Dr. Robertson McQuilkin alitumika kama mmishenari huko Japani kwa kipindi cha miaka 12. Baadaye akawa raisi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Columbia. Alijulikana sana kama mwandishi, mzungumzaji, na mwalimu. Mkewe Muriel aliugua ugonjwa wa ubongo unaoathiri uwezo wa mtu wa kufikiri, kukumbuka na kuwasiliana. Wakati ugonjwa ulivyozidi kuendelea hadi kufikia kwenye hali ambayo Muriel alihitaji awe chini ya uangalizi wa mara kwa mara, Dr. McQuilkin alijiuzulu kutoka kwenye uraisi wa chuo ili aweze kumhudumia mke wake. Alisema kwamba alikuwa anatimiza ahadi yake waliyowekeana wakati walipooana. Aliamini kwamba kwa kutunza mke wake lilikuwa jambo la maana zaidi kuliko kuendelea kutunza nafasi ya raisi katika chuo kikuu.
Taasisi ya Mungu ya Ndoa.
Ndoa ilisimikwa na Mungu kwa ajili ya mwanamume na mwanamke wa kwanza aliokuwa amewaumba. Ndoa iliundwa na Mungu kuwa kitu ambacho watu walihitaji. Iliundwa haswa kwa ajili ya asili ya mwanadamu. Katika kila kitu ambacho Mungu huumba na katika kila kitu anachokihitaji, kila siku anatutakia kilicho chema zaidi (Kumbukumbu la Torati 6:24). Mungu alikusudia kwamba mpango wake wa ndoa umpe kila mwenzi wa ndoa hali bora ya hisia, ya kimahusiano na hali bora ya kiroho.
Mungu alisema kwamba katika ndoa mwanamume na mwanamke huachana na wazazi wao na kuungana pamoja. Ndoa huwaweka watu kwenye urafiki na uhusiano ulio na nguvu na ukaribu zaidi kuliko uhusiano wowote wa kibinadamu. Ndoa siyo tu kwa ajili ya watu wawili kwenye uhusiano mdogo. Maisha yao yameunganishwa ili kwa maana fulani wawe kama mtu mmoja. Hii haina maana kwamba haiba zao binafsi zinafutika, lakini ni umoja wa aina yake.
Ndoa ya Kibiblia
Ndoa ya Kibiblia ni kitu kizuri sana. Lakini wanandoa wanaotaka kuona uzuri wake na kuonja wema wake lazima wachunguze kile ambacho maandiko yanafundisha kuhusiana nacho, na kisha waendeleze utii katika kile watakachojifunza. Ndoa yenye kuridhisha inahitaji juhudi na kujitoa dhabihu.
Ndoa ya Kibiblia ni kwa ajili ya Ushirika
Kitabu cha Mwanzo kinaelezea uumbaji wa Mungu wa ndoa. Kila sehemu ya maelezo inatoa heshima kwa ndoa.
Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwanzo 2:18).
Kama vile ambavyo Mungu ni Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu walivyo katika ushirika, Mungu alitufanya sisi tuwe jamii. Alitufanya kwa ajili ya kuwasiliana. Alituumba kwa ajili ya urafiki wa karibu sana na ushirika wa pamoja. Mungu alisema haifai mtu kuwa peke yake!
Mungu aliuchukua ubavu kutoka kwa mwanamume na kuufanya kuwa mwanamke mzuri sana, mtu mwingine – aliyeumbwa kuwa sawa na sura ya Mungu, mwenye usawa katika thamani, lakini aliye kiumbe tofauti katika kutengenezwa – ambaye alimkamilisha mwanamume. Huyo mwanamke “huletwa kwa heshima maalumu kwa mwanamume kama uumbaji wa mwisho na mkamilifu zaidi wa Muumba.”[1]
Ndoa inapaswa kuwa muungano wenye furaha.
