Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 14: Karama za Kiroho

16 min read

by Stephen Gibson


Kuorodhesha Karama za Kiroho

Tafsiri ya Karama za Kiroho

Karama ya kiroho ni uwezo aliopewa mtu aliyaemini kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya matumizi katika huduma ya kanisa. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kupitia kwa mtu aliyeamini, lakini bado mtu aliyeamini hufanya uchaguzi wa jinsi ya kutumia karama yake na inawezekana pia akaitumia kwa njia isiyofaa. Karama ya kiroho siyo sawa na uwezo wa asili wa mtu, lakini karama zinaweza zikaambatana na uwezo wa asili wa mtu husika na hauwezi kutofautishwa kirahisi.

Karama za kiroho na majukumu ya huduma yameorodheshwa katika maeneo mbalimbali ya Agano Jipya. Orodha hizi ziko sawa lakini hazifanani. Biblia haijatupa sisi orodha ya karama zote za kiroho

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Waefeso 4:7-12 kwa ajili ya kikundi.

Aya za 7-8 zinatuambia kwamba neema ya Mungu inatolewa kwa kila mtu kwa njia ya karama za kiroho. Inavyoonekana mtume hazungumzi kuhusu neema ya wokovu, kwa sababu kwenye aya ya 11 ameorodhesha majukumu ya huduma mbalimbali ambazo Mungu ametoa.

Mungu anawaita watu kwa huduma maalumu na anatoa karama za kiroho wanazozihitaji. Paulo aliorodhesha baadhi ya huduma, badala ya kuorodhesha karama za kiroho kama alivyofanya katika 1 Wakorintho. Majukumu ya huduma yaliyoorodheshwa ni mtume, nabii, mwinjilisti, mchungaji na mwalimu. Kwa hakika, haijamaanisha kuwa hii ni orodha kamili iliyokamilika ya majukumu ya huduma zote.

Mtume

Mitume walikuwa wanachaguliwa maalumu kuliendeleza kanisa baada ya huduma ya Yesu kukamilika hapa ulimwenguni. Walijulikana kwa miujiza iliyotendeka katika huduma zao (2 Wakorintho 12:12). Wote walimjua Yesu kibinafsi wakati wa huduma yake hapa ulimwenguni (1 Wakorintho 9:1, Matendo 1:21-22).

Katika kitabu cha Ufunuo tulisoma kwamba misingi kumi na miwili ya jiji iliwakilisha mitume kumi na wawili, ikimaanisha kwamba walikuwa ni watu wa kipekee kabisa katika historia ya kanisa (Ufunuo 21:14). Aya nyingine zinazoonyesha kwamba kuna mitume kumi na wawili tu ni Mathayo 10:2 na Matendo 1:26. Yuda 17 anaonyesha kwamba mitume walikuwa ni kwa siku zilizopita. Hakuna tena mitume walio hai kwa wakati wa sasa.

Nabii

Baadhi ya watu wanadhania kwamba unabii ni utabiri wa mambo yajayo, lakini Agano Jipya linarejelea kwenye kuhubiri kama unabii. Kwenye Agano la Kale, unabii mara nyingi ulijumuisha utabiri, kwa sababu hiyo ilikuwa ndiyo njia mojawapo ambayo nabii alithibitisha kwamba ujumbe wake ulikuwa unatoka kwa Mungu. Kwenye nyakati za Agano la Kale, mambo mengi yaliyoko kwenye Biblia yalikuwa bado hayajaandikwa.

Nabii ni mtu anayepokea ujumbe kutoka kwa Mungu, ambao unaweza au usiweze kujumuisha utabiri. Mamlaka ya ujumbe wake kwa kawaida ni Biblia.

Mwinjilisti

Neno mwinjilisti linatokana na neno injili. Mwinjilisti ni mtu anayewasilisha injili, aidha kwa watu binafsi au kwenye kusanyiko. Kila Mkristo anapaswa kushirikisha injili, lakini baadhi wamejaliwa kipekee kupata karama kwa ajili ya kazi hiyo. Mchungaji anapaswa kufanya uinjilisti kama sehemu ya huduma yake (2 Timotheo 4:5).

