Katika somo lililopita, tulijifunza kuhusu upendo wa kujitolea binafsi usiokuwa na masharti. Pia tulijifunza kwamba kuna angalau njia tano tofauti (lugha) ambazo ndani yake upendo unaweza ukadhihirishwa. Kwa kawaida watu wengi hutambua na kudhihirisha upendo kimsingi katika moja au mbili ya hizi njia tano.
Tulijadili kuhusu maneno ya kuthibitisha na tukagundua njia za kivitendo za kuwasilisha upendo wetu kwa wanafamilia. Kwenye somo hili, tutajifunza kuhusu aina nne zilizobakia za lugha za upendo, kisha tutafanya matumizi maalumu kwa ajili ya kudhihirisha upendo wetu kwa watoto wetu.
Lugha ya Upendo ya 2: Muda ulio Bora.
Watu ambao lugha yao ya msingi ya upendo ni Muda ulio Bora hujisikia kuwa wamependwa zaidi wakati watu wengine kwa kukusudia wanatenga muda wao binafsi ili kuwa pamoja nao. Muda huu unatengwa kwa uangalifu sana kwa ajili ya kuwa pamoja, mwelekeo ukiwa ni kwa kila mmoja. Ni muda wa kufurahia na kufanya ushirika pamoja.
Muda ulio bora hauji kwa bahati mbaya au kama muda wa ziada. Ikiwa umekwama kwenye foleni au unasubiri miadi, unapaswa kutumia muda huo kwa busara sana, lakini muda huo kwa kawaida si sawa na ubora wa wakati wa kawaida wa pamoja. Mwenzi au mtoto wako anaweza akafanya kazi kwenye mradi mmoja na wewe, na hilo ni jambo la thamani, lakini muda huo wa pamoja hauwezi siku zote ukakidhi hitaji lenu kwa ajili ya muda ulio bora pamoja nawe.
Mazungumzo yasiyoingiliwa na jambo lolote au kitu chochote ndiyo aina bora kabisa ya muda ulio bora. Katika mazungumzo ya aina hiyo, kila mtu anakuwa yuko makini kabisa kumsikiliza mwenzake. Kila mmoja hupuuzia usumbufu wa aina yeyote kama vile meseji zinazoingia kwenye simu au miito ya simu ili aweze kuuweka mwelekeo wake kwa mtu aliye naye na kwenye mazungumzo yao.
Hapa kuna njia nyingine chache ambazo wewe unaweza ukaonyesha na kudhihirisha kwamba unasikiliza kwa umakini mkubwa:
1. Dumisha mtazamo wa macho.
2. Sikiliza kiutendaji. Toa majibu kwa kile ambacho mtu mwingine anasema. Usifikirie tu kile ambacho utataka ukiseme baadaye. Badala yake, chukua muda wa kukagua uelewa wako kuhusu kile ambacho mtu mwingine anafikiria na kusema. Unaweza kuthibitisha kwamba unayaelewa mazungumzo kwa usahihi kwa kusema kitu kama, “Kama ninakusikia vizuri na kwa usahihi, unahisi kwamba….”
3. Usiingie katikati ya mazungumzo. Msikilizaji mara nyingi hujifikiria kwamba tayari ameshaelewa wazo na kwa haraka huingilia mazungumzo akitaka atoe maoni yake. Hali hii humfanya muongeaji kujisikia kana kwamba msikilizaji hakutaka kuchukua muda wa kuelewa kiuhalisia.
4. Sikiliza kwa kujisikia, na siyo tu kwa yale yaliyotendeka au kufanywa. Wakati tunapojaribu kutaka kuelewa mitazamo ya watu wengine, tunakuwa tunaonyesha kwamba tunafikiri mazungumzo ni ya thamani. Tunaposikiliza kwa umakini wote wa mioyo yetu, tunawasilisha kwamba maoni na hisia zao ni muhimu sana kwetu; na kwamba wao wenyewe pia ni muhimu kwetu!
Muda ulio bora zaidi ni wakati ambapo hufanyi jukumu lolote lakini unawasiliana na kila mtu, aina nyingine za muda pia ni za thamani. Familia zinaweza zikatumia muda ulio bora kwa pamoja kila siku kwenye muda wa chakula, wakiweka mwelekeo wao juu ya kila mmoja wanapokuwa wanakula kwa pamoja.
Kusoma hadithi kwa watoto wadogo, kucheza pamoja, au kufanya shughuli ya burudani pamoja ni njia nyingine ambazo familia zinaweza kutumia muda ulio bora kwa pamoja. Kufanya mradi au mambo ya ufundi kwa pamoja ambavyo ni kwa ajili ya kufurahisha tu, siyo kwa ajili ya shule, au kazi, au huduma, pia ni muda ulio bora.
Wakati mtu anapokuwa mbali na nyumbani kwake, muda ulio bora unaweza kutumika kwa kutembeleana kwa njia ya simu kwa ajili ya kuwasiliana pamoja.
Muda ulio bora ni uliotengwa, usiovurugwa, usioharakishwa katika kuweka mwelekeo na kufurahia ushirika wa kila mmoja. Ni bora zaidi kutenga muda ulio mzuri na mwenzi wako pamoja na watoto kila siku.
Wakati Muda unapokuwa Haujatengwa.
Wakati mwenzi au mzazi anapokuwa ni kiongozi wa huduma, ni vigumu sana kwake kutenga muda ulio bora pamoja na familia yake. Watoto wa mchungaji mara nyingi watakuwa wanahisi kwamba mtu mwingine anaweza kumwita na kumpata kwenye simu na kupata usikivu wa baba yao, lakini akawa ana shughuli nyingi akashindwa kuchukua muda wake kwa ajili yao. Inaweza ikaonekana kwamba muda kwa ajili ya familia unatolewa kafara kwa ajili ya huduma.
Vipingamizi haviwezi kuepukika kabisa kwa mtu aliyeko kwenye huduma, lakini ni lazima kujaribu kutenga muda kwa ajili ya familia. Kama utafanya hivyo, watakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kuelewa majukumu yako ya kawaida na usumbufu wa ziada unaojitokeza ambao hauwezi kuepukika.
Mtu ambaye lugha yake ya msingi ya upendo ni muda ulio bora hujisikia anayependwa kwa kiasi kidogo sana wakati anapokuwa hana muda wa makusudi na muda wenye mwelekeo na familia yake. Hujisikia kujeruhiwa sana wakati muda ulio bora haupewi kipaumbele, na wakati ambapo mipango iliyopo kwa ajili ya muda ulio bora inapowekwa pembeni wakati Vipingamizi vinapojiinua. Inakuwa ni vigumu sana kwake wakati familia yake inapokuwa na shughuli nyingi za kuwafanya washindwe kuwasiliana na yeye. Hujisikia mwenye kuthaminika kwa kiasi kidogo sana wakati wanafamilia wanapokuwa hawamsikilizi wakiwa na umakini uliogawanyika.
