Marcus alipokuwa mtoto, wazazi wake walimfundisha jinsi ya kufanya kazi vizuri. Alikuwa na furaha kila wakati alipopata nafasi ya kufanya kazi na kujipatia pesa. Siku zote alikuwa tayari kufanya kazi yoyote ambayo mtu angemuajiri. Kama kijana alifanya kazi ya kutunza mazingira ya uani, kusambaza magazeti, na kutengeneza baiskeli. Marcus alikuwa na matamanio ya kuwa mfanyabiashara lakini pia alijua kwamba Mungu alikuwa anamwita kwenye huduma. Marcua alijifunza katika chuo cha Biblia. Ili aweze kulipa gharama za chuoni, alifanya kazi za usafi wa maofisi, kazi za hotelini, na kazi za uani. Alipohitimu, alianzisha huduma, lakini wakati mwingine alikuwa anafanya kazi za kupaka nyumba rangi au kufanya matengenezo ya nyumba kwa sababu huduma yake ilikuwa haina uwezo wa kumlipa. Wakati wote alijitahidi kufanya majukumu ya huduma na maendeleo binafsi kuwa ni vipaumbele vyake badala ya kufanya faida kuwa ndiyo kipaumbele chake, ingawa alikuwa na mke na mtoto aliopaswa kuwatunza. Hatimaye ilifika kipindi ambacho huduma yake iliweza kumsaidia kabisa.
Ukomavu na Tabia
► Wanafunzi wanapaswa wasome 1 Timotheo 4:12 na Maombolezo 3:27 kwa ajili ya kikundi.
Waraka wa 1 Timotheo uliandikwa kwenda kwa kijana ambaye alikuwa na majukumu ya kusimamia makanisa kadhaa. Katika 1 Timotheo 4:12 tunaona kwamba Mungu hutegemea vijana waliookoka kuwa vielelezo katika tabia zao na mienendo yao. Wanapaswa kuifanya kuwa kipaumbele kuanzishwa katika mafundisho ya Kikristo. Wanapaswa wadhihirishe usafi na upendo usio na ubinafsi kwenye kila mwingiliano na watu wengine. Tabia zao na maneno yao yanapaswa yamheshimu na kumletea Mungu utukufu.
Vijana walioamini/waliookoka wanapaswa waishi maisha ya uangalifu na yenye malengo. Hawapaswi kutumia vibaya nguvu walizopewa na Mungu kwenye hatua hii ya maisha. Hawapaswi kupoteza fursa za kujifunza, kuendeleza ujuzi wao, kuwahudumia watu wengine, na kuchukua majukumu. Miaka ya ujana na utu uzima haipaswi itumike kwenye matamanio ya mambo ya kibinafsi. Ni miaka iliyo bora kwa ajili ya kukua na kuhudumia. Mungu anaweza akawawezesha vijana waliookoka kujifunza kujitawala binafsi ili waweze kuzaa matunda kwa ajili yake.[1]
[1]Kupata zaidi kuhusu somo hili, ona somo la 12 katika kitabu cha Muundo wa KirohoSpiritual Formation, kinachopatikana kutoka Shepherds Global Classroom.
Kazi
Mitazamo juu ya Kazi
Katika tamaduni nyingine, ni jambo la kawaida kuwaona watu wakiwa wamekaa na hawafanyi kazi, ingawaje wanaweza kuwa ni vijana wadogo na wenye afya nzuri. Ingawa wanayo mahitaji na wanawajibika kwa watu wengine, hawana motisha wa kufanya kazi. Wanadai kwamba wangeweza kufanya kazi endapo wangeajiriwa kwa malipo mazuri. Hawako tayari kufanya kazi kwa malipo kidogo au kufanya kazi ambazo zinaonekana kuwa ni za hali ya chini ya kiwango. Hawataki kufanya kazi kuboresha mazingira yao hata kama wanufaika hawatakuwa ni wao wenyewe.
Wakati mwingine watu walioajiriwa wanafurahia kwa kuwa na ajira. Labda wanaishi katika nchi ambayo asilimia kubwa ya watu hawana uwezo wa kupata ajira iliyo nzuri.
Wanafurahia wanapokuwa wamevalia sare za kampuni na wanajivunia viwango vya hadhi walizo nazo katika hizo ajira zao. Lakini wakati wakiwa wanafurahia viwango na hadhi zao katika kazi hawafikirii sana jinsi ya kumhudumia mwajiri au kuwahudumia wateja. Wanajivunia kuwa sehemu ya jamii ya kampuni, lakini hawatambui ni kwa nini waliajiriwa.
