Katika kozi hii, tutajifunza zaidi kuhusu familia inayoishi pamoja kwenye eneo moja la kuishi. Michanganyiko mingi tofauti ya watu huunda vikundi vinavyoishi katika nyumba pamoja na huitwa familia. Kuna familia ambazo zina mzazi mmoja, kuna familia ambazo zimegawanyika kwa kupeana talaka, Kuna familia zilizo na mzazi mmoja, familia zilizogawanyika kwa sababu ya talaka, familia zilizounganishwa na ndoa ya pili, familia ambazo zimeasili watoto, familia zenye vizazi vingi, na familia ambazo zinazohudumia watoto au watu wazima kwa muda.
Kila mmoja wetu ana dhana ya kiakili ya nini maana ya familia. Majadiliano kuhusu familia huunda hisia tofauti ndani yetu, kulingana na uzoefu wetu wa kibinafsi.
Jinsi Utoto Unavyotuathiri
Labda una kumbukumbu nzuri za utoto wako, au labda unapambana na hasira kwa sababu ya mambo uliyokutana nayo wakati wa utoto. Labda wanafamilia wako mara nyingi husaidiana na kutiana moyo, au yumkini wanakwepana kila mmoja na mwenzake na wana migogoro kila wanapokuwa pamoja. Unaweza kuhisi kuwa familia yako imekuwa msingi na msaada mkubwa kwa maisha yako, au labda nyumba yako ilikuwa kama jela, ikiwa na mazingira machungu yaliyoleta hamu ya kutoroka. Labda unapoona familia zinazoonekana kuwa bora zaidi kuliko zako, unahisi kwamba familia yako haikukufanikisha.
Uelewa wetu wa familia zetu ni muhimu kwa sababu unaathiri uelewa wetu wa maisha na ufahamu wetu kuhusu Mungu ni nani. Biblia inazungumza juu ya Mungu kuwa Baba wa watu wake. Mahusiano yetu na wazazi wetu – hasa baba zetu – huunda na kutengeneza dhana yetu juu ya Baba yetu wa Mbinguni. Ikiwa baba yetu wa kibinadamu alikuwa hayupo, mwenye lugha chafu, asiyejali, mwenye kudai, mwenye hila, mwenye kukaa tu bila hisia, au mwenye kuumiza kwa njia yeyote ile, dhana yetu ya Mungu kuwa Baba ingeweza kuharibiwa. Hadi pale tutakapomjua Mungu kupitia Neno Lake, kupitia maisha ya Yesu, na kupitia kutembea kwetu kibinafsi pamoja naye, tunaweza tukapata ugumu wa kumwona yeye kama Baba mzuri. Kwa kweli yeye ni baba mzuri ambaye huwalinda na kuwaandalia watoto wake kwa vitendo. Yeye husikiliza na kuzungumza na watoto wake, huwaongoza, na hufurahia hali zao njema. Mungu anaweza kutusaidia kutengeneza kwa upya tena uelewa wetu kumhusu Yeye kwa kadri tutakavyoweza kumjua Yeye.[1]
Jinsi Tofauti za Kiroho Zinavyotuathiri
Baadhi yetu tumekataliwa na familia zetu kwa sababu ya kuamua kumfuata Kristo. Yesu alisema kwamba tunapaswa kutarajia mateso kutoka kwa wanafamilia ambao hawajaamini kwa sababu ya kujitoa kwetu kwa ajili yake. Katika maeneo mengi waumini wanasalitiwa, wanaaibishwa, wanapuuzwa, wananyanyaswa, na wanauawa na wanafamilia wao wenyewe ambao wamekataa kumkubali Kristo.
► Mwanafunzi anapaswa asome Mathayo 10:21-22, 28, 32-39. Baada ya kuzisoma hizi aya, yajadili maswali yafuatayo:
Kwa mujibu wa aya hii, je, waumini wanapaswa kutarajia nini?
Ni ahadi gani zinazotolewa hapa?
Ni kwa jinsi gani waumini wanapaswa kufikiria kuhusu mateso?
Watu wengine miongoni mwetu wanaweza wasipatwe na matatizo kutoka katika familia zao lakini wanaweza kupatwa na changamoto za mahusiano kwa sababu ya imani yetu. Inawezekana mahusiano ya familia zetu yana shida, ni ya Umbali, ni madogo, kwa sababu kama waumini maisha yetu yako tofauti sana na maisha waliyo nayo wanafamilia wetu. Tunaweza tusieleweke au tusipewe heshima zinazostahili. Huenda watu wa familia wakajaribu kuzuia huduma zetu. Hata Yesu mwenyewe alikutana na magumu haya (Marko 3:21, Yohana 7:3, 5), kwa hiyo hatupaswi kushangaa tukifanyiwa hivyo pia.
[1]Ili kujifunza jinsi ya kufanya upya uelewa wako kuhusu Mungu ni nani, ona Somo la 4 la Malezi ya Kiroho kutoka Shepherds Global Classroom.
Wewe na Familia yako
Kwa dakika chache, utajitambulisha kwa wanafunzi wenzako, lakini hutataja tu jina lako, bali pia utashirikisha wewe ni nani katika muktadha wa familia yako.
Kwanza fikiria kuhusu nyadhifa zako zote ulizo nazo katika familia yako, kama vile mtoto wa kiume au wakike, mume au mke, mjomba au shangazi, au kama ni bibi au babu. Je, unaweza ukafikiria kuhusu vyeo vingine vya ziada? Inawezekana una vyeo vingine kadhaa.
