Hadi kufikia mwishoni mwa somo hili, mwanafunzi atapaswa:
(1) Atambue na athamini uhusiano ambao Mungu anataka awe nao Pamoja nasi.
(2) Aelewe na athamini sura ya Mungu kwa kila mtu.
(3) Atambue kwamba sisi tunawajibika kwa Mungu kwa ajili ya chaguzi mbalimbali tunazozifanya katika mahusiano yetu.
(4) Afahamu kwamba Biblia ndiyo mwongozo wetu kwa ajili ya mahusiano ya kimungu, na kwamba tunapaswa tumtafakari Mungu katika mahusiano yetu.
Mahusiano na Mungu
Kwenye Maandiko, tunajifunza kwamba Mungu ni Mungu aliye na nafsi, mwenye mahusiano na anayewasiliana na wengine (Waebrania 1:1-2). Maandiko yanatuonyesha kwamba Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu wamekuwa kwenye uhusiano kati yao kwa umilele wote.[1]
Mungu aliziumba mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo. (Kutoka 20:11). Zaburi 8:3-8 inatuonyesha kwamba ubinadamu ulikuwa ndio uumbaji uliokuwa bora na muhimu Zaidi. Mungu aliumba watu kama viumbe vya uhusiano, kama yeye alivyo ni kiumbe wa uhusiano.
Katika Maandiko yote, Mungu huwaalika watu kwenye mahusiano ya maisha ya uzima pamoja na yeye mwenyewe.[2]
Ni ajabu gani kutambua kwamba Mungu, aliye Muumbaji wa ulimwengu, anatamani awe na uhusiano na wewe pamoja na mimi!
► Mwanafunzi anapaswa asome Mwanzo 3:8-9 kwa ajili ya kikundi.
Hebu jaribu kutulia kwa muda, funga macho yako, kisha uwazie tukio ambalo umesoma hapa hivi punde. Tumia mawazo yako kufanya Aya hizi ziwe halisia hai. Ukiwa umesimama kwenye bustani nzuri zaidi sana katika sehemu yenye baridi ya siku, jisikie upepo wa kupendeza ukikupulizia usoni mwako. Sikiliza sauti ya nyayo za Mungu na usikie mwitikio wa kimya wa viumbe wake wawili wapendwa; kisha swali la Mungu, “Uko wapi?”
Je, unaweza kufikiria wakati huo ulikuwaje, wakati Mungu akiita kwa ajili ya kuwa na ushirika na mwanamume na mwanamke? Tulia tena katika kuutafakari moyo wa Mungu. Mungu anatamani na anatafuta kuwa na ushirika kati yake na Adamu na Hawa, pamoja na wewe, na mimi!
Ingawaje tumejitenga sisi wenyewe kutoka kwa Mungu kwa kutokumtii kwetu (Isaya 59:2), Mungu bado anatamani kuwepo na uhusiano na kila mtu anayeishi. Luka 19:10 anatuonyesha kwamba Mungu anamtafuta kila mwenye dhambi. Mungu angali bado anauliza, “Uko wapi?” Kwa kuwa Yesu alikufa kwa ajili yetu, tunaweza tukarejea tena kwenye uhusiano sahihi na yeye (Waefeso 2:13, 19). Wewe na mimi tumeumbwa kwa ajili ya uhusiano na Mungu.
[1]Kwa mfano, maandiko haya yanaonyesha mahusiano kati ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu: Yohana 17:22-24; Yohana 14:16, 26; na Yohana 15:26. Ingawaje aya hizo hazizungumzii ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu ni wa milele, tunajua kutokana na aya nyingine, kama vile Waebrania 9:14, kwamba yeye pia ni wa milele.
Wale watu ambao hawaamini katika uumbaji wenye upendo na kusudi la Mungu, wanajitahidi kuunda utambulisho wao na kusudi lao wenyewe. Ni vigumu kabisa kuuelewa kwa usahihi ubinadamu kama siyo kutokana na uhusiano na Mungu. Mtu anayeishi kwa ushauri wa kutafuta hekima ya kidunia iliyoelekezwa katika kufuatilia furaha, - hawezi kuyaelewa Maisha kwa usahihi.