Tofauti na watu wanaokataa kufanya kazi, baadhi ya watu wamejielekeza kwenye kupata kazi au jinsi ya kupata fedha. Labda waliohamia kwenye eneo ambalo ajira inalipa mshahara mkubwa zaidi kuliko maeneo ya vijijini walikotoka. Wanataka wafanye kazi na kujipatia fedha za kutosha kwa kadri inavyowezekana. Wanapuuzia maeneo mengine muhimu ya maisha, kama vile kustawisha mahusiano yao na Mungu pamoja na familia zao.
Watu katika jamii wanaweza wakafanya mambo haya, lakini waamini hawapaswi kufanya yale mambo ambayo ni ya kawaida tu katika utamaduni wao. Badala yake, ni lazima watafute Mungu anasema nini, na kisha wamtii. Biblia ina mambo mengi ya kusema kuhusu kazi, bidii, na tija.[1]
Asili ya Kazi
Mungu ni muumbaji (Zaburi 104:24). Mungu ni mzalishaji (Zaburi 104). Mungu kwa wakati wote anatenda kazi, akihusika na maisha ya kila mtu binafsi na katika mambo yote ya dunia kwa wakati wote (Yohana 5:17). Wakati Mungu alipoumba watu, aliwaumba kwa sura yake, kwa mfano wake mwenyewe. Alihitaji watu wawe wabunifu na wasimamizi wenye kuleta tija katika uumbaji wake. Mungu aliwapa wanadamu mamlaka juu ya wanyama wa dunia, viumbe wa baharini na angani (Mwanzo 1:26). Aliwafanya watu kuwa wasimamizi na watumishi wa rasilimali zote za dunia (Mwanzo 1:28-30).
Kazi ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha ya mwanadamu. Tangu mwanzo, Mungu aliwapa watu wajibu mkubwa wa kufanya. Kila mmoja wetu atamjibu iwapo tumefanya kwa uaminifu kazi aliyotuachia.
Kanuni kutoka katika kitabu cha Mithali
Kitabu cha Mithali kiliandikwa mahususi kwa ajili ya vijana, kuwafundisha jinsi ya kufikiri na kutenda kwa hekima. Kitabu cha Mithali kina mambo mengi ya kusema kuhusu kazi:
► Wanafunzi wanapaswa wasome kila kifungu cha andiko kwenye Mithali kwa ajili ya kikundi.
Mithali 6:6-11, Mithali 10:5.
Mchwa ni mfano mzuri wa kuangaliwa kwa ajili ya wanadamu.
Wanafanya kazi kwa bidii sana ingawa hakuna anayewalazimisha kufanya kazi. Hakuna anayewaambia wanachopaswa kufanya au ni kwa jinsi gani wanapaswa kufanya, lakini bado wanafanya kwa tija kubwa. Kutokana na mchwa, tunajifunza kwamba hatupaswi kulazimishwa kufanya kazi. Tunapaswa tupende kufanya kazi kwa sababu hivyo ndivyo Mungu anavyotupatia mahitaji yetu.
Wanafanya kazi wakati wa kufanya kazi. Kuna wakati wa kufanya kazi, na kuna wakati wa kufanya shughuli nyingine, na kuna wakati wa kupumzika. Inaweza kusaidia kuuliza, “Je, ninapaswa niwe ninafanya nini kwa sasa hivi?”
Wanafanya kazi wakati kukiwa bado kuna fursa za kufanya kazi. Misimu inabadilika, na fursa za kupata rasilimali zinaweza zikapita. Fursa zetu pia huja na kutoweka. Ni lazima tutumie fursa tulizo nazo kwa sasa, au itapotea bure.
Wanafanya kazi ili baadaye wapate chakula wanachohitaji. Hatupaswi kulala au kupumzika wakati wa kufanya kazi. Kama tutakuwa wavivu katika wakati ambao tunapaswa tuwe tunafanya kazi nzuri, mahitaji yetu ya baadaye hayatapatikana. Tunapaswa tufanye kazi leo ili kuweza kupata mahitaji yetu ya kesho.
Mithali 19:15, Mithali 20:4, Mithali 12:24. Mungu ameiweka dunia katika namna ambayo uchaguzi wetu una matokeo halisi (Wagalatia 6:7).
Ikiwa tutendelea kuchagua kuwa wavivu kupitia miili yetu, tutakuwa wadhaifu kimwili. Kama tutaendelea kuchagua kwa wavivu katika mawazo yetu, uwezo wetu wa kujifunza, kufikiri na kuwaza utapungua.
Kama tutakataa kufanya kazi wakati tukiwa na uwezo, Mungu anasema tunastahili tukae bila ya chakula (Soma 2 Wathesalonike 3:6-12).
