► Someni Ufunuo 21 pamoja. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu mustakabali wa waumini?
Uumbaji wote upo kwa ajili ya utukufu wa Mungu, lakini mbinguni ndio kitovu cha ulimwengu, mahali ambapo Mungu anaabudiwa kwa kiwango cha juu zaidi na viumbe alioumba kwa mfano wake. (Soma Ufunuo 5:11-14.) Utukufu wa Mungu utafunuliwa mbinguni kikamilifu kiasi kwamba mahali hapo patakuwa nuru ya mji (Ufunuo 21:23). Ni mahali ambapo tutamjua Mungu kikamilifu kiasi kwamba tutauona uso wake (Ufunuo 22:4).
Mbinguni, waumini watapata furaha kamili katika kumwabudu Mungu. Zaburi 16:11 inasema, “Mbele za uso wako ziko furaha tele; na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele.” Inafaa kwamba furaha na ibada vinahusiana. Mungu alituumba kwa mfano wake, ili tuweze kuelewa asili yake vya kutosha kiasi kwamba tuweze kumwabudu jinsi alivyo. Tumepewa hisia, uwezo wa kupenda, na akili ili tuweze kumwabudu Mungu.
Yesu alitoa kauli hizi kwa wanafunzi wake:
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo (Yohana 14:1-3).
Maneno ya Yesu yanatuambia mambo fulani kuhusu mbinguni. Jambo muhimu zaidi ni kwamba mbinguni ni makao ya Mungu. Yesu alisema ni nyumba ya Baba yake. Jambo lingine muhimu ni kwamba siku moja tutaweza kuishi huko pamoja na Mungu.
Ahadi ya kuishi mbinguni inapaswa kuongoza jinsi tunavyoishi duniani.[1] Mtu anayeishi kwa msingi wa maadili ya milele atafanya mema zaidi duniani. Mtu anayetarajia thawabu ya mbinguni ana motisha ya kuvumilia hali ngumu na kujitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu. Yesu anawaambia wale wanaoteseka, “Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (Mathayo 5:12).
Sifa za Mbinguni
► Je, baadhi ya mambo tunayojua kuhusu mbinguni ni yapi?
Wakati mwingine watu duniani hawawezi kununua nyumba wanayotaka, au hawawezi kuifanya nyumba yao iwe kama wanavyotaka iwe. Lakini Mungu ana uwezo na rasilimali zisizo na kikomo, hivyo tunajua kwamba nyumba yake iko jinsi anavyotaka iwe. Kwa hivyo, mbinguni panalingana kikamilifu na asili ya Mungu.
Hakutakuwa na dhambi mbinguni. Viumbe wote mbinguni, iwe ni malaika au wanadamu au viumbe wengine, watakuwa watakatifu kikamilifu. (Soma Ufunuo 21:8, 27.)
Mbinguni patakuwa huru kutokana na matokeo yote ya dhambi, ikiwa ni pamoja na uchungu, huzuni, migogoro, na hatari. (Soma Ufunuo 21:4.) Hakutakuwa tena na laana juu ya uumbaji, ikiwa ni pamoja na ugonjwa, kuzeeka, na kifo. (Soma Ufunuo 22:3.)
Uzuri wa mbinguni hauwezi kuelezeka. Maelezo tuliyopewa ni pamoja na kuta za yaspi, malango ya lulu, misingi ya vito adimu, na barabara za dhahabu. (Soma Ufunuo 21:18-21.)
Nani na Wakati Gani?
Mbinguni pameandaliwa kwa ajili ya wale wanaotubu dhambi na kumwamini Yesu Kristo kama Mwokozi na Bwana (Yohana 3:16). Biblia inatuambia kwamba tukiishi kwa msingi wa maadili ya milele, tunaweza kuwekeza katika hazina ya milele na iliyo salama mbinguni. (Soma Mathayo 6:20.) Mbinguni pana mamilioni ya watu waliokombolewa pamoja na malaika (Ufunuo 5:8-11).
Mtu huenda mbinguni wakati gani? Yesu alimwambia mwizi aliyekuwa anakaribia kufa msalabani kwamba watakuwa pamoja katika paradiso siku hiyo (Luka 23:43). Paulo alisema kwamba kutokuwepo katika mwili ni kuwa pamoja na Bwana (2 Wakorintho 5:8). Kwa hivyo, tunajua kwamba muumini huenda mbinguni wakati wa kifo. Waumini ambao bado wako hai wakati wa kurudi kwa Yesu wataenda mbinguni bila kupitia kifo. (Soma 1 Wakorintho 15:51-52; 1 Wathesalonike 4:13-18).
