Kila siku jioni, Martha alikuwa na muda wa kufanya maombi na kusoma Maandiko akiwa na watoto wake wawili. Atasoma baadhi ya Aya za Maandiko, atapumzika mwishoni mwa kila Aya na kuanza kuzungumzia kuhusu matumizi yake katika maisha. Watoto wake walipokuwa vijana, Martha aliwapa zamu za kusoma na kufafanua vifungu vya Maandiko. Walifafanua vifungu vya Maandiko vizuri sana kwa sababu walikuwa wamejifunza kwenye mfano wa mama yao. Walikuwa na uwezo wa kutumia maneno yao wenyewe kuelezea kanuni za maisha ambazo walikuwa wamejifunza kutoka kwa mama yao.
Kipindi cha Ujana
Kila jamii ina jina la kipindi kati ya utoto na utu uzima. Hiki ni kipindi ambacho kijana mdogo huanza kuwa na hamu ya kuwa mtu mzima, kama vile kujamiiana, lakini akiwa bado hawezi kuchukuliana na majukumu ya utu uzima. Kwenye baadhi ya nchi, mtu anahesabika kisheria kwamba ni mtu mzima anapokuwa na umri wa miaka 18. Kwenye nchi hizo, mtu aliye chini ya miaka 18 hawezi kuoa au kuolewa, kutumika jeshini, au kufanya mikataba ya kisheria bila ya kibali cha mzazi.
Umri wa kuhesabika kuwa kijana kamili haufanani kabisa kila mahali. Kwenye jamii nyingine, mtu anaweza kuhesabika kuwa ni mtu mzima mapema akiwa chini ya umri wa miaka 18, akiwa ameshajifunza mambo ambayo watu wazima anafanya. Kwenye jamii nyingine, mtu anaweza kuendelea kuwategemea wazazi wake kwa miaka kadhaa akiwa ameshapitiliza umri wa miaka 18, wakati akiwa bado anamalizia elimu yake.
► Je, ni neno gani katika jamii yenu linaloelezea kundi la vijana kwenye hatua ya utoto hadi utu uzima?
► Je ni nini maana ya mtu mzima?
Ufafanuzi mmojawapo wa mtu mzima unaotumika kwa pamoja kwa ajili ya watu na wanyama ni huu: Ni kiumbe ambacho kimekua hadi kufikia ukomavu wa kimwili. Hata hivyo, utu uzima wa binadamu unamaanisha zaidi ya ukomavu wa kimwili. Kijana mdogo anaweza akawa na umbo na nguvu kama za mtu mzima lakini unakuta bado hajaweza kuchukua majukumu ya mtu mzima.
► Je, ni tabia gani walizo nazo watu wazima mbali na ukomavu wa kimwili?
Kwa ujumla, mtu mzima ni yule mtu ambaye anaweza kujiongoza na kuwajibika kwa ajili ya maamuzi. Ufafanuzi huu siyo tafsiri kamili sana kwa sababu viwango vya majukumu binafsi vinatofautiana sana. Kila mtu ambaye hajatengwa kabisa anashawishiwa na watu wengine, na hata watu wazima hawana uhuru wote kamili katika kila uamuzi. Hata hivyo, utu uzima kwa ujumla una sifa ya kufanya na kuwajibika kwa maamuzi ya mtu mwenyewe. Mwishoni mwa kipindi cha ujana, mtu anapaswa kufanya maamuzi kwa ajili yake mwenyewe. Lengo la wazazi ni kuwaandaa vijana kwa ajili ya jukumu hilo.
Yesu alielezea hadithi moja ya mtoto ambaye alikwenda kudai urithi wake kutoka kwa baba yake, ambaye alikuwa bado hai (Luka 15:11-32). Mtoto alichukua fungu lake la fedha na akazipoteza kwa matumizi ya uzembe mkubwa sana. Huu ni mfano mzuri wa mtu ambaye amemaliza hatua ya ujana na kuwa kwenye hatua ya mtu mzima lakini hakuwa tayari kufanya maamuzi yenye hekima. Kuna vijana wengi ambao wanapatwa na madhila ya maamuzi mabaya waliyofanya kwa sababu hakukua vizuri kabla ya kupokea uhuru na majukumu ya mtu mzima.
Neno la Mungu lina hekima kubwa sana kwa ajili ya ujana, kipindi muhimu cha wakati wa kuendelea kukua kwa mwanadamu.
