Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 5: Uanachama wa Kanisa

16 min read

by Stephen Gibson


Utangulizi

► Je, mtu anaweza akawa Mkristo na akaishi maisha ya Ukristo bila ya kuwa na kanisa?

[1]Kuna sababu nyingi ambazo watu wanaweza wakawa nazo kwa ajili ya kuja kanisani. Mtu anaweza kuja kanisani kwa ajili ya kujifunza, kuuhisi uwepo wa Mungu, kupata kibali cha kukubalika na urafiki, kutiwa moyo, kubadilishwa, kumwabudu Mungu pamoja na washirika wengine, kudhihirisha kujikabidhi kabisa kwa Mungu na watu wake, kusaidia katika huduma za kanisa, na kutaka kuona kwamba ni kitu gani Mungu atatenda.

Kama mtu atakuwa haingii kwenye kanisa, mambo yaliyoorodheshwa hapa juu hayana umuhimu kwake. Atakuwa ni mtu wa aina gani asiyejali mambo hayo? Kuwepo katika kanisa siyo uthibitisho kwamba mtu ni Mkristo, lakini kama mtu hahudhurii katika kanisa, inawezekana akawa siyo Mkristo

► Je, kwa nini uanachama wa kanisa ni jambo la kujali sana? Je, haitoshi tu mtu kwenda kanisani na akafanyika kuwa Mkristo?


[1]

“Wale watu wa mwanzo walioamini walilipenda kanisa kwa sababu walimpenda Yesu.”
- Larry Smith, I Believe: Fundamentals of the Christian Faith

Uanachama wa Kanisa ni Uwajibikaji kwa ajili ya Mpango wa Mungu

Kwenye somo lililopita, tuliona kwamba huduma ya Paulo ilikuwa ni mahsusi ya kuelezea kuhusu kanisa. Paulo aliweka msisitizo wa kanisa kwa sababu ni njia ya Mungu ya kutekeleza mpango wake wa wokovu kwa dunia nzima.

Mtume Paulo alikuwa ameitwa:

na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu… ili sasa… kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane… (Waefeso 3:9-10).

“Siri” ni mpango wa Mungu wa kuelezea ukamilikaji wake wote na kuifunua hekima yake katika kanisa. Kanisa na ushirika wa watu ambao wamekubaliana na mpango wa Mungu na ambao wao wenyewe wamejikabidhi kabisa kwenye mpango wa Mungu. Kama mtu atakuwa hajaingia kwenye kanisa, mtu huyo hajajikabidhi kwenye mpango wa Mungu.

► Je, kuna sababu gani walizo nazo watu za kukataa kuwa na msimamo au kujikabidhi katika uanachama wa kanisa?

Nyumba ya kweli ya Mungu

Mungu huishi ndani ya kila mtu aliyeamini, lakini huishi ndani ya kanisa (kundi la watu waliojikabidhi kabisa) kwa njia ya pekee. Angalia mahali ambapo aya hizi zinasema kwamba Mungu huishi:

Katika yeye [Yesu Kristo] jengo lote linaungamanishwa vyema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho (Waefeso 2:21-22).

Mungu huishi ndani ya kanisa. Kanisa, ambalo ni kundi la waumini, ni nyumba ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa Roho.[1] Makao ya Mungu katika kanisa ni kwa makusudi zaidi ya yale yanayoweza kutimizwa na watu binafsi. Ikiwa mtu anakataa kujitoa kwa kanisa, anakataa kuwa sehemu ya mpango huu wa Mungu.


[1]Katika 1 Wakorintho 6:19, mwili wa mwamini binafsi unaitwa hekalu la Roho Mtakatifu; kwa hiyo si vibaya kufikiria watu mmoja-mmoja kuwa makao ya Mungu. Mahali pengine katika waraka huo huo, mwili wa mahali unarejelewa kwa pamoja kama hekalu la Mungu (1 Wakorintho 3:16-17).

