Marko na Mariamu waliishi katika nchi ya India. Walikuwa wameoana kwa miaka kadhaa bila kupata watoto na ghafla fursa ikawatokea. Mmoja wa ndugu wa ukoo wa Mariamu alikuwa amejifungua mapacha wawili wa kike na alihisi hawezi kuwatunza. Marko na Mariamu kwa pamoja walikubali kupokea zawadi ya watoto hao wawili kwa furaha kubwa, lakini walikabilikabiliwa na changamoto nyingi. Watoto hao walikuwa wamezaliwa njiti wakiwa na uzito wa takriban pauni tatu kila mmoja. Wazazi wapya walipata usaidizi mdogo au ushauri kutoka kwa marafiki walipokuwa wakijaribu kuwalisha na kuwatunza hawa mapacha wa kike. Walikesha mara nyingi bila ya kupata usingizi wa kutosha kwa ajili ya hawa watoto, lakini wasichana hawa waliishi na wakakua kwa jinsi ya ajabu na wenye afya njema.
Mtoto
Kukua kwa mtoto wakati wa Mimba
► Mwanafunzi anapaswa asome Zaburi 139:13-18 kwa ajili ya kikundi.
Kifungu hiki kinatupa taarifa kwamba Mungu alitujua mwanzoni tangu tulipotungwa mimba kwenye matumbo ya mama zetu, hata kabla miili yetu haijaumbwa (Aya ya 16). Mungu alikujua wewe na alikuwa na mpango kwa ajili yako kabla hata hajazaliwa.
Wakati manii kutoka kwa mwanamume zinapogusana na yai la mwanamke lililoko ndani yake, mtoto anatungwa – maisha mapya ya binadamu – kiumbe kipya – vinaanza kuwepo. Taarifa zote za kinasaba kwa ajili ya mtu huyo zinakuwepo ndani ya hiyo seli moja. Masaa 24 tu baada ya mimba kutungwa, seli hiyo hugawanyika na kuwa seli mbili. Kila mojawapo ya hizo seli mbili hugawanyika tena katika seli nyingine mbili. Katika kipindi cha wiki moja, mtoto sasa anakuwa kwenye seli nyingi ambazo hushikiliwa kwenye tumbo la uzazi la mama ambako hukua na kuongezeka. Kila seli inakuwa na “mfumo wa siri wa kanuni na taratibu” kwa ajili ya kumfanya mtu huyo (DNA). Seli hizo hufuata maelekezo ya “mfumo wa siri wa kanuni na taratibu” (DNA) na hufanya kazi mahususi ya kutengeneza kila sehemu ya mwili.
Kwenye wiki ya 3 ya umri wa mimba, uti wa mgongo wa mtoto na ubongo huanza kujitengeneza. Kwenye wiki ya 4 ya umri wa mimba, macho ya mtoto huanza kutengenezwa, moyo huanza kazi na mikono ya mtoto huanza kutengenezwa. Kwenye wiki ya 12 ya umri wa mimba, mwili wa mtoto una kila kiungo muhimu kinachohitajika.
Kufikia wiki ya 14 baada ya mimba kutungwa, alama za kipekee za vidole vya mikono ya mtoto huwa zimekamilika kabisa. Kufikia wiki ya 16-24 za ujauzito, mama anaweza kuhisi mtoto wake akicheza tumboni mwake. Kwenye wiki ya 26-28 mapafu ya mtoto huwa yamekua kiasi cha kutosha kuanza kupumua, na mtoto atakuwa na uzito wa paundi mbili. Kwa kawaida watoto huzaliwa kati ya wiki ya 38-40 tangu siku ya kupata ujauzito. Kila mtoto mchanga ni kiumbe cha ajabu, cha pekee kilichofanywa na Mungu Muumba wetu.
► Mwanafunzi anapaswa asome Mhubiri11:5 kwa ajili ya kikundi.
