Ruthi alilelewa katika familia moja ya Kikristo huko India. Siku moja familia yake ilimwambia kuhusu mhubiri mmoja kijana aliyeitwa Samweli ambaye alikuwa anahitaji kuwa na mke. Pia walizungumza na Samweli kuhusiana na Ruthi. Ruthi alisema kwamba hakuwa tayari kukutana na huyu kijana. Siku moja Ruthi alirejea nyumbani jioni na akamkuta Samweli akiwa amemsubiria pale kwa masaa kadhaa ili kukutana naye. Hakufurahia kumwona, lakini alikaa chini ili aweze kuzungumza naye. Alisema, “Mimi ni mwalimu wa chuo cha Biblia, Silipwi malipo makubwa. Pia ninasafiri kwenda kuhubiri Injili maeneo mbalimbali, na wakati mwingine huwa ninalala nje kwenye udongo. Je, uko tayari kupata mateso pamoja nami?” Ruthi alianza kulia alipokuwa akisema kwa sababu alijihisi kuwa Mungu alikuwa akimwambia kwamba huyu ndiye mwanamume ambaye angepaswa kuolewa naye. Baada ya mazungumzo yao, walikuwa wakionana mara chache sana, na hawakuwa peke yao, hadi ilipofikia wakati wa harusi. Kwa sasa wameshatumika kwa pamoja katika huduma kwa miaka mingi.
Chaguo la Mume au Mke
Chagua kwa Uangalifu!
Yesu alisema kwamba ndoa ni ahadi ya maisha yote, kwa mpango wa Mungu (Mathayo 19:6-8). Siyo tu kwamba ni kumwoa mtu sasa hivi. Unamwoa mtu wa kuwa na wewe kama mwenzi wako kwa maisha yote hadi mmoja wenu atakapofariki dunia (Warumi 7:2). Fanya uchaguzi wa busara!
Hutashiriki tu nyakati nzuri na furaha za maisha. Utashiriki katika matatizo, shida, maumivu ya moyo, migogoro, na misiba ya maisha. Kuna baraka nyingi zinazotokana na kuoa au kuolewa na mwenzi wako ambaye ni mcha Mungu katika nyakati ngumu. Lakini nyakati ngumu huwa mbaya zaidi wakati unapokuwa una mwenzi ambaye hana nguvu za Bwana. Unaoa au kuolewa na mtu ambaye atakuwa wako kwa maisha yako yote – na katika hali zote. Chagua mume/mke kwa uangalifu mkubwa!
[1]Unaingia kwenye ndoa na mtu ambaye utaanzisha naye familia. Unachagua watakaokuwa wazazi wa watoto wako na babu/bibi wa vizazi vyako. Unamchagua mtu ambaye maisha yake ya kiroho kwa kiwango kikubwa yatashawishi sana maisha ya kiroho ya watoto wako. Unamchagua mtu ambaye kwa mwenendo wake, tabia zake, na hulka zake zitakuwa zinaigizwa (Waefeso 5:1). Unamchagua mtu ambaye atawatengeneza na kuwafundisha watoto wako kupitia mifano na jinsi ya kuongea (Mithali 23:26). Chagua mtu ambaye atawalea na kuwatunza watoto wako, mtu ambaye atawaongoza na kuwafundisha nidhamu kwa uangalifu, bidii, na kwa upendo. Unamchagua mtu ambaye atakuwa na athira kwa vizazi – kwa manufaa au kwa madhara. Chagua kwa busara!
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 14:1, Mithali 24:3-4, na Mithali 31:10-12, 30 kwa ajili ya kikundi.
Uchaguzi wako wa mwenzi wa ndoa ni uamuzi wa pili muhimu sana ambao utakuwa umeufanya katika maisha yako; uamuzi wa kwanza kuliko wote ni ule wa kumchukua Yesu kama Bwana na Mwokozi wako. Uchaguzi wako utabadilisha mwenendo wa maisha yako, lakini utaathiri watu wengine pia. Uchaguzi wa busara utakuwa ni wa baraka kwako na kwa watu wengine wengi. Uchaguzi wa kipumbavu utakuwa ni wa madhara kwako na kwa watu wengine wengi. Chagua kwa maombi!
Hakuna watu walio wakamilifu duniani. Wewe una matatizo, madhaifu, na kushindwa. Mwenzi wako pia hatakuwa mkamilifu na atendelea kuwa mtu ambaye hajakamilika katika maisha yake yote. Kwa hiyo, usitake kutafuta mwenzi ambaye amekamilika. Badala yake, tafuta mwenzi ambaye ni mcha Mungu bila kubakiza lolote. Angalia mtu ambaye ni mnyenyekevu wa kutosha wa kukubali na kurekebisha makosa na kushindwa. Mwenzi wa jinsi hii atakuwa baraka kwako, na mnaweza kwa pamoja kupeana msaada kwenye maeneo yenye madhaifu.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Mithali 11:14, Mithali 12:15, Mithali 13:18, na Mithali 23:22 kwa ajili ya kikundi.
