Kiongozi wa darasa au wanafunzi waliochaguliwa watapaswa waelezee historia ya ukombozi wa Israeli kutoka utumwani Misri. Ruhusu wanafunzi mbalimbali wachangie mada hii. Kitabu cha Kutoka 11-12 kinaelezea kuhusu Pasaka ya kwanza.
Pasaka ilikuwa ni sikukuu ya Wayahudi iliyokuwa ikisherehekewa katika nyakati za usiku wakati taifa la Israeli lilipotoka Misri. Sherehe haikuwa tu kwa ajili ya kukombolewa kutoka Misri; ilikuwa ni sherehe iliyohusu rehema ya Mungu juu yao wakati alipowapiga Wamisri kwa vifo lakini akaziruka nyumba za wana wa Israeli bila vifo (Kutoka 12:27). Kwa hiyo, tukio hili lilikuwa ni ishara ya rehema za Mungu dhidi ya watu wake.
Baada ya kukombolewa kutoka Misri, Waisraeli walikuwa na sikukuu ya Pasaka kila mwaka. Mungu aliwapa vitu vya kusherehekea kwa ajili ya siku hiyo ikiwa ni pamoja na chakula maalumu na matumizi ya damu ya kusherehekea.
Tukio hilo lilikuwa kama aina ya wokovu. Hiyo haina maana kwamba watu waliokombolewa katika siku hiyo walisamehewa dhambi zao zote na kuwa katika uhusiano sahihi na Mungu. Hata hivyo, walikombolewa kutoka utumwani, walipokea neema kutoka kwa Mungu, na damu ilikuwa sehemu ya hitaji la Mungu. Mambo haya yote yaliyofanyika yanafanya tukio hili kuwa kama kielelezo cha wokovu ulioletwa na Kristo. Waisraeli walio wengi walisherehekea sikukuu hii bila ya kutambua maana yake kamili.
Kwenye Pasaka ya mwisho ambayo Yesu alishirikishana na wanafunzi wake, alielezea maana yake. Alianzisha sherehe ya kufanya kwa ajili ya kanisa wakati aliposema “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Luka 22:15-20). Makanisa huiita sherehe hii “Chakula cha Bwana,” au “Meza ya Bwana,” au “Ekaristi,” au “Ushirika Mtakatifu.”
Paulo aliandika kwamba mila hii itafanywa mara kwa mara na kanisa hadi hapo Yesu atakaporudi (1 Wakorintho 11:24-26). Kanisa lilikuwa na nyakati maalumu za sikukuu na ushirika ambazo hazipaswi zichanganywe na Meza ya Bwana. Kwa mfano, wakati Biblia inaposema kwamba waumini wa mwanzo walikuwa “wakimega mkate nyumba kwa nyumba,” tunapaswa tukumbuke kwamba maneno haya kuumega mkate yanarejelea tu kwenye kula (Matendo 2:46). Walikuwa wanafanya ushirika wa kula pamoja katika nyumba mbalimbali. Kanisa pia lilikuwa na “karamu za upendo” ambazo hazikuwa sawa na Meza ya Bwana (Yuda 1:12).
Maana ya Meza ya Bwana
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Yohana 6:47-58 kwa ajili ya kikundi.
Yesu aliushangaza umati aliposema kwamba alikuwa ni mkate kutoka mbinguni na kwamba walitakiwa waule mwili wake na wainywe damu yake.
► Je, Yesu alikuwa anamaanisha nini kwa kauli hizo?
Yesu alisema alikuwa anajitoa mwenyewe kwa ajili uhai wa ulimwengu (Yohana 6:51). Alikuwa anazungumzia kuhusu dhabihu yake mwenyewe ya kujitoa kwa ajili ya utakaso. Alilinganisha dhabihu yake kwa kutumia chakula na kinywaji. Kama vile ambavyo mtu huhitaji chakula kwa ajili ya maisha ya kimwili, ni lazima akubali dhabihu ya Kristo kwa ajili ya maisha ya milele.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Luka22:15-20 kwa ajili ya kikundi.