Familia ya Mungu

Mtu hupata utambulisho wake wa kiroho anapohukumiwa na dhambi, kisha hupata upendo, neema na kukubalika kwa Mungu. Anapotubu na kuweka imani yake kwa Kristo, anakuwa mtoto wa Mungu. Hiki ndicho kitambulisho muhimu zaidi ambacho mtu anaweza kuwa nacho.

Muumini pia ana utambulisho wa kiroho kama mshiriki wa familia ya Mungu (Waefeso 2:19). Waamini wengine ni ndugu na dada zake wa kiroho. Anahisi udugu na mkristo yeyote wa kweli ambaye anakutana naye.

Kanisa lipo kama familia ya Mungu ulimwenguni na pia kusanyiko la mahali pamoja katika mtaa ambalo linafanya kazi kama familia ya Mungu ya mtaa. Kama kaka au dada anakuwa na hitaji lake, ni familia yake ya kiroho ya mtaa inayomsaidia. Kama na ambavyo mtu aliyeamini anaweza akategemea familia yake ya kiroho iwe tayari kumpa msaada, anapaswa ajikabidhi kabisa kwenye familia hiyo na pia awe tayari kusaidia wengine. Msaada unaotoka katika familia hautaweza kuwepo kama hakungewepo na waumini ambao wamejikabidhi kabisa kwa muda wao na mali zao katika hilo.

Baadhi ya watu huomba msaada lakini hawapatikani katika kuwasaidia watu wengine. Hawaelewi ni nini maana ya kujikabidhi kabisa kwenye familia.

Watu wengine hujitazama au hujitunza wenyewe tu wakitegemea kwamba na watu wengine watafanya vivyo hivyo. Hawaelewi wajibu wao katika kukidhi vigezo ya watu wengine.

► Je, ni kwa jinsi gani unaweza kumwelezea mtu kwamba anapaswa ajikabidhi kabisa kwenye familia ya Mungu?

Kosa la Ubinafsi

Mtu anapaswa kwa binafsi yake mwenyewe awe anaamini ukweli wa Mungu na kwa binafsi yake mwenyewe aweze kumtii Mungu. Uhusiano wa mtu na Mungu huanza wakati anatubu na kuweka imani yake katika Kristo. Uhusiano binafsi wa mtu na Mungu haumtegemei mtu yeyote. Kila mtu aliyeamini anaye Roho Mtakatifu wa kumwongoza katika kulielewa Neno la Mungu.

Hata hivyo, Wakristo wengi wamegeuka kuwa watu wa kipekee kabisa katika tabia zao. Mitazamo yao ya kibinafsi inakuwa ndiyo uamuzi wao wa mwisho. Wanaamini tu tafsiri zao binafsi walizo nazo za Maandiko. Wanatafuta kusudi la kibinafsi kwa ajili ya maisha yao ambayo yataheshimu karama zao wenyewe, kuliko kutafuta ukamilifu kwa kutumia karama hizo zilizoko katika mwili wao. Maamuzi yao muhimu yameegemea kwenye maoni yao wenyewe, hisia zao wenyewe, na hayaongozwi na hekima za kanisa.

Watu wengi hawawezi kuelezea kusudi la kanisa. Wanaliona kanisa kama lenye manufaa tu ya kutoa faida kwa watu wachache. Hawajikabhi kabisa kama familia. Hawakubaliani na mamlaka yeyote ya kiroho. Ni wepesi kujitoa kwenye kanisa na kutafuta lingine kama kukatokea kuwepo na tatizo. Tatizo hili liko kila mahali, lakini watu kwenye baadhi ya tamaduni wana tabia ya kujitahidi kuishi maisha binafsi ya kiroho kwa sababu tamaduni zao zinasisitiza uhuru wa mtu binafsi (individualism).

