kueleza mawazo na hisia zetu. Uwezo wa kuwasilisha mawazo kupitia muziki unatokana na mfano wa Mungu ulio ndani yetu.
Uwezo wa Kufikiria
Uwezo wa kufikiria ni uwezo mwingine kama wa Mungu. Wanyama pia wana ubongo, lakini kulingana na ufahamu wetu, shughuli za ubongo wa wanyama haziwezi kufanya kazi zaidi ya kiwango cha silika na kutenda pasipo kufikiria. Wanadamu pekee ndio wenye uwezo wa kuchanganua, kutathmini, na kutafakari, kisha kuwasiliana kwa ushawishi.
Hatuwezi kufikiria tu, tunaweza hata kufikiria juu ya kufikiria. Tunaweza kuchanganua michakato ya mawazo. Hatuwezi tu kufikiria kimantiki, pia tunaweza kufikiria juu ya mantiki.
Uwezo wa Kuwasiliana
Wanadamu wana uwezo wa kuwasiliana. Uwezo huo unadhihirishwa na matumizi ya lugha, ambapo mawazo yanawekwa katika sauti au ishara ambazo watu wengine wanaelewa. Wanyama kama vile mbwa na ndege wanaweza kuwasiliana kupitia sauti, lakini hakuna chochote kinachokaribia uchangamani wa lugha ya mwanadamu kinajulikana kuwepo katika wanyama. Wanyama wana njia za kutishia wanyama wengine, kumiliki eneo fulani au kugawana chakula, lakini hawawezi kuwa na majadiliano kuhusu maana ya maisha.
Uwezo wa kuwasiliana hutegemea uwezo wa kufikiria na kutumia mantiki. Wanyama hawawezi kusema maneno, lakini hata kama wangeweza, hawangekuwa na mengi ya kusema.
Asili ya Kijamii
Wanadamu wana asili ya kijamii. Tumeumbwa kutangamana na watu wengine, kutoa ahadi kwa wengine na kutegemea wengine. Tunaanza maisha tukiwategemea wengine kikamilifu, na inachukua miaka mingi mtoto kuwa mtu mzima. Hiyo ni kwa sababu mahusiano ni muhimu kwa Mungu.
Mungu amepanga maisha ya mwanadamu ili watu wafanye kazi pamoja na wadumishe mahusiano ili mahitaji yao ya kila siku yakidhiwe. Hata kama mtu angeweza kupata vitu kama vile chakula na makao bila msaada wa mtu yeyote, bado atakuwa na mahitaji muhimu ambayo yanaweza kukidhiwa tu katika uhusiano na wengine. Asili ya kijamii ya mwanadamu inaakisi asili ya Mungu. Mungu ni Utatu na daima yuko katika uhusiano.
Mahusiano ya kibinadamu yana matatizo mengi. Kwa sababu ya matatizo hayo, watu wengine hufikiri wanahitaji kujitegemea zaidi. Wanataka kuishi bila kutegemea mtu yeyote. Kuishi peke yako si suluhisho wala si maisha ambayo Mungu alitupangia. Badala yake, alitupa kanuni za kuishi katika uhusiano. Matatizo huja wakati hatufuati mpango wa Mungu.[1]
Dhamiri ya Kimaadili
Tuna dhamiri ya kimaadili ambayo ni sehemu ya asili yetu. Kuna kitu ndani yetu ambacho hutuambia kwamba matendo mengine ni sahihi na mengine si sahihi. (Soma Warumi 1:20; Warumi 2:15.) Inatuambia wakati ambapo ni sahihi kufuata tamanio fulani na wakati ambapo hatupaswi kufanya hivyo. Adamu na Hawa waliumbwa wakiwa watakatifu na waliweza kufuata mapenzi ya Mungu kikamilifu.
Kwa sababu wanadamu wameanguka katika dhambi na kuharibu mtazamo huo wa msingi wa kimaadili, bado kumebaki ndani ya kila mmoja wetu uwezo wa kuelewa dhana ya mema na mabaya ingawa uwezo huo si sahihi kikamilifu.
