Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Mafundisho Na Mazoezi Ya Kanisa
Audio Course Purchase

Search Course

Type at least 3 characters to search

Search through all lessons and sections in this course

Searching...

No results found

No matches for ""

Try different keywords or check your spelling

results found

Lesson 3: Kanisa la Mahali

10 min read

by Stephen Gibson


Utangulizi

► Je, kanisa la mahali ni kitu gani? Je, lina tofauti gani na aina nyingine zote za vikundi?

Tafsiri hii ya kanisa la mahali inaweza kugawanywa kwenye maeneo makuu saba muhimu. Maeneo haya yanaelezewa kwa uwazi zaidi katika kozi hii yote.

Ufafanuzi ya Kanisa la mahali

Kanisa la mahali ni kikundi cha waumini ambacho kinafanya kazi kama familia ya kiroho na jamii ya imani; wakitoa injili na ushirika wa kanisa kwa kila mtu anayetubu; wakitekeleza tendo la ubatizo na ushirika wa meza ya Bwana, wakishirikiana katika kumwabudu Mungu, ushirika, uinjilisti, uanafunzi, na kukamilisha kazi ya mwili wa Kristo kwa karama za Roho Mtakatifu; waliojitoa kabisa kwa ajili ya Neno la Mungu; wakiwa na umoja ulio katika msingi wa mafundisho ya imani ya kibiblia, wakiwa na uzoefu wa neema, na maisha ya Roho Mtakatifu.

[1]Hapa chini sehemu za tafsiri hiyo zimerejewa zikiwa na maelezo yaliyofuatana nazo.

► Kwa kila kipengele kinachofuata, jadili ni kwa nini ni muhimu kuwepo na tabia hii ya kanisa. Je, ni matokeo gani yatakayoonekana kama kanisa litakosa kuwa na tabia hii?

Kanisa la mahali ni kikundi cha waumini ambacho kinafanya kazi kama familia ya kiroho na jamii ya imani…

Kanisa ni kikundi kilichoanzishwa kutokana na imani ya Kikristo. Kina mahusiano mazito kuliko hata kikundi kingine katika dunia.

[2]…wakitoa injili na ushirika wa kanisa kwa kila mtu anayetubu…

Kanisa haliwezi kuwatenga watu wa kikundi cha utamaduni fulani au kabila fulani au kwa madaraja ya watu na bado likandelea kuwa mwaminifu kwa injili. Hakuna umuhimu wa mambo ya utamaduni au kabila, au madaraja ya kijamii. Pia, kanisa haliwezi kukataa kusamehe baadhi ya dhambi kama limesimama kwenye uaminifu wa injili.

…wakitekeleza tendo la ubatizo na ushirika wa meza ya Bwana…

Yesu alitoa maagizo kwa kanisa kwa ajili ya kutekeleza sherehe hizi. Ubatizo unawakilisha kuingia katika kanisa kwa kuokoka. Ushirika wa meza ya Bwana unamaanisha neema inayodhihirishwa kutoka katika injili.

…wakishirikiana katika kumwabudu Mungu, ushirika, uinjilisti, na uanafunzi…

Haya ni makusudi ya msingi ya kanisa. Ushirikiano ni muhimu kwa ajili ya kanisa kukamilisha makusudi muhimu.

…kukamilisha kazi ya mwili wa Kristo kwa karama za Roho Mtakatifu…

Majukumu ya kiroho ya kanisa kamwe hayawezi kukamilishwa kwa uwezo wa kibinadamu peke yake.

…waliojitoa kabisa kwa ajili ya Neno la Mungu…

Kanisa linaitegemea Biblia kwa ajili ya injili yake, mafundisho ya imani, na mamlaka. Kama kanisa litachagua kutokuitii Biblia, kanisa litakuwa limepoteza mamlaka yake kwa ajili ya kufundisha.

…wakiwa na umoja ulio katika msingi wa mafundisho ya imani ya kibiblia, wakiwa na uzoefu wa neema, na maisha ya Roho Mtakatifu.

Washirika wa kanisa wanaweza wakajikabidhi mmoja kwa ajili ya mwingine kwa sababu wanayo haya mambo matatu kwa pamoja. Bila ya haya mambo matatu, ushirika wa kweli wa Kikristo hautawezekana kuwepo.


[1]

“Watu walioamini hawajaitwa kibinafsi kuishi tu kwa kuwa na uhusiano binafsi na Mungu bali wameitwa kwa pamoja na kushikamanishwa kwa pamoja kama watu.”

