Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 10: Ubatizo

15 min read

by Stephen Gibson


Mwanzo wa Desturi ya Ubatizaji

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Mathayo 3:1-12 kwa ajili ya kikundi.

Kwenye Agano Jipya, tunatambulishwa dhana ya ubatizo kupitia huduma ya Yohana Mbatizaji. Hata hivyo, Yohana hakuanzisha ubatizo. Mafarisayo waliwabatiza Mataifa walioamini na kuingia katika Uyahudi. Mafarisayo Hawakuwabatiza Wayahudi, kwa sababu walichukulia kwamba Wayahudi tayari walikuwa ni watu wa Mungu. Yohana alitekeleza kwa jinsi ya tofauti kabisa desturi hii kwa sababu yeye aliwabatiza Wayahudi.

► Je, Yohana alimkataa nani kwenye ubatizo? Kwa nini? Hali hiyo inatufahamisha nini kuhusiana na hitaji la ubatizo?

Baadhi ya Mafarisayo walijitokeza ili wabatizwe na Yohana, lakini Yohana aliwakataza kwa sababu walikuwa hawajatubu.

Mafarisayo walidhania kwamba wao hawakuwa na hitaji la kutubu na kupata msamaha kwa sababu walikuwa Wayahudi. Yohana aliwataka waelewe kwamba watu halisi wa Mungu ni wale wanaompenda na kumtumikia yeye. Watu wanaojinadi kuwa wao ni watu wa Mungu kwa sababu ya kuzaliwa kama Wayahudi ni kama miti ya matunda ambayo haizalishi matunda. Mungu aliwakataza.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Yohana 3:22-23 na Yohana 4:1-2 kwa ajili ya kikundi.

Ni dhahiri kwamba Yesu alisisitiza kuhusu ubatizo katika huduma yake. Yesu mwenyewe hakubatiza, lakini aliikabidhi jukumu hilo kwa wanafunzi wake. Walibatiza watu wengi kuliko hata ilivyokuwa kwa Yohana.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Mathayo 28:18-20 kwa ajili ya kikundi.

Mwishoni mwa huduma ya Yesu hapa duniani aliwaagiza wanafunzi wake waende mahali popote duniani wakawafanye watu kuwa wanafunzi. Aliwaagiza wabatize.

Tunajua kwamba agizo hili halikuwa tu kwa ajili ya mitume, kwa sababu huduma ya umisheni itachukua karne nyingi kumalizika. Yesu alitoa ahadi kwamba atakuwa pamoja nao “hadi mwisho,” hii ikionyesha kwamba hili agizo na ahadi hii ni kwa ajili ya kanisa katika vizazi vyote.

Tunaona kutoka katika nyaraka za Agano Jipya kwamba kanisa la karne ya kwanza lilitii agizo hili neno kwa neno (Matendo 2:38, Matendo 8:38).

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 1:12-17 kwa ajili ya kikundi. Kwa nini Paulo alifurahia kwamba yeye mwenyewe hakubatiza watu wengi katika Korintho?

Ubatizo uliwakilisha kuingia kwenye kanisa. Kanisa la Korintho lilikuwa limegawanyika na waumini wake wanachama walikuwa wanafuata viongozi mbalimbali. Paulo anawakumbusha kwamba ubatizo hauna maana kwamba watu wanafanyika kuwa ni wafuasi wa mtu fulani; bali inamaanisha kwamba wanafanyika kuwa ni wafuasi wa Kristo. Alikuwa amefurahia kwamba yeye mwenyewe hakuwa amebatiza watu wengi miongoni mwao, ili kwamba hakuna mtu yeyote atakayefikiria kwamba alikuwa anawataka wawe wafuasi wake binafsi. Kipaumbele cha Paulo kilikuwa ni kuhubiri injili.

► Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusiana na zoezi la kawaida la ubatizo kwenye kanisa la mwanzo?

Kifungu hiki kinatuambia kwamba kanisa la mwanzo lilibatiza waumini kila mahali. Walikuwa wanafuata agizo la Yesu. Ubatizo haukuwa tu kwa ajili ya watu katika Israeli. Haikuwa ni desturi ya muda mfupi tu. Ilifanyika kila mahali ambapo injili ilikwenda.