Chagua kwa busara. Chagua kwa ajili ya maisha ya kudumu. Pata ushauri kutoka kwa watu wenye kumcha Mungu na kwa wazazi wako. Sikiliza maonyo yao. Usipende tu kusikiliza hisia zako mwenyewe. Uchaguzi huu ni wa muhimu sana ambao hautakiwi kabisa wewe kuwa mzembe.
Usioane na mtu ambaye Hajaokoka
Jambo moja ambalo ni la maana sana kwa Mungu ni kwamba watu wake wafunge ndoa na waumini wenzake tu. Hii ni kwa sababu uhusiano wa mtu na Mungu ndilo jambo muhimu zaidi katika maisha yote na hata kwenye umilele. Ndoa – uhusiano wa karibu zaidi kati ya wanadamu—huathiri uhusiano wa mtu na Mungu. Ni jambo gumu zaidi kwa mtu aliyeokoka kudumisha na kutembea kwa ukaribu na kwa uangalifu zaidi na Mungu wakati akiwa anaishi na mwenzi ambaye hajaokoka.
Zaidi ya hapo, kutokuamini kwa mzazi kunaathiri sana watoto dhidi ya Kristo. Kwenye familia ambazo mzazi mmoja anakuwa bado hajaokoka, ni nadra sana kwa watoto wote kuweza kumtumikia Bwana. Mungu huwa anatutaka sisi kumtumikia yeye, na Mungu anatuambia kwamba tuwalee watoto wetu ili waweze kumtumikia Yeye (Mwanzo 18:19; Kumbukumbu la Torati 6:2, 7; Malaki 2:15).
Kwenye Agano la Kale, wana wa Israeli hawakuruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu yeyote nje ya familia ya imani.[2] Mungu alitambua kwamba ndoa kwa watu ambao hawajaamini itasababisha watu kuabudu miungu mingine, huku wakiharibu uhusiano wao na Mungu mmoja tu wa kweli! Agano la Kale linatuonyesha sisi kwamba hilo ndilo jambo hasa lililotokea kwa Israeli.[3]
Bado hata sasa, watu waliookoka/walioamini wanapaswa kuwa kwenye ndoa na watu waliookoka tu. Usikubali kuingia kwenye maelewano ya kukubaliana kubatilisha chochote kwenye jambo hili. Usitake kusamehe suala la uhusiano wa mapenzi na mtu ambaye hajaokoka.
► Wanafunzi wanapaswa wasome2 Wakorintho 6:14-18 and 1 Wakorintho 7:39 kwa ajili ya kikundi.
Wakati mwenzi wako siyo mtu aliyeokoka
Mungu hataki kabisa mwamini ambaye hajaingia bado kwenye maisha ya ndoa kuoa au kuolewa na mtu ambaye hajaamini. Jambo hilo ni hakika. Lakini wakati mwenzi mmoja kutoka kwenye nyumba ya familia ambayo haijaamini anapokuja kwa Kristo kuupokea wokovu, atapaswa abakie na mwenzi wake ambaye hajaokoka, isipokuwa kama mwenzi wake atakataa kuendelea kuishi naye (1 Wakorintho 7:12-16). Katika baadhi ya matukio, wenzi walioko kwenye ndoa ambao hawajaokoka wamepata kupokea wokovu kwa sababu ya imani ya mume au mke wake aliyekwisha kuokoka (1 Wakorintho 7:14, 16; 1 Petro 3:1-2). Lakini Wakristo ambao bado ni waseja kamwe hawapaswi kufikiria kufunga ndoa na mtu ambaye hajaokoka.
Sifa za kuwekea maanani kwa Mwanandoa Mtarajiwa
Wakati wa maandalizi kwa ajili ya ndoa, watu binafsi wanapaswa kukuza sifa pambanuzi na au bainishi ambazo zitawasaidia katika kuwapata wenzi wazuri. Wanapokuwa wanatafuta mtu wa kuingia naye kwenye ndoa, wanapaswa kuangalia mtu ambaye pia anaendelea kukua katika sifa hizi zinazofanana.
[4]1. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye uhusiano wake na Kristo utakutia wewe moyo katika uhusiano wako binafsi na Kristo na kukuwezesha wewe kuendelea kukua kiroho (2 Petro 1:5-9, 2 Petro 3:18).
2. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye ana tabia nzuri. Katika Waefeso 5:33 wanawake wanaagizwa kuwaheshimu wanaume wao pasipo kutia maanani tabia zao, lakini hii ni rahisi sana kufanya wakati wanapokuwa wameoana na wanaume wanaostahili kupewa heshima. Tabia nzuri huwa ni pamoja na zile tabia za kusamehe, kuwa na kiasi, kuwa mnyenyekevu, kuwa na bidii pamoja na kuwajibika na kuwa na roho inayofundishika. Mtu unayetaka uingie naye kwenye ndoa hataweza kuwa mkamilifu lakini anapaswa aweze kuwa mtu wa kukua katika tabia hizi.
Mungu ana viwango vya juu kwa ajili ya viongozi wa kanisa pamoja na wake zao (1 Timotheo 3:2-4, 8-9, 11-12; Tito 1:6-8). Ikiwa kiongozi wa kanisa yuko kwenye ndoa na mwenzi ambaye ana tabia mbaya, huduma itakuwa na kipingamizi kikubwa.
3. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye anajijengea sifa ya usafi na tabia njema (1 Timotheo 2:9-10, 1 Timotheo 3:7, 2 Timotheo 2:19, Tito 1:15, Tito 2:4-5).
4. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye anajifunza kibiblia (Zaburi 119:66). Wakati wa kukabiliana na majaribu, hofu, mtazamo mbaya au nia mbaya, wanajifunza kukumbuka, kuamini, na kutii neno la Mungu (Mithali 4:4-6, Joshua 1:7-8). Wanapokabiliwa na hali ya kuwa wahitaji, hali ya hatari, taabu, au matatizo ya aina yeyote, wanakuwa wanajifunza jinsi ya kuelekeza mwelekeo wao kwa Mungu na kupata msaada wanaouhitaji kutoka kwenye Neno Lake (Zaburi 119:50, 92, 114).
5. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye anaweza kuwa baba au mama mzuri kwa watoto wako: Mtu ambaye ataweza kuwafundisha njia za Mungu na jinsi ya kuishi maisha ya Kikristo yenye uthabiti mbele yao (Mithali 6:20-23, Waefeso 6:4, 2 Timotheo 1:5, 2 Timotheo 3:14-15).
6. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye amechagua kushawishiwa na marafiki wacha Mungu na washauri (Zaburi 119:63, 2 Timotheo 2:22).
7. Ingia kwenye ndoa na mtu ambaye ni mnyenyekevu kwa mamlaka. Mwanamume ana busara ya kutafuta mwanamke mnyenyekevu ili awe mke wake (Waefeso 5:22). Mwanamke naye pia anapaswa aingie kwenye ndoa na mwanamume ambaye ni mnyenyekevu kwa Mungu na kwa wale wote ambao Mungu amewaweka kwenye mamlaka juu yake katika kanisa, kwenye kazi yake, na serikalini (Warumi 13:1, Waefeso 6:5-8, Waebrania 13:17, 1 Petro 5:5). Kwa kiwango kile cha unyenyekevu wa mume wake kwa Mungu, mwanamke atakuwa amelindwa na kubarikiwa.
► Je, kati ya sifa zilizoorodheshwa hapo juu, ni sifa zipi zinazoonekana kuwa za muhimu sana kwako? Je, umeshawahi kuona mifano gani inayoonyesha umuhimu wa tabia hizi?
Mwanamume na mwanamke hawapaswi kuingia kwenye ndoa na mwingine hadi kila mmoja aseme kwa moyo safi kwamba, “Nitaweza kuwa na uwezo wa kumtumikia Mungu vizuri zaidi nikiwa niko ndani ya ndoa na wewe kuliko mimi kubakia kuwa mseja.”
Ndoa zinazoandaliwa na Wazazi
Kwenye tamaduni nyingi, ni jambo la kawaida kwa wazazi kuandaa shughuli ya ndoa kwa ajili ya watoto wao. Kwa mfano, kwenye nchi moja kubwa, wazazi hutafuta mwenzi wa ndoa kwa ajili ya watoto wao na kufanya mazungumzo na wazazi wa upande wa pili. Kwa kawaida wao hupanga jinsi ya mtoto wa kiume na wa kike watakavyoweza kukutana. Watoto hawa wanaweza wakawa wakikutana labda mara moja, mbili au tatu, kabla ya kufanya maamuzi ya kuingia kwenye ndoa. Watoto wa kike wanaweza kuruhusiwa kuchagua ikiwa kama watakubaliana na chaguo la wazazi, lakini huwa hawapati muda wa kufahamiana vizuri.
Wazazi walio Wakristo kwenye tamaduni hizi wanapaswa wafuate maadili ya kibiblia wanapokuwa wanatafuta wenzi watarajiwa kwa watoto wao. Wanapaswa kuwatafuta wenzi wacha Mungu, wenye hekima, na waliokomaa kwa ajili ya watoto wao. Wanapaswa kutafuta watu binafsi ambao wanakuwa wamemweka Mungu kama kipaumbele kwenye maisha yao. Mambo haya yote yanatakiwa yawe ni kichocheo kikubwa zaidi kwa wazazi katika kuwachagulia wenzi watoto wao na siyo zaidi sana kwenye elimu ya mtu, hadhi yake katika jamii, au kiwango chake cha fedha.
Ndoa za Kujitegemea
Hekima kwa wazazi na Watoto wazima Wanaochagua Wenzi wao.
Kwenye jamii na tamaduni nyingi, zikiwemo za Ulaya na Marekani ya Kaskazini, ni jambo la kawaida kwa vijana kuchagua wenzi wao wa ndoa bila ya kupata mwongozo mwingi kutoka kwa wazazi wao.
Wazazi Wakristo walio katika tamaduni hizi wanaweza wakajihisi kwamba wana ushawishi mdogo sana kwenye maamuzi ya harusi ambayo hufanywa na vijana wao waliokomaa. Wazazi wanaweza wakajihisi kwamba hawapaswi kupinga hata kama hawajamthibitisha mtu ambaye mtoto wao amedhamiria kwa ajili ya kufunga naye ndoa. Huenda wakahofu kwamba ukosoaji unaweza kuleta matatizo ya mahusiano kwa mtoto wao na kwa mkwe wao katika siku za baadaye.