Ili kuelewa kwa ukweli utambulisho wetu (kwamba sisi ni nani), kusudi letu (kwa nini tunaishi), na jinsi tulivyoumbwa, ni lazima tulijue kusudi la Muumba wetu, ambalo linapatikana kutoka katika Biblia Takatifu, Mungu tayari alishatengeneza utambulisho wetu; sio jambo ambalo tunazua. Ametuumba kwa ajili ya kusudi na ametutengeneza kimakusudi. Ni pale tu tunapokuwa tumeelewa mpango wake juu ya maisha yetu pamoja na mahusiano yetu ndipo tutakapoweza kutegemewa tuwe kama tunavyotakiwa tuwe na tutakapoweza kukamilisha kusudi lake kwa ajili ya kuwepo kwetu.
Kuumbwa katika sura ya Mungu kunamaanisha kwamba watu waliumbwa kwa ajili ya kuwa na uhusiano wa kipekee. Kama vile Mungu alivyo kwenye uhusiano, aliwafanya watu nao wawe viumbe vyenye uhai. Mungu aliumba nafsi, roho na mwili wa kila mtu kwa ajili ya uhusiano na Mungu na pamoja na watu wengine.
Mwongozo Wetu kwa ajili ya Mahusiano ya Kibinadamu
Ukweli kwamba Mungu aliumba watu kwa ajili ya uhusiano unadhihirisha kwamba anazo kanuni na miongozo kwa ajili ya mahusiano yetu. Mtengenezaji wa bidhaa huandika mwongozo kuhusiana na ile bidhaa ambao unaelezea jinsi ile bidhaa ilivyotengenezwa na jinsi ya kuitumia. Vivyo hivyo, Mungu ametupa Neno lake Biblia, ambayo inaelezea muundo wetu na jinsi maisha na mahusiano yetu vinavyoweza kufanya kazi kwa njia nzuri kabisa.
Biblia inaelezea kwa uwazi majukumu ambayo Mungu ameweka kwa ajili ya mahusiano ya kibinadamu. Inashughulikia majukumu ya waume na wake; wababa, wamama, na watoto; wakaka na wadada; mababu na mabibi; marafiki; maadui; majirani; serikali na raia; waajiri na waajiriwa. Kanuni za Neno la Mungu zinatufundisha muundo wake kwa ajili yetu, haijalishi hali au mazingira yetu. Biblia inatufundisha mapenzi ya Mungu kwetu katika kila hatua ya maisha.
Jamii na tamaduni za kibinadamu zinaonyesha muundo wa Mungu, ingawaje siyo kwa ukamilifu sana. Tamaduni huelezea tabia ya kawaida ya kibinadamu kwenye mahusiano na hali za aina zote. Kila utamaduni una njia zake za kukuza watoto na kudumisha uhusiano wa ndoa. Tamaduni zinaonyesha tofauti kubwa katika mila, mazingira, maumbile, na matukio muhimu, lakini kila utamaduni unashiriki maadili ya msingi. Kwa mfano, kila utamaduni una aina yake ya ndoa.
Hata hivyo, tabia zote zinapaswa zifanyiwe tathmini na kanuni za kibiblia, na siyo kwa kanuni za kitamaduni. Biblia ni mamlaka yetu; lakini siyo utamaduni (Warumi 12:2).
Maelezo ya kina ya kitamaduni siyo lazima yafungamane na upande wowote, na hatupaswi kutegemea iwe hivyo (Waefeso 2:2). Tamaduni huwa zinakuzwa na watu walioanguka ambao huchochewa na tamaa mbaya na ubinafsi. Jamii inaweza ikawa na ujuzi fulani wa ukweli wa kibiblia, lakini bado hakuna jamii inayofuata mara kwa mara viwango vya Mungu vya mema na mabaya. Hakuna kitu chochote kinachostahili kuhesabiwa haki kwa sababu tu ni cha kitamaduni. Biblia peke yake kwa ukamilifu wake ndiyo inayotuonyesha kiwango cha Mungu (Zaburi 19:7-11).
Kama ukiweza kuitembelea nchi ya Libya na ukashuhudia jinsi ambavyo Walibya wanavyoendesha magari bila kujali usalama, unaweza ukafikiri kwamba, “Huo ni utamaduni wao tu; mtindo wao wa uendeshaji unafaa kwa ajili yao.” Ni ukweli kwamba Libya ina kiwango kikubwa cha vifo vya ajali mbaya za magari duniani. Kiwango chao ni mara mbili ya nchi ambayo ina kiwango cha pili cha vifo vya magari duniani. Kwa uhakika, utamaduni wao haujaweza kujenga mtindo mzuri wa kuendesha magari.