[1]Tangu mwanzo, kanisa limekuwa likifanya huduma ya ubatizo kama ushuhuda katika jamii au kwa jamii hadharani kwamba mwenye dhambi ametubu na ameingia kwenye ushirika wa watu walioamini.

Kwa watu wengi, ubatizo siyo katika wakati ambapo wanafanyika kuwa Wakristo. Mwenye dhambi anayetubu anakuwa ameokoka na wakati huo yeye mwenyewe akiwa ameiweka imani yake kwa Kristo. Baada ya kuwa ameokoka, anapaswa aheshimu na kutii agizo la kubatizwa kama udhihirisho wa maisha yake mapya ya utiifu kwa Yesu kama Bwana na Mwokozi. Kuna watu ambao ni tofauti, kwa sababu ilikuwa wakati wa ubatizo ni kwamba waliiweka imani yao katika Kristo na uzoefu wa kuokoka. Lakini, kwa kawaida, ubatizo ni ushuhuda kwamba wokovu tayari umeshatokea.

► Je, utamwambia nini mtu anayesema kwamba alifanyika Mkristo wakati alipobatizwa?


[1]

“Ubatizo wa Kikristo ni sakramenti inayoandamana na ibada za kidini kuashiria kukubalika kwa faida zinazotokana na kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo, na ahadi iliyo na kusudio kamili la utiifu katika utakatifu na haki.”

- Wiley & Culbertson,
Introduction to Christian Theology

Kosa la Kuepuka: Kufikiri kwamba Ubatizo ni sehemu ya Wokovu

Baadhi ya watu wanatafsiri aya kadhaa za Maandiko kumaanisha kwamba ubatizo ni sehemu ya wokovu. Wanaamini kwamba mtu huwa hajaokoka kabisa hadi atakapokuwa ameokoka. Anania alimwambia Sauli, “Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako” (Matendo 22:16). Hata hivyo, dhambi zetu huwa zinaoshwa kwa damu ya Kristo (1 Yohana 1:7). Utakasaji wa kutumia maji unaweza tu kuwakilisha uhalisia wa kiroho. Anania alikuwa anamwambia Sauli kwamba anapaswa afanye udhihirisho wa kimwili wa hatua ya imani. Ubatizo ulikuwa ni ushuhuda kwamba dhambi zake zimeondolewa kabisa.

Katika Waebrania 10:22, tunaambiwa kwamba waumini wanapaswa wamkaribie Mungu “hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.” Inawezekana maji yanarejelewa kuwa ni ubatizo. Hiyo siyo uhakika kabisa. Hata hivyo, hata kama inarejelea kuwa ni ubatizo, aya haijasema kwamba ubatizo unatuokoa. Inasema tu kwamba tunapaswa tutii agizo la Mungu la kubatizwa.

Katika Yohana 3:5 Yesu alimwambia Nikodemo kwamba mtu anapaswa “azaliwe kwa maji na kwa roho.” Taarifa hii inafuatia taarifa yake kwamba mtu anapaswa azaliwe tena kwa mara nyingine, jambo ambalo lilimchanganya Nikodemo. Nikodemo alikuwa akifikiria kuzaliwa kunakofanyika kimwili. Yesu alikuwa akisema kwamba mtu ni lazima azaliwe siyo tu kimwili, bali pia kiroho, ili kuweza kuingia kwenye ufalme wa mbinguni. “Kuzaliwa kwa maji” ndiko kuzaliwa kimwili.

Ubatizo ni katika Kumtii Kristo

Ubatizo siyo kazi ambayo mtu anaifanya ili kukidhi sifa ya wokovu au kupata wokovu. Baadhi ya watu hufundisha kwamba kwa kuwa ubatizo siyo kazi ambayo inaleta wokovu, hatupaswi tuutekeleze. Wana wasiwasi kwamba watu watafanya waweke imani yao kwenye ubatizo badala ya kutegemea neema iliyotolewa katika upatanisho. Hata hivyo, agizo lolote linalotokana na Kristo tunapaswa kulitii, na hatupaswi kufikiri kwamba utiifu wetu katika maagizo ya Mungu ndio unaotuletea wokovu wetu.