Maendeleo ya Kimwili na Kiakili
► Mwanafunzi anapaswa asome Luka 2:40, 52 kwa ajili ya kikundi.
Yesu aliingia kwenye ujana akiwa anakua kiakili na kimwili. Katikati ya hizi Aya mbili, kuna simulizi la Yesu kutembelea hekalu ili kuongea na waalimu wa dini. Siyo tu kwamba alikuwa anaongezeka kukua kimwili, lakini pia alijisikia mwenyewe kama angeweza kuwa huru zaidi. Alikuwa pia tayari kushirikishana mawazo na watu wengine zaidi ya familia yake marafiki zake.
Mariamu na Yusufu walishangazwa na mazungumzo ya Yesu na waalimu wa dini, lakini Mariamu alimwambia Yesu kwamba yeye pamoja na Yusufu walikuwa na wasiwasi kwa siku tatu (Luka 2:46-48). Yesu akawaambia kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa sababu alikuwa anaanza kutekeleza kazi ya Baba yake (Luka 2:49). Akiwa kijana alikuwa na matamanio ya kawaida ya kuanza kufuata shauku ya maisha yake. Hata hivyo, alirejea nyumbani na kutii mamlaka ya wazazi wake kwa miaka yake yote ya ujana yaliyokuwa yamebakia (Luka 2:51).
Wakati wa ujana wa mapema, mwili wa mtoto hubadilika kuwa kama mtu mzima. Mtoto anaweza kukua haraka kwa kuongezeka urefu. Nywele huanza kukua katika maeneo kadhaa kwenye mwili. Sauti inaweza ikabadilika na kuwa nzito. Baba au mama anapaswa kuhakikisha mtoto wake anaelewa kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida. Mungu alipanga ukuaji wa kawaida wa kimwili na kiakili kwa mwanadamu.
Kuwa na uhusiano mzuri na watoto wako kutawasaidia kujisikia kwamba wana uwezo wa kuanzisha mazungumzo ya wazi na wewe katika kipengele hiki cha maisha. Mtoto ambaye hajisikii kuwa na amani kuzungumza na mzazi wake kuhusu mambo haya anaweza kuwa na hofu ya siri na anaweza akatafuta kupata taarifa kutoka kwa marafiki na kwenye mitandao.
Maendeleo ya Kihisia
Ujana siyo tu mwendelezo wa maisha ya mtoto kama ilivyokuwa hapo awali. Wazazi wanakosea kufikiri wanaweza kuendelea kutoa maelekezo na kufundisha kijana kama vile wangemfundisha mtoto mdogo. Ufahamu wa kijana na mambo anayoyapendelea hubadilika. Anahisi kuwa na shauku ya kuwa kijana aliye huru, mwenye mafanikio, na heshima. Vijana huchanganyikiwa wakitendewa na au kuchukuliwa kama mtoto mdogo.
Katika Maandiko yote kuna mifano ya vijana wadogo wenye kufanya maamuzi ya hekima, kama Yesu, au maamuzi ya ovyo, kama tunavyosoma katika hadithi iliyosimuliwa na Yesu (Luka 15:11-32). Wazazi wanapaswa kuelewa jinsi ambavyo kijana au binti yao anakua kihisia. Lengo la mzazi ni kumsaidia kijana aweze kusitawisha udhibiti wake binafsi wa maeneo yake yote, ikiwa ni pamoja na hisia, ili kwamba udhibiti wa baba au mama hautakuwa unahitajika tena.
► Soma Waefeso 6:1-4. Je, ni maelekezo gani maalumu tunapata kutoka katika kifungu hiki?
Watoto wanapaswa kuwatii wazazi wote, ikimaanisha kwamba baba na mama wanapaswa kushirikiana. Kifungu hicho kinaunganisha kwa uzito mkubwa utii kwa wazazi na wajibu wa kumtii Mungu. Wazazi ambao hawawafundishi watoto wao kutii wanakuwa hawawapi maandalizi ya kumtii Mungu. Kuruhusu watoto kufanya uasi dhidi yako kama mzazi kunawaandaa pia kumwasi Mungu.