Ingawa wazazi Wakristo hawawezi kupanga ndoa moja kwa moja kwa watoto wao, wanapaswa kuwa na mchango wa kuelekeza au kushawishi uchaguzi wa mwenzi wa maisha. Wazazi wanapaswa wazungumze kuhusu mambo haya na watoto wao wakati wakiwa bado wadogo. Wazazi kwa makusudi wanapaswa watengeneze mawazo ya kufikiri na maadili ya watoto wao. (Kumbukumbu la Torati 6:5-9). Je, wewe kama mzazi unawezaje kufanya hili?
1. Kuwa mfano mzuri wa mwenzi na mzazi mcha Mungu. Isipokuwa uwe ni mfuatiliaji wa kanuni za Mungu katika maisha yako mwenyewe, maagizo yako ya maneno tu kwa watoto wako hayatakuwa na maana yeyote. Kama mfano wako haulingani na kile unachokisema, watoto wako watasikiliza mfano wako tu badala ya maneno yako.
2. Fanya msisitizo wa viwango vya kimungu kwa kusudi la maisha, kusudi na maana ya ndoa, na ni nini kitazamiwe kutoka kwa mwenzi wa ndoa (Zaburi 34:11-12). Wakati tunapokuwa tunatazama, tunasikiliza, na kuangalia kanuni za kidunia, tunakuwa tunawafundisha watoto wetu kwamba dunia ndiyo kielelezo chetu badala ya Neno la Mungu kuwa kielelezo chetu, Badala ya kufanya hivyo, tunapaswa tustawishe matamanio ya kimungu ndani ya watoto wetu kwa kuwadhihirishia watu/kuvuta nadhari ya watu ambao wanafuata mipango ya Mungu iliyo mizuri. Tunatakiwa tuonyeshe matokeo mazuri ambayo watu hawa wanayafurahia kwa sababu ya utii wao kwa Mungu.
3. Wafundishe watoto wako kwamba tabia ni kitu cha kujali na kuzingatia sana kuliko kitu kingine chochote wakati wa kuchagua mwenzi. Kuanzia wakati wangali watoto wadogo, wafundishe watoto wako kutazama kwa ajili ya thamani ya tabia njema kutoka kwa watu wengine, zaidi ya miili ya kuvutia au haiba. Wafundishe kutambua kama wenzao walio nao ni wanaowajibika au kama ni wavivu, watiifu au ni waasi, waaminifu au ni wadanganyifu. Wafundishe jinsi ya kujitunza zaidi na tabia zao wenyewe kuliko jinsi ya kutunza mionekano yao.
Ikiwa kama wazazi wanataka watoto wao wawatambue wakati wanapokuwa wanachagua wapenzi wao wakiwa vijana wakubwa, wanapaswa wawafundishe watoto wao wakiwa wadogo kwamba kuwasikiliza baba na mama ni jambo la busara sana! (Mithali 1:8.). Kwenye ujana au utu uzima ni kuchelewa sana kufundisha jambo hili; wazazi ni lazima wafundishe jambo hili wakati watoto wao wangali wakiwa bado wadogo (Mithali 4:3-9). Kuwasikiliza wazazi wenye kumcha Mungu ni njia ya Mungu kwa ajili ya watoto kupata ulinzi na baraka.
Kama ilivyojadiliwa katika Somo la 4, wazazi wana wajibu wa kuwasaidia vijana wao wadogo kuyaendesha mahusiano yao kwa usafi wa maadili mema. Ili kufanya hivi, unapaswa tayari uwe una uhusiano mzuri na wa wazi na mtoto wako, ambao unawafanya wawajibike kwa hiari kwako na kukubaliana na ushauri wako. Aina hii ya uhusiano inajengewa msingi wake kwenye miaka ya mwanzo ya utoto unapowafundisha kwa bidii, kuwafanyia mazoezi, kuwaongoza, na kila siku kuwaweka kwenye hali ya nidhamu.
Hekima kwa ajili ya Kijana Anayechagua Mwenzi Mtarajiwa
Mungu anayo hekima kwa ajili ya vijana waliookoka ambao ni lazima wafanye maamuzi yao wenyewe kuhusiana na ndoa. Hapa kuna ushauri mdogo wa hekima kwa ajili ya kufanya maamuzi mazuri:
(1) Kataa uchaguzi wowote usiokuwa wa kibiblia
Kwa mfano, tunajua kwamba siyo mapenzi ya Mungu kwa watu waliookoka kufunga ndoa na watu wasiookoka, kwa hiyo hatupaswi hata kufikiria kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye hajaokoka.
(2) Omba kwa ajili ya kupewa hekima (Mithali 2; Yakobo 3:13, 17).