Wakati Adamu aliposema, “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu” (Mwanzo 2:23) alikuwa akionyesha heshima na furaha. Adamu hakusema, “Hatimaye, nimepata mtumwa! Sasa ni mtu wa kunifulia nguo, kupika chakula changu, kukanda mgongo wangu, na kufanya kazi zangu!” Hapana, Adamu alisema, “Mwishowe, nimempata msaidizi anayenikamilisha mimi!”
Ndoa inapaswa kuwa muungano wa wenza walio sawa.
... msaidizi wa kufanana naye (Mwanzo 2:18).
Mungu alimuumba mwanamke wa kumfanania na kumkamilisha mwanamume.
Mathayo Henry anatukumbusha kwamba, “Mwanamke aliumbwa kutoka katika ubavu uliotoka kwa Adamu; siyo kutoka kichwani kwake kusudi amtawale, wala kutoka katika miguu yake ili kukanyagwa naye, bali nje ya ubavu wake ili awe sawa na yeye, awe chini ya mkono wake kwa ajili ya kulindwa, na awe karibu na moyo wake kwa ajili ya kupendwa.”[2] Mwanamke hakuwa duni wala bora zaidi kuliko mwanamume, lakini alifananishwa na yeye.
Ndoa inapaswa iwe muungano wa agano.
Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (Mwanzo 2:24).
Ndoa zenye nguvu hazitegemei hisia za kimapenzi za siku zote (hisia siyo za siku zote), au raha, (ingawa katika ndoa zenye afya huleta furaha), au utimilifu wa kibinafsi (ingawa katika ndoa imara huleta utimilifu). Faida nzuri za ndoa hazisababishi ndoa imara; ni matokeo ya ndoa imara. Ndoa imeanzishwa juu ya msingi usiotikisika wa agano – mume mmoja na mke mmoja wakiwa wamejitoa kipekee kila mmoja kwa mwingine kwa maisha yao yote.
Ndoa inatakiwa iwe ya wazi, ya kuaminika, na yenye uhusiano unaokubalika — “Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya” (Mwanzo 2:25). Kwa kuwa dhambi ilikuwa bado haijaharibu kutokuwa na hatia kwa wanandoa wa kwanza, ndoa yao ilikuwa isiyo na hukumu, isiyo na aibu, na isiyo na hofu. Agano la Jipya linatueleza kwamba, “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi” (Waebrania 13:4).
Ndoa yenye imara haiwezi kuwepo mahali ambapo kuna ukosefu wa usalama, kutoaminiana, kutiliwa mashaka au woga, au ambapo w anandoa hawana uhakika wa kila mmoja kujitoa kwa ajili ya mwenzake katika ndoa hiyo. Ndoa imara huhitaji ahadi ambayo itaisha pale tu ambapo mwenzi mmoja atakuwa amefariki dunia (Warumi 7:1-2).
Kusudi la Mungu ni kwamba ndoa iwe ya agano la kudumu kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja (Mathayo 19:3-6). Paulo alisema kwamba waumini hawako chini ya kifungo wakati wake zao wasioamini wanapotengana nao. (1 Wakorintho 7:15), lakini mwenzi aliyeamini hapaswi kutaka kutengana na mwenzi asiyeamini (1 Wakorintho 7:12-14, 16). Hapo awali Paulo alikuwa ameandika kwamba Bwana alikuwa amesema jambo linalofanana: Watu walioamini hawapaswi kuchagua kuachana/kutengana kutoka kwa wenzi wao, lakini kama wakiamua kufanya hivyo, hawapaswi kuoa au kuolewa na mtu mwingine tena (1 Wakorintho 7:10-11, Mathayo 5:31-32, Mathayo 19:9).
Upendo wa agano ni wa kujitoa kabisa, ni wa heshima, na wenye kupendeza hata wakati ambapo uhusiano uko kwenye matatizo (1 Wakorintho 13). Ahadi dhaifu husababisha juhudi zisizo thabiti, kukosa muungano wa kihisia, kujiondoa, na majaribu.