Maandiko haya yanatoa mwongozo mahususi kwa akina baba. Akina baba wanapaswa kuleta nidhamu katika njia ambayo kwamba haiwachanganyi au kuwakatisha tamaa watoto kufanya yale mambo ambayo ni sahihi.Adhabu na masahihisho ni mambo muhimu, na hayamfanyi mtoto kuwa na furaha mara moja, lakini baba anapaswa awe asiyebadilika mara kwa mara na mwenye upendo. Hii inamaanisha kwamba baba anapaswa aelewe kitu kuhusu maendeleo ya kihisia ya mtoto.
Baba hapaswi kutoa marekebisho tu, lakini pia malezi ya kiroho na mafundisho kutoka kwa Bwana. Hatuwaendelezi watoto wetu kwa kushambulia tu makosa yao. Ni lazima tujaribu kuwaelewa na kuwatia moyo watoto wetu. Tunatumia ukweli wa Mungu na siyo tu matakwa yetu wenyewe. Tunadhihirisha kwamba sisi pia tunaishi kwa kumtii Mungu.
Wakati mtoto anapokuwa amejifunza kuheshimu na kutii katika miaka yake ya utotoni, mafunzo yake kwenye ujana yanakuwa rahisi zaidi! Uhusiano ambao wazazi walianzisha kwa watoto wao wakati wakiwa wadogo utasaidia sana wakati wa mabadiliko ya kimwili, kihisia, na kiroho ambayo vijana wanapitia. Hakuna maelekezo kwa ajili ya kufanya malezi yawe marahisi, lakini kukuza mahusiano mazuri ya mapema kunafanya mawasiliano yawezekane katika ujana wote.
Wazazi wanatamani watoto wao wawe wasikivu, lakini mara nyingi baba au mama lazima wasikie kwanza. Tafadhali kwa ajili yako na wao – weka chini simu yako, kitabu chako, kazi, au kitu chochote unachokifanya na uwape umakini wako wa kuwasikiliza wanapotaka kuzungumza. Wasikilize kwa makini kana kwamba hakuna kitu kingine tena cha kufanya. Sikiliza bila kurekebisha makosa yao hadi pale utakapokuwa umeelewa kwa uhakika kwamba wanataka kusema nini. Wanataka wajisikie kwamba unawathamini kwa ukweli pamoja na mitazamo yao, na kwamba unawaheshimu kama watu. Hata kama hawapendi ushauri wako,watauheshimu zaidi baada ya kujua kwamba kwa uhakika umewasililiza.
Huenda ikawa ni vigumu kusikiliza wakati kijana anapoonyesha kuchanganyikiwa, hasira, au kutaka kujiondoa. Kumbuka kwamba kijana haelewi kabisa hisia zake mwenyewe. Wakati mwingi kijana husema yale anayoyasema kwa sababu hisia zake zimeathiriwa na mazingira, mahusiano, na miili yao. Mambo haya yote yanaweza yakaathiri hisia ya kijana: msongo wa mambo kutokea shuleni, shinikizo la kukubaliwa na marafiki, wasiwasi kuhusiana na mabadiliko ya mwili, chuki kwa ajili ya kuhisi kutothaminiwa au kutoheshimiwa, kile ambacho kinafanywa na homoni zao, na uchovu unaotokana na tabia ya kutolala kwa nyakati zinazofanana.
Maendeleo ya Kiroho
► Soma Mhubiri 11:9-12:1, 13. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuelezea amri zilizopo kwenye Aya hizi kwa kijana?
Dunia inaweza kutoa udhuru kwa tabia ya uzembe na uasherati kwa vijana, lakini Aya hizi zinawataka vijana wakumbuke kwamba watahitajika kuwajibika kwa Mungu kwa matendo yao. Yeye peke yake ndiye jaji au mwamuzi wao.
Kufundisha Neno la Mungu katika nyanja mbalimbali za maisha bado ni muhimu sana kwenye hatua hii ya maisha (Kumbukumbu la Torati 6:6-7). Hata hivyo, ni vigumu zaidi, kwa sababu kijana anakuwa na shughuli nyingi za kufanya nje ya kikundi cha familia. Wanakuwa na mambo wanayoyataka wao wenyewe, shughuli za elimu, shughuli za michezo, na kushiriki katika vikundi vya marafiki. Wazazi wao hawawezi kuwa pamoja nao kwa muda wote, lakini Mungu anaweza, na wazazi wanapaswa wawe waaminifu kuomba kwa ajili yao. Wababa na Wamama anapaswa watafute hekima kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kupata muda wa kuwa na mazungumzo mahususi pamoja nao. Ni muhimu sana kwa wazazi waendelee kuhusika na kuwa makini na vipengele mbalimbali vya maisha ya vijana wao.