Ikiwa tutafanya kazi kwa bidii, mara nyingi Mungu atatupa thawabu ya kuongezeka kwa fursa na wajibu mkubwa.
Mungu ameweka matokeo ya ujumla kawa ajili ya chaguzi zetu. Hatuwezi kuchagua matokeo yetu, lakini tunaweza kuchagua ni kitu gani tutafanya!
Mithali 14:23, Mithali 20:6. Watu wengine wanajiona kwamba wana akili sana, lakini wanakataa kufanya kazi. Wanapenda kuota ndoto na kuzungumzia jinsi ambavyo mambo yanaweza kuwa, lakini wao wenyewe hawanyi jambo lolote. Kwa hakika, Mungu anatutaka tufanye kazi, na siyo kuzungumzia tu kuhusu jambo hilo. Anatutaka tuwajibike na kuwa waaminifu katika mambo tuliyosema kwamba tutafanya.
Mithali 15:19. Wakati mwingine watu huwa wavivu kuhusu jinsi wanavyofanya jambo fulani. Wanapenda kuchagua njia iliyo rahisi, hata kama haitakuwa na matokeo mazuri. Labda watafanya kitu ambacho hakina gharama, lakini kile wanachofanya hakitadumu baada ya muda fulani. Labda njia yao inahitaji juhudi kidogo sana, lakini umaliziaji wa pale mwishoni utakuwa wa thamani kidogo sana. Inawezekana wanakubali shinikizo kutoka kwa watu wengine badala ya kuwa tayari wao wenyewe kufanya kazi kupitia changamoto na kufanya kitu kilicho sahihi.
► Ni mifano gani unaweza kufikiria ambapo watu ni wavivu katika mbinu zao za kufanya jambo fulani?
Mithali hii inatufundisha kwamba tutakapokuwa wavivu katika kufanya yale tunayopaswa kuyafanya, itatuletea matatizo kwetu sisi na kwa watu wengine baadaye. Lakini tutakapofanya jambo ambalo ni sahihi, tutapata thawabu ya matokeo mazuri. Tunapaswa tuwe waangalifu na tulio wazi sasa, ili tuweze kufurahia matokeo mazuri baadaye.
► Je, ni mifano gani unaweza kufikiria ambayo uvivu umesababisha matatizo na migogoro mikubwa ya baadaye? Je, ni mifano gani unaweza kufikiria ambayo wakati kulipokosekana uaminifu na bidii kulisababisha kutokuwepo na matokeo mazuri?
Mithali 12:11, Mithali 21:20, Mithali 28:19. Kwenu ninyi vijana, Mungu hakukupa nguvu na afya uliyo nayo ili uweze kuzipoteza bure kwa kufuatilia mambo yasiyofaa. Amekuamini uwe msimamizi mzuri wa uwezo wako wa kimwili na kiakili. Amekupa fursa ya kumtumikia yeye. Kuwa mtumishi mzuri kunakuhitaji wewe uweze kujidhibiti mwenyewe. hautaweza kutimiza mambo yote kwa ajili ya furaha. Utalazimika uelekeze nguvu zako, rasilimali, na muda wako kwa ajili ya kutimiza makusudi ya Mungu.
Mungu anakutarajia utoe mahitaji yako mwenyewe, mahitaji ya familia yako (1 Timotheo 5:8), na kwa ajili ya mahitaji ya wale wote ambao wanahitaji msaada na hawana mtu mwingine wa kutoa kwa ajili yao(1 Timotheo 5:3-16, Waefeso 4:28, Yakobo 1:27, Yakobo 2:15-16).
1 Wathesalonike 4:11-12 inasema,
…Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu chochote.
Haya ni mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu wote ambao wameokoka/wameamini.
► Je, aina gani za kazi ambazo watu waliookoka/walioamini wanapaswa kuwa tayari kuzifanya? Je, kuwa na hadhi kuna umuhimu? Kama ni ndivyo, ni kwa njia gani au kwa kiwango gani?
Tutajenga juu ya mada ya kazi kwa kujadili fedha. Tumetoka tu kuzungumzia sababu muhimu sana ambazo Mungu anatutaka sisi tufanye kazi, ikiwa ni pamoja na kutupa sisi mahitaji yetu na mahitaji ya watu wengine. Kazi ni njia ya kawaida ya Mungu kwetu ya kutupa mahitaji yetu muhimu – chakula na mavazi (1 Timotheo 6:8). Katika maeneo mengi, watu hupata fedha kwa kufanya kazi, na kisha kuzitumia katika kupata mahitaji ya kimwili. Katika maeneo mengine, watu wanalipwa kwa kupewa chakula, mali, au kupatiwa huduma nyingine badala ya fedha. Kwa njia yeyote ile, Mungu anatoa kwa ajili ya mahitaji ya watu kupitia kazi zao.
