Stefano na Sara walikuwa wakijaribu kutambua kama ndoa yao ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa ajili yao. Sara alitambua kwamba kama ataolewa na Stefano – ambaye alikuwa mmishenari – maisha yake yangebadilika kwa namna na njia nyingi. Angehamia nchi nyingine, angejifunza lugha mpya, na angejizoeza kuwa kwenye utamaduni mpya. Alijua kwamba angepaswa kuachana na kile alichokuwa amekizoea na kuridhika nacho. Itabidi kuwepo na mambo ya kufadhaisha na ya kujitoa dhabihu. Ndoa ingekuwa tu siyo ahadi ya upendo kwa mume wake, bali tendo la imani na upendo kwa ajili ya Yesu.
Baada ya kitambo kidogo, Stefano na Sara walitambua kwamba hawakuwa wakiendana sawia, na kwamba hawakupaswa kuoana. Sara alijihisi kukata tamaa.
Aliomba kuhusu kukatishwa kwake na tamaa. Aliomba kwamba Mungu amsaidie ili azae matunda kwa ajili yake kwenye kipindi hiki cha maisha yake. Alipokuwa akiomba, alijitambua kwamba kujisalimisha huku kwenye mapenzi ya Mungu kulikuwa tu kitendo cha imani na upendo kwa Yesu kama ambavyo ndoa ingepaswa iwe.
Useja
Katika kozi hii tunatafiti mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa. Kutoka katika maandiko tunajifunza kuhusu makusudi ya Mungu kwa ajili ya ndoa. Tunajadili maelekezo ya Mungu kwa ajili ya ndoa na njia za vitendo za kuimarisha ndoa zetu. Tunauona uzuri wa mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa.
Kwa watu walio wengi, ndoa ni mapenzi ya Mungu. Lakini watu wengi huishi kwa miaka kadhaa kama waseja kabla ya ndoa. Wakati mwingine huu muda wa kuishi kiseja unakuwa ni mrefu sana. Baadhi ya watu hupitia tena kwenye kipindi kingine cha useja baada ya kifo cha mwenzi wao au baada ya kupeana talaka. Watu wengine huamua kukaa bila ndoa kabisa.
Mtu anaweza akawa hana ndoa kwa sababu moja au zaidi ya hizi zifuatazo:
Wanapendelea manufaa ya kuwa waseja badala ya kuwa kwenye ndoa.
Wana wasiwasi kuhusu ndoa kwa sababu hawajawahi tena kuona mahusiano mazuri ya ndoa.
Kwa sasa wanajielekeza katika malengo ya elimu au taaluma nyingine.
Hawajihisi hitaji la kimwili kwa ajili ya ndoa.
Hawajawahi kupata fursa kwa ajili ya ndoa nzuri.
Kwa kuwa chaguzi za mseja zinaathiri sana uhusiano wa Mungu na watu wengine, somo hili litajielekeza kwenye maisha ya mtu aliyeokoka/mwamini ambaye hana kabisa ndoa.
Walichokisema Yesu na Paulo kuhusu Useja
Mafarisayo walimwuliza Yesu swali lililohusiana na talaka. Baada ya kuwa wamelisikia jibu la Yesu, wanafunzi wake wakaishia kusema haifai kuoa (Mathayo 19:10). Yesu ambaye hakuwahi kuoa na alikuwa mseja katika maisha yake yote hapa duniani, akajibu kwamba, watu wengi wanahitaji kuoa na wachache tu ndio waliojaliwa uwezo wa kukubali kuishi katika useja wa muda mrefu (Mathayo 19:11-12).
Mtume Paulo – ambaye aidha alikuwa hajaoa kabisa au pengine alikuwa mgane – alikuwa na ushauri unaofanana kwa watu waliookoka ambao walikuwa hawana ndoa katika mji wa Korintho. Kwa sababu ya jaribu la zinaa, watu wengi wanapaswa kuoa (1 Wakorintho 7:2, 8-9). Paulo alijua kwamba Mungu alikuwa ameumba uhusiano wa ngono katika ndoa ili iwe zawadi nzuri (1 Wakorintho 7:7, 1 Timotheo 4:1-5, Waebrania 13:4). Alisema kwamba tendo la kujamiiana halipaswi lifanyike nje ya ndoa (1 Wathesalonike 4:3-4).
Paulo alielezea faida ya maisha ya kutokuwa na ndoa. watu waliookoka/waumini wanaweza wakaelekeza muda wao, nguvu zao, na jitihada zao katika kumpendeza Bwana na kuhudumu katika huduma (1 Wakorintho 7:32-35).