Ni ukweli kabisa kwamba ni muujiza jinsi Mungu anavyoumba, anavyotengeneza na anavyokuza mtoto kwenye tumbo la uzazi la mama yake. Watu kamwe hawawezi kufahamu mchakato wote au mambo yote yanavyofanyika. Lakini bado, kupitia mabara yote ya dunia, jamii na tamaduni zote, maendeleo ya wanadamu hufuata mlolongo na mpangilio ulio sawa usiobadilika. Ubunifu wa Muumbaji ni wa uhakika ulio mkamilifu!
► Mwanafunzi anapaswa asome Ayubu 10:8-12 kwa ajili ya kikundi.
Katika hizi aya za Ayubu anatumia mlinganisho unaorejea mimba na ukuaji wa mtoto akiwa tumboni mwa mama yake. Ayubu anatuambia kwamba Mungu Muumbaji ndiye anayetoa au mpaji wa uhai.
Thamani ya Kuumbwa katika Sura ya Mungu
Mwanzo 1:26-27 na Mwanzo 9:6 tunaambiwa kwamba tumeumbwa kwa sura ya Mungu. Maisha yote ya mwanadamu ni ya heshima sana. Kwa sababu hiyo, ni dhambi kumwua mwanadamu yeyote (Mwanzo 9:5, Kutoka 20:13).
Katika Ezekieli 16:20-21, 36, 38 Mungu anazungumzia vikali dhidi ya wale wote watakaomwondolea mtoto uhai wake. Anawaonya wana wa Israeli kuhusu utoaji wa dhabihu za watoto wadogo kwa madhabahu za kishetani na anatangaza kwamba adhabu yao ni kubwa sana.
Katika Isaya 46:3-4, Mungu anazungumzia kuhusu uangalizi wake kwa ubinadamu katika hatua zote kukua kwa mwanadamu anapotoa kauli hii nzito:
Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani; na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.
Hii ni ahadi bora sana!
Watu wote ni wa thamani, ikiwa ni pamoja na watoto ambao bado hawajazaliwa, walemavu, wenye mahitaji maalumu, na wazee. Thamani ya mtu haitegemei kile kitu anachoweza kukifanya, au ikiwa kama angeweza kuishi ikiwa angekuwa pake yake. Kila mtu ana thamani kwa sababu watu wote wameumbwa kwa sura ya Mungu.
Biblia inatuambia kwamba kila mtoto ni wa thamani mbele za Mungu tangu wakati ule wa kutungwa kwa mimba yake (Zaburi 139:13-18). Kwa sababu hiyo, tunajua kwamba sisi ni wanadamu tangu siku ile ya kutungwa mimba. Kutoa mimba kwa kukusudia ni kumuua mwanadamu.
Kuna angalao njia nne tu ambazo wafuasi wa Kristo wanapaswa kufanyia kazi ili kulinda maisha ya watoto ambao hawajazaliwa pamoja na kuwahudumia akina mama:
1. Wanapaswa kushawishi serikali zao na taratibu za mahakama za mataifa yao kutengeneza sheria na kupitisha hukumu kali ka ajili ya kuwalinda watoto ambao hawajazaliwa kutokana na kuuawa.
2. Wanapaswa kutoa msaada wa vitendo kwa wanawake ambao wanajisikia kwamba uchaguzi wao wa mwisho ni kutoa mimba, ili waweze kujisikia kwamba wana uwezo wa kuyalinda maisha ya watoto wao.
3. Wanapaswa wawatunze watoto wanaotupwa au kuachwa.
4. Wanapaswa kutoa neema na usaidizi wa kiroho kwa wanawake ambao wametoka katika hatia ya kutupa mimba zilizopita.
Utunzaji wa Mtoto ambaye Hajazaliwa
Ni jambo muhimu kutambua kwamba mtoto anayekuwa amebebwa na mama katika tumbo lake la uzazi ana hatima yake ya milele. Mtu huyo atakuwepo milele. Kwa sababu hiyo, wazazi wanapaswa kuwajali na kuwatunza watoto wao katika vipengele vyote vya maisha yao: kimwili, kiakili, kijamii/kimhemuko, na kiroho!
