Susanna Wesley alizaa jumla ya watoto 19, lakini kutoka na hali za nyakati zile, watoto tisa (9) hawakuweza kuishi kwa muda refu wakifariki dunia. Watoto kumi (10) aliowalea ni pamoja na Yohana na Charles Wesley. Mtoto wake Yohana, baada ya kuwa mtu mzima, alimsihi mama yake amwandikie maelezo kuhusiana na mbinu zake za kulea watoto, na mama akamtumia barua yenye maelezo haya.[1]
Watoto walikuwa wamefundishwa kuhusu Sala ya Bwana mara tu walipoanza kuongea, na walikuwa wakiirudia kila siku asubuhi na jioni. Watoto walikuwa wakisoma sura moja ya maandiko kwa pamoja kila siku. Nyakati hizo wanawake wengi walikuwa na elimu duni, lakini Sussana alisisitiza kwamba watoto wake wote wanapaswa wafundishwe kusoma. Alipa kipaumbele ufahamu wa kusoma na kuandika kuliko kujifunza kazi.
Susanna alisema, “Ubinafsi ndio shina la dhambi na taabu zote.” Aliwafundisha watoto wake jinsi ya kudhibiti misukumo yao na kujikabidhi kwa mamlaka halali. Alisema kwamba kila kitendo cha utii kinapaswa kupongezwa hata kama hakikufanyika vizuri au kwa ukamilifu. Makosa yanaweza kuvumiliwa, lakini kila uasi wa kukusudia unapaswa kuadhibiwa.
Siku zote familia walikula chakula wakiwa pamoja, na watoto walijifunza kula chochote ambacho kilitolewa bila ya kuwepo na manukuniko.
Biblia inatuambia kwamba, “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto…” (Mithali 22:15). Mtunga Zaburi anasema kwamba watoto huzaliwa wakiwa wanasema uongo, “...Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.” (Zaburi 58:3). Kwa kuwa jambo hili ni la kweli wazazi wana wajibu wa kusahihisha watoto wao.
Ikiwa ungempa mtoto wa miaka mitatu chaguo kati ya kuwa na bakuli la aiskrimu hivi sasa au kumiliki kiwanda cha aiskrimu mwaka mmoja ujao, angechagua kuwa na aiskrimu sasa. Hata kama mzazi ataelezea uchaguzi mwingine, mtoto angechagua aiskrimu sasa ikiwa angefanya uamuzi wake mwenyewe. Mfano huo unatuonyesha kwamba maelezo peke yake hayatoshi kumrekebisha mtoto.
Maelezo kuhusu mema na mabaya hayatoshi kumsahihisha/kumrekebisha mtoto, kwa sababu:
1. Mtoto hawezi kuelewa mawazo ya mtu mzima (1 Wakorintho 13:11).
2. Mtoto hawezi kuona matokeo kamili na ya muda mrefu kuhusiana na matendo yake.
3. Mtoto hajakomaa vya kutosha kuweza kudhibiti misukumo na matamanio yake kwa kufikiri.
Labda itaonekana ni ukatili kuleta maumivu ya kimwili kwa mtoto, lakini baba anayewapenda watoto wake atafanya hivyo ili kuzuia madhara mabaya zaidi: “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.” (Mithali 13:24). Kwa mfano, mtoto mdogo anayecheza karibu na moto anaweza akaanguka ndani yake na kusababisha kupata majeraha makubwa kwa sababu haelewi madhara ya moto. Lakini ikiwa mama yake atamrudi kwa kumchapa fimbo anaposogea kutaka kuwa karibu sana moto, yale maumivu madogo ya kuchapwa fimbo yatazuia kutokea kwa maumivu makubwa yatakayotokana na moto.
Baadhi ya watu wengine wamenyanyaswa kimwili na watu wengine ambao wasiowapenda. Uzoefu wao unawafanya wachukie wazo la mtu yeyote kumwadhibu mtoto kimwili. Hata hivyo, mzazi anayepuuza kumsahihisha mtoto ipasavyo husababisha matatizo mengi kwa mtoto wake baadaye.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 19:18 na Mithali 29:17 kwa ajili ya kikundi.
Masahihisho kwa mtoto yanapaswa yaanze wakati ana umri wa kutosha kuweza kuelewa kwamba anapingana na wazazi wake. Hata yule mtoto sana huwa anajua anachokifanya wakati anapokataa kuonyesha ushirikiano na mzazi.
Masahihisho mengi kwa mtoto ni lazima yafanyike wakati mtoto akiwa ni mdogo na mwepesi wa kuweza kuumia (Mithali 22:15). Kama vile udongo unavyozidi kuwa mgumu kadri muda unavyopita na kuwa vigumu kuweza kuufinyanga katika umbo unalolitaka, ndivyo tabia ya mtoto inavyokuwa ngumu zaidi kuitengeneza kadri muda unavyozidi kupita. Kama mtoto anaendelea kutotii wazazi wake baada ya umri wa miaka kumi (10), wazazi wanakuwa hawajafanikiwa kwenye masahihisho ya mtoto wao, na fursa zao za kufaulu kumsaidia kwa ukamilifu zinazidi kufifia. Masahihisho ya kimwili nayo huwa hafifu na yasiyotosha kadri mtoto anavyoendelea kukua. Ni makosa kwa mzazi kufikiria kwamba masahihisho kwa mtoto yatakuwa marahisi zaidi wakati atakapokuwa amekua katika umri mkubwa, itakuwa ni vigumu zaidi na hatimaye itakuwa haiwezekani tena kabisa.