Paulo alibakia bila kuoa (1 Wakorintho 9:5). Alichagua kubakia hivyo ili kwamba aweze kuelekeza muda wake kwenye kazi ya umishenari ambayo Mungu alikuwa ameiweka kwa ajili yake. Yeye aliuchukulia useja kama zawadi (1 Wakorintho 7:7-8). Alivumilia mateso mengi katika huduma yake (2 Wakorintho 11:23-28). Mateso yake haya yalikuwa ni rahisi kukabiliana nayo kwa sababu hakuwa na wajibu wa mke au watoto (1 Timotheo 5:8).
Ingawaje Paulo alichukulia kwamba useja ulikuwa ni faida kwa ajili ya huduma yake, kuna pia njia nyingine ambazo ndoa inakuwa ni faida zaidi kwa ajili ya huduma.
► Je, umeuonaje useja kama faida kwa ajili ya huduma? Je, umeshaona kwamba ndoa ni faida kwa ajili ya huduma?
Paulo alisema kwamba watu wanapaswa kuzingatia mambo kadhaa wanapokuwa wanaamua aidha waingie kwenye ndoa au la:
Uwezo wao binafsi wa kuweza kuishi au kutoweza kuishi kwenye useja (1 Wakorintho 7:9, 36-37)
Mazingira magumu ya sasa, kama vile mateso (1 Wakorintho 7:26)
Majukumu ya ndoa (1 Wakorintho 7:27-28, 32-35)
Vipaumbele Sahihi
Si useja wala ndoa ambapo kimoja ni bora au cha kiroho zaidi kuliko kingine. Kuna majaribu ya kipekee, matatizo, baraka, na nafasi kwenye kila kimoja. Kila kimoja kinafaa kwa nyakati tofauti na kwa watu tofauti.
Hatimaye, utimilifu na ukamilifu wa binafsi ni lazima utokane na uhusiano wa mtu na Mungu, aidha kama mtu ana ndoa au laa (Zaburi 73:25, Zaburi 107:8-9). Zaidi ya hayo watu wote waliookoka/waumini – wenye ndoa na wasiokuwa na ndoa – ni lazima waweke mwelekeo wao kwenye umilele kwa sababu maisha ni mafupi, na umilele ni hakika (1 Wakorintho 7:31).
► Mwanafunzi anapaswa asome Mathayo 6:26-33 kwa ajili ya kikundi.
Kwenye kifungu hiki, Yesu anaelezea kwamba maadili na vipaumbele vya dunia ni tofauti sana na vile vya watu waliookoka. Lengo kuu la watu waliookoka ni kuwa washiriki kwenye ufalme wa Mungu. Kipaumbele kikuu cha kwanza kwa watu waliookoka ni kuishi maisha ya haki kwa neema ya Mungu. Mungu anaahidi kutoa mahitaji kwa ajili ya mwili na haja nyinginezo za watoto wake wakati wanapokuwa wanayatii maneno ya Yesu katika Mathayo 6:33.
Je, ni wakati gani mwanamume Mkristo anapaswa kuoa? Ni wakati ndoa itakapokuwa inamsaidia zaidi kutumikia ufalme wa Mungu. Ni wakati ndoa itakapomsaidia kuishi maisha ya uadilifu, yenye matunda yenye ushindi.
Je, ni wakati gani mwanamume Mkristo anapaswa kubakia katika useja? Ni wakati harakati za kufunga ndoa au ndoa yenyewe inapomkengeusha atoke kwenye nafasi yake katika ufalme wa Mungu. Ni wakati atakapoweza kuzaa matunda zaidi kiroho akiwa kama mseja. Ni wakati anapoweza kuwa mshindi wa kiroho na kudumisha usafi wa kimaadili bila ya kuwa na urafiki wa kujamiiana unaotolewa katika ndoa.
► Kama wewe bado huna ndoa, tulia kwa ajili ya muda wa kutafakari kwa uaminifu:
Je, unaishi kwa utii kulingana na Neno la Mungu?
Je, Mungu amekupa nini cha kufanya kwenye ufalme wake kwa sasa hivi?
Je, unadhani Mungu amekuitia ufanye nini na maisha yako ya muda mrefu?
Je, unadhani ndoa itaweza kukufanya ufanye vizuri au vibaya kwenye uhusiano wako na Mungu na kazi yako kwa ajili ya Mungu hapa duniani?