► Mwanafunzi anapaswa asome Mathayo 18:2, 10 kwa ajili ya kikundi.
Tabia ya mwanaume inaweza kuathiri afya ya mtoto wake ambaye bado hajazaliwa na pia inaweza kumzuia ashindwe kuwa baba tangu mwanzoni. Ulevi wa pombe, madawa ya kulevya, au uvutaji wa sigara vyote vina uwezo wa kuharibu manii ya kiume na hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa utasa (kushindikana kupatikana kwa mimba) au mimba kutoka (mtoto kufa wakati wa mimba).
Mama mwenye mimba kutumia vitu ambavyo vina madhara, kama vile madawa (yaliyopigwa marufuku), ulevi wa pombe, au uvutaji wa sigara vina uwezo wa kuharibu kabisa na kusababisha madhara kwa mtoto. Vitu hivyo vinazuia kukua kwa mtoto na kusababisha azaliwe akiwa na matatizo ya kimwili au kiakili.[1]
Mojawapo ya nyakati ngumu wakati wa ukuaji wa mtoto kabla ya kuzaliwa ni wakati ambapo viungo vyake na tishu zake ndiyo kwanza vinaanza kukua, hasa kati ya wiki ya 3-4 ya umri wa mimba. Katika wakati huu, wanawake wengi huwa hawajijui kama wameshabeba mimba!
► Mwanafunzi anapaswa asome 1 Wakorintho 10:31 kwa ajili ya kikundi.
Ingawa mama hawezi kudhibiti afya ya mtoto wake ambaye hajazaliwa, anaweza akamsaidia mtoto kwa kadri inavyowezekana, kwa kuhakikisha kwamba anapata lishe bora na kuepukana na vitu vyenye madhara. Mungu anasema watoto ni wa thamani kubwa, na tunamtukuza Mungu wakati tunapowatendea kwa jinsi hiyo waliyo nayo.
Ni jambo liletalo huzuni sana wakati mtoto aliye tumboni haishi hadi kufikia wakati wake wa kuzaliwa. Kwa kawaida kifo cha kitoto kichanga tumboni ambacho hakijazaliwa siyo matokeo ya jambo lolote ambalo mama amelifanya. Kunakuwepo na hisia kubwa sana kwa wazazi ya kupoteza mtoto, kwahiyo, waumini wengine wanapaswa wajaribu kuwafariji katika kipindi hicho.
Kuzaliwa
Wakati kukiwa na tofauti nyingi za kitamaduni zinazozingatia uzoefu wa kuzaa, mambo mengi yanafanana takribani kila mahali ulimwenguni kote. Katika Mwanzo 3:16, Mungu alisema, “Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto….”
Karne nyingi zimepita, na maneno ya Mungu bado yameendelea kubakia kuwa ya kweli ulimwenguni kote. Matokeo ya dhambi ya kwanza ya Adamu na Hawa bado yameendelea kugusa mchakato mzima wa uzazi hadi sasa. Hata Mariamu, mama yake na Yesu, hakuachwa katika mchakato huu, kwani alipitia pia katika maumivu ya kuzaa (Luka 2:6-7).
[1]Greg Cook & Joan Cook, The World of Children, 3rd ed. (Pearson Education, 2013), 85.