► Soma 1 Wathesalonike 2:11-12 kwa pamoja. Je, ni jukumu gani ambalo Mungu amewapa wababa kwenye mahusiano yao na watoto wanaokua?
Wazazi, msidhanie kwamba kila kitu kiko shwari kwa sababu tu matatizo hayaonekani wazi. Ni jambo unalopaswa kutegemea kwamba kijana au binti yako atakabiliana na majaribu na kupitishwa kwenye madhaifu, kwa sababu ndivyo itakavyokuwa. Wasaidie ujuzi wa jinsi ya kuwajibika kwa ajili ya fedha zao, jinsi ya kutumia muda wao, chaguzi za mambo ya maisha wanayofanya, na usafi wao wa kijinsia. Omba hekima na ushauri kutoka kwa watu wengine. Sikiliza kutoka kwa waalimu na watu wengine ambao wanadhihirisha nia ya kuhusika. Hata kama hukubaliani na maoni ya mtu mwingine kuhusiana na mtoto wako, unapaswa usikilize na ujaribu kuyaelewa mahitaji ya mtoto wako.
Waombee vijana wako na uwaambie kwamba unawaombea. Ni vyema wasikie ukiomba kwa ajili yao. Shiriki nao maombi maalumu unayoomba. Kwa mfano, unaweza ukasema, “Naomba kwamba muwe wenye njaa na kiu ya haki (Mathayo 5:6); na kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji (Zaburi 42:1). Ninamwomba Mungu mjazwe na Roho Mtakatifu (Waefeso 5:18) ili umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote na jirani yako (au ndugu yako) kama nafsi yako (Mathayo 22:37-39).”
► Je, kuna vifungu gani vingine vya Maandiko ambavyo unaweza kuvitumia kwa ajili ya kuwaombea vijana wako?
Mwisho, kwenye hii safari ya kiroho pamoja na vijana wako, tumia Neno la Mungu pamoja nao:
Kuwa mfano kwao: Mara kwa mara tumia muda wako binafsi kwa kujifunza Biblia. Zungumza na kijana wako wa kiume au wa kike kuhusu kile ambacho Mungu anakufundisha wewe na ni kwa jinsi gani unalitumia hilo Neno la Mungu kwenye maisha yako. Hata kama hawatakuwa na jibu la shauku yao au hawataendelea na mazungumzo, wanasikiliza na watakuwa wanaguswa na Neno!
Kariri vifungu vya Maandiko kwa pamoja kama familia na rudia kutoka moyoni kwenye kila muda wa chakula au mwisho wa siku.
Soma na zungumza kupitia kitabu cha Mithali aya moja kwa wakati mmoja. Mithali ni kitabu cha ajabu sana na kizuri kutumika wakati wa nyakati fupi za ibada, kikiwa na hekima za vitendo kwa ajili ya maisha ya kila siku. Kitabu hiki kinatoa fursa nyingi kwa ajili ya majadiliano na kinaleta mguso mkubwa usiokuwa wa kawaida.
Maelekezo, kanuni, na mifano katika Maandiko yote yanatumika katika majira yote ya maisha, kwa hiyo jifunze Neno lote la Mungu ukiwa na vijana wako wa kiume na wa kike.
Maendeleo ya Kijamii
Andiko la Luka 2:52, linalofafanua maendeleo ya Yesu alipokuwa kijana, linasema kwamba alisitawisha uhusiano wake pamoja na wengine. Mungu anapendezwa sana na mahusiano yetu. Alituumba tuwe na mwingiliano wa kibinadamu na ushirika wa pamoja.
Kando na wanafamilia, tunashawishiwa na wanafunzi, majirani, vikundi vya kanisa, waajiri, waalimu, na viongozi wengine na vyombo vya habari. Kwa kawaida watu walio katika marika yanayofanana ndiyo wenye ushawishi mkubwa zaidi kwa mambo mema au mabaya. Wazazi wa Kikristo wanapaswa kufuatilia mwingiliano wa kijamii wa watoto wao na vijana.
