► Mwanafunzi atapaswa kusoma Matendo 2:42-47 kwa ajili ya darasa. Ni maelezo gani unayoyaona kuhusiana na ushirika wa kanisa baada ya Pentekoste?
Mara tu baada ya Pentekoste, kitabu cha Matendo kinaelezea kuhusu maisha ya kanisa. “Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika.” Watu wengi waliuza vitu vyao ili kusaidia maisha ya jamii ya kanisa. Walikuwa wakikutana mara kwa mara katika hekalu kwa ajili ya ushirika wa kumsifu Mungu na pia wakikutana kwa ajili ya ushirika wa nyumba kwa nyumba.
[1]Kwenye kipindi ambacho utendaji wa Roho Mtakatifu ulikuwa wa hali ya juu miongoni mwao, maisha ya jamii ya kanisa nayo yalikuwa katika kiwango cha juu sana. Kwa wale waumini wa mwanzo, kuwa sehemu ya kanisa ilimaanisha ni zaidi ya kushiriki kwenye ibada za Jumapili. Kila siku waumini walishirikishana kwa pamoja kuhusu maisha yao.
“Kwa pamoja kwenye Maandiko na kanuni za imani ushirika wa Kikristo unawakilishwa kama namna ya neema.”
- Wiley & Culbertson, Introduction to Christian Theology
Kwenye Agano Jipya, kanisa linaitwa ni familia (Wagalatia 6:10, Waefeso 3:15). Waumini wanaitwa ni watoto wa Mungu (Wagalatia 3:26, 1 Yohana 3:2), na kuwaita kila mmoja kaka na dada (Yakobo 2:15, 1 Wakorintho 5:11).
[1]Tuitafakari familia kama ambavyo kama ambavyo ilikuwa ikieleweka katika maeneo mengi ya dunia hadi wakati wa sasa. Mtandao wa ndugu (au jamaa) ulitengeneza ukoo, ambao ulikuwa sehemu ya kabila. Familia iliyopanuliwa ilitoa ulinzi, ilihusika katika upatikanaji wa haki, ilihusika katika kuwa na maeneo ya ardhi, kazi, ndoa, elimu, pia ilihusika katika kuwasaidia wazee, yatima na wajane. Mambo hayo yalikuwa ni vigumu kuweza kupatikana nje ya muunganiko wa familia.
Katika hali hiyo ya utamaduni, kila mtu ndani ya familia alikuwa ndani ya dini moja inayofanana. Suala la dini halikuwa linachukuliwa kama ni chaguo la mtu binafsi. Watoto walikuwa wanalelewa katika mafundisho yaliyoendana na utamaduni wa dini ya familia.
Watu wengi waliookoka na kuwa Wakristo walikataliwa kwenye familia zao. Walipoteza kila kitu ambacho kwa kawaida kilikuwa kinatolewa na familia. Kanisa lilifanyika kuwa ndio familia yao mpya. Hii ndiyo maana waliitana kila mmoja kwamba ni kaka na dada. Watu wa kanisa walimsaidia kila mtu na wakitegemeana kila mmoja
Kama watu wakionana kwenye siku za Jumapili tu, wanaanza kufikiria kwamba kukutana Jumapili tu ndio kanisa. Makanisa ya Agano Jipya yalikutana siku za Jumapili, lakini kanisa lilikuwa hai na likiendelea kufanya kazi kila siku.
► Je, ni kwa jinsi gani mambo yataweza kuwa tofauti kwa ajili ya kanisa ambalo linashirikishana masuala ya maisha kila siku?
Wachungaji wanapaswa wafahamu kwamba kuhudumia kusanyiko kwa muda wote wa wiki ni muhimu sana kama vile ilivyo muhimu kuongoza ibada ya kumwabudu Mungu. Aina zote za karama za kiroho na uwezo binafsi wa watu mbalimbali unahitajika, na siyo karama zitumike kwenye siku za ibada za kanisa tu. Kuna njia ambayo kila mtu anaweza akatumika. Watu katika jamii wataweza kuona inamaanisha nini hasa kuwa sehemu ya familia ya kiroho.