Mchungaji

Mchungaji siyo tu mhubiri, bali pia ni mtu ambaye hutoa malezi ya kiroho kwa kundi maalumu la watu.

Mwalimu

Katika kanisa, mwalimu ni mtu anayeelezea ukweli wa kibiblia na wa kiroho kwa watu wengine. Kila mchungaji anapaswa awe mwalimu (1 Timotheo 3:2, Tito 1:9), lakini watu wengine ambao siyo wachungaji wamejaliwa pia kupata karama za kuwa waalimu.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Warumi 12:6-8 kwa ajili ya kikundi.

Hapa mtume anasema kwamba mtu anapaswa kuelekeza juhudi zake katika karama ambayo Mungu amempa, badala ya kutawanya juhudi zake na muda wake kwenye huduma nyingi tofauti.

Baadhi ya maelekezo maalumu hutolewa kwa ajili ya aina fulani ya huduma. Kwa mfano, mtu anayeongoza ni lazima awe na bidii, na siyo kuongoza tu anapotaka kufanya hivyo, bali kuhakikisha kwamba majukumu yanatekelezwa wakati wote. Mtu anayetoa hapaswi kufanya hivyo katika njia inayomfanya aonekane bali atoe katika njia ya kawaida. Mtu anayeonesha huruma, kwa ajili ya kusaidia na hitaji la dharura anapaswa afanye hivyo kwa furaha, na siyo kwa shingo upande.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:28 kwa ajili ya kikundi.

Inaonekana Paulo hakukusudia kutoa orodha kamili ya karama zote au majukumu ya huduma zote katika aya hii. Kwa mfano, hakuwataja wachungaji kwenye orodha hii, ingawaje aliwataja kwenye orodha iliyoko kwenye Waefeso.

Mitume, manabii na waalimu walishajadiliwa mwanzoni katika somo hili.

Baadhi ya watu wanaitwa kwenye huduma za miujiza na uponyaji. Kila mtu aliyeamini ana fursa ya kuomba kwa ajili ya miujiza, na Mungu atajibu kwa ile imani. Hata hivyo, baadhi ya watu walioamini wanazo karama za kutambua mapenzi ya Mungu na kutumia imani kwa ajili ya miujiza.

Baadhi ya watu wanazo karama za usaidizi. Wanaona mahitaji kwa haraka zaidi kuliko watu wengine. Wanatambua nafasi za kutoa msaada kwa mahitaji ya watu binafsi au kwa kazi ya kanisa. Wanakuwa na uwezo wa aina mbalimbali wa kivitendo.

Baadhi ya watu wamepewa uwezo wa aina mbalimbali wa kuongoza na kutawala. Watu wengi wanafikiri kwamba viongozi ni watu muhimu zaidi, lakini uongozi utakuwa hauna thamani bila ya karama nyingine katika kanisa.

Karama ya lugha imeorodheshwa mwisho. Inawezekana mtume alitaka kusahihisha wale wanaofikiria kwamba hiyo ilikuwa ni karama muhimu sana kuliko nyingine.

Kanuni kutoka kwa Petro

Mtume Petro alielezea kwa kifupi kanuni muhimu zaidi kuhusu karama mbalimbali za kiroho.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Petro 4:10-11 kwa ajili ya kikundi.

Tunaweza tukaangalia angalau pointi sita muhimu kuhusu karama za kiroho katika aya hizi.

1. Waumini wameaminiwa karama za kiroho na Mungu. Kwa hiyo, wanawajibika kuzitumia kwa ajili ya Mungu na siyo kama wamiliki binafsi. Tunawajibika kwa Mungu kwa ajili matumizi yetu ya karama za kiroho.

2. Karama za kiroho zinahitajika zitumike kwa ajili ya watu wengine. Haziko kwa ajili ya kujikuza binafsi au kupata faida.