Mungu anajua ni kwa jinsi gani maisha yanavyopaswa kufanya kazi na ametupa sisi sheria. Hatupaswi tu kufanya majaribio na kuchunguza. Hatupaswi tu kufanya kile ambacho kinachoonekana kwamba kitatupatia kile tunachotaka. Hatupaswi tu kufikiria kupata kile tunachofikiria kwamba kitakuwa cha maisha ya furaha. Ni lazima tufuate mpango wa Mungu wa mahusiano.
Jambo zuri ni kwamba uaminifu kwenye maelekezo ya mambo ya Mungu ni jambo jema kwetu. Mungu ametupa amri kwa sababu anatupenda sisi (Kumbukumbu la Torati 6:24). Kwa kuzishika amri hizo, tunafurahia matokeo mazuri na tunalindwa dhidi ya matukio mengi mabaya. Mbunifu wetu anajua ni nini kilicho kizuri kwa ajili yetu, na tunapofuata mpangilio wake, tunabarikiwa.
Kuwajibika kwa Mungu katika Mahusiano
► Je, ni kwa jinsi gani mwenendo wetu dhidi ya watu wengine unaathiri mahusiano yetu na Mungu?
► Wanafunzi wanapaswa wasome kila moja ya vifungu vifuatavyo kwa ajili ya kikundi. Jadili kwa ufupi kile ambacho Mungu anataka katika mahusiano haya ya kibinadamu, na jinsi utii unavyoathiri uhusiano wetu na Mungu.
Mahusiano yetu na Mungu na Mahusiano yetu na Wanadamu.
Kifungu cha Maandiko
Mtu/ Jukumu
Anachokihitaji Mungu kwenye Mahusiano ya Mwanadamu
Athari kwenye uhusiano na Mungu
1 Petro 3:7
Mume
Kuwa na ufahamu na heshima kwa mke.
Maombi ya mume hayazuiliki.
Waefeso
5:22, 24, 33; 1 Petro 3:1-6
Mke
Kuwa mtiifu kwa mume.
Hivyo ndivyo mke anapokuwa mtiifu kwa Mungu. Mungu anathamini mtazamo huu na tabia hii ndani yake.
Wakolosai 3:20
Mtoto
Waheshimu wazazi katika mambo yote.
Tabia hii inampendeza Mungu.
Mathayo 6:12-15
Kila mtu
Kusamehe wale wote wanatenda dhambi kinyume chetu
Mungu anaweza kutusamehe.
Warumi 13:1-5
Kila mtu
Kutii mamlaka za kidunia
Ni kwa namna tunavyomtii Mungu.
1 Petro 2:18-20
Mtumishi
Vumilia kwa subira mambo unayotendewa yasiyokuwa ya haki.
Watumishi hupata kibali kutoka kwa Mungu.
Sisi ni viumbe wenye maadili, ikimaanisha kwamba tunaelewa kwamba matendo mengine ni mabaya na mengine ni mema, na tunawajibika kwa Mungu kwa chaguzi zetu tunazofanya. Hii inatupa uwezo na wajibu mkubwa.
Uchaguzi wetu unaathiri mahusiano yetu na Mungu. Utii kwenye maagizo ya Mungu kuhusiana na mahusiano siyo tu jambo lenye kutumika tu la jinsi tunavyoweza kuwa na furaha na kupata kile kilicho bora zaidi katika maisha. Tunawajibika kwa Mungu kwa maamuzi yetu na tabia zetu katika mahusiano (Warumi 14:10, 12).
Mungu ametuita sisi kuwatendea wengine haki, na kufanya kwa upendo na rehema (Mika 6:8). Tatizo ni kwamba, kwa sababu ya dhambi ya Adamu, wazao wake wote waliomfuata wanazaliwa katika hali ya dhambi (Warumi 5:12, 19). Kwa sababu hiyo, hatuwezi kutenda mema mara kwa mara kwa upendo, rehema, na njia za haki (Warumi 7:15-24). Lakini neema ya Mungu inatubadilisha tunapozaliwa mara ya pili. Roho Mtakatifu hutuwezesha kutimiza matakwa ya Mungu (Warumi 8:3-4).
Thamani ya Kila Mtu
► Wanafunzi wanapaswa wasome Isaya 44:24, Zaburi 139:13-16, Mwanzo 9:6, na Yakobo 3:9 kwa ajili ya kikundi. Je, Maandiko haya yanatueleza nini kuhusu thamani ya kila maisha? Je, Ni kitu gani kinachompa mtu thamani?