Wakati tunapokuwa tunatafuta kumwelewa Mungu kwa moyo wetu wote, anafurahishwa kutupatia sisi hekima. Hekima inapatikana kwa kujifunza kwa uangalifu na kutii Neno la Mungu. Mungu pia hutupa sisi hekima kupitia ushauri wa watu wanaomcha Mungu. Kukubaliana na hekima ya Mungu hutulinda sisi dhidi ya dhambi na madhara. Hekima yake hutupa sisi baraka zake, na hutupa fursa ya kupata uzoefu wa mpango bora kwa ajili ya maisha yetu. Jambo la muhimu zaidi ni kwamba tunapofanya maamuzi ya hekima, tunamtukuza Baba yetu wa mbinguni.
Kamwe, Roho Mtakatifu hatakaa atuongoze sisi katika kutotii Neno la Mungu. Badala yake, anatukumbusha kwa uaminifu (Yohana 14:26, Yohana 16:13-14). Anawalinda watoto watiifu wa Mungu wa Mungu kutokana na dhambi na kuwazawadia maisha na amani (Warumi 8:5-6, 13-14; Wagalatia 5:16, 22-25). Huenda siku zote usijue kwa undani mapenzi ya Mungu katika kila hali, lakini unapaswa kufuata kile ambacho unakijua kwa uhakika. Unajua kwamba Mungu anakutaka wewe mwenyewe uwe mwaminifu kiroho na kimaadili. Unajua kwamba Mungu anakutaka wewe uepukane na vitu fulani na ufuate vitu fulani. Fanya kile ambacho unajua ni sahihi wakati huo ukiomba kwa ajili ya kupata mwelekeo/mwongozo wa Mungu.
(4) Kuwa makini sana na ushauri unaotoka kwa watu wanaomcha Mungu.
Vijana wenye wazazi wao wanaomcha Mungu wanapaswa watafute hekima yao. Wanapaswa wawe wazi na waaminifu kwa wazazi wao kuhusiana na wanavyofikiria katika masuala yao ya ndoa. Wanapaswa wazingatie kwa umakini wa karibu mahangaiko yoyote ambayo wazazi wao wanakuwa wanayo. Mungu amewapa wazazi wao ili wawalinde dhidi ya madhara yeyote na kuwatendea mema. Vijana wanapaswa wasipoteze fursa za kubarikiwa kupitia njia hizi.
Vijana wengi wa Kikristo hawana mawaidha wanayopokea kutoka kwa familia zenye umri mkubwa katika kumcha Mungu. Kwa hakika wanapaswa wapokee ushauri kutoka kwenye familia zenye tabia za kimungu ambazo zimeonyesha uwezo wa kufanya maamuzi yenye hekima na matokeo yakawa yanakuwa mazuri.
Hata hivyo, vijana hawapaswi kudharau kupokea mawaidha kutoka kwa wazazi wao, hata ikiwa kwamba wazazi wao siyo watu wanaomtumikia Bwana. Inawezekana kukawepo na baadhi ya matukio ambapo kijana anatakiwa kwenda kinyume na matakwa ya wazazi wake ambao hawajaokoka/hawajaamini ili kumtii Mungu, lakini jambo hili kamwe halipaswi lifanyike kwa kuasi (1 Samuel 15:23) au kukosa heshima (Kutoka 20:12). Bila kujali wazazi wamekaaje kwa Mungu, Mungu ana uwezo wote wa kulainisha mioyo yao ili waweze kuwa ni baraka kwenye ndoa ya mtoto wao wa kiume au wa kike. Kuomba pamoja na kumngojea Bwana abadilishe mioyo ya wazazi wao kutapima na kuimarisha imani ya huyu mtoto wa kiume au wa kike.
► Jadili kanuni au mifano kutoka katika maandiko kuhusu ushiriki wa wazazi katika maamuzi ya ndoa. Je, wazazi wanapaswa wafanye nini ili kushawishi mchakato wa kuchagua mwenzi? Je, mtazamo wa kijana mtu mzima aliye Mkristo dhidi ya wazazi wake unapaswa uweje kwenye maamuzi ya ndoa?
Urafiki wa Wanandoa watarajiwa kabla ya Ndoa
Ikiwa uwepo wa kipindi cha uchumba ni jambo linalowezekana, ni bora zaidi kwa mwanamume na mwanamke kuutumia muda wake dhidi ya mwenzake katika mazingira mbalimbali tofauti. Hali hii inawawezesha kila mmoja kujua mwenzake ana tabia gani, anawasilianaje na watu wengine, anavyowajibika katika hali zinazojitokeza zisizotarajiwa, na jinsi anavyoitikia katika hali mbalimbali ambazo hazikutegemewa. Katika wakati huu kwa pamoja, kunaweza kuwasaidia kuelewa kama watakuwa wenzi wa ndoa wanaofaa.
Msimamo wa Usafi
► Wanafunzi wanapaswa wasome 1 Wathesalonike 4:1-8 na 2 Timotheo 2:19-22 kwa ajili ya kikundi.
Kwa upendo Mungu aliwaumba wanaume na wanawake wakiwa na matamanio na uwezo kwa ajili ya kuwa na vitendo vya kimwili kimapenzi na mihemuko. Kwa sababu ya haya matamanio, marafiki ambao wanatafuta kufunga ndoa wakati ujao lazima wawe waangalifu kwenye mahusiano yao wenyewe. Mungu anakusudia matamanio haya yakamilishwe ndani ya agano la kipekee la maisha yote ya ndoa.