Je, una majukumu gani mengine au nafasi gani nyingine katika familia yako? Wewe ndiyo mkubwa au ni mdogo zaidi? Wewe ni mtoaji wa fedha? Wewe ni mtu uliye na jukumu la kuitunza nyumba yako? Je, wewe unalo jukumu la kuwatunza wazee na watu wasiojiweza? Jaribu kufikiria tena majukumu mengine uliyo nayo ndani ya familia yako.
► Jitambulishe kwa wanafunzi wenzako, ukiorodhesha baadhi ya vyeo na majukumu yako ndani ya familia yako.
► Sasa, chukua muda wa kufikiri kuhusu jinsi ambavyo vyeo vyako na majukumu yako yanavyoshawishi: (1) Mtazamo wako juu yako mwenyewe, na (2) Jinsi unavyowaona wengine ndani ya familia yako.
Licha ya jinsi unavyoweza kuhisi kuhusu wanafamilia wako wa karibu au wa mbali, wao ni wako. pengine familia yako imevunjika, ina alama za maumivu na huzuni. Au labda watu wanakuonea wivu kwasababu familia yako inaonekana kuwa kamilifu: una ndoa nzuri, watoto wenye akili na afya njema, na nyumba iliyojaa upendo, amani na kicheko.
Aidha iwe familia yako inaonekana kuwa dhaifu au yenye nguvu, Mungu anapendezwa na anahusika kikamilifu na familia yako. Anao mpango kwa ajili ya familia yako.
► Orodhesha majina ya wanafamilia wako (angalao vizazi 3-4 vya wanafamilia). Kwa mfano, majina ya babu zako (kizazi cha 1), majina ya wazazi wako (kizazi cha 2), jina lako na ndugu zako (kizazi cha 3), majina ya watoto wako au wapwa - watoto wa kike au wa kiume wa kaka /dada - (kizazi cha 4).
Chora nyota kando ya majina ya wale ambao una mahusiano ya karibu na yaliyo mazuri. Chora alama ya pembetatu mbele ya majina ambayo una mahusiano madogo sana nao, na chora alama ya pembe mraba mbele ya wale ambao hamhusiani kabisa katika jambo lolote kwa sababu iwayo yeyote ile.
Je, wako watu ambao unawachukulia kama ni sehemu ya familia yako, ingawaje kwa uhakika siyo wenye kuwa na mahusiano na wewe: watu ambao wanahudhuria katika makutaniko na sherehe mbalimbali kana kwamba ni wanafamilia? Waandike na yawekee alama ya mviringo majina yao.
Familia ya Kwanza ya Kibinadamu
► Fungua Biblia yako katika kitabu cha Mwanzo tunapojifunza maisha ya Adamu na Hawa, na Ibrahimu na Sara.
Harusi ya Kwanza
Adamu na Hawa ilikuwa familia ya kwanza ya kibinadamu: mume mmoja na mke mmoja, mwanamume mmoja na mwanamke mmoja wakiunganishwa pamoja katika ndoa. Katika harusi ya kwanza, Adamu alisema, “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume” (Mwanzo 2:23).
Aya inayofuata inatoa ufafanuzi wa kibiblia kuhusu ndoa:
“Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwanzo 2:24).
Ufafanuzi huu wa kufanana umerudiwa tena katika Agano Jipya kwenye Mathayo 19:5 na Waefeso 5:31. Muunganiko wa mwili mmoja wa mwanamume na mwanamke ni wajibu usiokuwa na masharti, ahadi mbele ya Mungu na mwanadamu kwamba itakuwa ni ya kudumu kwa maisha yote.
Ndoa ni muujiza ulioko wa aina tatu. Ni muujiza wa kibiolojia ambao katika huo watu wawili wanafanyika hasa kuwa mwili mmoja; ni muujiza wa kijamii ambao kupitia huo, familia mbili tofauti hupandikizwa kuwa familia moja; ni muujiza wa kiroho ambao kwao uhusiano wa ndoa unatoa picha inayofananishwa na muunganiko wa Kristo na Bibi Harusi wake, yaani Kanisa.[1]
Ndoa inaakisi Mahusiano yaliyoko kwenye Utatu Mtakatifu wa Mungu
[2]Ndoa imekusudiwa kuakisi tabia ya Mungu na mahusiano yake. Mungu Baba, Mungu Mwana, Mungu Roho Mtakatifu kwa wakati wote wamekuwa na siku zote wataendelea kuwa kwenye uhusiano na kila mmoja. Kila mmoja ni wa kipekee kwenye jukumu lake, lakini nafsi zote tatu ni za kudumu na zenye asili moja. Kwenye uhusiano kati ya nafsi tatu za Utatu Mtakatifu wa Mungu, tunaona umoja, ukaribu, uaminifu, na upendo thabiti. Ndoa ya Kibiblia imeundwa baada ya uhusiano huu wa kushangaza. Mpango wa Mungu ni kwa kila mume na mke kuwa safi katika upendo wao na kila mmoja kujitolea kwa ajili ya mwingine kwa maisha yake yote.
Uhusiano wa ndoa ya kibinadamu unapaswa uakisi mahusiano yaliyoko ndani ya Utatu Mtakatifu wa Mungu kwa njia hizi:
1. Ndoa inapaswa isiwe na masharti, yenye ahadi ya kipekee kwa mwingine.
2. Ndoa ni kuwa na uhusiano wa upendo wa kujitoa mwenyewe.
3. Ndoa inapaswa iwe na uhusiano unaotoa matunda.
Agizo la Kwanza
Wakati wa harusi ya kwanza, ambayo ilifanywa na Mungu mwenyewe,
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi” (Mwanzo 1:28).