Kukubalina na vipaumbele vya Mungu kunawasaidia waumini ambao bado hawajaingia kwenye ndoa kuamua aidha waendelee au wasiendelee na mipango ya ndoa. Pia huimarisha ufahamu wetu wa kile tunachotakiwa kukiangalia katika kutafuta mwenzi muhimu. Kila mtu aliyeokoka aliye na matamanio ya kuwa kwenye ndoa, anapaswa amtafute mwenzi ambaye anamtanguliza Mungu kwanza, anayeishi kwa kulitii Neno la Mungu, na anayetafuta kuundeleza ufalme wa Mungu.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Waefeso 4:17-24 na 1 Yohana 2:15-17 kwa ajili ya kikundi.
Watu wa dunia huishi kwa ajili ya ubinafsi. Wanachagua kufanya yale mambo ambayo miili yao na akili zinataka (Waefeso 2:3), na wako tayari kutokulitii Neno la Mungu. Watenda dhambi mara nyingi huwa wanafanya kile ambacho wanakiona kwao kwamba ni kizuri, kinawafaa, au kitawafanya watu wengine wawe makini kuwaangalia. Kipaumbele chao muhimu ni kujifurahisha wenyewe. Wanaweza wakajenga mahusiano ya kimapenzi na mtu mwingine kwa sababu tu kimwili wanamvutia huyo mtu. Wanaweza wakawa kwenye mahusiano na mtu mwingine kwa sababu tu wana hisia zinazowaka wakati ule wanapokuwa wako na yule mtu.
Watu wenye ubinafsi hawatapenda kujitoa kabisa katika uhusiano wa kujiachilia kwa mwingine wa ndoa. Wanaweza wakawa tayari kuwa na mahusiano ya kufanya ngono bila ya ndoa ingawaje Mungu anasema kwamba mahusiano kama hayo ni uovu (1 Wakorintho 6:9-11).
Watu wenye ubinafsi wanaofunga ndoa wanaweza kukata tamaa kwa mwenzi wake wa ndoa wakati ndoa inapokuwa ngumu. Wanaweza kuachana na mwenzi wa ndoa na kuendelea katika mahusiano na mtu mwingine. Mungu analo jambo lililo bora zaidi kwa ajili ya wale watakaotii maelekezo ya Neno lake (Zaburi 19:8, 11, Kumbukumbu la Torati 6:24).
Yesu anatuita ili tumpendeze Mungu katika kila jambo (Mathayo 16:24, 2 Wakorintho 5:9, Wakolosai 1:10). Kwa kuwa sisi ni wafuasi wa Kristo, kipaumbele cha maisha yetu ya binafsi ni lazima kiwe ufalme wa Mungu na haki. Zaidi ya hayo kipaumbele katika harakati zetu za kufunga ndoa ni lazima ziwe ufalme wa Mungu na haki yake. Ni lazima tumsikilize Yesu kuhusiana na maadili yake na kutii yale ambayo anasema ni sahihi na mazuri. Kisha ni lazima tumheshimu Mungu kwa kutii matazamio aliyo nayo kwetu kama waume na wake.
Kwa Kila Jambo Kuna Wakati Wake
Utu uzima wa mapema ndiyo muda muafaka zaidi kwa ajili ya watu wengi kutafuta ndoa (Mithali 5:18, Malaki 2:15, Tito 2:4). Kwa kijana aliyekomaa kama mtu mzima, anapaswa awe tayari ameshafundishwa na kuwa tayari kwa ajili ya maisha yake. Mwanamume au mwanamke ni lazima awe aliyekomaa, aliye tayari kubeba jukumu, na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya hekima na au busara (1 Timotheo 4:12). Kimsingi, vijana waliokomaa kama watu wazima wako tayari kwa ajili ya kubeba majukumu ya ndoa na kulea watoto. Miili yao pia iko tayari kwa ajili ya kuzaa, na mara nyingi, wana tamaa kali ya kujamiiana na uhitaji wa urafiki wa ndoa.
Kwenye tamaduni nyingi kwa sasa, inakuwa ni jambo la kawaida kwa vijana waliokomaa kuchelewesha ndoa hadi pale watakapokuwa wamekamilisha elimu yao ya juu/vyuo, au watakapokuwa wamejiimarisha kabisa katika nafasi zao za kazi. Vijana wengine waliokomaa hawako na nia ya kuwa na ndoa kwa sababu wanataka kuishi bila kuwajibika.
Vijana wengi waliokomaa kama watu wazima huishi katika maisha ya uasherati kabla ya ndoa zao. Wana matamanio makali ya kufanya ngono. Katika hali ya Kihisia, wanataka ushirika wa karibu. Pamoja na hayo, bado hawataki kujiingiza kwenye ndoa na kuendeleza familia kwa sababu ya aidha malengo yao ya maisha au kutotaka kuchukua wajibu.