Kama mwanamume na mwanamke kwa makusudi hawatajihusisha wenyewe katika uangalifu na usafi, kuna uwezekano kwamba wataacha kumtii Mungu kwa kufuata hisia zao wakati wa kipindi cha majaribu. Kutotii matakwa ya Mungu ya usafi wa kimaadili kunaumiza kwa njia nyingi na huathiri sana watu wengi, siyo tu kwa mwanamume na mwanamke peke yao. Kutotii matakwa ya Mungu kwa ajili ya usafi wa kimaadili kunasababisha majuto, hali ya kufungwa, kujisikia hatia, aibu, woga, kutoaminiana, na kuvunjika kwa mahusiano.
[1]Kuna baraka nyingi kwa wale wanaofuata mpango wa Mungu wa usafi wa kimaadili. Wale ambao wanamheshimu Mungu kupitia utii wanaweza kupata kila lililo jema ambalo amekusudia kwa ajili yao. Badala ya madhara ya kutotii kwa kukosa utiifu, watakuwa na furaha na amani. Watakuwa na uwezo wa kila mmoja kumwamini mwenzake. Watakuwa na uwezo wa uhusiano wenye kustawi na Mungu pamoja na wao wenyewe.
Baraka hizi ni motisha wenye nguvu sana kwa ajili ya kuufuata mpango wa Mungu wa kwa ajili ya usafi wa kimaadili. Hata hivyo, motisha mkubwa zaidi kwa mtu aliyeokoka kwa ajili ya uangalifu katika eneo hili inapaswa iwe ni matamanio yao ya kumletea Bwana Yesu heshima kwenye kila eneo la maisha. Wenzi walioko kwenye uchumba wanapaswa wawe wanajiuliza, ‘Je, tunawezaje kumheshimu Mungu vizuri zaidi kwenye uhusiano wetu? Je, tunawezaje kumletea Yesu utukufu zaidi?”
[2]Ili kuepuka matendo yasiyokuwa masafi, wenzi walio wachumba wanapaswa wawe na tahadhari kutokana na ongezeko lolote la uhusiano wa kimwili linalojitokeza kati yao. Wanapaswa waepuke vipindi virefu vya kukaa peke yao kwenye maeneo ambayo wanadhania kwamba hakuna mtu mwingine atakayejua watakachofanya. Wanandoa hushindana na majaribu wakati kugusana kimwili kunapotokea kuwa ni muhimu katika mahusiano yao kuliko mawasiliano. Wanaweza wakashindwa kushughulika ipasavyo na masuala ya kiroho na kimahusiano kwa sababu fahamu zao na mioyo yao inakuwa imeshamiri matamanio ya kimwili. Mwanzoni mwa mahusiano, wote kwa pamoja fanyeni maamuzi kuhusu ni mambo gani mahususi mtayafanya (na yale ambayo hamtayafanya) kwenye mahusiano yenu kabla ya ndoa. Mipango yenu inapaswa iweze kumlinda kila mmoja dhidi ya kutenda dhambi, ikusaidie kuwapenda wenzi wako wa baadaye, na kukuwezesha kumheshimu Mungu. Jikabidhini kabisa ninyi wenyewe kwenye mpango wenu. Wajibika kwa washauri wacha Mungu na sikiliza ushauri wao na maonyo yao. Kwa pamoja tumieni muda wenu katika kushirikiana na marafiki wanaomcha Mungu na wanafamilia.
Shughuli Zinazokuza Ukuaji
Kwenye uchumba ndiyo wakati wa kufahamiana, lakini unapaswa pia kunatakiwa kuwepo na muda wa kukua. Yafuatayo hapa ni baadhi ya mawazo kuhusu shughuli za kufanya ambazo wachumba wanaweza kufanya kwa pamoja:
Shughulika na kazi za miradi.
Jifunzeni ujuzi ambao ni mpya kwenu ninyi wote wawili.
Soma na jadili vitabu vyenye maana.
Jifunze au kariri vifungu sawa vya maandiko, kisha vijadili.
Pangeni na kuendesha shughuli za huduma kwa pamoja.
Kuweni walezi wa watoto kwa pamoja.
Tumieni sehemu ya muda wenu kwa ajili ya kukaa na familia ya kila upande.
Shughuli hizi zitakuwa na matokeo yafuatayo:
Zitasaidia katika kufahamiana zaidi kwa mwanamume na mwanamke.
Zitawasaidia kujua kama wao ni wenzi wanaofaa mmoja kwa mwenzake.
Kuongeza uwezo wa kila mmoja kuwasiliana na mwenzake.
Kutawasaidia kukua.
► Je, ni kanuni na mawazo gani ya uchumba ambayo ni mapya kwako? Je, ni kwa jinsi gani watu waliookoka/waumini katika muktadha wako wanavyoweza kutumia kanuni kibiblia kwa ajili ya usafi wa kimaadili na kumheshimu Mungu katika mahusiano kabla ya ndoa?
Mada za Kujadili kabla ya Ndoa
Kwenye tamaduni ambapo wanandoa hufahamiana kama sehemu ya mchakato wa kufanya maamuzi, kuna masuala ambayo yanapaswa yajadiliwe kabla ya harusi kufanyika.