Kuzaa na kuongezeka ni agizo la kwanza ambalo Mungu alilitoa ndani ya Biblia. Ndoa imeundwa ili kuwa na uhusiano unaotoa matunda kwa upendo wa kujitoa mwenyewe. Uzazi ndani ya ndoa unamtukuza Muumbaji, kwa kuwa mume na mke kwa pamoja humletea Mungu utukufu kwenye kazi yake ya uumbaji na huwaleta watu wengi zaidi kwenye uhusiano wa kifamilia.
Huu ni upendeleo na uwajibikaji!
► Mwanafunzi anapaswa asome Zaburi 127:3-5 kwa ajili ya kikundi.
Kifungu hiki kinatumia picha za maneno kuelezea watoto. Picha za maneno ni nini? Kulingana na picha hizi za maneno, je, tunapaswa kuwafikiriaje watoto wetu?
Biblia inatuonyesha kwamba watoto ni zawadi, ni mali ya thamani sana ya kuwa nayo. Hawapaswi kufikiriwa tu kwamba ni matokeo ya mahusiano ya tendo la ndoa. Iwe au isiwe kwamba mazingira yanayohusika ya utungwaji wa mimba wa mtoto ni wa kutaka au wa haki, Mpaji wa Uhai anakuwa na makusudi wakati wa kutungwa kwa mimba na kuzaliwa kwa kila mtoto, ikiwa ni pamoja na wewe na mimi. Mungu analo kusudi na kila mtu bila kujali mazingira ya kuzaliwa kwake.
Hakika, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini pia ni zawadi ya wazazi kwa Mungu.
Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana” (Malaki 2:15).
Watoto ni amana takatifu. Mungu anatarajia wazazi wawalee watoto wao kwa ili kutimiza makusudi yake mwenyewe.
Mungu anataka awatumie watoto wetu kwa ajili ya kuuendeleza ufalme wake (Mwanzo 18:19). Mungu ametuamini kuwatayarisha watoto wetu kwa ajili ya maisha ya kumtumikia yeye (Kumbukumbu la Torati 6:2). Hatuwalei ili watutumikie au kutimiza ndoto zetu. Tunapaswa tuwaone watoto kama mishale ya kurushwa nje ili kupiga shabaha ambayo Mungu anayo kwa ajili yao.
Anguko na Kuvunjika kwa Familia ya Kibinadamu
Katika Mwanzo 3, familia peke yake ambayo ni kamilifu kuwahi kuwepo ilianguka katika hali ya kuvunjika na kuhitaji Mkombozi. Adamu na Hawa walitenda dhambi, na laana ya kifo ikawaangukia wanadamu wote. Uhusiano kati ya Adamu na Hawa uliharibika kabisa, nao walitengwa na Mungu.
Kwa pamoja mwanamume na mwanamke walipata laana zaidi.
Kuzaa kutakuwa kwa uchungu.
Waume watatumia mamlaka yao vibaya.
Wake watakuwa wakaidi na wasio na heshima.
Kazi zitakuwa za kukatisha tamaa na zilizo ngumu.[3]
Mpango wa Mungu ulio mkamilifu kwa ajili ya familia ulivurugwa kwa sababu watu walikubaliana na uongo wa Shetani.
Mwanzo 4 panaendelea kudhihirisha kuvunjika kwa familia ya kibinadamu iliyoanguka.
Angalia taarifa iliyoko katika Mwanzo 4:1, kuhusu mimba ya kwanza na kuzaliwa. Aya hii inahusu muda wa miezi tisa – kipindi kati ya kutungwa kwa mimba ya mtoto hadi kuzaliwa kwa mtoto. Jaribu kujituliza kidogo ufikirie kuhusu hiyo miezi tisa ya uja uzito ilivyopaswa kuwa kwa Hawa, wakati akijaribu kushirikishana kuhusu mashaka na furaha yake pamoja na Adamu.
Hakukuwa na mtu wa kumpa ushauri, wala mtu wa kujibu maswali yake. Tumbo lake lililokuwa likiongezeka, mateke ya mtoto wake, na mchakato wa kujifungua akiwa na mivutano mbalimbali mwilini pamoja na maumivu vyote vilikuwa ni uzoefu wa mara ya kwanza kwa mwanamke yeyote wa kibinadamu.
Hakuna mashaka kwamba Hawa alisema kuhusu kuzaliwa kwa Kaini, “Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana” (Mwanzo 4:1).
Muda ulipita, na katika aya inayofuata, tunajifunza kuhusu mimba ya uzazi wa pili. Sasa Adamu na Hawa wana familia ya watu wanne. Katika nusu ya sehemu ya pili ya Aya hiyo hiyo ni muhtasari wa taaluma za watoto wao. Kufikia Aya ya 3, wavulana hao tayari ni watu wazima na katika Aya inayofuata tunasoma hadithi ya kutisha ya mauaji ya kwanza. Mtoto mkubwa wa Adamu na Hawa alimuua ndugu yake kwenye tendo la hasira na wivu. Je, unaweza kufikiria kuhusu mshtuko huo, huzuni, maswali, uchungu na maumivu?
Jibu lako katika maswali hayo linaweza kuwa “Ndiyo! Ninaweza nikafikiria hivyo. Kwa uhakika, mimi nimewahi kupata uzoefu unaofanana na hali hiyo. Acha nikutie moyo: Hauko peke yako. Familia yako inaweza kukombolewa. Kuna habari njema kwa kila familia.
