Somo linalohusu zaka ni lenye kuelekea kuleta mabishano kwenye maeneo mengine. Watu wengine wanafikiri kwamba wazo la utoaji wa zaka halikubaliani au halipatani na wokovu kwa njia ya imani. Wanasema inaelekea kana kwamba ni malipo kwa ajili ya wokovu. Watu wengine hawataki kujisikia wana jukumu la kutoa msaada kwa kanisa. Wanatoa tu kile wanachojisikia kutoa ili mradi ametoa. Katika somo hili tutaangalia kwenye misingi ya Biblia na makusudi ya vitendo ya zaka.
► Je, ni mambo gani umesikia kutoka kwa watu wakisema sababu zilizo kinyume na utoaji wa zaka?
Mkristo anaelewa kwamba Mungu ndiye Mmiliki wa kila kitu katika ulimwengu huu. Mungu anatumiliki kama Muumbaji wetu. Alitufinyanga sisi, akatupa uwezo wa aina mbalimbali, na akaumba rasilimali zote tunazotumia. Kila kitu kiliumbwa na yeye, anaendelea kuwepo kwa uwezo wake, na yupo kwa ajili ya utukufu wake (Wakolosai 1:16-17).
Mungu pia anatumiliki kwa njia ya ukombozi. Alilipa gharama kwa ajili ya ukombozi wetu. Alitukomboa sisi kutoka katika hukumu tuliyokuwa tumestahili kwa sababu ya dhambi. Tunawiwa maisha yetu kwake kwa sababu Yesu alikufa kwa ajili yetu (2 Wakorintho 5:14-15).
Mungu pia anatumiliki sisi kwa njia ya wokovu. Kama wenye dhambi tulikuwa chini ya nguvu za Shetani na dhambi. Wokovu unatuondoa sisi kutoka kwenye kongwa la uovu (Matendo 26:18).
Kwa kuwa sisi ni mali ya Mungu, pia kila kitu tulicho nacho ni mali ya Mungu.
► Toa mfano ni kwa jinsi gani unasimamia mali na vitu vyote ulivyopewa kwa ajili ya Mungu.
Maelekezo Maalumu ya Mungu.
Wakati mwingine Mungu huonyesha umiliki wake wa kila kitu kwa kutoa maelekezo maalumu kwa ajili ya ile sehemu ya kile tulicho nacho. Tunapokuwa tumetii maelekezo ya Mungu katika sehemu hiyo, tunaonyesha kwamba kwa hiari yetu tuko tayari kumtii yeye katika kila jambo.
Kwa mfano, wakati Mungu alipomweka Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni, aliwakataza wasile tunda kutoka katika mti fulani. Maagizo maalumu yaliyokuwa yametolewa yalihitaji udhihirisho wa utiifu.
Mahitaji maalumu ya Mungu yanatupa sisi nafasi ya kudhihirisha utiifu. Kama mtu hayuko tayari kuwa mtiifu kwa maelekezo maalumu ya Mungu kuhusiana na sehemu fulani za maisha yake, inaonyesha kwamba siyo mtiifu kwa maelekezo ya jumla ya Mungu kwa yale mengine yote yaliyoko.
Mwanamke mmoja alilalamika kwa mchungaji wake kwamba hakuwa ameelewa ni kwa nini Mungu alikuwa hambariki. Mchungaji alimwuliza kama alikuwa anamtii Mungu. Yule mama akasema, “Ndiyo, najitahidi kufanya yale ambayo ni sahihi. Sijui jambo lolote ninalofanya tofauti.” Mchungaji akamkumbusha kwamba alikuwa hahudhurii ibada. Akasema, “Unaweza usijue Mungu anataka ufanye nini katika baadhi ya siku, lakini ukajua ni nini anachotaka ufanye kwenye siku ya Jumapili. Kama hufanyi kile unachojua kwamba ni sahihi katika siku hiyo, inawezekana humtii Mungu kwenye siku nyingine.”
Kuna mifano mingi ya kibiblia ya nyakati ambazo Mungu alitoa maelekezo maalumu kuhusiana na kipengele cha maisha ya mtu. Mungu hutoa zawadi kwa ajili ya kuwa mtiifu na hutoa adhabu kwa kutokuwa mtiifu. Zawadi na adhabu hazikuathiri tu sehemu ya maisha ambayo ilikuwa chini ya mahitaji. Wanayoyachagua na kuamua yalileta madhara kwenye kila sehemu ya maisha yao.