Jinsi kijana wako anavyoendelea kuwa mtu mzima, fikiria kwa uangalifu na kwa maombi ni jinsi gani atakavyoweza kushughulika na hali hiyo. Kwenye kompyuta na vifaa vingine vya kiselula vya familia yako, tumia manenosiri ya kufunga na kufungua baadhi ya programu mahususi kwa ajili ya kuilinda familia yako katika kuingia na kuangalia mambo ya uovu. Weka muda maalumu wa kufungua na kutumia vifaa hivyo. Fuatilia tovuti, filamu, vipindi vya televisheni na majukwaa ya mitandao ya kijamii. Kwa jinsi ile ile ambayo huwezi ukaruhusu vijana wako kutumia muda wao na baadhi ya watu fulani kwenye ujirani wako, pia usiwaruhusu wafuatilie au kuunganika na watu wabaya kwenye vifaa vyao vya kielektroniki.
► Haitoshi tu kuwalinda vijana wako. Katika ujana, pia unamwandaa kijana wako wa kiume au wa kike kuchukua majukumu kwa ajili ya kufanya maamuzi yao wenyewe yenye hekima na ambayo yanampa Mungu utukufu na kulinda roho zao. Je, ni kwa njia zipi unazoweza kuwafundisha vijana wako majukumu na uwajibikaji kwenye matumizi ya teknolojia katika jamii yao ya dunia?
Vijana hupenda kuunda vikundi vya marafiki ambavyo hutumia muda wao mwingi kwa pamoja. Wanajifunza kushirikishana mambo wanayoyapendelea, kama vile kufurahia aina za burudani zinazofanana. Wanaanza kushirikishana tabia zao zinazofanana dhidi ya kanisa, wazazi wao, shule, na taasisi nyingine. Mara nyingi wazazi hushangaa wanapoona mabadiliko yao katika hatua hii ya ujana. Vijana wakati mwingine wana maoni na shutuma zisizotegemewa au kutarajiwa na wanatumia misamiati ambayo huwa wamejifunza kutoka kwa marafiki zao. Kundi la marafiki hujitokeza kuwa ni familia mbadala inayowapa wanachama wake hadhi ya kukubalika. Kijana anavutiwa kwa nguvu sana kuwa kwenye familia mbadala kama familia yake mwenyewe haimpi hisia ya thamani, utambulisho na kukubalika.
Mzazi huona ni vigumu sana kumtoa kijana wake katika kundi la marafiki alilojiunga nalo au kupunguza ushawishi wa hilo kundi. Wakati mzazi atakapokosoa hilo kundi au watu binafsi, kijana hutaka kuwalinda kwa kuwatetea na anahisi kwamba mzazi wake haelewi. Baba au mama wanaweza kumsaidia kijana kwa kuonyesha kumjali, kutambua anayoyataka, na kumpenda. Wakati mzazi anapotoa mahitaji ya mihemuko ya kijana, huwa hawana haja tena ya kutegemea kundi la marafiki kwa ajili ya kuwa familia mbadala.
► Je, ni kwa jinsi gani wazazi wa familia kadhaa wanaweza kufanya kazi kwa pamoja ya kuwasaidia vijana wao?
► Je, ni kwa jinsi gani kanisa lako linaweza kuwasaidia wazazi wa vijana wanapokuwa wanawasaidia vijana wao waweze kuwa na maisha bora yenye nguvu na jamii inayomheshimu Mungu?
Matatizo ya kipindi cha mpito kuelekea Utu Uzima.
Mtoto hawezi akawa mtu mzima kwa wakati mmoja au mara moja. Mtoto huwa anapitia kwenye kipindi cha mpito ambacho kinafikia mwisho baada ya miaka kadhaa.
Kati ya Maandiko yote, kitabu cha Mithali kiliandikwa mahususi kwa ajili ya vijana. Katika Mithali, Mfalme Sulemani anazungumza na kijana wake aliyekuwa anajifunza kuhusu maisha na kukuza mtazamo wake wa kidunia. Sulemani alizungumza na mwana wake kuhusu kila sehemu ya maisha, kuhusu thawabu zinazoweza kupatikana kwa kuchagua kwenda katika njia za Mungu na kuhusu hatari na au madhara ya kukataa hizo njia za Mungu.
Imani zilizoundwa wakati wa utoto na kwenye miaka ya ujana, na chaguzi zilizofanywa katika kipindi hicho ni muhimu sana kwenye maisha ya mtu. Tunapochunguza changamoto kadhaa za kipindi cha mpito cha kuingia kuwa mtu mzima, tutazame ni kwa jinsi gani Neno la Mungu linavyoweza kutusaidia tusafiri kwenye miaka ya ujana na vijana wetu.
