Uinjilisti katika Historia: Mifano ya John Wycliffe na John Wesley
John Wycliffe alikuwa mchungaji nchini Uingereza. Aliishi kuanzia mwaka 1324-1384. Wakati ule, Biblia ilikuwa haipatikani kwenye lugha za watu zinazoeleweka. Watu walikuwa wanategemea kile kilichokuwa kikifundishwa kutoka katika Kanisa Katoliki la Kirumi. Watu wengi walikuwa hawaijui injili. Hata makasisi wengi wa Kikatoliki walikuwa hawaijui Biblia vizuri. Makasisi walisafiri nchi nzima wakifanya mila za kidini na kutaka wapewe fedha. Makanisa mengi yalikuwa yanaongozwa na makasisi ambao walikuwa hawahubiri injili. Wycliffe na wasaidizi wake waliitafsiri Biblia kwenda katika lugha ya Kiingereza. Uchapishaji kwa mashine haukuepo kwa wakati huo, kwa hiyo walinukuu maandiko kwa kutumia mikono. Walisafiri wakiwa watu wawili wawili na kufundisha Biblia kwa makundi mbalimbali kila mahali. Watu waliwaita “makasisi maskini” kwa sababu walikuwa hawaombi fedha.
Mbinu za uinjilisti ni lazima zitumiwe kutokana na mazingira ya jamii. Wycliffe na wasaidizi wake walikamilisha sehemu yao ya msingi ya uinjilisti; waliupeleka ujumbe wa Bibilia moja kwa moja kwa watu.
John Wesley aliishi katika nchi ya Uingereza kuanzia mwaka 1703-1791.[1] Kuanzia wakati ule, Kanisa la Anglikana lilikuwa limefanyika kuwa ni kanisa la matajiri. Walikuwa watu wa matambiko na hawakufundisha injili iliyo wazi. Watu wengi katika taifa waliokuwa maskini sana hawakualikwa waingie makanisani na walikuwa hawaijui injili. Wesley alikuwa ni kasisi wa Kianglikana, lakini alikuwa anataka aipeleke injili kwa watu. Siku moja asubuhi, alikwenda kwenye shamba ambalo wachimba mkaa wengi walikuwa wakipita njiani kuelekea kazini. Alianza kuhubiri, na wachimba mkaa wengi wakasimama ili kusikiliza. Baada ya hapo, alikuwa anahubiri mikutano ya nje kila siku kwa kipindi chote cha maisha yake. Maelfu ya watu walibadilika kupitia huduma yake.
► Je, ni mmisionari gani anayekumbukwa kwa kuwa mtu wa kwanza kuleta injili kwenye eneo lako?
[1]Image: "John Wesley preaching on his fathers grave", by Currier & Ives, retrieved from the Library of Congress Prints and Photographs Division, https://www.loc.gov/pictures/item/2002707689/, "no known restrictions."
Hitaji la kurekebisha Mbinu
Katika mwaka wa 2003, mtu mmoja alikuwa anasafiri nchini Uingereza pamoja na familia yake na akasimama katika bustani kwa ajili ya mapumziko. Alimwona mwanamke mmoja akiwa amesimama kwenye kilima kimoja cha ile bustani. Alikuwa na Biblia na alikuwa akiongea. Alimsogelea karibu na akawa anamsikia akizungumzia kitu kama cha kidini. Alitambua kwamba alikuwa na rafiki aliyekuwa amesimama pembeni mwake, kwa hiyo akamwuliza yule rafiki yake ni nini kilichokuwa kinaendelea mahali pale. Yule rafiki akamjibu, “Sisi ni sehemu ya kikundi ambacho tunaendeleza mila ya kuhubiri mikutano ya nje kama alivyokuwa anafanya Wesley. Mara kwa mara tunaenda kwenye maeneo ya wazi ya kijamii kwa ajili ya kuhubiri.” Hata hivyo, yule mtu aliangalia kwa makini na kuona kwamba yule mama alikuwa amekaa kwenye eneo ambalo watu wachache walikuwa wakipita, siyo wote waliokuwa wanamsikia, na mbinu yake aliyokuwa akitumia ilikuwa haina ufanisi wa kufanya watu waliokuwa kwenye maeneo hayo ya nje waweze kumsikiliza. Alikuwa anajaribu kuendeleza mila, lakini alikuwa amepoteza kila kitu ambacho hapo awali kilifanya mbinu za kuhubiri mikutano ya nje kuwa na ufanisi.