Vijana wa Kikristo ambao wanajichelewesha kuingia katika ndoa wanapaswa kufikiria kwa uangalifu vipaumbele vyao. Wanapaswa wahakikishe kwamba wanaishi maisha ya utauwa, yaliyo safi, na yenye kufuata mapenzi ya Mungu. Baadhi yao watahitajika kutafakari umuhimu ambao Mungu ameuweka\katika ndoa na katika kukuza/kulea watoto wenye kumcha Mungu.
Wenzi wanaoishi pamoja ingawaje bado hawajaoana
Wakati mwingine, mwanamume na mwanamke huishi pamoja kwenye mahusiano ya ndoa, lakini wakichelewesha kufunga ndoa. Wanaweza wakawa wamejikabidhi mmoja kwa mwingine, lakini bado wanakuwa hawajafanya agano loa ndoa. Watu wanaofanya hivi wana sababu tofauti za kuwa hivyo:
1. Wakati mwingine matarajio ya kitamaduni yenye mambo mengi ya kuchanganua na gharama za harusi huzuia wenzi ambao siyo wenye uwezo mkubwa kuweza kuwa na harusi inayokubalika.
2. Wakati mwingine wenzi hawajiingizi kwenye ndoa kwa sababu ya hofu kwamba ndoa yao haitadumu. Wanaweza wakafikiria kwamba kutengana kutakuwa na madhara kidogo endapo watakuwa bado hawajafunga ndoa. Wanaweza kutarajia uhusiano wao kuwa na nguvu wakati wakiwa wanaishi pamoja.
Mungu amehifadhi uhusiano wa kimapenzi kwa ajili ya ndoa (Waebrania 13:4). Wenzi wanaoishi pamoja lakini bado hawajafunga ndoa wana hatia ya kutotii Neno la Mungu. Ukaribu wao hauwezi kamwe kuwa vile unavyopaswa kuwa, kwa sababu ya ukosefu wa ahadi ya kudumu na ya kipekee kwa wao kwa wao, pamoja na ukosefu wa uaminifu wa pande zote.
Watu waliookoka hawapaswi kabisa kufuata mfano wa watu ambao hawajaokoka badala yake wanapaswa walitii Neno la Mungu. Kanisa ni lazima lishikilie matarajio ya Mungu kwa ajili ya maadili na kutoa usaidizi wa vitendo ili kuwasaidia wanandoa kufuata mpango wa kimaandiko kuhusiana na ndoa. Kwa mfano, wanandoa wanapokuwa hawawezi kufanya harusi ya gharama kubwa, familia ya kanisa inapaswa iwape msaada ili kuwawezesha kuwa na harusi ya gharama ndogo. Hili litawasaidia wanandoa kutii kiwango cha Mungu kwa ajili ya maadili kwa kufunga ndoa. Pia ingesaidia wanandoa wasianze ndoa yao kwa kuwa na deni la kifedha. Wakristo ni lazima wakumbuke kwamba ndoa ni muhimu zaidi kuliko sherehe ya harusi yenyewe, hata hivyo, ahadi ya ndoa ya uhakika na ya kudumu ni lazima ifanywe.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Warumi 12:2 na Wafilipi 2:15-16 kwa ajili ya kikundi. Jadili jinsi ambavyo kujitolea kwa waumini katika maadili kunavyoweza kubadili utamaduni unaowazunguka.
Useja wenye Afya
Suala la Kujisalimisha
[1]Kila mtu aliye mtoto wa Mungu ni lazima akabidhi matamanio yake kwa Yesu. Yesu ni Bwana. Katika maisha yote, kila muumini atapimwa katika uaminifu wake kwa Yesu kama Bwana wake. Kitu kigumu kitatokea… au au kitu kizuri tunachokitamani hakitatokea…na Yesu atatuuliza sisi, wafuasi wake, “Je, mimi ni Bwana wenu? Je, mtaamini wema wangu? Je, mtaamini kwamba ninao mpango mzuri? Je, mtanitii? Je, mtajisalimisha kwangu? Je, mtanyenyekea katika kile ninachokifanya? Je, mtanitukuza mimi katika hili?
Baadhi ya waseja wanafurahia kuendelea kuwa waseja. Lakini wale wanaotamani kufunga ndoa na hawajapata fursa nzuri ya kuoa au kuolewa wanapaswa kukubali kwa unyenyekevu uchaguzi wa Mungu wa kuizuia ndoa.