Mifano ya Maelekezo Maalumu
(1) Mti uliokuwa umekatazwa katika Bustani ya Edeni
Mungu alikuwa amewaagiza Adamu na Hawa wasile tunda la mti fulani. Walibarikiwa na kuishi katika uwepo wa Mungu, mpaka pale walipoacha kutii. Wakati walipokiuka katazo la kutokula kutoka katika mti mmoja, Walipoteza uhuru wa kuwepo tena ndani ya Edeni, wakavunja uhusiano wao na Mungu, na wakaleta laana kwa wanadamu wote (Mwanzo 3:17-19).
(2) Siku ya Sabato
Mungu alikuwa ametoa makatazo kadhaa kuhusiana na Siku ya Sabato. Mtu ambaye hakuweza kutii maelekezo ya Mungu kuhusiana na siku hiyo alikuwa pia siyo mtiifu kwa siku nyingine zilizokuwepo. Kukosa utiifu kulileta laana kutoka kwa Mungu kwenye kila sehemu ya maisha (Isaya 58:13).
(3) Yeriko
Yeriko ulikuwa ni mji wa kwanza uliokuwa umeharibiwa na Israeli wakati wa kuingia kwenye Nchi ya Ahadi. Mungu aliwaambia kwamba kila kitu kitakachokuwa kimechukuliwa kutoka katika mji wa Yeriko kitengwe kwa ajili ya Mungu. Miji mingine haikuwa na hitaji hili, lakini Mungu alitoa maagizo maalumu kwa ajili ya Yeriko. Kutokutii kulisababisha kushindwa katika vita, kifo cha watu thelathini na sita na kifo cha familia moja (Yoshua 7:5).
(4) Sauli na Amaleki
Mungu alimwambia mfalme Sauli wa Israeli kulipiga na kuliharibu taifa la Amaleki na kuwauwa watu na wanyama wote waliokuweko. Sauli aliwaacha wengine wakiwa hai. Alijinadi kwamba alikuwa amemtii Mungu, ingawaje hakuwa ameitii amri iliyokuwa maalumu. Mungu alimkataa Sauli kuendelea kuwa mfalme (1 Samweli 15:3, 9, 20-23).
(5) Sabato za Ardhi
Ardhi ilikuwa inatakiwa ipumzishwe katika kila mwaka wa saba. Watu walikataa kumtii Mungu na hawakuzingatia kuitimiza Sabato kwa ajili ya ardhi. Kama mkulima hakuweza kumtii Mungu kwenye mwaka wa saba, inawezekana hakuwa anamtii Mungu kwenye miaka mingine. Wakati watu walipokataa kutii, Mungu aliruhusu waipoteze ardhi yao kabisa. Sabato za ardhi zilitekelezwa kwa miaka sabini ya kukaa utumwani (2 Mambo ya Nyakati 36:21).
(6) Mazao ya Kwanza
Waisraeli walipaswa wampe Mungu mazao ya kwanza ya ardhi. Kama wangetii, Mungu alibariki mavuno ya mashamba yao (Mithali 3:9-10). Baraka hiyo haikuwa tu kwa ajili ya ile sehemu waliyotoa, bali kwa ajili ya mazao yote. Kama hawakuweza kutimiza hili hitaji, ardhi haikubarikiwa. Kama mtu hatatoa sehemu ya kile ambacho Mungu anakitaka, hata kwenye sehemu nyingine pia hamtii Mungu.
(7) Zaka
Mungu anaamuru kila sehemu ya kumi itolewe. Kama mtu hatatoa, anaonyesha kwamba fedha yake hajaikabidhi kwa Mungu. Aidha pia hatumii asilimia tisini zilizoko kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Mungu atabariki vyote alivyo navyo kwa mtu anayetoa zaka (Malaki 3:10). Kama mtu hatatoa kwa ajili ya kuwezesha huduma, vitu vyote alivyo navyo vitakuwa vimelaaniwa (Hagai 1:6).