Mume anaonyesha upendo wa agano anapokataa kukata tamaa kwa mke wake hata anapokuwa hajali, hana heshima, au anaumwa. Mke anaishi katika upendo wa agano wakati anapochagua kuheshimu na kumtii mumewe, kwa ajili ya Kristo, hata wakati ambapo mume wake hampendi.
Upendo wake unamfanya mkewe amuheshimu, na heshima yake inamfanya mumewe ampende zaidi. Kwa pamoja, wanazidi kuimarika na kukua katika uhusiano wao!
► Je, ni matatizo gani hutokea ikiwa watu watafunga ndoa huku wakiwa wanafikiria kwamba wanaweza kubadilisha maamuzi yao baadaye kama watakuwa hawana furaha na ndoa yao? Je, kujitolea kwa ukamilifu kunaleta tofauti gani ikiwa mtu anaamini kwamba ndoa ni ya kudumu?
Ndoa Ya Kibiblia ni Mahali Pa Utimilifu wa Mapenzi na Kuzaa
Mungu alifanya tendo la ndoa liwe la kufurahisha kabisa na lenye nguvu ya kipekee. Ni tendo linalokusudiwa kuleta umoja kimwili, kihisia, na kiroho. Maisha ya tendo la ndoa lenye afya siyo tu kusisimua na kuleta umoja, lakini linafanya uhusiano kunawiri. Kwa wale wanaotaka kufuata maadili ya kibiblia katika tendo la kujamiiana, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu iliyotolewa kwa ajili ya kufurahia kikamilifu ndani ya ndoa.[3]
► Wanafunzi wanapaswa wasome 1 Wakorintho 7:1-5 na Waebrania 13:4 kwa ajili ya kikundi.
Kwenye aya za 1 Wakorintho tunaambiwa kwamba kusudi moja la ndoa ni kuridhishana katika matamanio ya kujamiiana. Mume na mke kila mmoja amejitoa kwa ajili ya mwenzake na wameachana na madai yao ya umiliki wa miili yao kwamba ni mali yao wenyewe. Hiyo inamaanisha kwamba mtu aliyeko kwenye ndoa asitegemee kujihusisha na kujamiiana tu kwa wakati anaouchagua yeye lakini pia anatakiwa aweze kuitikia tamaa ya mwenzi wake wa ndoa. Mistari hiyo haifundishi kwamba mtu anaweza kulazimisha kutimiziwa mahitaji yake bila ridhaa ya mwenzi wake. Badala yake, inahimiza kila mmoja kuzingatia na kujibu mahitaji ya mwenzake kwa upendo na heshima.
Kifungu hiki kinatueleza kwamba watu walioko kwenye ndoa hawapaswi kumnyima mwenzake fadhila hii. Kipindi kifupi cha kuacha kujamiiana kukiambatana na kufunga kwa maombi ni halali, lakini utengano wa muda mrefu utasababisha majaribu kwa sababu ya matamanio yasiyoridhika.
Wakati mwingine wanandoa huchagua wenyewe kutenganishwa kwa miezi kadhaa au zaidi kwa sababu mtu huenda kazini au kusoma mahali pa mbali. Kabla ya kufanya uamuzi kama huo, wanapaswa kuzingatia kama mpango wao huo unalingana na mpango wa Mungu au la. Wanaweza kupata matatizo kwa sababu ya kutengana kwao kwa muda mrefu.
Watu wengine huamua kuishi bila watoto, lakini Biblia inafundisha kwamba Mungu husherehekea wazazi wanapokuwa na watoto wanaomcha (Malaki 2:15). Ni jambo la muhimu kutambua kwamba siyo uzazi tu Mungu anaoutaka, bali watoto wanaomcha Mungu. Wazazi wameitwa na Mungu kuwafundisha watoto wao kumfuata Kristo.
Ndoa ya Kikristo ni kwa ajili ya Kristo
► Wanafunzi wanapaswa wasome 1 Petro 3:1-7 na Waefeso 5:22-33 kwa ajili ya kikundi. Kikundi kitapaswa kiweke vifungu hivi wazi kwa ajili ya kuvifanyia kazi wakati wa majadiliano haya.
