[1]► Soma Mathayo 18:2-6, 10-14. Je, kuna maonyo gani tunayoyaona katika aya hizi? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuelezea umuhimu anaouna Mungu kwa watoto?
Mara nyingine watu husema kwamba watoto ni muhimu kwa sababu ni kizazi cha kesho, ni kanisa la baadaye, na viongozi wa baadaye. Hayo yote ni kweli; lakini mwanzo wa yote, watoto ni muhimu kwa sababu wao ni watu. Mara nyingine wazazi huonekana kusahau kwamba watoto ni watu wenye roho za milele na umaarufu na wana nguvu ambazo hazijaonekana bado.
Mtu mmoja msafiri alisimama kwenye kijiji kimoja kidogo. Alimwona babu mmoja akiwa amekaa kando ya barabara na akasema, “Sijawahi kamwe kusikia lolote kuhusu kijiji hiki kabla ya hapo. Je, watu maarufu hawakuwahi kuzaliwa hapa? Yule babu akajibu, “Hapana. Ni watoto tu.”
Mungu aliwapa watu wa kale wa Israeli Agano. Aliahidi kuwabariki na kuwaweka kwenye uangalizi wake. Aliwapa mambo ya kufanya waliyotakiwa kuyatii.
Mungu alitaka agano lake liwe ni kwa ajili ya vizazi vyote. Aliwaambia, “Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii” (Kumbukumbu la Torati 6:6-7).
Kuwakuza watoto katika kufuata mapenzi ya Mungu lilikuwa ni jambo muhimu kwa ajili ya agano, kwa sababu wingi wa baraka za Mungu zilikuwa na vigezo vya kufuata na ilitegemea kama watu wake wataendelea kumtii. Kama kizazi kilichofuata kingechagua kutokuwa waaminifu na watiifu kwa Mungu, basi wangepoteza manufaa yote ya uhusiano na yeye. Hii inamaanisha kwamba umakini mkubwa katika kufundisha watoto ulikuwa ni muhimu sana
► Je, unafikiri Waisraeli wangefanya nini katika kuhakikisha kwamba watoto wao wangekuwa ni watu wa kuamua kumfuata Mungu?
Mungu aliwapa maelekezo ya jinsi ya kuwafundisha watoto wao.
Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako (Kumbukumbu la Torati 11:19-20).
Ni kitu gani Mungu alikuwa analenga hapa? Ilikuwa wawafundishe kwa bidii, kwa uaminifu, na kwa uendelevu, na siyo tu kwa mara chache. Walipaswa wawe na vitu vya kuwakumbusha kuhusu sheria za Mungu ambavyo vingewekwa kwenye maeneo yaliyo wazi. Walikuwa wayaone Maandiko kila mahali. Kamwe walikuwa hawatakiwi kusahau au kudharau maagizo ya Mungu
Mafundisho ya mara kwa mara yalimaanisha kwamba hawakutakiwa kuwa na mapambo, au sherehe au tabia ambazo zingekuwa kinyume na sheria ya Mungu.
Kwa hiyo, aya hizi msisitizo kwa wazazi kwamba wanawajibika kuwafundisha watoto wao maadili ya Mungu mara kwa mara na kwa uthabiti na kuwalinda kutokana na mafundisho na mifano ambayo vitawafanya waende kinyume chake.
► Agizo hili lilitolewa kwa wazazi. Je, ni mambo gani tuyafanye kwa ajili ya kutumika kwenye huduma ya kanisa?
Kwanza, tunajua kwamba kuwafundisha watoto ni wajibu wa kwanza wa wazazi. Kanisa linapaswa liwafundishe wazazi jinsi ya kuwafundisha watoto wao. Kamwe hatupaswi kuwa na dhana kwamba watoto wanatakiwa wapate tu maelekezo ya kiroho kutoka kwenye kanisa kwa sababu wazazi hawawezi kufanya hivyo.