Makanisa mengi wamekubaliana na dhana kwamba watu wako huru kiroho. Mahubiri yao hutoa maelekezo ya jinsi watu watakavyoweza kufanya maamuzi binafsi katika kupata matokeo yaliyo mazuri zaidi. Makanisa mengi yanaongozwa na timu ya watu ambao wanatengeneza programu, na makusanyiko yanakuwa ni makundi ya watazamaji tu. Aina nyingine ya kanisa ni kampuni binafsi ya mchungaji, anajaribu kutoa faida za kutosha kuweka watu na kukusanya msaada wao wa kifedha.

Maelezo ya Agano Jipya kuhusiana na kanisa ni kusanyiko la mahali pamoja la mahali ambalo hushirikishana majukumu. Haiwezekani kwa kanisa kukamilisha majukumu yake bila ya kuwepo na kusanyiko lililojikabidhi kabisa na lenye watu wanaoshirikiana. Takribani nyaraka zote za Agano Jipya hazijaelekezwa kwa watu binafsi, bali kwa makanisa, na zinapaswa zitafsiriwe na zitumike kwa njia hiyo.

Baadhi ya Malengo ya Kanisa la mahali/Mtaa Yanayoonekana kwenye Agano Jipya

► Kwenye kila kipengele kilichoko katika orodha hii hapa chini, elezea ni kwa jinsi gani kusanyiko la pamoja la kanisa litaweza kushirikishana jukumu hili na kufanya vizuri zaidi kuliko ambavyo ingefanywa na mtu binafsi.

1. Kufanya Uinjilisti (Mathayo 28:18-20).

2. Kuabudu kama kusanyiko (1 Wakorintho 3:16).

3. Kudumisha fundisho la imani (1 Timotheo 3:15, Yuda 3).

4. Kutoa msaada wa kifedha kwa wachungaji (1 Timotheo 5:17-18).

5. Kutuma na kuwapa msaada wamisionari (Matendo 13:2-4, Warumi 15:24).

6. Kuwasaidia washirika wa kanisa walio wahitaji (1 Timotheo 5:3).

7. Kuwaweka katika nidhamu wale wanaoanguka katika dhambi (1 Wakorintho 5:9-13).

8. Kufanya ubatizo na kushirikisha Meza ya Bwana (Mathayo 28:19, 1 Wakorintho 11:23-26).

[1]9. Kuwakamilisha kwenye uanafunzi waumini hadi wafikie kwenye utimilifu (Waefeso 4:12-13).

Mambo mengi yaliyoko hapa hayawezi kufanywa na mtu mmoja anayejinasibu kufanya akiwa mwenyewe. Mambo haya yanategemea ushirikiano wa kikundi cha waumini na muundo wa uongozi.

Mungu humwita kila mtu aliyeamini kuingia kwenye kanisa la mtaa na kulisaidia kanisa hilo kutimiza malengo yake hapa duniani. Endapo mshirika atakuwa hatumiki ndani ya kanisa, atakuwa hatimizi kusudi la Mungu kama mshirika wa mwili wa Kristo

Mungu anao mpango kwa ajili ya kundi la mtaa la watu walioamini. Anatoa kile kinachohitajika na anahitaji msimamo kutoka kwa mshirika.


[1]

“Ni wajibu wa kila Mkristo siyo tu kukiri kwa uwazi imani yake iliyo katika Kristo, bali kuingia kwenye ushirika wa kundi la watu walioamini katika jumuiya yake, na kubeba yeye mwenyewe majukumu ya kuwa mwanachama wa kanisa.”

- Wiley & Culbertson,
Introduction to Christian Theology

Mfano wa Mwili

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:12-27 kwa ajili ya kikundi.

Paulo alisema kwamba washirika wa kanisa wanapaswa wafanye kazi pamoja kama viungo vya mwili wa kawaida. Kiungo hakipaswi kijaribu kujiondoa chenyewe kutoka katika viungo vingine. Kiungo kimoja hakiwezi kukamilisha mambo bila ya kutegemea viungo vingine.

