Andiko tunalokwenda kujifunza katika somo hili linahusika mahususi kwa wachungaji na mashemasi, lakini pia kwa viongozi wengine katika kanisa. Mtu yeyote anayefundisha darasa, anayeongoza katika nyumba ya kanisa, au anayeongoza ibada pia ni kiongozi. Watu hao wote ni mfano wa aina ya watu wa kuigwa waliothibitishwa na kanisa. Kwa hiyo, ni muhimu kwamba wawe ni mfano mzuri wa tabia ya Kikristo.
Tabia binafsi ya kiongozi ni muhimu zaidi kuliko hata uwezo wake wa asili alio nao. Mungu humpa kiongozi wa Kikristo uwezo unaohitajika kwa ajili ya huduma.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Timotheo 3:1-7 kwa ajili ya kikundi.
Siyo vibaya kwa mtu kuwa na matamanio ya nafasi ya uchungaji kama anakuwa anayo nia sahihi. Kama atakuwa ni mtu anayetaka apewe heshima na mamlaka au nafasi ya kujipatia faida ya fedha, mtu kama huyu hana moyo wa kichungaji. Anapaswa atamani nafasi ya kuhudumu.
Tuna aya mbili za maandiko kuhusu sifa za wachungaji na mashemasi. Ziliandikwa na mtume Paulo kwa Timotheo na Tito. Timotheo alikuwa kiongozi wa makanisa yaliyokuwepo Efeso; Tito alikuwa kiongozi wa makanisa ya Krete. Walikuwa na kazi ya kuteua wachungaji kwa ajili ya kila kanisa la mtaa.
Jaribu kufikiria ilikuwaje kwa mtu kuwa mchungaji katika karne ya kwanza ya kanisa! Alikuwa hajawahi kuwa na mafunzo ya kitaaluma. Hakukuwa na vitabu kuhusiana na huduma kwa ajili yake ili ajifunze. Hakuwahi kuwa na nafasi ya kuangalia wanavyofanya wachungaji wengine. Hakuwahi kuwa hata na nafasi ya kuangalia maisha ya kanisa kwa muda mrefu kwa sababu kanisa lilikuwa jipya. Hata sehemu kubwa ya Agano Jipya ilikuwa bado kuandikwa.
Paulo alimwambia Timotheo jinsi ya kupata heshima kutoka kwa watu wake. Alimtaka awe kielelezo katika usemi, na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi (1 Timotheo 4:12). Mchungaji hapewi heshima kwa kudai aheshimiwe.
► Je, ni kwa jinsi gani mchungaji hupata heshima?
Mtume aliwaeleza Timotheo na Tito sifa zinazohitajika kwa ajili ya kuwa mchungaji. Sifa nyingi zimerejea kwenye tabia na kukomaa Kikristo kuliko vipaji au uwezo binafsi wa mtu. Kwa hiyo, kila Mkristo anapaswa kutiwa moyo kusitawisha sifa hizo.
Mchungaji hapaswi kuwa mtu anayeonekana na hatia au anayetenda mambo ya uovu. Mchungaji hawezi kumwongoza mtu mwingine afanye jambo sahihi kama yeye mwenyewe hafanyi mambo yaliyo sahihi. Mchungaji ni lazima awe mtu ameonyesha tabia endelevu ya Kikristo kwa kipindi cha muda mrefu. Jambo hili ni muhimu ili kwamba kanisa liweze kumwamini na kuwa na ushuhuda mzuri katika jumuiya.
(2) Mume wa mke mmoja
Katika maeneo mengi ya dunia, ndoa ya wake wengi ni utamaduni wa kawaida. Mpango wa Mungu ni kwa mwanamume kuwa na mke mmoja. Wachungaji wanapaswa waweke mfano huo.
(3) Kuwa Macho
Mchungaji ndiye mlinzi wa kusanyiko lake. Anapaswa awe makini na mafundisho ya dini ya uongo na ushawishi mbaya. Ni lazima awafundishe watu wake ili waweze kuwa salama katika mafundisho yao mbalimbali ya imani. Ni lazima awe tayari kuwaonya watu wake kuhusiana na hatari yeyote ya kiroho.
► Je, itatokea nini kama mchungaji hana habari na hatari za kiroho wanazokutana nazo watu wake?
