Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 12: Nidhamu ya Kanisa

15 min read

by Stephen Gibson


Utangulizi

Katika Somo la 3, tulijifunza tafsiri hii kuhusiana na kanisa la Mahali au mtaa:

Kanisa la mahali ni kikundi cha waumini ambacho kinafanya kazi kama familia ya kiroho na jamii ya imani; wakitoa injili na ushirika wa kanisa kwa kila mtu anayetubu; wakitekeleza tendo la ubatizo na ushirika wa meza ya Bwana, wakishirikiana katika kumwabudu Mungu, ushirika, uinjilisti, uanafunzi, na kukamilisha kazi ya mwili wa Kristo kwa karama za Roho Mtakatifu; waliojitoa kabisa kwa ajili ya Neno la Mungu; wakiwa na umoja ulio katika msingi wa mafundisho ya imani ya kibiblia, wakiwa na uzoefu wa neema, na maisha ya Roho Mtakatifu.

Sasa tutafakari tafsiri ya nidhamu ya kanisa.

Tafsiri ya Nidhamu ya kanisa

nidhamu ya kanisa ni umoja wa kanisa, wenye lengo la kuwajibisha dhambi inayotendwa na mwanachama kukiwa na makusudi manne ya kulinda um/oja wa kanisa, kusimamia ukweli, kulilinda kusanyiko kutokana na ushawishi mbaya, na kumrejesha tena mwanachama aliyeanguka dhambini kwenye wokovu na ushirika.

► Angalia tafsiri ya kanisa na tafsiri ya nidhamu ya kanisa. Kwa kuzingatia kanisa ni nini, elezea ni kwa nini nidhamu ya kanisa ni muhimu.

Umuhimu wa Nidhamu ya Kanisa

Kunatokea nini wakati mwanachama wa kanisa anaporejea kwenye dhambi, lakini bado anashiriki kuja kwenye kanisa? Itakuwaje kama mwanachama kwa uhakika haamini misingi ya mafundisho ya imani ya kanisa na anafundisha imani potofu? Inakuwaje kama mwanachama amemtendea mtu mwingine mambo yasiyostahili na hayuko tayari kukiri makosa yake?

Baadhi ya makanisa yalikemewa na Yesu kwa sababu yalishindwa kufanya nidhamu ya kanisa. Kanisa la Pergamo lilikuwa na waalimu wenye kufundisha mafundisho ya imani potofu ambayo ilipaswa kuondolewa, lakini haijaondolewa.(Ufunuo 2:14-16). Kanisa la Thiatira lilikuwa na mwanamke ambaye Yesu alimwita Yezebeli, ambaye aliwaongoza watu kufanya uasherati na kuabudu sanamu; kwa hiyo, Bwana akalikemea kanisa (Ufunuo 2:20).

Biblia inatueleza kwamba haiwezekani kuwepo na ushirika kati ya nuru na giza, au kati ya watu wanaomtumikia Kristo na watu wanaotumikia miungu mingine (2 Wakorintho 6:14-15).

Hapa tutaangalia sababu nne zinazofanya nidhamu ya kanisa iwe muhimu sana. Tukiendelea na somo hili, tutaangalia msaada wa kimaandiko kwa ajili ya hizi sababu, lakini tunaziandika hapa kwa muhtasari ili kuzifanya ziwe nyepesi kujifunza.

1. Nidhamu ya kanisa ni muhimu kwa sababu kanisa ni lazima liwe na umoja. Umoja wa kanisa una msingi wake katika mafundisho ya imani ya Biblia na maisha ya Roho. Tafsiri ya kanisa inaonyesha ni kwa jinsi gani wanachama wa kanisa wanapaswa wawe katika ushirika wa kiroho. Ushirika wa kiroho una msingi wake katika uhusiano wao na Mungu na uzoefu wa neema. Kama mtu atakuwa amepoteza uhai wake wa kiroho, hawezi tena akawa na ushirika wa Kikristo. Kama mwanachama atakataa kukubaliana na ukweli, akatubu dhambi, au akakubaliana na makosa, anakuwa hana tena umoja na kanisa.