Ili kuwa na uhusiano mzuri wenye nguvu pamoja na watu wengine, ni lazima tuwathamini watu kama vile ambavyo Mungu anavyowathamini. Kila mtu ameumbwa kwa sura ya Mungu na ni wa thamani kwa sababu hiyo tu. Kila mtu kwa binafsi yake ni kiumbe pekee cha Mungu. aidha awe mwanamume au mwanamke, mwenye afya njema au mgonjwa, mzima au kilema, kijana au mzee, tajiri au maskini (Mithali 14:31), ambaye tayari ameshazaliwa au ambaye bado yuko kwenye tumbo la mama yake bado kuzaliwa, chochote kilicho kivuli cha ngozi zao; na bila kujali uwezo wao wa kiakili au kimwili au mapungufu (Kutoka 4:11).
Kuna tamaduni ambazo wazee husahaulika, wanawake huchukuliwa kwamba ni duni kuliko wanaume, au watoto huchukuliwa kuwa kero. Kwenye baadhi ya tamaduni, vilema huchukuliwa kama ni waliolaaniwa na hufichwa au kukataliwa kutoka kwa jamii. Duniani kote ubaguzi wa rangi umekuwa ni jambo la kawaida: Kabila moja au kikundi fulani cha ukoo kinajiona na kujichukulia chenyewe kama kilicho bora zaidi kuliko wengine na kuwatendea wengine mambo ya aibu.
Kila moja ya vitendo hivi vinashusha thamani ya watu, ambao ni wa thamani zaidi ya uumbaji wote wa Mungu. Ili kuwa na mahusiano yenye afya, yanayomheshimu Mungu, ni lazima kwanza tufikirie watu wote jinsi walivyo—wachukuaji sura ya Mungu.
Kuumbwa kwa ajili ya Mungu, Kuumbwa kwa ajili ya watu wengine.
Ufunuo 4:11 inatueleza kwamba Mungu aliviumba vitu vyote kwa ajili yake mwenyewe. Hii kwa uhakika inahusisha ubinadamu. Tumeumbwa na Mungu , kwa ajili ya Mungu. Tunachotakiwa kufanya, tunatakiwa tufanye kwa ajili ya utukufu wa Mungu (1 Wakorintho 10:31, 1 Petro 2:12). Tumeumbwa pia kwa ajili ya kuwa faida kwa ajili ya watu wengine.
Tuliumbwa ili tufanye kazi na watu wengine katika kukamilisha makusudi ya Mungu. Ndoa ni mfano mmojawapo wa muundo wa Mungu kwa ajili ya kufanya kazi pamoja. Mara tu baada ya kuumbwa kwa binadamu wa kwanza, Mungu alisema, “Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye (Mwanzo 2:18). Mwanamke ni sawa na mwanamume katika njia nyingi muhimu, lakini tofauti katika njia nyingine muhimu. Kwa pamoja wanaweza kukamilisha makusudi ya Mungu kwa ajili ya uwepo wao. Mungu aliwapa -kwa pamoja- kazi ambayo wangepaswa kuifanya (Mwanzo 1:26-28).
Kanisa ni mfano mwingine wa mpango wa Mungu kwa watu kufanya kazi kwa pamoja. Mtume Paulo alitumia kielelezo cha sehemu za mwili (1 Wakorintho 12:12-26). Mtu hapaswi kufikiri kwamba anaweza kutimiza kusudi la Mungu akifanya kazi peke yake au kwamba hahitaji watu wengine. Ndoa na Kanisa ni mifano miwili tu kati ya mifano mingi ya mpango wa Mungu kwa ajili ya watu kufanya kazi kwa pamoja.
Tuliumbwa kwa ajili ya kutumikia watu wengine (Wagalatia 5:13-14). Tumeumbwa kwa ajili ya mahusiano yenye upendo na wengine, ambamo tunajitoa ili kuwanufaisha wengine.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 17:17, Wagalatia 6:2, na Wafilipi 2:4 kwa ajili ya kikundi.
Tuliumbwa kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu wengine. Kila hitaji ambalo Mungu hutufanya katika Neno lake Linahusiana na aidha uhusiano wetu Naye, uhusiano wetu na wengine, au mahusiano yote mawili. Kwa hakika, Yesu alisema kwamba kila jambo ambalo Mungu anataka tufanye linaweza kufupishwa kwa amri za kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, nafsi yetu yote, na akili yetu yote na kuwapenda watu wengine kama tunavyojipenda wenyewe.
► Mwanafunzi anapaswa asome Mathayo 22:36-39 kwa ajili ya kikundi.