Kwenye chakula cha mwisho cha Pasaka pamoja na wanafunzi wake, Yesu alisema kwamba mkate ulikuwa ndio mwili wake na divai ndiyo damu yake. Atautoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wao.
Mkate na Divai
► Je, kwa nini Yesu alitumia mkate na divai kwa ajili ya Meza ya Bwana?
Kunaweza kuwepo na sababu nyingi ambazo zinaonyesha ni kwa nini Yesu alitumia mkate na divai kwa ajili ya Meza ya Bwana.[1] Mkate ulikuwa ndio chakula kikuu cha msingi, kama ilivyokuwa kwenye maeneo mengine ya dunia. Mkate hauwakilishi tu chakula kwa ujumla, lakini pia unawakilisha uhai kwa sababu chakula ni muhimu kwa ajili ya uhai. Divai ilikuwa ndicho kinywaji kinachotumika kwa wakati ule, ukiacha maji. Divai pia inawakilisha sherehe au maadhimisho.
Baadhi ya makanisa ya sasa yanatumia divai kwa ajili ya Meza ya Bwana hata kama hawanywi divai kwa nyakati nyingine zote. Makanisa mengine yanatumia juisi ya zabibu au mvinyo ambao haujachachuka kwa sababu hawataki kuhamasisha unywaji wa aina yeyote ya pombe. Juisi ya zabibu ilijulikana kama mvinyo kwenye Agano Jipya ikiwa aidha bado ni mbichi (haijachachuka) au ikiwa kwenye hatua yeyote ya kugeuka kuwa pombe (kuchachuka).
Baadhi ya makanisa yamebadilika kabisa kutumia vitu vingine vya kula na kunywa kwa ajili ya Meza ya Bwana. Tunapaswa tuwe waangalifu sana kuhusiana na matumizi ya kitu kingine kwa ajili ya Meza ya Bwana. Wamomoni wanatumia mkate na maji, lakini hawaamini katika fundisho la imani la Kikristo kuhusiana na upatanisho.
Katika maeneo mengine ya dunia inawezekana mkate na divai visiweze kuwa vinapatikana kama kawaida; vitu vingine vinaweza kuwa vya msingi kama chakula na kinywaji. Katika hali kama hiyo, kanisa kwa njia ya maombi linaweza kufikiria njia nyingine za kutumika.
[1]Image: “The Lord's Supper” taken by Allison Estabrook on Oct. 14, 2022, retrieved from https://nidhamu.flickr.com/photos/sgc-library/52476662295/, licensed under CC BY 4.0.
Siyo Mwili au Damu ya Kawaida
Kanisa Katoliki na Kanisa la Othodoksi ya Mashariki yanaamini kwamba mkate na divai ndivyo mwili na damu halisi ya Yesu. Kuna makanisa mengine yanayoamini kwamba mwili wake na damu yake ni kweli kabisa viko kwenye mkate na divai. Makanisa mengi ya Kiprotestanti yanaamini kwamba mkate na divai vinawakilisha mwili na damu ya Yesu bila ya uwepo wake katika hali yake ya mwili halisi.
Wakati Yesu alipowahudumia wanafunzi wake kwenye Pasaka, alisema, “Hii ndiyo damu yangu…huu ndiyo mwili wangu.” Yesu bado alikuwa amesimama pale, katika hali ya kimwili pamoja nao. Mwili na damu yake vilikuwa bado havijatolewa kama dhabihu. Inaonekana wazi aliimaanisha kwamba mkate na divai vilikua ni ishara ya mwili na damu, na siyo mwili na damu katika hali yake ya uhalisia. Mkate na divai vinavyotumika katika Meza ya Bwana vinapaswa vichukuliwe na kufikiriwa hivyo.