Hali ya Mwanzo ya Utotoni
Kukua Kimwili
Mtoto hukuza uwezo wa kimwili katika hatua zinazotabirika. Mtoto kwanza atainua kichwa chake, kisha kukaa, kisha kutambaa, kisha kutembea. Wakati mojawapo ya haya hayafanyiki ndani ya muda uliotarajiwa, wazazi huanza kuwa na wasiwasi. Jinsi watoto wanavyoendelea kukua, tunawategemea wawe na uwezo wa kurukaruka, kupanda na kukimbia wanapokuwa kwenye umri wa miaka 4-5 tangu kuzaliwa. Wanaendelea kutoka kwenye kunywa maziwa pekee hadi kula vyakula vigumu. Wanafamilia hufurahia, na hushanglia kwa kuendelea kutia moyo katika hatua hizi za maendeleo ya kawaida ya kimwili ya mtoto wao.
Kukua Kiakili
Walezi husikilizia kilio cha kwanza cha mtoto mchanga na kutarajia mtoto kutoa sauti za furaha akiwa kwenye takribani miezi miwili ya umri wake tangu kuzaliwa. Baadaye, mtoto huanza kunguruma na kurudiarudia sauti mbalimbali. Wazazi hufurahishwa sana wanaposikia mtoto akisema “Mama” au “Baba” anapokaribia kuwa na umri wa miezi sita (6) ya kuzaliwa kwake. Kwa kawaida watoto huanza kutamka maneno wakati wakiwa na umri wa mwaka mmoja (1), na huanza kutengeneza sentensi zilizokamilika na kueleweka wakiwa katika umri wa miaka miwili (2).
Watoto wadogo hutushangaza kwa mambo wanayokumbuka. Wanauliza maswali mengi sana. Siku zote watakumbuka kama ulishawaahidi kufanya jambo la kipekee au maalumu pamoja nao. Ukuaji wao wa kiakili hutokea kwa sababu ya mpango wa Mungu aliouweka, lakini malezi ya wazazi na walezi wengine huleta tofauti kubwa katika kuwasaidia kukua hadi kufikia kwenye uwezo wao kamili.
Kukua Kijamii na Kimhemuko
Watoto wanahitaji wazazi wao kuwasaidia kuwa na afya njema ili waweze kukua kimwili. Hata hivyo, wanahitaji kutiwa moyo kwa ajili ya maendeleo yao ya kijamii na kihisia hata zaidi. Wazazi, walimu, na walezi wengine wanapaswa kumsaidia kimakusudi kila mtoto kukua kijamii na kihisia.
Jinsi wazazi watakavyokuwa wanafanya mambo yaliyoko kwenye orodha, kadhalika watoto wao wanasaidiwa kustawi na kukomaa kijamii na kimhemuko.
► Soma hadi mwisho orodha hii. Kisha ipitie tena orodha hii kwa mara ya pili. Kando ya kila kitu ambacho wewe kama mzazi unajaribu kukifanya vizuri, andika mfano wa njia mahususi unayotumia kufanya hivyo. Weka alama pembeni mwa orodha ambayo kwa makusudi hujamudu kufanyia kazi. Kama wewe siyo mzazi, unaweza ukachagua vipengele kwenye hiyo orodha ambavyo unaweza kufanyia kazi kwa ajili ya watoto ambao ni wa jamii zako au ambao ni wa karibu na familia yako.
Njia ambazo unaweza Kuwasaidia watoto wako Wakomae[1]
(1) Kwa kujijali mwenyewe:
Dhibiti mifadhaiko yako ya binafsi.
Dhibiti rasilimali za familia yako.
Toa msaada kwa wazazi wenzako.
Omba na ukubali usaidizi kutoka kwa watu wengine inapohitajika.
Tambua uwezo wako wa binafsi na uwezo wako wa malezi.
Kuwa na makusudi yaliyo wazi katika kupanga malengo ya kulea watoto.
(2) Kwa kuwa mtu mwelewa:
Angalia na uwaelewe watoto wako na maendeleo yao.
Tambua jinsi watoto wanavyoathiri na wanavyoitikia kile kinachowatokea.
(3) Kwa kuweka mwongozo:
Fanyika mfano sahihi unaofaa, na tabia inayohitajika.