Kama unashindwa kumpa mwenzi au mtoto wako umakini na uangalifu wa binafsi, hawawezi kuhisi upendo ulio nao kwao, ingawaje unafanya mambo mengi kwa ajili yao. Mwanamume anaweza akawa anafanya kazi ngumu kwa ajili ya familia yake, lakini bado mke wake akajisikia kwamba hapendwi kwa kuwa mume wake ana shughuli nyingi sana zinazomfanya akose kuwa na wakati pamoja naye.
Mvulana mdogo alikwenda kwa baba yake kumwelezea hadithi ambayo alikuwa ameisikia katika siku za karibuni. Baba yake alikuwa anasoma kitabu, lakini akatulia ili aweze kumsikiliza kwa dakika moja, kisha akaendelea na kusoma kitabu chake wakati kijana wake akiwa katikati ya masimulizi ya hadithi yake. Katika maisha yake yote yaliyoendelea, kijana alikuwa anakumbuka jinsi alivyokuwa amejisikia katika wakati ule.
► Je, muda ulio bora kwa kawaida unaonekanaje ka familia yako? Je, ni matatizo gani uliyo nayo ya kuyashinda ili uweze kutumia muda wako wenye maana pamoja na familia yako?
Lugha ya Upendo ya 3: Zawadi
Watu ambao lugha yao kuu ya upendo ni kupokea zawadi hujisikia kuwa wanaopendwa zaidi sana wakati watu wengine wanapowapa kitu ambacho kinaonyesha kwamba walikuwa wanawafikiria.
Zawadi zinazoweza kuwafanya watu wajisikie kama wanaopendwa ni zawadi ambazo zinatolewa kwa kufikiria sana. Zinachaguliwa kwa kuangalia hali ya matamanio ya mpokeaji. Siyo lazima ziwe za vitendo au ambazo zinazohitajika. Zawadi za upendo hazitolewi tu kwa sababu mtoaji alikuwa hazihitaji tena. Zawadi zinatakiwa zichaguliwe kwa makusudi fulani au zitengenezwe na mtoaji mwenyewe.
Zawadi inayomfanya mtu ajisikie kwamba anapendwa siyo lazima iwe ya gharama kubwa. Inaweza ikawa ni kitu kisichodumu kwa muda mrefu kama vile, chakula maalumu au peremende; au inaweza ikawa ukumbusho wa kudumu unaoonekana kuwa wenye uhusiano na mtoaji.
Kwa mtu ambaye lugha yake kuu ya upendo ni kupokea zawadi, siku za kuzaliwa, maadhimisho ya kumaliza miaka kadhaa, na siku za mapumziko ni za muhimu sana. Ni muhimu sana kwa ajili ya wanafamilia kukumbuka siku hizi wakiwa pamoja na zawadi maalumu kwa ajili ya mtu husika. Kutokupokea zawadi katika sikukuu hizi maalumu kiuhalisia inakuwa ni kuchungu sana kwa huyu mtu.
Kutoa zawadi hakupaswi kufungamana na siku maalumu tu, ingawaje; inapaswa kiwe ni kitu endelevu katika maisha. Mwanandoa, mzazi, au mtoto wa mtu fulani ambaye lugha yake ya msingi ya upendo ni kupokea zawadi anapaswa ajenge tabia ya kuangalia zawadi ambazo zitawasaidia wapendwa wao kukumbuka kwamba wanafikiriwa na kupendwa.
Mke ambaye lugha yake ya msingi ya upendo ni kupokea zawadi anaweza akajisikia asiyependwa kabisa kama atafikiria kwamba mume wake alijaribu kuokoa gharama kwa kumpatia zawadi ambayo ingeweza ikaonekana kama tu ni muhimu. Labda anahitaji ufagio mpya, na akamletea ufagio mmoja. Ni vyema kwake kuwa na huo ufagio, lakini zawadi hiyo haiwezi kumsaidia ajisikie kwamba anapendwa.
Zawadi ni za muhimu wakati zinapodhihirisha kwamba mtoaji alikuwa anaelewa na kujali kuhusu anayekwenda kuipokea zawadi hiyo. Zinakuwa ni za muhimu wakati ambapo kulikuwa hakuna ulazima huo. Zawadi inakuwa muhimu wakati mtu anapokuwa amejifikiria, akaweka juhudi na gharama katika kuipata.
Watoto ambao lugha yao kuu ya msingi ya upendo ni kupokea zawadi hujisikia kupendwa zaidi wakati baba anapowanunulia aiskrimu kuliko anapowalipia malipo yao ya shule, ingawaje malipo ya shule ni makubwa na muhimu zaidi. Badala ya kudai kwamba wanafamilia wakubaliane na kile ambacho ulikuwa unakitoa kama utaratibu wa mazoea wa kawaida, tafuta njia ya kufanya jambo ambalo litakuwa ni maalumu kwao.
Watu wengine huwafanya watoto au wenzi wao kuwa waombaji wa kila kitu. Mtu anayetumia fedha sana na mara chache hujinunulia vitu kwa ajili yake mwenyewe anaweza asione kuwa ni jambo rahisi kuwa mkarimu na kutoa zawadi zinazoonekana kwake kwamba siyo muhimu. Anakuwa hataki wanafamilia wake waanze kutegemea kupata zawadi kutoka kwake. Lakini kama angekuwa na mwenzi wake au mtoto ambao zawadi ni muhimu kwao, atafanya kazi ya ziada ili kuishinda tabia yake ya kawaida. Atajaribu kuziona zawadi kama zinavyoonekana kwao – zenye umuhimu na thamani. Wakati wa kutoa zawadi, toa kwa uhuru, ukiwa na furaha!
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Wakorintho 9:6-9 kwa ajili ya kikundi. Kwenye kifungu hiki, Paulo anawaasa Wakorintho waliookoka kwamba watoe kwa ukarimu kwa waumini wenzao walio katika uhitaji. Kutokana na Aya hizi, jaribu kutambua aina nne au tano za motisha kwa ajili ya ukarimu. Je, ni kwa njia gani kanuni hizi kutoka katika Aya hizi zinavyotumika kwa ajili ya ukarimu ndani ya wanafamilia wetu?