Kadri mtoto anavyousogelea utu uzima, inakuwa haiwezekani tena kumsahihisha kimwili kama wakati alivyokuwa mtoto. Kijana wa kiume au wa kike anahitaji heshima hata kama tabia zao hazijakomaa. Mzazi anaweza akatumia njia nyingine za kufanya masahihisho kama vile kupunguza muda wa burudani kwa mtoto, au muda wa matumizi ya simu au shughuli za kijamii, lakini mawasiliano ya upendo na yaliyo makini yatakuwa ni ya muhimu zaidi. Ni lazima mzazi atambue kwamba kijana anafanya maamuzi ya kweli, na ingawa mzazi ana ushawishi wake, hawezi kumzuia kijana asitumie mapenzi yake binafsi na kupata matokeo ya maamuzi.
Baadhi ya wazazi hawana uhakika wa jinsi ambavyo wanapaswa kuwa wakali wakati wa kutoa adhabu ya kimwili kwa mtoto. Kama mtoto atakuwa bado ni mwenye hasira na mwenye kuendelea kuasi baada ya masahihisho, adhabu itakuwa haikuwa nzito ya kutosha kumwadhibu (kanuni hii haiwezi kutumika kwa mtoto ambaye ni mkubwa sana kiasi kwamba hawezi kurekebishwa kwa njia ya adhabu ya kimwili kwa ufanisi). Masahihisho yanapaswa yawe makali sana ili kumfanya mtoto ajutie kutotii kwake na achague kutii mamlaka. Masahihisho hayapaswi yasababishe madhara ya kimwili. Masahihisho ambayo husababisha michubuko au kuweka alama zinazobakia kwa muda mrefu kwenye ngozi ya mwili inaweza ikawa ilikuwa ni kali sana kupita kiasi.
Biblia inatumia mfano wa adhabu ya kimwili kuelezea njia ambayo Mungu hushughulika na watoto wake.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 3:11-12 na Waebrania 12:5-8 kwa ajili ya kikundi.
Vifungu hivi vya maandiko vinatuambia kwamba Mungu huwaadibisha watoto wake kwa sababu anawapenda. Vivyo hivyo, Baba humuadhibu mtoto wake kwa sababu anampenda. Kuadhibiwa kiukamilifu ni ishara ya upendo. Kukosekana kwa nidhamu ni ukosefu wa upendo.
Marekebisho ya kimwili humfundisha mtoto kujidhibiti yeye mwenyewe kwa sababu hujifunza jinsi ya kujizuia na vishawishi, kwa sababu anajua kwamba atakutana na adhabu kama akitenda makosa. Anapokuwa anapinga vishawishi vya kutenda maovu, anajenga tabia yenye nguvu. Anapokuwa mtu mzima atakuwa na uwezo wa kujizuia na majaribu kwa sababu ana uelewa wa madhara na au matokeo yake na siyo kwa sababu ya adhabu ya kimwili. Hata hivyo, mtoto ambaye hapatiwi masahihisho ya mara kwa mara anakuja kuwa mtu mzima ambaye ni mdhaifu sana kuweza kuzuia majaribu hata wakati anapotambua kwamba ni mabaya kwake.
Jaribu kufikiria mzazi anayempa mtoto wake peremende tu za kula kwa sababu mtoto anataka. Hataki kumfanya mtoto asiwe na furaha, lakini anafanya jambo litakaloletea madhara kwa mtoto. Vivyo hivyo, mzazi anayekubaliana na au anayetetea tabia mbaya ya mtoto wake kila wakati anafanya uharibifu mkubwa kwenye tabia ya huyo mtoto na kwenye hali yake ya baadaye. Hata hivyo Biblia inasema kwamba mzazi asiyetumia fimbo yake kumsahihisha mtoto wake anamchukia (Mithali 13:24).
Mtoto anayeishi katika nyumba isiyo na mipaka hana furaha. Mipaka huleta usalama Ikiwa mtoto anajifunza kwamba huwa anapata kitu anachokitaka kwa kugombana na kupandishiana hasira, atakuwa anafanya hivyo kila wakati, lakini hatafurahi. Watoto wanakuwa na furaha wanapojiona wako kwenye usalama na wanaongozwa chini ya misingi yenye mipaka, bila kuhisi kwamba ni lazima wapigane na kukataa udhibiti ili kuwa na chochote. Mtoto asiye na nidhamu huwa na furaha mara chache.
Wakati mtoto mdogo anapofikia kuwa mtu mzima, dunia haitaweza kumpatia chochote atakachokihitaji. Hataheshimiwa na kukuzwa ikiwa hana adabu, ni mtu mbinafsi, na asiyewajibika. Mzazi anapaswa kumlea mtoto wake katika njia ambayo itamtayarisha kwa ajili ya maisha. Wazazi ni lazima wakumbuke kwamba hawalei watoto wadogo; bali wanalea watu wazima.
Mzazi anapaswa kueleza na kuonyesha kwamba kumsahihisha mtoto wake ni kwa kusudi la kumsaidia mtoto asitawi na kuwa mtu wa tabia nzuri anayeweza kutegemewa na kuheshimiwa.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 22:15, Mithali 23:13-14, na Mithali 29:15 kwa ajili ya kikundi.