Mmiliki wa duka aliondoka akasafiri. Kabla ya kuondoka, alimwambia mfanyakazi wake, “Angalia hili duka na uhakikishe unalifanyia usafi na kusafisha sakafu yake.” wakati aliporudi, sakafu ilikuwa haijafanyiwa usafi. Mfanyakazi akasema, “Nililiangalia duka kwa ajili yako.” Mwenye duka akasema, “Kwa kuwa hukufanya lile maalumu nililokuwa nimekuagaiza, ninajua kwamba katika kazi zako zote ulijifurahisha mwenyewe tu badala ya kunifurahisha mimi.”
► Je, ni kwa jinsi gani mtu anaweza kuonyesha kwamba anamtii Mungu?
Makusudi ya Asili ya Utoaji wa Zaka
► Je, zaka ilikuwa inatumika kwa ajili ya nini?
Huduma ya kikuhani ya wakati wa Agano la Kale ilikuwa inawezeshwa kwa njia ya utoaji wa zaka (Hesabu 18:20-21). Walawi ambao walikuwa ni kabila lililokuwa na makuhani, hawakupewa urithi wa ardhi (Kumbukumbu la Torati 18:1-4). Walikuwa wanawezeshwa kifedha kwa ajili ya huduma zao ndani ya hekalu. Mpango wa Mungu kwa ajili ya Walawi ulikuwa ni waweze kujielekeza tu kwenye huduma na siyo kujihusisha na mambo ya biashara.
Zaka lilitumika katika kuwezesha ibada ya hekalu na wale wote ambao walikuwa wanahusika kwa ajili ya ibada hiyo. Zaka lilitumika pia kwa ajili ya sikukuu za jamii zilizohusika na ibada, ambazo maskini walikaribishwa (Kumbukumbu la Torati 12:17-18, Kumbukumbu la Torati 14:22-29). Zaka lilitumika katika kusaidia watu waliokuwa maskini, wajane, yatima na wageni wote waliofika malangoni kwao (Kumbukumbu la Torati 26:12).
► Je, ni tofauti gani unazoziona kwenye matumizi ya zaka kwa wakati wa sasa?
Baada ya kujua kwamba wametoa zaka zao kwa uaminifu, watu wa Israeli walikuwa wanaweza kuomba kwa ajili ya baraka za Mungu. (Kumbukumbu la Torati 26:12-15). Kukataa au kuacha kutoa zaka ni kumwibia Mungu, lakini kutoa zaka kwa ajili ya “Ghala la Yesu” kutaleta baraka zisizoweza kuondosheka (Malaki 3:8-10).
► Je, utawezaje kusema kwa mtu ambaye anajinadi kwamba yeye ni maskini sana na hawezi kutoa zaka?
Umuhimu wa Utoaji wa Zaka kwa Wakati wa Sasa
Baadhi ya watu Wanasema kwamba utoaji wa zaka ulikuwa ni mfumo tu kwa ajili ya wakati wa Agano la Kale.
► Je, kuna sababu zozote za kuamini kwamba mfumo wa utoaji wa zaka haukuwa hitaji la muda mfupi la Agano la Kale?
(1) Ibrahimu
Ibrahimu alitoa zaka kwa Melkizedeki muda sana hata kabla ya Kutolewa kwa sheria ya Musa kwa ajili ya Israeli. Hii inaonyesha kwamba ilikuwa ni kanuni ya ujumla kabla ya Musa. Utoaji wa zaka haukuanza na sheria ya Agano la Kale, bali ilikuwa ni kanuni iliyokuwepo tangu mwanzo (Mwanzo 14:20; Waebrania 7:4).
(2) Yakobo
Yakobo aliahidi kumtolea Mungu zaka (Mwanzo 28:20-22), ingawaje sheria ya Musa ilikuwa bado haijatolewa. Yakobo alijua kwamba tayari ilikuwa ni kanuni iliyokuwepo kwa ajili ya kumtolea Mungu.
(3) Yesu
[1]Yesu aliithibitisha kuhusu utoaji wa zaka na hakusema kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya wakati uliopita tu (Mathayo 23:23).
(4) Paulo
Paulo aliwaambia waumini wa kanisa wawe wanatoa “kwenye kila siku ya kwanza ya juma” kwa kadri ya kufanikiwa kwao (1 Wakorintho 16:2). Kwa hiyo, walikuwa wanatakiwa kutoa kiwango kilichokuwa kinalingana na jinsi walivyokuwa wakipokea au wakipata. Mwongozo wa Agano la Kale wa asilimia kumi (10%) unaonyesha kile ambacho Mungu aliona kwamba kilikuwa ni kiwango sawa cha uwiano kinachotakiwa kitolewe. Hakuna sababu ya kufikiria kwamba mawazo ya Mungu yamebadilika.