Ubatizo kama Njia ya Neema

Ubatizo unaweza ukaitwa ni njia ya kupokea neema. Hiyo haimaanishi kwamba unatuokoa sisi, au kwamba kitendo hicho moja kwa moja kinatupa neema. Kama mtu akibatizwa bila ya kuwa na imani, ubatizo huo hauna thamani yeyote. Ubatizo ni njia ya neema kwa sababu ni kitendo ambacho Mungu alikitengeneza kwa ajili yetu. Tunapokifanya kitendo hiki kwa utiifu na kwa imani, Roho wa Mungu hufanya kazi ndani ya mioyo yetu katika kutuweka kwenye maisha ya Kikristo.

► Je, ni kwa nini tubatizwe?

Ishara ya Kitheolojia

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 6:3-11 kwa ajili ya kikundi. Je, ubatizo unaashiria nini kwa mujibu wa kifungu hiki cha Maandiko?

Biblia inatuambia kwamba ubatizo ni ishara ya kifo, kuzikwa na kufufuka kwa Yesu. Wakati mtu aliyeamini anapobatizwa anashuhudia kwamba anajiungamanisha na upatanisho uliotolewa na Kristo. Mtume aliweza hata kutumia tamko kwamba sisi sote “tuliobatizwa katika Kristo.”

Katika wokovu, tunapokea faida za kifo cha Yesu; lakini, katika ufahamu wa kipekee, tunashiriki pia katika mauti yake. Yesu alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, na siyo kwa sababu ya dhambi zake, bali dhambi za dunia. Vivyo hivyo, katika wokovu tunakufa kwa dhambi, kwa sababu tunatubu na kugeuka mbali na dhambi.

Somo lililoko katika Warumi 6 ni ushindi juu ya dhambi. Halirejelei tu kwenye msamaha. Ni wazi kwamba mtu aliyeamini anapaswa kuwa huru kutokana na utawala wa dhambi (12-14) na siyo kuendelea katika dhambi (1).

Kwenye wokovu tunashirikishana katika kufufuka kwa Yesu. Kama vile alivyotoka kutoka kwa wafu, na sisi tunaanza maisha mapya tunapokufa kwa dhambi. Tunaanza maisha ya ushindi na uhuru kutoka katika dhambi.

Suala la kuhusiana na Aina ya Ubatizo

Swali linalohusu aina ya ubatizo ni hili: je, mtu aliyeamini abatizwe kwa kuzamishwa ndani ya maji, kwa kumiminiwa maji au kwa kunyunyiziwa maji?

Wengi wa Wakristo wengi katika dunia hii ambao wanafanya ubatizo wa watu walioamini wanafanya ubatizo kwa kuzamisha ndani ya maji.

Kuna sababu kadhaa ambazo Wakristo wengi huamini kwamba ubatizo kwa kuzamisha ndio njia iliyo sahihi.

1. Neno batiza (baptize au baptizo) linatokana na neno la Kiyunani linalomaanisha kuzamisha au kutumbukiza ndani ya maji

[1]2. Ubatizo unaashiria kifo cha Yesu, kuzikwa na kufufuka kwake, ambako kunaashiriwa na tendo la kuzamishwa au kutumbukizwa ndani ya maji (Warumi 6:3-5).

3. Ndani ya Biblia, watu walikwenda kwenye maeneo yenye maji wakaingia ndani yake kwa ajili ya kubatizwa (Marko 1:10, Matendo 8:38).

4. Kanisa la mwanzo lilifanya ubatizo kwa njia ya kuzamisha ndani ya maji isipokuwa tu pale ambapo ilikuwa haiwezekani kwa sababu ya afya mbaya ya mtu au ukosefu wa maji. Didache, ulikuwa ni muhtasari wa mafundisho ya mitume ulioandikwa karibu mwaka wa 70 B.K., ukisema kwamba mtu aliyeamini anaweza kubatizwa kwa maji ya kumiminiwa endapo maji mengi yatakuwa hayapatikani.

Kwa ajili ya sababu hizi, Wakristo wengi wanaamini kwamba aina ya ubatizo wa kuzamishwa ndani ya maji ndio wa kibiblia na wa kihistoria.