Pili, kanisa linapaswa kuhudumia watoto kwa muktadha wa familia zao kwa kadri inavyowezekana. Wasaidie watoto kwa kuwasaidia wazazi wao. Wakati wa kufanya uinjilisti kanisa lijaribu kuwa kivutio cha kuzileta familia kwenye kanisa.
Baadhi ya watoto kutoka kwenye nyumba za familia zenye watu ambao hawajaokoka huja kanisani na kuokoka. Jambo kama hilo linapotokea, kanisa lijaribu kutoa huduma kwa ajili ya hiyo familia. Kama wazazi hawataitikia hilo, kanisa ni lazima liwe ni familia ya kiroho ya watoto hao. Washirika wa kanisa watapaswa wawe kama ndugu wakubwa kwa watoto hao ambao wataonyesha kuwajali na kuwatunza kiroho.
Kufanya Tathmini ya Huduma ya Kanisa kwa Watoto
► Je, ni kwa jinsi gani unaweza kufanya tathmini ya mafanikio ya huduma ya watoto katika kanisa?
Huduma yako ya watoto siyo ya mafanikio hata kama…
Waalimu wako wa watoto wana uwezo mkubwa.
Idadi ya watoto na waalimu inaongezeka.
Watoto wanajifunza habari muhimu za Biblia.
Waalimu wanatumia vifaa vya thamani ya juu kufundishia.
Watoto wanaifurahia huduma.
Tabia hizo zitakuwepo endapo huduma kwa watoto ni ya mafanikio. Kama huduma itakosa tabia hizi, kutakuwepo na tatizo. Hata hivyo, inawezekana kwa huduma kuwa na baadhi ya tabia, au kuwa nazo zote, lakini bado ni wa kushindwa.
Huduma yako ya watoto itakuwa ya mafanikio kama…
Watoto watakuwa wamebadilika na kuokoka pamoja na kuwa na uhakika wa wokovu.
Watoto hatua kwa hatua wanakua kiroho.
Watoto wanavyozidi kuwa wakubwa, wanafuata maadili au kanuni za Mkristo.
Huduma yako haijafanikiwa ikiwa na mtoto ambaye…
Siyo Mkristo.
Amechagua kufuata mifano ya watu wengine wa kidunia.
Anafuata sherehe na mahusiano machafu kadri anavyozidi kukua.
Anakataa mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yake na anafuata tamaa zake mwenyewe.
Kutengeneza maisha yafanane na ukweli wa Mungu ni kazi ya ufuasi. Ni kumwendeleza mtu awe mfuasi wa Yesu aliyekomaa. Wakati wa kubadilika au kuokoka hakumwingizii mtu hapo hapo ukweli wa Mungu kupitia mwelekeo wake wa mawazo, tabia, dhana, na mfumo wa maisha. Kuingia huko kwa uweli huchukua muda. Hilo ndilo jukumu hasa la kufanya ufuasi.
Kitu cha Kwanza cha Lazima kwa ajili ya Huduma ya Watoto
► Je, unafikiri ni kitu gani cha kwanza unachohitaji kwa ajili ya huduma ya watoto?
Huduma ya watoto kwa haraka hutengeneza kikundi cha washiriki ambacho huhusisha watoto na wazazi wanaohusika nao. Kikundi hiki kinakuwa na viongozi wake wa kiasili, watu wanaokuwa na ushawishi kwa wengine kutokana na haiba zao, hata kama hawako kwenye nafasi za utendaji zilizo rasmi. Miongoni mwa wazazi na miongoni mwa watoto kuna viongozi wa asili.
Kitu cha kwanza kwa ajili ya huduma ya watoto ni mazingira ya Kikristo yenye hali chanya ya kiroho. Hapo unaweza kuwalea Wakristo wachanga kiakili, kimwili. kiroho na kijamii.
Hii ina maana kwamba watu wazima ni lazima wawe watu ambao ni mifano ya kiroho. Huwezi ukawatumia watu kwa ajili ya huduma ya watoto ambao siyo wakristo makini na wenye msimamo. Watoto wanaoshawishi watoto wengine kukataa ujumbe wako hawawezi kushiriki.