Mkristo anapaswa atambue kwamba vipawa vyake vinapata thamani yake kwenye maisha ya kanisa. Kama vile ambavyo jicho au sikio lisivyokuwa na manufaa hadi pale linapokuwa linafanya kazi kwa ajili ya mwili, vile vile kuna uwezekano wa mtu kutokuona kusudi muhimu kwenye mapenzi ya Mungu hadi pale atakapowajibika kama mshirika wa kanisa mwenye msimamo kabisa.

Mchakato wa Uanachama

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Matendo 2:46-47 kwa ajili ya kikundi.

“Bwana akalizidisha kanisa kila siku.” Kujiunga na kanisa halikuwa jambo lililokuwa gumu kwenye siku za mwanzo za kanisa. Ushuhuda kuhusiana na kuokoka na imani ndio uliokuwa msingi wa uanachama. Hata bila ya utaratibu wa kawaida wa mchakato wa uanachama au orodha ya masharti ya uanachama, ilikuwa rahisi kumwona ni nani aliyekuwepo ndani ya kanisa.

Mara nyingi kanisa huanza bila ya kuwepo kwa utaratibu wa uanachama. Mwanzoni kanisa linakuwa na timu ya uinjilisti. Kisha, watu wa mtaa ambao wamekubaliana na huduma hujiunga na kuwa wahusika. Kikundi hukutana mara kwa mara kwa ajili ya majadiliano kuhusiana na mambo ya vitendo ya kufanya, mambo ya kiroho, maono kwa ajili ya wakati ujao, na vipengele vya kushirikishana maisha pamoja. Hakuna orodha ya uanachama, lakini kila mtu anatambua kwamba ni watu gani wenye msimamo au waliojikabidhi kabisa.

Kwa kadri kanisa linavyoendelea kukua, maswali huanza kujitokeza. Watu wengi hulitembelea kanisa na kushiriki katika shughuli zake; lakini ni watu gani halisi walio wa kanisa? Kanisa linapaswa liwe ni shahidi, lakini litakuwaje shahidi kama jamii iliyopo haijui ni nani mshirika halisi wa kanisa? Tunafundisha kusanyiko kujikabidhi kabisa katika kuwasaidia watu wengine walioko kwenye kundi hilo, lakini watajuaje ni nani walioko? Kama mtu atakataa kupokea marekebisho ya maisha yake na akaendelea kuishi maisha ya dhambi hadharani, anawezaje kutofautishwa kutoka kwenye kundi la waumini waliojikabidhi kuwa na msimamo kabisa wa kuishi maisha ya uaminifu?

Makanisa mengi ya wakati wa sasa yana vigezo vingi vinavyohusiana na uanachama wa mtu. Wana tamko la mafundisho ya imani, masharti yanayohusiana na maisha ya mshirika, na kipindi cha katika matazamio. Siyo rahisi kwa mtu mpya aliyeokoka kwa haraka kuwa mshirika wa makanisa hayo.

Mtu mpya aliyeokoka anastahili akubalike mara moja kwenye ushirika wa kanisa. Anahitajika awe ni sehemu ya kundi la waumini ambao wamemaanisha na kujikabidhi kabisa kwa ajili ya wengine. Huwa anapoteza marafiki ambao siyo Wakristo anapokuwa ameokoka, na kwa ajili hiyo anahitaji ushirika wa Kikristo.

Mtu mpya aliyeokoka pia anahitaji afundishwe uanafunzi unaotokana na ushirika wa karibu na Wakristo wengine. Atabadilishwa kutokana na thamani ya watu waliopo ambao hushirikishana maisha yao pamoja naye.

Inakuwaje kama mtu aliyeokoka hawezi kujiunga na kanisa kwa sababu ya masharti mazito ya uanachama ambayo hawezi akayaelewa? Kama atakuwa hashirikishwi kwenye uanachama, anajihisi kwamba hakubaliki ndani ya kanisa. Anahitajika apate aina fulani ya uanachama haraka kadri itakavyowezekana. Kanisa la kwanza liliweza kuwahusisha waongofu kama washiriki haraka.