Katika Waefeso 5:30-32, Roho Mtakatifu wa Mungu anafunua kwa undani zaidi maana ya ndoa, iliyofichwa hadi Yesu atakapokuja. Ndoa ni kivuli cha kidunia – kuakisi – uhusiano kati ya Yesu Kristo na Kanisa.
Paulo anaianza sehemu hii kwa kuwahimiza waumini wajazwe na Roho (Waefeso 5:18). Ni katika muktadha huu ndipo anapotoa maelekezo yafuatayo kuhusiana na ndoa.
Bibi-harusi aliyejazwa na Roho atajinyenyekeza kwa bwana-harusi wake (“kichwa chake”) katika Bwana, kama jinsi ambavyo waumini hujinyenyekesha kwa Yesu (Waefeso 5:24, 32; ona pia 1 Petro 3:1). Hii ndiyo njia ambayo bibi-harusi anaweza kuonyesha heshima kwa Yesu na kwa mume wake. Mke anapaswa akubaliane na uongozi wa mume wake hata kama mume siyo mtu aliyeamini/aliyeokoka. Ikiwa atafanya hivyo, mume wake ambaye hajaokoka ana uwezekano mkubwa wa kuokoka.
Ni muhimu sana kwa kila mke kuwa na Bwana kwenye akili katika utii wake. Ni kwake na kwa ajili yake kwamba ananyenyekea na siyo kwa ajili ya mume wake. Jicho lake linamwangalia Yesu, ambaye peke hajawahi kuwa na makosa. Mke kujitiisha kwa hiari kwa ajili ya mume wake ni kitendo cha ibada kwa Yesu. Utii wa Kibiblia, kama vile upendo, hauwezi kuwa wa kulazimishwa (Waefeso 5:33). Utii wa Kibiblia ni zawadi ambayo wake huwapa waume zao kwa heshima kuu kama kwa Yesu.[4]
Kujitoa kwa mke kwa ajili ya mumewe ni tendo la heshima (Waefeso 5:33) kwake, kama sehemu ya maisha yaliojazwa na Roho (Waefeso 5:18-21). Heshima hii inayotoka katika roho ya upole na utulivu ni ya thamani sana mbele za Mungu (1 Petro 3:4).
Bwana-harusi aliyejazwa na Rohoatampenda bibi-harusi wake kama vile Yesu alivyolipenda Kanisa lake (Waefeso 5:25). Bwana harusi ni lazima ampende mke wake kama anavyoupenda mwili wake mwenyewe (Waefeso 5:28-29). Ni lazima kujidhabihu kwa kujazwa na Roho kama vile Yesu alivyodhihirisha kwa kanisa lake wakati alipojitoa kwa ajili yake. Hiki ndicho kitendo chake cha kujisalimisha kwa Mungu (Waefeso 5:21).
Mtoa maoni mmoja aliliweka jambo hili kama ifuatavyo:
Kama Yesu alivyojitoa kufa msalabani ili kuokoa kanisa, vivyo hivyo tunapaswa kuwa tayari kujinyima na kuvumilia [kazi ngumu na matatizo], ili tuweze kuleta furaha kwa mke. Ni wajibu wa mume [kufanya kazi kwa bidii] kumuhudumia; kukidhi mahitaji yake; kujinyima raha na mapumziko, ikibidi, ili kumtunza anapokuwa mgonjwa; kumlinda mbele ya hatari; kumtetea anapokuwa [katika hali ya hatari]; kuvumilia tabia yake anapokuwa na hasira; kushikamana naye anapojaribu kumsukumia mbali; kuomba naye anapokuwa na matatizo ya kiroho; na kuwa tayari kufa ili kumuokoa. Kwa nini isiwe hivyo? Ikiwa watakuwa katika ajali ya meli, na kuna ubao mmoja tu wa kuokoa maisha, je, haipaswi awe tayari kumweka mke wake juu yake, na kuhakikisha usalama wake kwa gharama yoyote kwake mwenyewe? Lakini kuna zaidi… mume anapaswa kuhisi kuwa lengo kuu la maisha yake ni kutafuta wokovu wa mke wake. Anapaswa kumpatia yote anayohitaji kwa ajili ya roho yake… Na anapaswa kuwa mfano; kumpa ushauri ikiwa anahitaji ushauri; na kuifanya njia ya wokovu iwe rahisi kwake iwezekanavyo. Ikiwa mume ana Roho na kujikana nafsi kama Mwokozi, hataona dhabihu yoyote kuwa kubwa sana ikiwa inaweza kuendeleza wokovu wa familia yake.[5]
Bwana harusi anapaswa atafute usafi wa bibi harusi wake kama ambavyo Kristo alimtaka bibi harusi wake, yaani Kanisa (Waefeso 5:26-27).