Huduma yako kwa watoto inakuwa tayari inaanguka kama …
Watu wazima ambao wanatoa msaada kwenye huduma wako pale kwa sababu ya uwezo wao maalumu walio nao, au kwa sababu nyingine yeyote, lakini siyo watu walio mifano mizuri ya kiroho.
Watoto wasio na shauku ya mambo ya kiroho wanatawala mazungumzo na mambo mengine ya kijamii ya kikundi.
Shughuli zote za kiroho zinaongozwa na watu wazima tu ambao hawana ushiriki wowote muhimu kwa watoto.
Watoto wachache tu ndio wanaotaka kushirikiana na kuonyesha shauku ya kiroho, lakini kijamii hawakubaliki na wengi miongoni mwa wenzao.
Angalia kwenye kikundi cha watoto na jiulize mwenyewe maswali haya. Kama kijana mdogo mgeni wa kiume ameanza kuhudhuria kwenye huduma yetu, ni watoto gani kwenye kikundi watakuwa na uwezekano mkubwa wa kumfuata? Kama kijana wa kike ameandikishwa, atataka afuatane na nani? Je, aina hizo za ushawishi ni nzuri au ni mbaya?
Kitu cha kwanza kwa ajili ya huduma ya watoto ni mazingira ya Kikristo yenye hali chanya ya kiroho. Huduma ya watoto ni lazima ianze na kitu hiki cha kwanza. Kama huduma itakuwa tayari imepoteza mwelekeo huo, kwa vyovyote itabidi ianze upya, vinginevyo haitatimiza lengo sahihi.
Kanuni ya Maisha ya Kuwasiliana
Maarifa ya Mungu huja katika mahusiano.
Wakati Mungu aliposema na Yakobo, alijitambulisha mwenyewe. Hakusema, “Mimi ni Mungu wa ulimwengu,” au “Mimi ni Mungu niliyeumba ulimwengu;” ingawaje kauli yeyote katika hizo mbili ingeweza ikawa kweli. Mungu alisema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka” (Mwanzo 28:13). Mungu hujidhihirisha mwenyewe kupitia watu.
Ibrahimu alikuwa mtu wa imani na wengine walimwamini Mungu kwa sababu yake yeye. Mtumishi wake Eliezeri aliomba kwa “Mungu wa bwana wangu Ibrahimu” (Mwanzo 24:12).
Kuna watu wanaotokea kumfahamu Mungu zaidi kwa sababu ni Bwana wao.
Wakati mwingine tunadhania kwamba huduma ya ufuasi ni kuwaambia tu watu klie wanachotakiwa kukijua na kile wanachotakiwa kukifanya. Sivyo ilivyo. Jambo la kwanza, unapaswa uwaoneshe maisha ambayo wanataka kuyafuata. Kama wanataka kuishi kama wewe unavyofanya, basi, watasikiliza maelekezo yako kuhusu jinsi watakavyofanya.
Ufuasi ni maisha ya kuwasiliana. Ni mtindo wa maisha, ulio na makusudio yake, na sababu za kutenda na maadili ya msingi ambavyo huhamishwa kutoka kwa mwangalizi hadi kwa mwanafunzi.
Kanuni ya uhamisho wa maisha inatamka kwamba ufuasi unatokea wakati mwalimu anapopandikiza mtindo wake wa maisha, makusudio yake na maadili ya msingi kwa mwanafunzi.
Rabi wa Kiyahudi wa karne ya kwanza walielewa ufuasi kama ni uhamisho wa maisha. Wakati kijana alipokuwa anataka kuwa mwanafunzi wa rabi, alikuwa anapaswa kumwomba rabi amkubali. Kama akikubaliwa, ataanza kujishirikisha katika maisha ya rabi. Atakuwa naye kwa muda mwingi, siyo tu kwa ajili ya kujifunza imani kwake, bali kujifunza njia yake ya maisha.