Uanachama wa Ujumla wa Kanisa/Uanachama wa Ushirika

Kanisa litakuwa linafanya vyema katika kuwafanya watu wapya waliookoka kuwa washirika haraka, hivyo uanachama wa kanisa utawajumuisha pia Wakristo ambao hawajakomaa. Watu wapya wanaookoka hawana ufahamu wote kuhusiana na mafundisho ya imani yaliyo muhimu kwa kanisa. Wanakuwa bado hawajakuza mfumo wa maisha ya Mkristo aliyekomaa. Kwa hiyo, hawapaswi kuwajibika katika kufanya maamuzi kwa ajili ya kanisa. Kwa kuwa uanachama wa kanisa unahusisha pia watu ambao siyo Wakristo waliokomaa, uanachama wa ujumla wa kanisa haupaswi kufanya maamuzi yanayohusiana na mwelekeo wa kanisa.

Ndani ya uanachama wa jumla kunapaswa kuwepo na washirika ambao wanakuwa ni sehemu ya baraza la uongozi. Baraza la uongozi la kanisa linapaswa liundwe na Wakristo waliokomaa ambao wanaelewa mafundisho ya imani na mfumo wa maisha unaofundishwa na kanisa. Hili ni kundi ambalo linafanya maamuzi kwa ajili ya kanisa. Uanachama katika kundi hili unahitajika uwe wa vigezo vya sifa za juu kuliko ulivyo uanachama wa jumla wa kanisa. Kutoka katika kundi hili, washirika wanaweza kutumika kama waalimu na viongozi ndani ya kanisa. Baraza la uongozi linahakikisha kwamba kanisa linabaki kuwa la kweli kwenye mafundisho yake ya imani pamoja na malengo yake.

Uanachama wa jumla unawakubali watu wapya waliookoka walio na msimamo wa kujikabidhi kabisa kwa kanisa. Vigezo vilivyopo kwa ajili ya uanachama wa jumla ndiyo mambo ya msingi ya Ukristo na msimamo wa kujikabidhi kabisa kwenye hilo kanisa. Mtu aliyeokoka anaweza kukubaliwa haraka kuingia kwenye uanachama wa jumla endapo ataonekana kwamba kwa ukweli ameokoka. Mtu aliyeokoka hupokelewa kwenye ushirika na kuwajibika ndani ya kanisa kwa haraka kama anavyohitaji. Baadhi ya makanisa yanauita huu uanachama wa jumla kwamba ni “Ushirika.”

► Je, ni kwa nini mtu mpya aliyeokoka anahitajika kuhusika kwa haraka ndani ya kanisa?

► Katika mfumo wa uanachama ulioelezewa katika sehemu hii, je, ushirika ni nini, na ni aina gani ya mtu ambaye ni mwanachama wake?

► Katika mfumo wa uanachama ulioelezewa katika sehemu hii, je, Baraza la Uongozi ni nini, na ni aina gani ya mtu ambaye ni mwanachama wake?

Ushirika na Baraza la Uongozi ni mfumo mmoja wa uanachama. Katika sehemu zinazofuatia hapa chini, aina nyingine mbili za mifumo zimejadiliwa.

Uanachama wa Mkristo Aliyekomaa

Dhana moja ya uanachama inahitaji wanachama wawe wenye weledi au ufahamu mkubwa katika mafundisho ya imani na wawe wamekomaa kikamilifu kiasi cha kwamba wanaweza kukubalika kuwa wapiga kura kwenye maamuzi ya kanisa. Kundi hili huchagua watu watakaochukua nafasi za utumishi, ikiwa ni pamoja na mchungaji. Aidha wanapiga kura kwenye maamuzi ya utendaji au kuchagua kikundi cha wawakilishi ambacho kitakuwa kikifanya maamuzi hayo.