Kumbuka kwamba kusudi la kufanya masahihisho ni kumkuza mtoto. Mtoto anapokuwa ameelewa kosa alilolifanya na tayari akaonyesha kujuta, masahihisho ya kimwili hayawi ya lazima tena. Kusudi kubwa ni masahihisho, na siyo kumhukumu; mzazi hana hitaji tena la kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata adhabu inayostahili.
► Je, marekebisho ya mzazi yana tofauti gani na matendo ya mtu anayedhulumu na kusababisha madhara ya kimwili ili kuwafanya watu wafanye anachotaka?
Mtu mjeuri yuko tayari kuwadhuru watu wengine ili kupata kile anachotaka. Mzazi anampenda mtoto wake. Masahihisho ya kimwili ni kwa manufaa ya mtoto. Mzazi mwenye upendo hatataka amdhuru mtoto wake. Mtu hawezi kuhisi kwamba mnyanyasaji au mkandamizaji anampenda, lakini mtoto anaweza kujua kwamba anapendwa hata anaporekebishwa. Anaweza akatambua kwamba anapendwa hata katika wakati ambao amefanyiwa masahihisho. Anaweza akatambua kwamba maisha kwake ni mazuri zaidi kutokana na mamlaka ya wazazi wake.
Baadhi ya wazazi huadhibu kwa ukali sana na kwa mambo yasiyokuwa sawa kwa sababu ya hasira au ukatili. Wanamdhuru mtoto wao kimwili na kimhemuko. Wanawaadhibu watoto wao kama njia ya kuwaondolea mfadhaiko au kuchanganyikiwa na maisha. Hili ni tatizo kubwa ambalo halipaswi kuendelea kuvumiliwa na watu wengine wanaoliona. Marafiki, majirani, na jamaa wa ukoo wanapaswa kukabiliana na mtu anayemdhulumu mtoto. Mwenzi wa mzazi anayemnyanyasa mtoto anatakiwa atafute msaada kutoka kwa jamaa wa ukoo, marafiki au mchungaji. Ni jambo la muhimu sana kumlinda mtoto.
► Baadhi ya wazazi huwadhalilisha watoto wao hadharani wanapokuwa wamefanya makosa. Je, hii ni njia nzuri ya kufanya masahihisho?
► Mwanafunzi anapaswa asome Waefeso 6:4 kwa ajili ya kikundi.
Mtoto anahitaji kuwa na uhakika kwamba wazazi wake wanampenda na kwamba masahihisho yeyote yanayofanywa ni kwa ajili ya manufaa yake. Wakati mtoto anapokuwa amenyanyaswa na wazazi wake, hujisikia kutopendwa. Anaweza kuwa na uchungu na kujihisi kwamba mamlaka ya wazazi wake ni jambo baya sana analohitaji aliepuke. Wazazi wanapaswa kuwarekebisha watoto wao faraghani na kuepuka kuwaadibisha watoto wao mbele ya kadamnasi ya watu. Wazazi wanapaswa wawaelekeze na kuwasahihisha watoto wao kwa upole na uvumilivu.[1] Kwenye Mithali 16:21b tunaambiwa kwamba "...Utamu wa maneno huongeza elimu."
► Jaribu kufikiria kwamba ulimwambia mtoto wako akusaidie kulisha wanyama wako. Uliporudi nyumbani jioni ukakuta kwamba bado wanyama hawakulishwa. Umechoka kwa kufanya kazi siku nzima, lakini sasa ni lazima ulishe wanyama kabla hujaanza kupumzika kwa sababu mtoto wako hakutaka kukutii wewe. Je, utashikwa na hasira? Je, ni kosa kwa mzazi kuwa na hasira dhidi ya mtoto wake?
Mzazi anapaswa akumbuke kwamba kusahihisha kunapaswa kumnufaisha mtoto. Mzazi anapokasirika kwa sababu anajisikia kutoheshimika au kwa sababu ya mtoto kutomtii kunamsababishia usumbufu na au maudhi, anakuwa na hasira isiyoweza kufanya jambo lolote jema (Yakobo 1:20). Hasira yake ni ya ubinafsi.
Mzazi anaweza kudhihirisha hasira yake ifaayo kwa mtoto kwa njia hii: “Mwanangu, hukuwalisha wanyama wangu kama nilivyokuwa nimekuagiza. Wanyama walikuwa na njaa, na wangeendelea kuwa na njaa hata usiku kama siyo mimi kuchukua hatua ya kuwalisha. Ilibidi niamue kuwalisha ingawaje nilikuwa nimechoka sana kwa kazi za siku nzima. Nina hasira kwa sababu sitaki uwe mtu unayepuuzia mahitaji ya watu wengine kwa ajili ya wewe kutotimiza wajibu wako. Katika Mithali 12:10 tunafundishwa kwamba, ‘Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.’”
Rebeka aliwaambia watoto wake wasichukue chakula au kinywaji kwenye chumba ambacho kilikuwa na zulia jipya sakafuni. Siku iliyofuata aliona mmoja wa watoto akila chakula kwenye lile zulia, akamkemea. Baadaye tena mmoja wa watoto wake alitembea kwenye zulia akiwa amebeba bilauri ya juisi na akamkemea. Katika siku chache nyingine zilizofuata wakati mwingine watoto walikuwa wanachukua vinywaji ndani ya kile chumba, lakini Rebeka akawa katika shughuli zake nyingi na akashindwa kuwasahihisha wale watoto. Siku moja kijana wake alimwaga Coca-Cola kwenye lile zulia. Rebeka alikasirika na kumpiga.
► Je, kuna shida gani kwenye njia ambayo Rebeka alikuwa anaitumia katika kuwasahihisha watoto wake?
