Paulo alipanga kufanya safari ya kwenda Rumi. Alikuwa anahitaji kwenda kuhubiri injili katika eneo hilo, (Warumi 1:15). kuwaimarisha waamini, (Warumi 1:11-12). na ili kupata msaada wa kanisa la Rumi kwa ajili ya safari yake ya umisheni ya kwenda Hispania (Warumi 15:24).
Kusudi la barua kwa Warumi ilikuwa ni kumtambulisha Paulo na theolojia yake ya wokovu kwa waamini wa Kirumi. Barua inaonesha misingi ya kazi ya umishenari duniani kote kwa kuelezea thelojia ya wokovu.
Paulo alipanga kulitumia kanisa la pale Rumi kama kituo chake cha kuzindulia juhudi za umishenari katika nchi ya Hispania, amabyo ilikuwa ni koloni la zamani la Kirumi katika eneo la magharibi na kitovu cha ustaarabu wa Kirumi katika eneo hilo la Dunia wakati huo.
Ziara ya Paulo Rumi haikutokea kama alivyokuwa amepanga. Alikamatwa akiwa Yerusalemu. Ilipoonekana kwamba hatapata haki, alikata rufaa kwa Kaisari. Baada ya safari ndefu ya hatari, iliyokuwa ni pamoja na kuvunjika kwa meli yake alifika Rumi kama mfungwa mwaka wa 60 B.K. Ingawaje alikuwa amefungwa, alikuwa huru kupokea wageni, na alikuwa na huduma yake ambayo ilifika katika jiji lote (Matendo 28:30-31). Paulo alisema kwamba mfuatano wa matukio hayo ulitokea kwa ajili ya “kupeleka injili mbele” (Wafilipi 1:12). Kulikuwa na watu wapya ambao walishabadilika hata katika nyumba ya Kaisari. Aliachiliwa baada ya miaka miwili. Haijulikani kama alifanikisha kuendelea na safari yake ya kwenda Hispania au la.
Kuna maswali kadhaa ambayo katika hali ya kawaida yatainuka kuhusiana na ombi la Paulo kwamba asaidiwe kuzindua safari yake ya umishenari. Mtu anaweza akauliza, “Kwa nini uwe wewe ndiye unayetaka uende?” Kwa hiyo, Paulo alianza barua yake kwa kutaja kujitoa kwake kwa ajili ya kazi ya umisheni (Warumi 1:1). Baadaye alielezea wito wake maalumu kama mtume kwa Mataifa (Warumi 15:15-20).
Swali lingine ambalo linaweza kuulizwa ni, “Je, kwa nini kila mtu anataka aisikie injili? Inawezekana ujumbe huu hautakiwi kila mahali.” Paulo alifafanua uzito wa injili kwa mwanadamu katika ulimwengu wote (Warumi 1:14, 16; Warumi 10:12). na uharaka uliopo wa kazi ya umishenari (Warumi 10:14-15). Alionesha kwamba ujumbe unahusika kwa kila mtu ulimwenguni na kwamba kila mtu ana hitaji kubwa la kuusikia.
Kitabu cha Warumi kuanzia Wakati Ule hadi Sasa
Waraka huu bado unatimiza kusudi lake la awali la kutoa msingi wa kazi ya umishenari. Hata hivyo, unafanya kazi ya ziada. Kama Paulo alivyoelezea ni kwa nini kila mtu anahitaji kusikia ujumbe, alieleza kwamba ujumbe ni nini na ni kwa nini watu wanaweza tu wakaokolewa kwa njia hii. Alijibu baadhi ya upinzani wa kawaida. Maelezo haya na utetezi wa ujumbe aliohubiri unachukua sehemu kubwa ya kitabu na unatoa muundo wake.
[1]Tunachokipata katika kitabu cha Warumi ni maelezo ya theolojia ya wokovu. Theolojia ya wokovu ya Paulo inayotetewa kwenye waraka ilitoa ulinzi wa mara moja dhidi ya Wayahudi; na unatumika pia katika kusahihisha makosa ya wakati wa sasa katika elimu ya wokovu (imani za wokovu).