- Thomas Oden,
Life in the Spirit

[2]

“Kanisa la Kristo linaloonekana ni mkusanyiko wa watu waaminifu ambao Neno kamilifu la Mungu linahubiriwa na sakramenti zinatolewa kwa mujibu wa agizo la Kristo…”

- Kanuni za Dini
za Kanisa la Methodisti

Uwekezaji wa Mungu kwa Kanisa

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Waefeso 3:1-10 kwa ajili ya kikundi. Je, kuna baadhi ya mambo gani ambayo Paulo aliyasema kuhusiana na huduma yake?

Paulo alisema kwamba sehemu muhimu ya huduma yake ilikuwa ni kuelezea kuhusu kanisa, kwa hiyo tunaelewa kwamba kuelezea kanisa kunapaswa kuwe ni sehemu muhimu ya huduma kwa wakati wa sasa. Mungu alipanga kwamba watu wanaoamini kutoka kwa Mataifa waletwe kwenye nyumba ya Bwana (Kanisa) na kwamba kanisa litapaswa lidhihirishe hekima ya Mungu kwa ulimwengu.

Tunapaswa tukumbuke kwamba kanisa siyo jengo. Wakristo hawakuwa na majengo kwenye vizazi kadhaa vya mwanzo vya kanisa. Hii ina maana kwamba wakati kitabu cha Agano Jipya kinapokuwa kinazungumzia kuhusu kanisa, kinazungumzia kuhusu watu.

Waefeso hueleza jinsi kanisa lilivyo muhimu kwa mpango wa Mungu.

…Akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote (Waefeso 1:22-23).

Aya hii inasema kwamba Yesu ni kichwa cha kanisa, na kwamba kanisa ndiyo mwili. Inasema kwamba kanisa lina ukamilifu wote wa Mungu.

Jaribu kufikiria kuhusu mto ambao unatoa maji yake yote kwa ajili ya jiji kubwa. Mamilioni ya watu wanayatumia maji hayo, lakini kiasi cha maji wanachotumia ni kidogo kuliko kiasi cha maji kinachotiririka kwenda katika mto. Ni vigumu sana kuweza kufikiria ni kiasi gani cha maji kilichopo.[1]

Lakini inakuwaje kuhusu ukamilifu wa Mungu? Kama ingekuwa Mungu angetengeneza konteina au mfereji wa kumwagia baraka zake na neema yake na nguvu zake kwa ajili ya ulimwengu, ni konteina ya aina gani ambayo ingeweza kushikilia ukamilifu wa Mungu? Aya hii inasema kwamba kanisa ndiyo hiyo konteina. Kanisa lina baraka za Mungu kwa ajili ya ulimwengu.

Kumbuka kwamba, kanisa lililo na baraka za Mungu siyo jengo, bali kundi la watu lililo katika ushirika wa Kikristo.

Mpango wa Mungu kwa ajili ya kanisa ulikuwepo tangu mwanzo wa dunia. Kwa ajili hiyo, Mungu alikuwa na kusudi gani katika ufahamu wake kwa ajili ya kanisa?

Angalia tena Waefeso 3:10-11.

Ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Namna nyingi inamaanisha “aina zote.” Mungu anazo hekima kwa kila hali na kwa kila kipengele cha maisha. Hekima ya Mungu inapaswa idhihirishwe kwa ulimwengu wote, ikiwa ni pamoja na ulimwengu wa kiroho, kwa yale ambayo Mungu anayafanya kupitia kwa kanisa. Mtu hupata ufahamu wake kuhusiana na Mungu kwa kile anachokiona katika kanisa. Kwa kuliona kanisa kunamfanya mtu amwabudu Mungu. Anapaswa aione hekima ya Mungu ikitenda kazi ndani ya kanisa. Dunia haiwezi kuyaona haya yote kutoka kwenye ibada za Jumapili. Wanayaona yote kupitia matendo ya kanisa ya kila siku na kwenye kila hali ya maisha.

► Je, kuna baadhi gani ya mifano ya hali za maisha ambapo hekima ya Mungu ni muhimu?

Je, hekima ya Mungu kuhusu “namna nyingi” inahusisha pamoja na matatizo ya familia, umaskini, ukosefu wa kazi, uhaba wa nyumba za kuishi, Elimu duni, uhalifu wa vijana, kuwatupa watoto, matatizo ya kiafya, na matatizo mengine ya kibinadamu? Kwa hakika jibu ni ndiyo, kwamba inahusisha. Je, dunia itawezaje kuiona hekima ya Mungu? Wanapaswa waione ikidhihirishwa na kanisa, kama nalo kanisa linavyodhihirisha jinsi mambo yanayotatuliwa na Mungu jamii ya imani inavyoyaishi.

► Mwanafunzi atapaswa kusoma Waefeso 3:20-21 kwa ajili ya kikundi.