Kwa sababu tuna dhamiri ya kimaadili, tunahisi tuna wajibu wa kufanya mema, na tunahisi kuwa na hatia tukitenda dhambi. Sisi si kama wanyama, ambao hufuata silika zao za asili bila hisia ya hatia.
Uwezo wa Kuchagua
Uhuru wa kuchagua, au uwezo wa kuchagua, ni tabia ya wanadamu. Kinyume chake, machaguo ya wanyama yako kwenye kiwango cha msukumo wa muda mfupi na silika. Wanyama hawafanyi maamuzi yaliyofikiriwa kwa uangalifu yanayozingatia maadili au matokeo ya kiutendaji ya matendo yao. Wanadamu wana uwezo wa kufanya maamuzi yenye maana, yenye kubadilisha maisha. (Soma Yoshua 24:15.)
► Kwa nini uhuru wa kuchagua ni kipengele muhimu cha ubinadamu?
Kwa sababu tunafanya maamuzi halisi, tunawajibika kwa Mungu. Ataadhibu dhambi na kutoa thawabu kwa wenye haki (Ufunuo 20:12-13).
Kwa sababu tumezaliwa na asili ya dhambi, hatutumii uhuru wetu wa kuchagua kwa njia inayomheshimu Mungu. Mtu kwa asili yake ni mtumwa wa dhambi (soma Warumi 6:16-17, Waefeso 2:1-3), hawezi kutenda mema, lakini neema ya Mungu inamfikia kila mtu, ikitoa hamu na uwezo wa kuitikia injili. Ndio maana mtu anaweza kuchagua kutubu na kuamini injili. (Soma Marko 1:15.)
Kutokufa
Kutokufa ni sifa muhimu ya mfano wa Mungu. Kuna wakati ambapo hatukuwepo, lakini kila mtu atakuwepo milele tangu wakati wa utungaji wa mimba yake. Sisi si viumbe wa kimwili tu, bali pia ni roho ambazo zitaishi milele, na hata miili yetu itafufuliwa katika umbo la milele. (Soma 1 Wakorintho 15:16-22, 52-54.) Mungu alimuumba kila mmoja wetu kwa kusudi la milele. Kutokufa kunafanya maamuzi yetu yawe muhimu milele kwa sababu tutaishi milele mbinguni au jehanamu.
Uwezo wa Kupenda
Uwezo wa kupenda ni sehemu ya mfano wa Mungu. Miongoni mwa wanyama, mahusiano ni machache sana, na yanadhibitiwa zaidi na silika.
Tabia zingine za ubinadamu ni muhimu kwa sifa hii. Upendo usingekuwa na maana kama tusingekuwa na uwezo wa kuwasiliana, uwezo wa kuchagua na kutoa ahadi kwa wale tunaowapenda na uwezo wa kuitikia kwa busara tunapopokea upendo kutoka kwa wengine.
Upendo wa kibinadamu unadhihirishwa kwa furaha katika uhusiano, kutoa na kutimiza ahadi, kutoa na kutumika kwa kujinyima, na msamaha. Yote haya ni madhihirisho ya upendo wa Mungu.
Uwezo wa Kuabudu
Sifa muhimu sana ni uwezo wetu wa kuabudu. Fikiria nyimbo unazozipenda zaidi za kumtukuza Mungu. Tunaimba, “Mungu wetu ni Mungu wa ajabu.” “Jinsi Wewe Ulivyo Mkuu” ni wimbo usiopitwa na wakati wa kuabudu kwa dhati. Mtunga Zaburi alisema, “Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu” (Zaburi 103:1). Maneno haya yanawezekana kwa sababu mfano wa Mungu ulio ndani yetu unamtambua na kumwitikia Mungu ambaye tumeumbwa kwa mfano wake!