William Tyndale, kwenye utangulizi wa kitabu cha Warumi, alisema, “Wazo kuu la Paulo katika waraka huu lilikuwa ni kutambua na kutoa kwa ufupi mafunzo yote ya injili ya Kristo na kuandaa utangulizi kutokana na yale yote yaliyohusika na Agano la Kale.”[2]
Kupitia katika historia, Mungu ameutumia waraka wa Warumi kurejesha kwa upya kweli nyingi zilizokuwa muhimu wakati zilipokuwa zimesahaulika.
Katika mwaka wa 386, Agustino alijiondoa kwenye maisha yake ya dhambi baada ya kuwa amesoma Warumi 13:13-14.
Katika mwaka wa 1515, Martin Luther alitambua maana iliyokuweko katika Warumi 1:17. Aliona kwamba mtu atakayeachwa kwenye hukumu ya Mungu ni Yule aliye na imani iokoayo. Jambo hili lilimpa msingi wa uhakika wa wokovu ambalo kwa muda mrefu alikuwa amelihitaji. Ilikuja kuwa ndio msingi wa ujumbe wake kwamba imani peke yake ndio njia inayoweza kutufanya tuokoke.
Katika mwaka wa 1738, John Wesley alipata uhakika wa wokovu alipokuwa kwenye kikao na vijana wadogo waliokuwa wanakutana mara kwa mara kujadili jinsi ya kufuata Ukristo wa kimaandiko. Wakati mtu mmoja alipokuwa akisoma Utangulizi wa Luther kwa kitabu cha Warumi, Wesley alijisikia moyoni mwake “moto wa ajabu ukiwaka.” “Nilijihisi kuwa mtiifu kwa Kristo, Kristo peke yake, kwa ajili ya wokovu wangu: na uhakika ulitolewa kwangu kwamba amezifuta dhambi zangu, hata mimi, na akaniokoa kutoka katika sheria ya dhambi na mauti.”[3]
Kwa hawa watu wote watatu, kuelewa ujumbe wa kitabu cha Warumi kulikuwa ni motisha kamili ya kufanya uinjilisti kwa ari kubwa. Kitabu hiki bado kinakamilisha kusudi lake la kutoa msingi kwa ajili ya umisheni kwa kuelezea theolojia ya wokovu.
Kitabu chote cha Warumi ni ufafanuzi wa maelezo yote yaliyoko katika Warumi 1:16-18.
Kila kitu kwenye aya 1-14 ni mwendelezo hadi aya ya 15 ambapo Paulo anasema, “Niko tayari kuhubiri injili,” Aya za 16-18 zinaelezea kwa muhtasari injili ni nini na ni kwa nini kila mtu anaihitaji. Injili ni ujumbe ambao wenye dhambi wanaweza kuhesabiwa haki kwa imani. Sababu iliyopo ya kila mtu kuhitaji ujumbe huu ni kwamba wako chini ya laana ya Mungu.
Njia nyingine ya kuelezea kusudi la msingi la kitabu cha Warumi ni kwamba ni ufafanuzi wa injili, iliyo katika msingi wa tamko la Mungu kwamba kila aaminiye ataokoka, na kila asiyeamini atahukumiwa.
Kilele cha kitabu kiko kwenye Warumi 10:13-15, ambapo Paulo anaelezea kwa nini ni jambo la haraka kwa wajumbe kupeleka injili. Watu wanaokoka kwa kuamini, lakini hawawezi kuamini pasipo kuisikia injili.
[1]“Kusudio la ujumla la waraka huu ni kuudhihirisha umilele, kusudi lisilobadilika au tamko la Mungu, ambalo ni, ’Kila aaminiye ataokoka: na kila asiyeamini atahukumiwa.”