Baadhi ya Wakristo wanaamini kwamba aina nyingine ya ubatizaji ni wa kimaandiko. Agano la Kale linaelezea sherehe mbalimbali za unyunyizwaji wa maji kuashiria kwamba ni uwakilishwaji wa utakaso. Pia Agano Jipya linarejelea kwenye unyunyizwaji wa damu. Kwa kuwa unyunyizwaji wa damu inaweza ikawa ni ishara ya upatanisho, ubatizo kwa kunyunyiza pia ungeweza kuashiria upatanisho (Kwa ajili ya kurejelea kuhusu kunyunyiziwa ona Kutoka 24:8; Waebrania 9:19-20, Waebrania 10:22, Waebrania 12:22-24; Hesabu 8:6-7; Isaya 52:15; Ezekieli 36:25; na 1 Petro 1:2.)

Kwa kuwa kamwe Biblia haitoi taarifa ya uhakika ya njia gani ya ubatizo inavyotakiwa itumike, tunapaswa tuwe wavumilivu kwa Wakristo ambao wana mtazamo na au maoni tofauti kuhusiana na jambo hili.


[1]

“Neema tunayoihitaji haiko katika maji, bali iko katika kazi ya Roho Mtakatifu ambayo matumizi yake katika ubatizo yanaashiria; si katika mkate na divai, bali katika upatanisho ambao matumizi yake ya kisakramenti yanamaanisha.”

- John Miley,
Systematic Theology

Suala la Ubatizo wa Watoto Wadogo

Kanisa ni jumuiya ya wanaoishi kwa imani kwenye agano na Mungu. Wakati mwenye dhambi anapotubu na kujiunga na jumuiya ya imani, ubatizo unakuwa ni ushuhuda wa nje wa kuokoka kwake.

Lakini inakuwaje kwa mtoto mdogo aliyezaliwa na wazazi wa Kikristo walioko katika kanisa? Mtoto ni sehemu ya jumuiya ya imani. Mtoto mdogo anakubalika na Mungu hadi pale atakapokuwa amekua ya kutosha katika kuweza kuchukua maamuzi yake mwenyewe ya kuokoka.

Baadhi ya makanisa yanaamini kwamba mtoto mdogo anapaswa kubatizwa kama ishara kwamba yuko kwenye jumuia ya imani. Kama mtoto atakapokuwa na umri wa utu uzima na akakubaliana na mafundisho ya imani ya kanisa, makanisa haya hufanya sherehe wanazoziita “ubarikio.” Baadhi ya makanisa hawachukulii maanani kwamba kuokoka ni muhimu kwa sababu mtoto alizaliwa katika mazingira ya kanisa na kukubali kile alichokuwa anafundishwa (Mifano halisi ni Wakatoliki, Walutheri, na Kanisa la Uingereza.) Makanisa mengine yanayobatiza watoto wadogo yanaamini kwamba kuokoka ni muhimu (Kwa mfano, Wamethodisti wa mwanzo waliokuwa wakiongozwa na John Wesley waliamini kwamba kuokoka ni muhimu hata kwa mtu ambaye alibatizwa wakati akiwa mtoto.)

Baadhi wanaamini kwamba kutahiriwa kulitimiza kusudi linalofanana katika Agano la Kale. Mtoto alikuwa anatahiriwa ili kuonyesha ishara kwamba alikuwa kwenye agano. Alikuwa hangojei hadi awe mzee kamili ili kuelewa agano lilikuwa linamaanisha kitu gani.

Inaelekea Kanisa la mwanzo lilikuwa linafanya ubatizo wa watoto wadogo. Hippolista aliandika kuhusu mila ya kitume katika mwaka wa 212 B.K. na akasema kwamba watoto wanapaswa wabatizwe; na, kama ni watoto sana wasioweza kuzungumza wenyewe, wazazi wao wanaweza wakawasemea. Origen aliandika katika mwaka wa 248 B.K. kwamba mitume walikuwa wakifanya ubatizo wa watoto wadogo. Augustine aliandika katika mwaka 400 B.K. kwamba ubatizo wa mtoto mdogo alikuwa ukifanyika katika kanisa lote tangu wakati wa mitume na kwamba kamwe alikuwa hajawahi kusikia mtu yeyote akipinga au kukataa ubatizo wa watoto wadogo.

Kwenye kitabu cha Matendo, wakati mwingine mitume walibatiza familia nzima (Matendo 11:14, Matendo 16:15, 33). Tunaweza tukasadiki kwamba pia walibatiza watoto wadogo.