[1]Kupata zaidi kuhusu somo hili, ona somo la 3 katika kitabu cha Kuishi Maisha ya Kikristo kwa Vitendo kinachopatikana kutoka Shepherds Global Classroom.
Kuhusu Fedha
Vifungu vingi vya Maandiko vinazungumzia mada ya fedha. Jinsi tunavyofikiri na kushughulika na fedha huathiri sana uhusiano wetu na Mungu na watu wengine. Kwa kuwa ni jambo muhimu sana, Mungu anatutaka sisi tuwe na ufahamu sahihi kuhusu fedha na matumizi yake.[1]
Kanuni kutoka katika kitabu cha Mithali
► Wanafunzi wanapaswa wasome kila kifungu cha andiko kwenye Mithali kwa ajili ya kikundi.
Je, ni nini chanzo cha usalama wetu?
1. Mungu ndiye mtoaji wa mwisho kwa wenye haki (Mithal 10:3).
2. Hatupaswi kupenda na kutumaini utajiri, kwa sababu una mipaka katika uwezo wake na ni wa muda kwa kipindi fulani (Mithali 11:4, 28).
► Je, ni mawazo gani, mitazamo, na matendo gani yanayoonyesha kumtumaini Mungu kuwa mpaji na usalama wa mtu?
Kuna mambo mengi yaliyo muhimu zaidi kuliko utajiri; kwa mfano:
1. Kuwa na mahusiano mazuri na watu wengine (Mithali 15:17).
2. Kuwa na maarifa na hekima (Mithali 8:10-11).
3. Kuwa na hofu ya Mungu na kuwa katika uhusiano sahihi na yeye (Mithali 15:16).
4. Kuwa na heshima kwa sababu ya kuwa na tabia njema (Mithali 11:16).
5. Kuwa mwaminifu, mpole na mwenye upendo (Mithali 19:22).
► Je, ni kitu kipi katika haya ambacho kina changamoto zaidi kwako kwa ajili ya mazingira yaliyopo?
Kanuni za kusimamia fedha kwa usahihi:
1. Kupata fedha kupitia kazi ya bidii na uaminifu (Mithali 10:4).
2. Kusanya pesa kwa uvumilivu na kwa muda (Mithali 13:11).
3. Mheshimu Mungu kwa kumpa fungu la kumi la mapato yako ya kwanza. (Mithali 3:9-10).
4. Kuwa mkarimu kwa maskini (Mithali 11:24-25, Mithali 14:21, Mithali 19:17, Mithali 21:13).
► Je, ni kitu kipi katika haya ambacho kinakufanya uhangaike zaidi?
Maonyo dhidi ya kuwa na matumizi mabaya ya fedha:
1. Kamwe usiliasi Neno la Mungu kwa ajili ya fursa ya kupata fedha (Mithali 10:2, Mithali 15:27).
2. Usifanye maamuzi ya haraka au ya kizembe (Mithali 21:5).
3. Usiahidi kulipa madeni ya watu wengine (Mithali 6:1-5; Mithali 17:18).
► Je, ni kanuni ipi kati ya hizi za Mithali ambayo imepuuzwa sana katika utamaduni wako?
[1]Kupata zaidi kuhusu somo hili, ona somo la 9 katika kitabu Kuishi Maisha ya Kikristo kwa Vitendo, kinachopatikana kutoka Shepherds Global Classroom.
Marafiki wa Karibu
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 13:20 na 1 Wakorintho 15:33 kwa ajili ya kikundi.
Urafiki wa karibu ni mojawapo ya ushawishi mkubwa zaidi katika maisha ya kijana mkomavu. Kwa kawaida watu hufanyika kuwa marafiki wa karibu na wale wanaoshirikishana maadili yao. Lakini urafiki humbadilisha kila mtu aliyeko kwenye urafiki, kwa mazuri au mabaya. Kuendelea kuwa marafiki wa karibu na mtu baada ya muda kutakushawishi. Mtazamo wako, falsafa zako, vipaumbele vyako, tabia yako, chaguzi zako na mwenendo wako vitaathirika. Marafiki wako wa karibu watakushawishi kwa mifano yao ya maisha, kwa wao kuidhinisha au kutoidhinisha chaguzi zako na kwa maneno yao ya kuvutia na au kushawishi.
► Kila mwanafunzi anapaswa kuandika majina 1-5 ya watu mahususi katika kujibu kila moja ya maswali haya:
Je, kwa kawaida ni nani namtegemea ili kupata kibali na uthibitisho?