- John Wesley
[2]William Tyndale, "Prologue to Romans," English New Testament, 1534.
[3]John Wesley, The Works of John Wesley, (Kansas City: Nazarene Publishing House, n.d.), 103
Uwasilishaji wa Injili kutoka katika Kitabu cha warumi
Injili inaweza kufafanuliwa kwa kutumia aya peke yake kutoka katika kitabu cha Warumi. Uwasilishaji huu wa injili mara nyingine unaitwa “Barabara ya Kirumi.”
Sentensi ya kwanza ya ufafanuzi kwa kila kinachorejewa ni jambo muhimu sana la kukumbuka.
Warumi 3:23
“Wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”
Kila mtu amefanya dhambi kwa kufanya mambo anayojua kwamba ni uovu. Aya hii inaonyesha tatizo halisi watu walilo nalo. Hawajamtii Mungu; kwa makusudi wamekataa kumtii Mungu. Hakuna hata mtu mmoja ambaye anaweza kuepukana na hili. Hakuna mtu ambaye anaweza kukubaliwa na Mungu kwa msingi kwamba mara zote anatenda yaliyo mema.
Kwa msisitizo zaidi katika suala hili, unaweza ukatumia Warumi 3:10 (“Hakuna mwenye haki hata mmoja.”) na Warumi 5:12 (“mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi”).
Warumi 6:23
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Wenye dhambi wamevuna kifo cha milele, lakini Mungu anatoa maisha ya milele kama zawadi kupitia kwa Yesu.
Aya hii inaonyesha ni kwa jinsi gani dhambi ilivyo na madhara makubwa. Kwa sababu ya dhambi, adhabu ya kifo imepitishwa kwa kila mtu. Ni kifo cha milele, adhabu ya Mungu ambayo kila mwenye dhambi anastahili.
Kwa ulinganifu wa kifo ambacho tulikivuna, Mungu anatoa zawadi ya maisha, kitu ambacho hatujawahi kukivuna.
Warumi 5:8
“Bali Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu.”
Zawadi ya Mungu ilitolewa kwa kifo cha Kristo kwa sababu yetu.
Mungu alikuwa hayuko tayari kutuachia sisi tuchukue hukumu tuliyostahili. Kwa kuwa anatupenda, aliandaa njia kwa ajili yetu ya kupokea rehema. Yesu alikufa kama dhabihu ili kwamba tuweze kupokea msamaha. Mungu hakutungojea sisi tufanye jambo lolote linalostahili wokovu – lilikuja tu kwetu “tukiwa wangali bado wenye dhambi.” Wokovu hautolewi kwa watu wema, bali kwa wenye dambi.
Warumi 10:9
“Kwa sababu, ukimkiri Yesu… na kuamini… utaokoka.”
Hitaji peke yake kwa ajili ya wokovu ni kwa mwenye dhambi kukiri kwamba yeye ni mwenye dhambi na aamini ahadi ya Mungu ya msamaha kwa sababu ya kifo na kufufuka kwa Yesu.
Vipi kuhusu toba? Kama mtu atakiri kwamba amefanya makosa na anahitaji asamehewe, inaonyesha kwamba huyu mtu yuko tayari kuachana na dhambi kwa hiari yake mwenyewe.
Warumi 10:13
“Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.”
Sadaka ya wokovu ni kwa ajili ya kila mtu.
Hakuna mtu hata mmoja aliyetengwaa katika hili. Hakuna sifa nyingine zozote zinazohitajika.
Warumi 5:1
“Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu.”
Kuamini ahadi ya Mungu kunatufanya sisi tuwe rafiki wa Mungu, hatuhesabiwi wenye hatia tena.
Kuwa na amani na Mungu inamaanisha kwamba sisi siyo maadui wa Mungu tena; tumepatanishwa. Dhambi ambayo ilitutenganisha na Mungu inaondolewa kwenye njia zetu. Kuhesabiwa haki inamaanisha kwamba tunahesabika hatuna hatia tena. Kuhesabiwa wenye haki kwa imani ina maana kwamba kuamini ahadi ya Mungu ndiyo kitu peke yake muhimu kinachohitajika kwa ajili ya msamaha wetu.