Kwenye tamaduni kadhaa, mipango ya ndoa hairuhusu mazungumzo hayo ya kina kabla ya harusi. Ili kuwepo na ukamilifu wazazi wa pande zote hushirikishana taarifa kuhakikisha kwamba vijana wao wanandoa wanaendana vizuri kwa pamoja.
Katika hali nyingine ambazo mwanandoa mmoja anafunga ndoa akiwa anamfahamu mwenzake kwa sehemu kidogo sana, wanatakiwa wayafanyie kazi masuala haya baada ya kuwa wameoana tayari, lakini masuala haya hayawezi kubatilisha chaguo lao kwa sababu kila mmoja tayari alishaweka ahadi kwa mwenzake pamoja na Bwana.
Kadiri mwanamume na mwanamke wanavyofanana katika imani, asili, utamaduni, malengo ya maisha, na maadili, ndivyo wanavyoweza kuwa sambamba zaidi katika ndoa. Ikiwezekana, wanandoa wanaofikiria kufunga ndoa wanapaswa kutumia muda kujadil:
Malengo yao ya maisha
Maadili ambayo ni muhimu kwa kila mmoja
Utoto wao wenyewe na jinsi walivyolelewa
Mahusiano yao na wazazi wao na jamaa wengine
Mafundisho binafsi ya imani na desturi za imani, kama vile nidhamu binafsi za kiroho, kuhudhuria ibada za kanisa, matendo ya kuhudumu na huduma
Uelewa wao na imani yao kuhusiana na mambo mengi ya kulea watoto, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha, kuwaweka watoto katika nidhamu, na kuwafundisha kumjua na kumtii Kristo
Maoni yao kuhusu fedha, ikiwa ni pamoja na matumizi, na kuishi katika nyakati ngumu za matatizo
Uwepo wowote wa matatizo yeyote ya kimwili au kiakili au ulemavu wowote walio nao, na matatizo ya kiafya ambayo ni ya kawaida kwenye familia zao
Katika sehemu hii ya uhusiano, utapaswa kuzungumzia juu ya matatizo katika maisha na mada za maisha magumu. Mkishaweka ahadi zenu kwa Mungu na kila mmoja na mwenzake, mnakuwa mmeoana kwa ajili ya mema au mabaya. Katika ndoa, mume na mke hushirikishana yote jinsi walivyo na yote waliyo nayo kila mmoja, kwa hiyo mawasiliano ya uaminifu kuelekea kwenye ndoa ni ya muhimu sana. Mawasiliano yanapaswa kuzidi kuwa ya wazi na ya kina. Ikiwa mtu unayetaka kuwa kwenye ndoa na mwenzake hayuko tayari kuwa wazi kuzungumza kuhusiana na mambo muhimu yanayowahusu, hiyo ni ishara ya hatari sana.
Muda mfupi kabla ya kufanyika kwa harusi yao, wanandoa wanapaswa wajadili mambo yanayohusiana na imani zao, matarajio yao, na matamanio yao kuhusiana na mahusiano au kujamiiana wakiwa ndani ya ndoa. Kujadili mapema mambo ya kujamiiana wakati wa mahusiano kunaweza kusababisha majaribu yasiyo ya lazima, lakini ni muhimu kuyazungumzia muda mfupi kuelekea ndoa kufungwa.
Mambo ya msaada kwa mwanamume na mwanamke wanaoingia kwenye ndoa:
Kufanana kiakili
Kuwa na matarajio yanayofanana katika maisha ya ndoa
Kuwa na mafundisho ya imani na mazoea ya kiroho yanayofanana
Kuwa na maadili na mazoea yanayofanana kwa ajili ya matumizi ya fedha na muda
Kuwa na ushirikishwaji na uelewa wa kina wa maisha na ukuzaji wa watoto
Ishara za Hatari katika Uchumba
John Drescher anaorodheha matatizo manane ambayo yanaweza kusababisha mwanamume au mwanamke kufikiria kwa dhati kukatisha kabisa uhusiano wa uchumba:[3]
1. Wewe na rafiki yako mmekuwa na hali ya kuzozana mara kwa mara.
2. Unakwepa kujadili wewe na mwenzako mambo yaliyo nyeti kisa tu kwa sababu una wasiwasi wa kumwumiza mwenzako kimhemuko. Kama utajiambia mwenyewe, “Ni bora zaidi nisizungumze lolote kuhusiana na jambo hili” – hii ni alama ya hatari. Ndoa ni kumaanisha kwamba unawajibika kujadili mambo mengi kwa ujasiri na upendo.
3. Uhusiano wako unaongezeka kuwa wa kimwili zaidi. Kadri mtakavyokuwa mnaendelea kuhusika zaidi kimwili mkiwa ni wenzi ambao bado hamjafunga ndoa, mtajifunza kwa kiwango kidogo sana kuwasiliana kwa maneno, sauti, sura ya uso, na lugha ya mwili. Kugusa mwili zaidi na kuzungumza kidogo kunaweza kuwa ishara halisi ya hatari.