Gordon Wenham anaandika,
…Ujumbe wa kitabu cha Mwanzo…Ni hadithi ya ushindi wa neema, licha ya dhambi ya mwanadamu, ya ushindi wa neema hata katika familia ambazo zimevunjika kutokana na dhambi. Kitabu hiki kinaanza na dokezo la hali ya juu ya uumbaji wa ulimwengu likimalizia na uumbaji wa mwanadamu katika sura ya Mungu na Mungu akitangaza kwamba kila kitu alichokifanya na alichokiumba vilikuwa vizuri sana…Ni katika sura ya 3 tu ndipo tunapoona mambo yakianza kwenda vibaya, ikiwa ni pamoja na kutotii [migogoro], na kifo kikichukua nafasi ya utii, upatanifu, na uhai. Mambo yanaendelea kuwa mabaya zaidi katika sura ya 4…na kufikia katika [kiwango cha chini sana] katika sura ambako dunia inasemekana kuwa katika hali kamili ya vurugu (Mwanzo 6:11, 13).[4]
[1]Biblia ya Mafunzo kwa Mwanamke (The Woman’s Study Bible,) (Thomas Nelson, Inc., 1995), 9.
Udhihirisho wa tabia ya Mungu kama mfanyaji wa agano mkuu na mshikaji wa agano. Katika agano, vipengele muhimu ni uaminifu, na uadilifu, na siyo mhemuko.”
- Robertson McQuilkin,
Utangulizi wa Biblia kuhusu Maadili
(An Introduction to Biblical Ethics)
[3]Ni muhimu kutaja hapa kwamba uzazi wa mtoto haukuwahi kuwa sehemu ya laana.
Maumivu wakati wa uzazi wa mtoto ni matokeo ya laana, lakini uzazi wa mtoto siku zote umekuwa ni mpango wa Mungu wa ajabu wa kuzalisha kizazi kijacho. Aidha kazi haikuwa laana, bali ugumu wa kazi ndiyo uliokuwa laana. Kwa hakika, kwenye maagizo mengine ambayo alimpa Adamu na Hawa katika Mwanzo 1:28 zinaonyesha kwamba tumeumbwa kwa ajili ya kazi! Kazi ni mojawapo ya njia tunazoakisi sura ya Mungu.
[4]Gordon Wenham akiandika katika Familia ndani ya Biblia (Family in the Bible,) na kuhaririwa na Richard S. Hess na M. Daniel Carroll R., Grand Rapids, MI: Baker Academic, 2003, 29
Uvunjikaji katika Familia ya Ibrahimu
Ukiendelea zaidi katika kitabu cha Mwanzo, tunasoma kuhusu Ibrahimu, baba wa taifa la Waebrania (Mwanzo 11:27-25:11).[1] Ilikuwa ni kupitia katika familia ya Ibrahimu kwamba Mungu angemleta Mkombozi kwenye familia ya kibinadamu.
Mwanzo 11 inaorodhesha ukoo wa Abramu, ambaye alikuwa ni uzao wa Shemu mwana wa Nuhu. Mwanzo 11:30 tunaelezwa kwamba Sarai mke wa Abramu hakuwa amejaliwa kupata watoto. Aya hiyo ni ya machozi, uchungu, huzuni, kuchanganyikiwa, ubatili, hasira na masikitiko kwa wengi watakaokuwa wanaisoma. Kama utaweza kuliweka jina lako kwenye Aya hii likawepo badala ya Sarai, tambua kwamba hauko peke yako.
Kwa wale ambao wangependa kuwa na watoto, lakini wanapitia katika hali ya utasa, kusoma vifungu kama vile Mwanzo 1:28 na Zaburi 127:3-5 kunasababisha maumivu makali na huzuni. Ni hali ya kawaida kujihisi kwamba kukosa mtoto ni adhabu au laana.
Ukweli ni kwamba, wewe siyo mtu usiyekuwa wa muhimu kwa Mungu kwa sababu ya kutokuwa na watoto. Hujasahaulika. Utasa wako haimaanishi kuwa familia yako ni familia yenye kasoro . Wako watu wengine ambao walishakutana na kadhia hii ya majuto makali inayofanana na hii.
Jinsi wanandoa wanavyoshughulika kwenye kupitia utasa, wote kwa pamoja na kama mtu binafsi, ni muhimu sana. Maamuzi yasiyo na busara yanaweza kusababisha matatizo zaidi, kama tutakavyoona kwenye maisha ya Abramu na Sarai.
Kusubiria Ahadi
Kufuatia kifo cha baba yake, Abramu akawa baba wa ukoo wa familia yake. Mungu aliahidi kumfanya Abramu kuwa taifa kubwa (Mwanzo 12:2) na aliahidi kuwapa wazao wa Abramu nchi ya Kanaani (Mwanzo 12:7). Abramu sasa alikuwa na umri wa miaka 75 (Mwanzo 12:4) na Sarai mdogo miaka kumi (Mwanzo 17:17). Sarai alikuwa mwanamke mrembo isivyo kawaida mwenye umri wa miaka 65 (Mwanzo 12:11), bado akiwa tasa, na tayari alikuwa ameshapitiliza miaka yake ya kawaida ya kuweza kuzaa.