3. Neema za Mungu ni za namna tofauti (“namna nyingi”). Kuna mchanganyiko wa aina nyingi wa karama.

4. Kuzungumza kwa mtu kunatakiwa kuendana sawa na Biblia.

5. Mtu anapaswa ategemee nguvu kutoka kwa Mungu anapokuwa anafanya huduma.

6. Huduma zote zinapaswa ziwe na lengo la kumtukuza Mungu.

Kanuni kutoka kwa Paulo

Kanisa la Korintho lilikuwa limebarikiwa kuwa na karama za kiroho nyingi. Walikuwa na kutoelewana, kwa hiyo, mtume Paulo akawapa ufafanuzi kuhusu karama za Roho Mtakatifu kwenye 1 Wakorintho 12-14.

Sura hizi za Maandiko zinatufundisha sisi kanuni nyingi kuhusu karama za kiroho. Kanuni chache zifuatazo zimeandikwa hapa kwa ajili yetu kujifunza.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:1-3 kwa ajili ya kikundi.

(1) Kanuni ya kupima fundisho la imani. Mambo ya kiroho yanayofanyika yanatakiwa kufanyiwa tathmini kwa ule ukweli tunaoufahamu.

Waumini wa Korintho kabla ya hapo walikuwa wanaabudu miungu. Miungu haina uwezo wa kuongea lakini mapepo (au maroho machafu) yanaongea. Wafuasi wengi wa dini za kipagani wanajiweka wazi wenyewe kwa ajili ya matendo ya mapepo. Wanaelekea kufikiri kwamba uzoefu wowote wa kiroho ni mzuri. Wanatafuta kupagawa na kupoteza akili au mihemuho ya kiuwazimu. Wanafurahia kuwa chini ya mapepo, hata kama itawafanya kuongea au kufanya matendo kwa njia ambayo ni ya kichaa au maneno machafu.

Mtume alionya kwamba hakuna mtu yeyote anayeongea kwa Roho Mtakatifu atakayesema mambo mabaya kuhusiana na Yesu. Kama maroho machafu yakichukua umiliki wa ibada, itawasababishia watu kutomheshimu Mungu kwa mambo wanayofanya na kunena. Roho Mtakatifu hawezi kuongoza katika njia ambayo haitamheshimu Mungu.

[1]Hatupaswi kudhania kwamba shughuli za kiroho ni kitu kizuri kwa sababu tu ni za kupita akili zetu. Kipimo hapa ni kulinganisha na 1 Yohana 4:1-3. Kama roho anasema kitu kilicho kinyume na Neno la Mungu, hakipaswi kukubalika.

► Je, ni dini gani zinazoruhusu mapepo au maroho machafu kumiliki watu waabuduo?

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:4-11 kwa ajili ya kikundi.

(2) Kanuni ya karama mbali mbali: Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa kila mtu aliyeamini, lakini katika njia zinazotofautina.

Aya hizi zinaweka msisitizo kwamba Roho Mtakatifu aliye mmoja tu hufanya kazi kwa kutumia njia mbalimbali. Anachagua jinsi ya kugawa karama za kiroho. Kila mtu aliyeamini ana angalau karama moja ya kiroho. Hakuna hata mtu mmoja mwenye kuwa na kila karama.

Mwanachama wa kanisa anapaswa atumie karama yake ili kuupa faida mwili wa Kristo. Mungu hakutoa karama kwake kwa ajili ya kujifaidisha yeye mwenyewe.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:12-26 kwa ajili ya kikundi.

(3) Kanuni ya mwili: Kila mwanachama wa kanisa ni muhimu, na kila mmoja anamhitaji mwenzake.

Mtume alilinganisha wanachama wa kanisa na viungo vya mwili. Wana uwezo na makusudi tofauti. Hakuna kiungo cha mwili kinachofikiria kwamba ni lazima kifanane na kingine ili kiwe katika mwili. Kwa mfano, sikio haliwezi kufikiri ni lazima liwe jicho ili liweze kuwa kwenye mwili. Hakuna karama fulani ambayo mtu ni lazima awe nayo kwa ajili ya kuwa kwenye mwili.