2. Nidhamu ya kanisa ni muhimu kwa sababu kanisa ni lazima lisimamie ukweli. Kuendelea kumruhusu mwanachama wa kanisa aendelee kutenda dhambi ni kushindwa kusimamia ukweli. Kanisa haliwezi kusimama kwa ajili ya ukweli mbele ya ulimwengu kama wanachama wake wanaishi katika kukiuka ukweli.

[1]3. Nidhamu ya kanisa ni muhimu kwa ajili ya kuzuia watu wa kanisa kutokana na ushawishi mbaya. Kama mwanachama wa kanisa bado anaendelea katika dhambi ya wazi na bado anaendelea kupewa heshima kama Mkristo, wanachama wengine watashawishika kufanya vivyo hivyo.

4. Nidhamu ya kanisa ni muhimu katika kumrejesha tena mwanachama aliyeanguka dhambini. Kama mwanachama wa kanisa anaishi katika dhambi na hakabiliwi kwa matendo yake, kuna uwezekano mdogo sana wa kuweza kutubu. Kama atakabiliwa vilivyo anaweza akakasirika, lakini baadaye atakuwa na uwezekano mkubwa wa kuweza kutubu.

Adhabu siyo sababu ya nidhamu ya kanisa. Adhabu siyo jukumu la kanisa kwa mwanachama wake. Mungu peke yake ana uwezo wa kuadhibu kwa ajili ya dhambi. Kitendo cha kanisa kinapaswa kiwe ni kwa ajili ya kusudi la kurekebisha, na siyo adhabu.

► Je, ni kitu gani kitakachotokea kama kanisa litashindwa kuchukua hatua za nidhamu kwa mwanachama anayetenda dhambi wazi wazi?


[1]

“Serikali ya kanisa la Kristo kwa mapana yake ni tofauti na serikali za kidunia. Inaundwa kwa unyenyekevu na upendo wa kindugu: inatokana na Kristo, kiongozi mkuu wa kanisa, na siku zote huongozwa kwa hekima zake na katika Roho.”

- Adam Clarke,
Christian Theology

Maelekezo kutoka kwa Yesu kuhusu Nidhamu ya kanisa

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Mathayo 18:15-20 kwa ajili ya kikundi.

Yesu alikuwa ametoa maelekezo kwa ajili ya kushughulika na migogoro kati ya waumini wawili. Kama muumini anafikiri kwamba kuna mtu aliyemtendea jambo lililo baya, anapaswa azungumze na huyo mtu kibinafsi. Matatizo mengi yanatatuliwa katika hatua hii. Wakati mwingi kumekuwepo na kutoelewana. Kama waumini wawili ni waaminifu na wanyenyekevu, wanaweza wakatatua tatizo lililoko kati yao.

Uhusiano miongoni mwa waumini ni jambo la thamani sana. Kama mtu anaamini kwamba mtu mwingine amemkosea, uhusiano unakuwa umeharibika. Anapaswa aende kwa huyo mtu aliyemfanyia ubaya kwa unyenyekevu na upole na aonyeshe kwamba uhusiano ni kitu muhimu sana kwake. Anaweza akasema neno kama hili: Ndugu yangu, nathamini baraka ulizonazo katika kanisa. Wewe ni rafiki muhimu. Lakini nina wasiwasi kwa sababu ninahisi ulinifanyia mabaya. Ninazungumza na wewe peke yako katika jambo hili kwa sababu ninataka uhusiano wetu uwe wa kweli.” Elezea hilo jambo ulilofanyiwa ubaya, lakini kuwa mwangalifu usiwe mkali sana au mwenye kulaumu. Kuwa tayari kusikiliza. Kuwa tayari kusamehe.

Kwa mujibu wa maelekezo ya Yesu, kama mtu kiuhalisia ametenda ubaya na hataki kukiri kosa, mtu mwingine atazungumza naye tena akiwa na mtu mmoja au wawili wenye heshima zao. Kwa mara nyingine tena, sisitiza kwa aliyekukosea kwamba yeye anapendwa na kwamba uhusiano ni jambo muhimu.

Kama mtu aliyekukosa ataendelea kukataa kukiri kosa lake, itabidi taarifa zake zipelekwe kwa viongozi wa kanisa. Watatakiwa wazungumze na yeye. Kama bado ataendelea kukataa kusikiliza, kanisa likubaliane kwa pamoja kumwona kama mtu asiyeamini.