Wokovu uko katika dhabihu ya mara moja tu ya Yesu. Kifo chake hakitokei kwa kurudiarudia. Kwa kuwa Meza ya Bwana ni kitendo cha ibada na imani katika tukio moja tu la kifo cha Yesu, hakuna ulazima kwa mkate na damu vifanyike tena kwamba ni mwili na damu halisi ya Yesu.
Kwa kuwa Wakatoliki wanaamini kwamba kanisa lina mamlaka ya kutoa mwili na damu halisi ya Yesu, waumini wengi miongoni mwao wanaamini kwamba kanisa lina mamlaka juu ya kufanya ni nani anaweza kuokoka. Wanafikiri kwamba mtu hawezi kuokoka kama kasisi atamkatalia kumpa Meza ya Bwana. Mamilioni wanafikiri kwamba mtu huwa ameokoka kwa kutumia Meza ya Bwana.
Mtazamo sahihi wa Meza ya Bwana ni kwamba ni kitendo cha ibada kinachoashiria kifo cha Kristo kwa ajili yetu, wakati ambapo Mungu anaachilia neema yake kama majibu kwa imani ya mtu anayeshiriki. Ni kwa ajili ya watu waliookoka, na ambao wokovu wao hautegemei kupatikana kwa Meza ya Bwana.
► Je, kwa nini hatupaswi kufikiri kwamba Yesu alimaanisha kwamba mkate na divai vilikuwa ni mwili na damu yake halisi?
► Je, ni kwa nini siyo lazima kwa ajili ya wokovu kwamba Meza ya Bwana iwe ni mwili na damu halisi ya Kristo?
Njia ya Neema
[1]Meza ya Bwana mara nyingi huitwa njia ya neema. Mungu ameiandaa Meza ya Bwana kama njia ya neema wakati inapopokelewa kwa imani kwenye upatanisho wa Kristo. Mkristo anapaswa kumtii Mungu kwa kufuata maagizo yaliyoko kwenye maandiko. Mkristo hapaswi kupuuzia njia hii ya neema.
Endapo mtu atatumia Meza ya Bwana bila ya imani katika Kristo, haiwezi yenyewe ikaleta neema kwake ya moja kwa moja.
Endapo mtu ataitumia bila ya kuheshimu kwa ajili ya kile kinachomaanishwa, anajiletea hukumu juu yake yeye mwenyewe (1 Wakorintho 11:27-29).
Kutubu na imani ni mambo muhimu katika wokovu. Meza ya Bwana siyo jambo lililo muhimu kwa ajili ya wokovu. Meza ya Bwana ni kitendo cha utii na kudhihirisha imani. Mkristo hataacha kuendelea kuwa Mkristo kama hatakuwa na uwezo wa kupata Meza ya Bwana.
► Je, ni jambo la lazima kwa Mkristo kutumia au kushiriki Meza ya Bwana? Toa ufafanuzi wa Jibu lako.
“Njia za neema ni njia za kiungu zilizochaguliwa ambazo kwa kupitia hizo ushawishi wa Roho Mtakatifu unaungamanishwa na roho za wanadamu.”
- Wiley & Culbertson, Introduction to Christian Theology
Njia Sahihi za Utumiaji wa Meza ya Bwana
Mtume Paulo alitoa masahihisho kwa Wakorintho kutokana na utumiaji mbaya wa Meza ya Bwana uliokuwa ukifanyika. Maelekezo yake pia yako kwa ajili yetu sisi.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 11:20-34 kwa ajili ya kikundi. Je, ni mambo gani ambayo Wakorintho walikuwa wanafanya vibaya?
Walikuwa wanaleta chakula na kukifanya ni chakula cha Meza ya Bwana. Kila mtu alikula chakula chake mwenyewe kuliko kushirikishana na wenzake. Hakuna mtu aliyekuwa akimsubiri mwenzake ili waweze kuanza kula kwa pamoja na kwa wakati mmoja. Watu wengine walikuwa wakila kupita kiasi, na wengine bado wakiwa na njaa. Wengine walikuwa wakinywa sana hata kulewa.