Hakuna mwanachama wa kanisa anayepaswa kufikiri kwamba kwa sababu ya karama zake hawahitaji tena wanachama wengine. Mwili hauwezi kufanya kazi bila ya kuwa na viungo vyake yote.

Karama nyingine hupata nafasi ya kujulikana zaidi kuliko karama nyingine. Watu hufikiri kwamba karama fulani za kiroho ni alama au ishara ya hadhi ya kiroho. Mungu huchagua ni kwa jinsi gani atoe hizo karama za kiroho. Hakuna mtu aliye bora au muhimu zaidi kuliko mtu mwingine kwa sababu ya zawadi fulani aliyo nayo.

► Je, utasemaje kwa mtu anayefikiri kwamba mtu anayehubiri ni wa kiroho zaidi kuliko mtu anayeshughulika na kufanya usafi wa jengo la kanisa?

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 12:27-31 kwa ajili ya kikundi.

(4) Kanuni ya majukumu ya huduma: Mungu humpa kila mwanachama wa kanisa kile anachokihitaji kwa ajili ya kukamilisha kusudi la huduma yake maalumu.

Sehemu hii ya maandiko inatoa muhtasari wa sura ya 12. Mungu anawaita watu kwa kusudi la kukamilisha huduma mbalimbali. Huduma haiko kwa ajili ya mtu kuitumia kwa kujikuza yeye mwenyewe, bali kwa kulihudumia kanisa.

Mwalimu wa darasa atapaswa asome maswali yaliyoko katika 1 Wakorintho 12:29-30, na darasa linapaswa litoe majibu. Kwa mfano, wakati kiongozi wa darasa anapolisoma swali “Je! Wote ni mitume?” darasa linatakiwa lijibu: “Hapana.”

Kwa kuwa huduma zinatofautiana, karama nazo ni tofauti. Paulo aliuliza msururu wa maswali, kila moja likitoa jibu kwamba ni “Hapana.” Anaelezea kwa uwazi kwamba hakuna karama inayotegemewa kukaa kwa kila mtu aliyeamini.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 13 kwa ajili ya kikundi.

(5) Kanuni ya Upendo: Upendo ni kipaumbele cha milele, na karama za kiroho siyo za kudumu.

Aya tatu za mwanzo zinaonyesha kwamba upendo ukikosekana hatuwezi tukafidia kwa vipaji vya asili, karama za kiroho, na dhabihu binafsi.

Kwa kujipima wewe mwenyewe, jaribu kuliweka jina lako badala ya upendo kwenye aya ya 4-7 na uangalie ni kwa jinsi gani hapo unaingia vizuri.

Aya ya 11 siyo wito wa kukua. Mtume alilinganisha maisha yetu ya hapa duniani na wakati wa utotoni na akalinganisha maisha ya mbinguni na wakati wa utu uzima. Upo wakati fulani ujao ambao tutakuwa hatuhitaji vitu ambavyo tunavihitaji kwa sasa. Unabii na karama au vipawa vya maarifa vinahitajika kwa sasa kwa sababu ufahamu wetu bado haujakamilika. Kwenye umilele, karama za kiroho zote zitakuwa hazihitajiki tena na zitawekwa mbali kama vile ni “vitu vya utotoni.” Hata imani na matumaini kuna siku ambayo vitakuwa havina umuhimu tena kwa sababu kila kitu kitakuwa kimekamilishwa, lakini upendo utakuwa bado ni wa thamani kuu.

Sura ya 14 ya 1 Wakorintho inaweka msisitizo kwenye kanuni moja: kanuni ya mawasiliano. Kweli nyingine zote zimefundishwa kwenye sura hii, lakini mara nyingi mtume alifafanua na kuelezea kwa mifano au vielelezo kuhusu kanuni hii.