Kusudi la kila kitu Mungu alichokifanya ni ili kimtukuze Mungu. Kwenye kanisa, ndiko mahali ambapo Mungu anatukuzwa hasa, kwa sababu:

  • Ndiko mahali ambapo upendo na ukombozi unadhihirishwa.

  • Ndiko mahali ambapo viumbe walioumbwa kwa mfano wake kwa hiari yao wenyewe wanamwabudu na kumtii Mungu.

  • Ndiko mahali ambapo familia ya watu wenye imani hudhihirisha maisha ambayo yamebarikiwa na Mungu.

  • Ndiko mahali ambapo watu waliokombolewa wanashiriki kwenye ukombozi wa watu wengine kwa njia ya uinjilisti.

Mungu atatukuzwa ulimwenguni kote na kwenye umilele kupitia kile ambacho kanisa linafanya kwa sasa. Kazi ambayo kanisa lako la mtaa linafanya itasimama kama mnara wa milele kwa ajili ya utukufu wa Mungu.


[1]Kielelezo kingine: Kuna kampuni inayoitwa Carbonite ambayo huhifadhi taarifa zote za kompyuta za watu binafsi. Wanaweza kuhifadhi kila kitu kilichoko kwenye kompyuta yako endapo itatokea lolote la uharibifu katika kompyuta hiyo. Jaribu kufikiria aina ya chombo cha kuhifadhia wanachotakiwa kuwa nacho kuhifadhi maudhui yaliyomo katika maelfu ya compyuta hizo.

Utoshelevu wa Kanisa la mahali

Biblia inazungumzia kuhusu kanisa moja, lakini pia inazungumzia kuhusu makanisa ya mahali. Kwa mfano, Mtume Yohana aliandikia makanisa saba ya Asia (Ufunuo 1:4). Paulo alitaja kuhusu “makanisa ya Mungu” (1 Wakorintho 11:16).

Kusanyiko la mahali ni sehemu ya kanisa lililo moja, lakini bado linaitwa ni kanisa. Takribani nyaraka nyingi katika kitabu cha Agano Jipya zimeelekezwa kwa makanisa yaliyokuweko kwenye maeneo maalumu.

► Je, ni kipi kinaweza kuitwa hekalu la Mungu, kanisa la ulimwengu wote au kanisa la mahali?

[1]Katika Waefeso 2:20-21, Paulo alisema kwamba kanisa moja, kwenye msingi wake wa asili, ni hekalu la Mungu. Katika aya ya 22, alisema kwamba waumini wa Efeso walikuwa maskani ya Mungu. Kwenye mstari mwingine aliwaambia waumini wa Korintho kwamba walikuwa ni hekalu la Mungu (1 Wakorintho 3:16). Kwa hiyo, tunaona kwamba kanisa la ulimwengu ni hekalu la Mungu; na hata kanisa la mahali pia ni hekalu la Mungu.

► Je, ni kipi kinaweza kuitwa mwili wa Kristo, kanisa la ulimwengu wote au kanisa la mahali?

Paulo alizungumzia kanisa moja kama mwili wa Kristo (Waefeso 1:23). Hata hivyo, akiandika kwa kanisa la Korintho, Paulo alisema, “Ninyi mmekuwa mwili wa Kristo” (1 Wakorintho 12:27). Hakusema kwamba waumini wa Korintho ni sehemu tu ya mwili wa Kristo. Walikuwa ni mwili wa Kristo kwa ajili ya eneo lile.

Mungu anakusudia kila kusanyiko litende kazi kama kanisa lililokamilika, ikiwa ni pamoja na chochote wanachohitaji ili kuweza kufanyika ni mwili wa Kristo katika eneo husika.

Paulo alilinganisha washirika wa kanisa la mtaa na viungo vya mwili wa Kristo, kama macho, miguu na mikono, Bila shaka, viungo vya mwili vinapaswa viwe pamoja kwenye eneo moja ili viweze kufanya kazi. Hakuwa anasema kwamba vilikuwa viungo vya mwili na kwamba viungo vingine vya mwili vilikuwa vimetawanyika katika dunia yote. Vilikuwa ni mwili kamili uliokuwa umekamilika katika eneo husika.

Paulo alisema kwa Wakorintho kwamba baadhi ya mambo yalipaswa yafanyike “wakati kanisa lote linapokuwa pamoja katika eneo husika.” Bila shaka hakuwa anazungumzia kanisa la ulimwengu wote, bali kanisa la mahali. Kusanyiko la mahali pamoja lina mamlaka maalumu linapokuwa linafanya kazi zake kama kanisa.

Mungu hutoa karama za Roho Mtakatifu zinazohitajika kwa ajili ya kanisa la mahali. Washirika huwajibika kwa pamoja wakiwa na karama za kukidhi vigezo ya kusanyiko la mahali pale.