Sheria ya Rebeka ilikuwa ni kwamba watoto walipaswa wasipeleke vyakula au vinywaji kwenye chumba kilichokuwa na zulia, lakini baadaye akawavumilia wakati wakiwa wanavunja sheria yake hadi wakati Ilipotokea ajali. Aliadhibu ajali badala ya uvunjaji wa sheria. Hali hii ni fundisho kwa watoto kwamba walikuwa na uwezo wa kuvunja sheria ali mradi wajizuie na kusababisha ajali au matukio mabaya. Wazo hili linakuza tabia mbaya kwa sababu ndio msingi mkuu wa uvunjaji wote wa sheria. Mtu anavunja sheria kwa sababu anafikiri kwamba anaweza kupata matokeo anayoyataka yeye wakati huo akijizuia na matokeo mabaya. Wazazi wanapaswa wasahihishe ukosefu wa utii kuliko kutoa adhabu kwa watoto kwa ajili ya kufanya ajali.
Michaeli aliwaambia watoto wake kufungia baiskeli zao ndani kila ifikapo jioni. Kila siku katika wiki, wakati Michaeli alipokuwa akirejea nyumbani, baiskeli zilikuwa bado ziko nje hazijafungiwa ndani. Kisha siku moja Michaeli akiwa kazini alipoteza chombo kimojawapo cha kufanyia kazi zake, na kwa bahati mbaya alikuwa amejiumiza kidole chake, na akawa na pancha ya tairi katika gari lake wakati akiwa anarejea nyumbani. Wakati alipofika nyumbani alikuta bado baiskeli hazijafungiwa ndani, na akachukua hatua ya kuwaadhibu vijana wake.
► Je, kuna shida gani kwenye njia ambayo Michaeli alikuwa anaitumia katika kuwasahihisha vijana wake?
Wazazi wengi wana tabia ya kuvumilia uvunjifu wa utiifu wakati wanapokuwa katika hali nzuri na kuadhibu uvunjifu wa utiifu wanapokuwa kwenye mazingira magumu ya kimaisha. Watoto hawajifunzi kutii isipokuwa pale wazazi watakapokuwa wakiwasahihisha mara kwa mara.
► Angalia vipengele vifuatavyo na elezea ni kwa nini kila kimoja ni muhimu. Je ni nini kinachotokea endapo mzazi hataweza kufuata maelekezo haya?
Mahitaji yanapaswa yaendanae na uwezo na ukomavu wa mtoto.
Adhibu tu jambo lililofanyika kwa kutotii, lakini siyo kwa jambo lililofanyika kwa bahati mbaya.
Sheria na mahitaji yanapaswa yawe wazi na yenye kueleweka.
Wakati mtoto anapokosa kuwa mtiifu, mzazi anapaswa kueleza ni nini ambacho mtoto alipaswa kufanya.
Kamwe usimwadhibu mtoto kwa kitu ambacho hakikuwa chini ya udhibiti wake.
[1]Ingawaje katika 2 Timotheo 2:24-25 na Wagalatia 6:1 ziliandikwa kwa ajili ya kushughulika na dhambi ndani ya kanisa, maelekezo kuhusu kudhihirisha uvumilivu na upole wakati wa kufanya masahihisho kwa wale ambao wamekosa zinahusika pia kwenye muktadha wa malezi ya wazazi kwa watoto.
Maelekezo ya Vitendo Kutoka kwa Watoto
Miaka kadhaa iliyopita, mwanasaikolojia wa Uingereza, Dr. R.F. Hertz, alifanya mradi wa utafiti. Aliwauliza watoto 100,000 waliokuwa na umri kati ya miaka 8na 14 kutoka katika nchi 24 ili kupata orodha ya sheria kwa ajili ya wazazi. Utafiti huu hauna mamlaka ya Neno la Mungu, lakini angalao unatuonyesha sisi baadhi ya mahitaji ambayo watoto wanahitaji.
Hapa kuna baadhi ya majibu ambayo ni ya kawaida sana:
Usigombane mbele ya watoto wako.
Usiseme uongo kwa mtoto.
Siku zote jibu maswali kutoka kwa watoto wako.
Watendee watoto wako kwa uwiano unaolingana.
Ni lazima kuwepo na [urafiki] kati ya wazazi na watoto.
Watendee marafiki wa watoto wako kama wageni waalikwa.
Usipende kuwalaumu na kuwagombeza na au kuwaadhibu watoto wako mbele ya marafiki zao.
Jikite katika vipengele vizuri kutoka kwa watoto wako na usitake kuweka mkazo sana kwenye mambo aliyoshindwa.
Kuwa thabiti na imara katika hali yako ya upendo na hisia zako.
Mzazi mmoja anapomchambua mwenzake kila mara mbele ya watoto, watoto wanaweza kujidhania kwamba hata wao wanapaswa kutokukubaliana na kuona makosa ya mzazi asiyeheshimiwa.[1] Wazazi wanapaswa kujadili kutokukubaliana kwao kwa baadhi ya mambo wakiwa peke yao faraghani na kutengeneza sera ambazo wataweza kuzifuata kwa ushirikiano.
Wazazi hawapaswi kusema uongo kwa mtoto wao (Wakolosai 3:9), hata kumpa sababu za kushirikiana au kumwondolea wasiwasi. Mtoto anapotambua kwamba mzazi wake anamdanganya, hajisikii salama tena. Baadhi ya wazazi hawana uwezo wa kuwafariji au kuwaelekeza watoto wao wanapokuwa na mashaka kwa sababu unakuta watoto hawaamini yale yanayosemwa na wazazi wao.