[3]Miaka iliendelea kupita, na bado akawa hajapata mtoto, ingawaje ahadi ya Mungu ilikuwa imefanywa upya katika Mwanzo 13:14-17. Abramu alionekana amekataa tamaa ya kuwa baba wa mtoto wake mwenyewe, kwa sababu katika Mwanzo 15:2-3 anaonekana akimwambia Mungu kwamba mtumishi wake ndiye atakayekuwa mmiliki wa nyumba yake. Bwana alimjibu, “Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi (Mwanzo 15:4). Kisha Mungu akampa Abramu picha ya pili ya ahadi ya uzao usiokuwa na hesabu, na Abramu akamwamini Bwana (Mwanzo 15:6).
Jaribu kufikiria ni kwa jinsi gani miaka hii yote ya kusubiria ingekuwaje kwa Sarai.
Kama vile maumivu ya hukumu ya wengine ingeweza kuwa imefanyika kwa Sarai, ilikuwa ni ukatishwaji tamaa (mkali) ambao ulikuwa umemuumiza zaidi. Pengine hakuwa ametamani tu sana utimizwaji wa ahadi ya kuwa mama bali pia kwa ajili ya heshima na stahiki inayopewa kwa wamama wazazi katika jamii ambayo wanawake hawakuwa na lolote la kuhesabika wa maana badala yake. Tunajua kwamba utasa wa kiume unaweza kuwa sababu ya mwanamke kutobeba mimba lakini hakukuwepo na ujuzi huo wa kibiolojia wakati wa ulimwengu wa Sarai. Utambulisho wa Sarai kama mwanamke, na kama mtu wa thamani, ulitegemea aweze kuzaa na kunyonyesha watoto. Hakuweza kupata thamani machoni pa wanaume kwa kuwa kiumbe mwenye haki na mwaminifu, ila kwa kuzaa watoto wa kiume ambao wangekuwa warithi kwa mume wake. Tumbo tupu lilimaanisha maisha matupu.[4]
Suluhisho la Kibinadamu na Matokeo Yenye Maumivu
[5]Abramu alipokuwa wa umri wa miaka 85, Sarai alikuwa na wazo – suluhisho kwa jinsi gani Abramu atakavyoweza kupata mtoto. Mjakazi wa kike wa Sarai angeweza akawa mzazi wa mtoto wao (Mwanzo 16:1-4). Lakini kile ambacho Abramu na Sarai walikuwa wamedhamiria kwamba kingekuwa ndicho suluhisho sahihi na kiliharibu amani katika nyumba yao Hajiri alipobeba mimba. Kilichoonekana kuwa ni kizuri sana kimekuwa ni kibaya sana. Jaribio lao la kumsaidia Mungu kutimiza ahadi yake lilisababisha tu ugomvi na mafarakano. Watu wanaposhindwa kuamini mpango na wakati wa Mungu, matokeo yake ya kawaida ni mahusiano kuvunjika na hisia za kuumiza.
Katika miaka iliyofuata, mivutano, maumivu, kutoelewana, matatizo ya mawasiliano, hasira, utelekezwaji, na kukataa tamaa viliongezeka (Mwanzo 16-21), siyo tu kwenye nyumba ya Abramu na Sarai, lakini pia kwenye familia ya mpwa wao Lutu.
Familia zenye mapungufu
Abramu alikuwa amechaguliwa na Mungu kuwa baba wa taifa kubwa, ukoo ambao Yesu angezaliwa kupitia humo. Inaonekana kama Abramu alikuwa anaharibu mpango wa Mungu, kama walivyokuwa wanafanya watu wengine wa familia yake. Kwao ilikuwa ni mfano wa familia zilizokuwa na mapungufu sana.
Katika Mwanzo 49:33, Abrahamu na Sara, Isaka na Rebeka, Yakobo na wake zake walikuwa wote wamekufa. Pamoja na watoto wa Yakobo, walikuwa familia yenye kushindwa katika mambo mengi sana. Mapigano, mabishano, upendeleo, udanganyifu, utelekezwaji, mashindano baina ya wanandugu, ubakaji, na zinaa ya kifamilia vote vilikuwa sehemu ya hadithi ya familia yao. Hakuna hata neno moja kati ya maneno hayo linalofafanua familia yenye kustawi na amani.
Jambo la kusikitisha ni kwamba, hadithi hii inaweza kurudiwa katika Biblia yote na katika dunia yote kwa karne zote zilizopita. Bila shaka, hata katika familia hizi kulikuwa na nyakati za furaha, hadithi nzuri za upendo, na hata wanaume wachache waadilifu.
Katika kupitia haya yote, Mungu kamwe hakusitisha mpango wake wa kuwakomboa wanadamu. Na hakubadili kusudi lake kwa ajili ya familia. Ukiendelea kusoma Agano la Kale, utagundua mada nzuri sana ya ukombozi kupitia taarifa ya familia ya Kiebrania. Matukio mengi yameelekezwa kwa Yesu kwa siku za mbele. Sadaka ya Ibrahimu ya Isaka, Pasaka na kuondolewa kwa Waisraeli katika utumwa wa Misri; kukombolewa kwa Rahabu kutokana na hukumu na kujumuishwa kwake kwenye kundi la watu wa Mungu; na matukio mengine mengi ambayo yameeleza kwa uzuri sana ahadi kwamba Mkombozi angekuja na kuwakomboa wanadamu.
[1]Mungu alibadilisha majina ya Abramu na Sarai kuwa Abrahamu na Sara katika Mwanzo 17:5, 15.
[2]Ona Somo la 10 kwa ajili ya mambo mengi zaidi katika mada hii..
