Pamoja na nyongeza ya aya za Maandiko zitakazojadiliwa katika somo hili, Kuna aya nyingine nyingi zilizoonyeshwa kwenye tanbihi. Inawezekana kusiwepo na muda wa kutosha kwa darasa kupitia na kuzisoma aya zote wakati wa kipindi cha darasani. Kiongozi wa darasa anaweza kuchagua baadhi kwa ajili ya kusomwa.
Neno kuokoka linahusika na mabadiliko yanayotokea wakati mtu anapookoka. Kusudi la uinjilisti ni kumwongoza mwenye dhambi aweze kufikia kuokoka.
► Soma 1 Wathesalonike 1. Je, kuna mabadiliko gani ya ndani kwa Wathesalonike wakati walipookoka
Ili kuelewa ni kwa nini mtu anahitajika kuokoka, na kuelewa ni nini kinachotokea wakati mtu anapookoka, ni lazima tuelewe hali ya mtenda dhambi kabla ya kuokoka.
► Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuielezea hali ya mwanadamu kabla hajaokoka?
Kwa sababu ya dhambi ya Adamu, kila mtu ametengwa na Mungu anapokuwa amezaliwa (Warumi 5:12). Hii inamaanisha kwamba kila mtu ni mbinafsi na anayeenda katika njia zake kwa jinsi anavyotaka.
Tabia Nne za Mwenye Dhambi
Mara tu mtu anapofikia umri wa kufanya maamuzi, anaanza kuteda dhambi. Kila mwenye dhambi ana hatia kwa matendo yake mengi ya uovu (Warumi 3:23).
Dhambi ni kukiuka sheria ya Mungu (1 Yohana 3:4, Yakobo 2:10-11). Kwa kuwa Mungu ni mwenye haki yote, haipuuzi dhambi, na kila mtu atahukumiwa kwa yale yote aliyoyatenda (2 Wakorintho 5:10, Ufunuo 20:12-13). Hakuna maswali kuhusu hatia ya mtu au adhabu anayostahili. Kila mtenda dhambi tayari ni mhukumiwa (Yohana 3:18-19).
Mtenda dhambi ni adui wa Mungu (Warumi 5:10). Mwenye dhambi hawezi kuwa kwenye uhusiano na Mungu hadi hapo makosa yake yaliyo kinyume na Mungu yatakapoondolewa.
Mtenda dhambi pia yuko katika hali inayomfanya asiwe mtu wa kufaa kwenye uhusiano na Mungu kwa sababu ni mtenda mabaya kwa ajili ya tamaa zake (Waefeso 2:3). Kwa kuwa yeye ni mtumwa wa dhambi, mwenye dhambi hana uwezo wa kuibadili hali yake (Warumi 5:20, 7:23).
Kwa hiyo ni nini anachohitaji mtenda dhambi? Kwa kuwa mtenda dhambi ni mwenye hatia, wokovu kwake unamaanisha ni kusamehewa. Kwa kuwa ni adui wa Mungu, wokovu kwake unamaanisha ni kupatanishwa. Kwa kuwa ni mtenda mabaya, wokovu kwake unamaanisha ni kutakaswa. Kwa kuwa hana uwezo, wokovu kwake unamaanisha ni kuwekwa huru. Hivi ni vipengele vichache tu vya wokovu ambavyo mwenye dhambi anavihitaji.
Wakati wa kuokoka, mwenye dhambi husamehewa, hupatanishwa na Mungu, hutakaswa, na huondolewa kutoka katika nguvu ya dhambi. Paulo anaelezea hali ya awali au ya nyuma ya dhambi ya waamini wa Korintho zikiwemo dhambi za kutisha. Kisha akasema, “Lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki…” (1 Wakorintho 6:11).
Umuhimu wa Msalaba
Hakuna mtu anayeweza kutoa malipo kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe. Dhambi ni kwenda kinyume cha Mungu wa milele. Na ubinadamu hauna chochote chenye thamani ya umilele cha kulipia.
Hakuna chochote ambacho mwanadamu angeweza akafanya kwa ajili ya hitaji lake mwenyewe; kwa hiyo, hakuna chochote ambacho mwanadamu angetakiwa kutoa kwa ajili ya wokovu (Wagalatia 3:21). Kama kungekuwa na uwezekano wa mwanadamu kufanikisha wokovu wake mwenyewe, hakungekuwepo na haja yeyote ya Yesu kufa kifo cha msalaba (Wagalatia 2:21).