“Leo watu wanajaribu kushikilia hadhi ya mwanadamu, lakini hawajui jinsi ya kufanya hivyo, kwa sababu wamepoteza ukweli kwamba mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu.... Tunatazama utamaduni wetu ukitekeleza ukweli kwamba unapowaambia wanadamu kwa muda wa kutosha kwamba wao ni mashine, hilo huanza kuonekana katika matendo yao baada ya muda mfupi”
Francis A. Schaeffer
Kusudi la Mfano wa Mungu katika Ubinadamu
Ni vizuri kutafakari kwa nini Mungu alituumba kwa mfano wake. Kwa nini sisi ni tofauti sana na viumbe wengine wote? Jibu ni kwamba tumeumbwa kimahususi kuwa katika uhusiano na Mungu na kumwabudu.
Biblia inatuambia kwamba uumbaji kwa ujumla humletea Mungu utukufu. Tunaona ukuu wa Mungu katika vitu alivyoviumba. Lakini viumbe wengine wanamtukuza Mungu bila ufahamu. Hawawezi kuelewa jinsi Mungu alivyo kwa sababu hawana asili inayoweza kuhusiana naye.
Tunaweza kuvutiwa na ubunifu wa Mungu usio na kipimo kwa sababu tuna kiwango fulani cha ubunifu. Tunaweza kuabudu utakatifu na haki yake kwa sababu tuna dhamiri ya mema na mabaya. Tunaweza kustaajabishwa na upendo wake usio na kipimo kwa sababu tuna uwezo wa kupenda.
Kadiri tunavyomjua Mungu vizuri zaidi, si tu katika ufahamu wa kiakili bali katika uhusiano, ndivyo tunavyompenda na kumwabudu zaidi. Tunapata shangwe na uradhi katika uhusiano na Mungu kwa sababu alituumba kwa ajili ya uhusiano huu.
Mawazo Mengine Muhimu
(1) Wanadamu wote wana mfano wa Mungu (Mwanzo 1:27). Kuna watu ambao kwa sababu ya mapungufu ya kiakili hawawezi kufikiria kimantiki, kujieleza kwa ubunifu au kutumia uhuru wa kuchagua. Mfano wa Mungu umeumbwa ndani yao, lakini hauwezi kutumika katika maisha yao ya kidunia.
(2) Maisha ya kila mwanadamu yana thamani ya milele na isiyo na kipimo. Wakati mwingine tunaona thamani ya mtu ya kiutendaji, mambo kama vile akili, elimu, vipawa au nguvu yake. Lakini kila mtu ana thamani ambayo ni muhimu zaidi kuliko thamani yake ya kiutendaji, kwa sababu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Ndio maana kila mtu anastahili heshima kama binadamu, hata kama anakosa vitu vinavyowapa watu thamani ya kiutendaji, na hata kama yeye ni mtu mwovu. Mfano wa Mungu pia ndio sababu kwa nini kila mtoto ni wa thamani kwa Mungu, na kutoa mimba ni dhambi mbaya sana (Mwanzo 9:6, Zaburi 139:13-14, Isaya 44:24).
(3) Malaika pia ni wa kipekee katika uumbaji. Wana akili nyingi, uwezo wa kufikiria kimantiki, uwezo wa kuwasiliana na uwezo wa kuabudu. Kwa hivyo wana baadhi ya vipengele vya mfano wa Mungu na wanaitwa wana wa Mungu katika maandiko (Ayubu 1:6). Kwa sasa uwezo wetu ni duni ukilinganishwa na uwezo wa malaika (Zaburi 8:5), hata hivyo, wanatutumikia (Waebrania 1:14). Katika uzima wa milele, tutakuwa na nafasi ya juu kuliko malaika (soma 1 Wakorintho 6:3), na tutatawala pamoja na Kristo. Hilo linamaanisha kwamba wanadamu wameumbwa kwa mfano wa Mungu kwa ukamilifu zaidi kuliko malaika.
(4) Ulimwengu hauko katika umbo lake la asili. Fikiria mchoro wa kuvutia, uliochorwa na mchoraji stadi. Fikiria mchoro huo umetupwa sakafuni, na watu wakaukanyaga na viatu vyenye matope. Ukiangalia mchoro huo, bado unaweza kuona ustadi mkubwa uliouchora, lakini mchoro huo hauko jinsi ulivyokuwa wakati mchoraji aliumaliza hapo mwanzoni. Uumbaji uko hivyo. Hauko kama vile Mungu alivyokusudia uwe, lakini utukufu wake bado unaonekana.