Kama familia ya watu wenye imani, kanisa wanatumia rasilimali watu na kupata rasilimali za Mungu vya kukidhi mahitaji ya kila aina kwa ajili ya wale walioko kwenye ushirika, wakidhihirisha kwa ulimwengu hekima ya Mungu katika kila kipengele cha maisha na kuwakaribisha watu ambao hawajaokoka ili waokoke na kuingia kwenye familia.
"Kwa maana kanisa ni familia ya Mungu, ambapo kwa kuzaliwa na kwa damu sisi ni mali—jumuiya ya urithi na upendo ambayo tunaingia kwa kuzaliwa upya, kuokolewa kwa damu ya Yesu."
- Larry Smith, I Believe: Fundamentals of
the Christian Faith
Vipengele vya Maisha ya Pamoja
Kama watu wanashirikishana maisha pamoja, kuwa kwao kwa pamoja kutahusisha vipengele vifuatavyo:
1. Huduma inapangika na kukamilika kwa pamoja. Katika makanisa mengi, timu ndogo inahusika kwenye kupanga na kuwajibika kwa ajili ya kanisa. Kila mtu katika kanisa anapaswa aweze kushiriki kwenye kuwajibika kwa ajili ya kanisa, ikijumuisha waongofu wapya.
2. Mahitaji yanatimizwa kwa pamoja. Kama mtu atakuwa na tatizo, ataweza kuwategemea marafiki zake walioko kwenye kanisa kwa ajili ya kupewa msaada. Hiyo haimaanishi kwamba mtu atakuwa anaruhusiwa kutowajibika, lakini kama anafanya lile lililo kwenye uwezo wake kulifanya, familia ya kanisa inapaswa iwe tayari katika kusaidia.
3. Majukumu yanakamilishwa kwa pamoja. Uhusiano mzito unajengwa wakati waumini wanapowajibika kwa pamoja katika kumsaidia mtu mmojawapo katika ushirika. Wanaweza pia wakawajibika kwa pamoja katika kuzisadia familia zao wenyewe.
4. Muda wa kuburudika unafanyika kwa pamoja. Watu katika kanisa wanapaswa wapate nyakati za kufurahia kwa pamoja katika kula, kutembelea, na kufanya shughuli nyingine mbalimbali.
5. Nyakati maalumu za maisha husherehekewa kwa pamoja. Siyo tamaduni au mila zote zinazokuwa na matukio maalumu yanayofanana. Nyakati zingine maalumu ambazo watu husherehekea ni kama kuzaliwa, kuhitimu shule, kubatizwa, kumbukumbu za siku za kuzaliwa, kufunga ndoa, kupata watoto, maziko, na shughuli nyingine za nyakati maalumu. Watu katika dini nyingine kwa kawaida wanakuwa na siku mahsusi kwa ajili ya kusherehekea nyakati hizi. Kanisa linapaswa liwe na njia ya kushirikishana nyakati hizi maalumu za maisha kwa pamoja.
Kutoa zaka wakati wa Agano la Kale.
Wakati wa Agano la Kale, zaka hazikuwa tu kwa ajili ya kusaidia hekalu na wale waliokuwa wakiendesha ibada. Zaka zilikuwa zinatumika pia kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya wajane, yatima na wageni wahamiaji (Kumbukumbu la Torati 26:12). Zilikuwa pia ni kwa ajili ya mikusanyiko maalumu (Kumbukumbu la Torati 12:17-18). Matumizi ya zaka yanatuonyesha sisi kwamba vipengele vyote vya maisha kwa pamoja ni vya muhimu kwa ajili ya kanisa.
Ushirika na Uchumi
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Yakobo 2:15-16 kwa ajili ya kikundi. Je, aya hizi zinadokeza nini kuhusiana na ushirika wa Kikristo?
Wakati mwingine watu huishi kana kwamba mahitaji ya kifedha hayana uhusiano na ushirika wa waumini. Lakini Maandiko yanatueleza kwamba kuwa sehemu ya familia ya watu wenye imani ni kumaanisha kwamba tunapaswa tuwajibikie mahitaji.