Kumwona mtu kama asiyeamini haimaanishi kwamba ni kumtendea ukatili. Inamaanisha kwamba hatakuwa tena mshirika au mwanachama wa kanisa au wa huduma yeyote ya kanisa. Hawezi akashiriki katika Meza ya Bwana kwa sababu anachukuliwa kama ni mtu wa mataifa (aya ya 17). Kanisa litapaswa limjulishe kwamba hawamtambui tena kama mwamini wao na kwamba bado wanamwombea ili aweze kutubu.

Baada ya maelekezo haya yote, Yesu alitoa somo lililohusiana na msamaha (Mathayo 18:21-35). Kama mtu akikiri makosa yake na kutubu, tunapaswa tuwe tayari kusamehe.

► Je, utazungumzaje na mtu ambaye amekukosea wakati unapojaribu kurejesha uhusiano?

Maelekezo kutoka kwa Paulo kuhusu Nidhamu ya Kanisa

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 5 kwa ajili ya kikundi. Je, kuna hali gani ambayo Paulo ameielezea katika sura hii?

Mtume Paulo alitoa maelekezo ya nidhamu ya kanisa kwa ajili ya kadhia maalumu iliyokuwa katika kanisa la Korintho. Mwanachama mmoja katika kanisa alikuwa kwenye uhusiano wa uasherati.

Paulo aliwaambia kwamba Nidhamu ya kanisa siyo kwa ajili ya watu walioko nje ya kanisa, bali kwa wanachama hai wa kanisa (11-12). Kanisa lilikuwa lichukue hatua katika umoja (“mkiwa mmekusanyika pamoja”). Walipaswa wamwondoe huyu mtu kutoka kwenye ushirika wao.

Ikiwa mtu anayeitwa ndugu anafanya dhambi kama wale walioorodheshwa katika mstari wa 11, Wakristo wakatae kabisa kuwa kwenye ushirika pamoja naye. Kusudi ni kuhakikisha kwamba mtu huyo anatambua kuwa yeye siyo Mkristo (hajaokoka) na ni kwa ajili ya dunia itambue kwamba mtu huyu siyo sehemu ya kanisa tena. Hii ni pamoja na kumwondoa katika nafasi yeyote ya uongozi aliyo nayo katika kanisa. Hawezi kushiriki Meza ya Bwana kwa sababu hiyo itamaanisha kwamba yuko karibu sana kwenye ushirika wa Kikristo kuliko hata kushiriki chakula kwa pamoja.

Paulo alikusudia malengo mawili katika kitendo hiki. Lengo moja lilikuwa kanisa liweze kuwa safi (6-7). Haiwezekani kanisa liwe kwenye umoja kama wanachama wake ni watenda dhambi.

Lengo la pili ni kumrejesha mwenye dhambi kwenye wokovu (“roho yake iokolewe”).[1] Kama kanisa litaendelea kumkubali kuwa mwanachama wakati akiendelea kutenda dhambi, atajiona kwamba yuko tu sawasawa hana tatizo na uwezekano wa kutubu hautakuwepo. Uwezekano wa kutubu utakuwepo kama hatua za nidhamu ya kanisa zitatekelezwa.

Hatua hii inaitwa “kumpa Shetani mtu huyo” Kulikuwa na kadhia nyingine ambapo Paulo aliwatoa kwa Shetani waalimu wa uongo wa mafundisho ya imani (1 Timotheo 1:20). Mwenye dhambi anapaswa ajitambue kwamba hayuko chini ya baraka na ulinzi wa Mungu. Kama mtenda dhambi yuko nje ya kanisa na ni mtumwa wa Shetani. Maisha ya dhambi yatamharibu kabisa kama hatataka kutubu.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Tito 3:10-11 kwa ajili ya kikundi.

Kama mtu atakuwa anafundisha mafundisho ya uongo ya imani, kanisa linapaswa lijaribu kumrekebisha angalao mara mbili kuhusu mafundisho hayo. Baada ya hapo, inabidi akataliwe. Biblia inatueleza sisi kwamba mtu kama huyu anakuwa tayari ameshakiuka dhamira yake mwenyewe.