Wakristo wanaume na wanawake… wanatambua kwamba ikiwa Mungu atawataka wafunge ndoa, ataliweka jambo hilo liwe wazi kwa ajili ya wakati na njia yake kamili. Lakini ni lazima siku zote aje kwanza, na siku zote ataendelea kuwepo [aaminiwe kabisa]. [2]
Mungu ni mwaminifu na ni mwema. Kuna kazi ambayo anataka kuifanya kwenye moyo na maisha ya mwamini ambaye hajaingia kwenye ndoa. Siku zote Mungu ataruhusu kile ambacho ni bora zaidi kwa watoto wake, na muhimu zaidi sana, kile ambacho kitamletea Yesu utukufu mzuri zaidi. Katika mambo yote, Mungu anafanya kazi ya kutufanya tumfanananie Yesu katika mwenendo wetu (Warumi 8:28-29), na kutuwezesha sisi kumwabudu Yesu jinsi tunavyopaswa kumwabudu hata milele (1 Petro 1:6-7).
Mungu anao uwezo kamili wa kumpa kila mmoja wa watoto wake mke mcha Mungu. Anaweza kumsaidia mwanamume Mkristo kumpata mke mwenye kumcha Mungu, huku mwanamume naye akiwa anatafuta mwanamke mwema ambaye atamheshimu Mungu katika maisha yake (Mithali 18:22, Mithali 19:14, Mithali 31:10).
Mwanamke ambaye hajaolewa lakini anaishi kwa ajili ya Kristo anaweza kumwamini Mungu katika kushughulikia mahitaji yake kwa njia iliyo bora kabisa, iwe au isiwe kama Mungu atamwongoza mwanamume kwake kwa ajili ya kutaka kumwoa. Anaweza akaishi maisha makamilifu na yenye matunda ya kiroho kwa sababu ya utoaji na uaminifu wa Mungu.
Ikitokea kuwa useja ni chaguo la Mungu kwake, atamwona Mungu kuwa mpenzi sahihi, mpaji, mlinzi, na kiongozi. Yesu anaweza kuwa mume wa moyo wake (Isaya 54:5), na anaweza kumpenda, kumheshimu, kujitoa kwake, na kumtii yeye, kama mbadala wa mume wa kidunia.
Ikitokea kuwa ndoa itakuwa ndiyo chaguo la Mungu kwake, muda wake alioutumia katika useja utakuwa umeshamfundisha jinsi ya kumtii Mungu (ambaye peke yake ndiye mpenzi mkamilifu, mpaji, mlinzi, na kiongozi), hata atakapokuwa anaendelea kujifunza kumpenda, kumheshimu, na kujitoa kwa mume wa kibinadamu, asiye mkamilifu.
Ukamilifu katika Kristo
[3]Waumini wote ni lazima wapate utimilifu wao ndani ya Kristo, na siyo kutoka kwa rafiki wa kibinadamu. Hata kama mtu angependelea kuwa katika ndoa, useja wa muda mrefu unatoa fursa ya kuhakikisha kwamba kwa uhakika amekamilishwa ndani ya Yesu. Useja unatoa fursa ya kuthibitisha kwamba Yesu anatosha (Wafilipi 4:11-13).
Ukweli kwamba Mungu aliumba ndoa, na kwamba tunapaswa kuiheshimu kama taasisi takatifu, ni dhahiri katika maandiko yote…Haikuwa ni jambo jema kwa Adamu kuwa peke yake, lakini hiyo haikuwa ni kwa sababu Mungu mwenyewe hakutosha kutimiza mahitaji ya Adamu? Hakika hapana! Kama Biblia inavyofafanua kwamba, Mungu alimwumba Hawa kwa sababu Adamu alihitaji awe na msaidizi, rafiki wa kufanya kazi hapa duniani ambayo Mungu alikuwa amemuita kuifanya. Ndiyo, kulikuwa na baraka na faida nyingi ambazo zilikuja kwa pamoja kwa Adamu na Hawa kupitia urafiki wao, lakini ndoa kamwe haikuchukua nafasi ya Mungu. Yeye bado alikuwa ni Mungu, na bado alikuwa amemaanisha kuwa ndiye kusudio lao la kwanza na la msingi la upendo na kuabudu. [4]
Mtu anaweza kujifunza kujionea upendo zaidi wa Mungu wakati akiwa hana mwenzi au familia kwa ajili ya kutoa huba na mhemuko wa kimwili. Maandiko kama Zaburi 73:25-26 ni faraja wakati wa kupitishwa katika mhemuko na majaribu ya kimwili:
Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele.
Kama Leslie Ludy anavyoandika,
Daudi mwimba Zaburi alikuwa wenzi/marafiki wengi wa kike katika maisha yake. Lakini ni uhusiano wa urafiki wa karibu na Mungu ambao ulimletea utoshelevu uliokuwa kamili kama Aya hizi zinavyofafanua. [5]
Muumini aliye mseja atagundua kwamba Yesu anatosha; na uhusiano na Mungu unaridhisha.