► Je, utoaji zawadi una nafasi gani katika familia yako? Je, unapata matatizo yoyote katika kudhihirisha upendo kupitia utoaji wa zawadi? Je, matatizo hayo ni yapi na ni kwa jinsi gani unaweza kuyashinda?
Lugha ya Upendo ya 4: Matendo ya Huduma
Watu ambao lugha yao ya msingi ya upendo ni matendo ya huduma hujisikia kupendwa zaidi wakati watu wengine wanapofanya mambo kadhaa kwa ajili yao.
Matendo ya huduma yanakidhi mahitaji ya vitendo. Yanaweza yakawa au yasiwe kwamba ni mambo ambayo mtu alikuwa anashindwa kufanya kwa ajili yake mwenyewe. Huduma inaweza kuwa ni rahisi sana kama vile mtu anapokuwa anampatia mtu mwingine kinywaji. Inawezekana ikawa ni kumtunza mtu ambaye ni mgonjwa. Inaweza ikawa ni kusaidia mtu katika hali ya uhitaji.
Kwenye familia nyingi, kunatokea kuwepo na vipindi vya muda mrefu ambavyo mwanafamilia mmoja atahitaji apewe uangalizi binafsi wa kila wakati. Kwa sababu ya upendo wa familia na kujitolea kwa ajili ya mtu huyo, wanaendelea kufanya vitendo vingi vya huduma kwa ajili yake. Ingawaje muda mwingi huwa unatengwa kwenye matendo ya huduma, wanafamilia wanapaswa kudhihirisha upendo kwa mtu mwingine, kwa njia yenye maana pia, hasa kama lugha ya msingi ya upendo ya mtu siyo matendo ya huduma.
Baadhi ya vitendo vya huduma hasa vya kufanana ni mpangilio wa kawaida wa kila siku na vinaweza vikadharauliwa au vikachukuliwa kama ni vya kawaida tu. Wanawake wengi wanadhihirisha upendo wao kutokana na vyakula vizuri wanavyopika kila siku na kutunza nyumba. Mwanamume anaweza kufanya kazi kwa ajili ya kutoa matumizi kwa familia yake. Kama tayari unaihudumia familia yako kila siku katika njia kama hii, bado unatakiwa utafute njia nyingine maalumu za kufanya matendo ya huduma kwa ajili ya wanafamilia wako kwa njia hii ya msingi ya lugha ya upendo.
Wakati mwanamke anapoonyesha kutokuwa na shauku na mahitaji madogo ya mumewe, anashindwa kuzungumza lugha hii ya upendo. Labda anafikiri kwamba, “Anaweza akajichukulia maji ya kunywa yeye mwenyewe.” Lakini kama atanyanyuka na kumchukulia hayo maji ya kunywa, itadhihirisha kwake upendo wake maalumu.
Vivyo hivyo, mume naye anapaswa kuonyesha kumfikiria mwenzake. Wakati anapompa mke wake mapumziko kutokana na jukumu ambalo kwa kawaida analifanya, kwa kufanya jambo hilo kwa ajili yake, anampa heshima kwa jukumu lake na anatambua kwamba kazi yake ni ngumu na ni ya muhimu.
Mume anaweza kuhisi kwamba tayari anafanya kazi za kutosha, na kwamba jukumu la mke wake ni kushughulikia kazi zote za nyumbani. Anaweza hata kufikiri kwamba anapaswa kuwa na ufanisi zaidi kuliko alivyo. Ikiwa anadhani kwamba kazi za nyumbani ziko chini ya hadhi yake, inaonyesha kwamba anawachukulia wanawake kama wa chini na wanaostahili kazi za chini. Wanawake si wa chini, na kazi za nyumbani si za chini zaidi kuliko kazi za nje ya nyumba.
Mwanamume anaweza kujihisi kwamba ni kama anafanya jukumu la mtumishi wa nyumbani (aliye chini ya mke wake) wakati anapokuwa anasaidia kufanya kazi za nyumbani, lakini hivyo siyo kweli. Kama atajitolea kufanya kwa kutoa utumishi huo, anaonyesha thamani ya kazi hiyo na thamani ya mtu ambaye anamsaidia kufanya kazi hizo. Utumishi wake humheshimu mtu ambaye kwa kawaida ndiye anayefanya majukumu hayo na huonyesha uthamini wake kwao. Mkewe hatamwona mume wake kama ni mtumishi tu bali pia anayeheshimika zaidi.
Iwapo watu wanasaidiana kwa hasira na kwa shingo upande, wanaonyesha kwamba wanaolazimishwa kusaidia. Kitendo chao cha kufanya huduma hakiwasilishi dhana ya upendo. Kama watafanya matendo ya huduma kwa uaminifu na kufanya kwa juhudi zao zote, itaonyesha kwamba wako huru kuchagua kuhudumia, kwa sababu hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwalazimisha kufanya huduma kama hiyo. Huduma hii ya furaha hudhihirisha upendo kwa uwazi. Inasaidia pia kupata heshima kutoka kwa wapendwa wao.
► Je, ni wakati gani unaouona ni mgumu kwako kutoa huduma kwa familia yako? Je, ni kwa jinsi gani kufikiri kuhusu huduma kama udhihirisho wa upendo kunavyobadilisha mtazamo wako?
Lugha ya Upendo ya 5: Mguso wa Kimwili
Watu ambao lugha yao kuu ya upendo ni mguso wa kimwili hujisikia kuwa wanapendwa zaidi wakati wanapoguswa kwa upendo na wanafamilia wao.
Kuna njia tofauti za kuonyesha upendo kupitia mguso wa kimwili. Baadhi zinafaa na ni sahihi katika mahusiano kadhaa lakini siyo yote, na katika mazingira fulani lakini zinakuwa hazifai katika mazingira mengine ya mahusiano. Hapa kuna mifano michache:
Kukumbatiana
Kuweka mikono kuzunguka mgongoni na juu ya bega la mtu
Kuwekeza mikono yako juu ya mabega ya mtu
Kupapasa mgongo au bega la mtu
Kukaa pamoja
Kushikana mikono
Kila mmoja kumbusu mwenzake
kukanda mgongo
Kumshikilia mtoto
kuchana nywele za mtoto
Kutoa huduma ya taratibu na kwa upole wakati mtu akiwa ni mgonjwa au akiwa ana udhaifu mwingine wa kimwili
Mguso pia unaweza kuwa na maana ya kipekee wakati mtu anapokuwa anapitia katika wakati mgumu wa maisha. Wakati wa huzuni, uchungu, upweke, na mfadhaiko, kukumbatiana na kupeana busu kunaweza kuwa na maana zaidi kwa mtu ambaye lugha yake ya msingi ya upendo ni mguso wa kimwili kuliko maneno au matendo ya huduma mengine yoyote.