Mafundisho ya imani potofu siyo mambo madogo ya mabadiliko katika mafundisho ya imani. Ni a fundisho potofu la imani linalopingana na misingi ya mafundisho ya msingi ya imani ya Biblia. Tusiwe wepesi kumshutumu mtu kwa mambo ya kusikia. Mtu anaweza akawa mpotoshaji kwenye baadhi ya mafundisho yake ya imani na bado akawa anaendelea kuwa ni mfuasi mwaminifu wa Kristo.

► Angalia katika 2 Wathesalonike 3:6, 14-15. Toa ufafanuzi wa maelekezo yaliyotolewa katika aya hizi.


[1]1 Wakorintho 5:5 NENO: Neno: Bibilia Takatifu 2025

Nidhamu kwa Mchungaji

Mara nyingi wachungaji ni wa kulaumika. Wachungaji mara nyingi wanakuwa kwenye mazingira ambayo wanaweza kushutumiwa kwa uongo. Ni muhimu kwa mchungaji kujenga imani ya watu wake kwa siku zote kuwa mfano mzuri wa kuigwa.

Mashitaka dhidi ya mchungaji hayapaswi kuchukuliwa maanani isipokuwa kuna mashahidi wawili au watatu (1 Timotheo 5:19). Viongozi wa ushirika wa kanisa au dhehebu wana jukumu la kuwafanya wachungaji wawajibike na wanapaswa kuhusika endapo kutahitajika kumchunguza mchungaji au kumuondoa. Wanaweza wakasaidia katika kulifanya kanisa liwe kitu kimoja wakati huduma ya kanisa inapokuwa katika walakini.

► Je, kwa nini dhambi ya mchungaji ni jambo zito sana?

Mchakato wa Urejesho

Tunapaswa tukumbuke kwamba lengo moja la nidhamu ya kanisa ni kumrejesha mwanachama kwenye wokovu na ushirika. Hakuna ulazima wa kanisa wa kuhakikisha kwamba mwanachama aliyetenda dhambi ameadhibiwa vya kutosha. Wakati mwanachama amejitoa kukiri dhambi yake na kutubu, kanisa linapaswa lianze mchakato kwa ajili ya urejesho.

Katika baadhi ya makosa, kama mwanachama amekiri haraka bila kupoteza nafasi makosa yake na kuirekebisha tabia yake, ataweza kuendelea na ushiriki wake katika kanisa. Makosa mengine mazito yameorodheshwa katika 1 Wakorintho 6:9-10, ikiwa ni pamoja na uasherati, wizi, na ulevi. Mwanachama wa kanisa anayetenda uovu katika mojawapo ya dhambi hizi atapaswa aondolewe kwenye uanachama na nafasi yeyote ya uongozi aliyokuwa nayo.

Mchakato wa urejeshaji huanza wakati mwanachama anapotubu dhambi yake. Kwenye shauri la dhambi nzito zaidi, hawezi kwa mara moja akarudishwa kwenye nafasi yake ya uongozi au ushiriki kama uanachama. Wakati mwingine panahitajika mchakato wa urejeshaji ulio mkamilifu:

(1) Kukiri

Mwanachama anapaswa kukiri kosa lake kwa wale aliowajeruhi, kwa wale walioshiriki kutenda kosa pamoja naye, na kwa wale walio na mamlaka ya kiroho juu yake.

(2) Kutengwa

Mahusiano mabaya ni lazima yakomeshwe. Mahusiano ambayo yana ushawishi mbaya ni lazima pia yakomeshwe. Vitu vyote ambavyo vinatumika tu kwa ajili ya kutenda dhambi ni lazima vitupwe. Inawezekana kuna vitu ambavyo vimetumiwa vibaya kusababisha dhambi navyo pia vitahitajika vitupwe. Mwanachama anayehusika anapaswa aonyeshe kwamba hakusudii tena kurejea kwenye dhambi.

(3) Kuwajibika

Hii ni hatua inayochukua muda mrefu. Mwanachama aliyeko katika mchakato wa kurejeshwa anapaswa atoe taarifa mara kwa mara kwa mamlaka ya kiroho ya kanisa, ambayo inaweza ikawa ni mchungaji au baraza la mashemasi. Atapaswa aweze kutoa taarifa ya ushindi dhidi ya majaribu. Atapaswa aonyeshe kwamba yuko makini na mwangalifu katika kutoangukia tena kwenye majaribu.