Katika 1 Petro 3:7 panasema kwamba mume anapaswa aishi na mke wake kwa njia ya kuelewana, ikimaanisha kwamba atapaswa afanye kila linalowezekana katika kumwelewa mke wake. Anapaswa kumsoma ili aweze kuelewa mahitaji yake. Katika aya hii, mwanamke anaitwa “chombo kidhaifu.” Mke anahitaji kuzingatiwa na mume wake. Anapaswa amlinde siyo tu kwenye madhara ya kimwili, lakini pia kutoka katika wasiwasi na mhemuko unaotokana na msongo wa mambo.
Mume anapaswa kutoa kila njia muhimu itakayohitajika kwa ajili ya kumstawisha mke wake; uaminifu, upendo usiokuwa na masharti, ufahamu/uelewa, ushauri, kufundisha, na huruma.
Inapotokea mume kutendea mke wake kwa upendo kama huu, atalipwa kwa furaha. Paulo anasema kwamba, “Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe” (Waefeso 5:28). Waume wanaowapenda wake zao kwa njia hii ya kujidhabihu watalipwa zaidi na Bwana, na uwezekano mkubwa ni kwa heshima, upendo na uaminifu wa mke wake.
► Je, ni mambo gani mahususi ambayo mume anapaswa kuyafanya ili kutoa msaada wa kiroho kwa mke wake?
Ni muhimu kukumbuka jinsi maagizo katika mistari hii yanavyotolewa. Mume hakuagizwa kutumia mamlaka kwa nguvu juu ya mke wake. Ingawa mke ameagizwa kumtii mumewe, mume hakuambiwa amfanye mkewe kumtii kwa kulazimisha.
Kipaumbele cha mume hakipaswi kiwe ni kudumisha mamlaka yake bali kutoa utunzaji wa upendo. Kipaumbele cha mke hakipaswi kiwe ni kudai matunzo kwa ajili yake mwenyewe bali kumheshimu mume wake.
Mtume Petro anamuonya mume kwamba maombi yake yatazuiliwa kama hatachukua jukumu la kumtunza mke wake inavyostahili. Kutokana na maneno ya Paulo na Petro, tunaweza kuona kwamba mume ambaye hamjali mke wake kama ambavyo ingetakiwa afanye atakuwa pia hampendi Mungu kama inavyotakiwa iwe. Mwanamke ambaye hawezi kumheshimu mume wake anakuwa pia hamheshimu Mungu kama ambavyo ingepaswa iwe. Tabia zetu kwenye ndoa zinaathiri uhusiano wetu na Mungu.
[4]Kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa mada ya uwasilishaji wa Biblia, ona Somo la 10 la Malezi ya Kiroho, linalopatikana kutoka Shepherds Global Classroom.
Mungu alipanga ndoa iwe kitu cha kudumu. Katika ndoa, mwanamume na mwanamke kila mmoja anatoa ahadi ya kuwa mwaminifu kwa mwenzake kwa muda wote watakaokuwa wanaishi pamoja wakiwa hai.