► Je, ni maelekezo gani maalumu waliyopewa na Paulo?
Aliwataka wasifanye Meza ya Bwana kama ni chakula. Makanisa yalikuwa na vyakula vya sherehe au ushirika, lakini hivyo havikuwa ni Meza ya Bwana. Aliwataka wasubiriane kila mmoja na mwenzake ili waweze kuanza kwa pamoja.
Paulo alifanya mapitiyo ya njia ambazo Yesu aliweka mila ya kufuata kwa ajili ya kanisa. Yesu alitoa mkate, kisha mvinyo, na akiwa anaelezea maana yake. Ni muhimu sana kwa mshiriki kuvipokea kwa heshima, akikumbuka Meza ya Bwana inamaanisha nini.
Paulo alisema kwamba kila mtu na ajihoji mwenyewe ili kuhakikisha kwamba hashiriki katika Meza ya Bwana “isivyofaa.” Baadhi ya watu wanatafsiri kwamba hiyo inamaanisha mtu hapaswi kushiriki katika Meza ya Bwana hadi awe amejihakikisha kwamba maisha yake yanampendeza Mungu katika kila jambo. Hayo sivyo aya inavyofundisha. Mtume alikuwa anazungumzia kuhusu njia ya kushiriki Meza ya Bwana. Mtu anakuwa amehukumiwa endapo atakuwa ameipokea kwa njia isiyo ya kawaida na kutojali.
Ni vyema kwa kusanyiko kuomba pamoja wakati wa kushiriki Meza ya Bwana. Watu tofauti wanaweza wakaandaliwa kuongoza maombi kwenye wakati tofauti wa ibada. Kikundi kinaweza kuimba kwa pamoja wakati wowote wakihitajika. Ibada inatakiwa ifanyike katika hali ya ukimya na yenye mpangilio uliokamilika. Haipaswi iwe ni wakati wa sauti kubwa au kujifurahisha wenyewe. Ni wakati wa kutafakari juu ya dhabihu ya Yesu iliyotolewa kwa ajili ya ukombozi wetu.
Watu sahihi wanaostahili kushiriki katika Meza ya Bwana
► Je, ni nani aruhusiwe kushiriki katika Meza ya Bwana?
Yesu alifundisha jambo la kufanya kwa wanafunzi wake na akawaambia wafanye kwa pamoja, kwahiyo tunajua kwamba Meza ya Bwana ni kwa ajili ya Wakristo. Meza ya Bwana haipaswi Kutolewa kwa mtu ambaye ni mfuasi wa dini nyingine. Mtu anayeabudu miungu mingine anaabudu mashetani. Hawezi pia akamwabudu Kristo (1 Wakorintho 10:20-21).
Kama mtu anaishi katika dhambi ya wazi na bado hajatubu, hapaswi kushirikishwa katika Meza ya Bwana. Kushirikishwa katika Meza ya Bwana ni kuthibitisha kwamba tumejitambulisha pamoja katika kifo cha Kristo. Mtu ambaye anaendelea kwa hiari yake kuwa mtenda dhambi hana ushuhuda huo.
Mtu anayeishi kwenye dhambi ya wazi ya kujitakia kama vile uasherati, ibada ya sanamu, au ulevi siyo Mkristo (1 Wakorintho 6:9-10). Biblia inatuambia kwamba hatuwezi kuwa kwenye ushirika mmoja na mtu anayetenda dhambi hizi na bado anajinadi kwamba yeye ni Mkristo (1 Wakorintho 5:11). Kwa hiyo halitakuwa jambo sahihi kumshirikisha katika Meza ya Bwana.
Kama mwanachama ametenda dhambi na amekataa marekebisho ya kanisa, achukuliwe kama mtu ambaye hajaokoka (Mathayo 18:17), na kwa ajili hiyo hatapaswa kushirikishwa Meza ya Bwana.