Kwa mtu ambaye lugha ya msingi ya upendo ni mguso wa kimwili, ni muhimu kuendelea kudhihirisha upendo wako kimwili hata wakati ambapo wao ni wagonjwa, ikiwa uwezekano huo utakuwepo. Kumbuka kwamba upendo siyo wa masharti na ni wa kujidhabihu binafsi. Yule baba katika Luka 15:20 alimkumbatia na kumbusu mtoto wake aliyekuwa ametubu, ingawaje mtoto huyo alikuwa ananuka harufu mbaya, alikuwa mchafu, na asiyependeka kwa njia yeyote ile.
Lugha ya upendo ya mguso wa kimwili siyo lazima iwe kuhusu kujamiiana. Shughuli ya kujamiiana ni kategoria ya mguso. Matamanio ya kugusa na kuguswa inaweza kupelekea kuwa ni kichocheo na udhihirisho wa kusababisha tendo la kujamiiana, lakini tendo la kujamiiana peke yake halitamtosheleza mtu ambaye lugha yake ya msingi ya upendo ni mguso wa kimwili.
Matamanio ya kuhisi kwamba unapendwa kupitia mguso wa kimwili yanaweza kumfanya mtu ashawishike kuingia kwenye tendo la uasherati. Ni muhimu sana kwa wazazi kutoa midhihirisho ya kutosha isiyohusiana na mambo ya kujamiiana ya mguso wa kimwili kwa vijana wao wa kike na wa kiume, ili kwamba mahitaji ya watoto wao ya mguso wa kimwili yaweze kufikiwa. Mtoto anayejisikia kupendwa ana ujasiri mzito wa kujizuia na vishawishi au majaribu.
Dhambi Zinazotokana na Mguso wa Kimwili
Wale ambao lugha yao kuu ya upendo ni mguso wa kimwili wanahisi kuumizwa au kuvunjiwa heshima na ukatili wa kimwili. Kumpiga mtu kwa hasira (Wagalatia 5:20), Kumpiga mtu makofi usoni kwa madhumuni ya kumdhalilisha (Mathayo 5:39) au kumpiga mtu kama matumizi mabaya ya mamlaka (Mathayo 24:48-49) ni kufanya uovu. Kutokana na maandiko haya, tunajua kuwa wazazi kamwe hawana haki ya kuwaumiza watoto wao, hata kama wanahisi hasira na kuchanganyikiwa. Mungu pia anasema kwamba ni uovu kwa watoto kuwapiga wazazi wao (Kutoka 21:15).
Nidhamu ya kimwili ifaayo na inayodhibitiwa ya watoto inayotolewa na wazazi kwa roho ya upole (Wakolosai 3:21), kwa ajili ya kuwasahihisha na kuwaongoza kwa ya haki, siyo dhambi. Badala yake, ni takwa la Mungu kwa wazazi la kuwawezesha kuokoa nafsi za watoto wao (Mithali 13:24, Mithali 19:18, Mithali 29:15, Waebrania 12:5-7).
Vitendo vyote vya uasherati na unyanyasi wa kingono, pamoja na kujamiiana watu wa ukoo mmoja ni uovu (Mambo ya Walawi 20:11-12, 14).
Kutambua Lugha yako kuu ya Upendo
Watu si mara zote wanatambua lugha yao kuu ya upendo. Wanaweza hata wasiwe wanafikiria kuhusu njia ambazo watu wengi mara nyingi hudhihirisha upendo wao kwa watu wengine. Wanaweza hata wasiwe na ufahamu kuhusu mambo mengine yanayofanywa na watu wengine ambayo yanawafanya watu wao wajisikie wanapendwa. Chukua muda kidogo wa kutafakari tena kuhusu yale unayoyajua kuhusu lugha tano za upendo.
► Je, ni kwa lugha gani ya upendo ambayo unaitumia zaidi sana katika hali ya kawaida na mara kwa mara katika kudhihirisha upendo wako kwa ajili ya watu wengine?
► Je, lugha yako kuu na ya pili ya upendo ni zipi? Ikiwa unapata ugumu kutambua ni maonyesho yapi ya upendo yanayokupa maana zaidi kwako, hapa kuna maswali kadhaa ya kukusaidia kupata jibu kamili:
Je, ni mifano gani ya mambo yanayokufanya wewe uwe na furaha?
Je, mambo yako muhimu ya kukumbuka unayopendelea sana ni yapi?
Je, huwa unalalamika kuhusu mambo gani (hata katika ukimya tu)?
Je, ni mambo gani yanayokufanya wewe ujisikie kuumizwa sana?
Lugha Tano za Upendo na Watoto
Watu wote mara kwa mara wanahitaji kupokea udhihirisho wa upendo katika lugha zote tano za upendo, lakini jambo hili ni la kweli hasa kwa watoto. Ili watoto waweze kuwa sawasawa, watoto wenye afya kihisia, wanahitajika kuambiwa mara kwa mara na kila wakati kwamba wanapendwa na wazazi wao bila ya masharti yoyote. Wazazi wanapodhihirisha upendo wao kwa ajili ya watoto wao kwa njia mbalimbali, mara nyingi kila siku, ni kama mvua inayonyesha polepole na kuitunza ardhi ya mioyo ya watoto wao.
Usitake kudhania kwamba watoto wanajua na wanajihisi upendo wako kwa ajili yao. Ni lazima mara kwa mara na kila wakati waone ukidhihirisha upendo wako katika lugha yao ya msingi ya upendo na pia katika lugha nyingine za upendo.
Kutambua Lugha ya Msingi ya Upendo ya Mtoto
Gary Chapman na Ross Campbell wametoa orodha ya mawazo ya jinsi utakavyoweza kugundua lugha ya msingi ya upendo ya mtoto wako:[1]
1. Angalia kwa makini ni kwa jinsi gani mtoto wako anavyodhihirisha upendo wake kwako.
2. Angalia kwa makini ni kwa jinsi gani mtoto wako anavyodhihirisha upendo wake kwa watu wengine.
3. Kuwa msikivu na yale mambo ambayo mtoto wako anaomba mara kwa mara.
4. Tambua yale mambo ambayo mtoto wako anayalalamikia mara kwa mara.
5. Mpatie fursa mtoto wako awe na uchaguzi kati ya mambo mawili ya kuchagua.
Huenda isiwezekane kubainisha lugha ya msingi ya upendo ya mtoto kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.
Vidokezo maalumu kuhusu Lugha za Upendo kwa ajili ya Watoto.