(6) Kanuni ya mawasiliano: Huduma hutegemea mawasiliano ya kweli katika njia ambayo inaeleweka.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 14:1-5 kwa ajili ya kikundi.

Kuhubiri ni jambo muhimu zaidi kuliko hata kuongea kwa lugha nyingine.

Kutoa unabii haimaanishi tu kwamba ni kutabiri kuhusu mambo yajayo. Unabii ni kuhubiri. Kwenye Agano la Kale, unabii mara nyingi ulijumuisha utabiri, kwa sababu hiyo ilikuwa ndiyo njia mojawapo ambayo nabii alithibitisha kwamba ujumbe wake ulikuwa unatoka kwa Mungu. Kwenye nyakati za Agano la Kale, mambo mengi yaliyoko kwenye Biblia yalikuwa bado hayajaandikwa.

Kwa wakati wa sasa mtu anaweza kuhubiri kutoka kwenye Biblia na akaonesha kwamba ujumbe wake unatoka kwa Mungu. Bado kuna vipengele visivyo vya kawaida ya kibinadamu ambavyo Mungu humpa mhubiri ufahamu maalumu wa kuutumia ukweli kwenye mazingira mbalimbali.

Kuongea hakuwezi kusaidia hadi pale watu watakapokuwa wameelewa lugha inayozungumzwa. Kama mtu atazungumza katika lugha ambayo watu wengine hawaielewi, ni Mungu peke yake atakuwa anamsikia.

Watu wengine huchukulia maneno “hakuna mtu anayemwelewa” [2] wakimaanisha kwamba msemaji hata yeye mwenyewe hajielewi, lakini hiyo siyo maana asilia ya sentensi hii. Kama Mjerumani atatoa ushuhuda katika kanisa letu na baadaye tukaanza kusema, “Hakuna mtu aliyemwelewa,” haitakuwa tumemaanisha kwamba yeye mwenyewe hakujitambua.

Kama maneno hayatakuwa yamefafanuliwa, kanisa litakuwa halijajengeka kimaadili.

► Je, mchungaji afanye nini kuhusu mtu anayeongea mara nyingi katika kanisa katika lugha ambayo hakuna mtu anayeielewa na hakuna mtu anayeitafsiri?

Kwenye aya ya 5, Paulo anasema kwamba litakuwa ni jambo jema kama wote kwa pamoja wangekuwa wanaweza kunena kwa lugha; lakini ona pia kwenye 1 Wakorintho 4:8 na 1 Wakorintho 7:7. Alisema kwenye aya ya 4:8 kwamba litakuwa ni jambo jema kama wangetawala kama wafalme, lakini kwa uhakika hakuwa na mategemeo kwamba wawe hivyo kwa sababu hata mitume wenyewe walikuwa wanapitia kwenye mateso. Alisema kwenye 7:7 kwamba ingelikuwa ni jambo lililo jema kama wote kwa pamoja wangekuwa mabikira wasioolewa kama yeye; lakini alisema kwamba sio watu wote walioitwa kuwa katika hali hiyo, na tunajua kwamba ndoa ni mpango wa Mungu kwa watu wengi. Kwenye 14:5 anathibitisha tu kwamba litakuwa ni jambo lililo jema kama kila mtu angeweza kuwa na karama ya kunena kwa lugha; lakini haimaanishi kwamba kila mtu ataweza kuwa hivyo. Kwenye 12:29-30, anaelezea kwa uwazi kwamba hakuna aina fulani ya karama ambayo kila mtu anapaswa awe nayo.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 14:6-19 kwa ajili ya kikundi.

Hotuba haina thamani kama itakuwa haieleweki.

[3]Kwenye aya ya 6, mtume aliuliza swali, “Je, “nitawafaidia nini?” Endapo itakuwa kitu hakieleweki, halitakuwa na faida yeyote. Hata vyombo vya muziki ni lazima vipigwe kutokana na mfumo fulani au mlingano wa sauti au vinginevyo havitakuwa na maana yeyote, isipokuwa kelele za sauti tu. Tarumbeta zinatumika kwa ajili ya ishara kwenye jeshi. Kama tarumbeta itatoa makelele ambayo hayako kwenye mpangilio wa kutoa ishara, hakuna mtu atakayejua kama ni ishara ya kumfukuzia adui au kama ni ya kuanua mahema. Mawasiliano ndiyo msisitizo wa sura hii yote.