► Je, kama Yesu angetaka kusamehe dhambi, kwa nini asingefanya hivyo bila ya msalaba?
Kwa kuwa Mungu ni mtakatifu, ni lazima atafanya hukumu kwa mujibu wa kweli na haki (Warumi 2:5-6 ).
Jaribu kufikiria kama dhabihu ya Kristo haingefanyika. Je, ingekuwaje kama Mungu kirahisi tu angeamua kusamehe dhambe bila ya kuwepo kwa upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu?
Kama Mungu angesamehe dhambi bila ya kuwepo kwa upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu, ingeonekana kwamba dhambi siyo kitu hatari. Ingeonekana kwamba Mungu siyo mwenye haki na vile vile siyo mtakatifu. Ingeonekana kwamba mbele ya macho ya Mungu kuna tofauti ndogo sana kati ya mtu anayetenda mema na mtu anayetenda maovu.
Kama msamaha ungekuwa bila ya kuwepo kwa upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu, Mungu hangeweza kuwa anaabudiwa kama mwenye haki na mtakatifu. Msamaha bila ya kuwepo kwa upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu mwisho wake ungekuwa ni kutomheshimu Mungu badala ya kumheshimu.
Mungu ni wa upendo na anataka kusamehe. Hakutaka kuwaacha wanadamu kwenye hali ya dhambi ambayo ingekuwa ni kupotea milele, ingawaje ndio halali yao waliyokuwa wanastahili.
Dhabihu ya Yesu juu ya msalaba ilitoa dhabihu yenye thamani ya milele iliyokuwa inahitajika. Yesu alistahili (1)kwa kutokuwa mtenda dhambi (2 Wakorintho 5:21) (mkamilifu na asiyehitaji wokovu wake mwenyewe), na (2) kufanyika kwake kuwa ni Mungu na Mwanadamu kwa wakati moja.
Upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu ulitoa kilichokuwa kinahitajika kama msingi wa msamaha. Kwa sasa, Mungu anaweza kumsamehe mtu ambaye anatubu na kuamini ahadi yake. Hakuna mtu yeyote anayeelewa kuhusu dhabihu ya msalaba anayeweza kufikiri kwamba dhambi siyo kosa kubwa mbele ya Mungu.
Upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu ulitoa njia ambayo Mungu anaweza kuichukulia kwamba ni ya haki kwa mwenye dhambi anayeamini katika ahadi yake na bado akawa mwenye haki. Warumi 3:20-26 inatoa ufafanuzi wenye mantiki wa jinsi upatanisho wa Mungu na binadamu kwa maisha na kifo cha Yesu unavyofanya kazi.
Biblia inatueleza kwamba njia ya ukombozi ambayo Mungu aliitoa ndiyo njia peke yake. Kama mtu ataukataa wokovu kwa njia ya neema, hawezi akaokolewa (Marko 16:15-16, Matendo 4:12, Waebrania 2:3).
Hii ndiyo sababu ni muhimu kuelewa kuhusu imani ya wokovu kwa njia ya neema peke yake, inayopokelewa kwa imani peke yake. Wokovu ni kwa njia ya neema peke yake kwa sababu hakuna lolote tunaloweza kulifanya ili kupata wokovu au kustahili wokovu. Ni kwa njia ya imani tu tunayoweza kufanya katika kuufanikisha wokovu. Tunawza tu kuamini ahadi ya Mungu.
Neema ya Kwanza
► Je, ni kitu gani kinachotangulia kwanza: Mwitikio wa mwanadamu kwa Mungu au kazi ya Mungu ndani ya mwanadamu?
Nema ya Mungu hufika hadi kwenye moyo wa mwenye dhambi, inamhukumu kuhusiana na dhambi zake na inamsababishia awe mwenye kuhitaji msamaha (Tito 2:11, Yohana 1:9, Warumi 1:20). Mwenye dhambi hana nguvu za kuachana na dhambi zake bila ya msaada wa Mungu (Yohana 6:44). Mungu humpa mwenye dhambi uwezo wa kuipokea injili. Kama mtu akiwa hajaokoka, siyo kwa sababu hakuwa na hiyo neema, ila ni kwa sababu hakutaka kuipokea neema ambayo Mungu ameitoa kwake.
Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi ya ulimwengu, na Mungu anamtaka kila mtu aokoke (2 Petro 3:9, 1 Yohana 2:2, 1 Timotheo 4:10). Neema ya Mungu inampa kila mwanadamu uwezo wa kukubali kupokea, lakini hamlazimishi mtu yeyote. Hiyo ndiyo sababu Mungu anamwita kila mwenye dhambi kuchagua kutubu na kuamini (Marko 1:15).
Kuelezea maana ya Toba
► Je. Toba ni nini?
Toba maana yake ni kwamba mwenye dhambi anajisikia mwenyewe ni mwenye hatia na anayestahili adhabu na kwamba yuko tayari kuachana na dhambi zake.
Aya hii kutoka katika Isaya inafafanua kuhusu toba:
Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa (Isaya 55:7).
Toba haimaanishi kwamba mwenye dhambi ni lazima ayarekebishe maisha yake na ajihesabie mwenye haki mwenyewe kabla Mungu hajamsamehe. Kwa jinsi hiyo haiwezekani kwa sababu mtu kama huyo yuko kifungoni na hawezi akajifungua mwenyewe; badala yake mwenye dhambi anapaswa awe na hiari kwa ajili ya Mungu kumtoa katika dhambi zake.
► Wokovu unapokelewa kwa imani; sasa ni kwa nini toba iwe ni muhimu kwa ajili ya wokovu?
Imani ndiyo peke yake hitaji la msamaha, laini imani iliyo ya kweli ndani ya Kristo siku zote itasababisha watu kutubu dhambi zao. Kumgeukia Kristo (kuamini) na kugeuka kutoka katika dhambi (kutubu) kutatokea kwa wakati mmoja, lakini ni imani inayofanya kugeuka kutoka katika dhambi kuwe jambo linalowezekana. Hii imani yenye kuokoa ni kipawa kutoka kwa Mungu (Waefeso 2:8-9). Kama mtu hayuko tayari kutubu, ni kwamba hayuko tayari kuokolewa kutoka katika dhambi.
Kama mtu hatatubu, ni kwamba hataki kukiri uovu wa dhambi. Kama hawezi kujiona ni kwa nini aachane na kutenda dhambi, basi mtu huyo hazioni dhambi zake kama kweli ni uovu. Kama hawezi kuona kwamba dhambi zake ni uovu, kwa uhakika haelewi ni kwa nini anahitaji msamaha
Kama mtu hawezi kujiona mwenyewe kwamba ni mwenye hatia, bila ya kujitafutia sababu, na anayeitaji adhabu, bado anakuwa hajatubu. Kama atakiri kwamba yeye ni mwenye dhambi lakini anahitaji kukaa na dini ambayo itamwachia mwanya wa kuendelea kutenda dhambi, bado anakuwa hajatubu kwa sababu bado anataka aendelee kufanya kile kilichomfanya awe mwenye hatia.
Kuelezea maana ya Imani Iokoayo
► Kama mtu anayo imani iokoayo, je, inamaanisha nini kwamba ameamini?
(1) Anajiona kwamba hawezi kufanya lolote la kuweza kujihesabia haki yeye mwenyewe.
Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu (Waefeso 2:8-9).
Anajitambua kwamba hawezi akafanya lolote (matendo) litakalomfanya astahili kuokolewa, hata kwa sehemu kidogo tu.
(2) Anaamini kwamba dhabihu ya Kristo inatosha kwa ajili ya msamaha wake.
Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote (1 Yohana 2:2). Kituliza hasira, kiombea msamaha
Kipatanisho maana yake ni kwamba dhabihu ndiyo inayofanya msamaha wetu kuwa jambo linalowezekana.
(3) Anaamini kwamba Mungu atamsamehe yeye kwa sharti la imani peke yake.
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote (1 Yohana 1:9).
Ikiwa atafikiria kwamba kuna masharti mengine, maana yake kwa sehemu, anategemea kusamehewa kwa matendo yake badala ya kusamehewa kikamilifu kwa neema.