4. Ikiwa unahisi kwamba uko kwenye uhusiano kwa sababu ya hofu ya aina fulani. Kwa mfano, “Ninataka nisitishe uhusiano, lakini nachelea nisije nikamkwaza mtu yeyote.”
5. Kama rafiki yako hayuko tayari kukubaliana na lawama. Je, rafiki yako anapokosea, huwa anakataa kuomba msamaha? Huo ni uharibifu kwa sasa, na utakuwa ni uharibifu mbaya zaidi baadaye, endapo mtaoana.
6. Kama wazazi na marafiki wako muhimu watakuwa na upinzani kuhusu uhusiano wako na uwezekano wa kuwepo kwa ndoa. Hii kwa hakika inaweza kuwa ni ishara ya hatari ambayo itakulazimu wewe ufikirie kusitisha uhusiano. Ni kweli kwamba hauingii kwenye ndoa na mtu tu, bali unaingia kwenye familia ambayo itakuwa na athari kwenye usalama na mafanikio ya ndoa yako.
7. Rafiki yako ni mtu wa wivu mwingi unaopitiliza au wa kutilia mashaka. Kwa mfano, kama rafiki atakuwa anahoji sana maneno yako, au kwa maneno mengine ni kwamba hakuamini, hii ni ishara ya hatari. Kwa hiyo, sitisha uhusiano wako wakati unapokuwa ungali unajimudu kama rafiki yako ni mwenye wivu wa kupitiliza na asiyekuamini.
8. Kama hisia zako hazikufanyi kujisikia kuwa na amani ya moyoni kuhusiana na uhusiano wako. Hali hii itatokea wakati hasa unapokuwa uko peke yako na rafiki yako. Unajikuta una mawazo au maono kwamba, “Jambo fulani ni baya.” Kuwa makini na hali hiyo ya ukosefu wa amani ya moyo!
Kujidhibiti kwako kwa leo ni zawadi kwa mwenzi wako wa baadaye. Mwenzi wako atajihisi kuwa anayelindwa na kuheshimiwa kwa sababu ya uchaguzi wako wa kumtii Mungu. Mwenzi wako atajihisi kuwa anayependwa sana.
[3]Nukuu kutoka kwa John Drescher, For Better, For Worse: A Premarital Checklist, (Morgantown, PA: Masthof Press, 1999), 30-31.
Hitimisho
Mithali 24:3-4, “Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika, Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.”
Chaguo la mwenzi ni moja ya chaguzi muhimu sana katika maisha ambazo mtu anaweza akafanya. Mungu anapenda kusaidia watoto wake kufanya chaguzi za busara wanatafakari na kutaka kuzoeana na wenzi watarajiwa.
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Je, ni maudhui gani mapya kwako ambayo umeyapata kutoka katika somo hili? Je, kwa nini yamekuwa ni muhimu kwako? Je, kuyaelewa maudhui haya kutakusaidiaje katika mahusiano yako? Je, kwa kuyaelewa vizuri haya maudhui kutaathiri vipi huduma yako kwa watu wengine?
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kutuongoza na kuwa mtoaji kwa ajili yetu sisi. Asante kwa ajili ya kanuni zako ambazo umetupa sisi kupitia katika Neno lako ambalo linatusaidia sisi katika kufanya chaguzi za busara kuhusu maamuzi muhimu katika maisha yetu.
Tunakuomba utusaidie sisi kuwa na vipaumbele vyako tunapokuwa tunachagua wenzi wetu. Tusaidie katika kuwa wanaume na wanawake unaoututaka sisi tuwe. Tusaidie tuwe wanyenyekevu na wenye kusikiliza ushauri wa watu wanaomcha Mungu.
Tunataka tuishi maisha ya utakatifu, yenye kuzaa matunda ambayo yatakuletea wewe heshima.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Chagua sehemu yeyote kutoka katika somo hili ambalo utafundisha kwa muktadha wa huduma yako. Unaweza ukawa unamfundisha mtu mmoja au kikundi cha vijana. Mjulishe kiongozi wako wa darasa utakapokuwa umemaliza huduma ya kufundisha nje ya darasa.
(2) Kwa maandishi, elezea tabia za uhusiano wa mwanamume na mwanamke wanaomcha Mungu kutoka kwenye utamaduni wenu ambao bado wanatafakari kuhusu kuingia kwenye ndoa au ambao tayari wamepanga kuingia kwenye ndoa.
(3) Aidha uwe uko kwenye ndoa au laa, fanya marejeo ya orodha iliyotolewa kuhusu sifa za kuzingatia wakati wa kumchagua mwenzi muhimu. Soma kila andiko lililoandikwa kwa ajili ya kufanya marejeo. Mwombe Mungu akusaidie kukuonyesha ni kwa jinsi gani unapaswa kukua.
(4) Kama wewe ni mseja na una mpango wa kuingia kwenye ndoa wakati fulani ujao, tengeneza orodha yenye kuelezea ni mambo gani unayotaka uyaone kwa mwenzi wako mtarajiwa. Hautahitajika kumshirikisha jambo hili kiongozi wako wa darasa, lakini mtaarifu tu kwamba umeshamaliza kuifanya kazi iliyotolewa.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.