Weka na udumishe mipaka inayofaa.
Wape watoto fursa wajifunze jinsi ya kuwajibika. (Fursa zinatakiwa ziende sambamba na hatua ya maendeleo yao).
Fundisha ujuzi wa kutatua matatizo.
Weka umakini wako kwenye shughuli za watoto.
Kusimamia jinsi watoto wanavyowasiliana na uzoefu wao na watoto wengine pamoja na watu wazima.
(4) Kwa Kulea:
Onyesha mapenzi na huruma.
Kuza kujiheshimu na matumaini ya watoto.
Sikiliza na uhudumie hisia na mahitaji ya watoto
Fundisha kuhusu wema.
Toa mahitaji ya lishe, malazi, mavazi, afya na usalama kwa ajili ya watoto.
Furahia maisha pamoja na watoto.
Wasaidie watoto wajisikie kwamba wameunganishwa katika historia ya familia na urithi wa asili.
(5) Kwa Kuhamasisha:
Wafundishe watoto kuhusiana na wao wenyewe, watu wengine, na dunia inayowazunguka.
Chochea hamu ya kudadisi, mawazo, na utafutaji wa ujuzi.
Weka mazingira ya kujifunza yaliyo na manufaa.
Wasaidie watoto katika kuchakata na kudhibiti taarifa.
(6) Kwa Kutetea:
Tafuta, tumia, na anzisha rasilimali za jamii kwa ajili ya kuwafaidia watoto wako mwenyewe na jamii ya watoto.
Changamsha mabadiliko ya kijamii ili kutengeneza mazingira yatakayokuwa ni msaada kwa ajili ya watoto na familia.
Jenga mahusiano na familia, majirani na vikundi mbalimbali vilivyoko katika jamii.
Maendeleo ya Kiroho
Kwa sababu Mungu alituumba na maisha ya kiroho (Mwanzo 2:7), tunapaswa kuwafundisha watoto wetu kuhusu imani na kuwaongoza kuishi katika uhusiano na Mungu.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Zaburi 78:5-8 na Kumbukumbu la Torati 6:4-9 kwa ajili ya kikundi.
Je, unatumia njia gani katika kutii maagizo ya Mungu ya kufundisha watoto wako kwa bidii? Je, kuna maeneo gani ambayo unahitaji kuyaendeleza?
Ni lazima tuzingatie kwa kumaanisha maagizo ya Mungu kuhusu kufundisha familia zetu. Vinginevyo, tunashindwa kuishi katika kumtii Mungu, na watoto wetu pia watakuwa ni wa kukataa mamlaka ya Mungu.
Kuna aina mbalimbali za ufundishaji wa watoto, ikiwa ni pamoja na: Kusoma Biblia, Kuimba nyimbo zinazohusiana na Yesu, Kukariri maandiko, Maombi, Kufundisha kwa kutumia maswali na majibu,Kuwa na majadiliano ya kila siku. Kushiriki katika kanisa pia ni muhimu kwa ajili ya familia nzima.
Wakati mwingine mzazi anaweza kuwashikila watoto kwa muda wanapotaka kwenda kulala waimbe nyimbo zinazohusiana na imani na upendo wa Yesu kwa ajili yetu. Watoto hukuza imani iliyo na nguvu sana wanaposikia kuhusu upendo wa Mungu na uaminifu wake wakati wakiwa katika uangalizi wa upendo wa wazazi wao.
[1]Imenukuliwa kutoka kwa Charles A. Smith, et al., National Extension Parent Education Model. (Manhattan, Kansas: Kansas Cooperative Extension Service, 1994). Imepakuliwa kutoka https://www.k-state.edu/wwparent/nepem/nepem.pdf Julai 31, 2023.