Mungu anafanya kazi ya kutufanya sisi tumfananie Yesu. Wakati mwingine Mungu anatufanya tuwe na subira, kwa sababu kupitia kipindi cha kusubiri anaweza kufanya kazi ndani ya mioyo yetu ambapo kwa vinginevyo haingewezekana.
[4]David na Diana Garland, Flawed Families of the Bible, Grand Rapids, MI: Brazos Press, 2007, 21-22
“Mungu anazo sababu takatifu za kusubiria wakati tunapokuwa tu wahitaji, kama alivyokuwa amefanya kwa Elizabethi (Luka 1:7, 13), na kuendelea hata zaidi kabla hatujawa tayari, kama alivyofanya kwa Mariamu. (Luka 1:34).
Tunapokuwa tunamtii na kumwabudu Yeye, anatuelekeza, anatuelimisha, na anatoa kwa ajili ya mpango wake, ambao hauzuiliki kamwe na kile ambacho hatuwezi kufikiria.”
- Nukuu kutoka kwa Shauna Letellier, Remarkable Advent
Kazi ya Ukombozi wa Mungu kwenye Familia
Katika Waefeso 5 tunaelezwa kwamba Mungu aliitengeneza ndoa ili iwe picha ya uhusiano Kati ya Kristo na bibi harusi, yaani Kanisa. Kama vile Kristo aliye kichwa anavyojitoa mwenyewe kwa ajili ya Kanisa, vivyo hivyo kila mume, kama kichwa kwa mke wake, anapaswa ajitoe mwenyewe kwa ajili yake. Vilevile, kila mke anapaswa afuate mfano wa Kanisa. Kama ambavyo Kanisa limejitoa kwa ajili ya Kristo, kila mke anapaswa ajitiishe kwa mume wake.
Anguko la mwanadamu liliharibu mpango wa awali wa Mungu uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya familia za wanadamu na kusababisha madhara katika mahusiano ya ndoa. Kila familia inakabiliwa na madhara ya kuanguka kwa mwanadamu katika dhambi. Hata hivyo,
Yesu alikuja kwa ajili ya ukombozi wa mambo yote, ikiwa ni pamoja na ndoa. Alikuja kukomboa na kurejesha mambo yote ambayo dhambi iliharibu na kuharibiwa. Mahali ambapo hatukuweza kuishi kutokana na mpango wa Mungu wa ndoa, Yesu alikamilisha viwango vyote vya Mungu kwa ukamilifu. Yesu alilipenda Kanisa kiasi cha kufa kwa ajili yake. Alijitiisha kikamilifu kwa mpango wa Mungu Baba. Yesu ndiye utimilifu kamili na mkamilifu wa mpango wa Mungu na wa kile ambacho ndoa zetu hushindwa kufanya: upendo na utii. [1]
► Yesu ni mfano wa mtazamo wa tabia gani ambao mtu aliyeoa anapaswa kuwa nao?
Yesu sio tu kwamba anatimiza mapenzi ya Mungu katika kujitiisha kwake kikamilifu na kwa upendo wake mkamilifu, bali anawawezesha waume na wake kushinda katika mielekeo yenye uharibifu ambayo ni asili ya ubinadamu ulioanguka. Kwa neema yake, waume kwa wake wanaweza kutimiza mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa wanapoiishi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wa Mungu (Waefeso 5:18).
Hakuna familia iliyokamilika, lakini Mungu anatamani aiokoe kila familia. Neema ya Mungu inaweza kufanya kazi ndani ya familia ikiwezesha watu binafsi wawe kama ambavyo Mungu alikuwa amewakusudia wawe tangu mwanzo.
Kama ambavyo watu binafsi katika familia huchagua kutii maagizo ya Mungu, utii wao husaidia kushinda baadhi ya kasoro na mapungufu ambayo ni ya asili kwa kila familia. Matokeo ya Anguko ambayo yanaathiri mahusiano ya kibinadamu yanapungua wakati tunapokuwa tumejisalimisha kwenye mapenzi ya Mungu.
Kwa mfano, mume mcha Mungu anapotii maagizo ya Mungu kwake kwenye Waefeso 5, anakuwa ameshinda mwelekeo wake wa asili wa matumizi mabaya ya mamlaka yake dhidi ya mke wake. Utiifu wake kwa Mungu ni wa ukombozi kwa sababu anapunguza madhara ya Anguko. Utii huu ungeweza pia ukamchochea mke wake kujisalimisha mwenyewe kwake.
Inapotokea mke anapotii kwa mume wake katika kutii agizo la Mungu (Waefeso 5:24), anakuwa akishinda mwelekeo wake wa asili wa dhambi wa kuzuia mamlaka ya mume wake. Utii wake kwa Mungu ni ukombozi, unaosaidia uhusiano wao uwe wa kufanana zaidi kama Mungu alivyokusudia ndoa iwe (1 Wakorintho 11:3, 1 Petro 3:1-7).
Mungu ametoa maelekezo ya ukombozi kwa familia za Kikristo ikituonyesha sisi kwamba mahusiano ya familia ni ya muhimu sana kwa Mungu.
Kuna vifungu vingi katika Maandiko ambavyo vinazungumzia kuhusu hitaji la wazazi na mababu kuwafundisha watoto na wajukuu zao njia za Mungu.
Tutaziangalia tatu kwa kifupi:
► Mwanafunzi anapaswa asome Waefeso 6:4 kwa ajili ya kikundi.
Aya hii inamaanisha nini?