Biblia inarekodi maneno ya Yesu kuhusu ndoa aliyozungumza kwenye mahojiano yake na Mafarisayo.
► Mwanafunzi anapaswa asome Mathayo 19:3-8 kwa ajili ya kikundi.
Yesu alisema kwamba Mungu alikusudia ndoa iwe ya kudumu. Alisema kwamba talaka ilianzishwa kwa ajili ya watu wasiomfuata Mungu.
Kuna sababu nyingi ambazo zilimfanya Mungu apange ndoa iwe ya kudumu, na baadhi ya sababu hizo tulizizungumzia katika sehemu ya mwisho. Sababu nyingine ya ndoa kuwa ya kudumu ni kwa sababu ya watoto. Kutii mpango wa Mungu katika ndoa husababisha kuwepo na mazingira bora zaidi ya kulea watoto. Wazazi wanapomheshimu Mungu kwa Kutii kanuni zake katika ndoa na familia zao, wataweza kulea watoto wanaomcha Mungu (Malaki 2:15).
Mungu alipanga maisha ya mwanadamu kwa njia ambayo watoto huchukua miaka kadhaa ya kukua na kuwa watu wazima. Wakati wa kipindi hiki, watoto huwa ni tegemezi kwa wazazi wao kwa ajili ya ulinzi, kuwapatia mahitaji, na mafunzo. Hii ni tofauti na wanyama ambao hukua na kukomaa kwa kipindi kati ya mwaka mmoja au miwili tu. Watu wanahitaji muda zaidi ili kuweza kukuza tabia iliyokomaa. Mungu alipanga familia kama njia ya kulea watoto. Matatizo mengi katika jamii yanatokana na ukosefu wa familia zilizo na wazazi waaminifu.
Ndoa inahitaji watu kutoa ahadi ya kukabidhiana maisha yao yote. Kila tamaduni ina aina yake na sherehe ya kuonyesha kwamba ndoa ni ahadi nzito. Sherehe ni njia mojawapo ya mwanamume na mwanamke kuweza kutamka hadharani kwamba wanafanya ahadi hii ya maisha yao yote.
Serikali nyingi hutunza kumbukumbu za ndoa zilizofungwa. Sheria kuhusu ndoa zinagusa umiliki wa mali, utunzaji wa watoto, na urithi.
Huu hapa ni mfano wa viapo vya harusi ambavyo vimetumiwa katika harusi nyingi:
Mimi [...] ninakuchukua wewe kuwa [mume/mke] wangu wa ndoa, kuanzia siku hii na kuendelea, kuwa nawe na kukushikilia, kwa mema na mabaya, kwa utajiri na umasikini, katika ugonjwa na afya, kukupenda na kukuthamini, hadi kifo kitakapotutenganisha, kulingana na amri takatifu ya Mungu; na kwa hayo, najitoa kwako.
Hisia za mapenzi haziwezi kuwa za kudumu nyakati zote. Ndoa haiwezi kutegemea hisia za kibinafsi ambazo zinaweza zikabadilika. Viapo vya ndoa vinaamaanisha kwamba mwanamume na mwanamke wanaahidiana kuwa waaminifu kwa kila mmoja wao kwa muda wote ambao wote wawili watakuwa wanaishi, na kwamba ahadi hiyo haihusiani na masharti yoyote.
Kwa sababu ya kudumu kwa ndoa, wakristo hawapaswi kamwe kutoa kauli ambazo zinaonyesha kwamba wako tayari kuvunja ndoa zao kwa sababu za matatizo ya mahusiano. Mtu hatakiwi kusema, “Laiti nisingelikuoa wewe,” au “Labda tuachane.” Wakati mwingine, kauli hizo ni jaribio la kumshawishi mwenzi mwingine kuonyesha kwamba anajali ndoa. Mtu hufikiri kwamba mwenzi wake ataweza kujitahidi zaidi kumpendeza kwa sababu ya kauli hiyo kali, lakini mara nyingi hilo halitokei. Badala yake, mwenzi mwingine hujilinda kwa kusema, "Sawa, tunaweza kuachana kama unataka." Hivyo basi, wote wawili huonyesha kuwa wako tayari kumaliza ndoa kwa sababu ya matakwa yao binafsi, na mahusiano huwa mabaya zaidi.