Tuliumbwa kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu wengine; mambo haya mawili yanahusiana kwa karibu sana. Mojawapo ya maeneo ya msingi ambayo tunamtukuza nayo Mungu na kuonyesha mfano wake ni katika mawasiliano yetu na wengine. Tabia na matendo ya Mungu yanatuwajibisha kuwa kama yeye (1 Petro 1:16, Mathayo 5:48). Watu wote wameumbwa katika sura ya Mungu, lakini sisi huonyesha asili na tabia ya Mungu tunapotenda kama yeye anavyotenda.
Mtu anapoonyesha kuwa mwenye huruma kwa wahitaji, huruma yake ni mfano wa huruma ya Mungu, na tendo lake la huruma ni kuiga kazi ya Mungu. Jambo hili ni la ukweli bila kujali kama anayeonyesha huruma ni mtu aliyeokoka au ambaye hajawahi kuokoka kabisa. Hata hivyo, tunamuiga Mungu vizuri zaidi tunapokuwa tumepatanishwa naye na Roho wake kufanya kazi ndani yetu.
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Petro 1:2-11 kwa ajili ya kikundi.
Kifungu hiki kinaelezea mpango wa ajabu wa Mungu kwa ajili ya kila mfuasi wa Kristo. Kutokana na kifungu hiki tunajifunza kwamba:
1. Kwa utukufu na wema wake, Yesu kwa pamoja ametuita na kutupa sisi ahadi nzuri za ajabu (Aya ya 3-4).
2. Kupitia ahadi hizi nzuri za ajabu, wale ambao miongoni mwetu wanamjua Kristo tunaweza tukawa na asili ya kiungu ya Mungu ndani yetu (Aya ya 4).
3. Kupitia uhusiano wetu na Mungu aliye Baba na Yesu, tuna kila kitu tunachohitaji kwa ajili ya maisha na utauwa (Aya ya 3).
4. Kwa sababu ya mambo haya yote, tunaweza tukaishi kama Yesu alivyoishi na kama alivyotuita sisi tuishi (Aya ya 5-8).
► Ni kwa jinsi gani inawezekana kuakisi tabia na asili ya Mungu katika mahusiano yetu?
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Wakorintho 4:4 kwa ajili ya kikundi. Ni nani aliye picha kamilifu kwa ajili ya Mungu?
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Wakorintho 3:18 kwa ajili ya kikundi.
Roho Mtakatifu huwabadilisha waumini ili wazidi kuakisi utukufu kwa ajili ya Bwana. Kwa kumwangalia Yesu, tunafanywa kuwa zaidi na zaidi kama yeye katika mitazamo na tabia zetu. Huu ndio uzuri wa Injili. Kupitia nguvu za Mungu Baba, Yesu na Roho Mtakatifu, tunaweza kutafakari na kuiga tabia ya Mungu.
Kwenye mahusiano yetu na watu wengine, Mungu anatutaka tumwige (Waefeso 5:1). Kama vile ambavyo mtoto anavyomtazama na kumwiga mzazi wake, ndugu, au dada yake mkubwa, tunapaswa tuangalie kutoka katika mfano wa Yesu kisha tuige tabia zake, mitazamo yake, na matendo yake tunapokuwa tunashirikiana na watu wengine (Wafilipi 2:5-7, Waefeso 5:2).
► Wanafunzi wanapaswa wasome vifungu vifuatavyo kwa ajili ya kikundi. Zingatia: (1) Tabia au kazi ya Mungu, na (2) Matarajio ya Mungu kwa ajili yetu. (Maelezo ya vifungu viwili vya kwanza tayari yameandikwa kama mfano. Mwishoni mwa somo hili, Kazi ya kufanya ya 2 ni mwendelezo wa fundisho hili.)
Jinsi Mahusiano ya Wanadamu Yanavyoakisi Utukufu wa Mungu
Andiko
Anachokifanya Mungu/
Alichokifanya Kristo
Kitendo Chetu kinachomwakisi Mungu
Wafilipi 2:3-8
Aliachilia haki zake.
Alifanyika kuwa mtumwa.
Alijinyenyekeza kabisa akawa mtiifu.
Kuacha haki zetu.
kujali maslahi ya wengine.
Kuwa mnyenyekevu.
Yohana 13:3-5, 12-15
Aliwahudumia wanafunzi wake, katika mahitaji yao halisia.
Kuwahudumia waumini wengine.