(4) Anayejitawala
[1]Mchungaji ni lazima awe makini kuhusiana na huduma yake. Hapaswi awe mtu anayelipuka ambaye hufanya maamuzi ya pupa au ya haraka sana. Anapaswa awe na uwezo wa kufikiri akiwa ametulia kuhusu masuala nyeti. Hapaswi kuruhusu akili yake ivurugwe na mambo ya binafsi, starehe, au majaribu.
(5) Anayeheshimika
Mchungaji anapaswa awe na tabia ya utaratibu. Hapaswi kuonyesha tabia ambayo haistahili. Anapaswa ajifunze jinsi ya kuonyesha heshima na unyenyekevu kwa misingi ya tamaduni za mahali ambapo huduma yake ipo.
(6) Mkarimu
Mchungaji anatakiwa awe mtu anayewajibika na mahitaji ya watu wengine. Anapaswa awe tayari kushirikishana katika mambo ya ukarimu. Anapaswa awe rafiki na mwenye msaada kwa watu hata kwa watu ambao anakutana nao kwa mara ya kwanza.
(7) Ajuaye kufundisha
Mchungaji ni lazima awe na uwezo wa kuelezea ukweli ili watu waweze kuulewa. Ni lazima achukue jukumu la kusoma na kujielimisha yeye mwenyewe.
(8) Asiwe mlevi
Mchungaji asiruhusu yeye mwenyewe kushawishiwa na vinywaji vya kulevya. Hapaswi kamwe kufanya kama mtu ambaye ana uraibu na ulevi. Kanuni hii inahusiana na kitu kingine chochote ambacho kina madhara yanayofanana.
(9) Asiwe mgomvi bali awe mpole
Mchungaji asitake kupeleka suala kwa njia vitisho vya kutumia nguvu. Hapaswi kuwa tayari kumwumiza mtu yeyote anayemuudhi au anayemkosea. Ona pia 2 Timotheo 2:24-25.
► Je, ni njia zipi sahihi kwa mchungaji za kuweza kuonyesha aina sahihi ya hasira au ghadhabu anayoweza kuwa nayo?
(10) Asiwe na tamaa wala mpenda fedha
Watu wa dunia hii hubadili wayasemayo ili kupata faida. Watu kwenye nafasi zao mbalimbali kama wanasheria, wafanyabiashara, au wanasiasa wanajaribiwa kuubadili ukweli kwa ajili ya kuwafurahisha watu. Mchungaji pia hujaribiwa, kwa sababu ukweli wa Neno la Mungu haumfurahishi kila mtu. Mchungaji ni lazima awe mwaminifu kwenye ukweli aidha kama unamfaidisha kifedha au la.
Mchungaji atapenda kuona huduma ya kanisa ikiwezeshwa kifedha. Ni lazima aongoze kanisa kufanya kazi kama familia inayojali kwa ajili ya wanachama wake, kuliko kila siku kufikiria ni nini watakachoweza kumpa.
(11) Aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri
[2]Uwezo wa mchungaji wa uongozi ni lazima uthibitike kuanzia nyumbani. Atapaswa awe na uongozi kwa watoto wake. Kama hawezi kuiongoza nyumba yake mwenyewe, hatakuwa na uwezo wa kuliongoza kanisa. Hii haijumuishi watoto ambao wameshakuwa watu wazima wanaojitegemeza wenyewe na ambao hawako kwenye mamlaka yake kwa sababu bado hawawajibiki kwa ajili yao tena.
(12) Asiwe mtu aliyeokoka karibuni.
Kama mtu atawekwa kwenye nafasi ya mamlaka kwa haraka sana, ni rahisi kushawishika kuwa na kiburi. Kiburi ndiyo dhambi iliyomsababisha Shetani kuanguka. Upandishwaji kwenye ngazi nyingine ya mamlaka unapaswa ufanyike polepole ukiambatana na uzoefu.
► Je, kunakuwa na uharibifu gani kama atawekwa kwenye mamlaka kwa haraka na akawa hafanyi vizuri?
(13) Awe na sifa njema
Kabla mtu hajateuliwa kuwa mchungaji, ni lazima awe mtu mwenye sifa njema miongoni wa watu nje ya kanisa. Wanapaswa waelewe kwamba ni mtu wa ukweli na mwaminifu katika yote ayafanyayo. Kama atakuwa ni mtu ambaye hakuwa na sifa nzuri kabla ya kuokoka, patahitajika awe na muda maalumu wa kutengeneza sifa zake kabla hajafanyika kuwa mchungaji.
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Tito 1:5-11 kwa ajili ya kikundi.