Je, huwa ninazungumza na nani kuhusu matatizo yangu ya maisha?
Je, ninatafuta ushauri wa nani ninapokuwa nataka kufanya uamuzi?
Je, ni tabia ya nani inayoleta ushawishi kwenye tabia yangu?
Je, ninashirikishana na nani falsafa zangu?
Fikiria juu ya watu ambao umeandika majina yao. Tabia zao zikoje? Mazungumzo yao yakoje? Kama utafuata mfano wao, je utakuwa unamfuata Kristo? (1 Wakorintho 11:1).
Je, ni watu walio na sifa hizi?
Wenye kuwa na hofu ya Mungu (Kumbukumbu la Torati 10:12, 20, Zaburi 112:1).
Wanaimarishwa na Neno la Mungu (Yohana 17:14-17).
Wanafanya kipaumbele cha kwanza ni kumpendeza na kumtii Bwana katika kila kitu (2 Wakorintho 5:9-10).
Je, wanakushawishi wewe kutembea na Mungu kwa ukaribu na utiifu? Je, wanakuambia yaliyo kweli (yale yanayopatana na Neno la Mungu), au je, wanakuambia lililo rahisi kusikia? Je, wanakutia moyo kufanya jambo ambalo ni sahihi mbele za Mungu hata inapokuwa ni katika hali ya matatizo?
Wakati fulani kulikuwa na kijana ambaye alikuwa na ushawishi sana. Vijana wengine walimtegemea sana kwa ajili ya kupata kibali cha tabia zao. Walipotaka kuongea kitu ambacho ni cha kejeli au chenye maneno machafu, walikuwa wanamtazama ili kuona kama alikuwa anacheka. Walipofanya jambo la uasi walimwangalia kama atapepesa jicho lake, kuonyesha kukubaliana nao. Walikuwa wanataka wamfurahishe. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyeacha kufikiria na au kujiuliza maswali haya: Je, kwa nini ninahitaji kibali chake? Je, yeye ni mtu ambaye ninapaswa niwe najaribu kumfurahisha? Je, tabia na mwenendo wake ni kielelezo kizuri kwa ajili yangu?
Inahitaji juhudi kufikiria kuhusu masuala haya. Waumini wanapaswa wawe na kusudi ambalo litawafanya watake kuchagua marafiki wa karibu na wenye ushawishi mkubwa. Bila shaka, Mungu anataka watu wake wawe wanawashawishi watu wengine ambao hawajakomaa kiroho au ambao bado hawajaokoka, lakini watu hao hawana sifa ya kuwa marafiki wetu wa karibu, washauri, au watu wa kutushawishi. Hatupaswi tuwe tunatafuta kibali kutoka kwao.
► Mwanafunzi anapaswa asome Zaburi 101 kwa ajili ya kikundi.
Zaburi hii iliandikwa na mfalme Daudi. Alikuwa na hofu ya Mungu. Alijikabidhi kabisa kwa Bwana kwamba angeishi maisha ya uadilifu. Alijua kwamba watu aliowaruhusu wawe kishawishi kwake aidha watamsaidia kukamilisha ahadi yake au wangemzuia asiifanye. Kwa sababu hiyo, alidhamiria kuchagua watu wachache tu walio waaminifu na wenye kumcha Mungu wawe washawishi wake.
Sisi siyo mfalme kama Daudi alivyokuwa na kwa kawaida hatuna mamlaka au wajibu wa kuwaadhibu watenda maovu kama Daudi alivyokuwa ameahidi kufanya. Hata hivyo, tunapaswa kufuata mfano wa Daudi kwa namna nyingine. Ni lazima tujitolee kabisa kuishi maisha ya uadilifu. Ni lazima tuamue kwamba tutachagua watu wacha Mungu tu kama marafiki wetu wa karibu na washawishi wakubwa zaidi.
Kufanya Maamuzi
Utu uzima wa mapema ni wakati ambao unafaa kwa kufanya maamuzi mengi, ambayo baadhi yao yatakuwa na matokeo ya maisha yote (yumkini hata milele).[1] Yafuatayo ni baadhi ya maswali machache ambayo tunapaswa tuyazingatie katika akili zetu wakati tunapofanya chaguzi zetu mbalimbali:
Je, kitendo hiki kinalingana na jinsi Mungu anavyotaka niwe? Jamii inatuambia kwamba, “Kuwa wewe mwenyewe.” ”Kuwa mkweli wewe mwenyewe.” “Fuata moyo wako mwenyewe.” Lakini tumeitwa kuwa waaminifu kwa Kristo, siyo kwa ajili yetu wenyewe. Kwa hakika, anatuambia sisi tuseme, “Hapana” kwa matamanio yetu wenyewe yanapokuwa yanapingana na utii wetu kwake (Mathayo 16:24-26). Mungu anatuita tuishi katika kiwango chake cha haki. Anaelezea kuhusu watu ambao watabarikiwa, wenye hofu na utii kwenye kila jambo (Zaburi 15, Zaburi 112, Mathayo 5:3-11). Jinsi tutakapokuwa tunamfuata kwa uaminifu, ndivyo tutakavyokuwa tunafanyika kuwa watu wa Mungu kama anavyotutaka tuwe.