Maneno ambayo hayaeleweki ni kwamba “hewani” tu (9). Hii ni kusema kwamba maneno kama hayo hayana thamani kabisa.

Paulo alisema kwamba kama watu hawataelewana, wanakuwa kama watu ambao kila mmoja anamwona mwenzake hana ustaraabu (11). Kama mtu atataka kuendelea kuongea tu bila ya kuwa anaeleweka, atakuwa halijengi kanisa katika maadili bali anataka kukamilisha baadhi ya malengo yake mwenyewe (12).

► Je, kutakuwa na sababu gani za mtu kuongea mambo ambayo hakuna mtu yeyote anayeelewa?

Paulo alisema kwamba kama mtu ataongea katika lugha ambayo haieleweki kwa watu wengine, anachokielewa yeye mwenyewe hakina matunda (14). Paulo alikuwa hasemi kwamba mtu hawezi akajifahamu yeye mwenyewe, lakini kujifahamu kwake mwenyewe tu hakutasababisha uwepo wa jambo lolote zuri kwa watu wengine.

Alisema kwamba njia nzuri ni kufanya huduma katika Roho na kuwa na uelewa kwa wakati mmoja (15). Kuwa katika Roho haimaanishi kwamba mtu hawezi akaeleweka.

Alisema kwamba mtu ambaye hajaelimika ana uwezekano mkubwa wa kutoweza kuelewa kile kinachosemwa (16). Hii inathibitisha kwamba anazungumzia kuhusu lugha mbalimbali za kawaida. Alisema hatupaswi kusema, “Amen” kwa kitu tusichokielewa.

Paulo alisema kwamba alikuwa anafurahia kuwa na uwezo wa kuongea mchanganyiko wa lugha nyingi. Hata hivyo, alisema kwamba maneno matano tu yanayoeleweka ni bora zaidi kuliko maneno elfu kumi yasiyoeleweka (18-19).

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 14:20-25 kwa ajili ya kikundi.

Maneno yenye upako wa Roho na yanayoeleweka yanampa Mungu utukufu.

Kusudi la kunena kwa lugha ni kuwasilisha injili (ona Marko 16:15-17).

Baadhi ya watu huamini kuwa kipawa cha kunena kwa lugha ni ishara kuwa mnenaji ana Roho Mtakatifu, lakini aya ya 22 husema kuwa kipawa cha kunena kwa lugha si ishara ya kuthibitisha chochote kwa waamini. Hii humaanisha kuwa kipawa cha kunena kwa lugha haithibitishi chochote kwa mtu aliye nacho au kwa waamini wanaokiona kipawa hicho. Ni ishara kwa wasioamini pale tu ambapo kitatumika kufikisha injili kwa namna inayo eleweka kwa wasioamini.

Inawezekana kuwa kipawa cha kiroho kikaendelea kufanya kazi kwa mtu kama ataanguka tena dhambini na kuvunja uhusiano wake na Mungu. Hivyo basi, kipawa cha kiroho hakithibitishi kuwa mtu huyo anatenda sahihi au kuwa ameokoka

Kama mgeni katika kanisa akisikia watu wote wakinena kwa lugha na haelewi chochote kinachosemwa, atafikiria kwamba watu wamepagawa. Lakini kama mtu aliyeamini akisikia ukweli unaomhukmu moyo wake, atatambua kwamba Mungu yuko mahali pale.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 14:27-35 kwa ajili ya kikundi.

(7) Kanuni ya utaratibu: Kanisa ni lazima liweke utaratibu katika ibada.