Uwajibikaji unatakiwa uimarishwe kwa kukutana mara nyingi zaidi na mshauri wa kiroho aliyethibitishwa na mamlaka ya kiroho. Mshauri atakuwa anazungumza na mwanachama mara kwa mara, ikiwezekana kila siku kwa muda. Mshauri atapaswa awe wa jinsia moja na yule anayeshauriwa.

Uwajibikaji utatakiwa uwe angalao miezi kadhaa. Kwenye suala la dhambi ya kimaadili ambayo iliwahusisha wengine, na hasa kama dhambi iliyotendwa iliendelea kwa muda mrefu, uwajibikaji itabidi pia uwe wa muda mrefu zaidi. Kwenye kipindi hiki, mwanachama hataruhusiwa kuongoza au kufundisha kwa njia yeyote ile. Ataruhusiwa kushiriki Meza ya Bwana kama kutubu kwake kumethibitika kwamba kulikuwa ni kweli.

Sababu za kuwepo kwa muda wa uwajibikaji haimaanishi kwamba mwanachama siyo Mkristo. Kama atakuwa ameshatubu, amesamehewa na ameokoka. Muda uliowekwa ni kwa ajili ya kumwezesha kupona kutokana na madhara ya dhambi, kujenga nidhamu thabiti ya kiroho, na kudhihirisha maisha endelevu ya Kikristo.

Biblia inatueleza kwamba mtu hapaswi kuwa kiongozi hadi hapo atakapokuwa na mtazamo wenye sifa njema kwa watu wa nje ya kanisa (1 Timotheo 3:7, 10). Kama mtu atakuwa ameokoka kutokea kwenye maisha ya dhambi ya wazi, dunia inapaswa imwone waziwazi kama Mkristo kwa muda kabla hajaweza kupewa uongozi. Vinginevyo, itaonekana kwamba kanisa linachagua watenda dhambi kuwa viongozi. Kanuni hii inatumika pia kwa mtu ambaye amerejeshwa baada ya kuwa ameanguka katika dhambi.

(4) Kuthibitishwa

Huu ni urejesho mkamilifu. Mwanachama sasa anao uhakikisho wa kanisa na anaweza kushiriki kikamilifu kama mwanachama katika jambo au shughuli yeyote ambayo kanisa litampatia afanye. Muda mrefu unaweza kuwa ni muhimu kwa nafasi za uongozi wa juu, hasa kwenye jukumu la mchungaji.

► Elezea muda wa uwajibikaji. Ni kwa jinsi gani unafanya kazi, na lengo lake ni nini?

Yanayohitajika kwa Unachama wa Kanisa.

Makanisa mengi yana matamko ya mafundisho ya imani ambayo yanapitiliza hata misingi ya mafundisho ya imani ya Ukristo. Maelezo haya ya mafundisho ya imani yanalitofautisha kanisa na makanisa mengine. Makanisa yenye mafundisho ya imani yanayotofautiana wazi yanatambulika kwa majina kama Methodisti, Presbyteriani, Lutherani, Baptisti, au mengineyo. Kwa kawaida tofauti zilizopo katika makanisa siyo mafundisho ya imani potofu, na mtu hapaswi kuitwa mwenye dhambi kwa sababu tu ya tofauti hizo.

Makubaliano kuhusu maelezo ya mafundisho ya imani ni muhimu kwa ajili ya wanachama wa kanisa kuweza kuabudu pamoja na kushirikiana katika huduma. Kwa hiyo, kanisa linaweza kuwataka wanachama wake kuunga mkono tamko lake la mafundisho ya imani. Hawapaswi kusema kwamba mtu ni lazima aamini mafundisho yao ya imani ili aweze kuwa Mkristo, lakini ni ili kuwa katika umoja na hilo kanisa fulani la mahali au mtaa.

Kama mtu hawezi kuamini mafundisho ya imani ya kanisa fulani, kanisa hilo lina haki ya kumkataa kuendelea kuwa mwanachama wake. Kama mwanachama atafundisha au atataka kuingiza mafundisho ya imani yaliyo kinyume na ya kanisa, anaweza akaondolewa uanachama wa kanisa.