Hatutaingia kwa kina kuhusu kila kipengele cha lugha za upendo hapa kwani kila kimoja kilishajadiliwa hapo awali. Badala yake, tutazingatia tu vidokezi maalumu na matumizi yake kwa ajili ya kuonyesha upendo kwa watoto.
Maneno ya Uthibitisho.
Inajitokeza kuwa ni vigumu kutoa uthibitisho hasa wakati ambapo mtu kila mara anafanya makosa na hatendi vizuri. Lakini kama unaweza kutafuta au kupata kitu cha ukweli na chenye kuthibitisha kwa kusema, kinaweza kuwahamasisha watoto wako, na kuna uwezekano mkubwa kwamba wao wenyewe watakuwa na uwezo wa kukua.
Muda ulio bora.
Ni jambo la manufaa sana kwa familia kula pamoja angalao mlo mmoja kwa siku na kuweka mwelekeo wa kutembeleana wakati huo.
Katika familia mbalimbali zilizo na watoto wengi, n rahisi kupuuzia suala la muda ulio bora pamoja na mtoto binafsi. Hata hivyo, kutenga muda wa kuweza kufanya jambo la kipekee na kila mtoto binafsi kutawasaidia kujihisi upendo wako kwao. Muda wa kuwa katika faragha nao pia kunawapa nafasi isiyokuwa na usumbufu ya kushirikishana mawazo binafsi ambayo wangekuwa hawako tayari kuyashirikisha wakiwa mbele ya ndugu zao au wanafamilia wengine.
Mara nyingi, watoto wataomba kwa ghafla kuwa na muda ulio bora wa kukaa peke yao na mmoja wa wazazi wao. Wakati mwingine katika kipindi cha kulala mtoto mmoja anaweza kuwa wazi na kuomba kuongea na mzazi juu ya jambo fulani ambalo linawaumiza na au kuwaelemea katika mioyo yao. Ni muhimu sana kwa wazazi kupata muda wa kuwasikiliza watoto wao katika nyakati hizi. Mara nyingi, mtoto anashughulika na jambo la kiroho, na kwa kuja kwa mama na baba yake faraghani, anatafuta kupata msaada wa kiroho. Wazazi wana nafasi maalumu ya kuwaongoza watoto kwa Yesu katika nyakati hizi.
Katika wakati wako bora na watoto wako, jifunze kuwauliza maswali ya wazi ambayo yatakusaidia wewe kuelewa jinsi wanavyofikiri, na ni kwa jinsi gani wanavyojihisi. Maswali ya wazi hayawezi kujibiwa kwa maneno, “Ndiyo” au “Hapana.” Maswali ya wazi hayana jibu maalumu. Maswali ya wazi kwa kawaida huanza na “Kwa nini…” “kwa vipi…” au “Nini…” Mazungumzo ya wazi huanza na misemo kama, “Niambie kuhusu…” au “Je, unafikiria nini kuhusu….”
Mtoto wako anapokuwa anajibu swali lako, hakikisha unakuwa makini sana kusikiliza majibu yao na kuchukua hatua ipasavyo. Katika nyakati nyingine utaweza kutaka kuuliza swali la kufuatilia. Wakati mwingine utataka kubainisha kuhusu maswali yao ili kutaka kuhakikisha kwamba unaelewa kile wanachojaribu kuelezea. Wakati mwingine unapaswa kuwathibitisha katika kile ambacho wanakiona na kukihisia. Ni muhimu sana kwamba mtoto asijisikie kana kwamba anahojiwa, lakini mazungumzo yawe ya asili na kawaida. Umakini wako wa kusikiliza utamsaidia mtoto wako kujisikia kwamba anasikilizwa, anathaminiwa, na kupendwa.
Kuchukua muda hasa katika kumsikiliza mtoto akielezea hadithi yake pia kunawasilisha upendo wako kwake katika njia ambayo ni ya muhimu sana kwa ajili yao. Kuchukua muda wako ili kuwasiliana nao hadithi au jambo la historia pamoja na kusoma vitabu ni njia nzuri ya kushiriki muda ulio mzuri kwa pamoja.
Kucheza michezo pamoja au kufanya mradi wa kufurahisha pamoja ni njia nyingine ya kushirikishana muda ulio bora pamoja na watoto wako.
Wazazi wengine hawawapatii watoto wao muda ulio bora. Wanajaribu kufidia hili kwa kuwapa watoto wao zawadi. Zawadi haziwezi kuwa mbadala wa muda ulio bora. Watoto wanahitaji muda ulio bora zaidi na wazazi wao, haijalishi lugha yao ya msingi ya upendo ni ipi. Hakuna kiwango chochote cha zawadi kitakachoweza kuwa mbadala wa kutumia muda ulio bora na watoto wako.
Zawadi
Ni mara chache sana wazazi kuwanunulia watoto toyi za kuchezea au vitabu vya hadithi au vya kuvutia., kwa sababu vitu hivyo vinaonekana havina ulazima. Vitu hivyo vinaweza kusaidia sana ukuaji wa mtoto, mbali ya kuwa ni udhihirisho wa upendo.
Matendo ya Huduma
Mawazo bainifu ya kudhihirisha upendo kwa ajili ya mtoto wako kwenye matendo ya huduma:
Andaa chakula wanachokipenda kwa ajili ya kumbukumbu ya sikukuu zao za kuzaliwa.
Wapatie utunzaji wa huruma wanapokuwa wagonjwa.
Msaidie mtoto wako katika kuifanya kazi aliyopewa shuleni.
Fanya kazi za nyumbani na mtoto wako na uonyeshe shukrani kwake kwa kazi yake aliyoifanya.
Fanya kitu chenye msaada pamoja na mwanao kwa ajili ya mtu mwingine ambaye siyo wa nyumba yenu.
Mguso wa Kimwili
Watoto wadogo na pia wale wachanga ni lazima wapate upendo kupitia mguso wa kimwili. Watoto wachanga wana mahitaji yao ya vitendo, kama vile kulishwa chakula na kubadilishiwa nepi zao, lakini pia wanahitaji kushikwa, kubebwa, kubembelezwa, na kubusiwa. Mguso huu wa upole wa kimwili huwasilisha upendo kwa njia wanayohisi ni muhimu kwao kwa ajili ya mhemuko wa kiafya na kiakili.
Kwa baba kuvurumishana na watoto wake inaweza kuwa ni udhihirisho wa upendo kwao. Ushindani huo haupaswi ulete hatari ya kuumiza, kuacha kutawala, kushindwa kudhibiti, au kusababisha hasira.