► Chagua mojawapo ya vipengele vilivyoorodheshwa hapo juu kisha elezea matatizo yanayojitokeza endapo mzazi hatafuata mwelekeo huo.
[1]Maelekezo na kanuni kutoka katika Waefeso 4:29-32, Waefeso 5:33; 1 Petro 3:7-12 zote zinatumika hapa.
Nyumbani kwa Mkristo
► Anapokuja mgeni nyumbani kwako, je, anaona kwa mara moja kwamba ni nyumba ambayo Wakristo wanaishi? Kwa namna gani?
► Mwanafunzi anapaswa asome Kumbukumbu la Torati 6:6-9 kwa ajili ya kikundi.
Waisraeli walipaswa kuzingatia kuchagiza maisha yajayo kwa kuunda tabia ya watoto. Wangefanyeje? Walipaswa kuwa na mazingira yaliyolindwa kwa ajili ya mafunzo ya watoto wao kwa mujibu wa kanuni za kibiblia. Walikuwa wabandike Maandiko kila mahali (wayaandike juu ya miimo ya milango ya nyumba zao na juu ya malango yao.”) Siyo tu kwamba Maandiko yanapaswa yabandikwe kuhalisi nyumbani, lakini muhimu zaidi, kila kitu nyumbani kilipaswa kuendana na Maandiko.
Familia hizi hazikupaswa kuweka Amri Kumi za Mungu kwenye ukuta mmoja na picha nyingine ya mtenda dhambi kwenye ukuta mwingine. Hali hiyo ingekuwa inachanganya sana ufahamu wa watoto kuhusiana na maadili.
Watoto huathiriwa sana na mambo wanayoyaona na kuyasikia kila siku. Kama kituo cha redio kinaweza kusikika kikipiga muziki nyumbani kwao kila siku, wao watachukua baadhi ya falsafa ambazo msingi wake ni ule muziki.
Haiwezekani kwa wazazi kuwakingia watoto na kila falsafa mbovu au ushawishi wa kidunia, lakini wazazi wa Kikristo ni lazima wawafundishe watoto wao kufanya tathmini ya kila kitu wanachosikia na kuona ambacho kinakuja kwao kupitia Neno la Mungu. Yesu aliomba kwamba, “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu… Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli (Yohana 17:15, 17).
Watoto hugundua ni nani wazazi wao wanamvutia kama shujaa wao. Wanajua ni nani wazazi wao wanamheshimu. Ni jambo lisilokubalika kwa mzazi kuwafundisha watoto wake kuhusu ukweli wakati yeye mwenyewe anashikamana na kupendezwa na watu wa kidunia wasiokuwa na maadili. Mzazi anayefanya hivyo ni kama kumjulisha mtoto wake kwamba angefurahi zaidi awe mwanamuziki wa kidunia mwenye mafanikio kuliko kuwa Mkristo mwaminifu.
Baadhi ya wazazi hufikiri ni jambo lililo sawa kuruhusu mtoto wao ajiingize kwenye mambo ya dhambi kama watakuwa wamemweleza huyo mtoto kwamba ni kwa nini hayo mambo ni mabaya. Hebu fikiria kuhusu hili: Kama ulikuwa unajaribu kumfanya mtoto wako ale chakula kilicho kizuri, hutapenda kuweka lundo la peremende na keki mbele yake, na kisha ujaribu kumweleza ni kwa nini anapaswa ale mboga za majani. Maelezo yote kuhusiana na vitamini hayataweza kushinda matamanio yake ya asili ambayo yanachochea ale peremende zilizoko mbele ya macho yake.
Baadhi ya wazazi huruhusu televisheni zao kuwa wazi muda wote bila hata ya kuonyesha kuwa wasiwasi na kuhusika na kile ambacho watoto wao wanaangalia. Wakristo wanapaswa wakumbuke kwamba jamii inafundisha kwamba dhambi ni jambo la kawaida lisilokuwa na shida mradi tu matokeo yake yadhibitiwe. Televisheni huonyesha watu wanaoishi kwa dhambi na hawajapatwa na matukio yeyote, lakini hayo siyo maelezo ya kweli ya maisha halisi. Televisheni humfanya mtoto aone kwamba wazazi wake wanamzuia yeye kutofurahia maisha, na atangojea muda ambao anaweza kufanya vile anavyotaka yeye mwenyewe.
Wakristo wengi wanaishi kwenye nyumba zao pamoja na ndugu ambao siyo Wakristo. Kwenye hali kama hizo, nyumba siyo mazingira ambayo yamelindwa dhidi ya kuvutia mambo mabaya. Ni muhimu kwa mzazi Mkristo kuweka mfano wa upendo, uaminifu, usafi, na furaha, huku akiomba kwamba Roho Mtakatifu amsaidie mtoto katika kuweza kuchagua mwelekeo sahihi wa maisha.
Familia zisizo kamilifu
Kwa kuwa familia hazijakamilika, mahusiano mara nyingi huwa yanakuwa na historia ya makosa mengi yaliyopita na migogoro ambayo haijatatulika.
Hata wazazi wa Kikristo hawajakamilika. Huenda zisiwe thabiti kila wakati katika kutengeneza na kutekeleza sheria zake. Hawaelewi kila wakati kuhusu hali ya kijana wao – mambo yamebadilika kwenye kizazi kipya. Kila wakati hawawezi kuwa na huruma ya kutosha kwa ajili ya maswala halisi yanayohusiana na mtoto wao. Siyo mara zote huwa na msimamo ulio bora na wanaweza wakasema maneno yenye kuumiza.