Mtume aliuliza, “Kwa nini kila mtu anafikiri kwamba wanahitaji kufanya jambo fulani kwenye ibada?” Waumini wa Korintho walifikiri kwamba mtu alikuwa muhimu kama akisema kwa lugha au akiongoza ibada, kwa hiyo kila mtu alitaka awe na kitu cha kufanya.

Alisema kwamba kama mtu anazungumza katika lugha ambayo watu wengine hawaielewi, ni lazima itafsiriwe. Hawapaswi watumie muda mrefu wakati wa ibada kwa ajili ya vitu vinavyoweza kutafsiriwa (27).

Mtu anayeongea lugha ambayo watu wengine hawaijui, hawapaswi kuongea kama hakuna mtu wa kuweza kuitafsiri (28).

Kamwe haipaswi kuwe na watu wawili wanaoongea kwa wakati mmoja (31). Inavyoonekana ni kwa sababu kila mmoja anataka aongee, baadhi ya watu walikuwa wakiongea kwa pamoja kwa wakati mmoja. Ibada ilikuwa ni ya machafuko.

Baadhi yao inawezekana walikuwa wanasema hawawezi kuwa chini ya sheria kwa sababu wakati roho anapokuwa amejidhihirisha kwao wanakuwa hawawezi kujizuia wenyewe. Paulo alisema kwamba mtume anaweza kujizuia mwenyewe (32). Akisema kwamba Mungu hawezi akaleta machafuko kwenye kanisa (33). Roho Mtakatifu hawezi akamwongoza mtu kufanya kitu ambacho ni kinyume na mafundisho ya Biblia.

► Je, kuna taratibu gani nzuri za kuiweka ibada iwe kwenye utaratibu wakati wa ibada?

Inavyoonekana, wanawake wa kanisa la Korintho walikuwa wanasababisha mtafaruku. Walikuwa wanaweza kuwa wanauliza maswali na kubishana, kwa sababu Paulo alisema wanapaswa wawe chini ya mamlaka na wangojee wakaulize maswali yao wakiwa nyumbani. Katika mazingira yaliyo bora zaidi, wanawake wanaweza wakaruhusiwa kuwa na huduma na kushiriki ibada, lakini wakiwa katika hali ya unadhifu.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Wakorintho 14:36-40 kwa ajili ya kikundi. Je, Paulo alikusudia nini kuhusu uhusiano wao na makanisa mengine?

(8) Kanuni ya kitume: Kila kanisa linatakiwa kutii mafundisho ya asili ya imani ya mitume.

Waumini wa Korintho walikuwa wamebarikiwa kuwa na karama za kiroho. Inawezekana walianza kufikiri kwamba hawakuwa na hitaji la kusikiliza mamlaka nyingine yeyote. Paulo aliwakumbusha kwamba injili ilikuwa imekuja kwao kupitia kwa watu wengine. Walitakiwa watii mafundisho ya imani ya kanisa lote la Mungu. Kama mtu atajinadi kwamba anajua zaidi kuliko maelekezo ya mtume, ni mjinga na anapaswa achukuliwe kama mtu asiyekuwa na hekima wala asiyekuwa wa kiroho.

Paulo aliwaambia kwamba wasikataze matumizi ya lugha mbalimbali. Kunena kwa lugha ni muhimu, hasa katika maeneo ambayo lugha tofauti tofauti hutumika; lakini, karama hiyo ni lazima itumike katika njia ambayo Biblia inaelekeza.


[1]

“Siyo kila mtu aongeaye katika Roho ni nabii, ila kama tu yuko katika njia za Bwana. Kwahiyo kutokana na njia zake nabii wa uongo na wa ukweli atajulikana.”

- Didache
(iliandikwa kwenye karne ya kwanza ya kanisa)

[2]1 Wakorintho 14:2 NENO: Neno: Bibilia Takatifu 2025
[3]

“Ni jambo linalopingana waziwazi na Neno la Mungu na desturi ya kanisa la kwanza kuwa na maombi ya hadhara kanisani au kuendesha sakramenti kwa lugha isiyoeleweka na watu.”