Vipingamizi vya Ubatizo wa Watoto Wadogo

1. Kwenye Agano Jipya, watu walioamini walikuwa wakibatizwa baada ya kupata ushuhuda wa imani. Walikuwa ni watu ambao walikuwa wametubu na wakaiamini injili. Hakuna maelekezo ya kubatizwa watoto wadogo.

2. Ubatizo wa watoto wadogo hauwezi kutimiza kusudi la asili la utoaji ushuhuda kwamba mwamini alikufa dhambini na anaishi kwa ajili ya Mungu.

3. Matokeo ya kihistoria ya ubatizo wa watoto katika maeneo mengi yamekuwa ni kutengeneza mikusanyiko ya watu ambao hawajaokoka na wanaofikiri kwamba wao ni Wakristo kamili.

Badala ya kubatiza watoto wadogo, baadhi ya makanisa yana sherehe kwa ajili ya watoto wadogo wanazoziita “Kuweka Wakfu.” Kwenye sherehe hiyo, wazazi huwaweka wakfu watoto kwa Mungu na kuahidi kuwakuza kwenye mafunzo ya Ukristo. Kwenye makanisa hayo, ubatizo haufanyiki hadi pale mtoto atakapokuwa amekuwa mkubwa wa kutosha kuelewa kuhusu kutubu na imani.

Wanapohubiriwa watu ambao walibatizwa wakiwa watoto, haina umuhimu wa kutia fedheha ubatizo wao. Badala yake, hubiri kwamba mtu hawezi kuwa ameokoka pasipokuwepo na kutubu dhambi na imani inayookoa. Kama mtu anaishi katika dhambi, ubatizo wake hautakuwa ni sababu ya kufikiri kwamba yeye ni Mkristo.

Suala la Muda

► Je, ni kwa muda gani kanisa litasubiri ili kumbatiza mtu mpya aliyeamini?

Kwenye Agano Jipya, watu wapya waliokuwa wameamini walikuwa wanabatizwa haraka bila ya kupoteza muda. Ubatizo haukuwakilisha kiwango cha ukomavu au ufahamu wa mtu.

Baadhi ya makanisa wanawataka watu wapya walioamini kuwa katika kipindi cha muda cha mafundisho na ukuaji wa Kikristo kabla ya kufikia hatua ya kubatizwa. Wanataka kuhakikisha kwamba watu wapya walioamini wanakuwa mifano bora ya Wakristo. Wanataka kuwaona wakiishi maisha ya Kikristo kwanza kwa muda fulani kwa kuwa wengine wataweza kuanguka kutoka katika wokovu baada ya kuwa wamekwisha kubatizwa.

Ubatizo ni ushuhuda kwamba mtu aliyebatizwa ameokoka. Siyo taarifa ya kukua kiroho au ufahamu. Kwa hiyo, ubatizo unatakiwa ufanyike mara tu mtu mpya anapokuwa ameamini au ameokoka. Kungojea kunamaanisha kwamba hatuna uhakika kama mtu husika kweli ameokoka. Inaonyesha kuna mashaka kwenye ushuhuda wake, jambo ambalo linaweza kumsababisha awe mdhoofu katika imani yake mwenyewe.

Ubatizo pia ni njia ya neema, kwa sababu jinsi mtu anapokuwa mtiifu katika imani na kulifanya tendo hili liwe udhihirisho kwa watu wote, Mungu humwezesha kuanza kwa neema. Kama tutamfanya mtu mpya aliyeamini awe mtu wa kusubiri wakati wa kuja kubatizwa wakati mwingine, tunamweka mbali na kuupata huu msaada katika wakati ambapo alikuwa anauhitaji sana kuliko kitu kingine.

Kama inaelekea kwamba mtu haonyeshi kuwa na uelewa wa injili na haonyeshi mabadiliko kwa njia ya neema, hapaswi kubatizwa. Kama atakuwa anazo hizo sifa, anatakiwa abatizwe haraka kama njia ya kuimarisha imani yake.

Suala la Ubatizo Uliocheleweshwa

Wakati mwingine watu wanaojinadi kwamba wao ni Wakristo hutaka kuchelewesha ubatizo wao. Husema kwamba wameiamini injili na kutubu, lakini bado hawajahitaji kubatizwa. Wakati mwingine huchelewesha hata kwa miaka. Wakati mwingine watu wanasubiri hadi wanakufa.