Je, kitendo hiki kitaathirije sifa yangu? Kwa kila uchaguzi tunaoufanya, tunajijengea sifa yetu wenyewe. (Mithali 20:11). Ni kweli kwamba tunapaswa tujali zaidi kuhusu kile ambacho Mungu anatuwazia sisi. Lakini tutakapokuwa tumefahamika kama ni watu wenye uadilifu, tunawashawishi watu wengine kwa mambo yaliyo sahihi na kuwa mashahidi waaminifu kwa ajili ya Kristo. Mithali 22:1 inatuambia kwamba tunapaswa kutanguliza kuwa na jina jema kuliko mali nyingi.
Je, ni matokeo gani yatafuata uchaguzi huu? Andiko la Mithali 22:3 linatuonyesha kwamba tunapaswa tujiandae kwa ajili ya baadaye kwa kufanya maamuzi mazuri leo. Tunapokuwa tunatafakari kuhusu chaguzi zetu, ni lazima tuzingatie yanayowezekana kutokea kwa kila moja. Je, ni kwa jinsi gani chaguzi zetu zinaweza kuathiri maisha yetu wenyewe na maisha ya watu wengine?
Andiko la Mithali 4:23 linatuambia kwamba chaguzi na tabia zetu zinatokana na misukumo iliyoko ndani ya mioyo yetu. Kama tunataka tufanye chaguzi zilizo nzuri na zinazompendeza Mungu, ni lazima tuhakikishe kwamba tunakuwa waaminifu kwake (Kumbukumbu la Torati 6:2, 5-6, Kumbukumbu la Torati 13:4).
[1]Kupata zaidi kuhusu somo hili, ona somo la 5 katika kitabu cha Kuishi Maisha ya Kikristo kwa Vitendo kinachopatikana kutoka Shepherds Global Classroom..
Afya ya Kimwili
Vijana wakomavu wanawajibika kwa ajili ya chaguzi binafsi, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na vile wanavyokula, shughuli zao za kimwili na ratiba za mazoezi yao ya mwili, na tabia zao za kulala. Kujidhibiti binafsi ni muhimu sana kwenye haya maeneo yote (1 Wakorintho 9:27). Watu waliookoka/waumini wanapaswa kutambua kwamba miili yao ni hekalu la Roho Mtakatifu na kwamba Tumekombolewa kwa damu ya Yesu (1 Wakorintho 6:19-20). Kwa kuwa pia sisi ni watumishi wa Mungu, tunapaswa tuitunze miili yetu na kujitia katika nidhamu ya kufanya chaguzi zilizo nzuri katika kila moja ya shughuli hizi, ili tuwe katika ubora wetu kwa ajili yake.[1]
► Wanafunzi wanapaswa wasome 1 Wakorintho 6:12-13, 19-20, na 1 Wakorintho 10:31 kwa ajili ya kikundi.
Fikiria kuhusu uchaguzi wako wa chakula na kiasi cha chakula kwa wiki zima iliyopita. Inawezekana ulikuwa na chakula kingi cha kutosha na chaguzi nyingi kuhusu kile ambacho ulikuwa unataka kula. Labda ulikuwa na chakula kidogo, ukiwa na uchaguzi mdogo wa vyakula utakavyokula. Kwa namna yeyote ile, kula na kunywa kwako kunapaswa kumpe Mungu utukufu. Kama kungekuwa na uwezekano wa Yesu kukaribishwa aje anywe na kula pamoja na wewe, je, ungechagua vyakula vilevile na kiasi kilekile unachochagua katika hali ya kawaida?
Swali hili linawezekana kuonekana kama ni lisilokuwa na maana, lakini labda linaweza kutumika kama ukumbusho wa kufikiria, kumshukuru, na kujidhibiti wakati wa kula chakula.
Usingizi ni eneo lingine ambalo waumini wanapaswa kudhihirisha jinsi ya kujidhibiti. Hatupaswi kuwa wavivu na kulala sana (Mithali 6:10-11, Mithali 20:13), wakati bado Mungu ameumba miili yetu katika uhitaji wa mapumziko ya mara kwa mara na yanayotosheleza (Zaburi 3:5). Watu wazima wenye afya njema wanahitaji masaa 6-8 ya kulala kwa kila usiku mmoja.