- Articles of Religion
of the Methodist Church

Mashindano ya Kanisa na Nguvu ya Kiroho.

Kuna baadhi ya makanisa ambayo hujaribu kuleta mvuto kwa kutumia udhihirisho wa nguvu ya kiroho. Wanaamini kwamba matendo ya miujiza karama za kiroho hulitambulisha vyema kanisa. Wanajinadi kwa matendo mengi ya miujiza ya uponyaji. Baadhi ya wanachama wanadai kupokea mara kwa mara maneno ya ufunuo kutoka kwa Mungu. Huduma zao za ibada zinaelekeza kwenye kulenga udhihirisho wa karama za kiroho kuliko ilivyo kwenye Biblia. Wanaamini kwa kila mkristo anapaswa kuwa na karama ya kunena kwa lugha, wanahitaji karama hii kujidhihirisha katika ibada zao za kuabudu. Wanahamasiaha sana watu kuwa na mpango katika ibada za kuabudu ili kwamba ibada zao ziwe zenye machafuko. Viongozi wao wanajitahidi wajulikane kwamba wao ni maarufu, wakijivunia kuhusu uwepo wa nguvu ya kiroho na kulaumu makanisa mengine.

Matatizo mbalimbali huonekana kwenye makanisa yanayoshindana kwa udhihirisho wa nguvu ya kiroho. Wengi wa wanachama wake, na hata viongozi wao, huishi maisha ya dhambi za wazi. Hawaelelwi kuhusu kukua kiroho kunakodhihirishwa kwa njia ya imani ambayo huleta kustahimili matatizo ya maisha. Wengi wa viongozi ni vijana ambao hawaishi kwa ushindi dhidi ya dhambi, na hawawaheshimu waumini wazee na walio waaminifu. Wanakuwa na matendo yasiyokuwa ya kibiblia ya kunena kwa lugha. Watu wao wengi kwa uhakika hawajawahi kuwa na uzoefu wa miujiza, lakini wana mategemeo ya kuwa nayo.

Kanisa ambalo lina upako wa kweli wa Roho Mtakatifu linapaswa kudhihirisha imani na karama za kiroho kufuatana na matendo ya kimaandiko. Kanisa linatakiwa liongoze wanachama wake wakue katika imani ambayo hustahimili nyakati ngumu za matatizo na inayoleta ushindi dhidi ya dhambi. Kuliko kutaka kudhihirisha karama za kiroho kama maonyesho, kanisa linapaswa litumie karama za kiroho katika kukidhi mahitaji ya familia ya imani.

► Je, kuna dalili gani za kanisa ambalo linajaribu kushindana na makanisa mengine katika kudhihirisha nguvu ya kiroho?

Taarifa Saba kwa Muhtasari

1. Karama ya kiroho ni uwezo unaotolewa na Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeamini kwa ajili ya kutumia kwa huduma ya kanisa.

2. Kila mtu aliyeamini hupokea karama za kiroho, lakini siyo kila mtu anayeweza kutegemewa kuwa na karama fulani moja.

3. Wanachama mbalimbali wa kanisa wanapaswa wafanye kazi kwa pamoja kama mwili mmoja kwa kila karama inayohitajika na umhimu wake.

4. Karama za kiroho huambatana na wito wa huduma mbalimbali.

5. Maneno yaliyotamkwa hayana thamani kama hayaeleweki.

6. Mtu aliyeamini ni lazima atumie kwa uangalifu karama zake katika kumletea Mungu utukufu na kuliimarisha kanisa.

7. Upendo kwa ajili ya Mungu na watu ni jambo la muhimu na la kudumu milele.

Kazi za kufanya Somo la 14

1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 14. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.

2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.

3. Mtihani: Kwenye mwanzo wa kipindi kingine cha darasa, unahitajika kuandika kutoka katika kumbukumbu za ufahamu angalao kanuni saba miongoni mwa kanuni nane kutoka kwa Paulo kuhusu karama za kiroho.

Next Lesson