Mungu aliumba watu wa kwanza na kuunda familia. Alimfanya mwanamume, akamfanyia na mke, na akawapa watoto wa kuwalea. Mungu anajua kila kitu. Mungu alijua kwamba wazazi watangefanya makosa lakini bado aliunda uzazi. Aliona kuwa hiyo ndiyo ilikuwa njia bora zaidi, pamoja na kasoro zote ambazo wanadamu wanazo. Hii inamaanisha kwamba ni lazima kuwepo na njia ambayo itaifanya familia ifanikiwe. Kuna faida nyingi za mfumo wa familia hata wakati ambapo inaonekana siyo kamilifu.
Ukweli kwamba Mungu alianzisha kuwepo na uzazi ni muhimu kwa ajili ya watoto. Hali hii inamaanisha kwamba wakati watoto wanapoasi wanakuwa wameamua kutokukubaliana na mfumo ambao Mungu ameuweka. Mungu alisema, "Enyi watoto, watiini wazazi wenu …” (Waefeso 6:1). Wazazi huwa waasi dhidi ya mfumo wa Mungu aliouweka wakati wanapopuuzia kutimiza majukumu ambayo Mungu ameyaweka juu yao. Kuukata mpango wa Mungu ni kuasi dhidi ya Mungu.
Jukumu katika Kumlea Mtoto
Katika hali hii ya kuwa mzazi, kuna maeneo matatu (3) ya kuwajibika: Mtoto analo eneo lake la kuwajibika. Mzazi analo eneo lake la kuwajibika. Mungu analo eneo lake la kuwajibika.
Tayari tumeshaangalia kwa kina eneo la uwajibikaji la mzazi katika haya masomo mawili yaliyotangulia. Kwa sasa tutazingatia uhusika wa Mungu kwenye maisha ya watoto na majukumu ya watoto.
Kazi ya Mungu kwenye Maisha ya Watoto
1. Mungu anataka watoto wawe na uhusiano wa kibinafsi na yeye kupitia imani iliyo katika Yesu Kristo. (Soma Mathayo 18:1-6 na Mathayo 19:13-15.)
2. Mungu ni mwaminifu kuwavuta watoto wetu kwenye uhusiano huu pamoja naye. (Soma Yohana 6:44.)
3. Mungu huzungumza na watoto wetu kupitia Neno lake. (Soma 2 Timotheo 3:14-15.)
Watoto katika Mahusiano na Mungu
1. Watoto wanaweza wakasamehewa dhambi zao. (1 Yohana 2:12).
2. Watoto wanaweza wakamjua Mungu (1 Yohana 2:13).
3. Watoto wanaweza wakakua kwenye mahusiano na Mungu (1 Samweli 2:26).
4. Watoto wanaweza kumwabudu Mungu (Mathayo 21:15-16).
5. Watoto na Vijana wanaweza wakatumiwa na Mungu (Yoeli 2:28).
Katika Maandiko kuna mifano mingi ya watoto na vijana wanaotumiwa na Mungu katika kufanikisha makusudi yake: Samweli, Mtumishi wa kike wa mke wa Naamani, kijana aliyetumiwa na Yesu kulisha makutano, Daniel, Yusufu, Daudi, na Mariamu, kwa kutaja tu wachache.
Jukumu la Mtoto
Jukumu la mtoto, kwa mujibu wa Neno la Mungu, ni kuwatii wazazi wake (Waefeso 6:1-3). Je, itakuwaje kama wakati mwingine mzazi anafanya makosa? Mtoto ni lazima atimize jukumu lake na siyo kuliweka jukumu lake katika masharti ya jinsi mzazi anavyofanya. Hilo siyo jukumu la mtoto. Jukumu lake ni kutii.
Kama mtoto ataamua tu kutii wakati anapofikiri kwamba mzazi yuko sahihi, mzazi hataweza kuwa na mamlaka. Hilo haliwezi likawa lile ambalo Mungu alikusudia, kwa sababu hilo litaharibu kabisa mfumo mzima wa malezi.
Siyo jukumu la mtoto kuwajibika na jinsi ambavyo mzazi anatumia mamlaka yake. Eneo lake la uwajibikaji ni kwenye kutii. Je, itakuwaje kama mzazi atamwambia mtoto kwamba afanye jambo lisilofaa, kama vile akamletee kinywaji cha bia kwenye jokofu? Mtoto hapaswi kuwa na jukumu la kuamua kama mzazi yuko sahihi au laa. Anaweza kutoa maoni yake kuhusiana na jambo hili kwa hekima na au heshima lakini ni lazima akubali kutii.
Mambo kinzani kwenye jukumu la kutii ambayo yanaweza kuleta madhara kwenye unyanyasaji wa kimwili au matendo ya uovu yanapaswa kutolewa taarifa kwa mamlaka ambazo zina majukumu ya kuwalinda watoto. Matatizo ambayo watoto huwa nayo kwa wazazi wao kwa kawaida siyo kwa sababu wanauliza kama maagizo hayo yanaenda sawasawa na kanuni za Kikristo. Mtoto aliye muasi kwa kawaida hukinzana na wazazi wake katika mambo ya kawaida, kama vile kufanya usafi wa chumba chake, kufanya kazi za nyumbani, kuwepo nyumbani kwa nyakati fulani, na vizuizi kwenye mambo mengine ya burudani zake.