Yesu alijitofautisha na mila ya wakati ule kwa kuchagua watu ambao walikuwa hawajaomba kuwa watakuwa wanafunzi wake. Lakini, alifuata mila ya kufanya ufuasi kwa kushirikishana maisha pamoja kwa lengo la kuhamisha mtindo wa maisha.
Baada ya kifo cha Yesu na kufufuka, baadhi ya wanafunzi wake walikamatwa na kupelekwa kwenye baraza lile lile ambalo yeye alihukumiwa. Baraza la Sanhedrini lilifikiri kuwa labda matatizo yao yatakuwa yamekwisha kwa kuwa Yesu alishauawa. Walidhania kuwa kwa kutumia vitisho vidogo tu vilikuwa vinatosha kuwanyamazisha kabisa wafuasi wa Yesu. Kwa kuwapima wanafunzi wa Yesu, waliwaona kwamba hawakuwa watu wenye elimu ya juu, hakika walikuwa hawajaelimishwa kuliko mjumbe yeyote wa baraza la Sanhedrini. Lakini, Maandiko yanasema kwamba baraza la Sanhedrini wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu (Matendo 4:13). Yesu alishaweka mhuri kwenye maisha yao.
Je, walisema nini juu ya Yesu aliyekuwa ndani ya wale wanafunzi? Je, ilikuwa ni tabia zake au mtindo wake wa kuongea? Inawezekana; lakini kulikuwa na zaidi ya hayo. Waliona ujasiri uliotokana na ufahamu wa wito wa kimungu. Waliona kujitolea kusikoyumba kwa uhakika kwenye ukweli kwa gharama yeyote ile. Waliona heshima kwa ajili ya mamlaka lakini walikataa kukubaliana kuwa na maelewano na unafiki. Kwa hakika mioyo ya wale wanasiasa wakorofi na viongozi wanafiki wa kidini ilipigwa na mshangao kwa kutambua kuwa matatizo yao bado yalikuwa hayajaisha na hapo ulikuwa ni mwanzo tu. Yesu alikuwa amewaongeza kwa idadi na aliendeleza ushawishi wake kupitia uanafunzi.
Dr. Paul Brand alikuwa anawatazama wanafunzi wake vijana wa udaktari walipokuwa wanafanya mazoezi ya kuwapima na kuwachunguza wagonjwa katika hospitali moja nchini India. Wakati alipokuwa anamtazama mmojawapo wa hawa wanafunzi akimhudumia mgonjwa kwa unyeunyekevu, alishangazwa na hisia iliyokuwa inaonekana kwenye uso wa kijana huyu aliyekuwa kwenye mazoezi. Ile hisia ilifanana sawasawa na hii iliyokuwa inaonekana kwa Dr. Pilcher, daktari wa upasuaji aliyekuwa mwalimu wa Dr. Brand huko Uingereza. Dr. Brand aliwaelezea wanafunzi wa mazoezi kwamba alibadilika kwa mshangao huo kwa sababu alijua kwamba Dr. Pilcher hajawahi kuwa India, na hakuweza kujua ni kwa vipi mwanafunzi huyo wa mazoezi aliweza kumuigiza yeye. Mwishowe, mmoja wa wanafunzi wa mazoezi akasema, “Hatumjui mtu yeyote kama Dr. Ficher, lakini Dr. Brand, hiyo ilikuwa ni uhusika wa sura yako aliyokuwa ameivaa.”[1]
Ni kile unachofundisha wakati hukusudii kukifundisha ndicho kitakuwa na matokeo makubwa. Huwa unafudisha sana wakati hukusudii kufundisha chochote. Kama mtu mmoja alivyosema, “Unafundisha kidogo kwa kile unachosema, unafundisha zaidi kwa kile unachofanya, na unafundisha sana kwa jinsi ulivyo.”
Kuwa na tahadhari sana kwa nguvu ya mfano wako ulivyo. Siku zote unafundisha. Zidi sana unafanya huduma ya uafusi kupitia mtindo wako wa maisha.