Ni mpango wa Mungu kwa wazazi kuwafundisha watoto wao kumjua na kumtii Mungu. Njia ambayo wazazi wanaitumia kuongoza, kuelekeza, kusahihisha, na kufundisha watoto wao inapaswa kuakisi njia ambayo Mungu hufanya mambo haya kwa ajili ya watoto wake.
► Mwanafunzi anapaswa asome Zaburi 78:1-8 kwa ajili ya kikundi.
Jibu maswali yafuatayo:
Ni, vizazi vingapi vya familia vimetajwa katika kifungu hiki?
Kila kizazi kina wajibu gani?
Ni mambo gani wazee wanapaswa kufundisha vijana?
Zaburi ya 78 imefurika kwa neema na rehema za Mungu za ajabu. Inaelezea kazi zake katika familia ya wana wa Israeli tangu walipotoka Misri hadi kwenye utawala wa mfalme Daudi. Zaburi hii inapaswa kuwapa wasomaji matumaini kwa ajili ya hali zilizopo kwenye familia zao.
► Mwanafunzi anapaswa asome Kumbukumbu la Torati 6:1-9 kwa ajili ya kikundi.
Kwa kuangalia kifungu hiki, Je, ni mambo gani ambayo sisi kama watu wa Mungu tunapaswa tuyafanye?
Andiko hili ni sehemu ya hotuba ya Musa kwa wana wa Israeli, kabla tu hawajaingia kwenye nchi ya ahadi ambayo Mungu alikuwa anawapatia. Walikuwa wanajifunza jinsi ya kuwa watu wa Mungu na kwamba ilimaanisha nini kuwa mali ya Mungu. Ukweli katika Aya hizi bado ni msingi wa kuishi kama watoto wa Mungu.
Mungu anatuamuru sisi kuwa watiifu katika kulisikia Neno Lake – na kufanya kila ambacho anakihitaji kutoka kwetu (Aya ya 3-4).
Tunatakiwa tufanye yafuatayo:
1. Kumpenda Bwana kwa moyo wote, kwa roho yote, na kwa nguvu zote (Aya ya 5).
2. Kuyaweka maneno ya Mungu katika mioyo yetu wenyewe (Aya ya 6).
3. Kuwafundisha watoto wetu kwa bidii jinsi ya kufuata Neno la (Aya ya 7).
4. Kuyaweka maneno ya Mungu kwenye fahamu zetu na yawe mbele yetu mara kwa mara (Aya ya 8-9).
Tambua kwamba amri hizi ni kwa kila kizazi (Aya ya 2). Mungu huwajibisha wazazi, mababu na mabibi kufundisha watoto wao na wajukuu wao kuishi kwa ajili yake. Kwa muda gani? Siku zote za maisha yao (Aya ya 2). Mungu anatuambia kwamba wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao njia zake kwa siku nzima, kila siku, kila mahali waendapo, na katika kila jambo wanalofanya (Aya ya 7-9).
Elimu ya kiroho kwa ajili ya watoto ilikuwa ni jukumu la mzazi. Mafundisho hayo yangefanyika kila siku kupitia kielelezo cha wazazi na vilevile kurudiwa kwa sheria. Umuhimu wa amri hii unaonekana katika kiwango ambacho wazazi walipaswa kwenda ili kuwafundisha watoto wao. Hii ilikuwa ni zaidi ya kufundisha mambo ya hakika ya sheria; ilikuwa ni udhihirishwaji wa mtindo wa maisha uliokuwa umesukiwa kwenye kitambaa kilichofumwa cha maisha ya kila siku. Ubunifu ulikuwa unahitajika katika kuwafundisha maadili ya Mungu wakati wakiwa wanajishughulisha na mambo ya kawaida kabisa ya nyumbani.[1]
Wazazi hawapaswi kufundisha tu akili za watoto wao, lakini pia na mioyo yao. Wanapaswa kuwafundisha watoto wao siyo tu ukweli kuhusu Mungu, bali pia matumizi ya vitendo vya jinsi ya kuishi kwenye uhusiano na Mungu na katika kumtii Yeye. Wazazi hufundisha watoto wao kwa maelekezo ya maneno na mfano wa maisha yao. Kwa pamoja vyote hivi ni vya muhimu.
Kifungu hiki kinaweza kuonekana kuwa rahisi, lakini pia ni cha muhimu sana. Kweli hizi na amri hutoa madhumuni na mwelekeo kwa watu binafsi na kwa familia. Jinsi wazazi ambavyo watakuwa wanaendelea kumtafuta Mungu vizuri zaidi na kumtii kikamilifu katika mambo yote, wanakuwa wanawafundisha watoto wao kufanya kama wao wanavyofanya. Wazazi wanapaswa kuwa na mtazamo wa maisha ya muda mrefu wa kujifunza na kutii. Huu ni mfano kwa watoto wao, na huwapa watoto kuwa na njaa kwa ajili ya Mungu.
► Je, ni njia zipi zinazofaa ambazo wazazi wanaweza kuwafunza watoto wao kila siku?
Uwanja wa Mafunzo ya Familia kwa ajili ya Kuwapenda Watu Wengine
► Mwanafunzi anapaswa asome 1 Yohana 4:7-13, 19 kwa ajili ya kikundi.
Mada ya kifungu hiki ni upendo. Ili tuweze kumjua Mungu katika utajiri wake kwamba ni nani, ni lazima tupendane. Hii ni pamoja na familia zetu. Moja ya sababu ambazo Mungu ametupatia familia ni ili tujifunze jinsi ya kuwapenda watu wengine. Tunapojifunza kuonyesha upendo kwa wanafamilia wetu (hata katika wakati ambapo ni mgumu), tunafanana zaidi na Mungu – kwa sababu Mungu ni wa upendo! (Aya ya 8).