Kubadilika na au Kuokoka
► Mwanafunzi atahitajika kusoma Matendo 26:16-18 kwa ajili ya kikundi. Je, aya hizi zinasema nini kuhusu huduma ya Paulo itakavyokuwa?
Huduma ya Paulo itakuwa ni kuongoza watu wafikie kuokoka. Aya ya 18 inaelezea kuhusu kuokoka. Inahususha pamoja na kugeuka kutoka katika giza na kurejea nuruni, na kutoka katika nguvu za shetani na kumrejea Mungu, kupokea msamaha, na kupokea urithi kwa wale wote ambao watatakaswa. Hayo yote yanapatikana kwa imani katika Kristo.
[1]Kubadilika na au uokoka kutoka kuwa mwenye dhambi hadi kufanyika Mkristo kamili ni mabadiliko makubwa sana. Biblia inataja kama ni uzao mpya (2 Wakorintho 5:17 ). Mambo ya kale yamepita, na kila kitu kimekuwa kipya.
Mtu aliyeokoka huachana na masanamu na taratibu zote za kidini ambazo zina mgogoro na uaminifu kamili kwa Mungu (1 Wathesalonike 1:9 ).
Mabadiliko kwa kawaida huwashangaza watu wengine (1 Petro 4:3-4 ). Hawaelewi ni kwa jinsi gani mtu anaweza akawa na mabadiliko makubwa hivyo. Marafiki zake wa karibu na jamii yake wanaweza wakamtesa (Mathayo 10:34-36).
Mtu aliyeokoka hashiriki tena na tamaa na vitu ambavyo ni vipaumbele vya kidunia. Tofauti hii ndiyo inayoonyesha shuhuda za kwamba mtu huyu ameokoka (1 Yohana 2:15). Mtu aliyeokoka anawapenda watu wengine walioamini na anatamani kuwa katika ushirika pamoja nao (1 Yohana 3:14).
Matamanio ya mtu hubadilika anapokuwa ameokoka. Bado ataendelea kuwa na majaribu, lakini anakuwa na uwezo wa kuhimili matendo ya kutenda dhambi kwa sababu hatawaliwi tena na tamaa za dhambi. Ana matamanio ya Neno la Mungu kwa sababu anakuwa ameshajionea neema ya Mungu (1 Petro 2:2-3).
Mtu aliyeokoka anampenda Mungu na atataka ampendeze yeye. Hatazichukulia amri za Mungu kama ni ngumu na zisizopendeza (1 Yohana 5:2-4 ).
Mtu aliyeokoka huuimarisha uhusiano endelevu na Mungu, na zaidi sana katika maombi (1 Wakorintho 1:2).
► Kwa maneno yako mwenyewe, elezea jinsi mabadiliko yanavyotokea wakati mtu anapookoka.
“Mchungaji mwenye uadilifu hataweza kuridhika na ‘maamuzi’ bali na waamini ambao wanaendelea mbele kwa bidii kwenye uhusiano wao na Kristo; waamini ambao wana njaa ya Neno la Mungu, wanaotembea kwenye upendo wa Kikristo, ambao daima hushiriki kwa imani katika kifo cha Kristo na kufufuka, na wanaoomba bila ya kukoma,”
- Timothy Keep,
“The Integrity of Biblical Evangelism
and Conversion”
Tabia za Uzao Mpya
Biblia inasema kwamba wakati mtu anapozaliwa mara ya pili, mambo yote hufanywa kuwa mapya. Mambo mapya ni pamoja na yafuatyo:
Asili mpya—asili ya kiroho (2 Petro 1:4 ).
Bwana mpya—Kristo kupitia Roho Mtakatifu (Mathayo 23:10, Warumi 8:14).
Hamu mpya ya Neno la Mungu (1 Petro 2:2 ).
Tabia mpya ya upendo (Warumi 5:5, 1 Yohana 4:7-8).
Uhusiano mpya na Mungu kama mwana au binti (Yohana 1:12).
Msaidizi mpya katika Roho Mtakatifu (Yohana 14:16, Warumi 8:26-27).
Wakili mpya katika Yesu Kristo kama tutaangukia kwenye dhambi (1 Yohana 2:1).
Matumaini mapya ya kuishi maisha ya milele (Warumi 8:12, 1 Yohana 3:2).