Unamwonesha mtu jinsi ya kuwajibika kwenye matatizo yake kwa njia ile ile ambayo wewe unawajibikia matatizo yako mwenyewe.
Upendo, heshima na uvumilivu ni mambo muhimu kwa ajili ya kumsaidia mtoto. Watu wengine wana uwezo zaidi wa kuwa na upendo, heshima, na uvumilivu kwa watoto kuliko watu wengine.
Unaonesha kwamba unamthamini mtu kama utampa ustahimilivu na umakini wote. Usiwe na papara au haraka wakati unapozungumza naye. Tafakari mnyumbuliko wa mwili wako unaelezea nini kama unataka kumwacha, unataka kwenda kwenye jukumu lako jingine, unafanya shughuli nyingine wakati yeye anaongea au umeelekeza umakini wako kwa mtu mwingine wakati uko naye.
Fanyia mazoezi tabia nzuri za kusikiliza. Ishara nzuri za kusikiliza ni mawasiiano ya macho, umakini unaoonekana dhahiri, kupuuzia mambo yanayotaka kuvuruga, na kuonesha mwitiko mzuri katika furaha ya anayezungumza au hisia zingine.
Kama kwa uhakika utakuwa ni lazima uharakishe na huwezi kutulia ili umsikilize, unaweza ukajieleza. Hilo halitawaudhi ikiwa kwa kawaida huwapa uangalifu wanaohitaji. Kama kwa ujumla unaona una majukumu mengi yatakayoweza kukukosesha nafasi kwa ajili yao, ukifikiria kwamba unahitaji kufanya jambo, unapaswa uache na ufikirie kazi yako ya uhakika ni ipi.
► Je, ni watoto gani walio sehemu ya maisha yako? Kuna njia gani unazoweza kuwaonesha kwamba wao ni muhimu? Je, unazo tabia ambazo unapaswa uzibadilishe?
Kupatikana kwetu kwa ajili ya Mungu ni muhimu zaidi kuliko uwezo wetu kimwili na kiakili. Mungu anataka kupatikana kwetu kuliko uwezo wetu kimwili na kiakili. Mungu atatoa uwezo wa kimwili na kiakili unaouhitajika kwa ajili ya kutimiza wito wake.
[2]Vijana wadogo wana tabia ya kutotulia katika mambo mengi. Kutoka siku moja kwenda siku inayofuata wanaweza wakabadilika kuonekana katika kiroho kwenda katika kuonekana waasi, Kutoka kwenye ukarimu kwenda kwenye uchoyo, au kutoka kukomaa kwenda kwenye utoto. Hiyo siyo kwa sababu ni wanafiki. Bado wako kwenye kuendelea kukua, na utu wao bado haujawa thabiti.
Vijana wadogo bado hawajatulia, lakini wanakutaka wewe uwe thabiti katika matarajio yako. Kama katika nyakati zao mbaya unawaambia ninyi hamtafaa kwa jambo lolote, unashusha matarajio yao. Bado hawajijui wanaenda kuwa nani, na tathmini yako itaathiri kile wanachoenda kuwa.
Zungumzia zaidi kuhusu mpango maalumu wa Mungu uliopo kwa ajili yao. Waambie kwamba Mungu amewapa kila mmoja wao uwezo maalumu wa kimwili na kiakili. Elezea kuhusu kuridhika kwa kutafuta mapenzi ya Mungu.
Kijana mdogo mwenye karama ya uongozi anaweza kuwa na mawazo mengi lakini asifanye vizuri katika kukataa yaliyo mabaya. Kipengele cha kukua ni uwezo wa kimwili na kiakili wa kutofautisha kati ya mawazo mzuri na yale mabaya. Msadie ajifunze kuhusu hekima, lakini usimkatishe tamaa katika kuwa na mawazo ya ina mbalimbali.