Wakati wanafamilia – aidha wawe wa kiroho au wa kimwili – wanapoonyesha kupendana, wanathibitisha kwamba wamezaliwa na Mungu (Aya ya 7). Wanapokuwa mmoja anampenda mwenzake, upendo wa Mungu unakamilishwa ndani yao (Aya ya 12).
Mungu hapendi tu tuwapende watu wengine, yeye kwanza alitupenda (Aya ya 9-11, 19). Alitupenda kwa kumtuma Yesu kuwa dhabihu kwa ajili ya dhambi zetu (Aya ya 10). Upendo wa Mungu kwetu sisi ni motisha kwa upendo wetu kwa ajili yawatu wengine (Aya ya 11).
Kupenda familia zetu kunaweza kuwa rahisi kwa wengine, na kwa wengine ikawa ni vigumu sana, lakini wote kwa pamoja tunaweza kuwa na kile tunachohitaji ili kutii maagizo ya Mungu – Mungu akikaa ndani yetu kupitia Roho Mtakatifu (Aya ya 12-13).
Mungu anatuita tupendane sisi kwa sisi, ikiwa ni pamoja na wazazi wetu, wenzi wetu, na watoto. Kuipenda familia yetu haimaanishi ni kuidhinisha ubaya au uovu. Haimaanishi kwamba hatuhitaji uwajibikaji. Inamaanisha kwamba tunataka kile ambacho ni kizuri zaidi kwa ajili ya wanafamilia wetu na kwamba kwa hiari tuko tayari kujitoa kwa ajili ya manufaa yao.
[1]The Woman’s Study Bible, Thomas Nelson, Inc. 1995, 292
Kwa ajili ya Majadiliano ya Kikundi
► Kwa maneno yako mwenyewe, elezea baadhi ya njia ambazo ndoa huakisi mahusiano yaliyoko kwenye Utatu Mtakatifu wa Mungu.
► Elezea ni kwa jinsi gani Mungu alivyoikomboa ndoa iliyokuwa imeharibiwa na dhambi.
► Toa ufafanuzi ni kwa nini maagizo ya Mungu kwenye ndoa ni ya ukombozi.
Maombi
Chukua muda wa kuomba na mshukuru Mungu kwa ajili ya familia yako. Ombea familia yako. Omba kuhusu maumivu na kushindwa, sherehe na furaha. Yatafakari maneno yaliyoko katika Kumbukumbu la Torati 6:4-9, ukiyaweka kwenye maombi ya kunyenyekea na dua.
Kazi za Kufanya
(1) Kariri akilini Kumbukumbu la Torati 6:4-9. Mwanzoni mwa kipindi cha darasa kinachofuata, andika au simulia hicho kifungu kutoka kichwani bila ya kunukuu popote.
(2) Kwenye Kumbukumbu la Torati 6:1-9, Mungu anatutaka sisi katika mambo manne. Kwa maombi na kwa uaminifu jitathmini mwenyewe katika haya maeneo manne.
Tunatakiwa tufanye yafuatayo:
Kumpenda Bwana kwa moyo wote, kwa roho yote, na kwa nguvu zote (Aya ya 5).
Kuyaweka maneno ya Mungu katika mioyo yetu wenyewe (Aya ya 6).
Kuwafundisha watoto wetu kwa bidii jinsi ya kufuata Neno la Mungu (Aya ya 7).
Kuyaweka maneno ya Mungu kwenye fahamu zetu na yawe mbele yetu mara kwa mara (Aya ya 8-9).
Andika kifungu kimoja cha maombi kwa kila kipengele. (Hutakiwi kushirikisha andiko hili kwa kiongozi wako wa darasa lakini unapaswa umpe taarifa kwamba ulishaifanya kazi hiyo.)
(3) Kutokana na maisha ya Abrahamu na Sara tunajifunza kuhusu nyakati zinazoongezeka kwa ajili ya kusubiria. Fikiria kuhusu maswali haya:
Je, ni lini umewahi kungoja wakati wa Mungu? Umejifunza nini kutoka kwa nayakati hizi za kungoja?
Je, ni kwa vizuri kiasi gani unaamini ahadi zilizoko kwenye Neno la Mungu? Je, kwa wakati huu unapambana na ahadi? Je, kupambana huko kunaathiri familia yako? Kwa vipi
Je, ulishawahi kufanya jambo lolote wewe mwenyewe au kwa ajili ya familia yako bila ya kumtumainia Mungu? Matokeo yalikuwa ni nini?
Je, ni kwa jinsi gani subira na ukosefu wa imani kwa njia hasi vimeathiri familia?
Andika jumla ya vifungu vitatu kwa ajili ya kujibu mada hii. (Hutakiwi kushirikisha andiko hili kwa kiongozi wako wa darasa lakini unapaswa umpe taarifa kwamba ulishaifanya kazi hiyo.)
SGC exists to equip rising Christian leaders around the world by providing free, high-quality theological resources. We gladly grant permission for you to print and distribute our courses under these simple guidelines:
No Changes – Course content must not be altered in any way.
No Profit Sales – Printed copies may not be sold for profit.
Free Use for Ministry – Churches, schools, and other training ministries may freely print and distribute copies—even if they charge tuition.
No Unauthorized Translations – Please contact us before translating any course into another language.
All materials remain the copyrighted property of Shepherds Global Classroom. We simply ask that you honor the integrity of the content and mission.