► Je, kwa nini ndoa inaanza na viapo vya harusi na siyo tu tamko la upendo?
► Je, kuna mtu anataka kushirikisha jinsi ambavyo yeye ameingia kwenye ndoa akitegemea manufaa zaidi lakini bila ya kutambua kwamba dhamira ni muhimu?
Ndoa kama ushirika wa Kikristo
► Mwanafunzi anapaswa asome 2 Wakorintho 6:14-18 kwenye kikundi.
Aya hizi zinatuambia kwamba kujitoa kwa muumini kunaweza kuzuiliwa ikiwa ameunganishwa kwa karibu sana na watu wasioamini. Kama vile ambavyo muumini hawezi kuabudu pamoja na mtu ambaye anamwabudu Shetani, hawezi kufuata mtindo wa maisha na vipaumbele vya watu wasioamini. Onyo hili linaweza kutumika kwenye aina kadhaa mbalimbali za mahusiano, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kibiashara.
Ndoa ni uhusiano ulio wa karibu zaidi wa kibinadamu. Mtu aliyeokoka hapaswi kabisa kufikiria kuoa mtu ambaye siyo mtu aliyeokoka kwa kumaanisha (1 Wakorintho 7:39). Mtu aliyeokoka akiolewa na mtu ambaye hajaamini atapata huzuni nyingi na vikwazo vingi katika kulea watoto na hata katika kufanya maamuzi ya mfumo wa maisha.
Kama mume na mke wote wameokoka lakini wanatoka katika makanisa tofauti ya watu walioamini, lazima wahakikishe kwamba wanakuwa kwenye makubaliano kuhusiana na masuala muhimu ya kiroho. Watatakiwa wapange kuwa sehemu ya kanisa moja la mtaa baada ya kuwa wameshaoana.
Njia Ambazo Wanandoa Wanaweza Kuimarisha Ndoa Yao
(1) Ni lazima washerehekee/wafurahie mpango wa Mungu wa asili wa uumbaji na kuthamini majukumu yao ya kipekee yaliyo ndani ya ndoa.
Mume ni lazima akumbuke kwamba mke ni zawadi kutoka kwa Mungu, na ni msaidizi anayemkamilisha. Anapaswa atoe uhai wake kwa ajili ya usalama wake na kwa ajili ya hali yake ya kiroho, mihemuko, na ya kimwili.
Ni lazima achague kuwa mtu wa shukrani kwa ajili yake na kumpenda hata katika wakati ambapo yeye hastahili kabisa, akitambua wazi kwamba ni Mungu peke yake awezaye kubadilisha kile kinachotakiwa kibadilike ndani yake. Mungu ataheshimu utii na imani ya mume.
Mke anapaswa aheshimu chaguo la mume wake kuwa kichwa chake, anapaswa amheshimu katika kila njia atakayoweza. Ni lazima achague kuwa na unyenyekevu na heshima hata anapokuwa amefanya makosa na kutostahili kabisa, akiomba Mungu kwamba abadilishe kile kinachotakiwa kubadilishwa ndani yake. Mungu ataheshimu utii na imani ya mke.
(2) Wanandoa waliooana ni lazima wastawishe urafiki wa karibu sana wa kiroho na kimwili.
Ni lazima watafute kujuana wao wenyewe pasipo kuwepo na mashaka, lawama, ulinganifu na wengine, unyanyasaji, tamaa ya ubinafsi, au udhalilishaji. Ni lazima waishi katika hali ya uwazi na uadilifu mbele za Mungu na wao wenyewe.
(3) Wanandoa waliooana ni lazima wafuate mfano wa neema ya Mungu wanaposhindwa kujipima.