(5) Dhambi imepotosha uwezo “kama wa Mungu” ulio ndani ya watu. Kwa mfano, kazi ya sanaa inaweza kudhihirisha moyo mwovu na inaweza kuwa chombo cha Shetani, ingawa kipawa chenyewe kinatoka kwa Mungu. Hata hivyo, kwa sababu ya neema kuingilia kati, dhambi haijaharibu kabisa mfano wa Mungu ndani yetu. Kwa neema Mfano wa Mungu ndani yetu unaweza kufanywa upya, kukuzwa na kudhihirishwa kwa utukufu wa Muumba wetu! (Soma Wakolosai 3:10; Waefeso 4:22-24; 2 Wakorintho 3:18.)
(6) Mfano wa Mungu ulio ndani yetu ndilo jambo muhimu zaidi kutuhusu. Mfano wa Mungu ulio ndani yetu unatuwezesha kuitikia injili. Dhamiri yetu ya kimaadili huwezesha neema kuamsha dhamiri zetu na kutusadikisha juu ya dhambi. Uhuru wa kuchagua uliorejeshwa kupitia neema inayofanya kazi ndani yetu unatuwezesha kuchagua ni nani tutakayemtumikia. Kupitia silika yetu ya ubunifu tunaweza kumletea Mungu utukufu na heshima. Kwa kutumia mantiki, tunaweza kuchunguza kweli zilizofichika na kuelewa mambo fulani kumhusu Mungu na njia zake. Kutafuta kumwelewa Mungu kunageuka kuwa ibada kadiri tunavyozidi kufahamu ukuu kamili wa Muumba wetu ambaye kwa neema kubwa ametuvika taji la utukufu na heshima!
Makosa ya Kuepuka
Wakati mwingine watu hufikiri kwamba uhusiano na Mungu una umuhimu kwa maisha ya baada ya kifo pekee. Wanafikiri kwamba ikiwa mtu anaishi maisha mazuri duniani, si jambo muhimu ikiwa yeye ni Mkristo au la. Lakini ikiwa tunaelewa kwamba asili ya ubinadamu imeumbwa kwa ajili ya kuwa na uhusiano na Mungu, tunatambua kwamba maisha yetu kwa kiasi kikubwa yanakuwa hayana maana ikiwa hatumjui Mungu. Tunahitaji Roho wa Mungu ndani yetu, akituongoza, akitimiza uwezo wetu, na akitupatia mtazamo wa milele kwa yote tunayofanya.
► Someni kauli ya imani pamoja angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Wanadamu wameumbwa kwa mfano wa Mungu kwa kusudi la kumpenda na kumwabudu Mungu. Mungu aliumba watu wakiwa na uwezo wa kufikiria, kuwasiliana na kupenda. Mtu ana dhamiri ya kimaadili, nia ya kibinafsi na roho isiyokufa. Neema ya Mungu humpa mtu uwezo wa kufanya maamuzi huru. Maisha ya kila mwanadamu yana thamani ya milele na isiyo na kipimo.
Mazoezi ya Somo la 4
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Mwanzo 3:1-6
Yoshua 24:14-18
Warumi 6:12-23
Warumi 8:22-26
Waefeso 2:1-9
1 Wathesalonike 5:23
Yakobo 1:12-15
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 4. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
Mtihani wa Somo la 4
(1) Kulingana na Mwanzo 1:26-27, watu ni wa kipekee kwa jinsi gani wakilinganishwa na viumbe wengine wote?
(2) Taja sababu tatu zinazotufanya tujue kwamba mfano wa Mungu katika ubinadamu si mfano wa kimwili.
(3) Orodhesha vipengele saba vya mfano wa Mungu katika ubinadamu.
(4) Je, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu kwa sababu gani mbili?
(5) Je, ni uwezo gani unatokana na dhamiri ya kimaadili?
(6) Je, uwezo wa watu wa kufanya machaguo halisi una umuhimu gani?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.