Juu ya mambo yote, kumbuka kwamba Mungu anao mpango wa mwisho kwa kila mtu, na anafanya kazi katika kuuleta juu utumike. Omba kwa ajili ya ufahamu ili uweze kufanya kazi pamoja na mpango wa Mungu wa maendeleo kwa ajili ya mwanafunzi. Omba kwa ajili ya miujiza ya neema na uangalizi wa kimungu katika maisha ya mwanafunzi ambayo yatampeleka kwenye mwelekeo sahihi.
[1]Paul Brand na Philip Yancey, In His Image (Grand Rapids: Zondervan, 1984), 18-19
“Wakati mtu mzima anapokuwa hamwonei tena huruma kijana mdogo,
manufaa yake katika ulimwengu huu ni kama yamemalizika.”
- George MacDonald
Kuboresha Mbinu za Kufundisha.
► Je, kuna tabia gani katika mbinu nzuri ya kufundisha? Je, unapomwona mtu akifundisha, unajuaje kama ni mwalimu mzuri?
Mwalimu ndiye mwenye kuthibiti mbinu ya kufundishia. Kuna vipengele kadhaa vya mbinu za kufundishia ambavyo mwalimu anapaswa avipange kwa makini.
(1) Kiwango cha Maelekezo
Watu ni kama majagi yenye shingo nyembamba. Kama utamimina kitu ndani kwa haraka sana, hakitaweza kwenda ndani chote. Kama utafundisha taarifa kwa haraka sana, hawataweza kujifunza. Mtu anapojifunza taarifa mpya, ni lazima aiunganishe na kile anachokijua. Ni lazima pia afikiri kwamba ni kwa jinsi gani taarifa hiyo itafanya kazi kwenye maisha yake. Kwa hiyo, kuna ukomo wa kasi ya mtu kujifunza kutokana na taarifa hizo.
Ni vyema kuweka jambo moja katika hali ambayo haitasahaulika kuliko kutaka kumaliza mambo mengi ambayo kwa vyovyote vile watasahau. Ni vyema wakajifunza jinsi ya kutumia kipengele kimoja kwa usahihi kuliko kusikia vipengele vingi vya taarifa ambavyo hawaoni umuhimu wake.
(2) Majadiliano ya Kikundi
Watu wengi wanahitaji kuwa na majadiliano na watu wengine wakati wanajifunza. Wanahitaji waweze kuuliza maswali na kurudia dhana katika maneno yao wenyewe. Kama mtindo wa mwalimu wa kufundishia hautaruhusu mjadala kutoka kwa wasikilizaji, hawataweza kujifunza mambo mengi
Unaweza ukatanguliza wazo la somo kwa njia ya swali, mfano “Kwa nini ni muhimu ku…?” au “Ni kitu gani muhimu sana unachojua kuhusu…?” Usipoteze muda mrefu kwenye majadiliano ya utangulizi, lakini tumia muda huo kuwafanya wawe na shauku ya kusikiliza.
Baada ya kuwasilisha baadhi ya taarifa, unaweza ukauliza swali ambalo litawafanya waweze kufafanua dhana kwa maneno yao wenyewe. Kwa mfano, “Kuna makosa gani aliyofanya mtu aliyeko kwenye taarifa…?” Uliza maswali ambayo yatakapojibiwa yataambatana na maelezo ya ufafanuzi, badala ya maswali ambayo yanajibiwa kwa ndiyo au hapana. Maswali yanabidi yawe marahisi katika kiwango cha kuwawezesha watoto wengi kupata majibu mazuri kutoka kwa watoto wenzao. Kwa kawaida kama majibu yao yataonekana yana makosa watapoteza hamu na au shauku yao.
Usimpe mtoto shinikizo la kushirikisha jambo fulani la binafsi. Badala yake, jaribu kutengeneza mazingira ambayo atajisikia yuko huru kuwasilisha yeye mwenyewe.
Usiruhusu wanafunzi wachache tu kuwa ndio wa kusema katika kila kitu. Unaweza ukaelekeza mambo mengine kwa wale ambao wanaonekana siyo wasemaji katika kikundi: “Je, unafikiri nini, Charles?” Unapaswa uwatie moyo na wengine kuwa washiriki: “Je, wengine mnafikirije?”