Meza ya Bwana inaonyesha umoja maalumu ambao unawahusu Wakristo. Neno Meza ya Bwana linakuwa na maana hiyo. Mtume alisema kwamba katika tendo la Meza ya Bwana tunadhihirisha kwamba tuko mwili mmoja (1 Wakorintho 10:16-17). Kwa hiyo, kama itajulikana kwamba mtu ni mzembe, asiyejali kuhusu kuwa mtenda dhambi, hawezi kushirikishwa katika umoja huo.
Mchungaji anapaswa kushirikisha Meza ya Bwana kwa Wakristo, lakini hawajibiki kuchunguza kila jambo lililo katika maisha yao. Kama mtu atajishuhudia kwamba yeye ni Mkristo na haishi katika dhambi ya wazi, mchungaji anaweza akaukubali ushuhuda wake.
Mtu yeyote ambaye kweli ameokoka anakuwa amepokea upatanisho ambao umewakilishwa na Meza ya Bwana, aidha awe au asiwe ni mwanachama wa kanisa fulani la mtaa. Kwa hiyo, uanachama wa kanisa la mtaa haupaswi uwe ni kigezo kwa ajili ya kushiriki Meza ya Bwana.
Mtu aliyeokoka kwa ukweli ana sifa zote za kushiriki katika Meza ya Bwana na ubatizo. Hapaswi aendelee kusubiri hadi baada ya ubatizo ndipo ashiriki katika Meza ya Bwana, ikiwa yuko tayari kubatizwa.
Kama kusanyiko ni mchanganyiko wa Wakristo na watu ambao hawajaokoka, ikiwa ni pamoja na watu ambao wanaishi katika matendo ya dhambi, Meza ya Bwana haipaswi ishirikishwe kwa kusanyiko lote kwa ujumla. Meza ya Bwana inaweza ikapangiwa wakati wake mwingine kwa ajili ya wale walio na sifa za kushiriki.
► Je, kuna sababu gani ambazo mtenda dhambi za wazi hapaswi kushirikishwa katika Meza ya Bwana?
Mzunguko wa Meza ya Bwana
► Je, Meza ya Bwana iwe inatolewa kwa mara ngapi? Kwa nini?
Baadhi ya makanisa hushirikisha Meza ya Bwana kila wiki. Makanisa mengine hushirikisha mara moja kwa mwaka. Mengine hufanya mara chache sana, bila ya ratiba.
Biblia haijatuambia ni mara nyingi kiasi gani tushirikishe Meza ya Bwana.
Baadhi ya watu kabla ya kuokoka walitumainia desturi za kidini kwa ajili ya wokovu. Wakati walipookoka na kuachana na aina hiyo ya desturi, wanaweza wasijisikie tena vizuri na aina yeyote ya desturi za kidini. Wanaweza wakafikiri kwamba Meza ya Bwana haipaswi ishirikishwe mara nyingi.
Baadhi ya watu kwa makosa huiweka imani yao kwenye desturi za dini. Wanataka wawe na Meza ya Bwana mara nyingi kwa sababu inawasaidia kufikiri kwamba wameokoka.
Ni jambo muhimu sana kwa mchungaji kuelezea maana ya Meza ya Bwana. Anapaswa awasaidie watu wake kuelewa jinsi ya kuitumia kama baraka kwao katika uhusiano wao na Mungu bila ya kuiamini kwa njia iliyo potofu.
Mamlaka Kamili kwa ajili ya Usimamizi wa Meza ya Bwana
► Je, ni nani mwenye haki ya kushirikisha Meza ya Bwana?
Biblia inatuambia kwamba kila mtu aliyeamini ni kuhani (Ufunuo 1:6, 1 Petro 2:5, 9). Hii ina maana kwamba tunaweza tukamwabudu Mungu moja kwa moja pamoja na kuwasaidia watu wengine waweze kumwabudu yeye. Hakuna mpatanishi yeyote duniani ambaye ni lazima kwa ajili ya kutuleta kwa mungu, kwa sababu Yesu ndiye Kuhani wetu Mkuu, na ametupa fursa ya kuingia (1 Timotheo 2:5, Waebrania 4:14-16). Kwa yeye, sisi tunapaswa bila kikomo tuendelee kutoa dhabihu zetu za sifa (Waebrania 13:15).