(5) Wakati wa sasa.
Mungu bado anao mpango kwa ajili ya wale wanaotumika kwenye huduma kwa muda wao wote waweze kuwezeshwa kifedha na huduma zao. “Wale wanaohubiri injili wanapaswa waishi kutokana na injili.” Mungu hajawahi kupanga wachungaji wafanye kazi na wajiwezeshe wenyewe na wasiwe na muda wa kuwajibika kwa ukamilifu kwenye huduma zao. Katika 1 Wakorintho 9:11-14 tunaambiwa kwamba mtu anayepanda vitu vya rohoni anapaswa kuvuna kifedha kutoka kwa wale anaowahudumia. Katika 2 Wakorintho 12:13 tunaonyeshwa kwamba makanisa kwa kawaida yalimwezesha Paulo kifedha wakati alipokuwa akiyahudumia.
“Na sasa wakati mwingine tunasikia mtu akisema kwa mshangao, ‘Mtu yule anatoa zaka!’ Ni kwa jinsi gani jambo hili ni fedheha, niliuliza, kwamba kile ambacho miongoni mwa Wayahudi hakikuwa ni jambo la mshangao au la umashuhuri sasa limekuja kuwa ni jambo la mshangao miongoni mwa Wakristo? Kama ingelikuwa ni jambo la hatari kushindwa kutoa zaka kwa wakati ule, basi, kwa uhakika ni hatari zaidi kwa sasa.”
- John Chrysostom Mahubiri kuhusu Waefeso
(Yaliandikwa kabla ya 400 B.K.)
Sera za Kanisa
[1]Utoaji wa zaka unapaswa utokane na wale walio waumini kamili wa kanisa. Kanisa halipaswi kufundisha kuhusu utoaji wa zaka kwa watu ambao hawajaokoka.
Mtu anayehudhuria kanisani kwa mara ya kwanza kamwe hapaswi kujisikia kwamba yeye anawajibika kutoa fedha kwa ajili ya kanisa.
Kanisa halipaswi lijaribu kukusanya zaka kutoka kwa watu ambao wamelitembelea kanisa na bado hawajajikabidhi kuwa wanachama kamili wa kanisa.
Kanisa linapaswa lihakikishe kuwa watu hawafikiri kwamba utoaji wa zaka ni sehemu ya wokovu. Hakuna mtu yeyote anayepaswa kufikiri kwamba zaka litamsaidia mtu kupata wokovu.
Kanisa linapaswa litoe huduma kwa kusanyiko na kwenye jumuiya waliyomo bila ya kudai malipo.
Waumini wote wa kanisa wanapaswa kujua ni kwa jinsi gani fedha za kanisa zinatumika. Kanisa linatakiwa lifuate hatua zilizo makini za utunzaji wa fedha ili kwamba kila mtu aweze kufahamu ni kitu gani kinachofanyika kwa uaminifu.
Zaka siyo mali ya mchungaji peke yake. Zaka inapaswa iwezeshe huduma za kanisa. Hata hivyo, kumwezesha mchungaji kunatakiwa kuwe ni kipaumbele cha kanisa.
“Zaka inapaswa lilipwe bila ya kujali nafasi aliyo nayo mtu.”
- Augustine
Taarifa Saba kwa Muhtasari
1. Mungu ndiye mmiliki wetu pamoja na vitu vyote tulivyo navyo.
2. Zaka ni uwajibikaji kamili kwa kanisa na Mungu kwa pamoja.
3. Mtu ambaye hayuko tayari kutoa zaka kwa ujumla hamtii Mungu kwa fedha zake.
4. Zaka siyo malipo ya wokovu.
5. Zaka ni mpango wa Mungu wa kuwezesha huduma ya kanisa.
6. Mungu hubariki utoaji wa zaka na utoaji wa dhabihu.
7. Zaka ni uwajibikaji wetu wa kumaanisha katika kumtegemea Mungu na utoaji wake.
Kazi za kufanya Somo la 9
1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 9. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.
2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.
3. Masailiano: Wahoji baadhi ya waumini wa kanisa lako kama huwa wanatoa zaka, na ni kwa nini wanatoa au hawatoi. Andika muhtasari unaohusiana na mahojiano hayo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.