Ni lazima kurekebisha mbinu ziendane na mazingira mbalimbali. Mara nyingine watu hudhania kwamba kuna njia moja tu ya kufanya uinjilisti, na wanaendelea na mbinu ambayo haina ufanisi tena. Mara nyingine, watu hufikiri kwamba mbinu iliyokuwa na ufanisi katika eneo moja itakuwa pia na ufanisi kila mahali katika maeneo mengine, lakini hiyo siyo kweli.
Katika maeneo mengi kanisa lilikuwa likifanya uinjilisti wa kwenda nyumba kwa nyumba, wakigonga hodi kwenye milango ya watu ambao walikuwa bado hawajawahi kukutana nao. Mbinu hii ilisababisha kuwepo na watu wengi sana waliobadilika na kuokoka, lakini haikuwa na ufanisi kwenye kila eneo.
Baadhi ya makanisa yalinunua mabasi na kuyatumia kuleta watu kwenye nyumba za ibada. Kila Jumapili asubuhi wataendesha basi katika maeneo yote ya jirani wakikusanya watu. Watu wengi walibadilika na kuokoka kupitia “huduma ya mabasi,” lakini mbinu hii hakufanya kazi kwa kila eneo.
Makanisa mengi yamekuwa yakifanya uinjilisti kwa kuhubiri injili kwa kundi la watu waliokuwa wanakuja kwenye nyumba za ibada siku za Jumapili. Wanawaalika kuja mbele madhdbahuni kwa ajili ya kuokoka. Maelfu ya watu wamebadilika na kuokoa kupitia mbinu hii, lakini watu wengi wasiookoka hawaji kwenye nyumba za ibada. Watu wengi hawataweza kuisikia injli hadi hapo mtu ashirikishane pamoja nao kibinafsi kwenye mazungumzo.
Mtume Paulo alikuwa ni mfano wa kuigwa wa kurekebisha mbinu za uinjilisti. Alikuwa anaweza kuzungumza ndani ya masinagogi ya Kiyahudi kwa sababu alikuwa ni rabi wa Kiyahudi aliyekuwa amefuzu, na aliweza kuwaelezea kwamba Yesu ni Masihi. Aliweza pia kuongea kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu waliokuwa wakipeana mawazo ya kifalsafa. Mara nyingine aliongea kwenye maeneo ya masoko. Mara nyingi alikuwa anaongea kwenye makundi yakiwa majumbani kwao.
Baadhi ya Mbinu za Kisasa
Watu wamekuwa wakitumia njia nyingi tofauti katika kuanzisha mazungumzo kuhusu injili. Baadhi ya makanisa wamekuwa wakitumia maswali ya kiuchunguzi. Wanaenda kwenye maeneo yote katika jamii na kuuliza mawali kama haya: “Je, unafikiri kanisa lifanye nini kwenye jamii? Ni imani gani muhimu sana ya Kikristo? Unawezaje kuelezea kuhusu Mkristo ni nani? Ni kwa jinsi gani mtu anakuwa Mkristo? Baada ya kusikiliza kwa ustahimilivu mkubwa maoni ya watu, Mkristo anaweza akauliza, “Je, ninaweza kukuonyesha kile ambacho tunaamini Biblia inasema kuhusu Mkristo ni nani?”
Wakati mwingine wainjilisti wakiwa kwenye maeneo ya wazi ya kijamii wanawafanya watu kuvutiwa pamoja na kuwa na umakini kwa kuweka bango lililochorwa picha au mchoro vikielezea kuhusu injili. Wengine hutengeneza michoro kwa kutumia chaki. Baadhi ya wainjilisti huweka picha nzuri za rangi kwenye mbao za matangazo huku wakiwa wanatoa maelezo yao.[1]
Baadhi ya makanisa kutoa semina juu ya somo la kivitendo linalohitajika na watu wa eneo husika katika jamii. Somo linaweza kuwa kuhusu ndoa, jinsi ya kuwakuza watoto, kanuni za biashara, afya, au mafunzo yanahusiana na aina fulani ya kazi. Kanisa linafanya jambo jema linapokuwa linatoa huduma kwenye mahitaji ya kijamii ya eneo husika. Kanisa lina wajibu wa kuonyesha jinsi kweli za Biblia zinavyofanya kazi kwenye maisha ya kila siku. Semina inaweza isilenge kwenye uwasilishaji wa injili moja kwa moja, lakini inafundisha ukweli wa Biblia na kukuza mahusiano kati ya kanisa na majirani zake.