Uhakika Binafsi wa Wokovu
► Je, sababu gani potofu ambazo zinamfanya mtu ajifiirie kwamba yeye ni Mkristo?
Mtu anaweza kujifikiria kwamba yeye ni Mkristo wa sababu zifuatazo:
Kwamba yeye alibatizwa.
Kwamba ni mshirika wa kanisa.
Kwamba anaamini baadhi ya imani za Kikristo (doctrine).
Kwamba anashika mapokeo kadhaa ya kidini.
Kwamba anafuata msingi fulani wa matendo ya haki.
Kwamba ana uzoefu na mambo kadhaa ya kiroho.
Kwamba alishafanya maamuzi na ukiri wa imani.
Kwa mujibu wa Biblia, hakuna hata kipengele kimoja katika hivi vyenye uhakika wa kutosha wa kumhakikishia mtu kwamba ni Mkristo.
Biblia inatueleza kwamba tunaweza kujua kwa uhakika kwamba tumeokoka. Tunaweza kuwa na uhakika na Mungu kwamba ametukubali. Hatuna sababu ya kuishi katika hofu, kwa sababu Roho wa Mungu anatuhakikishia kwamba ametuasili kuwa wana wa Mungu (Warumi 8:15-16).
Uhakika huu umekamilika kabisa kiasi kwamba hatupaswi kuwa na hofu ya Siku ya Hukumu (1 Yohana 4:17). Baadhi ya watu wanasema kwamba wanategemea wanaweza kupokelewa mbinguni, lakini sisi tunakuwa na uhakika zaidi ya huo. Haitoshi tu kuamini kwamba wokovu unatolewa kwa mwanadamu yeyote kwa ujumla; mtu ni lazima ajijue kama yeye binafsi ameokoka.
► Je, mtu anawezaje kujua kwa uhakika kwamba ameokoka?
Baadhi ya watu wanategemea hisia zao, lakini hisia hubadilika na zinaweza zikapotosha.
Maisha yaliyobadilishwa yanatoa ushahidi kwamba mtu ameokoka, lakini ushahidi huo haupo kwa wakati huo huo wa mwanzo. Matokeo ya wokovu hayana muda wa kutokea. Kwa hiyo, maisha yaliyobadilishwa siyo msingi wa uhakika.
Mwamini anaweza akawa na uhakika wa wokovu wake kwa kujua kwamba amefuata njia za wokovu za kimaandiko. Kama mtu kweli ametubu kama Biblia inavyoelekeza, ana haki ya kuamini kwamba Mungu amemsamehe. Wakati mtu anapotubu na kuamini, Mungu humpa ushuhuda wa Roho wake kwamba sasa amefanyika kuwa mtoto wa Mungu.
Kama mtu atajaribu kujihisi kwamba yeye ameokoka wakati kiuhalisia hajawahi kutubu, atajichanganya na atakuwa anajidanganya yeye mwenyewe.
Kama mtu (1) atatubu kwa ukweli, (2) ataamini ahadi ya Mungu katika Maandiko, na (3) atapokea ushuhuda wa Roho Mtakatifu, hataweza kudanganyika. Uhakika huu uko katika msingi wa Neno la Mungu, ambalo kwa uhakika linaaminika kabisa. Mungu siku zote hutimiza ahadi zake.
Maneno 10 yanayohusiana na Vipengele vya Wokovu.
Upatanisho: Neno hili linamaanisha kwamba waliokuwa maadui hapo mwanzo wamerejea kwenye amani tena. Katika wokovu, tunafanya aman na Mungu (2 Wakorintho 5:19, Warumi 5:1.[1]
Kufidia kosa: Neno hili linamaanisha kwamba kumbukumbu zimefutwa. Katika wokovu, kumbukumbu za makosa yetu zimefutwa (Waebrania 8:12).
Kipatanisho: Neno hili linamaanisha kwamba kuna kitu kilichofanyika ili kutuliza ghadhabu ya mtu mwingine. Katika wokovu, dhabihu ya Yesu ilibadilisha kabisa ghadhabu ya Mungu iliyokuwa juu yetu (1 Yohana 2:2).