Sifa nyingi za mchungaji zilizoorodheshwa katika Tito pia zimeorodheshwa kwenye kifungu cha kuanzia 1 Timotheo.
► Je, kuna sifa gani nyingine za ziada za mchungaji zilizoko kwenye kifungu kilichoko katika Tito?
Kifungu kinasisitiza juu ya uwezo wa mchungaji kudhibiti mafundisho potofu ya imani. Mchungaji ni lazima awe ameelimishwa vizuri na kwa upeo mkubwa kuhusu mafundisho ya imani ya kweli na awe na uwezo wa kuyaelezea kwa ushawishi mkubwa. Lengo ni kuwasahihisha wale walioko kwenye mafundisho ya imani potofu, na jambo lililo muhimu zaidi ya hapo, ni kulilinda kusanyiko katika kuingizwa kwenye upotofu.
“Kuhubiri injili, pamoja na uangalizi wa kichungaji ambao unahusiana na ofisi ya huduma, ni njia ya kiungu iliyowekwa kwa ajili ya kuwabadilisha wenye dhambi na ujenzi wa maadili wa kiroho wa waumini. Kwa hiyo ni sababu kuu muhimu kwamba Mungu anahitaji kufanya uteuzi wa maajenti wake mwenyewe, na hasa kuwaita kwenye huduma yake.”
“Mwenyezi Mungu, Baba yetu wa mbinguni, ambaye amekupa wewe mapenzi mema ya kufanya mambo haya yote, akupe pia nguvu na uwezo wa kutimiza mambo yote; na kwamba akamilishe ndani yako kazi njema ambayo ameianza, na kwamba uweze kupatikana mkamilifu na usiyelaumika katika wakati ujao, kupitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Amen.”
- “Kusimikwa kwa Maaskofu,” Kitabu cha Sala ya jumuiya
(Book of Common Prayer)
Sifa za Mashemasi
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Matendo 6:1-6 kwa ajili ya kikundi. Je, kuna tatizo gani lililoelezwa kwenye kifungu hiki?
Mashemasi wa mwanzo waliochaguliwa mara tu baada ya Pentekoste. Mitume walihitaji kuwa na fokasi yao kwenye maombi na kuhubiri. Watu wapatao saba waliteuliwa katika mambo ya kulisimamia kanisa. Shemasi humsaidia mchungaji katika mambo yote yanayohusiana na huduma ya kanisa. Shemasi anaweza akawa ni mhubiri, lakini pia siyo lazima.
► Je, sifa za mashemasi wa mwanzo zilikuwa ni nini?
Sifa za mashemasi wa mwanzo zilikuwa kwamba walikuwa na sifa ya kuwa watu wa ukweli na waliojazwa na Roho Mtakatifu na hekima. Wangekuwa wanasimamia pesa kwa ajili ya kanisa, kwa hiyo sifa ya kuwa mkweli ilikuwa muhimu. Kazi zao zilikuwa na matokeo ya kiroho katika kanisa, kwa hiyo ilikuwa ni muhimu kwao kuwa watu waliokuwa wamejazwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kupata uongozi wake, kupokea upako, na usafi. Walishughulika na hali nyingi zilizokuwa ngumu, kwa hiyo hekima ilikuwa jambo la muhimu.
Mtume Paulo aliorodhesha baadhi ya sifa kwa ajili ya mashemasi:
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Timotheo 3:8-13 kwa ajili ya kikundi.
(1) Anayeheshimika
Shemasi anapaswa awe mtu ambaye anaheshimika kwenye mahusiano yake na familia, marafiki, na jumuiya.
(2) Mkweli na mnyofu
Shemasi anapaswa awe mtu ambaye anaaminika katika yale anayosema. Atasikia malalamiko kuhusu watu ndani ya kanisa na atasikia maoni mengi sana kuhusu matatizo ndani ya kanisa. Anapaswa awe mtu ambaye ni mkweli.
(3) Asiye mlevi
Shemasi hapaswi awe mtu ambaye amedhurika na ulevi. Tabia yake inabidi iwe ya kuheshimika na iliyo thabiti.
(4) Asiye na tamaa
Shemasi atawajibika kutunza fedha kwa ajili ya kanisa na kujali mahitaji ya watu walioko ndani ya kanisa. Hapaswi awe mtu ambaye anajaribu kujipatia faida yeye mwenyewe kutoka katika huduma yake.