Mtoto anayeasi hupingana na dhana ya mamlaka ya mzazi kwa kudai haki ya kuamua wakati akitaka kuona kwamba amri za mzazi wake ni mbaya. Upinzani wake unatokana na matamanio ya msingi ya kupewa uhuru. kujitawala, kuwa na mamlaka binafsi, na uwezo wa kujiamulia atakavyo. Je, ni katika umri gani mtu anapatiwa mambo hayo? Kamwe hapana, na sivyo.
Dhana ya uhuru wa aina hii ni kama njozi. Daima utakuwa na majukumu yanayotokana na kuwafikiria watu wengine, Wakati wote kutakuwepo na kazi ambazo unajua binafsi kwamba unapaswa uzifanye, hata kama mama yako hayuko pale kukuambia uzifanye. Mtu anayesisitiza kuishi bila ya kuwajibika kwa watu wengine huwa anaacha mabaki ya maumivu na uharibifu, akiumiza mtu yeyote anayemwamini na anayemtegemea yeye.
Wakati mwingine watoto huchukizwa na mahangaiko ya wazazi wao, wakihisi kwamba wazazi wanapaswa wawaamini wao zaidi. Ikiwa mtoto anaweza kujaribu kuelewa na kuheshimu mahangaiko ya wazazi, mzazi anaweza kumwamini mtoto huyo zaidi na kuwa kurekebisha vizuizi vyake. Wakati mtoto anapokataa kuona mahangaiko ya mzazi wake, wazazi hujihisi kwamba kuna hitaji la kumwekea vizuizi zaidi.
Kukiri Makosa
Watu wengi wanaogopa kukiri kosa wawapo kwenye uhusiano kwa sababu Wanahofia kwamba ukiri huo unaweza kuwadhoofisha kwenye migogoro mingine ya baadaye. Kiuhalisia, nafasi ya kuwa mwaminifu na utayari wa kufanya jambo ambalo ni la haki ni nafasi kubwa ya kutaka mtu awepo. Njia pekee ya kuwepo kwenye nafasi hiyo na kukaa ndani yake ni kukiri makosa yako uliyoyafanya na kuanza kutenda yaliyo mema, na pia kuwa tayari kusahihishwa wakati wowote unapokuwa na makosa.
Wakati mwingine mtu aliyeko kwenye mamlaka huwataka watu walioko chini yake kukiri makosa yao lakini yeye hayuko tayari kukiri makosa yake mwenyewe kwa sababu anafikiri kufanya hivyo kutamshushia hadhi ya mamlaka yake. Hilo ni kosa. Kama mtu aliyeko kwenye mamlaka hawezi kukiri makosa yake, walioko chini yake hawawezi wakamwamini yeye. Kanuni hii inatumika kwenye nafasi ya aina yeyote ya mamlaka, ikiwa ni pamoja na wazazi.
Wazazi, kama mko kwenye mgogoro na mtoto wenu, huenda ikawa labda umefanya makosa ambayo inabidi yatambuliwe. Mtoto ataweza kuwa anajihalalishia makosa yake kwa kutumia makosa yako. Omba msamaha kwa maneno yako makali, majibu ya haraka haraka, na kushindwa kuitambua hali. Pengine kunaweza kusiwepo na maendeleo ya kumaliza mgogoro, hadi pale utakapokuwa umeweza kuomba msamaha, “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Yakobo 4:6b).
Aidha wewe ni mzazi au ni mtoto, unahitaji kukiri makosa yako. Kutubu, kuomba msamaha, na kujitiisha mara kwa mara kwa mamlaka iliyotoka kwa Mungu kwa kawaida itakupa ushirikiano ulio bora kutoka kwa watu wengine, lakini hiyo siyo sababu inayokupasa ufanye hivyo. Unapaswa ufanye hivyo ili kumpendeza Mungu.
Wakati unapokuwa umekiri makosa yako uliyotenda, huhitajiki tena kutaka kuhakikisha kwamba mtu mwingine anayehusika na yeye analaumika kwa makosa yake. Usiyatumie makosa ya mtu mwingine ili kupata radhi kwa matendo yako mabaya uliyoyafanya.
Uhusiano unaweza ukaimarika mara moja, au unaweza ukachukua muda. Wakati mwingine watu watalazimika waone mabadiliko yako kama ni halisi kabla na wao hawajaanza pia kubadilika. Lakini sababu ya kukutaka wewe kutenda lililo la haki siyo kwa ajili ya kumfanya mtu mwingine abadilike. Unapaswa tu ufanye kile ambacho Mungu anakutaka ukifanye. Inawezekana huyo mtu mwingine asibadilike, lakini utakuwa na dhamira iliyo safi na baraka za Mungu kwa sababu umetimiza jukumu lako. Mwamini Mungu katika kutimiza jukumu lake.
Umuhimu wa Kila Eneo la Maisha kuwekwa chini ya Mamlaka ya Mungu.
Jaribu kufikiria kisiwa kimoja kinachoitwa Zhivia. Kisiwa kingine kilicho karibu kiitwacho Grekia kinataka kukishinda Zhivia. Mtawala wa Grekia anaahidi serikali ya kisiwa cha Zhivia kwamba nchi zao mbili zinaweza kuwa na amani kama atakuwa tayari kumpatia ekari kumi (10) tu katikati ya kisiwa chao. Je, hilo litakuwa ni suluhisho zuri la kuleta amani? Ikiwa Zhivia atampa adui eneo katikati ya nchi yake, adui anaweza akajipanua katika eneo hilo kwa ajili ya kutaka kutawala eneo lingine zaidi.