Kwa kuwa kila mtu aliyeamini ni kuhani, tunaweza tukawa na sababu kwamba mtu yeyote aliyeamini anaweza kushirikisha Meza ya Bwana kwa waumini wengine, hasa wakati ambapo mchungaji hayupo. Hata hivyo, kuna sababu ambazo Meza ya Bwana inapaswa kwa kawaida ishirikishwe kwa maelekezo ya mchungaji.
Biblia haijatoa tamko la moja kwa moja kwamba Meza ya Bwana inapaswa ishirikishwe tu na mchungaji. Hata hivyo, Paulo alitoa maelekezo maalumu kwa ajili ya kushirikisha Meza ya Bwana kwa njia ya utaratibu na yenye heshima. Maelekezo hayo yalikuwa ni kwa ajili ya kikundi, na kiongozi alikuwa anawajibika kukiongoza kikundi. Katika hali ya kawaida washiriki wa kanisa watamtegemea mchungaji wao kwamba atahakikisha Meza ya Bwana itashirikishwa vizuri, na mchungaji atapaswa alichukue hilo jukumu.
► Angalia tena maonyo yaliyotolewa katika 1 Wakorintho 11:27-34.
Paulo alisema kwamba maelekezo yalikuwa ni muhimu kwa sababu ya heshima kwa ajili ya mwili na damu ya Kristo. Kama mtu alikuwa asiyejali, atakuwa mwenye hatia. Hukumu ya Magonjwa na vifo tayari imekuja juu ya walio wengi. Paulo alisema kwamba kama wangekuwa makini kujitathmini wenyewe, watakuwa wameepushwa na hukumu ya Mungu. Paulo alisema kwamba baadaye angekuwa na maelekezo ya ziada kwa ajili yao.
Ni jambo la muhimu kushiriki katika Meza ya Bwana kwa njia nzuri, siyo tu kwa ajili ya kukwepa madhara yanayotokana na matumizi mabaya, bali kupata faida ambazo Mungu ameziweka kwa ajili yetu.
Ni jambo la mantiki kufikiri kwamba mtume alitegemea viongozi wa kanisa waweze kuhakikisha kwamba maelekezo haya yanatekelezwa. Wanachama wa kanisa watapenda kuona wachungaji wao wakiwasaidia katika kushirikishwa Meza ya Bwana kwa njia nzuri kwa sababu ya umuhimu wake.
Mchungaji pia analo jukumu maalumu la kuangalia kwamba Meza ya Bwana haishirikishwi kwa mtu ambaye ni wa dini nyingine au dhambi ya wazi.
Kwa hiyo, Meza ya Bwana kwa kawaida inapaswa ishirikishwe na mchungaji au mtu mwingine chini ya maelekezo ya mchungaji. Mchungaji anaweza kuwaelekeza watu wengine wamsaidie yeye katika ibada ya kushirikisha Meza ya Bwana na anaweza kuidhinisha mtu kutumikia karamu ya Bwana akiwa hayupo.
Utaratibu kwa ajili ya kushirikisha Meza ya Bwana
Kukusanyika: Kutatakiwa kuwepo na utaratibu wa kukusanyika kwa watu ambao watashiriki katika Meza ya Bwana. Kama itapaswa ifanyike kwenye ibada ya kuabudu ya watu wote wa kanisa, viongozi wanaohusika ni lazima waweze kujua ni kwa jinsi gani watawahudumia watu wale tu walio sahihi kushirikishwa.