Katika Mhubiri 5:12 tunaelezwa kwamba usingizi ni zawadi kwa wale wanaofanya kazi kwa bidii. Mithali 3:24 na Zaburi 4:8 inazungumza juu ya usingizi mtamu, wa amani ambao Mungu huwapa watoto wake. Huu ni aina ya usingizi ambao unarejesha miili yetu. Kukiwepo na amani ya Mungu, tunawekwa huru kutokana na mashaka na mahangaiko ya siku, tukijua kwamba Mungu aliye mwaminifu anatuangalia sisi. Usingizi wenye utulivu huleta nguvu na akili kwa ajili ya miili yetu, na kututayarisha kwa ajili ya majukumu na huduma nyingine zinazofuata.
Mithali 3:24 inapatikana ndani ya sehemu ya kitabu cha Mithali inayojumuisha maagizo ya kuishi maisha yaliyojaa hekima, ufahamu, na busara za kuamua. Kama utataka kuwa na usingizi mtamu, unapaswa ufanye maamuzi ya busara kwenye maeneo mengine ya maisha yako, ikiwa ni pamoja na muda wako unaoutumia wa kuangalia runinga, au picha za video, kuperuzi mitandao ya intaneti, au matumizi ya simu, na kutumia muda mwingi pamoja na marafiki.
Usingizi unaweza kuharibiwa na chaguzi zako za vyakula na kiasi cha upatikanaji wake kwa siku, kiasi cha mazoezi ambayo umekuwa nayo, jinsi ulivyokabiliana au navyoshughulika na mambo magumu, na jinsi ambavyo unatumia fedha zako. Usingizi unaweza kuwa mtamu wakati mahusiano yetu na watu wengine yanapokuwa yamejazwa na tabia ya tunda la Roho yaliyoorodheshwa katika Wagalatia 5:22-23.
► Chukua muda kusoma Maandiko yaliyorejewa katika sehemu hii hapo juu.
Fanya tathmini kuhusu usingizi wako wa mujibu wa kanuni zinazopatikana katika maandiko haya. Je, unaupa mwili wako mapumziko yanayohitajika ili uweze kufanya kazi vizuri kama Mungu alivyokusudia?
Jaribu kuchunguza muktadha wa Aya zinazotoka katika kitabu cha Zaburi: Daudi anaziandika katika hali zenye mfadhaiko sana na bado anashuhudia uaminifu wa Mungu katika kumsaidia kurejesha hali ya mwili wake kupitia usingizi.
[1]Kupata zaidi kuhusu somo hili, ona somo la 13 katika kitabu cha Kuishi Maisha ya Kikristo kwa Vitendo kinachopatikana kutoka Shepherds Global Classroom..
Kushughulika na Mfadhaiko
Kwa utaratibu wa Mungu, miaka ya mwanzo ya mtu mzima imejaa majukumu na mambo mengi ya kuhudumia ambayo yanahitaji umakini mkubwa na yanayosababisha mfadhaiko (Maombolezo 3:27). Mtu anaweza akawa anajaribu kumaliza elimu yake ya shahada, aanzishe biashara, na kuwa anafanya kazi au kazi nyingine kadhaa. Kuna mahusiano mengi mchanganyiko ambayo yanahitaji umakini wa mwelekeo wa kimakusudi kutoka kwa kijana. Mambo ya fedha, mahitaji ya usafiri, na kuwa na nyumba yote haya yanahitaji umakini wa mtu, lakini yanaleta mfadhaiko mkubwa.
Mfadhaiko umefafanuliwa kama ni “mwitikio wa kimwili na mhemuko kutokana na matukio ambayo yanatutisha au kutupa changamoto.”[1] Jaribu kufikiria jinsi unavyoziangalia hali unazopitia. Je, akili yako inafanyaje kazi katika hali unayopitia sasa?
Kunapokuwa na Jambo mbele yako, ni kwa jinsi gani unakuwa ukilifikiria? Unaruhusu ujisikie mihemuko ya aina gani kuhusu uwezekano? Je, ni mtazamo gani unaoathiri jinsi ya kukabiliana na hali hiyo? Kwa ujumla silika na hulka yako ni nini? (Mithali 15:15)?