Usiruhusu watu katika darasa kuwa na mijadala yao wenyewe huku wakisahau kuwa wao ni sehemu ya kikundi.
Usiruhusu mtu yeyote kuingilia kati hata kama ni mtoto mdogo anaongea.
Jaribu kuthibitisha kila wazo linalotolewa kwa namna fulani kabla ya kukosoa hilo wazo. Kama linahitaji masahihisho, jaribu kufanya hivyo kwa kulipanua zaidi.
(3) Umuhimu
Wakati wote jiulize wewe mwenyewe swali hili. ”Je, kwa nini jambo hili ni muhimu?’ Kama wewe mwenyewe hujui, hata wao pia hawatajua. Je, kuna tofauti gani itakayofanyika ndani yao? Je, kuna mambo yoyote maalumu wanayopaswa kuyafanyia kazi kwenye maisha yao? Kama huwezi kufikiria lolote kati ya hayo, hata wao inawezekana wasiweze kufikiria jambo lolote.
Kama wataona kwamba mada hiyo ni muhimu kwao, watasikiliza kwa umakini mkubwa. Ili kuweza kulithibiti darasa, shughulika zaidi na kuifanya mada yako iwe ya kuvutia kuliko kushughulika zaidi na kudumisha nidhamu.
(4) Umuhimu
Onesha matokeo ya ukweli unaoufundisha. Je, kunakuwepo na matokeo gani wakati watu wanapoujua ukweli na kuufuata? Je, kunakuwepo na athari gani wakati watu wanapoukataa huu ukweli?
Watie moyo kwa mada zenye mvuto. Epuka kutumia muda mwingi kwenye mambo madogo madogo. Wasimulie hadithi nyingi kuhusu watu wengine ambao wamewahi kuishi sawa na ukweli unaoushirikisha. Hawataweza kuwa na kumbukumbu ya mihutasari yako ya masomo, lakini wataweza kukumbuka hadithi zako.
Waeleze kuhusu mashujaa. Wanataka wawaone watu ambao watawakubali na kuwaiga. Waelezee kuhusu mashahidi wa imani—siyo wale walioona miujiza mikubwa tu, lakini wale waliokamilisha kufanya matendo makubwa kwa kutumia nguvu za Mungu. Wasaidie waone kwamba jukumu la kanisa la kueneza injili na kufanya uanafunzi ni changamoto kubwa na kazi inayohitaji zaidi kukamilishwa duniani.
(5) Vielelezo vya Kufundishia
Kama kutakuwepo na uwezekano, tumia picha za rangi wakati unapokuwa unaelezea hadithi. Unapokuwa unafundisha dhana, andika maneno muhimu kwenye ubao. Watayakumbuka kwa wepesi zaidi kama wataona na kusikia.
(6) Vitendo
Watu hujifunza kwa kufanya kwa vitendo. Watoto wanaweza kujifunza kwa kutengeneza kitu fulani, au kwa kuigiza kutoka katika hadithi. Mwalimu hata anaweza kuwaelekeza kuigiza kutoka ndani ya Biblia kadri anavyokuwa anaielezea. Hatua hii inachukua muda, kwa hiyo huwezi kuwa na onyesho kwa ajili ya hadithi kila siku, lakini itakupasa uangalie njia ya kuweza kuwa na onyesho mara kwa mara.
► Baadhi ya watu katika kikundi wanaweza kuzungumzia kuhusu masomo au mahubiri ya hivi karibuni waliyowasilisha na wakaelezea jinsi ambavyo wangeweza wakavitumia vipengele hivi vinavyohusiana na mbinu vizuri zaidi. Baadhi wanaweza wakaelezea mambo ambayo tayari wanayafanya katika kutumia vipengele hivi.
Mtindo wa Injili kwa Watoto: Kitabu kisichokuwa na Maneno.