Fursa kwa ajili ya Huduma
[6]Wakati waumini ambao hawana ndoa wanapopata utoshelevu wao ndani ya Kristo, yeye huufanya useja wao uwe ni fursa ya kuwatumikia watu wengine. Badala ya kuweka mwelekeo wao kwenye mahitaji yao binafsi na kujisikia kutoridhika, wanaweza kujifunza kutambua na kukidhi mahitaji ya watu wengine. Kuwasaidia watu wengine ni mojawapo ya njia bora za kuleta kuishi maisha yenye matunda na utoshelevu. Tabia iliyokuzwa kupitia katika kipindi hiki cha maisha itawasaidia kuendelea kuzaa matunda mazuri katika maisha yao yote.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Wafilipi 2:3-4 na Tito 3:8, 14 kwa ajili ya kikundi.
Kama ambavyo imeelezwa hapo awali, hali tofauti za maisha hutoa fursa za kipekee. Katika kila hatua ya maisha, kuna mambo ambayo mtu anaweza akayafanya, na kuna mambo mengine ambayo hawezi kuyafanya. Dada mmoja mseja aliitengeneza orodha hii ya mambo ambayo anaweza kuyafanya hasa kwa sababu yeye ni mseja. Wanaume na wanawake waseja watakuwa na vitu vingine vya kuweka kwenye orodha zao.
Kwa kuwa mimi bado ni msichana mdogo niliye mseja, ni rahisi kwangu mimi kufanya yafuatayo:
Kuwatembelea wazee na kutumia muda wangu pamoja nao.
Kutengeneza na kuwapa chakula watu ambao hawana makazi.
Kujifunza Biblia kwa ukamilifu kisha kuandaa masomo ya Biblia\kwa ajili ya watoto.
Kuwahudumia wanawake na wasichana wa eneo la nyumbani kwangu
Kutumia muda wangu usiokuwa na usumbufu kwa ajili ya maombi na maombezi.
Kujifunza ujuzi mwingine mpya.
Kuandika barua na kadi za kuwatia watu moyo.
Kujitolea kuwasaidia watu wengine kwa miradi.
Kwa haraka hubadilisha ratiba yangu wakati kunapotokea kuwepo na hitaji au tukio la haraka lililojitokeza.
Kila mtu ana fursa au wajibu maalumu kwa sababu ya hali zao za maisha. Orodha ambayo mama mwenye watoto wadogo angeiorodhesha ingeweza kujumuisha mifano ya mambo ambayo anawafundisha watoto wake au njia ambazo anazitumia kuwafundisha. Kwa kuwa yeye ndiye mama yao, Mungu amempa fursa na jukumu la kuhudumu kupitia njia hizi. (Mwishoni mwa somo hili utaandaa orodha yako mwenyewe.)
Urafiki
Ni muhimu sana kwa wale ambao hawajafunga ndoa kujenga uhusiano mzuri wenye nguvu na watu wengine. Kama ambavyo imezungumzwa kwenye masomo yaliyotangulia, Mungu aliumba watu kwa ajili ya kuwa na mahusiano na yeye na pia mahusiano na watu wengine.
Watu wanaoishi katika useja wanahitaji mahusiano na watu ambao wanaweza kuwatumikia – labda watoto, vijana au wazee.
Watu wanaoishi katika useja wanahitaji washauri waliokomaa kwa ajili ya ushauri na uwajibikaji.
Watu wanaoishi katika useja wanahitaji marafiki walio katika hadhi na nafasi moja katika maisha, ili kwamba waweze kutiana moyo kila mmoja na mwingine katika Bwana na kuwa na ushirika wa pamoja.
Watu wanaoishi katika useja wanahitaji kuwa marafiki na wenzi walioko kwenye ndoa pamoja na familia. Kuna baraka nyingi za kushirikishana kwa faida ya wote kwenye urafiki kama huo.
Kuwa na mahusiano ya aina mbalimbali na watu wengine humpa mtu aliye katika useja fursa nyingi za kuhudumia. Kuwa katika urafiki huweza kupata baadhi ya msaada wa kihisia na kiroho anaouhitaji mtu aliyeko kwenye useja. Urafiki husaidia kutosheleza uhitaji wao wa familia hasa pale ambapo hawaishi karibu na familia zao wenyewe.
Tahadhari mbili ni lazima ziongezwe:
1. Mtu Mtu ambaye hajaoa au hajaolewa lazima awe mwangalifu ili kuepuka kuunda mahusiano yasiyo ya busara au yasiyo ya maadili kwa sababu ya mahitaji ya kihisia na kimwili.