Ushirika unamaanisha ni kushirikishana kuhusu maisha, ambapo huhusisha zaidi ya uzoefu wa kiroho. Neno la Kiyunani Koinonia, linalotumika kwenye Agano Jipya, mara nyingi linatafsiriwa kama “ushirika” na neno hili linatumika kwa ajili ya aina yeyote ya kushirikishana. Wakati mwingine linatumika katika kushirikishana mapato ya kifedha (2 Wakorintho 9:13, 2 Wakorintho 8:4; Warumi 15:26). Jamii ya Kikristo katika Yerusalemu kwenye karne ya kwanza, hakuna mtu aliyekosa kile alichokuwa anakihitaji (Matendo 4:34-35), kwa sababu watu walishirikishana vile vitu walivyokuwa navyo.
Kulipotokea kuwepo na ubaguzi kwenye utoaji wa msaada wa kifedha wa kanisa huduma hiyo ilizuiliwa. Tatizo hilo liliporekebishwa, injili iliendelea kuongeza watu wapya waliookoka (Matendo 6:1, 7).
Mnamo mwaka wa 125 B.K. Mkristo aliyejulikana kwa jina la Aristide aliandika:
Walitembea katika unyenyekevu wote na upendo, na hakuna uongo uliopatikana mingoni mwao, na walipendana kila mmoja na mwenzake. Hawakuwanyanyasa wajane na wala hawakuwahuzunisha yatima. Yeye aliyekuwa nacho, humgawia bila masharti yule ambaye alikuwa hanacho. Kama wakimwona mgeni, humleta malangoni mwao na kufurahia pamoja naye kana kwamba alikuwa ndugu yao: kwa kuwa wao wenyewe waliitana ndugu, siyo katika mwili, bali katika roho na Mungu; lakini mmojawao akitwaliwa kutoka katika ulimwengu huu (akifariki), na yeyote akienda kumwona, ndipo hutoa gharama za mazishi kwa kadri ya uwezo wake; na endapo wakisikia kwamba yeyote miongoni mwao amewekwa jela au kupewa mateso kwa ajili ya Masihi wao, wote kwa pamoja walitoa walivyokuwa navyo kwa ajili ya mahitaji yake; na ikiwezekana wao kumwokoa, wanafanya hivyo. Na kama miongoni mwao yuko mtu ambaye ni maskini na mhitaji, na hawakuwa na vitu vya kutosheleza mahitaji, walifunga kwa maombi kwa muda wa siku mbili hadi tatu ili kwamba waweze kutoa mahitaji pamoja na vyakula muhimu.
Julian mwasi, Mfalme wa Roma (361-363 B.K.) aliyelitesa kanisa, alitoa taarifa yake kuhusu Wakristo: “Wagalilaya makafiri hawawalishi maskini wao tu, bali na wetu pia.”[1]
Kanisa litatimiza nusu ya majukumu yake kama litahubiri kuhusu toba tu, endapo halimkaribishi mtu huyo aliyetubu kwenye familia ya watu wa imani ambako atajifunza jinsi ya kuendeleza maisha yake mapya. Kwa mfano, kama kanisa linamwambia mwanamke kuwa hawatampa pesa kwa kuwa ni kahaba, kanisa linapaswa limweleze ni kwa jinsi gani atafute msaada kutoka katika hiyo familia ya watu wa imani.
Kwenye maeneo mengine ya dunia, tunaona makusanyiko ya kanisa ambayo yanadhihirisha aina hii ya jumuiya ya Kikristo. Ushirika huu wa jumla siyo tu kwamba unatokana na kuwajali wanachama wake kwenye mambo ya kifedha, lakini pia unatokana na uwezeshwaji mkubwa wenye nguvu unaofanywa kwa ajili ya huduma.