Kila ukurasa wa Kitabu kisichokuwa na Maneno una rangi tofauti na unawakilisha sehemu fulani ya injili.
Ufuatao hapa chini ni muhtasari wa ujumbe unaokwenda na kila ukurasa. Wakati unapotumia Kitabu kisichokuwa na Maneno itakupasa uongezee ufafanuzi zaidi na umwache mtoto aingilie na kuuliza maswali.[1]
Kumbuka: Watu wengine huweka rangi ya dhahabu kwenye ukurasa wa kwanza, kisha kufuatiwa na nyeusi, na kuendelea na rangi nyingine kufuatana na utaratibu ulioonyeshwa hapa chini.
Dhahabu: Rangi ya Dhahabu huwakilisha mbingu, mahali ambapo Mungu anatuandalia sisi makao yetu. Maisha yetu hapa duniani yatakapokuwa yamemalizika, tutaishi na Mungu mbinuni mahali ambapo hakuna huzuni, maumivu au uovu.
Nyeusi: Rangi Nyeusi inatukumbusha kuhusu dhambi, na mambo mengi mabaya ambayo tumeyafanya. Biblia inasema kwamba kila mtu ametenda dhambi. Kwa ajili ya dhambi, tumekuwa kwenye matatizo na Mungu (Katika pointi hii, utapaswa umwambie mtoto akiri kwamba yeye ni mwenye dhambi.)
Nyekundu: Habari njema ni kwamba Yesu, Mwana wa Mungu, alikufa kwa ajili yetu ili tuweze kupata msamaha wa dhambi zetu. Rangi Nyekundu inawakilisha damu ya Yesu. Yesu alikufa, lakini alifufuka kutoka katika wafu na kwa sasa anaandaa makao huko mbinguni kwa ajili yetu.
Nyeupe: Wakati Mungu anapokuwa ametusamehe dhambi zetu anatufanya tuwe wasafi kwenye mioyo yetu. Huzichukua dhambi zetu zote tulizozitenda. Unaweza kusali na kumwomba Mungu akusamehe dhambi zako. Mungu yuko tayari kukusamehe ikiwa utajuta dhambi zako.
Kijani: Wakati unapokuwa umeshasamehewa dhambi zako, wewe ni mtoto wa Mungu. Utakuwa unakua kwenye uhusiano wako na Mungu. Rangi ya Kijani inaamaanisha kukua. Utajifunza zaidi kuhusiana na Mungu na utajifunza jinsi anavyokutaka uishi. Unapaswa usome Biblia yako, uombe kila siku, na usikilize kutoka kwa watu wengine ambao wanajua jinsi ya kuishi na Mungu kwa ukaribu zaidi.
(1) Angalia tena nyenzo zote zilizoko kwenye somo hili chini ya kichwa cha habari “Kanuni ya Uhamisho wa Maisha.” Tafakari muingiliano wako na watoto, siyo tu kwenye mafundisho, bali wakati wowote unapokutana nao. Je, unahitaji nini ili ubadilike? Fanya mazungumzo na mtu anayekujua vizuri. Mwoneshe (kama ni baba au mama) nyenzo za masomo ulizo nazo na mfafanulie tathmini inayohusiana na wewe mwenyewe. Omba wakupe maoni yao. Utahitajika utoe taarifa kwamba uliifanya kazi hii, lakini unaweza kuchagua aidha kutoa au kutokutoa undani wa tathmini yako.
(2) Andaa somo au mahubiri kwa ajili ya watoto. Yaandae kwa uangalifu mkubwa ukitumia vipengele vya mitindo. Uwe tayari kutoa ufafanuzi ni kwa jinsi gani uliyaandaa.
(3) Tafuta njia yeyote ya kununua au kutengeneza Kitabu kisichokuwa na Maneno. Jifunze ushirikishaji na ushirikishe kwa angalao watu wasiopungua watatu. Andika sura moja inayoelezea uzoefu wako kwa kila mmoja.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.