[1]Kama mwanachama ataondolewa kwa sababu ya tofauti za mafundisho ya kiimani ambayo siyo ya msingi kwa Ukristo, hiyo haitakuwa sawa na nidhamu ya kanisa kwa sababu ya mafundisho ya uzushi na dhambi ya asili. Kanisa halipaswi kusema kwamba mtu siyo Mkristo kwa sababu tu hajatimiza masharti ya uanachama.

Kama kanisa lina masharti ya uanachama yanayohusisha pamoja na sheria za mavazi, sherehe, au tabia nyingine zozote, mwanachama anaweza kuondolewa kwa kukataa kutimiza masharti hayo. Hii siyo sawa na nidhamu ya kanisa iliyo kwa ajili ya dhambi ya wazi. Kanisa halipaswi kusema kwamba mtu fulani siyo Mkristo kwa sababu tu hayuko tayari kujihusisha na masharti ya uanachama.

► Je, kuna mifano gani ya masharti ya uanachama yameshikiliwa na baadhi ya makanisa lakini hayajashikiliwa na makanisa mengine?


[1]

“Maandiko Matakatifu yana mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya wokovu, ili kwamba chochote ambacho hakitasomwa hapo ndani, au hakiwezi kuthibitika kutokea hapo ndani, hapaswi kuhitajika mwanadamu yeyote kuamini kwamba hicho ni kifungu cha imani au ifikiriwe kwamba kinahitajika au ni muhimu kwa ajili ya wokovu.”

- Kanuni za dini za Kanisa la Uingereza

Uongozi wa Ibada na Ushiriki

Ibada za kuabudu za kusanyiko la kanisa kwa kawaida zinatakiwa ziwe wazi kwa mtu yeyote. Watu wanahitajika waalikwe kuhudhuria.

Kanisa haliwezi kumruhusu mtu mwenye tabia ya kuvuruga aingie humo, kwa mfano mtu ambaye ni mlevi. Kanisa pia haliwezi kuruhusu kuingia mtu aliyevaa mavazi yasiyokuwa na heshima na yaliyovaliwa kwa njia ambayo kwa kweli yanatia au yanaleta aibu. Hata hivyo, ni muhimu kwamba watu wasitengwe kwa sababu ya uvaaji unaotokana na umaskini wao au kwa sababu hawajawa wazoefu na mazingira ya tabia sahihi ya kanisa. Ni janga kubwa wakati watu wanapohisi kwamba hawawezi kuhudhuria kwenye kanisa kwa sababu hawana mavazi mazuri ya kuvaa.

Kama mtu anakuwa ni wa vurugu wakati wa ibada, mchungaji au mtu mwingine yeyote aliyechaguliwa na mchungaji anapaswa kuzungumza naye. Kama atakataa kutoa ushirikiano unaohitajika, asiruhusiwe kuendelea kuwepo kwenye ibada za kanisa.

Wakati mwingine kanisa huruhusu mtu fulani kupiga vyombo vya muziki au kuongoza kuimba ingawaje maisha yake hayana mfano mzuri wa kuigwa. Mtu yeyote anayeongoza kuimba au kupiga vyombo vya muziki mbele ya watu katika kanisa anawakilisha tabia ya kanisa lilivyo. Kama anaishi kwenye dhambi, watu watafikiri kwamba kanisa linamkubali kama Mkristo sahihi, ingawaje anatenda dhambi.

► Je, kanisa linapaswa liwe na mahitaji au masharti ya aina gani kwa ajili ya watu wanaoongoza katika ibada?

Hitilafu za Kuepuka

Kuna Hitilafu tatu ambazo watu wa kanisa ni lazima waziepuke wakati wanaposhughulikia matatizo yanayojitokeza katika kanisa.

(1) Kutowiana

Dhambi zingine huonekana zina uzito zaidi kuliko zingine. Wakati mwingine tofauti huonekana kwa sababu ya mitazamo ya kitamaduni. Kanisa linaweza likawa na tabia ya kushughulikia kwa kumaanisha baadhi ya dhambi lakini likaonesha uvumilivu kwa dhambi zingine. Mungu ameliita kanisa kusimama katika ukweli wa maandiko na siyo tu kwa ajili ya kujali maadili ya utamaduni.