Hitimisho
Unapokuwa mzazi, siku zako ni nyingi. Ni siku za kazi nyingi; ni siku zinazochosha; siyo siku zako mwenyewe. Hata hivyo, katikati ya kilio, maziwa yaliyomwagika, nepi chafu, na ratiba zisizokuwa na mwisho, chukua muda wa kusitisha kwa muda ili upate mtazamo mwingine. Kumbuka kwamba unamtunza mmoja wa watoto wa Mungu, ambaye yeye, katika mpango wake wa milele, alikuamini wewe na kukukabithi. Hajakutaka wewe uwe na nyumba nzuri, bajeti nzuri inayovutia, milo ya kifahari, au mavazi ya gharama kubwa kwa ajili ya watoto wake. Anachokitaka Mungu kutoka kwako ni hiki hapa:
Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. (Kumbukumbu la Torati 6:5-7).
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, ni vipengele gani vya malezi ya watoto mara nyingi hupuuzwa katika jamii yako?
► Je, familia zinakabiliwa na matatizo gani? Je, kwa nini siyo jambo rahisi wao kutoa uangalizi wa mtoto kama inavyoelezwa katika somo hili?
► Je, ni kwa jinsi gani waumini wanaweza kuwasaidia wamama waja wazito waweze kujitunza wenyewe pamoja na watoto wao ambao bado hawajazaliwa?
► Je, ni njia zipi ambazo familia za Kikristo zingeweza kufanya kazi pamoja kubariki maisha ya watoto wadogo na mama zao?
► Je ni kwa jinsi gani kanisa linaweza kuandaa huduma ambayo itakuwa inajali mahitaji ya watoto wadogo?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Tunakuabudu wewe, uliye Muumbaji wetu wa kustaajabisha. Ulituumba sisi ndani ya matumbo ya uzazi ya mama zetu na umekuwa ukitujali katika maisha yetu yote. Unajua kila kitu kuhusiana na sisi hata kabla hatujazaliwa.
Tusaidie kufanya yale tuyawezayo kulinda watu walio katika mazingira magumu, kutia ndani wale ambao bado wako matumboni mwa mama zao. Wabariki wale wanaohudumia akina mama wajawazito.
Asante kwa kutuamini sisi kwa kibali na wajibu wa kuweza kuwakuza watoto wetu. Unapokuwa unawaumba na kuwaendeleza watoto wetu, tusaidie tuweze kuwa waangalifu na makini kwenye utunzaji wetu kwa ajili yao na mafunzo yetu kwa ajili yao pia.
Tunataka kuwa watiifu kwako kwa jinsi tunavyowalea watoto wetu. Tusaidie kukuwakilisha vyema kwa watoto wetu. Utuwezeshe kuwafundisha watoto wetu kukupenda na kukutii.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Soma 2 Timotheo 1:3-5; 1 Wakorintho 4:17; Wafilipi 2:19-23. Andika ibara moja yenye kujibu maswali haya:
Je, wanawake wawili waliotajwa ni kina nani na walikuwa na majukumu gani katika familia zao?
Je, inavyoonekana walikuwa na ushawishi gani juu ya Timotheo?
Je, kulikuwa na matokeo gani ya ushawishi wao kwa ajili ya maisha ya kanisa la mwanzo?
(2) Fanya marejeo ya vifungu vya maandiko ambavyo umekariri wakati wa kozi hii: Kumbukumbu la Torati 6:4-9, Warumi 6:11-14, Wakolosai 3:5-7 , na mistari uliyochagua ili kukariri katika Somo la 5, Zoezi la 4. Je, aya hii inakuathiri vipi unapofanyia kazi?
(3) Kariri Zaburi 78:4-8. Mwanzoni mwa kipindi cha darasa linalofuata, andika au nukuu kifungu kutoka kwa kumbukumbu..
(4) Omba kipekee kabisa kwa ajili ya kila mtu katika familia yako kwa mahitaji yao ya binafsi. Jiombee pia na wewe mwenyewe. Je, Mungu anakuita wewe uwe katika familia ya aina gani?
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.