Changamoto ya 1: Kijana hutathmini yale yote ambayo amefundishwa na kuamua ni kipi anachoweza kukiamini.
Kijana huwa anataka kile anachokiamini kiwe wazi kwenye akili yake, kwa hiyo hutathmini na kujiuliza maswali kwamba ni kitu gani amefundishwa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hatakubaliana na kila kitu ambacho wazazi wake walimfundisha. Wazazi huhofia hatari hiyo. Ikiwa wanajihisi kwamba hawawezi kumsaidia kuelewa masuala anayofikiria, wanaweza wakaanza kumchukulia kama ni mtoto tena, wakidai kwamba akubali yale wanayoyaamini bila kuuliza. Hali hii humfanya kijana ajisikie kwamba hawampi nafasi ya kufikiria na kujiamulia mambo yake mwenyewe.
Mzazi anapaswa kwa ustahimilivu aelezee sababu za kuamini yale wanayoamini na kumpa kijana nafasi ya kuweza kuzungumza na watu wengine ambao wanaweza wakasaidia kutoa ufafanuzi.
► Soma Mithali 23:22-23 kwa pamoja.
Katika mistari hiyo, Mungu anasema kwamba kijana anapaswa kuchagua kusikiliza hekima ya wazazi wake. Baba au mama hawawezi kufanya chaguo hili kwa kijana wao, lakini wanaweza kusitawisha uhusiano mzuri. Kama wazazi wataendelea kuwasiliana kwa uwazi na kwa heshima pamoja kijana wao wa kiume au wa kike, itawatia moyo vijana wao kufanya uchaguzi huu.
Changamoto ya 2: Kijana anaanza kuchukua jukumu kwa ajili ya kufanya maamuzi.
Kijana anaanza kuelewa jinsi maamuzi yanavyofanywa, na anajisikia mwenye uwezo wa kufanya maamuzi peke yake, lakini wazazi wake na watu wengine hudhibiti chaguzi zake. Atashawishika kufanya uasi dhidi ya mamlaka yao kwa sababu anafikiri hawatambui uwezo wake. Kwa kawaida, kama atafanya uasi, wazazi watajibu kwa kumwekea ukomo zaidi.
Wazazi wanapaswa kuweka msingi mzuri kwenye hatua hii ya maisha ya watoto wao wakati wakiwa wadogo zaidi. Wanaweza wakawaonyesha watoto wao kwamba kile wanachohitaji kwao ni kwa ajili ya manufaa yao wenyewe kama vile nidhamu ya Mungu ni kwa ajili ya manufaa yetu (Waebrania 12:9-10). Wazazi wanaweza wakadhihirisha kwamba hawatengenezi tu sheria ambazo zitawasaidia wao tu wenyewe kama wazazi.
Pili, wazazi wanaweza kuwapa watoto wao hatua kwa hatua jukumu la kufanya maamuzi makubwa na muhimu zaidi katika miaka yao yote ya utoto na ujana. Hilo huwawezesha vijana kujizoeza kuwajibika, kuthibitisha uaminifu wao, na kujitayarisha kwa ajili ya utu uzima.
Wazazi bado wanawajibika kwa Mungu katika kuwawekea vijana wao mipaka (1 Timotheo 3:4), lakini miaka ya ujana ni ya kujitayarisha kwa ajili ya utu uzima, wakati kijana atakapowajibika kikamilifu kwa Mungu kwa ajili ya maamuzi yake. Wazazi wanapaswa kuwaandaa vijana wao kwa ajili ya huu msimu unaofuata. Kitabu cha Mithali kimeandikwa na baba akimsihi mtoto wake afanye maamuzi ya busara. Sulemani alijua kwamba akiwa kama mzazi hangeweza kumfanyia mtoto wake maamuzi, lakini angeweza kufanya maamuzi yaliyo sahihi ambayo yangeonekana kuwa yenye mvuto zaidi.
Changamoto ya 3: Kijana hana ukomavu alio nao mtu mzima.