Makanisa haya ya maskini (katika Bolivia) yana kitu tunachoweza kukiita utumishi kwa ajili ya kuendelea kuishi. Makanisa yenye umaarufu yaliyoanzishwa miongoni mwa watu maskini hayawezi kuwa tegemezi kutoka kwenye utamaduni, kutoka kwenye msaada wa dola, kutoka kwenye mali zilizowekwa wakfu za watu matajiri, au kutoka kwenye kundi la wahudumu waliobobea kitaalamu. Wanapaswa wawepo kwenye ushirika ambao wanachama wake huunganisha nguvu zao katika kuifanya jumuiya iweze kuwa hai, iweze kukua, iweze kueneza imani, na iweze kudumu. Utumishi unaohusiana na ujumla wa maisha unazoeleka kama ni uhamasishaji wa ujumla wa umishenari. Kitu kinachoonekana kuwa vigumu sana kukipata kutoka kwenye makanisa yenye maendeleo na yaliyo imara ni uhamasishaji wa watu wa kawaida – ushiriki wa ujumla katika kujali ustawi wa jumuiya ya Kikristo. Miongoni mwa makanisa ya watu maskini, uhamasishaji huu ni mfumo wa kawaida wa maisha ya jumuiya. Kunakuwa hakuna njia nyingine ya maisha na uendeshaji wa huduma ni kitu kinachowezekana.[2]
Tunaweza tukafikiria kwamba kanisa ni lazima liwe na fedha nyingi sana kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ajili ya wanachama wake. Lakini aina hii ya jumuiya inadhihirishwa katika makanisa ya watu maskini katika nchi ya Bolivia.
Watu wa kila jamii wanashirikishana maisha ya kifedha kupitia uchumi wa jamii. Tunanunua vitu tunavyovihitaji na tunafanya kazi ili kujipatia fedha.
[3]Aina nyingine ya uchumi inafanya kazi kwenye familia. Kazi ambayo kila mwanachama anafanya kwa ajili ya familia haipimwi kwa viwango vya dola. Kila mtu anategemewa atoe msaada kwa namna yeyote ile kadri atakavyoweza, bila ya kuwekewa masharti magumu. Msaada unatolewa katika maudhui ya kifamilia. Haitegemewi kwamba kila mwanachama aweze kufanya mambo yanayofanana na mwingine au afanye kazi yenye thamani inayofanana, lakini atapaswa afanye kile kinachoweza kufanyika. Kama mwanachama wa familia hayuko tayari kufanya kwa hiari kile ambacho anaweza kukifanya, atafuatiliwa kuhusiana na hilo na anaweza asipatiwe msaada anaohitaji kutoka kwa wanachama wengine.
Uchumi wa kanisa unapaswa uwe zaidi ni uchumi wa kifamilia kuliko uchumi wa jamii. Ili uweze kufanya kazi, mahusiano katika kusanyiko la kanisa ni lazima yawe ya zaiidi ya sana urafiki wa kawaida. Maswali mengi yataulizwa wakati mtu atakapokuwa anaomba msaada baada ya kutokuwa na uwajibikaji kwenye rasilimali zake mwenyewe au baada ya kuwa hashirikiani na wenzake kwa hiari katika kusaidia watu wengine.
Kusanyiko la kanisa linajifunza jinsi ya kukuza uhusiano wake miongoni mwa watu wake. Ni lazima waweze kuelezea kanisa kuhusu watu ambao kamwe huwa hawako tayari kusaidia watu wengine lakini wao wanaomba wapewe msaada. Ni lazima wawafundishe watu ambao hawawezi kushirikiana na wenzao. Ni lazima wakabiliane na wale ambao wanajiona wako huru kufuata matakwa yao wenyewe kwa kufuata mambo ya maadili yao wenyewe na hawako tayari kupokea marekebisho ya kichungaji.
► Je, kuna mifano gani ya njia ambazo wanachama katika kanisa wanaweza kusaidiana wao wenyewe? (Kazi za bustani, kutunza watoto wadogo, kuajiriwa, nyakati za matatizo)
[1]Wakristo waliitwa “makafiri” au “wanaomkana Mungu” kwa sababu waliamini katika Mungu mmoja tu, na kwamba alikuwa ni Mungu asiyeonekana kwa macho, kuliko kuamini wingi wa msururu wa miungu ya sanamu inavyoonekana.