Kwa kuwa uanachama unathibiti serikali ya kanisa, muumini mpya hawezi kwa haraka akakaribishwa kuingia kwenye uanachama. Kwa kadiri ambavyo kanisa linakuwa kwenye hadhari na umakini, ni kwa jinsi hiyo hiyo kutakuwepo na orodha ndefu ya vigezo vya kuwa uanachama na muda mrefu kati ya mtu kuokoka na uanachama. Kanisa linaweka vigezo vya uanachama ambavyo ni pamoja na mambo yote ambayo Mkristo aliyekomaa anatakiwa awe, sio tu maelezo ya msingi ya mtu aliyeokoka. Mtu aliyeokoka anaweza akawa mshiriki wa maisha ya kanisa kwa miaka mingi bila kuwa na sifa za kufanyika kuwa mwanachama. Baadhi ya watu waliookoka wanaweza kuamua kuondoka kwa sababu hawawezi kuwa wanachama.

Uanachama wa Kusanyiko la Waumini

Kwenye baadhi ya makanisa, wale ambao kwa kawaida wanahudhuria ibada wanahesabika kuwa ni wanachama. Mamlaka nyingine zinaweza zikawa ndizo zenye maamuzi ya shughuli za kanisa, lakini yeyote anayehudhuria kwenye kanisa ni mwanachama. Hata hivyo, hata lile kanisa ambalo linadai kwamba halina orodha ya wanachama, kuna mfumo ambao haujaandikwa rasmi ambao unaangalia ni nani aliyeko pamoja nao na ni nani ambaye hayuko pamoja nao.

Kwenye kanisa ambalo lina uanachama wa kusanyiko la waumini, uimara wa kanisa unaweza kuwa kwenye mikono ya mchungaji au viongozi wanaotoka kwenye familia zenye ushawishi au umaarufu.

Endapo kanisa changa lina uanachama wa kusanyiko la waumini kama ndiyo mamlaka ya mwisho, kwa namna yeyote ile haliwezi likatabiri litakavyokuwa kwa miaka michache itakayokuja mbele.

Endapo kanisa la zamani lenye uanachama wa kusanyiko la waumini lina uimara au uthabiti, kuna uwezekano kwamba liliimarishwa na aidha kundi la familia au mchungaji mwenye nguvu aliyetumikia hapo kwa muda mrefu. Itakuwa ni vigumu kwao kuweza kuelezea masharti ambayo mambo yanafanyika, lakini wanawaamini wale walioko kwenye uthibiti au mamlaka. Kanuni zilizoandikwa zinaweza zisiwepo au zinaweza zikapuuzwa. Wakati ambapo mchungaji au viongozi wengine wanabadilishwa, kanisa linaweza kupitia kwenye mabadiliko makubwa.

► Je, kuna faida na hasira gani unazoziona kwenye hii mifumo miwili ya uanachama iliyoelezewa hapo juu?

► Tazama mifano miwili ifuatayo, moja kutoka katika kanisa lililopo Marekani, na mwingine kutoka katika kanisa lililopo Ufilipino. Jadili ni kwa jinsi gani haya maelezo ya aina mbili yanavyolinganishwa na uanachama wa kanisa kwenye makanisa unayoyafahamu.

Mfano wa Kwanza

Ushirika wa Kanisa la Ushindi (The Victory Chapel Fellowship)

Jamii (Watu wote) hualikwa kushiriki takribani kwenye shughuli zote za Kanisa la Ushindi ikiwa ni pamoja na ibada za kuabudu, mikusanyiko ya jumuiya za nyumbani, kushirikishana mahitaji, maombi, vyakula vinavyoandaliwa na usharika au kusanyiko, na mafundisho ya Biblia. Hata hivyo, Agano Jipya huonyesha kwamba kikundi cha watu wanaofanya kanisa la mtaa hakina budi kiwe kinachotambulika. Lazima kitambulike wazi kwa jamii kwamba ni watu gani wanaoshiriki katika kanisa hilo. Bila ya kikundi hicho kuwa kinatambulika, litakuwa ni jambo lisilowezekana kwamba kanisa lina ushuhuda mbele ya dunia, au kuweza kushirikisha ushirika wa kweli wa Kikristo ulio katika msingi wa umoja wa Ukristo usiokuwa na mipaka ya urafiki, kufanya nidhamu ya kanisa ya kibiblia, na kubeba kwa pamoja majukumu ya huduma kwa ajili ya kanisa. Kwa hiyo, majukumu kwa ajili ya huduma za Kanisa la Ushindi yanategemea kila kitu kutoka kikundi cha kusanyiko au usharika kinachoitwa “Ushirika.”