Huenda vijana wasielewe hatari na uthubutu ambao unawahusu wazazi wao. Vijana kwa kawaida huhisi kwamba wanaweza kukamilisha malengo yao na kuziepuka hatari mbalimbali zilizopo. Mara nyingi wanahisi kuchanganyikiwa kwamba wazazi wao hawana imani katika uwezo na utambuzi wao.
Mithali inatuonyesha kwamba ni muhimu kwa wazazi sio tu kuwaambia vijana wao yaliyo mazuri na mabaya au kuwawekea tu mipaka, bali kuzungumza na vijana wao kuhusu matokeo ya kila chaguo. Kusikiliza maagizo haya kutamsaidia kijana kujifunza kufikiri kwa njia ya ukomavu.
► Soma 1 Petro 5:5 kwa pamoja.
Jambo la busara zaidi ambalo kijana anaweza kulifanya ni kujikabidhi kabisa kwa mamlaka ya wazazi wacha Mungu na kusikiliza ushauri wao wa busara. Kama Petro anavyotuonyesha katika 1 Petro 5:5, kwamba kijana anayefanya haya ana upendeleo maalumu wa Mungu.
Changamoto ya 4: Kijana ana matamanio ya mtu mzima lakini hawezi kuwa na marupurupu ya mtu mzima.
Watu wazima wana fursa za marupurupu mengi ikiwa ni pamoja na ndoa, umiliki wa mali, nafasi za uongozi, na uhuru wa kufanya maamuzi. Kwa kuwa vijana bado hawawezi kuwa na marupurupu haya, ingawa wana matamanio ya asili ya mambo haya, wanajisikia kuchanganyikiwa. Matamanio yao husababisha vishawishi na au majaribu makali. 2 Timotheo 2:22 husaidia vijana kujua ni kitu gani wafanye kuhusu tatizo hilo.
► Soma 2 Timotheo 2:22 kwa pamoja.
Mungu ameachilia neema kwa vijana ambao wako tayari kumtii yeye. Atawasaidia katika kujitoa kabisa kwa mamlaka zao na kukataa kukamilishwa kwa matamanio yao ambayo yako nje ya wakati au mapenzi yake. Atawasaidia vijana wa Kikristo kuyageuza matamanio hayo kuwa motisha wa kujiandaa kuingia utu uzima kwa kukua katika ufahamu, tabia, na stadi za maisha.
Changamoto ya 5: Kijana huona kwamba kuna utofauti kati ya kinachosemwa na wanavyoishi wengine na anachukizwa kwa hilo.
Mara nyingi, vijana wamekatishwa tamaa na watu wengi ambao walipaswa kuwa mifano bora na viongozi bora wa kiroho. Hilo linapotokea, vijana hushawishika kutomwamini kila mtu. Kwa sababu hii, ni muhimu kwako kama kiongozi wa kanisa na kama wazazi kuishi maisha thabiti, ya kumcha Mungu. Mambo kinzani katika maisha yako yanaweza kusababisha vijana kutumia umilele kuzimu. Ingawaje Yesu alikuwa anazungumza kuhusu watoto, na siyo vijana, Mathayo 18:6 kwa hakika hapa inahusiana.
► Soma Mathayo 18:6 kwa pamoja.
Kijana Mkristo anaweza kuwa kielelezo cha mcha Mungu, hata kama hajawi kuona ukiwa kwa watu wengine. Katika Agano la Kale, Samweli ni mfano wa jambo hili. Samweli alilelewa kwenye familia ya kikuhani ambayo haikumcha Mungu na iliyokuwa fisadi kwa njia nyingi, hata hivyo aliamua tangu akiwa na umri mdogo kuishi kwa ajili ya Mungu (1 Samweli 1:20; 1 Samweli 2:11-18, 22-26). Hata akiwa bado mtoto na baadaye kijana, aliendelea kuyaishi maisha matakatifu (1 Samweli 3:19, 21).
► Soma 1 Timotheo 4:12 kwa pamoja.
Changamoto ya 6:
Kijana anakabiliwa na msisimko wa maamuzi mengi na fursa nyingi.
Vijana wanaiona dunia iliyojaa wingi wa fursa. Wanaweza wakajitahidi kutafuta mwelekeo kwa ajili ya maisha yao wenyewe. Wanapokea ushauri unaokinzana kutoka kwa watu mbalimbali.