Warumi 8:1
“Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”
Kwa kuwa tumeunganishwa kwa Kristo, hatuna hukumu tena kwa dhambi tulizotenda.
Yesu aliishi maisha yasiyokuwa na dhambi na akakamilisha mahitaji yote ya haki kwa kifo chake juu ya msalaba. Kwa imani, tunajinasibisha naye, na tumekubaliwa na Mungu aliye Baba yetu. Mungu anawajibika na sisi kana kwamba hatujawahi kutenda dhambi tena.
Hitimisho
Elezea kwamba mwenye dhambi anaweza akaokoka kwa kumwomba Mungu, akikiri kwamba yeye ni mwenye dhambi na akiomba msamaha kwenye msingi wa dhabihu ya kifo cha Yesu na kufufuka kwake.
Kwa ajili ya Kujifunza na kufanya Mazoezi
Njia nzuri ya kujifunza na kufanyia mazoezi mbinu hii kwanza ni kuweka alama kwenye kila aya itakayotumika katika kitabu cha Warumi kwa kuzungushia alama ya mviringo au kwa kupiga msatari. Kisha weka namba pembeni mwa kila kimoja kuonesha mtiririko wa matumizi yake. Kwa mfano: nyuma ya aya itakayonza kutumika kwanza, andika namba 1.
Fanya zoezi la kuwasilisha injili. Soma kila aya na toa maelezo yanayoendana na aya hiyo. Uwe na uhakika wa kuingiza maudhui yaliyoko kwenye sentensi ya kwanza baada ya kila aya. Ongeza hitaji lolote la maelezo yanayohitajika, kwa kutumia sentensi zinazofuata kama inaonekana zitakuwa na msaada. Siyo lazima kutumia maneno yale yale ambayo yametolewa kwenye somo hili.
Fanya mazoezi hadi utakapoona unaweza kufanya vyema bila ya kuangalia mahali pengine popote isipokuwa Biblia tu.
Kumbukumbu kwa kiongozi wa darasa: Wanafunzi wawili au watatu watapaswa kuonesha matumizi ya Barabara ya Kirumi kwenye kikundi. Kikundi kitajadili njia ambazo wanaweza kuboresha katika uwasilishaji. Kisha, wanafunzi itabidi wagawanyike kwenye kikundi cha watu wawili wawil kwa ajili ya kufanya mazoezi. Kila mwanafunzi atapaswa kufanya uwasilishaji mara mbili, kwa wasikilizaji tofauti.
Kazi za Kufanya
(1) Kwa kutumia Barabara ya Kirumi, wasilisha injili kwa angalau watu watatu. Andika aya moja kuhusiana na kila wasilisho ulilofanya na jiandae kutolea maelezo wakati utakapokuja kwenye kipindi kingine cha darasa kinachofuata.
(2) Jipange kuandika kutoka kwenye kumbukumbu zako (kwa kutumia Biblia yako tu) marejeo ya Maandiko ya Barabara ya Kirumi na angalao sentensi moja yenye maelezo ya kila kimoja mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.
(3) Somo linalofuata ni kuhusu mahubiri ya Kiuinjilisti. Kwa ajili ya maandalizi ya somo hili, andika muhtasari wa mahubiri ya kiuinjilisti ambayo ulishawahi kuyahubiri, moja ambalo umeshahi kulisikia, au moja ambalo utapenda kulitengeneza mwenyewe. Njoo pamoja nalo kwenye kipindi kingine cha darasa kinachofuata.
Andika kumbukumbu ya Maandiko yanayotumika katika uwasilishaji wa injili ya Barabara ya Kirumi. Chini ya kumbukumbu hizo, andika angalau sentensi moja yenye ufafanuzi. Usiziandike hizo aya.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.