[2]Samuel Escobar, katika The Urban Face of Mission: Ministering the Gospel in a Diverse and Changing World. Kimfanyiwa uhariri na Manuel Ortiz na Susan S. Baker. (Phillipsburg: P & R Publishing, 2002), 105.
“Onyesha kwamba unataka kuwa Mkristo kwa kutenda mema, hasa kwa wale wa jamaa ya imani... Waajiri wao badala ya wengine. Nunua kutoka yao sivyo kutoka mtu mwingine. Kusaidiana katika biashara. Hasa kwa sababu ulimwengu utapenda walio wake, na wao tu.”
- John Wesley
“Rules for the Society of the People Called Methodists”
Maelekezo ya Vitendo
► Mwanafunzi atapaswa kusoma 1 Timotheo 5:3-16 kwa ajili ya kikundi.
Kifungu hiki kinatoa maelekezo ya vitendo vya jinsi kanisa linavyopaswa kutoa msaada kwa wanachama wake walio wahitaji. Aya ya 16 inasema kwamba watu wanapaswa wawasaidie watu wao wenyewe ili kanisa nalo liweze kusaidia wale ambao hawana watu wa kuwasaidia. Mtume anachukulia kwamba msaada wa kifedha kwa wanachama wake ni jukumu la kanisa.
Ni wazi kwamba, kama kila mwanachama atakuwa analitegemea kanisa kifedha, kanisa halitaweza kumsaidia kila mtu. Kifungu hiki kinatoa maelekezo ya vitendo ili kwamba kanisa liweze kusaidia wale watu ambao kwa hakika wanahitaji msaada huo.
Kifungu hiki kinazungumzia mahsusi kuhusiana na wajane, lakini kanuni zinaweza zikatumika pia kwa watu wengine. Tunatambua kwamba kanisa lina wajibu kwa ajili ya watu wengine: Yakobo 2:15-16 anaonyesha kwamba tunapaswa tuwajibikie katika hitaji la kaka au dada; Yakobo 1:27 anataja kuhusu wajane na yatima.
Kanuni tatu kuhusu msaada wa kifedha wa kanisa kwa wanachama wake:
1. Familia ina jukumu la kwanza la kuwajibika. Watu katika familia wanalo jukumu la kusaidia jamaa zao wenyewe walio na mahitaji ya kusaidiwa ili kanisa lisibebe wajibu wa kuwasaidia (1 Timotheo 5:4, 16). Kama mtu hawezi kuisaidia familia yake mwenyewe, huyo mtu siyo mwamini (5:8). Kama mchungaji ataona kwamba katika kanisa kuna uhitaji, atapaswa kutafuta ni kwa jinsi gani jamaa zake wanaweza kufanya katika kutoa msaada.
2. Mwanachama mwaminifu anastahili apewe msaada. Mjane anastahili kupewa msaada kama atakuwa ameishi maisha ya uaminifu ya Kikristo na alikuwa akisaidia watu wengine (5:10). Kanuni hii inaweza kutumika kwa watu wengine mbali na wajane, endapo watakuwa ni wahitaji na hawana uwezo wa kujisaidia wenyewe.
3. Mwanachama atapaswa afanye jambo linalowezekana kufanywa na yeye mwenyewe na kwa watu wengine. Mkristo anapaswa afanye jambo linalowezekana kufanyika kwa ajili ya kuwa baraka kwa watu wengine (5:10). Kama atakuwa hana kazi ya kuajiriwa, anaweza akatafuta njia nyingine ambazo anaweza kusaidia nazo watu wengine. Mtu ambaye kwa hiari yake mwenyewe hataki kufanya kazi, hapaswi kabisa kusaidiwa na kanisa (2 Wathesalonike 3:10).
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Wathesalonike 3:6-12 kwa ajili ya kikundi.
Kifungu hiki kinatueleza zaidi kuhusu maisha ya kanisa la mwanzo. Kwa hapa Paulo anashughulikia tatizo la watu ambao walikuwa wanalitegemea kanisa kwa ajili ya kupewa misaada ili kwamba wao wasifanye kazi. Walikuwa Wanatumia muda wao kwa ajili ya kutembelea tu watu na kueneza majungu.