Kuokolewa: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anaokolewa kutoka katika mikono ya mtu mwingine mwenye nguvu. Katika wokovu, tumeokolewa kuwa chini ya nguvu za Shetani na dhambi (Luka 1:74; Warumi 6:6, 12-18).
Kukombolewa: Neno hili linamaanisha kwamba fidia inalipwa ili mtu aweze kuwekwa huru. Katika wokovu, kifo cha Yesu ni fidia kwa wengi ili tuweze kuwekwa huru kutoka katika kifungo na adhabu ya dhambi (Waefeso 1:7, Tito 2:14).
Kuhesabiwa haki: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anahesabiwa kuwa mwenye haki, na asiyekuwa na hatia. Katika wokovu, mwenye dhambi ambaye ana hatia anahesabiwa kuwa mwenye haki tena kwa sababu Yesu aliteseka badala yake (2 Wakorintho 5:19, Warumi 5:1).[2]
Utakaso: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anafanywa kuwa mtakatifu. Katika wokovu, mwenye dhambi anatakaswa na kufanywa mtoto mtakatifu wa Mungu (Waefeso 1:1, Wakolosai 1:1, Wafilipi 1:1).[3]
Kuasiliwa: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anafanywa kuwa mtoto halali kisheria wa mtu mwingine. Katika wokovu, tunafanyika kuwa watoto wa Mungu (Yohana 1:12, Warumi 8:15).
Urejesho/Uzao Mpya: Neno hili linamaanisha kwamba mtu anaanza tena maisha kwa upya. Katika wokovu, mwamini anaanza tena maisha mapya (Waefeso 2:1, Yohana 7:38-39, Wagalatia 4:29, Yohana 3:5).
Kutiwa muhuri: Neno hili linamaanisha kwamba kitu fulani kimefungwa kwa lakiri ili kuonyesha ni nani anayehusika nacho. Katika wokovu, Roho Mtakatifu ndani yetu anakuwa lakiri ya kututambulisha kwamba sisi ni mali ya Mungu (Waefeso 1:13).
[1]Aya hizi kwa pamoja zinaelezea kuhusu kuhesabiwa haki na upatanisho
[2]Aya hizi kwa pamoja zinaelezea kuhusu kuhesabiwa haki na upatanisho
[3]Nyaraka nyingi zimerejea kuhusu waamini kama “watu waliotakaswa”
Kosa la Kuepuka: Kuwa na Dini bila Toba
Kuna aina ya mtu ambaye kwa urahisi tu huwa anafikiria kwamba ameokoka anapokuwa akisikia kwamba wokovu ni kwa neema kupitia imani. Hajawahi kufanya toba ya kweli kwa sababu hakuona kama alihitaji hilo. Hakuwahi kujiona mwenyewe kwamba ni mwenye dhambi anayestahili adhabu ya Mungu. Anafikiria kwamba neema maana yake ni kufanya kwa jinsi yake anavyoona yeye mwenyewe. Kwa vile anakubali ukweli wa Ukristo, anajifikiria kwamba yeye ni Mkristo ingawaje hajawahi kufanya mabadiliko au mageuzi ya maisha yake. Kamwe hajawahi kusalimisha nia na dhamira ya mapenzi ya nafsi yake; badala yake, alimkubali Mungu tu kama sehemu ya maisha yake ya kawaida na bado kwa sehemu kubwa anaishi kufuatana na mapenzi yake mwenyewe. Huu siyo mwanzo wa uhusiano na Mungu unaookoa, kutokana na maelezo ya kimaandiko.
Kazi za Kufanya
(1) Katika somo hili tumejifunza maneno 10 yanayohusiana na vipengele vya wokovu. Elezea kwa kuandika aya chache ni vipengele gani vinavyoonekana kuwa muhimu sana kwako katika uhusiano wako na Mungu. Je, viko vingine unavyohitaji kuvifikiria zaidi?
(2) Kutokana na aina za Ukristo zinazoonekana katika nchi yako, na hususani katika mkoa wako, watu wanafikiri inamaanisha nini kuwa Mkristo? Kwenye kurasa 2-3, elezea aina mbalimbali za watu na jinsi wanavyouelezea Ukristo kwamba ni nini. Fafanua ni kitu gani kilichopotoka katika mtazamo wao kuhusu toba, imani inayofanya kazi, au imani nyingine yeyote.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.