Athari za muda mrefu za Matendo na Maneno ya Mzazi
Wazazi wanapaswa wafuate mfano wa Mungu katika kushughulika kwao na watoto wao. Mungu siku zote huwarudi watoto wake kwa upendo mkamilifu, wa kujitolea, na usio na masharti. Anaadabisha kwa nidhamu, anasahihisha, na kuwafundisha watoto wake kwa sababu ya upendo wake alio nao kwa ajili yao (Waebrania 12:5-7). Ni katika muktadha huu wa uhusiano wa baba na mtoto ambao unafanya kazi ndani ya maisha ya watu waliookoka ili kuwafanya wamfafananie yeye (Waebrania 12:10-11).
Siyo jambo la kufaa kwa upendo wa wazazi uwe kwenye kushikamanishwa na tabia ya watoto wake. Bila shaka, zawadi chanya au matokeo mabaya kwa ajili ya tabia za watoto wao ni sehemu ya mkakati wa kumfundisha mtoto, lakini udhihirisho wa upendo haupaswi usitishwe kutolewa au uzuiwe kwa ajili ya tabia ya mtu.
Ikiwa mtoto mara kwa mara anakuwa katika upendo wa wazazi wake usiokuwa na masharti kwa wepesi zaidi anaweza kumfahamu na kumwamini Mungu kwa ajili yake mwenyewe. Hata hivyo, ni vigumu zaidi kwa wale ambao walikuwa wamenyanyaswa na kukataliwa kama watoto kuweza kuelewa na kuamini katika upendo wa Baba wa Mbinguni, hata pale wanapokuwa wameshakuwa watu wazima.
Watoto kujielewa wenyewe- hasa thamani yao kama watu binafsi – takribani siku zote unatoka kwa yale mambo wanayoyasikia na kutambua kutoka kwa watu wengine. Matendo na maneno ya wazazi wao ni yenye ushawishi zaidi, lakini wanajamii na marafiki wana mguso mkubwa pia. Aidha iwe watoto wanapata au hawapati udhihirisho wa upendo ambao wanauhitaji inakuwa ni aina ya kile kitu ambacho kinaunda muonekano wao wa binafsi. Wakati upendo unapokuwa umeondolewa kwa watoto, au watoto wakakutana na unyanyasaji wa mihemuko au kimwili, inabomoa na kuharibu taswira ya uthamani wao katika njia ambayo inavuruga maisha yao yote.
Maneno ya wazazi huleta ushawishi wa uelewa wa watoto wao wenyewe. Kwa mfano:
Maneno ya uthibitisho: “Ninajivunia wewe kwa kufanya kazi kwa bidii sana! Najua una uwezo wa kufanya hivyo!” hii ni kuwaambia watoto kwamba jitihada zinafaa na kwamba unaamini wanaweza kufaulu.
Maneno yenye kuleta uharibifu: “Wewe ni mvivu sana. Siwezi nikakutegemea wewe kwa lolote!” Katika hali hii unaweza kusababisha mtoto kuamini kwamba hana uwezo wa kubadilika; hakuna sababu ya kujaribu kubadilika au kupata heshima yako, kwa sababu tayari umeshakata tamaa juu yao. Inaweza ikawafanya au ikajenga hisia kwa watoto kujisikia kwamba umeshawakataa.
Maneno ya uthibitisho: “Ni sawa. Sisi sote wakati mwingine hufanya makosa, na kisha tunajifunza jinsi ya kufanya vizuri zaidi wakati mwingine.” Hii ni kuwaambia watoto kwamba ni jambo salama kufanya makosa – upendo wako kwao hautegemei utendaji wao ambao hauna dosari. Pia hii ni kuwaambia watoto kwamba wategemee kuwa na uwezo wa kukua, na kwamba kuna kila sababu ya kuendelea kujaribu.
Maneno yenye kuleta uharibifu: “Wewe ni mpumbavu sana. Kila wakati wewe unavuruga.” Hali hii inaweza kusababisha mtoto akaamini kwamba ni ujinga kutaka kujaribu. Inaweza ikawasilisha ujumbe kwao kwamba thamani yao inategemea utendaji mkamilifu; na kwa kuwa wakati wote wanavuruga, kamwe hawana tena uwezo wa kuwa watu wa thamani. Hawatakuwa na thamani ya kupendwa tena…na wewe mwenyewe au na mtu mwingine yeyote.
Kujielewa kwa mtoto yeye mwenyewe kama mtu kunategemezwa na upendo ambao unawasilishwa au unashikiliwa kutoka kwake. Uwezo wake wa kujihusisha na watu wengine katika njia zenye ubora ni kwamba, aidha kunakuzwa au kunalemazwa na uhusiano wake na mzazi wake. Mtoto anayependwa vizuri ana uwezo wa kujifunza ya kuwapenda watu wengine kwa upendo wa kujitolea kabisa, usiokuwa na masharti. Pia ana hifadhi ya upendo ambayo anaweza kuitumia.
Upendo wa kweli ni mafuta ya mhemuko kwa ajili ya watoto, kama na vile ilivyo kwa watu wazima.
Faida za Tanki Lililojaa Hisia.
Kuna njia nyingi ambazo watoto hupata faida kutokana na kuwa na matanki ya mafuta ya hisia. Wakati watoto wanapojijua kwamba wanapendwa, wanakuwa na nguvu na utulivu wanaohitaji ili kukabiliana na changamoto na kukua ipasavyo.
Watoto wanaojijua kwamba wanapendwa bila ya masharti wanakuwa wako salama kihisia. Kwa sababu hiyo, wanakuwa na utayari zaidi wa kukubali nidhamu, masahihisho, na mwongozo kutoka kwa wazazi wao kuliko wangekuwa vinginevyo. Pia wanakuwa na uwezo wa kukataa vishawishi ambavyo husababishwa na makundi rika, kwa sababu wako salama kwa jinsi tu walivyo, na hawahitaji kujithibitisha wenyewe kwa watu wengine.
Msichana ambaye huchezea hisia za wavulana anaweza kuwa anafanya hivyo kwa sababu anaogopa kuwa, kama hatafanya hivyo, hawatampenda wala kumtilia maanani.
Msichana ambaye anaona aibu kwa wavulana anaweza kuogopa kwamba hawatampenda ikiwa ataonyesha tabia yake halisi. Binti ambao wanapokea uthibitisho na upendo kutoka kwa baba zao wana uwezo wa kuchangamana vizuri na vijana kwa njia zilizo nzuri na usahihi bila ya kuwachokoza au kuona aibu. Wanakuwa salama kwenye utambulisho wao kwa sababu ya upendo wa baba zao.