Wakati Adamu na Hawa walipoanguka katika dhambi na kujisikia wenye aibu na majuto, Mungu aliufunua uwezo wake kwa ajili ya kukomboa madhaifu yao. Mungu alimtoa mnyama akamfanya dhabihu na kutengeneza hapo makoti kwa ajili ya kuwafunika Adamu na Hawa wasitiri hali zao za kuwa uchi (Mwanzo 3:21). Kitendo hiki cha upendo kilichofanywa na Mungu kilikuwa ni picha ya neema na ya ahadi ya Mungu ya ukombozi kupitia Kristo. Kristo hutuwezesha sisi kusamehewa na kurejeshwa tena. Kupitia Kristo, wanandoa wanaweza kurudi katika hali ya kuwa na ukaribu bila aibu hata baada ya kushindwa.
Hitimisho
Ndoa ni mpango wa Mungu wa uumbaji, na siyo wa mwanadamu. Kwa hiyo, ni lazima tumwendee Mungu kwa ajili ya maelekezo, na siyo kwenda kwa dunia au kwenye tamaduni zetu. Mungu peke yake ndiye anayejua jinsi ya kuzifanya ndoa zetu ziwe zenye nguvu, endelevu, na zenye thawabu. Lakini kamwe haitawezekana tuwe wanandoa tunaotaka tuwe pasipokuwepo na uwepo wa Roho Mtakatifu!
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, kuna ukweli gani katika ndoa ambao unaonekana kusahaulika na watu wengi?
► Elezea kanuni ambazo kanisa linapaswa kufundisha ili kuimarisha ndoa. Kuna uelewa gani ambao kipekee unakosekana kwenye mazingira yako?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kutupa sisi zawadi nzuri ya ajabu ya ndoa. Asante kwa ajili ya njia nzuri uliyotumia kuiunda. Tusaidie sisi kujitoa kabisa kwa umuhimu wake kwa ajili yetu ili tuizoee ndoa katika njia ambayo uliipanga wewe.
Tusaidie katika kudhihirisha upendo ambao ni kama ule ulioko kati ya Kristo na Kanisa.
Tusaidie tuweze kwenda zaidi ya dhana za utamaduni wetu kwenye kuonyesha heshima kwa ajili ya mwingine.
Asante kwa ajili ya kazi ya Roho Mtakatifu ambaye hufanya mahusiano ya furaha na nguvu yawezekane.
Ameni
Kazi za Kufanya Mazoezi
(1) Chagua kanuni mbili ambazo zilikuwa mpya kwako kutoka katika somo hili. Andika aya kwa kila kanuni ukielezea kwa maneno yako mwenyewe.
(2) Andaa wasilisho fupi kuhusiana na mada zilizoorodheshwa hapa chini. (Kiongozi wa darasa atagawa mada kwa kila mwanafunzi.) Shirikisha wasilisho hili mwanzoni mwa kipindi cha darasa kitakachofuata. Mada hizo ni:
Mpango wa Mungu wa muunganiko katika ndoa
Madhumuni ya Biblia katika ndoa
Majukumu yaliyotolewa na Mungu ndani ya ndoa na umuhimu wa kujazwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kutekeleza majukumu hayo
Kudumu kwa ndoa
(3) Ikiwa bado hujaoa, lakini unapanga kuoa wakati ujao, andika vifungu viwili vya aya kuhusu ahadi ya kutii kanuni za Mungu kwa ajili ya ndoa yako wakati ujao. Ikiwa tayari ulishafunga ndoa, andika vifungu viwili vya aya kuhusu ahadi ya kutii kanuni za Mungu kwenye ndoa yako.
Heshima kwa Wanawake
Kabla ya kuendelea na Somo la 4, darasa linapaswa lijifunze na kujadili Kiambatanisho A. Huu ni mjadala mfupi kwa ajili ya heshima kwa wanawake, na ni mada muhimu sana inayohusiana na ndoa na familia.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.