Wanafikiri kwamba mtu anapaswa kuwapa kile wanachohitaji ili kufuatilia fursa zilizopo. Ni muhimu kwa vijana kujizoeza kuwa waaminifu katika mambo madogo na kumwamini Mungu katika kufungua fursa nyingi zaidi kwa ajili yao katika muda wake mkamilifu.
► Soma Luka 16:10 kwa pamoja.
Ni jambo la muhimu pia kwa vijana kuchagua kusikiliza ushauri wa kimungu.
► Soma Mithali 11:14 kwa pamoja.
Vijana watagundua kwamba kuna baraka na uhuru katika kufuata njia za hekima ya Mungu.
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, ni mawazo gani katika somo hili ambayo umeyaona ni ya msaada sana kwako? Je, ni kwa jinsi gani yatakugusa wewe na familia yako, jamii, na au kanisa lako?
► Ikiwa umewahi kuwa mzazi wa kijana wa kiume au wa kike, ni ushauri gani unaoweza kushirikisha kuhusu kustawisha uhusiano ulio wazi na wenye kuheshimika na mtoto katika hatua hii ya maisha? Kuwa mkweli kuhusu makosa yako.
► Je, ni mambo gani ya vitendo ambayo unaweza kuyafanya ili kusaidia vijana kujifunza jinsi ya kufikiri kwa hekima na kufanya maamuzi mazuri?
► Je, wewe kama mzazi unajuaje wakati wa kupanua mapendeleo na majukumu ya mtoto wako?
► Fanya majumuisho ya majukumu muhimu ya mzazi na majukumu muhimu ya mtoto akiwa amefikia kuwa kijana.
► Je, ni sehemu gani za maisha ambazo baba anapaswa atoe motisha, maonyo na kuwaongoza watoto wake wanapoendelea kukua kwenda ukubwani?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kutuamini katika majukumu uliyotupa ya kuwatunza watoto wetu hadi kufikia watu wazima waliokomaa. Jukumu hili ni ngumu kwa njia nyingi, na ni lazima tuwe na ufahamu kutoka kwako.
Katika Neno lako, tumeona jukumu letu la kuwafundisha watoto wetu hekima, kujidhibiti, na kukutii wewe. Tunaomba msamaha kwa nyakati zote ambazo tumeshindwa kuwa na mwelekeo juu ya vipaumbele hivi kwenye mahusiano yetu na vijana wetu.
Tumekuwa tunasoma na kulitii Neno lako, tupe hekima mahususi kwa ajili ya mahitaji ya watoto wetu. Ni matamanio yetu makubwa sana kwamba watakufuata wewe kwa uaminifu katika siku za maisha yao yote.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Tafuta angalao maandiko matatu, aya au vifungu ambavyo unaweza ukavitumia kwa ajili ya kuombea vijana kwenye familia yako au chini ya ushawishi wako. Tafuta vifungu vya maandiko vinavyohusiana na:
Mahitaji yao ya kiroho
Ukuzaji wa tabia zao
Mambo na watu ambao wanawashawishi
Njia ambazo watazihitaji kwa ajili ya kukua na kustawi
Andika vifungu hivyo mahali ambapo unaweza kuziona mara kwa mara. Anza kutumia Maandiko haya kwa ajili ya kuwaombea vijana wako kila siku.
(2) Chagua maswali mawili ya majadiliano ya kikundi kutoka katika mwisho wa somo hili. Andika angalao ibara moja inayohusiana na kila kipengele.
(3) Chagua kifungu cha maandiko kwa ajili ya kusoma:
Mithali 4-5
Mithali 6
Mithali 23
Mithali 24
Unapokuwa unasoma, tafakari maswali yafuatayo kutoka kwenye kifungu…
Je, ni vipaumbele gani mzazi wa kijana anapaswa kuwa navyo?
Je, ni vipaumbele gani kijana anapaswa kuwa navyo?
Je, mzazi wa kijana anapaswa awe na fikra/mitazamo gani?
Je kijana anatakiwa awe na fikra/mitazamo gani?
Je, mzazi wa kijana anapaswa afanye nini?
Je, kijana anapaswa afanye nini?
Je, ni maeneo gani katika maisha ambayo mzazi na kijana wanapaswa wawe wanaongelea?
Andika orodha ya taarifa kwa muhtasari za ujumbe wa kila kifungu kwenda kwa mzazi wa kijana. Andika orodha ya pili ya taarifa kwa muhtasari za ujumbe wa kila kifungu kwenda kwa kijana.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.