Upendo wa kweli wa wazazi usiokuwa na masharti unaodhihirishwa mara kwa mara katika lugha zote tano za upendo huwalinda watoto dhidi ya madhara mengi. Watoto wanaopendwa vizuri hawatafuti upendo na usalama kutoka kwa watu wengine ambao wana dhamira ya kuwadhuru.
Kwa muhtasari, kuna faida nyingi za kuwa na tanki lililojaa mafuta ya hisia kama mtoto:
Uelewa sahihi wa thamani ya mtu na chanzo chake.
Uelewa sahihi wa juhudi, makosa, ukuaji, na upendo usiokuwa na masharti.
Uwezo wa kujifunza jinsi ya kuwapenda watu wengine vizuri.
Nguvu na uimara wa kukabiliana na changamoto na kujiendeleza ipasavyo.
Usalama Kihisia.
Uwezo wa kukubaliana na nidhamu, masahihisho, na mwongozo.
Uwezo wa kukataa vishawishi vibaya kutoka kwa makundi rika.
Hawako katika hatari ya kudhalilishwa kwenye mahusiano ya baadaye.
► Je, ni njia gani nyingine umeona ambazo watoto hufaidika kutokana na kupendwa inavyopaswa?
Hasara za Tanki Tupu la Kihisia.
Watoto wanaohisi kwamba hawapendwi wanaweza wakapingana na miongozo inayotolewa kwao kwa sababu wanakosa hamasa ya kuwafurahisha mama au baba. Bila kuwa na tanki lililojaa mafuta ya hisia, watoto wengi hukosa uhusiano wenye nguvu na wa kimaadili wa uaminifu kwa wazazi ambao wanajaribu kuwaongoza.
Watoto ambao matanki yao ya mafuta ya hisia yako matupu wako katika hali ya hatari zaidi kuliko watoto walio katika mahusiano ya upendo wenye nguvu kubwa na wanafamilia wao. Kwa kuwa hawajisikii kwamba wanapendwa, wanaweza kutafuta kupendwa na watu ambao wanapenda kuwatumia na au kuwaletea madhara.
[1]Dr. Gary Chapman and Dr. Ross Campbell, The Five Love Languages of Children, (Northfield Publishing, Chicago, 1997), 101-103.
Sifa za Familia zilizo Imara
Katika mafundisho haya tumejifunza kuhusu aina tano za lugha za msingi za upendo. Ijapokuwa watu huwa na lugha moja au mbili za msingi za upendo, kila mtu anahitaji kupendwa mara kwa mara katika aina zote tano. Familia iliyo imara ni ile ambayo kila mtu kwa makusudi au malengo hukuza mahusiano na watu wengine kwa kila siku kuzungumza maneno yenye kudhihirisha upendo, kutumia muda ulio bora kwa pamoja, matendo ya huduma, na kutumia mguso wa upendo wa kimwili. K utoa zawadi kwa mtu mwingine inaweza isiwe tukio la kila siku lakini bado ni sehemu nyeti ya mahusiano yaliyo imara ndani ya familia.
► Je, ni kwa jinsi gani upendo hudhihirishwa mara kwa mara kwenye familia yako? Je, upendo hudhihirishwa katika aina zote tano za lugha za msingi za upendo? Je, udhihirishwaji wa upendo unashirikishwaje mara kwa mara?
Uchunguzi wa miaka 25 usiokuwa wa kidini kutoka katika familia 14,000 unaonyesha kwamba familia nyingi zilizo imara, zilizofanikiwa na zilizo na malezi yaliyokamilika kutoka katika malezi ya tamaduni mbalimbali zinashirikisha sifa kuu sita zinazofanana.[1] Baadhi ya sifa hizo zina uhusiano wa moja kwa moja na lugha mbalimbali za upendo, jambo linaloonekana kwamba kuna msisitizo wa udhihirisho wa aina mbalimbali kuhusiana na upendo. Stinnett na Beam waliorodhesha hizo sifa sita na kuzitolea maelezo kwa kila moja:
1. Kujitolea. Wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu wanakuwa wamedhamiria kukuza ustawi na furaha ya kila mmoja. Wanathamini umoja wa familia.
2. Kuthamini na kupendwa. Wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu huonyesha kuthaminika kwa kila mtu mara kwa mara. Wanaweza wakajisikia kwamba familia zao ni nzuri.
3. Mawasiliano chanya. Wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu wana ustadi mzuri wa kuwasiliana na hutumia muda wao mwingi sana kuzungumza na kila mmoja.
4. Muda wa kukaa pamoja. Wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu hutumia muda ulio bora kwenye mambo mengi ya ukarimu – na kila mmoja.
5. Ustawi wa kiroho. Aidha wawe wanakwenda kwenye ibada za kidini au hawaendi, wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu wana hisia zilizo kubwa za mambo mazuri au yenye nguvu katika maisha.
6. Uwezo wa kukabiliana na msongo wa mambo au migogoro.Wanafamilia katika familia zilizo imara na zenye nguvu wana uwezo wa kuona msongo wa mambo na au migogoro kama fursa za kukua.
[1]Dr. Nick & Nancy Stinnett and Joe & Alice Beam, Fantastic Families: 6 Proven Steps to Building a Strong Family, (Brentwood, TN: Howard Books, 2008)
Matumizi Binafsi
Tumezingatia mambo mengi katika mafundisho au masomo haya mawili. Tulianza na majadiliano kuhusu upendo wa kweli, kisha tukazitambua aina tano za lugha ambazo kwa kawaida hutumika kuwasilisha upendo. Tumejifunza kuhusu matanki ya mafuta ya hisia na hitaji la wanafamilia kuwa na uzoefu wa upendo kwa ajili yao katika lugha yao ya msingi ya upendo. Tulizungumzia kuhusu tofauti za tabia ndani ya familia zinavyoweza kutufanya tukue katika upendo.
Baada ya hayo, tulifanya upembuzi yakinifu kwa kila moja ya aina tano za lugha za upendo kwa kina, tukiangalia kila moja kwa mfano, na uharibifu unaosababishwa inapotokea kila moja kupuuzwa au kunyanyasika. Tumejifunza ni kwa jinsi gani watoto wanavyofaidika kwa kuwa na matanki yaliyojaa hisia, na jinsi wanavyoteseka wakati matanki yao yanapokuwa yamepungua sana. Tumezungumzia kwa marefu na mapana kuhusu kudhihirisha upendo wetu kwa watoto wetu. Kisha, tukaona jinsi kufanyia kazi aina tano za lugha za upendo zinavyounganika na sifa kuu sita za kawaida za familia zilizo imara na zenye nguvu.
Tunapofikia tamati ya masomo haya, tutajadili wajibu wako binafsi –ni nini utakachoweza kufanya na unachopaswa kufanya na kile ambacho ulijifunza katika masomo haya.