2. Mseja ni lazima aweke kipaumbele chake na Mungu kiwe juu ya uhusiano wowote wa kibinadamu.
Wazo la Maisha
Waumini wote ni lazima wafanye kazi kwa ajili ya kuweka mawazo ya maisha yawe masafi kwa neema ya Mungu yenye kuwezesha (Mithali 4:23). Zaburi 19:14 ni maombi, ya kumwomba Mungu atusaidie sis tuishi kwa uangalifu kwa ajili yake katika maneno na mawazo yetu. Maombi haya yanatukumbusha kwamba tunawajibika kwa Mungu kwa makusudio ya mawazo na maneno yetu tunayosema.
Tuna chaguzi mbalimbali kuhusu yale tunayoyaweka kwenye akili zetu (Wafilipi 4:8): yale tunayoyaona, tunayosikiliza, na kusoma. Kama tunataka tumheshimu Mungu, ni lazima tuchague chakula cha kiroho ambacho ni kisafi, na kitakachotuvuta karibu na yeye na kitakachotusaidia kumtii yeye (Warumi 12:2, Warumi 13:14).
Wafuasi wa Kristo hawapaswi kujiliwaza na dhambi za watu wengine (Zaburi 101:3, 1 Wakorintho 15:33). Kufurahia kutazama mambo na tabia chafu ni kushiriki katika dhambi ya mtu (Warumi 1:32). Kutazama na kusikiliza kunamfanya mwamini apate hisia ya kutenda dhambi na kumfanya kupoteza mwelekeo katika kumpendeza Mungu (Mithali 13:20). Neno la Mungu linasisitiza haja yetu ya kumcha Bwana kila wakati (Mithali 23:17) na kuchukia uovu kama yeye mwenyewe anavyochukia (Mithali 8:13). Tunapokuwa na hofu ya Mungu na kujiepusha na maovu, tunabarikiwa (Zaburi 111:10).
Wakati tunapokuwa tumeshindwa kutii maagizo ya Mungu kuhusu yale tunayopaswa kuyaweka katika akili zetu na yale ambayo ni ya kutafakari, ni lazima tukiri makosa yetu na kuacha kabisa kuendelea kufanya mambo hayo. Hata katika hali hizo wakati kwa bahati mbaya tunaweza kusikika au kuona jambo baya, ni lazima kwa makusudi tubadilishe mawazo yanayohusiana na mambo hayo kwa mawazo mazuri na ya kimungu.
► Wanafunzi wanapaswa wasome Zaburi 19:14, Zaburi 1:1-2, Wafilipi 4:6-8, na Waefeso 5:25-27 kwa ajili ya kikundi.
Aya kutoka kwa Wafilipi inatuambia kwamba Mungu anataka kulinda mioyo na akili zetu, lakini ni lazima tushirikiane naye kwa kutafakari kwa makusudi mambo yaliyo sahihi. Kutafakari juu ya maandiko ni muhimu sana kwa ajili ya mawazo ya maisha yenye afya na yaliyo safi. Tunaelezwa katika Waefeso kwamba Neno la Mungu linatutakasa na kutufanya tuwe wasafi. Kwa hakika jambo hili linahusisha akili zetu na mawazo yetu.
► Je, ni shughuli gani zinazokusaidia wewe kuwa na mawazo ya maisha ya kumtukuza Mungu? Je ni Aya gani nyingine ambazo zimeshawahi kukusaidia wewe katika mawazo yako ya maisha?
Useja na masuala ya ngono
Ikiwa unajifunza somo hili wewe mwenyewe kwa wakati wako, tafadhali pia soma na somo la 4 mahali ambapo usafi wa kijinsia na masuala ya maadili yamejadiliwa.
“Kutosheka ni kuridhika kunakotokana na kujua kwamba Mungu ndiye aliye mkuu na juu ya vyote katika hali zangu zote, na hunipa mimi kile ambacho ni bora sana kwa ajili yangu.”
- Phil Brown
[2]Nukuu kutoka kwa Leslie Ludy, Sacred Singleness (Eugene, OR: Harvest House Publishers, 2009), 24.
“Ikiwa kama wewe ni mseja, kumbuka haujaitwa kupoteza muda na uhuru wako kwa ajili ya kufuatilia shughuli zenye mrengo wa kibinafsi tu, bali kuhudumu kwa ajili ya kanisa na ulimwengu.”