Vigezo vinavyotekelezwa na wale walioko kwenye Ushirika

Tunatambua kwamba kuna vigezo vingine maalumu ambavyo ni udhihirisho wa kukua kiroho, lakini vigezo vinavyofuata vinatoa mambo ya msingi ambayo yanaonekana kuwa ni muhimu kwa ajili ya umoja na ushirika wa kweli wa kuabudu wa Kikristo.

(1) Maisha ya Kiroho

Dhihirisha ushahidi wa kuokoka, matamanio ya kiroho, na msimamo kabisa wa kuenenda kwa uhusiano wa utiifu pamoja na Mungu.

(2) Hamasa ya Kibiblia

Epukana na uasherati, matumizi ya madawa ya kulevya, kuvuta sigara, na vinywaji vyenye kulevya.

(3) Msimamo wa Kujikabidhi au kujitoa kabisa kwa Kanisa.

Hudhuria ibada zote za kanisa kwa uaminifu labda uwe umezuiliwa na hali ya kiafya, kuwepo kwenye huduma nyingine, au uwepo kazini ambao hauwezi kuzuilika kwenye siku za Jumapili. Toa zaka katika utoaji wa kanisa.

(4) Umoja wa fundisho la Imani

Umoja na uelewa wa kanuni ya imani ya Kanisa la Ushindi ni muhimu. Mchungaji huwajibika kushirikishana majadiliano ya Pamoja na muda wa maelekezo kwa kila mtarajiwa.

(5) Maadili ya Vitendo

Dumisha uaminifu katika aina zote za mahusiano na uaminifu katika yote uliyoamua kuwa na msimamo nayo. Dumisha tabia endelevu ya upendo na utiifu kwa wale wengine walioko kwenye ushirika.

Sera Mbalimbali

Tunatambua kwamba baadhi ya wanachama wapya hawataendelea kuwepo, lakini tunachagua kutokuwa na kipindi cha majaribio, kwa sababu waumini wapya wanahitaji kujihusisha mara moja katika shughuli za kanisa.

Baraza la uongozi litafanya tathmini ya jina lililopendekezwa kwa ajili ya Ushirika baada ya mtarajiwa kuwa amefanyiwa usahili na mchungaji.

Mtu aliyeokoka ambaye amekubalika kuwa kwenye Ushirika atapangwa kwa ajili ya kubatizwa labda iwe kwamba alishawahi kubatizwa (ubatizo wa maji mengi) hapo awali baada ya kuokoka.

Endapo muumini aliyeko kwenye Ushirika ataonekana kuwa amekiuka mahitaji ya vigezo vilivyowekwa, baraza la uongozi linaweza aidha kumwondoa kwenye ushirika au kutoa muda wa kuwa chini ya uangalizi na kuwajibika, na baada ya hapo suala lake litaangaliwa au litafikiriwa tena.

Mfano wa Pili

Kanisa la Biblia Methodisti la Ufilipino

Baada ya kumpokea Yesu kama Mwokozi wangu na Bwana, nikaamini katika kifo chake, kumwagika kwa damu yake na kufufuka kwake ikiwa ni ukamilifu wa wokovu wangu, ninajiunga sasa na mwili wa Kristo wa ulimwengu wote. Lakini kama ambavyo mwili na viungo vingi, vivyo hivyo na mwili wa Kristo. Kupitia maombi ya kweli, ninajisikia kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kujiunga na familia ya Kanisa la Biblia Methodisti la Ufilipino – kwenye ushirika wake, imani, na nidhamu ya kiroho kwa kadri Mungu atakavyozidi kuniwezesha. Kwa kufanya hivyo, ninajikabidhi mwenyewe kwa Mungu na kwa wanachama wengine katika kufanya yafuatayo:

Kwanza, kulinda umoja wa kanisa langu.