“Nikipata hamu ndani yangu isiyoweza kutoshelezwa na kitu chochote katika ulimwengu huu, yamkini ni kwa sababu niliumbwa kuishi katika ulimwengu mwingine….Yamkini anasa za dunia hazikukusudiwa kamwe kuitosheleza hamu hiyo, bali kuiamsha tu, kunionyesha nahitaji kitu kingine halisi zaidi.... Lazima nifanye lengo kuu la maisha yangu liwe kukaza mwendo kuelekea nchi hiyo nyingine na kuwasaidia wengine kufanya hivyo.”
C.S. Lewis
Mere Christianity
Sehemu ya 2: Hatima ya Milele ya Wasioamini
Adhabu duniani siku zote huisha wakati fulani, hata ikiwa ni wakati wa kifo cha yule anayeadhibiwa. Lakini Yesu alieleza adhabu ambayo ni ya milele. Alisema,
Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake…Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele (Mathayo 25:41, 46).
Yesu na mitume walithibitisha kwamba jehanamu, ziwa la moto, na adhabu ya milele zipo. Yesu alituonya tuepuke mahali hapo pa kuogofya sana. Hizi ni kauli kutoka kwa Yesu na mitume.
Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno (MT 13:49-50).
Akizungumza na Mafarisayo, Yesu alisema, “Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?” (MT 23:33).
Wakati fulani Yesu alipokuwa akizungumza na Mafarisayo, alieleza kuhusu mateso ya mtu aliyekufa na kwenda jehanamu:
Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, “Ee baba Ibrahimu,
nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu” (Luka 16:23-24).
Mtume Paulo anaandika kwamba Yesu atafunuliwa
…mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake (2 Wathesalonike 1:7-9).
Petro anaandika
…Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu (2 Peto 2:4).
Yohana anaandika
Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele…Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto (Ufunuo 20:10, 15).
Tazama aina ya maneno yanayotumika kueleza mahali hapo: moto, mateso, kisasi, maangamizi, giza, minyororo, hukumu, kilio, na kusaga meno.
Yesu alisema
Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum (Mathayo 5:29-30).
Yesu alisema afadhali kung'oa jicho lako la kulia na kukata mkono wako wa kulia kuliko kutupwa jehanamu ukiwa na jicho hilo na mkono huo. Yesu hakuwa anahimiza ukataji wa viungo vya mwili, bali kusitisha kitendo chochote kitakachotuongoza katika dhambi na jehanamu, haijalishi ni cha thamani kiasi gani duniani.
► Je, baadhi ya dini ambazo zimepotoka katika kanuni zao kuhusu jehanamu ni zipi?
Biblia inatuambia kwamba kifo hutamatisha nafasi ya mwanadamu ya kuchagua hatima yake ya milele, na kwamba jehanamu ni (1) ya milele, (2) haiwezi kutenguliwa, na (3) ni mahali pa uchungu mwingi. Ukweli huu wa Biblia unakataliwa na wakana Mungu wanaosema hakuna chochote baada ya kifo, pamoja na Mashahidi wa Yehova, Wamormoni, na dhehebu la Universalist wanaosema hakuna jehanamu. Ukweli wa kwamba kifo hutamatisha kipindi cha majaribio ya mwanadamu unakanushwa na Wakatoliki wanaoamini kwamba hali ya mwanadamu inaweza kurekebishwa baada ya kifo.
Kuna wale wanaokanusha kuwepo kwa jehanamu kwa sababu wanaona kuwa ni dhuluma. Wanasema kwamba ikiwa dhambi ilifanyika katika kipindi chenye kikomo, si haki kutoa adhabu ya milele dhidi ya dhambi. Mtakatifu Agostino alijibu pingamizi hili kupitia mfano wa sheria ya jinai. Wizi ukifanyika kwa dakika chache, je, mtu anapaswa kupewa adhabu ya dakika chache tu? Mauaji yanayotekelezwa haraka husababisha uharibifu usioweza kurekebishwa. Katika maandiko, tunaona kwamba dhambi dhidi ya Mungu wa milele na asiye na kikomo husababisha adhabu ya milele, ingawa dhambi hiyo ilitendwa katika maisha yenye kikomo.
► Je, kwa nini jehanamu ni ya milele?
Jehanamu ni ya milele kwa sababu
1. Dhambi ni kosa dhidi ya Mungu asiye na kikomo.
2. Wenye dhambi wasiotubu humnyima Mungu utumishi wa milele wanaohitaji kumpa.
3. Sisi ni viumbe wa milele na hatuna mahali pengine pa kwenda ikiwa tutachagua kutengwa na Mungu.
[1]Duniani, tunapenda kwamba tunaweza kubadilisha maamuzi yetu. Inaonekana ni jambo zito sana kwamba uamuzi unaweza kuwa na matokeo ya milele. Tunapenda kufikiria kwamba kutakuwa na nafasi ya pili katika siku zijazo, hata ikiwa tunafanya uamuzi wa kimakusudi sasa. Lakini ni jambo linaloeleweka kwamba Mungu ameweka kikomo katika nafasi yetu ya kuamua hatima yetu ya milele ili ifikie kikomo baada ya kifo.