- Nukuu kutoka kwa Paul Lamicela
Hitimisho
Useja huwapa waumini fursa za kipekee za kukua katika mahusiano yao na Kristo na kujifunza jinsi ya kuhudumia watu wengine. Watu ambao bado hawana ndoa wanapaswa watafute utimilifu wao katika Kristo huku wakiwa wanajenga uhusiano wao mzuri na watu wengine. Wanapaswa watumie fursa zilizopo za useja wao kwa ajili ya utukufu wa Mungu na uzuri wa ufalme wake. Vipaumbele vya Mungu husaidia waumini katika kufanya maamuzi mazuri ya kuzingatia uwezekano wa kuwepo ndoa.
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Taja na jadili vipaumbele kadhaa ambavyo vinaweza kuongoza maamuzi kuhusu miaka ya useja, chaguo la kuwa na ndoa, na kufuatilia ndoa.
► Je, ni kwa jinsi gani kanisa lako linaweza kuhudumu kwa ufanisi zaidi kwa washirika ambao bado ni waseja?
► Je, ni kwa jinsi gani familia yako inaweza kufanya urafiki na mtu ambaye bado ni mseja?
► Kama bado wewe ni mseja, ni kwa jinsi gani unaweza kuwa ni mchango kwa familia ya kanisa lako? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwa ni baraka kwa watu wengine wa vipindi vya marika mbalimbali ya maisha?
► Je, ni mawazo gani mapya uliyoyapata katika somo hili?
► Je, ni jambo gani lingine ambalo ungependelea liweze kujadiliwa katika somo hili?
► Jadili jinsi ambavyo maudhui yaliyoko katika somo hili yanavyofanya kazi kwenye vipindi vingine vya maisha.
Maombi
Baba wa Mbinguni,
Asante kwa kuwa mwaminifu kwetu katika kila kipindi cha maisha yetu. Asante kwa ajili ya mifano ya wale ambao wanaishi kwenye uwepo wako na kwa ajili ya utukufu wako katika miaka yao mingi ya useja.
Tusaidie tujikamilishe kwako kwa uaminifu wetu wote kupitia katika maisha yote. Tusaidie kutafuta na kupata utimilifu wako kwenye mahusiano yetu pamoja na wewe. Tusaidie katika kutumia fursa ulizotupa sisi kwenye wakati wetu wa sasa wa maisha yetu.
Tuwezeshe sisi tukuheshimu wewe siku zote katika chaguzi zetu, mawazo yetu, mahusiano yetu na watu wengine, na huduma zetu. Tufanye tuwe watu wa kuzaa matunda kwa ajili ya utukufu wako.
Ameni
Kazi za Kufanya
(1) Jaribu kufikiria hali ambayo Yesu amekutaka ujisalimishe kwenye mpango wake. Kwa takribani vifungu viwili, elezea mazingira na mwitikio wako kwa ajili ya jambo hilo. (Hali hii inaweza ikawa ni kwenye hali ya sasa tuliyopo au kitu chochote kinachotokana na wewe cha hapo nyuma.) Je, ni kwa jinsi gani imani yako ilikuwa inajaribiwa? Ni kwa jinsi gani Bwana anavyokuongoza? Je ulijisalimisha kwenye mpango wake? Ulimwambia nini? Utii ulionekanaje kwako katika hali hii?
(2) Je, ni fursa gani ulizo nazo kwa sababu ya hali yako ya ndoa, jinsia, au hali ya maisha? Kwa sasa usifikirie juu ya kile kitu ambacho huwezi kukifanya. Badala yake, chukua dakika chache za kuorodhesha mambo ambayo una uwezo wa kuyafanya kwa sababu ya mahali ambapo Mungu amekuweka kwa sasa. Andika, Kwa sababu mimi ni_________ninayo fursa ya kufanya_________.”
(3) Soma na utafakari juu ya kila moja ya maandiko yaliyonukuliwa hapa chini, ambayo kwa pamoja yalikuwa yamerejewa kwenye sehemu ya mwisho ya somo. Mwombe Mungu akuonyeshe chochote unachohitaji kubadilisha, ili kwamba mawazo yako ya maisha yawe safi na yenye kumpendeza Mungu. Andika maombi ya kukiri na kujikabidhi kwa utii.
Zaburi 1:1-2
Zaburi 19:14
Zaburi 101:3
Zaburi 111:10
Mithali 4:23
Mithali 8:13
Mithali 13:20
Mithali 23:17
Warumi 1:32
Warumi 12:2
Warumi 13:14
1 Wakorintho 15:33
Wafilipi 4:6-8
(4) Chagua Aya tatu kutoka katika sehemu ya 3 ya Kazi za Kufanya kwa ajili ya kuzikariri kwa kichwa. Mwanzoni mwa kuanza kwa kipindi cha darasa kinachofuata, andika au rudia kusema yale uliyokariri kutoka kichwani.
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.