Kwa kuwa kusanyiko la mahali pamoja ni mwili wa Kristo, hekalu la Mungu, na kanisa, inatosha kuwa ni kanisa mahali lilipo.

Utoshelevu wa kanisa la mahali inamaanisha kwamba kanisa la mahali lina karama na vianzo vya kufanyia kazi vinavyohitajika kwa ajili ya huduma katika eneo lake husika. Kanisa la mahali linaweza likafanya kazi kama kanisa kamili hata kama halina msaada kutoka mahali pengine. Viongozi wa kanisa la mahali wanasaidia washirika kuendeleza maono na malengo kwa ajili ya huduma. Kusanyiko la mahali pamoja huwajibika kwa pamoja katika kutoa ufadhili wa kifedha kwa ajili ya kusaidia huduma na kuwatunza washirika wa hilo kusanyiko la mahali pamoja.


[1]

“Mambo yote muhimu kwa ajili ya kanisa ni kiini tete kilichoko katika maelezo ya haya mambo manne yaliyoko kwa ajili ya kanisa [Matendo 2:42]: fundisho la mitume, ushirika, kuumega mkate, na kusali.”

- Thomas Oden,
Life in the Spirit

Umuhimu wa Kanisa

Ni vigumu sana kuwakuza watu wapya waliookoka kama hawataletwa kwenye maisha ya kanisa. Mtu aliyeokoka hawezi akafanyiwa uanafunzi ulio mzuri kama hataweza kushiriki kwenye kusanyiko la mahali pamoja. Mtu hawezi akafundishwa kwa ajili ya huduma bila ya kupata uzoefu wa kanisa.

Injili haina aina inayoweza kuonekana kwenye jamii hadi pawepo na kanisa. Aina hiyo ya muonekano haihusiani na jengo la kanisa, bali utendaji wa familia ya watu wenye imani unaodhihirisha maisha yenye kuonyesha ushirika na Mungu. Hadi hapo kanisa litakapokuwa lipo eneo husika, dunia haiwezi ikaona maana ya kuwa Mkristo. Jamii haiwezi ikafikiriwa kwamba imefikiwa kikamilifu na uinjilisti hadi kanisa litakapokuwa katika eneo hilo husika.

Taarifa Saba kwa Muhtasari

1. Mtu aliyeokoka hapaswi kuondolewa katika kanisa kwa sababu za ukabila, daraja lake katika jamii au kwa ajili ya dhambi zake alizozitenda wakati wa nyuma.

2. Majukumu ya kanisa yanaweza kukamilishwa tu kwa kazi ya Roho Mtakatifu kupitia kwa kanisa.

3. Umoja wa kanisa una msingi wake katika mafundisho ya imani ya kibiblia, uzoefu wa neema, na maisha ya Roho Mtakatifu.

4. Hekima ya Mungu hudhihirishwa katika ulimwengu kwa yale ambayo Mungu anayafanya kupitia kwa kanisa.

5. Utoshelevu wa kanisa la mahali inamaanisha kwamba kanisa la mahali lina karama na vianzo vya kufanyia kazi vinavyohitajika kwa ajili ya huduma katika eneo lake husika.

6. Kanisa ni muhimu kwa ajili ya kuwalea watu waliookoka, kuwafanyia uanafunzi waumini, na kutoa mafunzo kwa wahudumu.

7. Jamii haiwezi ikafikiriwa kwamba imefikiwa kikamilifu na uinjilisti hadi kanisa litakapokuwa katika eneo hilo husika.

Kazi za kufanya Somo la 3

1. Kariri taarifa Saba kwa Muhtasari kwa ajili ya somo la 3. Andika aya moja inayoelezea maana na umuhimu wa kila kipengele katika hizi Taarifa Saba kwa Muhtasari (jumla aya saba) kwa mtu ambaye siyo wa darasa lako. Wakilisha kwa kiongozi wako wa darasa kabla ya kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata. Kuwa tayari kushirikisha aya moja kwa kikundi kama kiongozi wa darasa atakutaka ufanye hivyo wakati wa majadiliano. Andika Taarifa hizi kutoka kwenye ufahamu wako bila ya kuangalia mahali popote mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata.

2. Kumbuka kutengeneza ratiba ya nafasi yako mwenyewe ya kufundisha kwa wakati ambao utakuwa nje ya darasa na utoe mrejesho wako kwa kiongozi wa darasa baada ya kuwa umemaliza kufundisha.

3. Kazi ya Kuandika: Soma Waefeso 5:25-32. Andika aya kadhaa zinazohusiana na uhusiano kati ya Kristo na kanisa.

Next Lesson