(1) Unawajibika kuipenda familia yako.
Unapaswa uwe tayari kubadilika kwa namna yeyote ile inayohitajika bila ya kusubiri wanafamilia wako wakupende wewe. Upendo wa kweli kabisa haungojei hadi mtu mwingine aonyeshe upendo kwako. Unajidhihirisha wenyewe hata wakati ambapo mtu mwingine anaonekana hastahili kabisa, kwa sababu upendo hautegemei uthamani wa mtu anayeupokea.
(2) Unawajibika kujitahidi kwa hali yako kudhihirisha upendo wako kwa ajili ya familia katika njia ambazo ni muhimu zaidi kwao.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba itakupasa uweke juhudi za ziada katika kudhihirisha upendo katika aina moja au zaidi ya lugha ambazo haziji kwako katika njia ya kawaida au ya asili. Mwanzoni, baadhi ya udhihirisho wa upendo unaweza kuhisi kwamba siyo wa kawaida au asili, ni wenye kufedhehesha au ni wa kipumbavu kwako.
Jifunze kutambua fursa zinazoonyesha upendo kwa wanafamilia wako. Kuwa makini na kile ambacho wanafamilia wanaweza wakahitaji katika wakati maalumu. Hapa kuna mfano wa kila moja ya aina za lugha za upendo:
Maneno ya Uthibitisho: Fikiria, “______ pengine anahisi kutokuwa na uhakika kuhusu kile alichosema hivi punde. Lakini alikuwa sahihi katika kile alichosema. Nahitaji kusema jambo la kuthibitisha.”
Muda ulio Bora: Uliza, “Je, ungependa kuzungumzia juu ya jambo hilo?” Kisha acha kile unachofanya, na wape umakini wako wote, na onyesha kwa njia ya lugha ya mwili kwamba kwa uhakika unawasikiliza.
Zawadi: Wakati unapokuwa unakabidhi zawadi sema kwamba, ”Nilikiona hiki na kikanifanya nikukumbuke.”
Matendo ya Huduma: Jaribu kuruka juu na uulize, “Je, ninaweza kukupatia hiyo?” au Je, ninaweza kukusaidia kwa hilo?”
Mguso wa Kimwili: Nenda kwa mtu huyo na umwambie, “unaonekana kama unahitaji kukumbatiwa” – huku ukimzungushia mikono yako kumkumbatia.
(3) Unawajibika kwa Hisia zako mwenyewe.
Mungu alikuumba ili uwe na mahusiano yaliyo imara na yenye afya na watu wengine. Lakini hilo liwe linawezekana au haliwezekani, Mungu mwenyewe ndiye chanzo chako kikuu pamoja na utoshelevu. Familia yako haiwajibiki peke yake kwa ustawi wa mihemuko yako. Mungu anakupenda kikamilifu, ingawaje kamwe hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo. Anaweza akafidia upungufu wowote utakaoweza kuwa nao, unapokuwa umeshikamana naye katika upendo wake (Yohana 15:9-11).
Familia yako inaweza isidhihirishe upendo kwako katika lugha yako ya msingi ya upendo. Inawezekana labda hawana ufahamu na lugha yako ya msingi ya upendo na mahitaji ya mihemuko yako. Huenda wanakosa motisha au ushawishi wa kudhihirisha upendo kwako kwa njia ambayo ni ya muhimu zaidi kwako. Unaweza kuwa na uwezo wa kuwaeleza ni kwa jinsi gani unajihisi kupendwa zaidi. Lakini huwezi kuwafanya wachague kudhihirisha upendo wao kwako kwa njia hiyo.
Huenda familia yako inadhihirisha upendo wao kwako kwa njia nyinginezo. Utakapokuwa una ufahamu wa lugha za upendo, utaanza kutambua njia ambazo familia yako tayari inazo kwa ajili ya kuonyesha upendo wao kwako. Kwa kuwa huna uwezo wa kuweza kuwabadilisha, unaweza ukachagua kukubali udhihirisho wao wa upendo na wewe ukaonyesha kuridhika nazo kwa ajili ya upendo huo.
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kunipa mimi familia. Nisaidie katika kumthamini kila mmoja wao kama ninavyokusudia, na kustawisha uhusiano mzuri na kila mmoja na kwa mwenzake.
Asante kwa fursa niliyo nayo ya kufikiria njia ambazo ninaweza kuonyesha upendo wangu kwa familia yangu. Nifundishe jinsi ya kumfanania Yesu: kuutoa muda wangu, nguvu za kimhemuko na za kimwili, na rasilimali za kuwabariki na kuwatia moyo familia yangu. Nisaidie niwe na moyo wa unyenyekevu, ili kwamba niweze kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya watu wengine kuliko ya kwangu. Nisaidie niwe na ufahamu wa fursa nilizo nazo za kudhihirisha upendo wangu kwa kila mwanafamilia wangu.
Baba, umenionyesha mimi kwamba upendo wa kweli ni upi. Unanitegemea mimi kufanya kitu kinachofanania huo upendo kwa familia uliyoitengeneza kwa ajili nyangu. Ninachagua kumpenda mwenzi na watoto wangu kwa upendo wa kujitoa kabisa na usiokuwa na masharti. Naomba unijalie neema na rehema kwa ajili ya njia nyingi ambazo nilishashindwa. Niwezeshe kuwapenda wote kwa kadri ninavyopaswa kufanya.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Fikiria kuhusu lugha za msingi za upendo za mwenzi wako na za kila mtoto wako. Orodhesha majina ya wanafamilia wako wote. Kisha orodhesha lugha moja au mbili za msingi za upendo kwa kila mwanafamilia.
(2) Je, ni udhihirisho gani wa upendo unaohitaji jitihada za ziada kwa sehemu yako? Ziwekee alama zote. Andika mawazo machache kuhusu ni kwa jinsi gani kwa kumaanisha unavyoweza kudhihirisha upendo wako kwa ajili ya familia yako kwa kutumia njia hizi.
(3) Chunguza utamaduni wako, haswa kikundi chako cha kijamii. Orodhesha lugha tano za upendo. Je, Katika utamaduni wako, kila moja ya lugha ya upendo inadhihirishwaje? Je, kuna yoyote kati ya hayo matano ambayo huwa hayazingatiwi? Je, ni baadhi ya njia zipi mahususi ambazo watu katika kikundi chako cha kijamii wanaweza kuonyesha upendo kwa njia bora kuliko ilivyo kawaida katika utamaduni wako? Andika aya kadhaa ukijibu maswali haya.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.