Baadhi ya makanisa yameanzisha vituo vya maombi vya muda kwenye maeneo ya wazi ya kijamii ambayo watu wanapita. Wanaweka hapo alama ya ishara inayosema, “Kituo cha Maombi” na hupanga kujitolea kuomba pamoja na watu wanaopita njiani. Wanauliza, “Je, unalo hitaji ambalo ungependa mimi niombe kwa ajili yake?” Wanaonyesha kuhusika na mahitaji ya watu na hawaanzishi mabishano. Mara nyingi, wanakuwa na nafasi ya kushirikisha injili.[2]
Hitaji la msingi na la muhimu sana la mbinu ya uinjilishaji ni kwamba injili inawasilishwa kwa uwazi kwa watu ambao wanahitaji kuisikia. Kwa kuwa Mungu hulipa nguvu Neno lake na Roho Mtakatifu huleta hukumu na mguso ndani ya wale wanaolisikia, mbinu ya uinjilisti ina uwezekano mkubwa wa kuleta ufanisi kama itawasilisha injili kwa uwazi na kwa njia ya moja kwa moja.
Changamoto ya kanisa katika maeneo yote na kila wakati ni jinsi ya kutafuta njia ya kuleta usikivu mkubwa wa watu na kufikisha injili kwenye jamii yote.
► Je, kuna njia gani ambazo kanisa katika mji wako au eneo lako linatumia katika kupata usikivu wa watu? Je, mbinu hizo zinafikisha ujumbe wa injili?
[1]Kwa ajili ya mifano ya mbinu hii, ona: The Open Air Campaigners websites: www.oacgb.org.uk and www.oacusa.org.
[2]Kwa ajili ya picha na taarifa, ona mitandao ifuatayo: www.prayerstations.org and www.prayerstand.com
Kufanya Uinjilisti kwa Marafiki
Aina ya uinjilisti ulio na ufanisi mkubwa sana ni ule ambao mtu anamweleza moja kwa moja mtu mwingine ambaye anamjua na anamwamini.
Mkristo anapaswa awe na ufanisi mkubwa wakati anaposhuhudia kwa marafiki zake, watu anaowafahamu na jamaa zake kwa sababu wanakuwa wameshaona mfano wa maisha yake. Kama maisha yake ni mazuri, kuna uwezekano mkubwa wao kuamini ushuhuda wake. Ni muhimu sana kwa Mkristo kudhihirisha imani yake ili siku zote watu wajue kwamba yeye ni Mkristo. Hapaswi kujisikia kwamba ni fedheha au anatahayarishwa kwa ajili ya watu kumwona akisoma Biblia au akiomba. Watu wanaomjua hawatamshangaa watakapokuwa wanamwona akifanya hayo kwa sababu wanatambua kwamba yeye ni Mkristo.
Mkristo anaweza akaheshimika kwa mfano wake shuleni au sehemu yake ya kazi hata na watu ambao hawaupendi ukristo. Hata wale watu wanaomsababishia mateso watamheshimu kama atakuwa ni mtu mwenye msimamo katika matendo yake na tabia zake. Baadhi ya watu watakuja kwake kwa ajili ya maombi na kupata ushauri.
Makabiliano binafsi ya Mtu kwa Mtu
Baadhi ya watu wanafikiri kwamba ni lazima wawe wanamjua mtu kwa kitambo fulani kabla ya kumshuhudia. Wanajaribu kuwa marafiki kwanza kabla ya kumshuhudia habari za Mungu. Ni ukweli kwamba mtu ana uwezekano mkubwa wa kumsikiliza rafiki yake. Hata hivyo, inawezekana kuonesha ukakumjali mtu kwa dhati usiyemfahamu na kuonesha hamasa kwa haraka sana. Kama hatutaweza kujifunza jinsi ya kushirikisha injili kwa watu tunaokutana nao, tutakosa upenyo wa nafasi nyingi zitakazotufanya tuwe na ufanisi. Somo lililotangulia kuhusu “Kufungua Milango” linatupa mbinu za kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya injili.
Mtu mmoja alisema, “Wakati wowote niwapo mwenyewe pamoja na mtu mwingine kwa dakika chache, ninautumia muda huo kama ni kikao kilichoandaliwa na Mungu. Alimaanisha kuwa anaamini kwamba Mungu humpa watu wa kukutana nao kwa kuwatumia kwa ajili ya injili.
Injili kwa Maandiko
Unaweza ukafanya jambo katika kupeleka injili ambalo Mtume Paulo hakuweza kulifanya.
Tunayo mbinu ya kupeleka injili ambayo ilikuwa haipatikani katika kanisa kwa karne nyingi: taarifa zinaweza kuchapishwa na mashine kwenye karatasi.