Jaribu kufikiria kwamba maisha yako ni kama nchi yenye mikoa/majimbo mbalimbali. Mkoa/Jimbo moja linaweza likawa ni ajira au shule. Mkoa/Jimbo lingine linaweza kuwa ni burudani. Eneo lingine ni uhusiano wako na wanafamilia. Kuna maeneo mengine mengi.
Nchi yote, ikiwa na mikoa/majimbo yote inapaswa iwe chini ya mamlaka ya Mungu. Unadhani ni nini kitatokea kama mkoa/jimbo moja la uhusiano wako na familia, likawa haliko chini ya mamlaka ya Mungu? Umemruhusu Shetani aingie na kukaa kwenye mkoa/jimbo hilo. Kutoka kwenye mkoa/jimbo hilo ataanza kuvamia mikoa/majimbo mengine ya maisha yako ili yawe chini ya mamlaka yake. Vivyo hivyo, kama mtu siyo msafi katika mambo yake ya burudani, maeneo mengine ya mikoa /majimbo ya maisha yake yataweza kuvamiwa na Shetani. Mkristo anapaswa aweke kila mkoa/jimbo la maisha yake chini ya mamlaka ya Mungu.
Vipengele kadhaa kwa Wazazi
► Wanafunzi wanapaswa wasome Waefeso 6:4, Wakolosai 3:21, 1 Wakorintho 13:11, na Wakolosai 3:8 kwa ajili ya kikundi.
Kama mtoto wako anaonyesha hisia kali, ya kuonyesha hasira au kuchanganyikiwa, anaweza kuhisi kwamba humwelewi. Huenda pia anahisi kwamba humjali vya kutosha katika kumsikiliza na kujaribu kumwelewa.
Jaribu kumsikiliza na kumwelewa. ikiwa mara kwa mara unapuuzia matatizo yake kama yasiyokuwa na maana au ni ya kijinga, hujamwelewa anakabiliana na nini hasa. Ikiwa inaonekana kama ni tatizo kubwa kwake, basi ni changamoto kwa imani na tabia yake. ikiwa huwezi kuelewa ni kwa nini anaonyesha hisia nzito kiasi hicho, basi huwezi kuelewa umuhimu uliojizingira katika hali yake iliyopo.
Kamwe usimkatie tamaa mtoto wako, na usitoe matamko yanayoonyesha kana kwamba sasa umefikia mwisho au huwezi tena.
Usifikiri kwamba watoto wako wote wanafanana.
► Mwanafunzi anapaswa asome Waefeso 4:30-32 kwa ajili ya kikundi.
Matatizo yanapojitokeza, usifanye marejeo ya historia ya mambo yaliyokuwa yameshindikana. Mtoto anataka kufikiria kushindwa kwake kwa zamani kama mambo yasiyo na umuhimu kwa hali ya sasa. Anafikiria kwamba kwa sasa amebadilika na itakuwa siyo kumtendea haki wewe kuendelea kumkumbusha kuhusu kushindwa kwake huko nyuma. Hata hivyo, usimtarajie kwamba atakuwa mkarimu sana kwako.
Kwa ajili ya majadiliano ya Kikundi
► Je, kuna maudhui gani kutoka katika somo hili ambayo ni mapya kwako? Je, ungependa kushirikisha baadhi ya mambo ambayo umepanga kuyabadilisha katika utendaji wako?
► Jadili njia nyingine za zaidi ambazo familia za kanisa zinaweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuendeleza maisha sehemu za nyumbani na kusaidia watoto wa kanisani.
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Tunataka nyumba zetu ziwe maeneo a upendo, usalama, na baraka. Tusaidie kuwa watakatifu na wenye upendo katika yale yote tunayoyatenda kwenye nyumba zetu.
Tusaidie tuweze kuwa na utaratibu unaowiana kwenye mafundisho na tabia ya Kikristo. Wape watoto wetu shauku ya kukufuata wewe.
Asante Bwana kwa kuwa mwaminifu kwa kila mmoja wa watoto wetu. Tunajua kwamba Roho Mtakatifu wako anafanya kazi ndani ya mioyo yetu.
Ameni.
Kazi za Kufanya
(1) Kusanya orodha ya maelekezo saba ya kibiblia kwa ajili ya familia. Kisha orodhesha matumizi maalumu kwa ajili ya hali halisi ya maisha. Andika maelezo yanayoelezea kila kipengele cha matumizi (jumla ibara saba).
(2) Chagua mojawapo ya mada zilizoorodheshwa hapa chini. Pitia kitabu cha Mithali na orodhesha Mithali zinazoelezea kuhusu mada hizo. Andika aya mbili zenye kuonyesha muhtasari wa kile ambacho Mithali anasema kuhusiana na mada. Kisha andika aya tatu kuhusu jinsi ambavyo mzazi anaweza kumfundisha mtoto au kijana wake kanuni zilizoainishwa. Mada ni kama zifuatazo:
Kusema ukweli
Mambo ya fedha
Tofauti iliyopo kati ya thamani ya hekima na thamani ya fedha
Uaminifu
Usafi wa kujamiiana
Unyenyekevu
Kupokea maelekezo na masahihisho
Kuwa na bidii/kuchukua hatua kwa kutumia akili yako mwenyewe
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.