(5) Anayeshika imani kwa dhamira safi
Wakati mtu anapoanguka katika dhambi, mara nyingi huanza kuamini mafundisho potofu ya imani. Kama mtu anaishi kwenye ushindi wa kiroho, atakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushikamana na mafundisho ya kweli ya imani.
(6) Apimwe kwanza uwezo wake au uzoefu wake
Kabla mtu hajapewa nafasi ya kuwa Shemasi, anapaswa awe na nafasi ya kuonyesha kwamba ana hekima na ni mwaminifu katika huduma. Viongozi wenye hekima watawapa watu wao nafasi za kutumika kabla ya kuwapa nafasi za mamlaka.
► Je, kuna mifano gani ya njia ambazo mtu anaweza kusaidia huduma ya kanisa bila ya kuwa amepewa nafasi ya mamlaka?
(7) Awe na mke mwaminifu.
Huduma ya Shemasi inapata madhara kama mke wake atakuwa ni mtu wa uvumi na siyo mfano wa Mkristo mwema.
(8) Awezaye kusimamia nyumba yake vyema
Kama ilivyo kwa mchungaji, Shemasi anapaswa aweze kuimiliki familia yake vyema.
Kipaumbele cha Kikundi kinachojituma.
Kanisa ni kikundi cha watu walioamini ambao wameweka msimamo wao kwa Mungu na kila mtu na mwenzake, wakijipanga kwa ajili ya kusudi la kukamilisha kazi ya umisheni ya kanisa la mtaa. Kazi na rasilimali za kufanya huduma iendelee hutoka katika kikundi hicho. Pasipokuwepo na kikundi hicho, kanisa halipo.
Mgeni ambaye anaingia katika eneo la biashara ni muhimu kwa sababu anaweza kuwa mteja. Vivyo hivyo, mgeni yeyote anayeingia kwenye kanisa ni muhimu kwa siku zijazo, anaweza kuwa sehemu ya kikundi kinachojituma. Mtu muhimu sana kwenye biashara ni yule mteja wa kila siku. Mtu muhimu sana kwenye kanisa ni yule ambaye anajitoa kwa kanisa.
Kwa hiyo, nafasi za wafanyakazi katika kanisa zinapaswa kutumikia kikundi kilichojitolea. Kila mchungaji na mwalimu atakuwa na kusudi la kuwatumikia wanachama wa kikundi na kuwavutia watu wengine wengi wajiunge nacho. Kikundi hukua katika idadi wakati watu wanapokuwa wanaokoka na wamejituma kwa kanisa, au wakati ambao watu waliokwishaokoka wanapojitambua kwamba wanahitaji wajiunge na kikundi hicho. Wafanyakazi wa kanisa watapaswa wajifunze mahitaji ya wanachama wa kikundi na kufanya uanafunzi au ufuasi, mwelekeo wa kiroho, mafunzo ya huduma, na aina nyingine zote kwa ajili ya ushirika. Watapaswa wakiongoze kikundi katika kufanya kazi kwa pamoja ili kukidhi mahitaji yote ya wale walioko kwenye kikundi.
Kama familia ya watu wenye imani, kanisa wanatumia rasilimali watu na kupata rasilimali za Mungu vya kukidhi mahitaji ya kila aina kwa ajili ya wale walioko kwenye ushirika, wakidhihirisha kwa ulimwengu hekima ya Mungu katika kila kipengele cha maisha na kuwakaribisha watu ambao hawajaokoka ili waokoke na kuingia kwenye familia.
► Je, itaonekanaje kwa viongozi wa kanisa kuwa na kipaumbele cha kukuza kundi la waumini ambalo linajitoa kwa kwa kila mmoja?
Kipaumbele cha Kiroho cha Kanisa.
Ingawaje masuala ya kifedha ni muhimu kwa ajili ya kanisa (kwa ajili ya uwezeshaji wa shughuli za kichungaji, uangalizi wa kusanyiko, na shughuli nyingine za huduma za ndani), kanisa linapaswa kimsingi kulenga kwenye vipaumbele vya kiroho vya uinjilisti na kuwafanya watu kuwa wanafunzi au wafuasi. Kimsingi mchungaji anapaswa awe ndiye kiongozi wa kiroho. Hii ina maana kwamba mchungaji asibebe mzigo mzito kupita kiasi wa kufanya biashara. Jambo lililo bora ni kwa wanachama wa kanisa kuwa wafanyakazi au biashara ambako wataweza kutoa zaka. Kwa biashara zinazoendeshwa na kanisa, mashemasi waaminifu wanaokubalika watapaswa wachukue jukumu kubwa la kuwajibika katika biashara hiyo. Mashemasi wa mwanzo waliteuliwa ili mitume waweze kutumia muda wao mwingi kwenye maombi na kwa ajili ya huduma ya Neno (Matendo 6:2-4).