► Je, unafikiri kulikuwa na tofauti gani kihuduma kabla ya kuwepo kwa uchapishaji?
Jaribu kufikiria huduma katika nyakati ambazo kulikuwa hakuna uchapishaji. Kila nakala ya kitabu ilihitaji siku nyingi za kufanyiwa kazi na mwanazuoni kwa sababu kilikuwa ni lazima kiandikwe kwa mkono. Unaweza ukafikiria kwamba vitabu kwa wakati huu ni ghali, lakini fikiria kulipia kitabu kwa bei ile ile ambayo ungepaswa kumkodisha mtaalamu mwenye ujuzi kwa kazi ya siku kumi.
Takribani hakuna mtu yeyote aliyekuwa na nakala yake mwenyewe ya Maandiko. Hata mchungaji ingewezekana asiwe na Biblia yote nzima. Fikiria kama hungekuwa huna uwezekano wa kusoma Biblia ukiwa nyumbani.
Mafunzo kwa wachungaji mara nyingi yalifanyika kwa kuzungumza, na walipaswa kujaribu kukumbuka kile walichokisikia. Kulikuwa hakuna jinsi yeyote ya kupeleka makabrasha ya mafunzo sehemu nyingine. Bila uchapishaji, hakuna kitu ambacho kingeweza kikaandikwa na kusambazwa kwa wingi.
► Je, kuna njia gani ambazo uchapishaji husaidia kuenea kwa injili?
Vipeperushi ni vipande vidogo vya karatasi vilivyochapishwa makala, kwa kawaida zikiwasilisha injili. Wakristo wanaweza wakavigawa kwa watu wanaokutana nao. Vinaweza pia vikatolewa kwa kiwango kikubwa kwenye maeneo ya wazi ya kijamii. Vinaweza vikaachwa katika maeneo ambayo watu watavisoma.
Kama mtu hajawahi kufanya sana uinjilisti kwa watu wageni, kugawa vipeperushi ndio njia nzuri ya kuanzia.
Kipeperushi kinahitajika kiwe cha kupendeza na chenye kichwa cha habari chenye mvuto. Wakati wa ugawaji wa vipeperushi kwa watu barabarani au maeneo mengine ya wazi ya kijamii, kuwa mtu wa kucheka na kusalimia watu. Unaweza ukasema, “Haloo, umeshapata mojawapo ya vipeperushi hivi?” Hiyo itawafanya watu kuwa na shauku ya kutaka kuona ni nini kilichopo.
Inawezekana ikaonekana kwamba watu wengi hawana shauku na vipeperushi ambavyo umewagawia. Watu wengi wanaweza wakavitupa bila hata ya kuvisoma. Hata hivyo, pia, kuna matokeo mazuri. Watu wengi wamebadilika na kuokoka kwa sababu ya ujumbe wa vipeperushi. Kwa kawaida hutajua matokeo yaliyotokana na vipeperushi ulivyogawa.
Kutana na mahitaji kwa vitendo
[1]Mara nyingine watu wana wasiwasi na hitaji halisi la maisha. Wanaweza wakawa hawana chakula cha kutosha, au maeneo ya kujisitiri kwa malazi, au matibabu. Wanakuwa na hisia kwamba mahitaji hayo ni muhimu na ya haraka kuliko hitaji la kiroho. Kanisa linaweza kushiriki kwa vitendo kwenye mahitaji haya kama njia ya kushirikisha injili. Tatizo la msingi hapa ni kwamba mtazamo wao unaweza ukaelekezwa kwenye mahitaji ya kidunia tu kuliko mahitaji ya kiroho, kama ulivyo mtazamo wa watu ambao hawajaokoka.
Kanisa linapaswa liwajibike kwa vitendo kwenye mahitaji halisi lakini ni lazima lidumishe baadhi ya taratibu ambazo zinaweka mkazo kwenye kipaumbele cha kiroho.
1. Wanapaswa watoe ufafanuzi kwamba wanashirikisha upendo wa Mungu wanaposhughulikia mahitaji ya watu.
2. Wanapaswa wafanye kazi kwa pamoja kama familia ya imani, kuliko kuwa ni shirika linalojitofautisha na kanisa.
3. Wanapaswa wawaalike watu washiriki kwenye ushirika wa kanisa mahali ambapo kila mtu anamjali mwenzake.
4. Wanapaswa kushirikisha injili, wakifundisha kwamba maisha ya milele na baraka zinatoka kwa Mungu aliye mjuzi wa mambo yote.