Wengine wanakataa kuamini kuwa kuna jehanamu kwa sababu wanashangaa jinsi Mungu mwenye upendo anaweza kumpeleka mtu mahali pa kuogofya kiasi hicho kama inavyoelezwa katika vifungu tulivyoona hapo awali. Ni lazima tukumbuke kwamba Mungu hataki
mtu yeyote apotee bali anataka kila mtu atubu na apate wokovu. Biblia inasema hivyo katika sehemu kadhaa. (Soma 2 Petro 3:9; 1 Timotheo 2:4; Matendo 17:30.) Wale wanaoenda jehanamu wamefanya maamuzi yanayowaweka mahali hapo pa kuogofya. Hakuna mtu anayejipata jehanamu kwa bahati mbaya. Wale wanaokwenda huko wamechagua mahali hapo kwa kumkataa Mungu, haki, na wokovu.
Kwa kuwa yote yaliyo mema hutoka kwa Mungu, kumkataa Mungu hatimaye ni kukataa yote yaliyo mema. Utulivu, usalama kutokana na hofu na uchungu, na mahali pa faraja ni mambo mazuri ambayo ni Mungu pekee ndiye anayeweza kutoa. Kutengana na Mungu kikamilifu kunamaanisha kukosa kila kitu ambacho ni kizuri, na hiyo ni jehanamu.
Mshukuru Mungu kwamba kupitia kazi ya upatanisho ya Yesu Kristo, upendo wake umefanya tuweze kuepuka ghadhabu inayokuja (1 Wathesalonike 1:10; 1 Wathesalonike 4:9). Badala ya mateso ya jehanamu, tunaweza kushiriki katika furaha ya wokovu na maajabu ya mbinguni. Tunachagua mbinguni kwa ajili ya hatima yetu tunapochagua kutubu kwa Mungu na kuweka imani katika Bwana wetu Yesu Kristo (Wafilipi 3:20, Matendo 20:21).
“Hatimaye mapingamizi dhidi ya kanuni zinazohusu jehanamu lazima yaibue swali hili: ‘Ni nini kingine unachomwomba Mungu afanye?’ Afute dhambi zao za zamani na awape mwanzo mpya, akitekeleza jambo hilo gumu kupitia msaada wa kimuujiza? Lakini tayari amejitolea kufanya hivyo. Awasamehe? Lakini wanakataa kusamehewa. Aachane nao? Nasikitika kwamba hivyo ndivyo anavyofanya.”
C.S. Lewis
Imefasiliwa kutoka kitabu kinachoitwa The Problem of Pain
Makosa ya Kuepuka: Kusahau Matokeo ya Milele
Katika maisha ya duniani, maamuzi mengi hayaonekani kuwa ya mwisho. Kukiwa na muda wa kutosha, makosa mengi yanaweza kurekebishwa. Ni lazima tukumbuke kwamba maamuzi mengi yana matokeo ya milele. Hatujui tutakufa lini, na nafasi yetu ya kuchagua hatima yetu ya milele itakuwa imekwisha. Baada ya kifo hatutaweza kubadilisha matendo ambayo yaliathiri hatima yetu ya milele au matendo ambayo yaliathiri wengine katika maamuzi yao.
► Someni pamoja kauli ya imani angalau mara mbili.
Kauli ya Imani
Kila mtu hatimaye ataishi milele mbinguni au jehanamu. Mbinguni ni makao ya Mungu ambapo waumini wataishi pamoja na Mungu, wakimwabudu kwa furaha. Mbinguni hakuna dhambi wala mateso yoyote yanayotokana na dhambi. Jehanamu ni ya milele, haiwezi kutenguliwa, na ni mahali pa adhabu yenye uchungu mwingi kwa wote ambao hawajaokolewa na Kristo kutokana nadhambi zao. Jehanamu ni adhabu ya haki kwa dhambi ya makusudi dhidi ya Mungu asiye na kikomo.
Mazoezi ya Somo la 13
(1) Zoezi la Kifungu cha Biblia: Kila mwanafunzi atapewa mojawapo ya vifungu vilivyoorodheshwa hapa chini. Kabla ya kipindi kinachofuata cha darasa, unapaswa kusoma kifungu chako na kuandika aya moja kuhusu kile ambacho kifungu hicho kinasema kuhusu mada ya somo hili.
Isaya 5:11-16
Mathayo 5:27-30
Luka 16:19-31
Ufunuo 22:1-5
Ufunuo 22:10-17
(2) Mtihani: Utaanza darasa linalofuata kwa kufanya mtihani juu ya Somo
la 13. Jiandae kwa kuchunguza maswali ya mtihani kwa makini.
(3) Zoezi la Kufundisha: Kumbuka kupanga na kutoa ripoti juu ya wakati wako wa kufundisha nje ya darasa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.