Hali hii inatuelezea nini kuhusiana na kanisa la mwanzo? walikuwa wanachukua jukumu la kuwajali watu wao. Kanisa lilikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote ndani ya kanisa mwenye njaa. Walikuwa kama wanafamilia.
Kwa kuwa walikuwa kama wanafamilia, ilikuwa ni rahisi kwa mtu kuwa mvivu na kuwa tegemezi kwa watu wengine. Paulo aliwaambia kwamba wanapaswa wamtake kila mtu afanye lile linalopaswa kufanyika. Kama mtu hataki kwa hiari yake mwenyewe kufanya linalowezekana kufanyika, hataruhusiwa kula chakula ambacho kimetolewa na watu wengine.
Ni jambo zuri sana wakati kanisa linapokuwa ni kama familia inayotoa mahitaji ya aina zote. Ili hilo liweze kutendeka, kanisa ni lazima liwe na kanuni za kufuata. Kanisa ni lazima liwe na mahitaji kwa ajili ya wale walio tegemezi kwa ajili ya kupewa msaada na kanisa. Bila ya mahitaji, kanisa katika muda mfupi litaelemewa na watu wavivu na halitakuwa na uwezo wa kuendelea kutimiza mahitaji.
Wachungaji na mashemasi ni lazima walielekeze kanisa lifanye kazi kama familia. Ni lazima wawajibikie katika mahitaji kwa upendo. Hata hivyo, upendo una maana kwamba watakuwa tayari kuzungumza ukweli. Kama mtu hataki kuwajibika, mtu mwingine ni lazima awe tayari kuzungumza naye kuhusu jambo hilo. Kama mtu hatoi msaada kwa watu wengine na kufanya lolote analoweza kufanya kwa ajili ya kujisaidia yeye mwenyewe, kanisa halipaswi liendelee kutoa msaada kwake.
Ni haki kuuliza maswali wakati mtu anapojitokeza kuomba msaada. Je, yeye yuko tayari kuwasaidia watu wengine? Je, anafanya kazi wakati anapokuwa anaweza? Je, anatumia fedha zake kwa busara? Je, anachukua jukumu la kuijali familia yake?
Watu wengi wanakuja kwenye kanisa kuomba misaada. Kanisa ni lazima liwe na njia ya kuwajali watu kwa mara ya kwanza wanapokuja, hata kabla mtu huyo hajaonyesha kuwajibika. Kisha, ni lazima kuwepo na njia ya kukuza uhusiano. Mtu huyo atapaswa afahamu afanye nini ili kuwa sehemu ya ushirika wa kanisa.
Taarifa Saba kwa Muhtasari
1. Kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya kanisa huwaleta wanachama kwenye uhusiano wa karibu kwa ajili ya kushirikishana maisha pamoja.
2. Kanisa ni familia inayoshirikisha maisha ya kila siku na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kukidhi kila hitaji.
3. Kanisa humkaribisha mwenye dhambi aliyetubu kwenye familia ya watu wenye imani ambapo hujifunza jinsi ya kuendeleza maisha yake mapya.
4. Kanisa linapokuwa linafanya wajibu wake kila siku, kunakuwepo na nafasi ya huduma kwa kila muumini.
5. Muda wa kanisa unapotumika kwa pamoja unahusisha huduma, mahitaji mbalimbali, kazi za kufanya, kuburudika, na nyakati za sherehe.
6. Ushirika wa Kikristo unahusisha pamoja na mambo mengine kushirikishana katika rasilimali muhimu.
7. Kanisa halipaswi kuwasaidia watu ambao hawataki kufanya lolote wanaloweza kufanya kwa ajili ya kujisaidia wao wenyewe na watu wengine.
Kazi za kufanya Somo la 6
1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 6. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.
2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.
3. Kazi ya Kuandika: Je, kuna njia gani mbalimbali ambazo watu wa kanisa lako kwa pamoja wanashirikishana maisha zaidi ya ibada ya kuabudu?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.