  • Kwa kufanya kwa upendo dhidi ya wanachama wengine (1 Petro 1:22)

  • Kwa kukataa umbeya na kusengenya (Waefeso 4:29)

  • Kwa kuwatii viongozi waliochaguliwa (Waebrania 13:17)

  • Kwa kuwa na huruma kwa ndugu ambao wameanguka kutoka katika neema ya Mungu (Wagalatia 6:1-2)

Pili, kushiriki katika majukumu ya kanisa langu.

  • Kwa kuomba kwa ajili ya kukua kwake (1 Wathesalonike 1:1-2)

  • Kwa kuwakaribisha watu ambao hawana kanisa waweze kushiriki (Luka14:23)

  • Kwa kuwakaribisha wageni kwa ukarimu (Warumi 15:7)

  • Kwa kuwatambulisha watu kwa Yesu Kristo (Matendo 8:33-35)

Tatu, kuwa katika huduma ya kanisa langu.

  • Kwa kugundua karama za kiroho (1 Petro 4:10)

  • Kwa kuwezeshwa kutumika pamoja na wachungaji (Waefeso 4:11-12)

  • Kwa kukuza moyo wa utumishi katika kuwahudumia watakatifu, kwa wenye njaa, kwa walio uchi, wagonjwa, wajane na yatima, na waliofungwa – kwa kadri ya uwezo na nafasi itakayopatikana (Mathayo 25:31-46; Wafilipi 2:3-7)

Nne, Kwa kuunga mkono ushuhuda wa kanisa langu.

  • Kwa kuhudhuria kwa uaminifu (Waebrania 10:25)

  • Kwa kupokea kwa unyenyekevu Neno la Mungu kama litakavyokuwa linahubiriwa, na kutembea katika nuru yake (1 Yohana 1:9-10)

  • Kwa kuishi maisha ya utakatifu (Waebrania 12:14; Wafilipi 1:27)

  • Kwa kukiri makosa (James 5:16)

  • Kwa kushiriki Meza ya Bwana (1 Wakorintho 11:23-26)

  • Kwa kutoa matoleo mara kwa mara (Mambo ya Walawi 27:30; 1 Wakorintho 16:2; 2 Wakorintho 9:7)

Imetiwa sahihi leo ____ tarehe ya ______________

Sahihi ya Mwanachama _______________________________

Imethibitishwa na: ____________________ Mchungaji wa Kanisa la Mtaa

 

Taarifa Saba kwa Muhtasari

1. Mungu huishi ndani ya kikundi cha waumini kwa njia maalumu.

2. Kanisa ni familia ya Mungu, mahali ambapo waumini huweka msimamo na kujikabidhi kabisa kwenye uhusiano wa kifamilia.

3. Uanachama wa kanisa ni njia mojawapo ya kujiweka kwenye msimamo na kujikabidhi kabisa kwenye mpango wa Mungu kwa ajili ya kanisa.

4. Kusanyiko au Usharika ni lazima uweze kushirikishana majukumu ya kanisa kwa pamoja.

5. Uwezo wa mtu binafsi ni muhimu sana unapotumika kwenye maisha ya kanisa.

6. Mtu mpya aliyeokoka anahitajika kuhusika kwa haraka ndani ya kanisa.

7. Ukomavu haupaswi kuwa kigezo cha uanachama wa kanisa.

Kazi za kufanya Somo la 5

1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 5. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.

2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.

3. Kazi ya Kuandika: Jaribu kukadiria asilimia (%) ya watu wanaohudhuria kwenye kanisa lako ambao ni wanachama wenye msimamo na wamejikabidhi kabisa. Elezea ni kwa jinsi gani mtu anafanyika kuwa ni mwanachama katika kanisa lako.

Next Lesson