Maagizo ya Yesu
► Mwanafunzi atapaswa kusoma Luka 10:1-9 kwa ajili ya kikundi. Je, kuna kitu gani kisichokuwa cha kawaida kuhusiana na maelekezo ya Yesu aliyowapa wanafunzi wake wakati alipowatuma kwenda kufanya huduma?
Wanafunzi walitumwa kuwa wa kwanza kuhubiri injili katika maeneo mengi ya vijiji. Yesu alikuwa na uwezo wote na nyenzo zote na alikuwa na uwezo wa kuwapa kitu chochote. Angeweza kuwapa fedha za kuwatosha katika kununua chochote ambacho wangehitaji katika kukidhi mahitaji ya watu wengine. Angeweza kuwapa nguvu za kujigawia mkate na Samaki wao wenyewe na kwa ajili ya watu waliokuwa wanawahubiria. Wangeweza kugawa chakula kwenye kila Kijiji walichokuwa wanakitembelea.
Badala yake, aliwatuma bila fedha. Aliwaambia wategemee kupata misaada yao kutoka kwa watu waliokuweko katika vijiji walivyotembelea. Mitume walikwenda kama Yesu alivyowaagiza, na walipatiwa mahitaji yao (Luka 22:35).
► Je, kwa nini Yesu aliwatuma kwa njia hii?
Huduma yao iliwavutia watu sahihi. Kwa kuwa walihubiri injili kwanza, waliwavutia watu waliokuwa wanahitaji injili. Kwa kuwa walikuwa na mahitaji, waliwavutia watu waliotaka kusaidia. Walikuwa na watu wazuri sana kwa ajili ya mwanzo wa kanisa.
Je, ingekuwaje kama wangeenda kwenye vijiji wakiwa na kila kitu ambacho walikuwa wanakihitaji pamoja na vitu vya kuwapa watu? Wangewavutia watu ambao siyo sahihi. Wangeweza kukusanya kundi la watu ambao wangekuja kwa ajili tu ya kupata kitu chochote. Baada ya hapo, huduma ingekuwa endelevu tu kwa kuendelea kuwapa vitu. Hawangeweza kupata wa kuwasaidia bila kuwalipa kwanza. Hawangeweza kuwa na kikundi cha watu ambao wangekuwa ni chanzo kizuri cha wao kuweza kuanzisha kanisa.
Mfumo ambao Yesu alikuwa amewapa uliweza kuanzisha kikundi ambacho kingefanyika ni kanisa. Lilikuwa ni kundi la watu walisisimka na ujumbe wa injili na kutamani kusaidia. Ni muhimu sana kwamba makanisa yaweze kuanza katika njia iliyo sahihi.