Sifa za Mchungaji Anayeliongoza Kanisa Vizuri
► Jadili umuhimu wa kila sifa, ukianzia na swali, “Je, kwa nini sifa hii ni muhimu?”
1. Uaminifu wake haujagawanyika kwa mashirika mengine.
2. Yuko tayari kujenga timu ya huduma na kutumia uwezo na vipaji vya watu wengine.
3. Anaongoza kusanyiko lake kushirikishana maisha kama familia ya kiroho, inayowajibika na mahitaji yote.
4. Analihudumia kanisa lake kwa upendo kwa ajili ya Mungu na watu, na siyo kwa ajili ya faida binafsi.
5. Vipaumbele vya kiroho kama vile ibada, uinjilisti, na kukua kiroho ni lengo la huduma yake.
6. Watu wake wanamwamini na kuwa na uhakika naye.
7. Yuko tayari kulijenga kanisa kama taasisi ya kudumu ambayo siyo mali yake
8. Analiongoza kanisa katika kukua, akifundisha kuhusu zaka na ushirika wenye kujali mahitaji ya wengine.
9. Ni mkweli katika mambo yote, ikiwa ni pamoja na matumizi ya fedha.
10. Anaonyesha uwezo wa kumiliki fedha pamoja na watendakazi.
Sifa za Kiongozi wa Mradi wa Huduma
Mtu anayechaguliwa kuongoza mradi wa biashara wa kanisa anapaswa awe na sifa hizi. Viongozi wa kanisa wanapaswa wafanye kazi ya kukuza sifa hizi kwa wanachama wake ambao wataweza kusaidia katika jukumu la kanisa na waingizwe kwenye timu ya viongozi.
► Jadili umuhimu wa kila sifa, ukianzia na swali, “Je, kwa nini sifa hii ni muhimu?”
1. Ni mwaminifu kwa kanisa la mtaa kwa mahudhurio yake, hutoa zaka, anashiriki na anao ushuhuda wa Kikristo unaoaminika.
2. Tayari anakuwa amewekeza juhudi zake na shauku yake katika kanisa la mtaa.
3. Anao uaminifu wa kutosha na hisia ya hali ya juu ya maadili.
4. Tayari anakuwa ameshaonyesha uwezo wa kuanzisha mambo na motisha wa kufanya vizuri kwa kadri inavyowezekana.
5. Binafsi ni mtu mwenye nidhamu, amehamasika, na siku zote akiendelea kuwa mzuri zaidi.
6. Anadhihirisha uwezo wake na kipaji cha kupanga na kuwaongoza watu wengine, siyo tu uwezo wa kufanya kazi wakati anapoelekezwa na mtu mwingine.
7. Anao uzoefu wa kutosha wa kutekeleza jukumu lake linalomhusu katika huo mradi.
Taarifa Saba kwa Muhtasari
1. Tabia binafsi ya kiongozi ni muhimu zaidi kuliko hata uwezo wake wa asili aliyo nao.
2. Mtu anapaswa aoneshe sifa za Ukristo kwa kipindi cha muda fulani kabla ya kuwa kiongozi.
3. Mtu aliye na majukumu katika kanisa ni mfano wa tabia kwa ajili ya kanisa.
4. Usimamizi wa fedha za kanisa ni muhimu kwa ajili ya kanisa, kumwezesha mchungaji, kuwasaidia wahitaji kwenye kusanyiko, na kusaidia huduma nyingine za ndani.
5. Kanisa kimsingi linapaswa kulenga kwenye vipaumbele vya uinjilisti na kufanya uanafunzi au ufuasi.
6. Viongozi katika kanisa wanapaswa kulenga katika kuendeleza kikundi cha watu ambao wamemaanisha na wamejitoa kabisa kwa ajili ya kanisa.
7. Kanisa ni lazima liwe imara kama taasisi ya kudumu ambayo ni mali ya kusanyiko.
Kazi za kufanya Somo la 13
1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 13. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.
2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.
3. Kazi ya Kuandika: Tafakari Ezekieli 34:1-10 kisha andika sentensi chache ambazo zinatoa muhtasari wa ujumbe wa kifungu hiki.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.