Pia kuna kutowiana katika njia ambazo makanisa yanashughulikia watu mbalimbali kwenye kusanyiko la kanisa. Kama mtu anatoka kwenye familia yenye umashuhuri, viongozi wanaweza wakawa waangalifu zaidi katika njia ambayo wanashughulika na tatizo lake; lakini Biblia inatuonya kwamba tusiwe watu wenye kupendelea watu wengine kwa sababu ya hali au hadhi zao (Yakobo 2:1-9).

(2) Kukosa subira

Wakati mwingine watu katika kanisa hufikiri kwamba tatizo halitatuliwi haraka inavyowezekana. Wanaanza kuongea kuhusu tatizo hilo kwa watu wengine mbalimbali, hata watu walioko nje ya kanisa. Wanakuwa na malalamiko kwamba viongozi wao hawashughuliki na tatizo lililopo. Hali hii inaleta matatizo mengine mapya katika kanisa kwamba inaumiza na kuleta madhara kwenye ushawishi wa kanisa.

(3) Kukosa upendo

Baadhi ya watu hufurahia kutafuta matatizo kwa watu wengine. Ni wepesi kuamini taarifa za matendo ya uovu yaliyofanyika. Wanawahukumu watu wengine kwa haraka, bila ya kutaka kuelewa. Hawana masikitiko au na majuto kwa dhambi za wanachama wa kanisa. Wamejawa furaha kwamba wanazo taarifa mbaya za kwenda kuelezea. Hawana cha kujali wala masikitiko kuhusu madhara ya ushuhuda wa kanisa.

Kila mchungaji na mwalimu wa Neno anapaswa kuzungumza dhidi ya dhambi ya umbea. Anatakiwa awafundishe watu wake kuchukia umbea au udaku na kukataa kuusikiliza.

Kama mtu anampenda Mungu, kanisa, na ndugu zake wa kiume na kike katika Kristo, atapaswa aione dhambi kama janga. Atapaswa awe na imani kwamba taarifa ya dhambi inayotolewa siyo ya kweli. Na kama taarifa ni ya kweli, atapenda kuona aliyetenda dhambi hiyo akirejeshwa tena. Atatakiwa asaidie katika kuzuia madhara yasilipate kanisa. Hatasambaza taarifa za kupitiliza zisizokuwa na umuhimu.

Taarifa Saba kwa Muhtasari

1. Nidhamu ya kanisa ina malengo manne ambayo ni kwa ajili ya kulinda umoja wa kanisa, kusimamia ukweli, kulilinda kusanyiko kutokana na ushawishi mbaya, na kumrejesha tena mwanachama aliyeanguka dhambini kwenye wokovu na ushirika

2. Mwanachama anayetenda dhambi na hataki kutubu hapaswi kutambuliwa kama ni muumini wa kanisa.

3. Kusudi la nidhamu ya kanisa siyo adhabu, bali masahihisho na marejesho.

4. Kanisa halipaswi kumfikiria kila mtu ambaye hakubaliani na mafundisho ya imani yanayotofautiana, na asiyekuwa na sifa ya uanachama kwamba ni mtenda dhambi.

5. Hatua za urejeshaji ni kukiri, kutengwa, kuwajibika na kuthibitishwa.

6. Urejeshaji huchukua muda kwa sababu mwanachama ni lazima apone kutoka katika madhara ya dhambi yake, ajenge nidhamu ya kiroho iliyo na nguvu, na adhihirishe maisha endelevu ya Kikristo.

7. Kanisa ni lazima lijihadhari au lijilinde na kutofuata utaratibu, kukosa subira, na kukosa upendo.

 

Kazi za kufanya Somo la 12

1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 12. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.

2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.

3. Kazi ya Kuandika: Marejeo ya maandiko hapa chini yatapaswa yagawanywe miongoni mwa wanafunzi wa darasa. Kila mwanafunzi atahitajika aandike ibara moja inayoelezea aya yake inatueleza sisi tufanye nini.

  • 1 Timotheo 5:13

  • Tito 2:3

  • Wagalatia 5:15, 26

  • Wagalatia 6:1

  • Wakolosai 3:8-9

  • Wakolosai 3:12-15

  • Wafilipi 4:8

  • Waefeso 4:29-32

Next Lesson