Maandiko: Kabla Meza ya Bwana haijaanza kushirikishwa, Maandiko yanapaswa yasomwe. Taarifa chache zinaweza Kutolewa kuhusiana na Maandiko hayo, lakini ziwe fupi. Mifano ya vifungu vya maandiko ambavyo vinaweza vikatumika ni pamoja na Mathayo 26:26-30, Markoo 15:22-28, Luka 22:14-20, Yohana 10:11-18, Yohana 19:1-6, Yohana 19:16-19, Yohana 20:26-29, 1 Wakorintho 11:23-26, Waebrania 10:11-17, Waebrania 9:24-28, Waebrania 4:12-16, Ufunuo 1:12-18, Isaya 53:1-5, au Isaya 53:6-12.
Maombi: Mtu mmoja ataongoza katika maombi. Maombi hayo yanapaswa yahusishe pamoja na taarifa kama hizi: “Bwana, tunasema asante kwa ajili ya ukombozi uliotupatia kupitia dhabihu ya Yesu. Tunasema asante kwa neema ya bure uliyotupatia sisi. Tunapoenda kushiriki Meza ya Bwana kwa pamoja tunashuhudia kwamba tunakutegemea wewe pekee katika maisha yetu ya kiroho. Tunadhihirisha umoja wetu tulio nao kwa pamoja kama waumini. Tunaomba kwa ajili ya neema yako itakayotuwezesha tuishi maisha ya kukupendeza wewe kila siku.”
Kugawa mkate: Mkate unaweza ukagawanywa na mchungaji au watu aliowachagua. Anaweza akasema, “Mkate huu unawakilisha mwili wa Kristo, uliotolewa kwa ajili ya wokovu wetu.” Kila mtu atapaswa anyamaze kimya na kuonyesha heshima wakati wote wa Meza ya Bwana. Kwenye makanisa mengine, mchungaji huwataka watu wanaoshiriki kushikilia mkate hadi kila mmoja anapokuwa amepata, kisha watakula kwa pamoja. Kwenye makanisa mengine, mila iliyopo ni kila mtu kula mkate wake akishaupokea.
Maombi: Mchungaji au mtu mwingine yeyote aliyechaguliwa anaweza akaongoza maombi mafupi ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya neema yake.
Kugawa Divai: Mchungaji anaweza akasema, “Divai hii inawakilisha damu ya Yesu, iliyotolewa kwa ajili yetu.” Baadhi ya makanisa hugawa divai ikiwa kwenye vikombe maalumu kwa kila mtu. Wengine hupitisha kikombe kimoja tu. Kwenye makanisa mengine, kila mtu hutumbukiza kipande chake cha mkate ndani ya kikombe kilicho na divai. Jambo muhimu hapa ni kwamba ushirikishwaji hufanyika katika mpangilio mzuri na kwa heshima.
Maombi: Mchungaji au mtu mwingine yeyote aliyechaguliwa anaweza akaongoza maombi mafupi ya kumshukuru Mungu.
Wimbo: Kikundi kinaweza kuimba wimbo wa pamoja.
Taarifa Saba kwa Muhtasari
1. Meza ya Bwana hutokana na sherehe za Wayahudi za Pasaka.
2. Pasaka iliashiria upatanisho uliotolewa na Kristo.
3. Mkate na divai ni ishara ya mwili na damu ya Yesu.
4. Meza ya Bwana haitoi wokovu wa moja kwa moja kwa mtu anayeishiriki.
5. Meza ya Bwana inaweza ikaleta neema kama mtu ataipokea kwa imani katika upatanisho wa Kristo.
6. Meza ya Bwana haipaswi kushirikishwa kwa watu wenye kutenda dhambi za wazi au wafuasi wa dini nyingine.
7. Mchungaji analo jukumu la kuhakikisha kwamba ushirikishwaji wa Meza ya Bwana unafanyika vizuri.
Kazi za kufanya Somo la 11
1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 11. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.
2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.
3. Masailiano: Fanya mahojiano na waumini watatu kuhusu Meza ya Bwana kwamba inamaanisha nini kwao. Andika muhtasari mfupi kuhusiana na mahojiano hayo.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.