Kama mtu anakuwa hayuko tayari kubatizwa kwa hiari, mara nyingi kunatokea kuwepo na jambo lililounganishwa na ubatizo ambalo hayuko tayari kulifanya. Inawezekana hapendi kufunganishwa kabisa na kanisa. Inawezekana kuna dhambi ambayo kiuhalisia hajaiacha bado. Inawezekana hapendelei kufanya ushuhuda wa wazi kwa watu kwamba yeye ni Mkristo.

Kama kweli atakuwa ameokoka, mtu huwa ni Mkristo kabla ya kubatizwa. Hahitaji ubatizo ili uweze kumfanya awe Mkristo. Hata hivyo, kama yeye binafsi hana hiari ya kutubu dhambi kabisa na kumshuhudia Kristo, bado yeye anakuwa siyo Mkristo.

► Je, utasemaje kwa mtu anayesema kwamba yeye ni Mkristo lakini hapendi kubatizwa?

Suala la Jina

► Je, mchungaji anapaswa aseme nini wakati anapokuwa anambatiza mtu mpya aiyeamini?

Wakati Yesu alipowapa mitume Agizo Kuu, aliwaambia wabatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19).

Kubatizwa “kwa jina la” Utatu Mtakatifu wa Mungu ilikuwa na maana ya kubatizwa chini ya mamlaka yao. Yesu alitumia neno jina sawa sawa na wakati aliposema hakuja kwa jina lake mwenyewe (Yohana 5:43).

Baadhi ya makanisa yanaamini kwamba mchungaji anayefanya tendo la ubatizo anapaswa aseme, “Ninakubatiza wewe kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.” Makanisa mengine yanaamini kwamba njia iliyo sahihi zaidi ya ubatizaji chini ya mamlaka ya Nafsi tatu za Utatu Mtakatifu ni kusema, “Nakubatiza wewe kwa Jina la Yesu.”

Kwenye Agano Jipya, tunapata huko mifano kadhaa yenye maelekezo ya kubatiza, na maneno yanatofautiana na maneno ya Yesu aliyoyatumia wakati alipowapa mitume wake Agizo Kuu. Kwenye siku ya Pentekoste, Petro aliwaambia watu wapya waliokuwa wameamini, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo” (Matendo 2:38). Paulo aliwabatiza watu wapya walioamini katika Efeso kwa jina la Yesu (Matendo 19:5). Petro aliwaambia watu wapya walioamini kwenye nyumba ya Kornelio, “wabatizwe kwa jina la Bwana Yesu” (Matendo 10:48). Paulo alionyesha kwamba waumini wapya katika Korintho walibatizwa kwa Jina la Yesu (1 Wakorintho 1:12-13).

Kwenye kitabu cha Matendo, ubatizaji kwa Jina la Yesu ulionyesha utofauti uliokuwepo kutokana na ubatizo wa Yohana (ambao pia umetajwa mara saba kwenye kitabu cha matendo) na aina za ubatizo wa dini nyingine.

Inaonekana kwamba njia iliyotumiwa na kanisa kukamilisha agizo la Yesu ilikuwa ni kuweka msisitizo wa jina la Yesu kwenye ubatizo. Kuna uwezekano kwamba mchungaji aliyekuwa akifanya tendo la ubatizo kwenye kanisa la karne ya kwanza alikuwa akisema, “Nakubatiza wewe kwa jina la Yesu.” Kwenye miaka ya mwanzo ya kanisa, imani katika Yesu ilikuwa ndio suala lililokuwa kubwa. Kama mtu aliweza kuamini katika Yesu, alifanyika kuwa Mkristo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa historia ya kanisa la mwanzo sana, kanisa lilitilia mkazo Utatu Mtakatifu wakati wa ubatizo. Ndani ya kizazi cha kwanza cha kanisa, kulikuwa na watu waliosema kwamba walimwamini Yesu, lakini hawakuwa wanaamini mambo ya kweli kuhusiana na Mungu. Andiko la Didache linasema kwamba watu wapya walioamini wanapaswa kuzamishwa mara tatu ndani ya maji kukiwa na kanuni za imani kwa kila nafsi ya Utatu Mtakatifu. Waandishi wengine, kwenye mwaka wa 248 B.K au kabla ya hapo, waliandika kwamba utaratibu wa kawaida wa kanisa ilikuwa ni kutaja Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu wakati wa ubatizo (Hippolita, Origen, Tertullian, na wengine).