Waefeso 4:32-5:2
Kwa asili, hakuna hata mmoja wetu ambaye anaonyesha upendo wa Mungu kwa sababu tumezaliwa tukiwa na asili ya ubinafsi. Mungu hutupa neema ya kuturejesha tena kwenye mpango wake kwa ajili yetu. Sala ya unyenyekevu ya kujisalimisha inaweza ikampeleka mtu kupita katika mabadiliko haya.
Hitimisho
Biblia inafunua kwamba Mungu kwa upendo wake aliwaumba watu kwa ajili ya mahusiano; uhusiano pamoja naye na mahusiano na watu wengine.
Kwa kuwa Mungu ndiye Muumbaji wa watu wote na Mbunifu wa mahusiano ni lazima:
1. Kupata mtazamo wake juu ya uhusiano wetu wa kibinadamu.
2. Kutambua uwajibikaji wetu kwake kwa ajili ya chaguzi mbalimbali tunazofanya katika mahusiano.
3. Kukubali na kufuata mpango wake kwetu kwa ajili ya mahusiano yetu.
Kozi hii ya mafunzo mahususi itakusaidia wewe kufanya mambo haya na itakutayarisha katika kufundisha wengine mapenzi ya Mungu kwa ajili ya mahusiano ya kibinadamu.
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, kwa nini utamaduni hautoshi kuwa ni mwongozo kwa ajili wa mahusiano ya kibinadamu?
► Je, umepata dhana gani mpya kwako kutokana na somo hili? Kwa nini ni muhimu? Je, kwa kuielewa dhana hii, itakusaidiaje katika mahusiano yako? Kwa kuielewa dhana hii, itaathiri vipi huduma yako?
► Je, ni kwa jinsi gani unatarajia kwamba utakua kwa sababu ya kusoma kozi hii?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kuniumba katika sura yako pamoja na kusudi kwa ajili ya maisha yangu.
Asante kwa kuniumba mimi katika sura yako ili niweze kuwa katika uhusiano na wewe na kufanya iwezekane kupitia kifo cha Yesu kwa ajili ya dhambi zangu.
Asante kwa hazina ya Neno lako, ambayo inanifundisha jinsi ya kuhusiana nawe, na jinsi ya kukutukuza wewe kwenye mahusiano yangu na watu wengine.
Kwa kupitia Neno lako na Roho Mtakatifu wako, nifundishe kuyashikilia maisha uliyoyapanga kwa ajili yangu.
Nisaidie mimi katika kukudhihirisha wewe kwa usahihi kwa kila mtu anayenizunguka, ili kwamba na wengine waweze kuja kukujua wewe.
Ameni
Kazi za kufanya
(1) Elezea jinsi ukweli juu ya uumbaji katika sura ya Mungu unavyompa kila mtu uthamani na jinsi ambavyo kukataliwa kwa uumbaji kunavyoondoa thamani ya ubinadamu.
(2) Soma kila moja ya Maandiko yafuatayo. Zingatia: (1) Tabia ya Mungu au kazi zake,
na (2) Matarajio ya Mungu kwa ajili yetu.
Jinsi Mahusiano ya Wanadamu Yanavyoakisi Utukufu wa Mungu
Andiko
Kile anachokifanya Mungu/
Alichokifanya Kristo
Kitendo Chetu kinachomwakisi Mungu
Zaburi 68:5;
Yakobo 1:27
2 Petro 3:9;
Tito 3:1-5
Mathayo 5:43-48,
1 Wathesalonike 5:14-15
Yohana 13:1, 34;
1 Yohana 4:7-8,
1 Yohana 4:11-12
(3) Ukiangalia Jedwali kutoka kwenye Kazi ya kufanya 2, na hili lililotolewa hapa mwishoni mwa somo, chukua muda wa kuchunguza maisha yako:
Je, kwa sasa unaakisi sura ya Mungu katika njia ambayo inamletea heshima na kumtukuza Yeye?
Je, kuna namna yeyote ile ya kutokutii ambayo ni lazima kutubu ili kwamba maisha yako yawe yanaenda kwa uwazi na kwa nguvu katika kusudi la Mungu kwenye maisha yako?
Je, ni hatua gani ambazo Mungu anakutaka wewe uchukue ili kukufanya wewe ufanane zaidi na Yesu?
Andika aya moja ya maombi kuhusiana na fundisho hili. (Hailazimiki kushirikishana andiko hili na kiongozi wako wa darasa lakini unaweza tu kutoa taarifa kwamba ulishakamilisha Kazi ya kufanya.)
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.