Huduma nyingi hutoa programu ambazo zinaendana na mahitaji ya vitu. Wanatoa huduma kwa mahitaji ya jamii kwa kiwango kile ambacho uwezo wa raslimali zao unaruhusu. Lengo lao ni kutengeneza upenyo wa nafasi wa kushirikisha injili. Wanafikiri kwamba kusaidia watu kwa njia za vitendo kutawafanya wawe marafiki wao na wataweka mkazo au ustahimilivu kwa ajili ya injili. Kanuni inayotumika hapa ni Programu, kisha Uhusiano, halafu Injili.
Kuna njia nyingi ambazo programu za msaada zinaweza kwenda vibaya. Inawezekana kwamba hakutakuwa na uhusiano. Watu watatarajia tu kupata vitu kutoka kwa kanisa. Mara nyingine injili huonekana haina uhusiano na vitu vinavyotolewa, na watu wanaweza kuwa wapokeaji wa msaada tu bila ya kuwa na shauku katika suala la injili. Hata watu wanaofanya kazi kwenye hiyo programu wanakuwa katika kutoa msaada tu na hawashirikishi injili.
Kanuni ni lazima igeuzwe. Kanisa ni lazima liweke msisitizo wake kwamba injli ndiyo kipaumbele chake wakati wa kukutana na kila mtu kwa mara ya kwanza.
Wakati kanisa linapowasilisha injili kwa ulimwengu, ni lazima wawe waaminifu kuingiza maelezo ya maisha mapya ndani ya kanisa. Kuokoka siyo tu jambo la binafsi, na uamuzi wa mtu binafsi ambao unamwacha mtu peke yake katika hali ya maisha mapya ya kushangaza. Wenye dhambi kwa kawaida hawatakubaliana na injili labda wawe wamevutiwa na jamii ya watu wa imani ambayo inawasilisha injili.
Katika huduma ya Yesu na ya mitume, tunaona kwamba injili ni “Habari Njema” za ufalme wa Mungu. Ni ujumbe ambao mwenye dhambi anaweza akasemehewa na akawa kwenye uhusiano na Mungu. Anakombolewa kutoka kwenye nguvu ya dhambi na kufanywa kiumbe kipya. Anaingia kwenye familia ya watu wa imani ambapo kaka na dada zake wa kiroho watamtia moyo na kumsaidia katika mahitaji yake.
Kanisa linapaswa lione msingi wake wa kwanza wa umisheni wa kueneza injili. Kanisa linapaswa lifanyie kazi jambo hilo wakati wote. Kila mtu anapaswa ajue kwamba kanisa ni kufanya kazi kwa ajili ya roho za watu ziokolewe. Linawavutia watu ambao wana shauku ya injili. Watu hawa huja kwenye uhusiano na kanisa, kwa hiyo, huduma ya injili hutengeneza uhusiano.
Kisha, kanisa husaidia watu walio katika uhusiano na kanisa. Inawezekana siyo watu wote katika watu hao ambao watakuwa tayari wameshaokoka, lakini wako kwenye uhusiano na wanavutiwa na huduma ya injili ya kanisa.
Kwa hiyo kanuni iliyogeuzwa itakuwa kwanza ni Injili, kisha Uhusiano, halafu Msaada (na siyo programu). Kanisa halipaswi liwe kama ni shirika linalotoa programu zake za misaada. Badala yake, kanisa ni kikundi cha watu ambacho kinasaidia watu walio kwenye uhusiano pamoja nao. Kama wataanzisha programu mbalimbali, watu watakuja kwa ajili ya hizo programu na siyo kwa ajili ya uhusiano.
“Wamisionari wa India, Uganda, na maeneo mengine wamekuwa wakilalamikiwa kwa kununua watu kuokoka kwa kuwapa fedha, misaada ya njaa, fursa za elimu, na huduma za matibabu, au kwa kuwapa mahitaji mengine yenye kipaumbele katika kuwahudumia.”
- J. Herbert Kane,
“The Work of Evangelism”
Kazi za Kufanya
(1) Angalia kwa makini mbinu za uinjilisti zinazotumiwa na makanisa katika eneo lako. Je, hizo mbinu zilifanikiwa kuwavuta watu walio nje ya kanisa? Je, zinaeneza injili kwa uwazi? Andika kurasa 2-3 juu ya mambo uliyoyaona katika uchunguzi wako.
(2) Sambaza angalao vipeperushi visivyopungua mia moja. Andika sentensi chache kuhusiana na uzoefu wako ulioupata.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.