Mtazamo, silika, na hulka yako vyote vina vinagusa jinsi unavyokabiliana na hali za maisha unazopitia na kiwango cha mfadhaiko utakachokuwa nacho. Wakati mfadhaiko ni sehemu ya kawaida ya maisha, namna ya kukabiliana na mfadhaiko huo ni jambo binafsi. Wakati mwingine wasiwasi husababisha maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, magonjwa, shinikizo la damu, vidonda vya tumbo, na matatizo mengine mbalimbali ya kiakili, kimhemuko, na kimwili (Mithali 12:25). Upokeaji mbaya wa mfadhaiko unaweza kuzuia sana huduma yako kwa ajili ay Kristo. Kwa sababu hiyo, siyo jambo la kushangaza kwamba Neno la Mungu linatuambia kwamba hatupaswi kuwa na wasiwasi au kuwa watu wenye dukuduku.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mathayo 6:34, 1 Petro 5:7, na Zaburi 105:4 kwa ajili ya kikundi.
Tunapokabiliwa na hali nzito zenye kutuelemea, ni lazima tuchague kumtumaini na kumtegemea Mungu, yeye peke yake asiyekuwa na mipaka. Yeye ni mkamilifu katika nguvu, hekima, na wema. Anawajali watoto wake kikamilifu. Anatutaka tutambue utegemezi wetu kwake, tumpelekee haja zetu zote, na tutafute nguvu zake kutoka kwake. Tutakapokuwa tunafanya hivyo, anaweza kutupa amani, pumziko, na mambo yote tunayohitaji kutoka kwake. Tukiwa katika ujana wetu, ni lazima tujifunze kuwa watulivu na wakimya mbele za Mungu na tumngojee yeye kwa ajili ya kutuongoza (Zaburi 46:10, Maombolezo 3:25-27).
► Orodhesha hali za mfadhaiko unazokabiliana nazo kwa sasa. Je, uwajibikaji wako unapaswa uweje kwa mujibu wa Neno la Mungu?
[1]Robert S. Feldman, Discovering the Lifespan, 2nd ed. (Upper Saddle River, NJ: Pearson, 2012), 317.
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Katika somo hili, je, ni mawazo au kanuni gani ambazo zimekuwa mpya kwako? Je, ni kanuni gani nyingine za kibiblia ambazo umezifikiria kwamba zinahusiana na maeneo haya ya maisha ya kijana mkomavu?
► Je, maisha yako binafsi yataguswaje na kile ambacho umejifunza katika somo hili?
► Katika kanisa lako, ni mada zipi katika hizi zinazohitajika kushughulikwa zaidi miongoni mwa waumini vijana wakomavu?
► Unawezaje kuwashawishi vijana wa Kikristo ambao unawajua waweze kufikiri na kuishi kibiblia katika haya maeneo ya maisha?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa ajili ya Neno lako ambalo linatufundisha jinsi ya kuishi kwa ajili yako katika kila hatua ya maisha yetu. Asante kwa kutuandaa tuweze kuishi maisha yenye matunda na tija katika miaka yetu ya ujana mkomavu.
Tusaidie tukutukuze wewe kwa kuwa watumishi waaminifu wenye nguvu rasilimali, na fursa unazotupa. Tusaidie tuwe mvuto wa kimungu kwa wengine na kuchagua marafiki ambao ni washauri na wacha Mungu.
Tuwezeshe tufanye maamuzi ya busara na kukuheshimu wewe kwa miili yetu, akili zetu, na roho zetu.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Katika 1 Timotheo 4:12, Paulo alimwagiza Timotheo kwamba alipaswa awe mfano kwenye maeneo mahususi. Kwa kuandika, Fafanua kila moja ya maeneo haya. Kisha elezea jinsi kila kimoja katika haya kinavyowezekana kwa kijana mkomavu kuishi. Toa angalau mfano mmoja wa vitendo kwa kila kipengele kimoja.
(2) Chagua mojawapo ya mada zilizopo katika somo hili:
Ukomavu na tabia
Tabia
Fedha
Marafiki wa karibu
Kufanya maamuzi
Afya ya mwili
Mfadhaiko
Andika angalau aya zisizopungua tatu kuhusiana na mada uliyochagua:
Tengeneza muhtasari wa kanuni zote za kibiblia zinazohusiana na mada hiyo.
Elezea baadhi ya matukio chanya yanayotokana na kuwa mtiifu kwa hizo kanuni.
Elezea baadhi ya matukio hasi yanayojitokeza wakati kanuni hizi zinapokuwa zimepuuzwa.
Utakapokuwa unaandika kuhusu haya matokeo chanya na hasi, hakikisha kwamba unafikiria kuhusu athari za chaguzi binafsi za mtu kwa ajili ya watu tofauti: mtu huyo mwenyewe, familia yao, jumuiya yao, na kanisa lao.
Print Course
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.