Tatizo la wakati wa sasa ni kwamba baadhi ya vikundi vya dini au madhehebu vinakataa uwepo wa Utatu Mtakatifu wa Mungu. Wanasema kwamba wanaamini katika Yesu, lakini hawaamini kwamba Yesu ni nafsi inayotofautiana na Baba na Roho Mtakatifu. Wanabatiza kwa jina la Yesu kwa sababu wanaamini kwamba jina hilo Yesu ndilo jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Wanaamini kwamba nafsi zote tatu ziko ndani ya mtu mmoja. Mfano mmojawapo wa kundi linaloamini hivi ni kanisa la United Pentecostal Church.

Kwa wakati wa sasa makanisa mengi yanayoamini katika Utatu Mtakatifu yanabatiza wakitumia maneno, “Nakubatiza wewe kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Wanathibitisha imani yao iliyo katika Yesu na kuamini katika Utatu Mtakatifu wa Mungu.

 

Namna ya Kufanya Ubatizo

Kusanyiko: Watu wapya walioamini ambao ndio wanaotegemewa kubatizwa watapaswa kusimama kwa pamoja ili kuonyeshwa kwa watu ambao wamehudhuria kuja kushuhudia. Wakati kundi likiendelea kukusanyika pamoja, mtu mmoja anaweza kuwaongoza katika kuimba kwa dakika chache.

Andiko: Mtu mmoja anaweza kusoma kutoka katika Mathayo 28:18-20.

Tamko: Mchungaji atatakiwa azungumze na kundi lililohudhuria na kusema, “Hawa walioko hapa kwa ajili ya kubatizwa wamethibitika kwamba wametubu na kuiweka imani yao kwa Kristo. Kwa kuwa ubatizo unawakilisha kifo na ufufuo wa Yesu, waumini hawa wanathibitika kwa njia ya ubatizo kwamba wamekufa kwa dhambi na sasa wanaishi kwa ajili ya Mungu. Wameanza maisha mapya ya utiifu kwa Mungu.”

Maombi: Kisha mchungaji ataliongoza kwenye maombi kwa ajili ya watu wapya walioamini ambao watapata ubatizo. Maombi yake yatahusisha pamoja na matamko kama haya: “Bwana, tunasema asante kwa ajili ya neema yako ambayo imewaleta watu hawa kwenye wokovu na maisha ya kiroho. Tunasema asante kwa sababu umewatoa katika nguvu ya dhambi. Tunaomba kwa ajili ya Roho Mtakatifu awajaze na kuwapa ushindi kila siku. Wafanye wawe mashahidi kwenye jumuiya zao na wawe baraka kwa kanisa.”

Ubatizo: Watu wapya walioamini ambao wamekuja kwa ajili ya kubatizwa wataingia mmoja mmoja ndani ya maji kumwendea mchungaji alipo. Kabla ya kumbatiza kila mmoja, mchungaji atapaswa kusema, “Nakubatiza wewe… kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”

Wimbo wa pamoja: Baada ya ubatizo kufanyika, kusanyiko linaweza kuimba wimbo wa pamoja. Mtu mmoja anaweza akaongoza tena kwenye kufanya maombi mafupi.

Taarifa Saba kwa Muhtasari

1. Wanafunzi wa Yesu walibatiza wakati wa huduma yake.

2. Kanisa la mwanzo lilibatiza watu kila mahali injili ilipokwenda.

3. Ubatizo unaashiria kifo, kuzikwa na kufufuka kwa Yesu.

4. Ubatizo ni ushuhuda wa wokovu na maisha mapya ndani ya Kristo.

5. Mtu mpya aliyeamini anapaswa kubatizwa mara moja baada ya kuokoka.

6. Mtu hapaswi kudhania kwamba yeye ni Mkristo kwa sababu tu alikuwa amebatizwa.

7. Kanisa linapaswa kuthibitisha imani ya Utatu Mtakatifu katika ubatizo.

 

Kazi za kufanya Somo la 10

1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 10. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.

2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.

3. Masailiano: Fanya mazungumzo na waumini watatu tofauti na uwaulize ubatizo wao ulimaanisha nini kwao. Andika muhtasari mfupi kuhusiana na mazungumzo hayo.

Next Lesson